• Sura 4: Mazungumzo na mawasiliano katika shughuli mbalimbali za kijamii

    Mada ndogo: Msamiati katika kazi za jumuiya

    A . Shughuli mbalimbali za jumuiya

    i) Mkutano wa kijiji chetu
    Kijiji ni mgao wa chini zaidi katika migao ya utawala. Kijiji aghalabu hujumuisha
    watu wanaotoka koo mbalimbali na ambao wanajuana. Watu hawa huja pamoja
    kufanya shughuli mbalimbali. Mikutano mbalimbali ya vijijini huweza kutumiwa
    kuinua hali ya maisha ya jamii ya vijiji hivyo.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Je, kijiji chenu kinaitwaje? Je, umewahi kuhudhuria mkutano wa kijiji chenu? Jiunge
    na mwanafunzi mwenzako na mjadilianeni shughuli mbalimbali ambazo hufanyika
    katika mikutano vijijini mwenu.

    Sasa tazameni michoro iliyopo hapa chini na msome kifungu cha habari.
    Mimi ni Munyana. Leo ni siku ya mkutano wa kijiji hiki chetu. Mwenyekiti wa
    kijiji chetu anamwomba Nziza kufungua                
    mkutano kwa maombi. Wanakijiji wote
    wanasimama na kuomba kisha wanakaa.

    “Asanteni sana kwa kuitikia mwaliko wa
     mkutano wetu. Shughuli yetu kuu siku
    ya leo ni kujadiliana kuhusu ugonjwa
    wa UKIMWI. Patakuwepo upimaji
    wa UKIMWI ndani ya hema. Upimaji
    utakuwa kwa hiari yako. Kwa sasa,
    ninamwalika mgeni wa heshima katika
    mkutano wetu huu wa leo atuhutubie.
    Mgeni huyo ni afisa wa afya kutoka
    Wizara ya Afya, Bi. Abigael Uwera.
    Tumkaribishe kwa makofi na vigelegele.”
    Watu wote wanasimama na kupiga
    makofi.

    “Mabibi na mabwana, UKIMWI ni ugonjwa usiojua umri, utajiri wala umaskini. Uwe
    tajiri au maskini unaweza kuupata. Unamshika yeyote anayeshiriki ngono hasa
    bila kutumia kinga. Pia, unaweza kuambukizwa ikiwa damu yenye maradhi haya
    imechanganyika na damu yako. Damu hizi zinaweza kuchanganyika kwa kutumia
    sindano au wembe mmoja au kugusa damu ya mtu aliyeambukizwa. Tukumbuke
    kuwa huwezi kupata UKIMWI kwa kumsalimia au kumkumbatia au kula pamoja na
    mtu aliyeambukizwa.”
    Watu wanatazamana na kunong’onezana. Ninainua mkono na kumwuliza mgeni
    wa heshima ikiwa ugonjwa huu una tiba.
    “La hasha! Ugonjwa huu hauna tiba. Hata hivyo, zipo dawa nzuri za kupunguza
    makali yake. Unapougua UKIMWI, ni sharti utumie dawa hizi tena kwa wakati
    uliopendekezwa bila kukosa. Ni vizuri sote tujue kuwa miili yetu ina chembechembe
    katika damu zetu ambazo hutukinga dhidi ya magonjwa. UKIMWI hudhoofisha
    chembechembe hizi. Miili yetu hukosa uwezo wa kupiga vita dhidi ya magonjwa.
    Hivyo, waathiriwa huweza kuuliwa na magonjwa kama vile malaria, kifua kikuu na
    magonjwa mengineyo.”
    Bi. Mutesi anainua mkono. Anapewa nafasi ya kuongea.
    “Mimi ni mwathiriwa wa ugonjwa huu wa UKIMWI. Bwanangu aliaga dunia kutokana
    na ugonjwa huu. Wanangu wawili pia wanaugua ugonjwa huu. Sote tumekubali
    hali zetu. Tunatumia dawa za kupunguzia makali. Tunakula vizuri na kuendelea na
    shughuli zetu za kila siku. Ningependa kuwaambia wenzangu ambao wanaugua
    ugonjwa huu wasiogope. Ninawashukuru sana wanakijiji hiki kwa kunionyesha
    mapenzi na kunisaidia kukubali hali yangu. Kwa wale ambao hawana UKIMWI,
    nawasihi mwepuke ngono nje ya ndoa. Wasichana kwa wavulana, jiepusheni na
    ngono hadi mfunge ndoa. Asanteni.”
    Tunampigia Bi. Mutesi makofi. Wengine wanasimama na kumkumbatia. Anaonekana
    mwenye afya nzuri. Kumbe mtu anayeugua UKIMWI huwa na afya nzuri! Huwezi
    kujua anayeugua ugonjwa huu kwa kumtazama. Njia ya kipekee ni kupitia upimaji.
    Ninasimama na kuwahutubia wanakijiji.
    “Mimi nipo tayari kupimwa. Baada ya kupimwa, nitakubali hali yangu. Ikiwa
    sina, nitajilinda. Baada ya kumaliza masomo na kuanza kufanya kazi, nitakubali
    kuchumbiwa. Nitamwambia mpenzi wangu tujipime ili tuwe na uhakika wa hali
    zetu. Nitakuwa mwaminifu kwake. Nipo tayari kushirikiana na wanakijiji wenzangu
    ili tuwapende na kuwasaidia waathiriwa wa UKIMWI. Pia, nipo tayari kujiunga na
    wanakiji kufanya kampeni ya kuwahamasisha wenzetu wajue kuhusu UKIMWI na
    waepuke kuambukizwa ugonjwa huu. Asanteni.”
    Wanakijiji wote wanasimama. Wanasema kwa pamoja kuwa wako tayari kujua na
    kukubali hali zao za UKIMWI.
    “Haya, twende tukajipime wenzangu,” anasema Kiongozi wa kijiji. Watu wote
    wanapiga foleni nyuma yake.

