• Sura 2: Utungaji

     

    Mada ndogo: Barua kuhusu matembezi, Barua za kirafiki,

                          Barua za mwaliko, Simu,Tangazo/Ilani.


    A Barua
    Barua ama waraka ni maandishi yaliyopangwa kwa utaratibu na mtiririko maalumu
    kwa minajili ya kuwasilisha ujumbe fulani. Zipo aina mbili kuu za barua: Ipo barua
    ya kirafiki ambayo pia huitwa barua ya kindugu na ipo barua rasmi.
    a) Barua za kirafiki
    Barua ya kirafiki ni barua ambayo huandikiwa mtu ama watu mbalimbali walio na
    uhusiano wa karibu na anayeandika; kama vile rafiki, mzazi, dada na kadhalika.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwenzako na mjadili barua zenu mlizoandika. Je, waandikiwa walikuwa
    kina nani? Ujumbe ulikuwa upi na ni lugha gani uliyotumia?

    Mifano ya barua za kirafiki
    i) Barua ya mwana kwa mzazi

                                                     

    Ukimwandikia mama barua, barua hiyo ni ya kirafiki

    Zoezi

    Mwandikie ndugu yako barua ukimweleza maendeleo yako katika masomo.
    ii) Barua ya mapenzi

                                      

                  

    Barua ya kindugu inaweza kuwa ya mapenzi pia.

    Zoezi

    Jifanye kuwa una zaidi ya miaka kumi na minane. Mwandikie mchumba wako barua
    ukimweleza sababu ya kumpenda na kutaka kumwoa.

    ii) Barua ya kutoa ushauri
    Isitoshe, barua ya kirafiki inaweza kuwa ni ya mzazi anayetoa ushauri kwa mwanawe.


    Zoezi

    Wewe ni mzazi ambaye mwanao amepotoka. Mwandikie barua ya
    kumwelekeza kuepukana na upotovu huo na arudie wema wake wa awali.
    Someni barua zenu mbele ya darasa.

    Sehemu kuu za barua za kirafiki

    Barua za kirafiki huwa na sehemu au muundo fulani maalumu.

    Kazi ya kikundi

    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Tazameni mifano ya barua za kirafiki iliyotolewa na mingineyo. Jadilianeni kuhusu sifa zinazofanana katika barua zote. 

    Tazama mfano wa muundo wa barua ya kirafiki. Kuna uhusiano gani kati ya yaliyomo na barua za kirafiki ulizosoma? 

             Anwani

            Tarehe 

            Kutaja mwandikiwa

            Utangulizi/salamu 

            Mwili wa barua           

            Hitimisho  

            Jina la mwandishi.

    Barua ya kirafiki huwa na sehemu kuu zifuatazo:
    i) Anwani moja ya mwandishi: Huandikwa juu, pembeni.
    ii) Tarehe: Huandikwa chini ya anwani kwa kuacha nafasi ya mstari mmoja.
    iii) Kutaja mwandikiwa: Huja chini ya tarehe kwa kuacha nafasi ya mstari mmoja.
    iv) Utangulizi: Hujitokeza katika aya ya kwanza. Mwandishi humjulia hali mtu
         anayeandikiwa na wenzake. Pia, husema hali yake.
    v) Mwili wa barua: Mwandishi hupitisha ujumbe wa barua/kuelezea kiini cha
        kuandikwa kwa barua husika.
    vi) Hitimisho/Kufunga barua: Mwandishi huhitimisha barua yake kwa kumtakia
         heri aliyeandikiwa. Jina la mwandishi wa barua huja chini ya hitimisho.

    Zoezi

    Tazama barua iliyopo hapa chini. Je, barua hii ina makosa gani? Andika upya barua
     hii kwa kusahihisha makosa yaliyopo na kuongezea sehemu zinazokosekana.

    Kwa Shangazi Mpendwa,
    S.L.P, 45
    Kigali
    Rwanda

    Wako Mpendwa,

    Ninajua wewe unapenda sana kilimo cha ndizi. Juzi tulisoma kuhusu kilimo bora
    cha ndizi. Mwalimu wetu alitufunza mbinu mpya za kupanda ndizi. Tukifunga,
    nitakutembelea ili nikufunze mbinu hii mpya itakayokupa mavuno mengi zaidi.

    Unisalimie wote waliopo nyumbani. Waambie nitawatembelea wakati wa likizo.

    Kwanza, ningependa kukueleza kuwa ninazidi kutia bidii katika masomo. Juzi
    tulifanya majaribio na niliibuka nafasi ya tatu katika darasa letu. Ninatia bidii zaidi.
    U hali gani? Mimi nipo salama. Nia yangu kuu ya kukuandikia barua hii ni kukujulisha
    kuhusu mambo mawili makuu.

    Kanuni za kuzingatiwa katika uandishi wa barua za kirafiki
    Zipo kanuni mbalimbali za kuzingatiwa wakati wa kuandika barua ya kirafiki.
    Soma kifungu kifuatacho ili kubainisha baadhi ya kanuni hizo.

