Jiunge na mwenzako. Chunguzeni michoro ifuatayo na mjaze mapengo kando yake.
C . Msamiati wa msingi kuhusu wanyama wa porini na umuhimu wake
i) Msamiati wa wanyama wa porini nchini Rwanda
Tazama wanyama hawa. Je, hawa ni wanyama gani? Wanyama hawa
wanapatikani katika mbuga na sehemu ipi ya Rwanda?
Kisome kifungu kifuatacho ili kujifunza msamiati wa wanyama wa porini.Mnyama wa porini ni mnyama anayeishi katika pori. Pori ni mahali penye miti na nyasi nyingi.
Mnyama wa porini hafugwi na binadamu. Wanyama wengi wa porini hupatikana katika mbuga
za wanyama. Mbuga za wanyama ni sehemu zilizotengwa na serikali kuwa ndio makazi ya
wanyama hao wa porini. Je, unafahamu mbuga gani za wanyama nchini Rwanda?
Nchi ya Rwanda ina wanyama wengi wa porini.
Nchi yetu ya Rwanda inasifika sana kutokana
na masokwe. Sokwe ni mnyama mkubwa zaidi
katika jamii ya nyani. Mnyama huyu hana
mkia. Sokwe ana akili nzuri inayokaribiana
na ile ya binadamu. Wana uwezo wa
kumwiga binadamu. Nchi yetu inajulikana
sana kutokana na masokwe. Masokwe hawa
wanapatikana katika mbuga zetu za wanyama.
Masokwe wengi wanapatikana katika Mbuga
ya Wanyama ya Volcanoes (Volkano).
Nyani ni mnyama wa jamii ya sokwe na tumbiri.
Nyani ni mdogo kuliko sokwe lakini ana akili nyingi zaidi.
Ana masikio makubwa nao mwili wake una rangi ya kaki ya
kijivu na ngoko nyekundu makalioni. Nyani huishi katika
vikundi vya majike na madume. Wana uwezo wa kuishi
kwa miaka zaidi ya arubaini.
Pia kuna tumbiri porini. Tumbiri ni mnyama mdogo
zaidi katika jamii ya nyani. Tumbiri hupenda sana
kukaa mitini. Hula vyakula mbalimbali kama vile
matunda, mazao ya mimea mbalimbali na kadhalika.
Simba ni mnyama mkubwa wa jamii ya paka.
Simba hula nyama. Anaitwa mfalme wa wanyama
au nyika. Simba huishi kwenye vikundi. Vikundi
hivyo huongozwa na simba dume.
Ndovu ndiye mnyama mkubwa zaidi wa porini.
Ndovu ana mkonga pamoja na pembe mbili
kubwa zenye thamani. Ndovu wana masikio
makubwa na miguu mifupi minene. Ndovu hula
nyasi, mizizi, matunda na mashina ya miti. Pia,
huishi katika vikundi. Kila kikundi huongozwa na
ndovu jike ambaye ana umri mkubwa zaidi kuliko
wote. Uwindaji wa ndovu na kuuza pembe
zake ni hatia. Sisi sote tunafaa kuwatunza ndovu na wanyama wote wa porini.
Chui pia hupatikana katika mbuga zetu. Chui ni
mnyama wa jamii ya paka lakini aliye mkubwa na
mkali na mwenye madoadoa ya manjano na meusi.
Chui hula wanyama wadogo wadogo wanaoishi porini.
Baada ya kuwinda, wao huficha nyama kwenye matawi
ya mti. Wao hupenda sana kutembea na kuwinda wakati
wa usiku na kupumzika wakati wa mchana.
Pundamilia pia ni mnyama wa porini wa jamii ya farasi.
Ana milia myeusi na myeupe katika mwili mzima.
Inaaminika kuwa milia hiyo huwawezesha kujificha
nyikani ili wasionekana na wanyama wanaowawinda.
Pundamilia hutembea na kula nyasi katika vikundi vikubwa.