    Maswali
    1. Bainisha msamiati wa kimsingi kifunguni kuhusu shughuli katika mkutano na
        uutolee maana.
        Mfano: kufungua mkutano: kutangaza rasmi kuwa mkutano umeanza.
    2. Ni nini kilichokuwa kiini cha mkutano uliopo kifunguni?
    3. Nani alikuwa mgeni rasmi katika mkutano wa kijiji?
    4. Eleza mambo muhimu yanayojitokeza katika kifungu hiki.
    5. Toa muhtasari wa kifungu cha habari ulichosoma hapo juu katika aya moja.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wenzako katika kikundi. Nyinyi ni wanachama wa kijiji kimoja. Mmeandaa
    mkutano. Jadilianeni kuhusu mambo mbalimbali mtakayofanya ili kuangamiza
    umaskini katika kijiji chenu.

    ii) Sherehe ya harusi ya rafiki yangu
    Kazi ya wanafunzi wawili wawili

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Jadilianeni kuhusu mambo muhimu ambayo

    hufanyika katika sherehe ya harusi. Kwa mfano:

    1. Watu huja pamoja kutengeneza hema la wageni.

    2. Maarusi huimbiwa na kuchezewa.

    Baada ya kujadiliana mambo muhimu katika harusi, simulianeni kuhusu sherehe ya harusi mliyohudhuria.

    Tazama michoro hii. Je, mambo gani yanafanyika?
     

      

    Someni mazungumzo haya na mjibu maswali chini yake.

    SHEMA: Hujambo mwenzangu?

    TONA: Sijambo, ulikuwa wapi wiki nzima?

    SHEMA: Nilihudhuria harusi ya rafiki yangu.

    TONA: Kumbe! Ndiyo sababu una furaha tele.

    SHEMA: Mbona nisiwe na furaha? Ndoa ni jambo linalowafurahisha watu wengi. Kutajwa tu kwa neno hili hufanya roho za kila mtu kusisimka kwa furaha.

    TONA: Haya! Hata mimi ipo siku nilikuwa mpambe nilipokuwa mdogo. Bibi. harusi alivaa mavazi yake maalumu ya kupendeza kweli. Sisi wapambepia tulinunuliwa viatu na nguo za kupendeza. Sisi na bibi harusitulipambwa tukapambika. Nieleze kuhusu harusi hiyo uliyohudhuria.

    SHEMA: Sikujua kuwa Ganza angeweza kumchumbia msichana mrembo kamayule. Aliponiambia eti posa yake imekubalika nilidhani ananitania.Aliniandikia barua kunieleza eti amepeleka mahari. Bado sikuamini hadi aliponitumia kadi ya kunialika harusini.

    TONA: Ehe...

    SHEMA: Mimi nilifika mapema na wenzangu kumsaidia rafiki yangu.Tulitengeneza mahema na kupanga viti hemani. Wengine walirembeshamahema kwa maua, baluni, na mapambo yenye rangi mbalimbali. Mahema yale yalivutia kwelikweli. Wengine walikuwa jikoni wakiandaa vyakula nao wengine walipokea wageni ambao walianza kuwasilimapema. Tukakodisha magari ambayo yangemsafirisha bwana na bibiharusi. Tukahakikisha kuwa vyombo vya burudani vipo katika hali sawatayari kuwatumbuiza wageni.

    TONA: Ahaa! Bibi harusi alikuwa wapi wakati huu wote?

    SHEMA: Ah! Kwani hujui? Bibi harusi alikuwa mahali kusikojulikana. Huko alikuwa na wapambe ambao walikuwa wakimrembesha.

    TONA: Ehe...

    SHEMA: Baada ya maandalizi, nikajiunga na wanaume ambao huandamana nabwana harusi. Pale, tulipewa mafunzo ya jinsi ya kutembea nakumsindikiza bwana harusi. Tukapima suti zetu nyeusi na kujaribu kutembea kwa viatu vyetu vipya. Bwana harusi naye akajaribu kuvaa pete ili ahakikishe kuwa inamtosha. Kila kitu kikawa shwari.

    TONA: Nieleze mambo yaliyojiri siku ya harusi.

    SHEMA: Harusi hiyo ilianza kwa watu kukaa kanisani kwa matarajio makubwahuku wakinong’onezana. Mara mfawidhi akatangaza kuwa tusimamekwa kuwa bibi harusi sasa anaingizwa kanisani. Bibi harusi akasindikizwa kanisani na babake na kupelekwa pale mbele alipokuwa akisubiriwa na mchumba wake pamoja na mchungaji. Hapo, waliapishwa na halafu kuvishana pete na mwishowe kutangazwa bibi na bwana. Wacha sasasherehe kamili zianze. Waliokula walikula na waliokunywa walikunywa.Nao waliocheza walicheza na waliofanya urafiki kwa matarajio yakufanya ndoa kama hiyo walifanya.

    TONA: Ama kwa kweli harusi hiyo ilifana kweli! Asante.

    SHEMA: Karibu.

    Maswali

         1. Kwa nini ndoa ni jambo la kufurahisha?

         2. Eleza maana ya msamiati uliowekewa wino nzito.

         3. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati ulioeleza hapo juu.

         4. Eleza mambo muhimu yanayofanyika harusini kwa mujibu wa kifungu hiki.

         5. Eleza umuhimu wa ushirikiano katika jamii kwa kurejelea matukio kifunguni.

         6. Toa muhtasari wa kifungu hiki cha habari katika aya moja.

    iii) Mazishi

    Mazishi ama maziko ni shughuli za kuzika mfu au wafu. Mfu ni mtu aliyeaga dunia. Shughuli hizi huendeshwa kutegemea utamaduni na imani za kidini za wahusika au waathiriwa.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tazameni mchoro ulio kwenye ukurasa ufuatao. Je, ni shughuli gani inayofanywa? Jadilianeni kuhusu shughuli ambazo hufanywa wakati wa mazishi katika jamii yenu.

    Soma kifungu kilichopo hapa chini na ujibu maswali chini yake.

    Sikujua kuwa sigara huua hadi nilipompoteza mjomba wangu mwaka jana. Mjomba aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa saratani ya mapafu. Alipenda sana kuvuta sigara. Aliaga dunia katika hospitali moja jijini Kigali. Punde tu alipofariki, mwili wa mjomba ulipelekwa katika mochari. Huko, mwili wake ulisafishwa na wahudumu wa mochari na kuwekwa katika jokofu.

