• Sura 3: Matumizi ya lugha katika mazingira mbalimbali

    Mada ndogo: Rejesta za mpira na burudani

    A   Rejesta mbalimbali nchini Rwanda 
    Rejesta au sajili ni lugha inayotumiwa mahali ama katika hali fulani na wala haiwezi
    kuhamishwa kutoka mazingira yale na kutumiwa katika mahali pengine. Lugha hizi
    hutofautiana kwa misingi ya msamiati, muundo wa sentensi na kadhalika. Kutokana
    na tofauti hizi, tunapata rejesta za aina mbalimbali. Baadhi ya rejesta hizo ni kama
    hizi zifuatazo.

    i) Rejesta ya mpira wa miguu
    Mpira wa miguu pia huitwa kandanda, soka au kambumbu. Huu ni mchezo
    maarufu sana hapa nchini Rwanda na duniani kote. Kwa mfano, mashindano ya
    kombe la dunia hutazamwa na watu wengi sana kote duniani. Mashindano hayo
    huandaliwa kila baada ya miaka minne. Pia, yapo mashindano ya Bara la Afrika,
    Kombe la Kagame, ligi mbalimbali na kadhalika.
    Baadhi ya watu hufuatilia mechi mbalimbali kupitia redio au televisheni. Wapo
    wanahabari ambao hutangaza mpira kupitia vyombo hivyo. Rejesta ya mchezo
    hujitokeza kupitia matangazo hayo.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tazameni mchoro huu. Jadilianeni kuhusu
    yaliyomo michoroni na myahusishe na mazingira yenu.

                                    

                    

    Soma kifungu hiki na ujibu maswali chini yake. 

    Matangazo ya kandanda sehemu I

    Hujambo msikilizaji. Karibu katika matangazo haya ya moja kwa moja ya kabumbu.
    Ni mimi mtangazaji wako, Teta. Huu ni mchuano wa fainali ya kuwania kombe la
    Fahari ya Rwanda kati ya shule ya wasichana ya Elimu Bora na Tusonge Mbele.
    Timu hizi mbili ni wapinzani sugu tangu jadi. Elimu Bora inajivunia historia nzuri
    kwa kushinda kombe hili mara kumi. Wao ndio bingwa tetezi. Tusonge Mbele
    imeshinda kombe hili mara tatu. Mwaka jana walitimuliwa katika nusu fainali.
    Katika awamu hii, wana rekodi ya kutoshindwa katika mechi zote hadi kufikia
    fainali. Je, rekodi hiyo itavunjwa na Elimu Bora?
    Naona timu zote mbili zikiingia uwanjani tayari kwa pambano. Kwa sababu ya muda
    sitataja majina ya wachezaji wote. Nitayataja kadri wanavyozidi kucheza. Kwa ufupi,
    kila timu ina golikipa mmoja. Elimu Bora wameweka wachezaji watatu katika safu
    ya ulinzi nao Tusonge wanawachezesha wachezaji wanne katika safu hiyo hiyo.
    Timu ya Elimu Bora wametia wachezaji watano katika kiungo cha kati nao Tusonge
    wanawachezesha wachezaji watatu. Elimu Bora wana washambulizi wawili nao
    Tusonge wana washambulizi watatu katika safu ya mashambulizi. Timu zote mbili
    zina wachezaji wa akiba watano. Refa mkuu anapuliza kipenga nao wasaidizi wake
    wawili wanakimbia pembeni mwa uwanja kuinua kijibendera. Mmoja anakimbia
    kushoto naye mwingine anakimbia kulia.
    Manahodha wa timu zote mbili wapo pale katikati ya uwanja kurusha sarafu ili
    kuamua timu inayoanzisha mpira. Mashabiki wa timu zote mbili wanaimba nyimbo
    za kushangilia timu zao. Nao makocha wao wamekaa pembeni mwa uwanja
    kushuhudia wasichana wao wakimenyana.
    Naam, refa anapuliza kipenga. Mpira unaanzishwa pale na Ikirezi na Uwamwiza
    wa timu ya Elimu Bora. Ikirezi anapiga pasi kwake Gwiza. Gwiza anapiga chenga.
    Anaangalia aupige wapi. Anapiga pasi safi kwake Umuliza. Umuliza na mpira.
    Umuliza anakwenda. Anapiga shoti ndefu kuelekea lango la Tusonge. Munyana
    anajibu kombora kwa kichwa. Mpira unakuwa mwingi na kutoka nje.
    Hee! Hee! Elimu Bora wameanza mchuano huu kwa kasi mno. Wanatafuta bao
    la mapema. Kamaliza anarusha ngoma ile kwake Muteteri. Muteteri anateleza
    na kuanguka. Refa anasema twendelee. Mutoni anachukua mpira. Tusonge
    wanafanya shambulizi la kujibu. Kamiza kwake Umuhire. Umuhire...Umuhire na
    mpira. Umuhire anakwenda. Umuhire anavuka mstari wa katikati. Anatoa pasi safi..
    go..go..ah! Kijibendera kipo juu. Tona amejenga kibanda katika ardhi ya wenyewe
    pasi ruhusa. Lo! Leo kuna kazi hapa.
    Msamiati
    kabumbu – mchezo wa mpira wa mguu/kandanda
    mchuano – mashindano baina ya timu mbili
    fainali – shindano la mwisho kabisa la kutafuta mshindi
    kuwania kombe – kushindania kombe/tuzo katika mchezo
    wapinzani – kikundi cha watu wanaoshindana na wengine
    bingwa tetezi – timu ambayo iliibuka mshindi/kuchukua kombe katika awamu
                             iliyopita ya shindano fulani.
    nusu fainali – mchezo unaotangulia fainali ambapo washindi hucheza katika fainali
    safu ya ulinzi – wachezaji ambao huzuia wapinzani kufunga bao
    kiungo cha kati – wacheza ambao hucheza sana katikati ya uwanja
    washambulizi – wachezaji ambao hucheza karibu na lango la wapinzani ili wafunge bao
    wachezaji wa akiba – wachezaji ambao hukaa nje ya uwanja na ambao huingizwandani kuchukua nafasi
                                        za wenzao waliopata jeraha au kuchoka
    kuinua kijibendera – kuonyesha kuwa mchezaji amekiuka kanuni za mchezo
    kurusha sarufi – kuamua timu gani inaanzisha mchezo kwa kurusha sarafu juu.
    anapiga pasi – mchezaji mmoja kumpigia mwenzake mpira
    anapiga chenga – kumhepa au kumpita mpinzani kwa mpira
    anapiga shoti – kupiga mpira kuelekea lango la mpinzani
    anajibu kombora – kuzuia mpira kwa kuupiga kuelekea upande wa pili
    mpira unakuwa mwingi – mpira kukosa kuthibitiwa na wachezaji
    mpira umetoka nje – mpira kuenda nje ya mstari wa nje uwanjani
    bao – mpira kuingia ndani ya lango
    shambulizi la kujibu – wachezaji kuelekeza mpira kwa kasi kuelekea lango la
                                        wapinzani punde tu baada ya mpira kuelekezwa
                                        langoni mwao
    kujenga kibanda/kuotea – kuvunja kanuni za ushambulizi kwa kushambulia
                                              ghafla nyuma ya mchezaji wa mwisho wa timu pinzani

    Zoezi

    1. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati uliotolewa maelezo hapo juu.
    2. a) Orodhesha na utoe maana ya maneno yote katika rejesta ya kandanda
            kifunguni humu lakini ambayo hayakuelezwa hapo juu.
        b) Tunga sentensi ukitumia msamiati uliotaja hapo juu.

    Kazi ya kikundi
    Wewe ni mtangazaji wa mpira wa miguu. Andika matangazo ya mchezo kati ya
    timu zozote mbili upendazo. Baada ya kuandika, jiunge na mwanafunzi mwenzako.
    Kila mmoja amsomee mwenzake matangazo yake.