Twiga naye ana shingo ndefu, rangi ya kahawia na madoadoa meusi.
Twiga ndiye mnyama mrefu zaidi. Yeye hula majani ya miti.
Kifaru pia hupatikana katika mbuga zetu. Ni mnyama
mkubwa afananaye na kiboko na mwenye kipusa usoni.
Nyati pia ni mnyama mkubwa sana. Hufanana na ng’ombe. Pembe zake zimepinda kwa mbele. Nyati hula nyasi. Wao pia huishi katika vikundi kutegemea jinsia. Nyati pia huitwa mbogo.
Swara ni mnyama mdogo anayefanana na mbuzi.
Swara anaweza kukimbia haraka. Yeye hula nyasi.
Wanyama hawa wa porini hupatikana katika mbuga zetu kama vile Akagera,
Nyungwe na Volcanoes. Wanyama hawa ni vivutio vikubwa vya watalii wanaotoka
ndani na nje ya nchi yetu.
Maswali
1. Andika orodha ya majina ya wanyama wa porini wanaokula:
a) nyama
b) nyasi
2. Eleza tofauti zilizopo kati ya sokwe na nyani.
3. Jaza kila pengo kwa jina sahihi la mnyama wa porini.
a) Mwenye tamaa kama______________.
b) _________ ana mkonga na pembe mbili.
c) _______ haoni kundule.
d) Ndovu pia huitwa_____________.
e) Nimemwona mnyama mwenye milia myeusi na myeupe mwilini.
Nimemwona__________.
4. Tunga sentensi sahihi ukitumia majina haya ya wanyama wa porini.
a) pundamilia b) simba c) tumbir
id) swara e) nyati f ) ndovu
5. Taja majina ya wanyama hawa:
6. Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Fanyeni utafiti kuhusu majina na sifa
za wanyama wa porini wanaopatikana ndani na nje ya Rwanda na ambao
hawajatajwa katika ufahamu.
ii) Umuhimu wa wanyama wa porini nchini Rwanda
Kufikia sasa, umesoma mengi kuhusu wanyama wa porini. Wanyama hao wana
umuhimu mbalimbali.
Tazama mchoro huu na usome kifungu chini yake.
KANYANA: Karibuni katika mbuga yetu ya Volcanoes.
UWASE
na HIRWA: Asante.
KANYANA: Hapa, mtaona wanyama wengi wa porini.
UWASE: Wanyama hao wana umuhimu gani?
NGABO: Wanyama hao wana umuhimu mkubwa sana kwa nchi hii yetu ya
Rwanda. Wanyama hao kama vile masokwe ni vitega uchumi. Kila
mwaka, watalii kutoka nchi za mbali huja hapa kwetu kuwaona
wanyama. Wajapo hivyo, huja na pesa za kigeni ambazo huinua sana
uchumi wetu.
KANYANA: Nyinyi pia ni watalii wetu hapa. Pesa mnazolipa mkiingia hujenga
uchumi wetu. Pesa hizo pia hutumiwa kutulipia mshahara. Mimi na
wenzangu tumeajiriwa kwa sababu ya wanyama wa porini.
HIRWA: Je, nchi yetu hunufaika na pesa za kiingilio peke yake?
NGABO: Hapana. Wageni wanapokuja, wanaleta manufaa mengi zaidi. Wao
hulipia huduma mbalimbali. Kwanza kuna malazi yao. Sisi
huwakaribisha katika hoteli kubwa kubwa na nzuri nzuri. Hoteli
hizo zimepanuka na kuwaajiri watu wengi kwa sababu ya wageni
hao wanaokuja kuangalia wanyama wa porini. Wageni hao pia
hulipia usafiri wao uwe ni wa ndege au gari. Usafiri huo huwapeleka
huko wanakopenda kwenda kuwaona wanyama.
KANYANA: Mbali na hayo, zipo bidhaa nyingi sana za hapa ambazo watalii hao
hununua kuwa ni ushahidi kwao kwamba kweli walikuwa hapa. Kwa
njia hiyo pia nchi hufaidika kiuchumi.