    Jamaa na marafiki walikuja pamoja kumpa mjomba heshima zake za mwisho. Wanakijiji na watu kutoka mbali walishiriki katika shughuli mbalimbali kufanikisha mazishi ya mjomba.

              

    Wanakijiji walichanga pesa za kulipia gharama za mochari na shughuli nyinginezo. Wengine walijitolea kutengeneza jeneza zuri la kumzikia mjomba. Wengine walinunua sanda. Wengine walichimba kaburi. Kila mtu alishiriki katika shughuli hizi kadiri ya uwezo wake.

    Mwili wa mjomba uliondolewa kwenye mochari baada ya wiki moja. Mwili huo ulisafirishwa hadi kanisani. Alifanyiwa ibada ya wafu. Jamaa na marafiki walifika kanisani kushiriki katika ibada hiyo.

    Baada ya maombi, watu walipewa ruhusa ya kutazama mwili wa mjomba. Hali ya huzuni ilitanda kanisani.Baada ya ibada, mwili huo ulisafirishwa nyumbani kwake. Mimi na jamaa za mjomba tulihuzunika. Wanakijiji na marafiki zetu walitufariji.

    Siku ya mazishi ilipofika, ibada ya wafu iliandaliwa. Mchungaji aliendesha shughuli akishirikiana na familia ya marehemu mjomba. Mchango wa kusaidia familia ya marehemu mjomba pia ulifanywa. Wanakijiji na wageni walitoa michango yao. Hatimaye wakati wa kuteremshwa kwa jeneza kaburini ulifika. Baada ya maombi mafupi kando ya kaburi, jeneza lilitiwa ndani ya kaburi. Mchungaji alituhutubia.

    “Tunasikitika kuwa marehemu aliaga dunia kutokana na uvutaji wa sigara. Nawasihi vijana kwa wazee mwepuke uraibu wa sigara na dawa za kulevya. Tumempoteza mwenzetu aliyekuwa na bidii ya mchwa. Tuige tabia zake nzuri na kuepuka zile mbaya. Ikiwa pana mtu ambaye mfu huyu alikuwa na deni lake, aseme sasa.”

    Hakuna aliyeinua mkono. Mhubiri alifanya ombi la mwisho kisha shughuli za kufunika kaburi zikaanza. Familia ya mjomba ilikuwa ya kwanza kuweka mchanga kwenye kaburi. Baadaye, wanakijiji walisaidia katika kufunika kaburi.

    “Asanteni kwa kushiriki katika mazishi haya. Tunamwomba Mungu amlaze mahali pema peponi,” mhubiri alisema kisha watu wakaondoka.

    Wageni kutoka mbali walipewa vyakula na vinywaji. Baadaye waliondoka kwenda zao.

    Maswali

    1. Kwa maneno yako mwenyewe, eleza maana ya mazishi.

    2. Bainisha na utoe maana ya msamiati mbalimbali kuhusu mazishi kifunguni.

    3. Tunga sentensi ukitumia msamiati uliotajwa hapo juu.

    4. Eleza shughuli muhimu za mazishi zilizotajwa kifunguni.

    5. Kwa maneno yako mwenyewe, eleza mambo muhimu kifunguni katika aya moja.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako. Jadilianeni kuhusu utaratibu wa mazishi ya kienyeji katika sehemu mtokako.

    iv) Kazi ya umuganda
    Umuganda ni mkusanyiko wa watu kutoka vijiji mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa taifa. Mnamo siku ya Jumamosi ya mwisho kila mwezi, Wanyarwanda wote walio na miaka kati ya kumi na minane na sitini na mitano hukusanyika katika makundi mbalimbali kushiriki katika kazi za umuganda.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na wanafunzi wenzako. Jadilianeni kuhusu shughuli mbalimbali ambazo hufanywa siku ya kazi ya umuganda.

    Tazama michoro hii kuhusu shughuli mbalimbali za umuganda na usome kifungu cha habari.

      
       
    Wanyarwanda hushiriki katika shughuli mbalimbali siku ya kazi ya umuganda. Umuganda huandaliwa kila Jumamosi ya mwisho ya mwezi. Kila kijiji huamua shughuli muhimu wanazostahili kufanya. Wao huchagua shughuli ambayo ina umuhimu kwao.

    Baadhi ya wanakijiji huweka vizuizi vya mmomonyoko wa udongo kwa kuchimba mitaro. Wengine wanajaza mitaro hiyo kwa magunia yaliyojaa mchanga. Wengine wanafunika magunia hayo kwa mchanga. Mvua inaponyesha, maji tu ndiyo hupita lakini udongo hubakia kwenye mitaro na magunia yaliyowekwa. Hivyo, rutuba hubakia kwenye udongo nayo ardhi huweza kutumiwa tena katika shughuli za kilimo.

               
    Wanyarwanda pia huja pamoja kusafisha maeneo wanamoishi. Watu hupewa majukumu mbalimbali wakati wa usafishaji. Baadhi ya watu huondoa taka kwenye mitaro ya maji machafu. Wengine hupewa jukumu la kuokota taka zilizotapakaa. Wengine huchoma taka hizo. Nao baadhi ya watu kufyeka nyasi zilizomea kando ya mitaro na maeneo mengineyo. Shughuli hizi hulenga kudumisha usafi katika miji na vijiji vyetu.



           
    Wanyarwanda pia hupanda miti siku ya kazi ya umuganda. Wao hupanda miti hasa kwenye ardhi tambarare. Wengine hunyunyizia miche maji. Miti mingi hupandwa na wanakijiji mbalimbali kwa kuwa miti ni muhimu katika mazingira yetu.

              
    Mbali na hayo, baadhi ya Wanyarwanda hulima na kupalilia mashamba yao. Wao huja pamoja kwa ajili ya kuwasaidia wenzao hasa wazee katika mashamba yao.

    Maswali
    1. Eleza umuhimu wa kazi ya umuganda katika jamii zetu.
    2. Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Kila mwanafunzi asimulie mambo muhimu yanayojitokeza katika shughuli ya kijamii aliyoshiriki zaidi.