                  

    USANASE: Hujambo, Gabiro?
    GABIRO:     Sijambo Usanase.
    USANASE: Unaonekana mwingi wa huzuni. Pana jambo linalokutatiza?
    GABIRO:    Ni kweli. Ninataka kuandika barua kwa mjomba. Sijui endapo pana
                        kanuni zozote ninazofaa kuzingatia.
    USANASE: Ahaa! Zipo kanuni za kufuatwa wakati wa kuandika barua ya kirafiki.
    GABIRO:    Kanuni hizo ni gani?
    USANASE: Kwanza, hufai kuandika kichwa.
    GABIRO:    Niandike tu moja kwa moja?
    USANASE: Naam. Kabla ya kuandika kiini au mwili wa barua, hakikisha kuwa
                        umeandika anwani yako kama mwandishi.
    GABIRO:    Anwani moja inatosha?
    USANASE: Naam. Chini ya anwani, andika tarehe kisha umtambulishe unayemwandikia.
    GABIRO:    Ninaweza kumtambulisha vipi?
    USANASE: Mtambulishe kwa kudhihirisha uhusiano uliopo baina yenu. Kwa
                        mfano, Kwa Mjomba Mpendwa.
    GABIRO:    Ahaa! Ninakupata vizuri sana. Je, ninafaa kujikita katika ujumbe
                        mmoja mkuu?
    USANASE: Hapana. Una uhuru wa kuzungumzia maudhui mengi. Unaweza
                        kutaja mambo mengi yasiyohusiana. Mfano, unaweza kumwambia
                        kuhusu hali ya anga na masomo shuleni. Baadaye, unaweza
                        kumwuliza kuhusu mazao yake yalivyo shambani na mambo mengi.
                        Uhakikishe kuwa kila maudhui au ujumbe upo katika aya yake.
    GABIRO:    Ninafaa nitumie kiwango gani cha lugha?
    USANASE: Hujafungwa katika kiwango fulani cha lugha. Lugha utakayotumia
                        inategemea uhusiano uliopo kati yako na mjomba au yeyote
                        unayemwandikia.
    GABIRO:    Kwa hivyo si lazima lugha yangu iwe rasmi?
    USANASE: Naam. Si lazima uzingatie kiwango cha juu cha adabu kama ilivyo
                        katika barua rasmi. Hilo halimaanishi kuwa unaruhusiwa kutumia lugha chafu au
                        lugha isiyokuwa na tasfida.
    GABIRO:    Kwa hivyo ninaweza kutumia lugha yenye utani, vichekesho na yenye
                        kuibua hisia ya huzuni, furaha au huruma.
    USANASE: Naam.
    GABIRO:    Je, ninafaa kuzingatia urefu kiasi gani?
    USANASE: Kama nilivyosema hapo mbeleni, una uhuru wa kuzungumzia
                        mambo mengi utakavyo katika barua ya kirafiki. Urefu utategemea
                        jumla ya mambo hayo. Una uhuru wa kuandika barua ndefu au fupi
                       utakavyo. Hakuna urefu maalumu.
    GABIRO:    Nikimaliza, ninafaa kutia sahihi?
    USANASE: La hasha! Barua ya kirafiki si lazima itiwe sahihi.
    GABIRO:     Asante sana rafiki yangu kwa maelezo hayo. Sasa ninaweza kuandika
                        barua yangu.
    USANASE: Karibu. Ukiwa na swali lingine, utaniuliza.

    Zoezi

    Jiunge na mwenzako na muigize mazungumzo yaliyopo hapo juu. Andikeni kanuni za kuzingatiwa katika uandishi wa barua za kirafiki zilizopo kwenye ufahamu.

    Kazi ya kikundi

    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Andikianeni barua za kirafiki kuhusu mada yoyote mpendayo. Someni barua zenu huku mkisahihishiana.

    b) Barua rasmi

    Tazama michoro hii. Je, mwalimu na wanafunzi hawa wanajadiliana kuhusu nini?
    Je, unajua jinsi ya kuandika barua rasmi?

                            

    Barua rasmi ni barua zinazoandikiwa mtu au watu wenye nyadhifa kwa lengo
    maalumu la kuwasilisha ujumbe rasmi.Mifano ya barua rasmi.

    i) Barua ya kuomba kazi

    Hii ni aina ya barua ambayo mtu huandika wakati anapotaka kuajiriwa mahali. Kuna aina mbalimbali za barua za kuomba kazi.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili

    Jiunge na mwenzako. Jadilianeni kuhusu jinsi ya kuandika barua ya kuomba kazi. Andikeni barua hiyo kwa msingi wa majadiliano hayo.


    Zoezi

    Andika barua ya kuomba kazi yoyote upendayo. Angazia mambo yafuatayo katika barua yako:

    i) jinsi ulivyopata kuwepo kwa nafasi ya kazi hiyo,
    ii) tajiriba yako, wasifu wako mfupi,
    iii) sababu ya kutaka kazi hiyo,
    iv) mambo mapya ambayo utafanya ukipewa nafasi hiyo na kadhalika.                                                                                                                                                                                                                                                                                      

    ii) Barua ya kuomba ruhusa

    Hii ni aina ya barua ambayo mwandishi huomba kupewa fursa ya kutoshiriki katika shughuli fulani muhimu. Unaweza kusema kwa nini hutakuwepo au usiseme. 



    Zoezi

    Mwandikie mwalimu wako barua ukiomba ruhusa yoyote. Mweleze sababu za kuomba ruhusa hiyo.                                              

    iii) Barua ya huduma

    Barua ya huduma ni aina ya barua ambayo humhitaji mtu, kundi la watu, shirika lisilo la kiserikali au idara ya serikali au kampuni kutoa huduma fulani katika jamii. Wakati mwingine huandikwa kutoa maoni kuhusu hatua ambazo jamii ingependa kuchukuliwa, kwa mfano, idara ya polisi ama hospitali kuweka visanduku vya kupokea maoni kutoka kwa wananchi kuhusu namna wangependa kuhudumiwa kwa ubora zaidi.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Nyinyi ni vijana wanaojihusisha katika
    kufanya utafiti wa mbinu bora za kilimo katika wilaya yenu. Kipeni kikundi chenu
    jina na mchague katibu mkuu. Andikeni barua kwa shirika lolote linalojihusisha
    na kilimo katika eneo lenu. Elezeni shirika hilo kuhusu utafiti mliofanya wa kukuza
    kilimo katika wilaya yenu na msaada mnaohitaji kutoka kwao.