    Sifa za rejesta ya mpira wa miguu
    Tazama matangazo ya mpira katika kifungu ulichosoma. Je, pana sifa gani katika
    rejesta hiyo?
    Zifuatazo ni orodha ya sifa za rejesta ya mpira wa miguu.
    i) Hujaa jadhba hasa baada ya mchezo kuanza,
    ii) Hujaa mazungumzo ya kuhamisha ndimi ambapo baadhi ya maneno ya
        Kiingereza na hata kienyeji hutumiwa,
    iii) Huwa na lugha ya kuchekesha na kuburudisha wanaoisikiliza,
    iv) Hujaa maoni mbalimbali kuhusu nani atashinda, nani mchezaji bora zaidi,
         na kadhalika,
    v) Huwepo kurudiarudia maneno kama vile majina ya wachezaji, dakika zilizopita,
        mabao yaliyofungwa na kadhalika,
    vi) Huwa na lugha ya kuibua hisia na kumfanya mtu kuingiwa na mahangaiko ya moyo,
    vii) Sentensi fupi fupi huweza kutumika pamoja na taswira ya kuchora picha kamili ya
         yanayotendeka.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwenzako mmoja. Someni kifungu hiki ili mbainishe rejesta ya mpira wa
    miguu na sifa zao.
    Matangazo ya kandanda sehemu II
    Mlinda lango wa Elimu Bora anaenda kupiga mpira wa madhambi. Anapiga kombora
    ndeeeefu na kutoka nje. Munyana anarusha ngozi iliyowambwa na kutengenezwa mpira.
    Kamiza anapiga chenga. Anatoa pasi kwake Usanase. Usanase anakwenda.
    Anaingia ndani ya kijisanduku. Hatari katika lango la Tusonge. Hatariiiii! Lo! Kayitesi
    ananawa mpira. Refa anasemaje. Naam, kipenga kinapulizwa. Refa anawapa Elimu
    Bora penalti. Shangwe na vifijo kutoka kwa mashabiki wa Elimu Bora. Kayitesi
    anaonyeshwa kadi ya manjano. Kayitesi amecheza rafu. Achunge asionyeshwe kadi
    nyingine ya manjano kwani atatolewa uwanjani.

    Haya! Tuone jinsi mambo yatakavyokuwa hapa. Refa anahesabu miguu kumi na
    miwili kutoka lango la Tusonge. Anaweka mpira chini. Ikirezi amesimama nyuma
    ya mpira ule tayari kupiga mkwaju wa penalti. Mlinda lango wa Tusonge, Kabatesi,
    amesimama mbele ya wavu. Refa anapuliza kipenga. Ikirezi anapiga hatua mbili
    tatu nyuma. Anapiga...go...goo... Nje! Heeee! Heee! Ikirezi ameshindwa kutikisa
    wavu. Alipiga kombora zito. Kabatesi akaruka na kuupiga mpira ule ukapitia juu ya
    mtambaa panya wa goli hadi nje. Kona! Kona ile inapigwa kutoka kushoto wa goli
    la Tusonge.
    Dakika zilizokatika hapa ni dakika kumi na tano. Bado dakika thelathini kipindi
    cha kwanza kikamilike. Tutakupa nafasi ya kuwasiliana nasi wakati wa mapumziko
    ambao utachukua dakika kumi na tano. Baadaye tutarudi hapa kwa kipindi cha
    pili ambacho kitachukua dakika nyingine arubaini na tano pamoja na dakika za
    nyongeza kutoka kwa refa mkuu. Ikiwa timu hizi zitatoka sare baada ya kipindi
    cha lala salama, dakika thelathini za ziada zitaongezwa. Ikiwa bado mshindi
    hatapatikana, watapiga penalti ya kuamua mshindi. Mshindi na mshinde sharti
    wapatikane leo kwa sababu hii ni fainali.
    Umuliza anapiga kona safi pale. Uwamwiza anakimbilia mpira ule. Anapiga kichwa..
    go..goo...goooooool! Mpenzi msikilizaji, hayawi hayawi huwa! Hatimaye Elimu
    Bora wamepata goli la kwanza. Uwamiza amecheka na wavu. Yeye ndiye mfungaji
    bora kufikia sasa. Mashabiki wote wa Elimu Bora na makochi wao wameacha viti
    vyao. Mashabiki wa Tusonge wameinamisha vichwa vyao. Wachezaji wa Tusonge
    wamepandwa na mori. Wamemzingira refa mkuu. Wanadai kuwa Uwamwiza
    alikuwa ameotea. Nahodha wao, Mutoni, ambaye ni beki wa kupanda na kushuka
    anammiminia refa maneno makali. Refa anatia mkono katika mfuko wa nyuma
    ya kaptura na kuchomoa kadi nyekundu. Salaale! Mutoni ameonyeshwa kadi
    nyekundu kwa kukosa adabu. Anasindikizwa nje ya uwanja. Timu ya Tusonge
    wamebaki na wachezaji kumi pekee. Je, itakuaje?

    i) Rejesta ya burudani
    Kama ujuavyo, burudani ni shughuli ifanywayo kwa ajili ya kuchangamsha na
    kufurahisha watu. Nayo mazingira ya namna hii yana msamiati wake ambao ndio
    lengo la sehemu hii.
    Tazama mchoro huu na ueleze mambo yanayojiri katika mchoro wenyewe.
                                                         
    Soma kifungu hiki cha habari na ujibu maswali chini yake.
    MFAWIDHI:Leo ni leo! Asemaye kesho....?
    WATU:        Ni mwongo!
    MFAWIDHI:Hapana! Asemaye kesho hayuko hapa. (Watu wanacheka) Leo showhii itakuwa ya kukata na shoka.
                       Kama huna shoka sijui utakata na nini.
    MTU I:        Tutakata na wembe.
    MFAWIDHI: Wembe utavunjika. (Watu wanacheka) Tuna wasanii wanaotajika ambao wamefika hapa kututumbuiza.
                        Mko tayari kuvunjika mbavu?
    WATU:        Ndiyooooo!
    MFAWIDHI: Shauri yenu. Mimi sitagharamia matibabu ya mbavu zitakazovunjika.
                        (Watu wanacheka) Mabibi na mabwana, sote tumkaribishe mwimbaji
                         katika jukwaa kwa makofi na vigelegeleeeeee!
                        (Watu wanapiga makofi. Mwimbaji anaingia.)
    MFAWIDHI: Kwenu mnanunua sindano kweli?
    MWIMBAJI: Hapana.
    MFAWIDHI: Ningeshangaa. Wewe ni sindano tayari. (Watu wanacheka)
    MWIMBAJI: Kwetu tuko wengi sana.
    MFAWIDHI: Mko wengi hadi mnapika chapati moja kisha mnapiga chapa.
                        (Kicheko). Kabla hatujaanza, ebu tupe historia fupi kuhusu safari
                        yako katika muziki.
    MWIMBAJI: Nilianza kwa kucheza kayamba kanisani.Hapo ndipo bendi ya
                        Umoja Jazz wakatambua kipawa changu. Wakanichukua kuwachezea
                         tarumbeta. Baada ya muda mfupi, nikaanza kujisimamia. Nikatunga
                        na kurekodi nyimbo zangu kama na kujichezea gitaa.
                        Hivi karibuni nitaunda bendi yangu.
    MFAWIDHI: Usikose kunijumuisha katika kwaya yako. Nitakuimbia soprano.
                        (Watu wanacheka) Leo umetuandalia nini?
    MWIMBAJI: Leo nitawatumbuiza kwa taarabu.
    MFAWIDHI: Haya haya! Wakati wa burudani umewadia. Kila mtu atafute nafasi
                        na mwandani wake. Muwe wawili wawili. Kama huna wako, eleka
                        jiwe. Kuna mawe mengi hapa. (Kicheko) Hakuna kukanyagana mguu.
                        (Watu wanacheka). Kama hujui kucheza miondoko ya taarabu,
                        kuja hapa mbele nikufunze. (Watu wanacheka). Haya twende kazi.
                        (Mwimbaji anaimba. Watu wanacheza.)

    Maelezo ya msamiati

    kukata na shoka – kufana
    kuvunjika mbavu – kucheka
    kayamba – ala ya muziki yenye umbo la kisanduku ambayo
                       hutengenezwa kwa matete na kutiwa punje kavu au
                       changarawe na hutikiswatikiswa wakati wa kuimba
    bendi – kikundi cha waimbaji wanaoimba pamoja
    tarumbeta – ala ya muziki ya kupuliza ambayo hutengenezwa kwa shaba na
                          hutoa sauti mbalimbali
    gitaa – ala ya muziki ambayo kwa kawaida huwa na nyuzi sita
    kwaya – uimbaji wa pamoja katika kikundi maalamu cha kuimba
    taarabu – muziki wenye mahadhi ya mwambao wa Afrika Mashariki
                    unaotumia mchanganyiko wa ala za Kiarabu, Kihindi na Kizungu

    Zoezi

    1. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati uliotolewa maelezo hapo juu.
    2. Toa mifano zaidi ya rejesta ya burudani. Andika msamiati wa kimsingi
         unaotumika katika rejesta hizo.
    3. Eleza sifa ya lugha iliyotumika kifunguni.