    Kazi ya kikundi

    Jiunge na wanafunzi wenzako. Jadilianeni kuhusu shughuli za kijamii mlizoshiriki kisha mziwasilishe mbele ya darasa.

    B. Namna sahihi ya kuuliza maswali

    Kufikia sasa, umejifunza mengi kuhusu shughuli mbalimbali za kijamii. Unaposhiriki katika mazungumzo kuhusu shughuli hizi za kijamii au mambo mengineyo, unaweza kuuliza maswali mbalimbali.

    Katika Kiswahili, zipo namna mbalimbali za kuuliza swali. Maneno ambayo hutumiwa kuulizia maswali huitwa viulizi. Zipo aina mbalimbali za viulizi. Je, unakumbuka viulizi hivyo?

    Viulizi huuliza maswali kuhusu jinsi kitendo kilivyotendeka (vipi), wakati kitendo kilipofanyika (lini), mahali kitendo kilipofanyika (wapi), aliyetenda kitendo (nani), kitendo chenyewe (nini), idadi (-ngapi) na namna ya kitendo au kifaa (gani).Hapa, maneno yaliyowekwa kwenye mabano ndiyo viulizi vinavyotumiwa kuulizia maswali.

    Soma kifungu hiki ili ujifunze mengi kuhusu namna sahihi ya kuuliza maswali.

        

    INEZA: Wenzangu, kwa nini hamkuhudhuria mkutano wa kijiji uliokuwepoJumamosi iliyopita?

    TONA: Shoga yangu, wewe unafahamu kuwa mamangu mzazi hajisikii vizuri.Sasa, siku hiyo ilibidi niondoke niende kumtazama.

    NDOLI: Nami wenzangu sina sababu ya kutohudhuria bali nilisahau tu na kutanabahi mkutano umekwisha. Mambo gani yalijiri mkutanoni humo?

    INEZA: Lo! Tulifanya shughuli mbalimbali...

    TONA: Samahani kwa kukutatiza usemi. Shughuli hizo mlizifanya wapi?

    INEZA: Tulikusanyika katika uwanja wa mkutano wa kijiji kisha tukajigawa katikavikundi mbalimbali. Kila kikundi kilishiriki kufanya kazi katika maeneo mbalimbali.

    NDOLI: Kwa jumla, vikundi vilikuwa vingapi?

    INEZA: Vikundi vyote vilikuwa tisa.

    TONA: Nani aliongoza kikundi chenu?

    INEZA: Kikundi chetu kiliongozwa na Bi. Kabatesi.

    NDOLI: Nini alichowapa kabla ya kazi?

    INEZA: Alitupa vifaa mbalimbali.

    TONA: Mlipewa vifaa gani?

    INEZA: Tulipewa mapanga na majembe.

    NDOLI: Mlifanya kazi ipi katika kikundi chenu?

    INEZA: Tulifyeka na kulima shamba la nyanyake Teta.

    TONA: Mkutano ujao utakuwa lini?

    INEZA: Mkutano ujao utakuwepo Jumamosi ya mwisho, mwezi ujao. Msikosekuhudhuria kikao.

    NDOLI: Ni vifaa gani vitahitajika katika kazi hiyo ya umuganda?

    INEZA: Vifaa vitakavyohitajika vitakuwa fagio, ndoo, majembe, mapanga namafyekeo. Msikose kushiriki.

    TONA na NDOLI: Tukijaaliwa tutakuwepo. Asante.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni maswali sahihi kuhusu shughuli mbalimbali za kijamii mkitumia viulizi vifuatavyo. Sahihishianeni majibu yenu.

          a) vipi

          b) lini

          c) wapi

          d) nani

          e) nini

          f ) -ngapi

          g) gani

    Kazi ya kikundi

    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Rejeleeni vifungu vya habari mlivyosoma kuhusu shughuli mbalimbali za kijamii katika vipindi vilivyopita. Tumieni viulizi mbalimbali kuulizana maswali kwa zamu kutokana na yaliyomo kwenye vifungu hivyo. Anayeulizwa ajibu kila swali kwa usahihi. Anapopata jibu, naye amwulize mwenzake swali.

    Mifano

    1. Afisa wa afya kutoka wizara ya kilimo alisema nini kuhusu UKIMWI?
    2. Nani alifanya harusi?

    C. Aina saba za maneno

    Lugha ya Kiswahili huwa na aina saba kuu za maneno. Maneno haya hutambuliwa kulingana na muundo na matumizi yake katika sentensi. Maneno hayo saba huwa nomino, vitenzi, vielezi, vivumishi, viwakilishi, viunganishi na vihisishi.

    Nomino

    Kufikia sasa, umejifunza mengi kuhusu aina mbalimbali za nomino. Je, unazikumbuka?Tunaweza kutumia nomino mbalimbali kutaja mtu au watu walioshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii. Pia, tunaweza kutumia nomino kutaja vifaa mbalimbali vilivyotumika kutendea shughuli fulani za kijamii, mahali shughuli hizo zilipofanyika na kadhalika. Tazama aina mbalimbali za nomino katika jedwali na usome mifano kando yake.

    Zoezi A

    Soma kifungu kifuatacho cha habari. Bainisha na uainishe nomino mbalimbali katika kifungu.

         

    Ama kwa kweli, ndoa ni jambo linalowafurahisha watu wengi. Kutajwa tu kwa neno hili hufanya roho za watu wengi kusisimka. Takriban watu wote husikia neno hili kwa upendo. Kwa nini upendo? Unapotajiwa neno hili, fikira ya kwanza kukujia ni raha. Watu husikia raha kwa sababu huwepo maakuli na vyakula vingi vya bwerere. Pia, harusi huleta heshima na umaarufu.

    Kabla ya kufanya harusi, yapo mambo mengi ambayo hufanyika. Kwanza kabisa, ni sharti mchumba apatikane. Halafu ni sharti ujumbe wa posa upelekwe na mshenga kwa kina mchumba. Ukikubalika, mahari huzungumziwa na kulipwa. Ni baada ya haya yote tu ambapo siku ya harusi huwekwa.