UWASE: Mbali na faida hizo za kifedha, zipo faida gani tena za wanyama hawa?
NGABO: Wanyama hawa hukuza elimu yetu. Wanafunzi, na hata watu wazima
huzuru mbuga zetu za wanyama ili kuwaona na kujifunza mengi
kuwahusu.
KANYANA: Isitoshe, wanyama wa porini ni hazina kwa vizazi vyetu vya baadaye.
Sisi sote tumewaona wanyama hawa. Vivyo hivyo, litakuwa jambo
zuri sana ikiwa wanetu, wajukuu, watukuu, vilembwe na hata
vilembwekeza wetu kuwaona wanyama wa porini pia. Hii ndiyo
sababu ya serikali yetu kuwatunza na kuwalinda wanyama wa porini.
UWASE
na HIRWA: Asanteni kwa maelezo yenu.
Maswali
1. Taja faida za wanyama wa porini.
2. Taja njia mbili ambazo serikali hutumia kuhifadhia wanyama wa porini.
Kazi ya kikundi
Jiunge na wanafunzi wenzako. Jadilianeni kuhusu umuhimu wa wanyama wa porini nchini Rwanda.
D . Matini ya Kiswahili kuhusu kilimo na ufugaji pamoja na vipengele vya kisarufi
Nomino
Je, unakumbuka maana na aina za nomino ulizosoma katika kidato cha kwanza?
Zitaje.
Nomino ni neno linalotaja mtu, kitu, hali au jambo. Zipo aina mbalimbali za nomino.
Zifuatazo ni baadhi ya nomino hizo.
a) Nomino za pekee
Nomino za pekee hutaja vitu au watu wenye sifa za kipekee. Zinapoandikwa katika
sentensi, lazima zianze kwa herufi kubwa hata zikiwa katikati au mwishoni mwa
sentensi. Kumbuka hapa ya kuwa majina haya hayachukui hali ya wingi.
Mifano ya nomino za pekee katika sentensi.
i) Rwanda ni nchi yenye wanyama wengi wa porini.
ii) Mukangango ananyoa sufu ya kondoo.
iii) Mwenyezi Mungu atujalie mvua nyingi ili tulime.
iv) Kigali ni jiji linalopendeza.
Zoezi
a) Andika sentensi sahihi ukitumia nomino hizi za pekee:
i) Munyana ii) Kamana iii) Mola
iv) Mei v) Mto Kivu vi) Msitu wa Nyungwe
b) Tambua makosa katika sentensi hizi na uyarekebishe.
i) Mimi na kayitesi tunapenda somo la kilimo.
ii) Nitavuna mihogo yangu mwezi wa februari.
iii) Ng’ombe anaitwaje kwa kinyarwanda?
b) Nomino za kawaida
Nomino za kawaida hutaja vitu vya kawaida vinavyoweza kuchukua umoja na
wingi kama jina lolote lile. Nomino hizo zinapoandikwa, huchukua herufi ndogo
isipokuwa pale zinapojitokeza mwanzoni mwa sentensi.
Mifano ya nomino za kawaida:
i) Nomino za viumbe wenye uhai:
ii) Nomino zinazomtambulisha mtu na kazi yake:
iii) Nomino za vitu vya kawaida
iv) Nomino za mahali: shambani, uwanjani, mbugani, zizini, porini
Kumbuka hapa kuwa nomino hizi za mahali huundwa kwa kuongeza ‘ni’ mwishoni
mwa nomino husika.
Mifano ya matumizi ya nomino za kawaida katika sentensi.
i) Mavuno ya mwaka huu ni mazuri.
ii) Niletee jembe hilo.
iii) Sufu za kondoo hutumiwa kutengenezea sweta.
iv) Mkulima hodari hupata mazao mengi.
v) Ndovu ni mnyama mkubwa wa porini.