    Aina zaidi za barua rasmi
    Mbali na mifano iliyotolewa, zipo aina zaidi ya barua rasmi. Barua hizo ni kama vile:
    i) Barua ya kuomba nafasi katika shule fulani
    ii) Barua ya kuomba msamaha
    iii) Barua ya shukrani
    iv) Barua ya malalamiko
    v) Barua kwa mhariri
    vi) Barua ya mapendekezo
    vii) Barua ya uteuzi
    viii)Barua ya kusimamishwa au kufutwa kazi.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Fanyeni utafiti kuhusu jinsi barua zilizotajwa
    hapo juu huandikwa. Kila mwanafunzi aandike mojawapo ya barua hizo kuhusu
    mada yoyote kisha amsomee mwenzake. Sahihishianeni.

    Sehemu kuu na kanuni za barua rasmi
    Barua rasmi huwa na sehemu au muundo fulani maalumu kama ufuatao:
    Anwani ya mwandishi
    Tarehe
    Anwani ya mwandikiwa
    Mtajo/Kutaja mwandikiwa kwa heshima
    Kichwa
    Utangulizi/Kutajwa kwa kiini
    Mwili wa barua
    Hitimisho
    Wako mwaminifu/mtiifu
    Sahihi
    Jina la mwandishi
    Cheo cha mwandishi (ikiwa mwandishi anaandika
    kwa niaba ya shirika fulani, kikundi au kampuni)

    Soma mazungumzo haya na ujibu maswali chini yake.
                                          

    UMUHIRE: Mwenzangu, nieleze kuhusu jinsi ya kuandika barua rasmi.
    NDOLI:       Lazima uandike anwani yako na ile ya mwandikiwa. Anwani yako
                       kama mwandishi huja juu. Unapoandika anwani ya mwandikiwa, ni
                       sharti uandike cheo chake kwanza kabla ya kuandika jina na anwani
                       ya kampuni chini ya cheo chake kama vile,  'MKURUGENZI MKUU,
                       MWENYEKITI, MWALIMU MKUU’ na kadhalika.
    UMUHIRE: Baada ya anwani, ninaandika nini?
    NDOLI:      Unaandika ufunguzi wa barua kama vile Kwa Mbunge Mheshimiwa,
                       Kwa Mheshimiwa, Kwa Meneja Mkuu, Kwa Meneja, Kwa Mgeni wa
                       Heshima na kadhalika. Unaweza kuandika jina lake la pili baada ya
                       Bw au Bi.
    UMUHIRE: Naam! Kwa hivyo, baada ya kutambulisha mwandikiwa, ninaandika
                       kichwa au vipi?
    NDOLI:       Naam, rafiki yangu. Kichwa hudokeza kiini cha kuandika barua yako.
                       Unapoandika kichwa, unaanza kwa kutumia kifupisho MINT: au KUH:
    UMUHIRE: MINT na KUH vinasimamia nini?
    NDOLI:       MINT husimamia Mintaarafu au kwa mintaarafu ya, KUH husimamia
                       kuhusu. Kichwa au mada yako haifai kuzidi maneno sita isipokuwa
                       pale ambapo pana lazima.
    UMUHIRE: Ninapoanza kuandika mwili, ninafaa kusema nini?
    NDOLI:      Ikiwa ni barua ya kuomba kazi, ni vizuri uanze kwa kurejelea tangazo
                      la kazi hiyo au jinsi ulivyopokea kuwepo kwa nafasi hiyo. Baadaye,
                      andika moja kwa moja kiini cha barua hiyo.
    UMUHIRE: Hakuna salamu?
    NDOLI:       Naam. Barua rasmi haina salamu. Unaeleza moja kwa moja kiini
                       cha kuandika barua. Unafaa kujikita katika ujumbe mmoja mkuu,
                       yaani jambo linalokufanya uiandike barua hiyo. Ikiwa unaomba kazi,
                       toa maelezo muhimu kukuhusu. Maelezo hayo yawe na uhusiano na
                       kazi unayolenga kupata. Epuka maelezo mengi yasiyokuwa na manufaa.
    UMUHIRE: Lugha yangu inafaa kuwa ya namna gani?
    NDOLI:       Lugha yako sharti izingatie adabu ya hali ya juu na kiwango cha juu cha urasmi.
                       Lugha yako iwe sahihi. Ikiwa unaandika kwa kalamu, tumia hati nadhifu. Usitaje
                       chochote cha kuonyesha mambo au hisia za kibinafsi au uhusiano wa kibinafsi
                       na unayemwandikia.
    UMUHIRE: Nini huandikwa katika hitimisho la barua hii rasmi?
    NDOLI:       Unaandika tumaini lako la majibu mazuri. Chini yake, unaandika:
                       Wako Mwaminifu au Wako Mtiifu kisha unaweka sahihi. Chini ya sahihi yako,
                       andika jina lako kamili. Ikiwa unaandika kwa niaba ya shirika au kampuni au kikundi,
                       andika cheo chako chini ya jina lako.
    UMUHIRE: Asante kwa maelezo haya.

    Maswali
    i) Je, barua rasmi ina kanuni zipi za kuzingatiwa?
    ii) Linganisheni sehemu na kanuni za kuandika barua za kirafiki na zile za
        kuandika barua rasmi. Jadilianeni kuhusu tofauti zilizopo kati ya barua za
        kirafiki na barua rasmi.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako. Tazameni mifano ya barua rasmi iliyotolewa na
    mingineyo. Jadilianeni kuhusu miundo ya barua hizo. Andikianeni barua rasmi
    kuhusu mada yoyote.
        