    Nayo matayarisho ya harusi huwa mengi. Bi harusi pamoja na wapambe wake sharti wanunuliwe mavazi mbalimbali ya harusi. Mavazi haya huwa pamoja na nguo maalumu za Bi harusi na wapambe wake. Pia ni sharti pawepo jozi mpya za viatu, pete ya harusi, mashada ya maua na kadhalika. Matayarisho mengine ni usafiri, waendesha harusi, kwaya, na matayarisho mengine mbalimbali.

    Hatimaye huja siku yenyewe ya harusi. Mfano mzuri wa siku hii ni harusi ya rafiki yangu Iliza iliyofanyika Ijumaa jijini Kigali. Umati wa watu ulihudhuria harusi hiyo. Baada ya ibada, tulienda katika Hoteli ya Serena ambapo sherehe kamili iliandaliwa.

    Zoezi B

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni sentensi zinazohusu shughuli mbalimbali za kijamii kwa kutumia nomino mbalimbali mlizobainisha kifunguni.

    Vitenzi

    Kitenzi ni neno lielezalo jambo la kutendwa au kufanywa.

    Je, unakumbuka mifano mbalimbali ya vitenzi ulivyosoma?

    Tunaposhiriki katika mazungumzo kuhusu shughuli mbalimbali za kijamii, ni sharti tutumie vitenzi mbalimbali.

    Tazama aina mbalimbali za vitenzi katika jedwali na usome matumizi yake.

    Zoezi A

    Soma kifungu kifuatacho cha habari. Bainisha na uainishe vitenzi mbalimbali vilivyomo kifunguni.

      
    “Tuharakishe. Ujenzi wa choo umeanza,” Ikirezi aliniambia. Alikuwa akihema. “Mimi ni mgonjwa. Ningali ninaumwa na tumbo lakini nitajikaza,” nilimjibu. Hatimaye tuliwasili penye mkutano. Watu walikuwa wamejigawa katika vikundi tayari kwa kazi mbalimbali.

    “Tazama. Kila mtu ameanza kujenga choo isipokuwa sisi,” nilimwambia Ikirezi. Kiongozi wa kijiji alinisikia.“Msiwe na shaka. Nyinyi mtaokota taka zote zilizopo pale uwanjani. Baada ya hapo, mtafagia kando ya barabara. Kazi hiyo si ngumu,” kiongozi wa kijiji alisema.

    Mimi na Abatoni tulitafuta fagio. Tuliongezewa vijana watatu ili watusaidie kufanya kazi hiyo. Tulifurahia sana kushirikiana na wanakijiji.

    Zoezi B

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni sentensi zinazohusu shughuli mbalimbali za kijamii kwa kutumia vitenzi mbalimbali mlivyobainisha kifunguni.

    Vielezi

    Vielezi pia huitwa viarifa nayo ni maneno yafafanuayo vitenzi, vivumishi au vielezi. Tunaweza kutumia vielezi kueleza jinsi shughuli mbalimbali za kijamii zilivyofanywa. Mathalan, ukisema: Anafanya kazi haraka neno haraka linaeleza jinsi kazi inavyofanywa.

    Je, unakumbuka vielezi ulivyosoma?

    Tazama aina mbalimbali za vielezi katika jedwali na matumizi yavyo.

    Zoezi A

    Soma kifungu kifuatacho cha habari. Bainisha na uainishe vielezi mbalimbali kifunguni.



    Ilikuwa siku ya Jumamosi. Ilikuwa siku ya kuwasaidia wazee kuandaa mashamba yao na kupanda mbegu. Wanakiji wote waliamka alfajiri. Mimi pia nilijiunga nao kwa hiari. Wa kwanza kusaidiwa aliitwa Abera. Tulitembea upesi kuelekea shambani mwake ili tufike mapema. Tulipofika ndani ya shamba, kila mtu alipewa jukumu. Wengine walifyeka majani marefu yaliyomea pembeni mwa shamba.

    Waliyafyeka majani kwa panga. Wengine walilima kwa jembe la mkono. Wengine waliondoa magugu hatari kutoka shambani na kuyachoma kwa moto. Sisi tulipanda mbegu. Kila mtu alipewa kazi ya kufanya mara kwa mara. Hakuna aliyekaa bure. Sote tulifanya kazi kijeshi.

    Zoezi B

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni sentensi zinazohusu shughuli mbalimbali za kijamii kwa kutumia vielezi mbalimbali mlivyobainisha kifunguni.

    Vivumishi

    Kwa kawaida, kivumishi ni neno linaloongezea nomino maana. Vivumishi vinaweza kutumiwa kuelezea sifa za mtu au watu walioshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii. Pia, tunaweza kutumia vivumishi kueleza sifa za vifaa vilivyotumika katika shughuli za kijamii na kadhalika.Kumbuka kuwa vivumishi ni sharti vitumiwe pamoja na nomino. Je, unakumbuka vivumishi gani ulivyosoma?

    Tazama aina mbalimbali zifuatazo za vivumishi huku ukisoma matumizi yaliyotolewa.

    Zoezi A

    Soma kifungu kifuatacho cha habari. Bainisha na uainishe vivumishi mbalimbali katika kifungu.

    Ni taifa gani ambalo halipendi maendeleo? Ama ni watu wepi ambao hawapendi kuendelea? Sisi Wanyarwanda tunapenda maendeleo ili taifa letu likue hata zaidi. Nchi yenye watu wanaopenda maendeleo hukua haraka. Ili jambo hili liwezekane, ni sharti tufanye mambo kadhaa.

    Kwanza kabisa, nchi yetu haiwezi kukua bila masomo. Lazima watoto wote waliofika umri wa kuenda shule waende shuleni. Nasi wanafunzi wenyewe tulenge kufikia elimu ya chuo kikuu. Ili kufaulu masomoni, ni sharti tushirikiane na jamii. Ujuzi huu tunaopata shuleni ni sharti tuutumie kusaidia jamii. Tusingoje hadi tumalize chuo kikuu ndipo tuanze kujenga taifa hili letu.