Zoezi
Tunga sentensi kumi sahihi ukitumia nomino za kawaida.
c) Nomino za jamii
Nomino za jamii pia huitwa nomino za makundi. Hizi ni nomino ambazo hutaja
jumla ya vitu vingi au vitu katika makundi.
Mifano ya nomino za jamii:
Mifano katika sentensi
i) Makole ya ndizi yamevunwa.
ii) Matuta yamepigwa shambani.
iii) Matita ya kuni yatatumika kuchomea nyama.
iv) Mitumba ya aina hii haifai wakulima.
v) Bunge letu limetenga pesa nyingi kwa wizara ya kilimo.
vi) Baraza la wafuga farasi limevunjwa.
vii) Hili ni robota la pamba.
Zoezi
Fanya utafiti kupata nomino kumi zaidi za jamii. Tunga sentensi ukitumia kila
nomino hizo katika umoja na wingi.
d) Nomino za dhahania
Katika kikundi hiki hupatikana nomino ambazo ni za kufikirika tu na wala
haziwezi kuguswa. Chukua nomino kama urafiki. Urafiki ni neno la kufikirika au
kudhaniwa tu na wala haliwezi kuonekana wala kushikika. Nomino hizi haziwezi
pia kuhesabika.
Mifano katika sentensi
i) Upanzi hufanywa mvua inapoanza kunyesha.
ii) Kilimo kinasaidia kumaliza umaskini nchini Rwanda.
iii) Ushirikiano wao katika kupalilia unawafaidi.
iv) Fikira za wafugaji hao ni za hekima.
v) Tutafanya uvunaji mwezi ujao.
Zoezi
Tunga sentensi zozote kumi kuhusu kilimo na ufugaji ukitumia nomino za jamii.
e) Nomino za wingi
Hizi nazo ni nomino za vitu ambavyo daima hupatikana kwa wingi pekee au umoja
pekee. Vitu vinavyotajwa na nomino hizi haviwezi kugawika.
Mifano ya nomino za wingi:
maziwa, sukari, chumvi, uji, chai, manukato, mvua na kadhalika.
Mifano katika sentensi:
i) Sukari ni zao la miwa.
ii) Maua yale hutumiwa kutengenezea manukato.
iii) Chai hii ni tamu.
iv) Maji yanyunyiziwayo hapa ni ya mto huo.
Zoezi
Soma kifungu kilichopo hapa chini. Tambua na uanishe nomino mbalimbali kifunguni.
Hapa nchini Rwanda, Mwenyezi Mungu ametujalia mazingira mazuri yenye
kufanikisha ufugaji. Ufugaji ni kazi ya kutunza wanyama, ndege na hata wadudu.
Mfugaji anaweza kufuga wanyama ama wadudu. Ikiwa ni wanyama, anaweza
kutunza ng’ombe, mbuzi, kondoo, farasi, nguruwe, na kadhalika. Ikiwa nia yake ni
kufuga ndege, anaweza kuwatunza kuku, bata na kadhalika. Hata hivyo, akichagua
wadudu huweza kuwafuga nyuki.
Ufugaji una kazi nyingi sana. Kwa mfano, mfugaji wa ng’ombe anapotaka matokeo
ya kuridhisha, itambidi atumie njia za kisasa katika ufugaji wake. Kwanza kabisa, ni
lazima awatafute ng’ombe bora wa maziwa. Ng’ombe hawa huleta mapato ya juu.
Mbali na hayo ni sharti ahakikishe kwamba wanyama wake wana lishe ya kutosha
hasa kwa ng’ombe wanaokaa ndani kwa ndani. Ng’ombe hawa, hasa ng’ombe jike,
wa kukaa ndani kwa ndani hulishiwa zizini na kulala humo humo zizini. Hata hivyo,
ni lazima zizi hilo liwe safi na ng’ombe huyo alale pahali safi. Kukosa kufanya hivyo
ni kukaribisha magonjwa ya namna kwa namna.