      B. Matangazo mbalimbali                             
    Tangazo ni mpangilio wa maandishi
    kwa mtindo maalumu kwa lengo la
    kupasha ama kupokeza ujumbe fulani
    wa kidharura au muhimu.
    Zipo aina mbalimbali za matangazo:

    i) Matangazo ya biashara
    Matangazo ya biashara ni maandishi
    ambayo yanalenga kutoa maelezo fulani
    kuhusu kitu, bidhaa, mahali au jambo
    kwa ajili ya kuwashawishi wasomaji
    kununuana kutumia bidhaa husika au

    kuzuru mahali husika. Matangazo haya yanaweza pia kuwajulisha watu kuhusu bidhaa mpya zilizoingia sokoni au kuimarishwa kwa bidhaa zilizopo kwa sasa.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Tajeni matangazo mbalimbali
    yaliyomo katika redio, televisheni, magazeti na vibango mbalimbali karibu na
    maeneo mnapoishi. Jadilianeni kuhusu jinsi istilahi au msamiati ulivyotumika
    katika matangazo hayo na malengo ya matangazo hayo. Je, istilahi hizo zimefaulu
    katika kuafikia malengo husika?



    Jinsi ya kufika huko
    Unaweza kusafiri angani kwa ndege hadi uwanja wa ndege wa Gisenyi. Hapo,
    waajiri wetu watakupokea kwa tabasamu na unyenyekevu.
    Ikiwa una gari, pitia barabara kuu ya Kaskazini Magharibi kutoka jijini Kigali.
    Itakuchukua saa tatu pekee.
    Tembelea hoteli ya Sabyinyo leo upate uhondo wa burudani.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Someni tena matangazo yaliyopo hapo juu kwa
    makini huku mkitambua sifa na miundo ya matangazo hayo.

    Sifa na miundo ya matangazo ya biashara
    Soma kifungu hiki na ujibu maswali chini yake.
    Matangazo ya biashara huwa na utangulizi wenye mvuto na hitimisho lenye
    ushawishi. Kumbuka kuwa lengo kuu la tangazo lolote la biashara ni kuwavutia
    wasomaji.
    Yapo matumizi ya takriri. Takriri ni kurudiarudia neno au maneno fulani. Kwa kuwa
    matangazo ya biashara hulenga kutambulisha bidhaa fulani au mahali fulani, bidhaa
    au mahali husika hurudiwarudiwa katika mwili wa tangazo ili wasomaji au wateja
    lengwa wazikumbuke. Pia, jina la bidhaa na kampuni hutajwa na kurudiwarudiwa.
    Watu hupenda sana kusoma maneno mafupi na ni rahisi kuyakumbuka. Maneno
    marefu kwa upande mwingine huchosha na huchukua nafasi kubwa. Matangazo
    ya biashara huandikwa kwa maneno mafupi mafupi yenye mnato na ujumbe mzito.
    Maneno mafupi hupunguza gharama ya matangazo hayo.
    Katika matangazo ya biashara kwenye redio na televisheni, matangazo hayo
    huambatana na sauti ya kimuziki. Sauti hiyo hulenga kuwavutia wanaosikiza
    matangazo hayo. Pia, huchangia katika kupitisha ujumbe uliokusudiwa.
    Wakati mwingine, matangazo hufuata mtindo wa dayalojia. Hapa, watu
    wanaohusika katika kutangaza bidhaa fulani huulizana maswali na kupashana
    ujumbe. Kwa mfano
    MTU I: Je, umejaribu sabuni hii?
    MTU II: Bado
    MTU I: Ijaribu leo. Hii ndiyo suluhisho ya kudumu kwa madoa sugu.
    Matangazo ya biashara pia hutumia lugha ya kushawishi. Lugha hiyo huwa sahihi
    au hukosa usahihi. Lugha inayotumika hutegemea umri, jinsia ya wanunuzi
    wanaolengwa.
    Matangazo ya biashara hueleza ubora wa bidhaa pekee na manufaa yake. Hutilia
    mkazo mambo haya kwa undani na wakati mwingine hutilia chumvi ubora na
    manufaa ya bidhaa husika.
    Matangazo mengi ya biashara hayataji bei ya bidhaa. Pia, hueleza zinakopatikana
    bidhaa zenyewe au jinsi ya kuzipokea mahali unapoishi. Wakati mwingine, hutoa
    mwito wa kutembelewa kampuni husika.

    Zoezi

    1. Taja sehemu kuu za matangazo ya biashara kwa mujibu wa kifungu na
         matangazo ya biashara uliyosoma au kusikia.
    2. Taja kanuni au sifa kuu za kuzingatiwa katika uandishi wa matangazo ya
         biashara.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Fanyeni mradi wa kuandika
    matangazo mbalimbali ya biashara kuhusu bidhaa mtakazojichagulia.

    ii) Matangazo ya mkutano
    Katika matangazo haya, mwandishi hutaja kiini au ajenda za mkutano, mahali pa
    mkutano, tarehe na wakati ambapo mkutano utaandaliwa na maelezo mengine
    muhimu.


    iii) Matangazo kuhusu ziara ya rais
    Ziara ni tendo la kwenda mahali kwa sababu fulani kama vile kuzindua ujenzi wa
    barabara, kuwahutubia wananchi na kadhalika. Nalo tangazo lake linaweza kuwa
    kama hili lifuatalo:


    Zoezi

    Liandike tangazo kwa watu wote waliomo shuleni mwenu kuhusu ziara ya
    waziri wa elimu shuleni humo. Liandike tangazo hilo kwa niaba ya mwalimu mkuu.

    iv) Matangazo ya kuwachagua watu kujiunga na kikosi cha polisi
    Huweza kutokea kwamba serikali inataka kuchagua watu kujiunga na kikosi cha
    polisi. Basi, huweza kulitangaza jambo kwa wananchi.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Someni tangazo lililopo hapo juu na matangazo
    mengineyo ya mikutano. Jadilianeni kuhusu sehemu muhimu za matangazo ya
    mikutano na kanuni za kuzingatiwa katika uandishi wa matangazo maalumu.

    v) Matangazo kuhusu nafasi za kazi
    Hutolewa kwa lengo la kufahamisha watu kuhusu kuwepo kwa nafasi fulani ya/za
    kazi katika kampuni, shirika ama idara fulani.

    Mfano

    HALMASHAURI YA WILAYA YA NYAGATARE
    Tarehe 3/07/2016.
    NAFASI ZA KAZI
    Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyagatare anatangaza kuwepo
    kwa nafasi zifuatazo za kazi:
    1. MWENYEKITI WA BODI YA AJIRA (Nafasi 1)
    Sifa za Mwombaji kazi
    Ni sharti awe:
    i) mkazi wa muda mrefu wa Wilayani Nyagatare,
    ii) na shahada ya uzamifu katika usimamizi,
    iii) mwenye umri wa miaka 35 au zaidi,
    iv) na tajiriba ya miaka 5 katika kusimamia watu katika shirika kubwa tajika,
    v) na rekodi nzuri ya utendakazi,
    vi) mwenye uwezo wa kuwatia motisha wafanyakazi ili kuinua hadhi ya bodi hii,
    vii) mtu mwenye kutoshawishika katika misimamo sahihi yake na ile ya
          halmashauri.
    Wajibu na majukumu
    i) Kutangaza nafasi za ajira,
    ii) Kupendekeza kupandishwa vyeo kwa wafanyakazi,
    iii) Kutoa mafunzo au maelekezo kwa waajiriwa wapya,
    iv) Kupendekeza nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi,
    v) Kutekeleza majukumu mengineyo kama itakavyopendekezwa mara kwa mara.

    Kiwango cha mshahara
    Kitajadiliwa wakati wa mahojiano.
    2. MAAFISA WA UCHUKUZI DARAJA LA II ( Nafasi 5)

    Sifa za mwombaji kazi
    Ili kufuzu katika nafasi hii, unahitajika kuwa na:
    i) shahada katika masuala ya usimamizi wa kibiashara,
    ii) tajiriba ya miaka 3 katika kitengo hiki,
    iii) uelewa wa masuala ya uchukuzi katika forodha na kanuni za barabara,
    iv) rekodi nzuri ya utendakazi,
    v) ufahamu wa matumizi ya kompyuta na mtandao.

    Majukumu
     i) Kutayarisha bajeti na kuendesha uchukuzi,
    ii) Kuhakikisha kuwa takwimu, stakabadhi na kumbukumbu zinazohusu vyombo
        vya usafiri pamoja na mitandao yake zinatunzwa vyema,
    ii) Kukusanya na kuandaa takwimu kuhusu maendeleo ya sekta ya uchukuzi na
        kuziwasilisha kwa wadau ndani na nje ya wilaya,
    iv) Kuweka faili za uchukuzi nchini,
    v) Kukadiria na kushauri juu ya utendaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya
        uchukuzi.

    Kiwango cha mshahara
    Kitajadiliwa wakati wa mahojiano.

    Ikiwa una sifa hizi na ungependa kujiunga nasi, tuma barua ukionyesha kazi
    unayoomba na uambatanishe wasifukazi wako wa hivi karibuni, nambari ya/za
    simu na warejelewa watatu kwa mawasiliano wakati wa mchana. Tuma kwa anwani
    hii kabla ya usiku wa manane ya tarehe 23/08/2016.
    J.M. Gatete,
    Halmashauri ya Wilaya ya Nyagatare,
    S.L.P. 3013,
    NYAG ATA R E .    
    Tanbihi
    Halmashauri hii ni huru katika utoaji wa nafasi sawa za kazi bila kubagua yeyote.
    Ombi litakataliwa moja kwa moja endapo anayeomba kazi atahonga afisa yeyote
    kwa ajili ya kupendelewa.

    Zoezi

    Tafuta matangazo mbalimbali kuhusu nafasi za kazi katika magazeti, mabango na
    kadhalika. Soma matangazo hayo na ubainishe sifa zayo na kanuni zilizozingatiwa
    katika uandishi huo.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Huku mkirejelea matangazo
    mbalimbali, jadilianeni kuhusu tofauti zilizopo katika matangazo hayo mkizingatia:
    i) sifa
    ii) sehemu kuu
    iii) kanuni
    iv) msamiati
    v) malengo

    C . Ilani
    Ilani ni tangazo ambalo hutahadharisha au kuarifu kuhusu aina ya jambo ama tukio
    ambalo linastahili kuepukwa, lau sivyo madhara hutokea.
    Ilani huwa na wazo moja tu maalumu. Hutolewa mahali penye shughuli nyingi ama
    palipo na watu wengi kama vile shuleni, chuoni, kanisani msikitini na kadhalika.
                      
    Ilani mara nyingi huwa na mtindo rasmi. Ilani nyingi huwekwa katika mabango
    makubwa, magazetini, kwenye majarida na kadhalika.