    Pili, usafi ni jambo muhimu sana. Jamii haiwezi kujenga taifa lake kama haina afya nzuri. Je, kina nani wanafaa kudumisha usafi huu? Watu hao si watu wengine bali ni mimi na wewe. Kila mmoja wetu ahakikishe kuwa anaishi katika mazingira safi kila siku.

                          

    Tatu, kuna shughuli ya mikutano tofauti tofauti ya kutangaza na kuhimiza maendeleo. Jamii inapokutana na kuelezwa maendeleo yaliyopatikana, hupata motisha ya kufanya mengi zaidi. Hali hii basi huwa ni msukumo muhimu katika kazi zao. Vilevile, vijiji hushindana katika maendeleo. Mashindano ya dhati kati ya vijiji huwa ni motisha nzuri ya ujenzi wa taifa. Kumbuka kuwa vijiji vikipiga hatua mbele nalo taifa hufanya vivyo hivyo.

    Jambo jingine linalohitajika katika huu ujenzi wa taifa ni kuwa na mikakati kabambe ya kushughulikia mikasa. Mathalan, tumejitayarisha vipi kukabiliana na mkurupuko wa magonjwa hatari na njaa? Ni sharti tushirikiane ili kuibuka na mikakati kabambe ya kukabiliana na mikasa kama hii.

    Ili haya yote na mengine mengi yafaulu, umoja na ushirikiano wetu lazima uwepo. Kumbuka kuwa kidole kimoja hakivunji chawa nalo jiwe moja haliinjiki chungu.

    Zoezi B

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni sentensi zinazohusu shughuli mbalimbali za kijamii kwa kutumia vivumishi mbalimbali mlivyobainisha kifunguni.

    Viwakilishi

    Viwakilishi ama vibadala ni maneno kamili ama viambata (sehemu za maneno) vinavyosimama badala ya majina. Je, unakumbuka viwakilishi ulivyosoma?Tazama aina mbalimbali hizi za viwakilishi katika jedwali lifuatalo huku ukisoma matumizi yake.

    Zoezi

    Soma kifungu kifuatacho cha habari. Bainisha na uainishe viwakilishi mbalimbali katika kifungu.

          
    Waliosema kuwa umoja ni nguvu hawakukosea bali waligonga ndipo. Mimi ninaamini sana katika msemo huu. Ninaamini kwa sababu ya mambo niliyoshuhudia nilipompoteza mama mzazi. Mama alikuwa mtu wa watu. Aliwapenda wanakijiji nao wanakijiji wa mbali na wa karibu wakampenda. Kifo chake kiliwashtua wengi. Kilifanya kijiji kizima kiomboleze. Watu walifurika nyumbani kwetu kutupa pole. Kuwepo kwao kulituliwaza. Licha ya machungu, tulihisi kuwa hatupo peke yetu. Nani angekosa kupata nguvu katika hali kama hii? Msiba huleta unyonge. Wetu ulileta nguvu kutokana na ushirikiano huo.

    Mbali na kutupa moyo, wanakijiji waligharamia mazishi. Wao walisimamia kila kitu. Sisi tulishuhudia tu mambo yakitendeka. Hawakutaka tushiriki katika shughuli zozote kutokana na huzuni. Waliopika walipika. Waliotengeneza jeneza walifanya hivyo tena kwa ustadi. Waliochimba kaburi hawakusita kumaliza mapema. Kila kitu kilifanywa kwa haraka na ustadi. Mama akalazwa na kupewa heshima zake za mwisho kwa ushirikiano wa wanakijiji. Wao hao wakatuchangia pesa za matumizi ya baadaye. Tulikosa maneno ya kuelezea furaha na shukrani zetu kwao. Kweli, umoja ni nguvu.

    Viunganishi

    Haya ni maneno yanayotumika kuunganisha maneno, vikundi vya maneno au sentensi ili kupitisha ujumbe fulani.

    Tazama mifano hii ya viunganishi.

       1. Tulikuja pamoja ili kuwafariji waliofiwa.

       2. Mkutano uliahirishwa kwa sababu mvua kubwa ilinyesha.

       3. Mbali na kufagia, wanakijiji hupanda miti na kujenga vizuizi vya kukinga mmomonyoko wa udongo.

       4. Tulisameheana maadamu tulishiriki kazi pamoja.

    Zoezi

    Soma kifungu kifuatacho. Bainisha aina mbalimbali ya viunganishi vilivyotumika.

       

    Kila jamii huwa na ngoma yao waipendayo. Aghalabu wao huipenda kwa sababu wameirithi kutoka kwa mababu zao. Mathalan, Waswahili hupenda sana msondo. Je, nyinyi mnapenda ngoma gani katika jamii yenu?Kwa kawaida, ngoma kama hiyo huchezwa na wale waliopo sasa. Baadaye hupitishwa kwa vizazi vijavyo. Kwa namna hiyo, ngoma husika huja ikawa sehemu kuu ya utamaduni wao japo baadhi ya mambo ya kisasa huongezwa. Mambo hayo ya kisasa huongezwa pasipo kubadilisha asilia ya ngoma hizo.

    Sisi Wanyarwanda pia tunapenda ngoma zetu za kiasili. Itokeapo shughuli muhimu, sisi hushiriki katika kuimba na kucheza ngoma zetu za kitamaduni. Hivyo basi, ngoma huchezwa kama njia mojawapo ya kujiburudisha. Shughuli hii huambatana sana sana na sherehe fulani kama vile siku za kitaifa, harusi, kusherehekea mavuno, siku ya kutoka jandoni au kuvunja ungo na kadhalika. Mbali na hayo, ngoma ni njia moja kuu ya kutuleta pamoja ili kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

    Aidha, tunapocheza ngoma fulani siku ya taifa, tunapata kumbukumbu muhimu katika historia yetu. Kwa mfano, tunakumbuka jinsi tulivyokuja pamoja kujikomboa kutoka kwa minyororo ya wakoloni. Ikiwa umoja wetu ulifukuza wakoloni sembuse umaskini?