Iwapo mfugaji atawalisha wanyama wake vizuri, atafaidika pakubwa. Ataweza
kupata maziwa ya kutosha. Atauza maziwa hayo na kujinunulia bidhaa nyinginezo
kama vile chumvi, sukari, chane za ndizi na kadhalika. Umaskini pia utaisha.
Vivumishi
Je, unakumbuka vivumishi mbalimbali mlivyosoma katika kidato cha kwanza?
Kwa kawaida, kivumishi ni neno linaloongezea nomino maana. Zipo aina mbalimbali za
vivumishi. Baadhi ya vivumishi hivyo ni:
a) Vivumishi vya sifa
Haya ni maneno yatajayo tabia au sifa za kitu, mtu ama jambo.
Zipo aina mbili za vivumishi vya sifa: vivumishi vya sifa vinavyochukua viambishi na
vivumishi vya sifa visivyochukua viambishi.
Mifano ya vivumishi vya sifa vinavyochukua viambishi:
-aminifu -zuri
-pana -kubwa
-pya -dogo
-bovu -fupi
Kumbuka kuwa kiambishi au viambishi vinavyochukuliwa na vivumishi hivi hutegemea ngeli.
Mifano katika sentensi:
ii) Vivumishi vya sifa visivyochukua viambishi
Hivi ni vivumishi ambavyo havibadiliki katika umoja na wingi au kutoka ngeli moja
hadi nyingine; hubakia jinsi vilivyo.
Mifano: bora, safi, hodari, bandia, haba, duni, laini na kadhalika.
Mfano katika sentensi.
Zoezi
a) Tunga sentensi sahihi kuhusu kilimo na ufugaji katika umoja na wingi ukitumia vivumishi hivi vya sifa.
i) -baya ii) -fupi iii) -dogo
iv) -ingi v) -chache
b) Tunga sentensi sahihi ukitumia vivumishi hivi katika umoja na wingi.
i) bora ii) dhalimu iii) duni
iv) tele v) laini
c) Andika sentensi hizi katika umoja au wingi.
i) Nipe ndizi chache.
ii) Mhindi mrefu unafaa.
iii) Farasi wakubwa watatubeba.
iv) Zizi safi halileti magonjwa.
v) Upanzi bora ni huu.
vi) Mkulima nadhifu anapita.
d) Tunga sentensi zozote kumi kuhusu wanyama wa porini na kilimo zenye
vivumishi vya sifa katika umoja na wingi.
b) Vivumishi vya pekee
Vivumishi vya pekee hutoa habari kuhusu nomino au kiwakilishi chake kwa njia ya
kipekee. Vivumishi vya peke ni sita katika Kiswahili kama ifuatavyo:
i) -enye
Huonyesha hali ya ‘kuwa na’ au ‘kumiliki’. Ni sharti kivumishi hiki kifuatwe na nomino wala si kitenzi.
ii) -enyewe
a) Hutumika mwanzoni mwa sentensi kuonyesha jambo au kitu kinachotarajiwa.
b) Hutumika mwishoni mwa sentensi kuonyesha kuwa jambo limetokea bila
kusababishwa na yeyote au chochote.
iii) -ote
Huleta maana mbili:
a) Kuonyesha kila sehemu ya kitu hasa katika umoja.
b) Kuonyesha kila kitu; bila kubakisha lolote hasa katika wingi.
Zoezi
Eleza maana ya sentensi ikiwa ni ‘kila sehemu’ au ‘kila kitu’.
i) Zizi lote limefagiliwa.
ii) Mazao yote yamevunwa.
iii) Paka amekunywa maziwa yote.
iv) Ndizi yote imeiva.
v) Simba wote wamepita.
iv) -o-ote
Huonyesha mojawapo ya vitu au baadhi ya vitu bila kubagua.
Zoezi
Tumia ‘-ote’ au ‘-o-ote’ pamoja na viambishi sahihi vya ngeli kujazia pengo katika sentensi zifuatazo.