    Sifa za rejesta ya burudani

    Rejesta ya burudani huwa na sifa mbalimbali. Tazama baadhi ya sifa hizo katika orodha ifuatayo:
    i) Kuwa na maneno ya raha,
    ii) Huibua hali za kutuliza na kupumbaza mshiriki,
    iii) Kuwepo na uwezekano wa washirika wake kukesha hadi che huku
         wakijifurahisha kwa namna wapendavyo,
    iv) Kuwepo bendi ya muziki na wanasarakasi,
    v) Hali ya kusahau shida na mahangaiko aliyonayo mshiriki angalau kwa wakati mfupi tu.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Fanyeni mazoezi haya:
    1. Toeni mifano zaidi ya rejesta za burudani.
    2. Jadilianeni sifa za lugha inayotumika katika rejesta mlizotaja.
    3. Linganisheni na mtofautishe msamiati uliotumika katika rejesta hizo mbalimbali za burudani.

    Umuhimu wa michezo na burudani
    a) Umuhimu wa michezo
    Michezo ni shughuli za kushindana kati ya timu au watu tofauti tofauti ili kutafuta ushindi.
    Je,wewe unapenda kucheza mchezo gani?

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tazameni michoro iliyopo hapo chini na mtaje yanayotendeka.
      

    Soma kifungu na ujibu maswali yaliyoulizwa chini yake.
    Michezo ina umuhimu mkubwa kwetu kutokana na sababu mbalimbali. Kwanza,
    mchezo huimarisha afya yetu. Wachezaji hufanya mazoezi ya viungo. Mazoezi
    hayo ya viungo husaidia miili yetu kuyeyusha mafuta ya ziada, kunyosha misuli,
    kuimarisha mapigo ya moyo na kadhalika.
    Pili, michezo huleta umoja miongoni mwa jamii. Watu wanapoenda kutazama
    mchezo kama vile kandanda, hujumuika pamoja kushabikia timu fulani. Pale,
    wao hujenga urafiki. Mathalan, timu yetu ya taifa inapocheza, Wanyarwanda
    wote huja pamoja kuishabikia. Tunapofanya hivyo, tunajenga umoja wetu kama
    Wanyarwanda. Baadhi ya mashabiki pia husafiri pamoja na timu yetu ya taifa
    wanapocheza nje ya Rwanda. Safari kama hizo huchangia kujenga umoja na
    urafiki miongoni mwa mashabiki hao.
    Tatu, michezo huleta fahari. Mchezaji mashuhuri, timu bora na taifa bingwa katika
    michezo fulani hujulikana kwingi na kusifiwa. Sifa hizi huinua hadhi ya mtu binafsi,
    timu na taifa kwa jumla. Nchi inayosifika kwa mchezo au michezo fulani huwa
    katika hali nzuri ya kuvutia watalii.
    Michezo huleta pato la kuridhisha. Pato hili huwa kwa mchezaji binafsi, kwa
    kilabu na hata kwa taifa. Wachezaji wa vilabu mbalimbali na timu ya taifa hulipwa
    mshahara na marupurupu mengi. Baadhi ya wachezaji hawa hasa wanaochezea
    vilabu vya kimataifa ni matajiri wa kutajika kutokana na michezo.
    Vilabu mbalimbali pia hunufaika pakubwa. Wao hukusanya pesa nyingi kutokana na
    mauzo ya tikiti, matangazo ya biashara katika viwanja vyao, kuuzwa kwa wachezaji
    wao kwa vilabu vinginevyo na kadhalika. Taifa zima pia hunufaika kutokana na
    ushuru mbalimbali unaolipwa na wachezaji pamoja na vilabu husika.
    Michezo huburudisha na kutuliza roho. Baada ya shughuli nyingi za siku au wiki,
    mashabiki hujipumzisha akili kwa kutazama michezo wanayopenda. Pia, kushabikia
    timu na kusherehekea ushindi huleta uchangamfu.

    Maswali
    1. Taja umuhimu wa michezo kulingana na kifungu hiki.
    2. Michezo ni njia bora kuu ya kuimarisha afya yetu. Tetea kauli hii.
    3. Eleza jinsi michezo huleta ushirikiano kati yetu.
    4. Jadilianeni kuhusu jinsi mnavyoweza kutumia michezo kukuza ushirikiano,
         kuboresha afya na kutatua matatizo yanayokumba jamii yenu.

    b) Umuhimu wa burudani
    Tazama michoro iliyopo hapa chini. Je, mambo gani yanafanyika?

    Soma kifungu kifuatacho na ujibu maswali chini yake.
    Kama ilivyo michezo, burudani ina umuhimu mkubwa kwa jamii. Kwanza, burudani
    hukuza umoja na utangamano miongoni mwa wanajamii. Watu wanapokuja pamoja
    kucheza densi, kutazama sarakasi, sinema na kadhalika, wao hujenga urafiki na
    uhusiano mwema miongoni mwao.
    Vilevile, burudani hukuza ushirikiano. Watu wanaoshiriki katika kuwaburudisha
    wanajamii huja pamoja ili kuafikia malengo hayo. Mfano, bendi au kwaya
    hushirikisha watu mbalimbali. Ushirikiano huu hukuza umoja miongoni mwa wahusika wote.
    Burudani pia hukuza afya yetu. Tunaposhiriki katika densi, viungo vya miili
    yetu hupata mazoezi muhimu ambayo huboresha afya yetu. Vilevile, akili zetu
    huchangamka kupitia burudani hasa baada ya kazi nyingi za siku au msiba.
    Uchangamfu huu huleta utulivu na liwazo katika akili zetu. Pia, hutuepushia
    huzuni ambayo ni hatari kwa afya yetu.
    Burudani hudumisha utamaduni. Hapa, chukua mfano wa ngoma zetu maarufu.
    Unapata kuwa ngoma hizo zilichezwa enzi za kale. Kupitia nyimbo hizo, tunafahamu
    hali ya maisha katika enzi hizo za kale. Kwa hivyo, hii ni njia moja ya
    kuhakikisha kuwa utamaduni wetu haupotelei mbali.
    Burudani pia ni chanzo cha ajira na pato. Watu wengi wameajiriwa kupitia burudani
    kama vile bendi, sarakasi, mchezo wa kuigiza na kadhalika. Burudani pia huweza
    kumletea mtu sifa nzuri. Kwa mfano, wapo waimbaji, waigizaji, wanasarakasi
    na kadhalika ambao wanajulikana kote ulimwenguni na kupendwa na wengi.

    Maswali
    1. Kwa maneno yako mwenyewe, eleza maana ya burudani.
    2. Je, ni jambo lipi unaloliona kuwa ni la muhimu zaidi kuhusu burudani? Kwa nini?
    3. Andika sifa ambazo zinafanya michezo na burudani kuwa sawa
    .4. Taja umuhimu wa burudani ambao haukutajwa kifunguni humu.


    Kazi ya wanafunzi wawili wawili

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Jadilianeni kuhusu umuhimu wa burudani kiafya na kiushirikiano

    iii) Rejesta ya hotelini

    Hoteli ni nyumba ambamo vyakula na vinywaji huuzwa. Vyumba vya kulalia pia
    hupatikana hotelini. Rejesta ya hoteli hutumika katika mazingira haya.

    Jiunge na mwenzako na msome kifungu kifuatacho.



    NDOLI:   Karibuni katika hoteli yetu! Jina langu ni Ndoli na mimi ndiye mhudumu.
    ITUZE:    Asante sana kwa makaribisho yenu.
    GANZA: Tunashukuru. Mna nini leo?
    NDOLI:  Tuna vyakula vingi kwenye ankra. Tuna tilapia, matoke, ugali, kisamvu na mizuzu.
                   Pia tuna vinywaji vingi. Tuna uji, chai na kahawa.
    GANZA: Niletee matoke sahani moja.
    ITUZE: Mimi juisi ya baridi. Nitaitisha vingine baadaye.
                 (Ndoli anaondoka na kurudi na vyakula vilivyoagizwa)
    NDOLI: Karibuni. Mjihisi nyumbani.
    GANZA: Asante. Nina swali kabla hujaenda. Sisi ni wageni hapa Kigali. Jioni tutahitaji mahali pa kulala.
                  Je, tunaweza kupata vyumba vya kukaa?
    NDOLI: Bila shaka vyumba mtapata. Vyumba vyetu vyote ni vya hali ya juu kwa wageni kama nyinyi.
                 Vyumba hivyo vina maji moto, televisheni nahuduma za bure za mtandao.
                 Pia, tunawapa wageni wetu kiamsha kinywa, chamcha na chajio.
    GANZA: Mna huduma gani zaidi?
    NDOLI: Tuna mabwawa ambapo wageni wetu huogelea. Pia, tuna ukumbi wa mazoezi ya viungo.
                  Mtakaa kwa muda gani?GANZA: Tutakaa kwa siku tatu. Tunahudhuria kongamano kuhusu
                 mbinu mpya za kilimo. Baadaye tutazuru mbuga ya wanyama ya Akagera.
    NDOLI: Karibuni tena.GANZA na ITUZE: Asante sana.