    Mifano

    i) Ilani kuhusu mkurupuko wa ugonjwa
    ILANI
    WIZARA YA AFYA, KUPITIA HOSPITALI KUU YA MKOA,
    INAWATANGAZIA KUZUKA KWA UGONJWA HATARI WA
    KIPINDUPINDU.
    WATU WOTE WANASHAURIWA KUZINGATIA USAFI WA MWILI NA MAZINGIRA.
    ILI KUJIKINGA KUTOKANA NA MAAMBUKIZI YA UGONJWA HUU
    HATARI, MAMBO YAFUATAYO NI SHARTI YAZINGATIWE:
    i) KILA MTU AHAKIKISHE ANATUMIA CHOO.
    ii) KILA MTU ANAWE MIKONO KWA MAJI SAFI NA SABUNI BAADA YA KUTOKA CHOONI.
    iii) HAKIKISHA UNAKULA KATIKA MAHALI SAFI
    iv) WATU WASILE KWENYE MIKAHAWA.
    v) ALIYE NA DALILI ZA KUENDESHA NA KUTAPIKA AKIMBIZWE MARA
        MOJA HOSPITALINI KWA UCHUNGUZI NA MATIBABU.
    vi) ALIYEAMBUKIZWA APEWE MAJI MENGI YA KUNYWA WAKATI
         ANAPOPELEKWA HOSPITALINI.
    vii) KILA MTU ACHEMSHE MAJI YA KUNYWA.
    viii)MTU YEYOTE ALIYEAMBUKIZWA ATENGWE NA WATU WENGINE.
          ONYO:
    MTU YEYOTE ATAKAYEPATIKANA AKIUZA CHAKULA KATIKA
    MAENEO WAZI ATASHTAKIWA.

    ii) Ilani kuhusu unywaji wa pombe

    Mfano

    POMBE HATARI
    Serikali, kupitia wizara ya afya, inawatahadharisha wananchi kuhusu kuzuka kwa
    pombe hatari ya SUMEDA inayonywewa sana katika sehemu mbalimbali nchini.
    SUMEDA ni pombe hatari kwa afya yako kwa kuwa inatengenezwa kwa kutumia
    dawa ya kuhifadhi maiti na kemikali nyingine hatari.
    Pombe hii hatari imesababisha vifo vya watu zaidi ya 50, kuwapofusha
    wengine wengi pamoja na kutoa mimba.
    Atakayepatikana akiuza ama kunywa aina hii ya pombe atakamatwa.
    Ofisi ya mkuu wa wilaya.

    iii) Ilani ya kutokanyaga nyasi

    Mfano

                                                  ILANI
                          HAPANA RUHUSA KUKANYAGA NYASI
                                             NA MENEJIMENTI

    Zoezi

    i) Tazama mifano ya ilani zilizotolewa hapo juu. Je, ilani hizo zina sifa gani?
    ii) Andika ilani kuhusu mada yoyote upendayo.

    Kazi ya wanafunzi wawili wawili
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Andikeni ilani kuhusu mada hizi na mziweke
    kwenye maeneo husika shuleni.
    i) Kutokanyagwa kwa sehemu fulani zenye nyasi.
    ii) Kuwepo kwa mjadala kuhusu: mbinu za kisasa za kilimo ni bora kuliko mbinu
        za jadi za kilimo.
    iii) Kuwafahamisha wanafunzi kunawa mikono watokapo msalani.
    iv) Kuzingatia usafi jikoni

    D. Mialiko
    Mwaliko ni mwito wa kumtaka mtu au watu kuhudhuria shughuli au hafla fulani.
    Wito wa namna hii huweza kufanywa kwa njia ya barua ya kirafiki au barua rasmi
    na hata kwa matangazo.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na mwanafunzi mwenzako na mchunguze mchoro huo uliopo hapo chini.
    Jadilianeni kuhusu mambo yaliyomo ubaoni.
                                         
    Mifano ya mialiko
    i) Mwaliko wa harusi
    Je, umewahi kualikwa katika harusi au kuona kadi ya mwaliko wa harusi? Je,
    mwaliko huo ulikuwa na mambo gani?
    Mwaliko wa harusi huwaomba jamaa na marafiki kuhudhuria sherehe ya harusi.
    Kadi za mialiko ya harusi huchukua miundo na sura tofautitofauti. Miundo ya
    kadi hizo hutegemea ubunifu wa anayeziunda au mapendekezo ya maarusi au
    waandalizi wa harusi.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako. Tazameni mialiko ya harusi iliyotolewa hapa chini.
    Jadilianeni kuhusu mambo yaliyomo katika mialiko hiyo.

    Mfano
                

      
                A .     



                 B. 


    Kanuni za kuzingatiwa katika uandishi wa mwaliko wa harusi
    Unapoandika mwaliko wa harusi, ni sharti utaje majina ya watu wanaofunga ndoa,
    tarehe ya harusi, mahali pa harusi na wakati sherehe itakapoanza.
    Watu mbalimbali huandika mialiko ya harusi kwa njia tofauti tofauti. Mara
    nyingi, kadi hutumika. Wao hurembesha kadi za harusi ili kuwavutia wasomaji
    na kuonyesha mapenzi yaliyopo kati ya maharusi. Wengine hunukuu maandiko
    takatifu yanayotaja mapenzi na ndoa. Almuradi, kila mwaliko wa harusi huwa na
    umbo lake maalumu.