1. Nitatumia jembe _____ nitakalopewa.
2. Miharagwe _________ imemea.
3. Kuku ______ wamepewa chakula.
4. Sitachukua nanasi ____________.
5. Fyeka nyasi____________.
v) -ingine
Kivumishi hiki cha pekee huweza kuwa na maana tatu:
a) Kuonyesha kitu tofauti na kile kilichotajwa au kilichopo.
b) Kuonyesha kitu zaidi/nyongeza
c) Kuonyesha ‘baadhi ya’
vi) -ingineo
Kivumishi hiki hutumika kuleta maana mbili:
a) 'zaidi ya'
b) Kuonyesha hitimisho ya orodha ambayo haikukamilika.
Zoezi
a) Tumia ‘-ingine’ au ‘-ingineo’ pamoja na viambishi sahihi vya ngeli kujazia mapengo.
i. Amevuna mananasi ____________.
ii. Sitaki panga hili, nipe panga _____________.
iii. Mama amepanda mbegu za maharagwe, mtama, mahindi na _____________.
iv. Usiwakame ng’ombe __________. Maziwa haya yametosha.
v. Mpe migomba hiyo na ______________.
b) Tunga sentensi tano sahihi kuhusu kilimo na ufugaji katika umoja na wingi
ukitumia nomino zozote na kivumishi cha ‘-ingine’.
c) Tunga sentensi tano sahihi kuhusu wanyama wa porini na mifugo katika
umoja na wingi ukitumia nomino zozote na kivumishi cha ‘-ingineo’.
c) Vivumishi vionyeshi
Vivumishi vionyeshi au viashiria ni maneno ya kuonyesha alipo mtu au kitu, yaani
ujirani. Kuonyesha huko kunaweza kuwa kwa ujirani wa karibu – hapa, ujirani wa
mbali kidogo – hapo, na ujirani wa mbali – pale.
Mifano ya vivumishi hivi ni hii ifuatayo:
Mfano katika sentensi:
i) Kijijini humu mna mfugaji hodari.
ii) Hizi juhudi zenu za kulima zitamaliza umaskini.
iii) Ng’ombe wale wanakunywa maji.
iv) Fyekeo hilo halikati majani.
v) Shambani pale pamepaliliwa.
i) Vivumishi vionyeshi radidi
Vivumishi hivi hutokana na kurudia vivumishi vionyeshi. Huleta maana ya kutilia mkazo.
ii) Vivumishi vionyeshi visisitizi
Hutumiwa kusisitiza jambo.
Zoezi
a) Jaza kila pengo kwa vivumishi sahihi vilivyowekwa katika mabano.
i. Mazao __________ yatajaza guni. (vionyeshi visisitizi vya karibu)
ii. Mkulima _________ analima. (vionyeshi vya mbali)
iii. Twiga __________ ni wengi. (vionyeshi viradidi vya mbali kidogo)
iv. Nyama __________ ni tamu. (vionyeshi vya karibu)
v. Wafugaji _________ wana bidii. (vionyeshi vya mbali kidogo)
b) Tunga sentensi tano tano kuhusu kilimo na ufugaji katika umoja na wingi
ukitumia vivumishi vionyeshi, vivumishi vionyeshi rejeshi na vivumishi
vionyeshi visisitizi.
d) Vivumishi vya idadi
Vivumishi vya idadi ni maneno yanayoonyesha idadi ya watu ama vitu.
Vipo vivumishi vya idadi kamili, vivumishi vya idadi ya jumla na vivumishi
vya idadi ya matokeo.
i) Vivumishi vya idadi kamili
Pia huitwa vivumishi vya idadi halisi au bainifu. Huonyesha hesabu halisi ya nomino
husika.Baadhi ya vivumishi hivi huchukua viambishi vya ngeli kutegemea nomino
inayohesabiwa.
Mfano: -moja, -wili, -tatu, -nne, -tano na -nane.
Baadhi ya vivumishi vya idadi kamili havichukui viambishi vyovyote vya ngeli.
Yaani hutumika jinsi vilivyo bila kubadilika.