    Ngoma vilevile hutukumbusha umuhimu wa kuwepo kwa amani. Pia, ngoma hutuonya dhidi ya kuchukiana. Hutukumbusha kuwa amani, upendo na umoja ni mambo muhimu katika ujenzi wa nchi yetu.

    Iwapo tutapenda ngoma zetu za kienyeji na kutunga nyimbo za kisasa zenye kukuza ushirikiano, basi tutapiga hatua kubwa katika maendeleo yetu.

    Kazi ya kikundi

    Jiunge na wanafunzi wenzako. Jadilianeni kuhusu aina na mifano mbalimbali ya viunganishi katika Kiswahili. Tungeni sentensi sahihi mkitumia viunganishi hivyo.

    Vihisishi

    Vihisishi ni maneno ambayo huonyesha hisia mbalimbali za mzungumzaji. Unaweza kuelezea hisia zako kuhusu shughuli mbalimbali za kijamii kwa kutumia vihisishi. Vihisishi hutumika pamoja na alama ya hisi (!).

    Tazama mifano iliyotolewa hapa chini.

      a) Huree! Tumemaliza kujenga nyumba.

      b) Alaa! Mbona harusi haijaanza?

      c) Ole wangu! Kumbe nilikosa mengi katika mkutano wenu!

      d) Inshallah! Tukutane kesho twendelee na kazi yetu.

    Zoezi

    Soma kifungu kifuatacho. Bainisha aina mbalimbali za vihisishi vilivyotumika.

      
    Sote tulifunga safari ya kumtembelea Gatete kijijini mwao. Lo! Hatukuamini macho yetu tulipofika huko. Kumbe kijiji hicho kilikuwa safi na tulivu mno!Gatete alipokuja kutulaki, tulimpa pongezi. “Hongera! Mnafanya kazi nzuri kweli,” Ndoli alisema.Gatete alimtazama Ndoli kwa mshangao. Hakuelewa sababu za hongera zake.

    “Jamani! Mbona kijiji hiki chenu ni safi namna hii?” nilimwuliza Gatete.“Ahaa! Sisi hutupa taka zote katika majaa. Pia, tunachimba mitaro ili tusiwe na vidimbwi vya maji. Yeyote, awe mdogo au mkubwa, huokota majani makavu au taka zozote popote,” Gatete alisema akitabasamu.“Maskini sisi! Hatufanyi hivyo hata!” Ndoli alisema.

    “Alaa! Mnafaa mwanze kufanya hivyo moja kwa moja. Usafi ni jambo muhimu sana katika maisha yetu.”“Naam! Kuanzia leo, nitahimiza wanakijiji wenzangu ili kwa pamoja tudumishe usafi.”

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako. Fanyeni utafiti kuhusu aina mbalimbali za vihisishi katika Kiswahili. Tungeni sentensi sahihi mkitumia vihisishi hivyo.

    Zoezi la ziada

    Soma kifungu hiki. Bainisha na uanishe aina saba za maneno ya Kiswahili (nomino, vitenzi, vivumishi, vielezi, viwakilishi, viunganishi na vihisishi)

                                            Kukoga mwaka


    Hapo zamani, watu tofauti walikuwa na itikadi mbalimbali kuhusu kuanza kwa mwaka. Baadhi yao walisherehekea siku hiyo kwa kuchinja na kuandaa karamu murua! Nao wengine waliwatambikia wazee wao waliofuata njia ya marahaba. Zaidi ya haya, baadhi ya watu waliamini kuwa ni lazima mwaka mpya uanze kwa usafi. Hii ndiyo ilikuwa sababu ya kukoga mwaka.

    Kukoga mwaka kulikuwa na utaratibu wake. Kazi hizo zote zilitegemea mwanzo wa mwaka wa kiasili bali si ule wa kizungu. Mwaka huo wa kiasili ulikuwa ukianza saa thenashara hivi za asubuhi. Hivyo basi, kabla ya wakati huo, wenyeji walirauka saa kumi. Madhumuni ya kuamka wakati huo yalikuwa kusafisha kila kitu kabla ya mapambazuko. Basi wanawake waliamka na kukusanya vitu vyote ambavyo viliweza kuoshwa na kuvipeleka mtoni. Wengine walibaki nyumbani kusafisha vile vitu ambavyo havikuweza kuchukuliwa mtoni lakini ambavyo vilihitaji kuoshwa au kusafishwa.

    Baadhi ya vitu vilivyooshwa mtoni vilikuwa nguo zilizomea koga, vyungu, sahani, sufuria na vyombo vinginevyo. Baadhi ya watu walisafisha vyombo hivyo kwa sabuni lakini wengine walivisafisha kwa majani maalum. Jambo lililokuwa la mwisho kufanywa huko mtoni ni kuwaosha watoto. Baadaye watu wazima wangeoga wao wenyewe. Wakati mwingine, watu wangeosheana miguu kama ishara ya upendo.

    Nao wanawake wale waliobaki nyumbani walikuwa na kazi kubwa ya kusafisha nyumba mbalimbali za msonge. Baadhi yao walipaka sakafu kwa samadi mbichi iliyochanganywa na udongo na maji. Nao wanawake wengine waliondoa masizi yaliyokuwa yakining’inia kwenye mapaa.

    Vijana nao walisomba maji kutoka mtoni. Maji hayo yangetumiwa na wanaume kuogea. Wao pia wangeoga baadaye.

    Wanaume nao hawakukaa bure. Ilikuwa kazi yao kufyeka na kusafisha uani, mbele na pande zote za nyumba. Pia ilikuwa kazi yao kufyeka nyasi zo zote zilizokuwepo pale kiamboni pamoja na kukata matagaa yasiyohitajika ili kwamba jua la mwaka mpya lichomozapo liangaze boma zima.

    Je, ni kwa nini kazi hizo zote zilifanyika? Hata wakati huo, wenyeji waliamini kuwa Mungu hakupenda uchafu. Isitoshe, waliamini kuwa mtu akianza jambo fulani kwa nuksi basi hatafanikiwa katika mambo mengi. Hivyo basi, imani yao ilikuwa kwamba mwaka ukianza kwa uchafu basi shughuli zao zote mnamo mwaka huo zingekumbwa na nuksi. Hapana hata mmoja aliyetaka kutofanikiwa. Naam! Mwaka mpya ungeanza kwa usafi kweli.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi mwenzako. Someni vifungu mbalimbali vya habari vilivyopo katika sura hii ya nne. Bainisheni na kuainisha aina saba za maneno ya Kiswahili katika vifungu hivyo.