    Kazi ya kikundi
    Jiunge na wanafunzi wenzako na mchukulie kuwa nyinyi ni wanachama wa kamati
    inayoandaa harusi. Mna nia ya kutengeneza kadi nzuri ya mwaliko wa harusi. Kila
    mmoja achore kadi ya mwaliko na aweke ujumbe wake. Linganisheni mialiko yenu
    na mchague mwaliko bora zaidi kisha muufanye urembeke zaidi. Onyesheni na
    mlisomee darasa zima kadi yenu.

    ii) Mwaliko wa kutembelea mbuga ya wanyama
    Mwaliko kama huu huchukua umbo la barua rasmi.

    ii) Mwaliko wa maonyesho ya vitabu

                        

      Zoezi

    i) Soma tena barua za mialiko hapo juu. Taja mambo muhimu yaliyozingatiwa
       katika uandikaji wazo.
    ii) Mwandikie aliyekuwa mwalimu wako barua ya kumwalika kwenu kwa
        sherehe ya kukuaga kwa safari ya kwenda ng’ambo kusoma.

    Zoezi la ziada
    Andika barua za mialiko kuhusu mada yoyote.

    E . Aina za alama za uandishi na matumizi yake
    Wenzetu wanapozungumza, tunaweza kutambua wanapomaliza usemi wao kwa
    kusikia sauti zao. Lakini katika uandishi, hakuna sauti. Badala ya sauti, zipo alama
    za uandishi ambazo hutumiwa kuwakilisha sauti katika uandishi. Kutokana na
    alama hizo, tunatambua kama usemi umekwisha, kuulizwa swali, kushangaa na
    kadhalika. Pia, tunaposoma, tunajua wapi tunafaa kupumua kidogo, kushusha au
    kupandisha sauti na kadhalika.
    Alama hizi huitwa viakifishi. Hivyo basi, viakifishi ni alama zinazotumiwa katika
    maandishi ili kuleta maana ikusudiwayo katika matini mbalimbali kama vile
    sentensi, aya, mtungo, barua, mialiko, matangazo, ilani na kadhalika.

    Aina za viakifishi
    Nukta (.)
    a) Huwekwa mwishoni mwa sentensi. Kwa mfano:
       i) Nimechoka.
       ii) Waziri mkuu wa Uchina amewasili mjini Kigali.
    b) Hutumiwa kuonyesha ufupisho wa maneno. Kwa mfano:
       i) S.L.P. – Sanduku la Posta
       ii) Bi. – Bibi
    c) Hutumika kubainisha saa na dakika au tarehe. Kwa mfano:
       i) 3.20 – saa tisa na dakika ishirini
       ii) 14.5.2016- tarehe kumi na nne, mwezi wa tano, mwaka wa elfu mbili na kumi na sita
    d) Hutumiwa kuonyesha vipashio vya pesa. Kwa mfano:
        Sh. 10.50 – shilingi kumi na thumuni hamsini
    e) Zikitumiwa mara tatu mfululizo (...), huonyesha kutokamilika kwa sehemu
        husika. Kwa mfano:
                        Nitakupa lakini ni sharti...
    Mkato/koma ( , )
    a) Hutumiwa kuonyesha pa kutua kwa muda mfupi katika sentensi. Kwa mfano:
        i) Nilipowasili nyumbani, nilienda kuteka maji kisimani.
       ii) Kwa kuwa tulijiandaa vilivyo kwa mtihani wa kitaifa, tulipita.
    b) Hutumiwa kutenga maneno yaliyo katika orodha:
        i) Kwenda sokoni ununue mboga, nyama, mafuta, na unga.
        ii) Mwanafunzi huyu ni mtiifu, mwerevu, mtanashati, na mwenye bidii.
    c) Hutumiwa kubainisha sehemu mbili za sentensi zilizo kinyume:
        i) Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
        ii) Aliniambia atakuja, hakuja.
    d) Hutumiwa kabla ya alama za mtajo. Kwa mfano:
        Mama akasema, “Niletee chumvi.”
    e) Hutumiwa wakati sentensi inapoanza kwa kiunganishi. Kwa mfano:
        Kweli, alikuwa mtu mwovu.
    f ) Hutumiwa unapoita mtu ili kupata usikivu wake kabla hujamwambia
        chochote. Kwa mfano:
        Nkusi, niletee kalamu.
    g) Hutumiwa unapokubali au unapokataa kitu. Mfano:
       i) Ndio, nitakuja.
       ii) Hapana, sitakulipa.

    Nukta mbili/koloni (smile
    a) Hutumiwa kutanguliza maneno yaliyo katika orodha.

    Kwa mfano:
        i) Nenda kaniletee: kalamu, karatasi na kifutio.
        ii) Amenunua: machungwa, sukari, na ndizi.
    b) Hutumiwa kuashiria maneno ya msemaji badala ya alama za mtajo hasa katika
         uandishi wa mazungumzo au tamthilia.
        i) Mama: Lazima uniambie ulikokuwa tangu jana.
       ii) Mwalimu alisema: Ingieni darasani.
    c) Hutenganisha numerali za saa.

    Kwa mfano:
           4:10 – saa kumi na dakika kumi
    Nukta na kituo (;)
    a) Hutumiwa kuunganisha vishazi vikuu bila kutumia kiunganishi. Kwa mfano:
        Sikwenda Kayonza; nilienda Kirehe.
    b) Hutumiwa kumpumzisha msomaji katika sentensi iliyo ndefu ili apumzike
        zaidi kuliko pale inapotumiwa koma. Kwa mfano:
        Alipofikiri sana, alitanabahi kuwa hakikuwepo cha kutorokwa; yeye angeweza
        kuondoka nyumbani au kumwacha mumewe, aende popote kufanya lolote.
    Kistari kifupi (-)
    a) Hutumiwa kuonyesha kuwa neno linakatwa kwa vile limefika ukingoni mwa
         mstari husika na bado linaendelea katika mstari unaofuatia.
         Tanbihi: Neno la silabi moja halikatwi.
    b) Hutumiwa kuunga maneno yanayojenga neno moja. Mtindo
         huu aghalabu hujitokeza katika maneno yenye asili ya kigeni. Kwa mfano:
        i) Idd-el-Fitri
        ii) Dar-es-Salaam
    c) Huweza kutumiwa badala ya koma. Kwa mfano:
        Nyimbo za asili-hasa rumba-zinapendwa na wengi.