    Maswali

    1. Eleza maana ya msamiati mbalimbali wa hoteli jinsi ulivyotumika kifunguni.
    2. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati uliotaja hapo juu.
    3. Je, pana umuhimu gani kwa mhudumu kuonyesha adabu na heshima
        anapozungumza na wateja katika hoteli?

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Fanyeni utafiti kuhusu lugha gani inayotumika
    katika mazingira ya hoteli nchini Rwanda. Wasilisheni matokeo yenu mbele ya darasa.

    Sifa za rejesta ya hotelini
    Rejesta ya hotelini huwa na sifa zifuatazo:
    i) Kuwepo kwa lugha ya vyakula mbalimbali,
    ii) Kupatikana kwa msamiati wa vinywaji vingi,
    iii) Wahudumu kuzungumza na wateja kwa unyenyekevu,
    iv) Kupatikana maneno ya huduma mbalimbali,
    v) Lugha ya mkato hutumika.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Fanyeni maigizo ya mazungumzo ya
    hotelini kati ya mhudumu na wateja. Zingatieni sifa mbalimbali za rejesta ya hoteli.

    iv) Rejesta ya mahakamani
    Mahakamani au kortini ni mahali pa kusikilizwa na kuamuliwa mashtaka na kesi mbalimbali.
    Yeyote anayefanyiwa mabaya ana ruhusa ya kumshtaki mahakamani aliyemfanyia ubaya huo.
    Je, umewahi kuhudhuria vikao vya mahakama?

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tazameni mchoro uliopo hapa chini.
    Jadilianeni kuhusu watu waliopo kwenye mchoro na shughuli zinazoendelea.
    Linganisheni yaliyomo humo na yale mnayofahamu kuhusu mahakama.

    Soma kifungu kifuatacho na ujibu maswali chini yake.

    Mahakamani sehemu I
    KARANI: Shughuli za korti hii zimeanza. Hakimu Ganza ndiye mwamuzi
                    katika kesi hii. Ketini tafadhali. (watu wanakaa)
    HAKIMU: Ninatangaza rasmi kusikilizwa kwa kesi ya Thierry Ngabo dhidi ya
                    Jane Usanase. Je, pande zote mko tayari?
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Tayari kwa niaba ya upande wa mashtaka,Mheshimiwa.
    WAKILI: Tayari kwa niaba ya mshtakiwa, Mheshimiwa.
    HAKIMU: Thierry Ngabo?
    MSHTAKIWA: Naam, mheshimiwa. HAKIMU: Natumai unajua haki zako.
                            Una haki ya kuwakilishwa na wakili mbele ya mahakama hii.
                            Una haki ya kunyamaza kimya au kujibu mashtaka. Pia,
                            una haki ya kukata rufaa ikiwa hutaridhika na uamuzi wa mahakama.
                            Je, ni kweli kuwa unajua haki hizi?
    MSHTAKIWA: Naam.
    HAKIMU: Unashtakiwa kwa mashtaka mawili. Katika shtaka la kwanza,
                    unashtakiwa kuwa mnamo usiku wa tarehe ishirini na tisa, mwezi
                    wa kumi na moja mwaka wa elfu mbili kumi na sita ulipatikana
                    ukiendesha gari la kibinafsi lenye nambari ya usajili ASA000R
                     katika barabara kuu ya kutoka Ngoma kuelekea Kirehe bila idhini
                     ya mmiliki wa gari hilo. Gari hilo liliripotiwa kupotea mnamo
                     tarehe ishirini na nane, mwezi wa kumi na moja mwaka wa elfu
                      mbili kumi na sita. Katika shtaka la pili, unashtakiwa kwa kukwepa
                      vizuizi vya polisi na kutumia njia mbadala polisi walipojaribu
                        kukusimamisha. Unakubali au unakataa shtaka la kwanza?
    MSHTAKIWA: Ninakataa.
    HAKIMU: Unakubali au unakataa shtaka la pili?
    MSHTAKIWA: Ninakataa.
    HAKIMU: Upande wa mashtaka.
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Asante Mheshimiwa. Nina ushahidi wa kutosha kuthibitisha
                                                    kuwa mshukiwa ana hatia kwa mashtaka mawili yaliyopo mbele
                                                    ya mahakama. Mheshimiwa, ushahidi utaonyesha kuwa gari
                                                    ASA 000 R liliibwa mnano tarehe ishirini na nane, mwezi
                                                    wa kumi na moja mwaka wa elfu mbili kumi na sita, usiku. Siku
                                                    moja baadaye, mshukiwa alipatikana akiendesha gari hilo.
                                                    Mheshimiwa, mshukiwa alishindwa kutoa idhini ya mwenyegari na stakabadhi za kumiliki
                                                    gari hili. Alama za vidole vya mshukiwa pia vilipatikana katika funguo bandia zilizotu
                                                    mikakatika wizi wa gari husika. Mheshimiwa, kwa mshukiwa kujaribukukwepa
                                                    vizuizi vya polisi ni ithibati tosha kuwa aliiba gari hili.
                                                    (Wakili anaomba nafasi ya kuchangia. Hakimu anampa nafasi.)
    WAKILI: Mheshimiwa, ni haki kwa Kiongozi wa mashtaka kudai kuwamshukiwa ana hatia bila kuthibitisha?
                   Mheshimiwa, kwa mujibu wa sheria kuhusu haki za mshtakiwa, mteja wangu hana hati
                   hadi mahakama hii itakapoamua kesi yake hii. Wakati wa kesi hii, utajua ukweli wa mambo.
                   Ngabo alikuwa akiendesha gari ambalo liliibwa na mtu mwingine. Ngabo alipogundua kuwa
                   gari limeibwa, alikuwa mbioni kurejesha gari hilo. Alikuwa amempigia polisi simu katika kituo
                   cha polisi mjini Kerehe kuwa gari analoendesha limeibwa. Hakuwa na nia ya kukwepa vizuizi vya polisi.
                  Alikuwa na nia ya kukwepa mlolongo mrefu wa magari ili afike mjini Kerehe mapema iwezekanavyo.
                  Mheshimiwa, mteja wangu ni mtu asiyekuwa na rekodi yoyoteya wizi.
                  Ndio maana alipewa dhamana bila kuhitajika mdhamini.
                  Kwa hivyo mteja wangu hana hatia.

    Msamiati
    korti – mahali ambapo kesi na mashtaka mbalimbali husikilizwa na kuamuliwa.
               Pia huitwa mahakama.
    hakimu – mtaalamu wa sheria anayeajiriwa kusikiliza mashtaka kortini na kutoa maamuzi
    kesi – mashtaka yanayosikilizwa mahakamani
    mshtakiwa – mtu anayefikishwa kortini kwa kudaiwa kufanya kosa
    mheshimiwa – jina la heshima ambalo watu hutumia kortini kumrejelea hakimu
    kukata rufaa – mshtakiwa kukataa hukumu aliyopewa kwa kuomba mahakama
                            ya juu isikilize tena kesi yake au ipunguze adhabu aliyopewa
    unashtakiwa kwa mashtaka mawili – makosa mawili yameletwa mbele ya mahakama dhidi yako.
    ushahidi – thibitisho kuwa jambo fulani lilifanyika au halikufanyika

    Maswali
    1. Bainisha msamiati zaidi wa kimsingi katika rejesta ya mahakama katika kifungu ulichosoma.
    2. Eleza maana ya kila msamiati na utungie sentensi sahihi.

    Sifa za sajili ya mahakamani
    Baadhi ya sifa zinazoweza kubainisha rejesta ya mahakamani ni:
    i) Matumizi ya lugha ya adabu,
    ii) Kuwepo tafsiri na fasiri ya yanayosemwa hasa ambapo mshtaki ama
        mshtakiwa haijui lugha rasmi ya mahakamani,
    iii) Mawakili hutumia lugha iliyojaa msamiati wa sheria,
    iv) Kunukuliwa kwa vifungu mbalimbali vya katiba au sheria,
    v) Kukosekana kupinga uamuzi wa korti papo kwa papo bali kupinga huja baadaye,
    vi) Kuwepo msamiati wa Kilatini.