    D. Matumizi ya wakati uliopita -li- hali yakinishi na hali kanushi


    Tunaweza kuzungumzia shughuli mbalimbali za kijamii tulizoshiriki muda au wakati uliopita. Wakati huu huwasilishwa na -li-. Vitendo katika wakati uliopita vinaweza kuwa katika hali yakinishi au katika hali kanushi. Hali yakinishi ni ya kukubali na hali kanushi ni kukataa.

    Tazama mifano ya matumizi ya wakati huu iliyotolewa kwenye jedwali lifuatalo.

    Je, unaona mabadiliko gani katika hali kanushi ya vitenzi hivyo? Katika jedwali lililopo hapo juu, vitenzi walihudhuria, nilienda na ilianza vipo katika hali yakinishi au kukubali kwa wakati uliopita.

    Vitenzi hawakuhudhuria, sikuenda na haikuanza vimo katika hali ya kukataa yaani hali kanushi kwa wakati uliopita. Kiambishi ‘li-‘ hakitumiki katika hali kanushi. Huondolewa.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili

    Jiunge na mwenzako. Tungeni sentensi sahihi kuhusu shughuli za kijamii mkitumia wakati uliopita katika hali yakinishi na kanushi.

    E. Matumizi ya wakati ujao -ta- katika hali yakinishi na hali kanushi

    Wakati ujao hutumiwa kuelezea mawazo au vitendo vitakavyofanyika baadaye. Kiambishi -ta- hutumika pamoja na kitenzi husika kuonyesha kuwa kitendo kitafanyika baadaye.

    Tunaweza kuzungumzia shughuli mbalimbali za kijamii ambazo zitafanyika baadaye. Mfano: unapoandika ratiba ya shughuli au kutoa maelekezo ya mambo yanayofaa au ambayo hayafai kufanywa, unatumia wakati ujao.

    Vitendo katika wakati ujao vinaweza kuwa katika hali yakinishi au kanushi. Hali yakinishi ni ya kukubali na hali kanushi ni kukataa.

    Tazama mifano iliyotolewa kwenye jedwali lifuatalo.

    Vitenzi vilivyopo katika jedwali viko katika wakati ujao.
    Je, unaona mabadiliko gani katika hali kanushi ya vitenzi hivyo?
    Katika jedwali lililopo hapo juu, vitenzi utaandaliwa, litatufaa na mtafyeka vipo katika hali yakinishi au kukubali kwa wakati ujao.
    Vitenzi hautaandaliwa, halitatufaa na hamtafyeka vimo katika hali ya kukataa yaani hali kanushi kwa wakati ujao.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwenzako. Tungeni sentensi sahihi kuhusu shughuli za kijamii mkitumia wakati ujao. Mzingatie hali yakinishi na kanushi.

    Mifano

    ABATONI: Vijana watafyeka barabara.
    NDOLI: Vijana hawatafyeka barabara. Watasomba maji ya kujengea nyumba.
    ABATONI: Wazee hawatasomba maji ya kujengea nyumba. Watatoa maelekezo.

        Maswali ya marudio


    1. Eleza mambo muhimu ambayo hutendeka katika shughuli za ubudehe.

    2. Linganisha na utofautishe shughuli za mazishi na harusi katika jamii.

    3.  a) Bainisha wahusika wakuu katika shughuli hizi za kijamii:

              i) Mazishi

              ii) Harusi

              iii) Ibada msikitini au kanisani

         b) Eleza tofauti za kimawasiliano katika shughuli zilizotajwa hapo juu.

    4. Tunga sentensi ukitumia msamiati ufuatao:

              a) kuchimba mitaro

              b) kusomba maji

              c) kula kiapo

              d) peleka mahari

    5. Taja sherehe nne muhimu za jamii katika eneo utokako huku ukiielezea kila moja umuhimu wayo.

    6. Wewe ni kiongozi wa kikundi kinachoshiriki katika shughuli fulani ya kijamii. Chagua shughuli upendayo kisha utoe maelekezo kwa wanachama wa kikundi chako.

    7. Eleza manufaa ya kazi ya umuganda kwa jamii ya Wanyarwanda.

    8. Taja mambo mawili yanayoweza kukuonyesha kuwa tungo ni swali.

    9. Tunga maswali matano ukitumia viulizi mwafaka.

    10. Zipo aina ngapi za maneno ya Kiswahili? Zitaje.

    11. Yataje maneno kumi ya Kinyarwanda ambayo ni sawa na yale ya vihisishi vya Kiswahili.

    12. a) Nomino ni nini na huweza kuitwaje pia?

          b) Tunga sentensi tano sahihi ukitumia aina mbalimbali za nomino.

    13. Tambulisha vitenzi katika maneno yafuatayo:msamaha samehe hisi kihisishi rehema kurehemu rehemu fikira fikiri kilio lia

    14. Zieleze aina zote za vivumishi ambazo umejifunza hadi sasa. Tunga sentensi ukitumia kila mojawapo.

    15. Eleza tofauti iliyopo kati ya viunganishi na vihisishi.

    16. Andika aya moja kuhusu shughuli fulani ya kijamii. Tumia maneno yote saba ya Kiswahili katika aya hiyo kwa usahihi.

    17. Pigia kistari sentensi zilizopo katika wakati ujao na useme ikiwa ni hali yakinishi au kanushi.

              i) Siendi Kigali.

              ii) Wanaenda harusini.

              iii) Nitashiriki katika kazi zote kijijini.

              iv) Aliniita sikusikia.v) Hawatachelewa leo.

    18. Eleza umuhimu wa ushirikiano katika jamii.

    19. Taja mambo yote muhimu uliyojifunza katika sura hii.

    Sura 3: Matumizi ya lugha katika mazingira mbalimbali Faharasa