    Alama ya mshangao (!)
    Hutumiwa kuashiria mahangaiko ya moyo kama vile hasira, hofu, mshangao na
    kadhalika.
           i) Lo! Mwanafunzi ameangusha kitabu cha mwalimu matopeni.
           ii) Wamefungwa mabao kumi kwa nunge!
    Alama ya kuulizia/kiulizi (?)
    a) Hutumiwa mwishoni mwa sentensi kuonyesha kuwa sentensi hiyo ni swali.

    Mwa mfano:
    Unaitwa nani?
    b) Hutumiwa kuonyesha ukosefu wa uhakika kuhusu jambo kama vile mwaka.
        Kwa mfano:
        Shule hii ya Tumaini ilianzishwa 1992 (?)

    Mabano/parandesi egg
    a) Hutumiwa kufunga maneno ya ziada katika sentensi. Kwa mfano:
        Nyamata (makao makuu ya Bugesera) inakua kwa kasi.
    b) Hutumiwa mwandishi anapotaka kutoa ufafanuzi kwa lugha nyingine tofauti
         na ile anayoitumia.
    Kwa mfano: Walowezi (settlers) walifukuzwa
    c) Hutumiwa kufungia herufi za kuorodhesha. Kwa mfano:
         (a) huelimisha,                  (b) huburudisha,                (c) huonya

    Mkato (/)
    Hutumiwa kuonyesha kuwa mojawapo ya vitu vilivyotajwa chaweza kutumiwa
    badala ya hivyo vingine.
    Tazama: Abera alishangaa/aliduwaa
    Mtajo: (“ ” au ‘ ’)
    Hutumiwa kuonyesha maneno halisi ya mzungumzaji. Kwa mfano:
    “Nitafika kesho jioni,” alisema mdogo wake.
    Herufi kubwa (H)
    Hizi ndizo alama za uandishi zinazotumiwa sana kuliko nyingine zote. Hutumiwa
    kila baadaya herufi kubwa.
    Mama anapika.

    Zoezi

    Kiakifishe kifungu kifuatacho
    Ilikuwa asubuhi na mapema bw butera alipotoka kwake kwenda kazini fikirani
    mwake alijikumbusha pindi nikifika ofisini nitaomba ruhusa niende nimlipie binti
    yangu karo
    aliabiri gari linaloelekea ruhango baada ya mwendo mfupi tu lo gari hilo lilipata
    ajali liligongana na lori japo ng'ombe waliokuwemo njiani walikufa takriban wote
    abiria walipata majeraha madogo madogo lakini ililazimu wapelekwe hospitalini
    hivyo butera hakutimiza azma yake

    Mazoezi ya ziada

    Zoezi A

    Andika kifungu cha habari kuhusu mada yoyote ukitumia alama za uandishi kwa
    usahihi.


    Zoezi B

    Jiunge na mwanafunzi mwenzako na msome vifungu mbalimbali vya habari
    vilivyomo katika kitabu hiki, magazeti, na vitabu vinginevyo. Bainisheni na kuainisha
    alama mbalimbali za kuakifisha zilizotumika na jinsi zilivyotumiwa.

                                                Maswali ya marudio
    1. Eleza maana ya barua ya kirafiki.
    2. a) Taja watu watano wanaoweza kuandikiwa barua ya kirafiki.
        b) Mwandikie mmoja wa hao uliowatajia barua ya kirafiki.
    3. Zitaje sehemu zote kuu za barua ya kirafiki huku ukizieleza.
    4. Eleza maana ya barua rasmi.
    5. Taja aina tano za barua rasmi.
    6. Mwandikie Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ulikosomea ukiomba nafasi ya
         kufunza katika shule hiyo.
    7. Zitaje sehemu kuu za barua rasmi.
    8. Eleza kanuni za kuzingatiwa wakati wa kuandika barua rasmi.
    9. Eleza tofauti zilizopo kati ya barua rasmi na barua ya kirafiki.
    10. Kwa maneno yako mwenyewe, eleza tangazo ni nini.
    11. Ipo tofauti gani kati ya matangazo na barua rasmi?
    12. Eleza tofauti kati ya tangazo la tanzia na tangazo la mkutano.
    13. a) Ilani ni nini?
          b) Andika ilani utakayoweka msalani ili kuwatahadharisha wanafunzi
               wenzako kuhusu madhara ya kutonawa mikono baada ya kutoka msalani.
    14. a) Eleza sifa za matangazo ya biashara.
          b) Andika tangazo la biashara kuhusu bidhaa upendayo.
    15. Eleza umuhimu wa mwaliko.
    16. Je, kuakifisha ni kufanya nini?
    17. Eleza umuhimu wa uakifishaji.
    18. Yataje kwa mifano matumizi matano ya nukta.
    19. a) Eleza maana ya mtajo.
          b) Andika mifano miwili ya matumizi ya mtajo.
    20. Eleza kwa ufupi mambo muhimu uliyojifunza katika sura hii. Taja jinsi mambo
          hayo yatakavyokusaidia na kuisaidia jamii yako.



    Sura 1:Mazungumzo na majadilianoSura 3: Matumizi ya lugha katika mazingira mbalimbali