    Soma mazungumzo haya ya mahakamani na ujibu maswali.
    Mahakamani sehemu II

    HAKIMU: Upande wa mashtaka, mna mashahidi?
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Naam, Mheshimiwa.
    HAKIMU: Walete kizimbani.
                    (Askari analeta shahidi wa kwanzaAnasimama kwenye kizimba.
                    Karani wa korti anaelekea alipo shahidi akiwa na Biblia na Kurani.)
    KARANI: Unaitwa nani?
    SHAHIDI I: Jane Usanase.
    KARANI: Uko mbele ya mahakama. Mahakama inataka kujua ukweli.
                    Usimwogope mshukiwa wala mtu yeyote. Ujikaze ili korti ijue
                    ukweli wa mambo. Utakula kiapo kwa Biblia au Kurani?
    SHAHIDI I: Biblia. (Jane anainua Biblia kwa mkono kwa kulia)
    KARANI: Uyarudie maneno haya kwa sauti. Mimi Jane Usanase.
    SHAHIDI I: Mimi Jane Usanase.
    KARANI: Ninaapa kwamba yale ambayo nitasema mbele ya korti hii ni ukweli.
    SHAHIDI I: Ninaapa kwamba yale ambayo nitasema mbele ya korti hii ni ukweli.
    KARANI: Ewe Mungu nisaidie.
    SHAHIDI I: Ewe Mungu nisaidie. (Karani anakaa. Kiongozi wa Mashtaka anaamka
                       na kuelekea alipo shahidi.)
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Unafanya kazi wapi?
    SHAHIDI I: Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kerehe.
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Unatumia mbinu gani za usafiri ukienda kazini?
    SHAHIDI I: Gari langu la kibinafsi.
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Gari hilo lilikuwa wapi mnamo usiku wa tarehe 29/11/2016?

    SHAHIDI: Nilikuwa nimeliegesha mbele ya hoteli ya Starehe mjini Kirehe.
    KIONGOZI WA MASHTAKA: Nambari ya usajili wa gari hilo ni A...
    WAKILI: (Baada ya kumwomba Hakimu nafasi ya kuongea) Mheshimiwa,
                   nihaki kwa kiongozi wa mashtaka kumwelekeza shahidi katika kutoa
                   ushahidi wake? Gari likiwa lake, mbona asiseme nambari yake
                   ya usajili bila kuambiwa?
    HAKIMU: Kiongozi wa mashtaka, shahidi anajua nambari ya usajili wa gari lake.
                    Mwache aitaje.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako na mfanye mazoezi haya:
    i) Jadilianeni kuhusu sifa za rejesta ya mahakamani.
       Rejeleeni vifungu mlivyopewa na ikiwezekana msikilize rekodi
       za matukio mahakamani au kuhudhuria vikao vya mahakama.
    ii) Kamilisheni kesi iliyopo mahakamani kuanzia ilipofikia katika kifungu cha pili kwa kuigiza.

    v) Rejesta ya bungeni
    Bunge ni baraza la taifa linalotunga sheria na lenye wajumbe waliochaguliwa na
    wananchi kwa kupigiwa kura ama kwa kuteuliwa na rais.
    Soma kifungu kifuatacho na ujibu maswali chini yake.
       



    KARERA: Jina langu ni Karera.
    RUSARO: Na mimi ninaitwa Rusaro.
    RURANGIRWA: Nami ninaitwa Rurangirwa.
    KARERA: Tupo hapa mbele yenu, wanadarasa wenzetu, kukuelezeni
                      mengi kuhusu bunge letu ama baraza letu la taifa. Mambo haya
                      tumeyapata kupitia kwa utafiti wa kina ambao tumekuwa tukiufanya.
    RUSARO: Wabunge wetu huwawakilisha watu waliowachagua amavikundi fulani
                      fulani vya raia wa jamhuri yetu.
    RURANGIRWA: Namo bungeni, yamo mambo mengi unayostahili kuyajua.
                              Mathalan, mwenye mamlaka ya kuongoza, kuamuru au kuzuia
                             shughuli bungeni ni spika ambaye husaidiwa na naibu wa spika.
    RUSARO: Spika ana mamlaka ya kuamua ni mbunge gani atazungumza,
                     atazungumzaje na kwa muda gani na kadhalika. Hapana lolote
                     linaloweza kuendelea bungeni bila yeye kuliruhusu.
    KARERA: Hali kadhalika, yamo mambo mengi mengineyo yanayopatikana bungeni.
                     Mambo hayo ni kama vile rais, makamuwa rais, sheria, kutunga sheria,
                     hoja, upinzani, kura, uchaguzi, wakala, eneo la ubunge, piga kura,
                     mjumbe mteule,  mjumbe wakilishi na kadhalika
    RUSARO: Tukianza na rais tunapata kuwa hakuna bunge bila kuwepo rais.
                      Yeye huhitaji kutawala serikali na nchi nzima kwa mujibu wa sheria.
    RURANGIRWA: Nazo sheria hizo ni lazima zitungwe na bunge. Kwa hivyo,
                               kila nchi huhitajika kutawaliwa na rais kwa sheria zilizotungwa
                               na bunge.Naye makamu wa rais ni yule anayemsaidia rais kutawala nchi.
                               Lakini, je, sheria nazo ni nini?
    RUSARO: Sheria ni kanuni za kutawalia nchi na ambazo, kama ilivyotajwa awali,
                       hutungwa na bunge. Wabunge huwasilisha hoja bungeni na zikajadiliwa.
                       Baadhi yazo hupitishwa kuwa sheria baada ya kuidhinishwa na rais.
                       Lakini zile hoja zinazopingwa na upinzani na kukataliwa haziwi sheria.
                       Nazo zile anazozikataa rais hurudishwa bungeni ama kurekebishwa
                       ama kutupiliwa mbali.
    KARERA: Nao takriban wabunge wote hupigiwa kura ili kuingia bungeni.
                      Wafikapo huko huwa ni mawakala wa wale waliowachagua kutoka
                      maeneo yao ya bunge na huhitajika kufanya juu chini ili kuwainulia
                      hali yao ya kimaisha.
    RURANGIRWA: Hata hivyo, huwepo wajumbe wateule ambao huteuliwa na rais
                                ili kuwakilisha sehemu fulani fulani. Kwa mfano, panaweza kuwepo
                                mbuge mteule anayewawakilisha masilahi ya wanawake ama vijana.
    KARERA: Isitoshe, ipo kura ya kutokuwa na imani na mtu ama tume fulani.
                      Inaweza kutokea kwamba kiongozi fulani anatuhumiwa kukosea.
                      Basi, bunge linaweza kupitisha kura ya kutokuwa na imani naye na akafutwa kazi.
                      Katika hali kama hii, mara nyingine huteuliwa tume ya kuchunguza ukweli wa tuhuma
                      kabla ya uamuzi kama huu kutolewa.

    Zoezi

    Bainisha msamiati maalumu wa bungeni kutoka katika kifungu huku ukiutungia sentensi sahihi.

    Sifa za rejesta ya bungeni
    Rejesta ya bungeni kama rejesta yoyote ile huwa na sifa zake. Ifuatayo ni orodha ya
    baadhi ya sifa hizo:
    i) Kumrejelea spika kila wakati kwa heshima,
    ii) Matumizi ya maneno yenye adabu,
    iii) Kutokuwepo ruhusa ya kumshtaki mzungumzaji kwa maneno aliyotamka,
    iv) Kuwepo kwa lugha ya kupiga kura kwa hoja fulani,
    v) Kuwepo kwa mtindo fulani wa kuandika ama kuwasilisha hoja,
    vi) Kuwepo kwa utaratibu wa kuzungumza,
    vii) Kurejelewa kwa vifungu vya sheria mbalimbali za bunge na katiba kila wakati,
    viii)Kutumika kwa lugha ya utafiti.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Sokoni ni mahali penye mkusanyiko wa watu wanaouza na kununua bidhaa mbalimbali.
    Wauzaji wengi huuza bidhaa zao kwa rejareja, kwenye kibanda au katika maduka.
    Baadhi ya masoko hutenga siku moja au mbili kama siku maalumu za soko kila wiki.
    Siku kama hiyo ya soko huitwa chete. Masoko mengine huendesha shughuli zake kila
    siku. Bidhaa nyingi huuzwa sokoni.

    Soma kifungu hiki ili kujifunza mengi kuhusu rejesta ya sokoni.
    (Umuhire anaingia sokoni. Sauti za wauzaji mbalimbali zinasikika.)

    SAUTI: Mia bei! Mia bei...Karibu mteja..Ni za leo...ni za leo...bei rahisi...bei ya
                 jioni...bei ya hasara...karibu, chagua...chagua...beba nguo na hamsini...
    MWUZAJI: (Umuhire anaingia katika kioski kimoja.) Karibu mteja wangu! Bei
                        rahisi kwa bidhaa nzuri! Karibu katika kibanda changu! Karibu
                        uchague bidhaa utakazo. Leo nina mboga safi safi, matunda
                        matamu matamu na nyanya kubwa kubwa.
    UMUHIRE: Ahaa! Leo sina pesa ya matunda. Nitanunua siku nyingine.
                      Una kitunguu?                              
    MWUZAJI: Siwezi kukosa                              
                       vitunguu, bi mdogo.                     
                        Ndivyo hivi hapa.
    UMUHIRE: Je, kifungu kimoja ni
                       pesa ngapi?
    MWUZAJI: Hicho ni bei rahisi sana.
                       Kila kifungu ni faranga kumi tu.
                       Nikufungie ngapi?
    UMUHIRE: Aa! Hiyo ni bei ghali mno.
                       Tafadhali, niuzie vifungu
                        vitano kwa faranga arubaini.
    MWUZAJI: Hapo umenizamisha, bi mdogo.
                       Sitapata faida yoyote. Bei ni hiyo tu.
    UMUHIRE: Wewe nawe!
                       Faida utapata  kwa       
                       bidhaa nyingine.
                       Hutaki nirudi tena?
    MWUZAJI: Ninataka urudi kila mara. Basi ongeza faranga tano nikufungie.
    UMUHIRE: Jamani! Unataka tule mboga bila chumvi?
                        Hiyo faranga tano ni ya chumvi.
    MWUZAJI: (Anacheka) Nami hutaki nile chamcha?
                        Hiyo faranga tano ni ya kujinunulia chakula.
                        Unataka babu yako afe kwa njaa?
    UMUHIRE: Haya! Chukua faranga zako arubaini na tano.
    MWUZAJI: Asante bi mdogo. Chukua bidhaa zako.
    UMUHIRE: Asante.
    MWUZAJI: Karibu tena. Mbona hununui mboga pia?
    UMUHIRE: Mboga ninazo katika shamba langu nyumbani.
    MWUZAJI: Pongezi sana. Una aina gani ya mboga?
    UMUHIRE: Nina sukumawiki.
    MWUZAJI: Unaweza kuniuzia gunia moja la sukumawiki?
    UMUHIRE: Sawa. Nitakuletea siku ya Jumamosi. Nyama inauzwa wapi?
    MWUZAJI: Nyama inauzwa kwenye buchari. Buchari ipo nyuma ya kibanda hiki.
    UMUHIRE: Nimeshukuru.: Jamani! Unataka tule mboga bila chumvi? Hiyo
                       faranga tano ni ya chumvi.
    MWUZAJI: (Anacheka) Nami hutaki nile chamcha? Hiyo faranga tano ni ya
                       kujinunulia chakula. Unataka babu yako afe kwa njaa?
    UMUHIRE: Haya! Chukua faranga zako arubaini na tano.
    MWUZAJI: Asante bi mdogo. Chukua bidhaa zako.
    UMUHIRE: Asante.
    MWUZAJI: Karibu tena. Mbona hununui mboga pia?
    UMUHIRE: Mboga ninazo katika shamba langu nyumbani.
    MWUZAJI: Pongezi sana. Una aina gani ya mboga?
    UMUHIRE: Nina sukumawiki.
    MWUZAJI: Unaweza kuniuzia gunia moja la sukumawiki?
    UMUHIRE: Sawa. Nitakuletea siku ya Jumamosi. Nyama inauzwa wapi?
    MWUZAJI: Nyama inauzwa kwenye buchari. Buchari ipo nyuma ya kibanda hiki.
    UMUHIRE: Nimeshukuru.

    Zoezi

    1. Eleza maana ya maneno yaliyokolezewa wino katika kifungu.
    2. Tunga sentensi ukitumia msamiati ulioorodhesha hapo juu.

    Sifa za rejesta ya sokoni
    Sifa zinazobainisha rejesta ya sokoni ni:
    i) Lugha ya kurudiarudia maneno hutumika huku bidhaa zikinadiwa,
    ii) Lugha ya kuwavutia wateja huweza kutumiwa,
    iii) Hutumika lugha isiyo rasmi na sarufi hukosa kufuatwa,
    iv) Kiimbo cha wauza bidhaa hutumika kama vile kuzungumza kwa upole kwa
         wazee na kutumia lugha ya kusifu kwa wateja wanaonekana tajiri,
    v) Lugha ya kununua na kuuza hutumiwa kama vile: panda bei, shuka bei

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Igizeni mazungumzo kati ya mwuzaji na mnunuzi.
    Zingatieni sifa za rejesta ya sokoni.

    vii) Rejesta ya kanisani
    Kanisa ni jengo ama mahali panapotumiwa na Wakristo kufanyia ibada.
    Ama pia neno hili lina maana ya Jumuiya ya Wakristo.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wenzako watano na mjadili mambo mnayoyaona katika mchoro ufuatao.


    Sasa someni kifungu kifuatacho na halafu mjibu maswali yaliyoulizwa.

    Mambo yote yanayohusu kanisa na imani ya mtu ni mambo magumu sana maishani mwetu.
    Amri Kumi za Mungu pamoja na amri nyingine zozote zinazohusu dini ya kweli,
    huhitaji mwanadamu kukaa katika mema na haki mbele ya Mwenyezi Mungu.
    Hayo ndiyo masharti ya Neno ama Biblia. Mitume na malaika wa Mungu
    waliwajia mara kwa mara waumini walioamini katika dini kuwakumbusha haya.
    Nayo misahafu dini mbalimbali za haki huyasisitiza yaya haya.
    Sasa ugumu huja katika kuyatekeleza.
    Hata hivyo, kupo kutubu. Huku kutubu ni njia ya pekee ya kuondoa ugumu huo.
    Kila atendaye dhambi mbele ya Mola ana ruhusa ya kutubu. Makasisi, mapadri,
    wachungaji, maaskofu, maaskofu wakuu pamoja na viongozi wengine makanisani
    wana jukumu la kuhakikisha kuwa waumini wao hutubu na kumrudia Manani.
    Nako kutubu huko kunaweza kufanywa wakati wa ibada wanapokuwa wanamwabudu
    Muumba ama wakati mwingine wowote. Kunaweza pia kufanywa kupitia kwa sala.
    katika haya yote, ni sharti ikumbukwe kwamba mwovu shetani hapumziki mpaka
    aone kuwa binadamu wengi ama wote wamo katika dhambi. Binadamu huyo akitubu,
    malaika mbinguni wanafurahi sana. Lakini shetani anatafuta njia nzuri
    nzuri za kumfanya mwanadamu yuyo huyo arudi dhambini tena.
    Mbinu zake nyingi huwa za msingi wa raha. Anajua kuwa binadamu ni mpenda raha.
    Hata hivyo, lipo Neno linalovunjavunja juhudi kama hizo.
    Kanisa huhubiri habari za jahanamu, kuangamia motoni, kuingia mbinguni, njia
    pana, njia nyembambana, msalaba wa Yesu, Mwokozi Yesu, Utatu wa Uungu, na
    hata siku ya kiama. Jahanamu ama ahera ni pahali ambapo inaaminika roho za wale
    waliokufa huenda kungoja siku ya kiama ambayo itakuwa siku ya kutolewa
    hukumu na Mungu Muumba. Swali kuu siku hiyo litakuwa, Umefanya nini na Neno langu?
    Wale ambao hawatajibu vilivyo watatupwa motoni na wale ambao watajibu vilivyo wataingia mbinguni.
    Jambo jingine kanisani ni msalaba. Yesu Kristo alisulubishwa kwenye msalaba
    ili amfie mwanadamu apate kuokolewa na damu yake. Kwa hiyo, msalaba ni
    ukumbusho kwamba tayari mwanadamu ameokolewa na analohitaji kufanya ni kuungama dhambi zake.
    Jambo jingine ni kwamba maeneo mbalimbali ya kuabudia huwa na maneno
    wanayochukulia kuwa yanawawezesha kuwasiliana vilivyo na Mungu.
    Maeneo hayo ni kama vile kanisani, msikitini, hekaluni na kwingineko kukiwa pamoja na barabarani.

    Zoezi
    Jiunge na mwenzako. Jadilianeni maana ya maneno yaliyokolezewa wino na
    msamiati zaidi unaotumiwa kanisani na msikitini.

    Sifa za rejesta ya kanisani
    Baadhi ya sifa za rejesta ya kanisani ni kama vile:
    i) Huwepo na pahali pa kumwabudia Mungu,
    ii) Katika baadhi ya dini, hutumika msamiati wa wale walioileta dini k.v. Kiingereza,
    iii) Huwezekana kuwepo mkalimani wa kutafsiri na kufasiri,
    iv) Baadhi ya wahubiri huanza kuzungumza kwa kasi wanapopandwa na jadhba,
    v) Sadaka hupewa majina mbalimbali na huwa ni sharti zitolewe,
    vi) Waumini hawana ruhusa ya kuulizia wasilolielewa wakati mhubiri anapokuwa anahubiri,
    vii) Ni sharti msamiati wa kidini utumiwe badala ya ule wa lugha ya kawaida,
    viii)Huwepo kwaya ama mwimbaji, ix) Vifungu mbalimbali vya Biblia hunukuliwa.

    viii) Rejesta ya sarufi ya Kiswahili
    Sarufi ni kanuni za lugha zitumiwazo ili kupata ufasaha katika lugha. Kila lugha
    huwa na sarufi yake. Hivyo basi, ipo sarufi ya Kiswahili ambayo ina rejesta yake.





    Someni kifungu kifuatacho ili kujifunza maneno zaidi ya sajili hii ya lugha.

    Fikiria ingekuwaje kama hatungekuwa na lugha? Hata ishara mbalimbali zina msingi wa lugha.
    Ama kwa kweli, mambo mengi yangalikwama kama hapangekuwa na lugha.
    Rejesta ya lugha ni muhimu kama lugha ilivyo kwa kuwa mambo hayo mawili
    ni jambo moja tu. Katika rejesta ya sarufi mna maneno kama vile sajili, sarufi,
    Kiswahili, sentensi, lafudhi, alfabeti, vitenzi, mnyambuliko, maandishi, majina,
    namna za majina, vivumishi, vielezi, viwakilishi, viunganishi, vihusishi, vihisishi,
    aya, kuakifisha na kadhalika.
    Ukija kuangalia maana ya maneno haya, unapata kuwa sajili ni rejesta kama
    ilivyoelezwa hapo awali lakini sarufi ni sheria ziongozazo lugha fulani. Nacho
    Kiswahili ni lugha izungumzwayo na Waswahili lakini sentensi ni tungo
    ijitoshelezayo na ambayo huhusisha mtendaji na kitendo. Nayo lafudhi au lafidhi
    ni namna maneno yanavyotamkwa ilhali alfabeti ni herufi za lugha ambazo
    zimepangwa kwa utaratibu maalumu.
    Navyo vitenzi ni maneno yakuambiayo cha kufanya na mnyambuliko ni namna
    vitenzi hivyo hujigeuzageuza ili kuleta maana ihitajikanayo. Maandishi nayo ni
    kuwakilisha sauti kwenye karatasi kwa kutumia kalamu ilhali majina ni neno la
    kumtaja mtu, kitu au jambo.
    Namna za majina ni vikundi vya majina yanayochukua sifa fulani inayoyasawazisha.
    Vivumishi ni maneno yaongezeayo majina maana na pia kujiongezea maana.
    Vielezi navyoni maneno yaongezeayo vitenzi maana ilhali viwakilishi ni maneno a
    ma viungo vya maneno vinavyosimamia majina.
    itoshe, kuna viunganishi, vihusishi, vihisishi, aya, na kuakifisha. Viunganishi ni
    maneno yanayounganisha maneno mengine lakini vihusishi huhusisha watu ama
    vitu na mahali. Navyo vihisishi ni maneno yanayoonyesha mahangaiko ya moyo
    ilhali aya ni fungu la sentensi lililo na maana kamilifu, yaani paragrafu. Nako
    kuakifisha ni kuwakilisha sauti kimaandishi. Ufahamu ni pale ambapo mtu husoma
    kifungu na halafu akapima ama akapimwa ufahamu wake kuhusu hayo aliyoyasoma.
    Imla nayo ni pale ambapo unasomewa maneno ama kifungu huku ukiandika.

    Zoezi

    Jiunge na wenzako watatu na mjadili maana na matumizi ya maneno haya yafuatayo:
    1. mtungo au insha                       2. msamiati                                  3. rejesta
    4. vitendawili                                 5. methali                                      6. misemo
    7. nahau                                        8. mafumbo                                  9. barua
    10. masimulizi                               11. dhahania                                12. istilahi
    13. kiimbo

    Sifa za rejesta ya sarufi ya Kiswahil
    Nazo sifa za rejesta ya sarufi ya Kiswahili zinaweza kuwa hivi:
    i) Imejaa maneno ya kitaalamu,
    ii) Hufundisha jinsi ya kutunga tungo sahihi,
    iii) Huwa na semi za kutia hekima,
    iv) Huwa ndio msingi wa maongezi yote katika lugha husika,
    viii)Huwezesha kuhifadhi mila za kabila husika,
    ix) Huwa na tamathali za usemi za kuungia usemi

    Zoezi la ziada
    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako na mjibu maswali yaliyopo hapa chini.

    Jazeni jedwali hili. Sehemu ya kwanza imejazwa kama mfano










    B . Matumizi ya majina ya ngeli ya KI-VI katika umoja na wingi

    Ngeli ya KI-VI hujumuisha majina mbalimbali. Majina yote katika ngeli hii huchukua
    upatanisho wa sarufi, ki- katika umoja na vi- katika wingi. Hii ndiyo sababu ya ngeli
    hii kuitwa ngeli ya KI-VI. Maumbo ya majina katika ngeli ya KI-VI hubadilika kutoka umoja hadi wingi.

    Je, unakumbuka majina yanayopatikana katika ngeli hii? Yataje matano katika
    umoja pamoja na wingi wayo.
    Tazama jedwali hili. Je, ni mabadiliko gani yanayotokea katika majina yanapotoka umoja hadi wingi?






    Yapo makundi mbalimbali ya majina yanayopatikana katika ngeli ya KI-VI.

    i)    Majina yanayoanza kwa ki- katika umoja na kuchukua vi- katika wingi
    Kundi hili la majina ndilo huwa na majina mengi ya ngeli hii ya KI-VI.


    Kumbuka
    Majina ya viumbe wenye uhai ambayo huanza kwa kiambishi ki- katika umoja na vi- katika
    wingi hayawekwi hapa bali huchukua viambishi ngeli vya ngeli ya A-WA

    Zoezi

    Andika majina kumi zaidi ya ngeli ya Ki-Vi pamoja na wingi wayo.

    ii) Majina yanayoanza kwa ch- katika umoja na kuchukua vy- katika wingi

    Kumbuka
    Majina ya viumbe wenye uhai ambayo huanza kwa kiambishi ch- katika umoja na
    vy- katika wingi hayawekwi hapa bali huchukua viambishi ngeli vya ngeli ya A-WA.

    Zoezi

    Andika majina kumi zaidi yanayopatikana chini ya orodha hii ya majina katika ngeli ya KI-VI.

    iii) Majina kutokana na vitenzi

    Yapo baadhi ya majina ambayo huundwa kutokana na vitenzi. Majina hayo pia hupatikana katika ngeli ya KI-VI.
    Mfano

    Zoezi

    Andika majina kumi zaidi yaliyomo katika kundi hili.

    iv) Majina yanayoanza kwa ki- lakini hayachukui wingi
    Yapo majina katika Kiswahili ambayo huanza kwa kiambishi ki- lakini hayana wingi.
    Majina haya huwa ya viumbe wasiokuwa na uhai.

    Zoezi

    Andika majina matano zaidi yanayopatikana katika kikundi hiki.

    v) Majina ya vitu katika hali ya udogo
    Katika Kiswahili, majina yanaweza kuwa katika hali ya wastani, udogo au ukubwa.

    Majina yote yanapoandikwa katika hali ya udogo, huwekwa katika ngeli ya KI-VI
    iwe majina ya viumbe wenye uhai au vitu visivyokuwa na uhai.
    Katika mfano uliotolewa hapo juu, mtu na mtoto ni viumbe wenye uhai.
    Majina haya hupatikana katika ngeli ya A-WA. Unaposema kijitu au kitoto,
    unarejelea mtu mdogo zaidi ya kawaida. Kwa hivyo, majina kitoto na kijitu yanawekwa katika
    ngeli ya KI-VI. Katika wingi huwa tunasema vitoto au vijitu. Vilevile, nyumba ipo katika ngeli ya I-ZI.
    Hata hivyo, kijumba (nyumba ndogo kupita kiasi) hupatikana katika ngeli ya KI-VI.
    Tazama mifano zaidi katika jedwali hapa chini.

    Zoezi

    Andika majina matano zaidi yanayopatikana katika orodha hii ya majina katika ngeli ya KI-VI.

    Matumizi ya majina ya ngeli ya KI-VI
    Kama ilivyoelezwa hapo mwanzoni, vitenzi vinavyoambatana na majina katika
    ngeli hii ya KI-VI huchukua kiambishi ki- katika umoja na vi- katika wingi.
    Tazama mifano iliyotolewa katika jedwali lifuatalo:

    Zoezi

    1. Eleza maana ya ngeli ya KI-VI.
    2. Eleza mabadiliko yanayotokea katika wingi ukirejelea majina haya ya ngeli ya KI-VI.
        i) chombo    ii) kioo    iii) kiti     iii) cheo
    3. Kamilisha sentensi zifuatazo:
       i) ___akula ___livyonunuliwa ___meliwa.
      ii) ___dege ___mekamatwa.
     iii) ___beti ___mejaa faranga.
     iv) ___sima vya maji ___nachimbwa hivi sasa.
      v) Niliwaambia waniletee ___uma ___livyokunjwa.
     vi) Nitasoma kwa bidii ili niingie katika __uo _kuu.
    4. Bainisha sentensi sahihi kutoka kwa zile zisizokuwa sahihi na uzisahihishe.
        Nambari za kwanza mbili zimetolewa kama mfano.
      i) Kiti hiki kinapendeza. SAHIHI
     ii) Choo vimebomolewa. SI SAHIHI. Vyoo vimebomolewa. SAHIHI
    iii) Viswahili kinazungumzwa Afrika Mashariki.
    iv) Kioo kinanipendeza.
     v) Kitoto anaruka.
    vi) Kijiti limevunjika.
    vii) Vyuo vikuu vinatoa elimu ya juu.
    viii)Vyuma kinachomwa.
    ix) Kigelegele kinasikika.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Tungeni sentensi sahihi katika umoja na wingi
    mkitumia majina ya ngeli hii ya KI-VI.

    Matumizi ya majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi
    Je, unakumbuka vivumishi ulivyosoma katika sura ya kwanza? Rejelea vivumishi hivyo.

    a) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi vya sifa
     Vivumishi vya sifa ni maneno yatajayo tabia au sifa za mtu, kitu au jambo.
    Mifano katika sentensi:


    Zoezi

    Tunga sentensi zozote kumi ukitumia majina ya ngeli ya KI-VI na vivumishi mbalimbali vya sifa.

    b) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi vya pekee
    Vivumishi vya pekee hutoa habari kuhusu nomino au kiwakilishi chake kwa njia ya kipekee.
    Huwa vitano.

    i) -enye           ii) -enyewe          iii) -ote          iv) -o-ote          v) -ingine
    Majina katika ngeli ya KI-VI huchukua kiambishi ch- katika umoja na vy- katika wingi yanapotumika pamoja na
    vivumishi vya pekee vyote isipokuwa -ingine au -ingineo.

    Hata hivyo, kivumishi cha pekee -ingine na -ingineo huchukua viambishi ki- katika umoja na vi- katika wingi kinapotumika na majina ya ngeli ya KI-VI.

    Zoezi

    Tunga sentensi zozote kumi ukitumia majina ya ngeli ya Ki-Vi pamoja na vivumishi mbalimbali vya pekee.

    c) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi vionyeshi
    Vivumishi vionyeshi au viashiria ni maneno ya kuonyesha alipo mtu au kitu, yaani ujirani.
    Kuonyesha huko kunaweza kuwa kwa ujirani wa karibu – hapa,
    ujirani wa mbali kidogo – hapo, na ujirani wa mbali – pale.

    Katika ngeli ya KI-VI, kivumishi kionyeshi cha karibu huwa: hiki (umoja) na hivi (wingi),
    kionyeshi cha mbali kidogo huwa hicho (umoja) na hivyo (wingi) na kionyeshi cha mbali huwa
    kile (umoja) na vile (wingi).

    Mfano katika sentensi:

    Zoezi

    Tunga sentensi zozote sita ukitumia majina ya Ki-Vi pamoja na vivumishi vionyeshi mbalimbali.

    d) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi vya idadi
    Vivumishi vya idadi ni maneno yanayoonyesha idadi ya watu ama vitu. Vipo vivumishi vya idadi kamili,
    vivumishi vya idadi ya jumla na vivumishi vya idadi ya matokeo.

    Majina ya ngeli ya KI-VI huchukua viambishi ki- katika umoja na vi- katika wingi
    yanapotumika pamoja na vivumishi vya idadi vinavyochukua viambishi.
    Kumbuka
    Idadi sita, saba, tisa na kumi hazichukui kiambishi chochote cha ngeli.

    Zoezi

    Tunga sentensi zozote kumi ukitumia majina katika ngeli ya KI-VI na vivumishi mbalimbali vya idadi.

    e) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi viulizi
    Hili ni kundi la vivumishi ambalo lina maneno yatumiwayo kuulizia maswali.
    Baadhi ya mifano ya vivumishi viulizi ni: -pi?, na -ngapi?

    Majina katika ngeli ya KI-VI huchukua kiambishi ki- katika umoja na vi- katika wingi yanapotumiwa pamoja na viulizi.
    Kumbuka
    Kiulizi -ngapi hutumika katika wingi pekee.
    Kiulizi gani? hakichukui kiambishi.
    Tunasema: Kijiko gani? au vijiko gani?

    Zoezi

    Tunga sentensi zozote tano ukitumia majina ya ngeli ya KI-VI na vivumishi viulizi mbalimbali.

    f) Majina ya ngeli ya KI-VI pamoja na vivumishi vimilikishi
    Maneno katika kundi hili la vivumishi hujibu swali mtu, kitu au jambo ni la nani?
    Maneno haya huwa sita pekee katika Kiswahili.
    -angu           -etu
    -ako             -enu
    -ake             -ao

    Katika ngeli ya KI-VI, kiambishi ch- hutumika katika umoja na vy- katika wingi.

    Zoezi

    Tunga sentensi zozote sita ukitumia majina katika ngeli ya KI-VI na vivumishi mbalimbali vya kumiliki.

                                  Maswali ya marudio
    1. Kwa maneno yako mwenyewe, eleza maana ya rejesta za lugha.
    2. Jaza jedwali hii kwa kuandika mifano kumi ya msamiati unaotumika katika kila rejesta iliyotajwa.
       
    3. Eleza sifa za rejesta zifuatazo:
        a) Michezo
        b) Burudani
        c) Hotelini
        d) Sokoni
    4. Pana tofauti gani kati ya rejesta ya burudani na ile ya michezo?
    5. Rejesta ya hotelini ni sawa kabisa na ile ya sokoni. Je, haya ni kweli? Kwa nini?
    6. a) Bainisha aina mbalimbali za michezo katika jamii.
        b) Eleza umuhimu wa michezo katika afya ya binadamu.
    7. a) Taja namna mbalimbali za burudani katika jamii.
        b) Eleza umuhimu wa burudani kiafya na kiushirikiano.
    8. Eleza umuhimu wa kuonyesha adabu na heshima kwa watu katika mazingira mbalimbali.
    9. Bainisha rejesta zifuatazo na utaje sifa zao za kimsingi:
       a) Mheshimiwa spika, sheria hii imekiuka katiba ya nchi yetu. Mheshimiwa spika,
           ikiwa sheria hii itapitishwa jinsi ilivyo, patatokea migogoro.
       b) Bei rahisi...bei imeshuka...njoo mteja..karibu..usitembee kwa miguu
           mitupu....nunua viatu kabla bei kupanda...
       c) Maandiko yanasema kuwa wenye dhambi watachomwa motoni.
    10. Linganisha na utofautishe rejesta ya bungeni na mahakamani.
    11. Rejesta ya hospitalini inaweza kufaa sana katika mazingira ya jikoni.
          Hili ni sawa? Kwa nini?
    12. Taja maneno sita ya rejesta ya utamaduni.
    13. Huku ukitoa mifano, eleza rejesta ya sarufi.
    14. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati ufuatao:
        a) mwana mpotevu
        b) baraka
        c) mpira umekuwa mwingi
        d) densi
        e) bei ghali
        f ) ankra
        g) kukata rufaa
    15. Andika maneno haya katika wingi:
       a) chombo
       b) kiti
       c) kioo
       d) choo
    16. Eleza muundo wa nomino za ngeli ya Ki-Vi katika umoja na wingi.
    17. Tunga sentensi tano tano ukitumia majina ya ngeli ya Ki-Vi na vivumishi
           vilivyotolewa hapa chini katika umoja na wingi.
        a) vivumishi vya sifa
        b) vivumishi vionyeshi
        c) vivumishi viulizi
        d) vivumishi vimilikishi
    18. Sahihisha makosa katika sentensi hizi:
         a) Kijiko vyangu kimenunuliwa.
         b) Vioo vikumi vitaletwa kesho.
         c) Niletee kitabu hivyo.
         d) Vyumba chote vimefagiliwa.
    19. Tunga sentensi sahihi ukitumia vivumishi vilivyotolewa.
         a) vyetu
         b) vinane
         c) kile
         d) kipi
         e) vyenyewe
    20. Eleza jinsi utakavyotumia ujuzi uliopata katika sura hii.

    Sura 2: UtungajiSura 4: Mazungumzo na mawasiliano katika shughuli mbalimbali za kijamii