Mfano: sita, saba, tisa na kumi, makumi, mia na kadhalika
ii) Vivumishi vya idadi ya jumla/isiyo kamili
Huonyesha idadi ambayo ujumla wake haujulikani. Baadhi ya vivumishi hivi
huchukua viambishi vya ngeli ya nomino.
Mfano: -chache na –ingi
Mfano katika sentensi:
1. Kuku hawa wametaga mayai machache.
2. Mwaka huu tumepanda mbegu nyingi.
3. Wakulima wengi wamevuna.
4. Wao huuza maziwa mengi sana.
Baadhi ya vivumishi vya idadi ya jumla havichukui viambishi vya ngeli.
Yaani hubakia vivyo hivyo.
Mfano: kadhaa, tele, kiasi, kidogo na haba.
iii) Vivumishi vya idadi ya matokeo
Pia huitwa vivumishi vya nafasi katika orodha. Vivumishi hivi huonyesha nafasi ya
nomino katika orodha.
Zoezi
a) Jaza kila pengo kwa kivumishi sahihi katika mabano.
i. Sungura ________ wanakimbia. (chache)
ii. Masokwe __________ wanacheza. (sita)
iii. Mkulima __________ atapewa mbolea. (moja)
iv. Amenunua maembe_________. (ingi)
v. Tumelima mashamba___________. (nane)
b) Tunga sentensi kumi sahihi kuhusu kilimo na ufugaji ukitumia vivumishi vya
idadi jumla na isiyo jumla.
e) Vivumishi viulizi
Hili ni kundi la vivumishi ambalo lina maneno yatumiwayo kuulizia maswali.
Baadhi ya mifano ya vivumishi viulizi ni:
i) Kiulizi -pi?
ii) Kiulizi -ngapi?
iii) Kiulizi gani?
Kiulizi hiki hakichukui kiambishi chochote cha ngeli.
Tanbihi
Kivumishi kiulizi kinastahili kuandamana na nomino au kiwakilishi cha nomino.
Viulizi ambavyo havitumiwi pamoja na nomino au viwakilishi vya nomino haviwezi
kuitwa vivumishi bali ni viulizi.
Mfano: lini, nani, nini, vipi. Hivi si vivumishi viulizi kwa sababu havitumiwi pamoja
na nomino au kiwakilishi cha nomino.
Zoezi
a) Tumia kiulizi ‘-pi’ kwa usahihi kujazia kila pengo.
i. Mashirika _________ yanasaidia wakulima?
ii. Mkahawa __________ unakatwa?
iii. Dawa _________ zinanyunyiziwa mimea?
iv. Niwaite wafugaji ________?
v. Kufyeka _______ kunafaa?
b) Tumia kivumishi kiulizi ‘-ngapi’ kwa usahihi kujazia kila pengo.
i. Tukupe magunia __________?
ii. Pembe _________ zimekatwa?
iii. Mbwa _________ wamechanjwa?
iv. Mipera ___________ inapandwa?
v. Vibuyu _________ vina maziwa?
f) Vivumishi vimilikishi
Maneno katika kundi hili la vivumishi hujibu swali mtu, kitu au jambo ni la nani au
lina nini? Vivumishi hivi huwa sita pekee katika Kiswahili.
-angu -etu
-ako -enu
-ake -ao
Kutokana na haya, unapata maneno kama vile:
wangu wetu
chako chenu
kwake kwao
Unaweza kutunga sentensi hizi ukitumia vivumishi vimilikishi:
1. Jibini hii ni yangu.
2. Mawele yako yameliwa na fukusi.
3. Mbatata zenu zinauzwa Zambia.
4. Njugu za kwao ni tamu mno.
5. Huwezi kusema kuwa huu ni mchicha wako!
Zoezi
Jaza kila pengo kwa kivumishi kiwakilishi sahihi.
1. Nyinyi mna mihogo. Mihogo ni ___________.
2. Sisi tuna maembe. Maembe ni _____________.
3. Wao wana sufu. Sufu ni _____________.
4. Mimi nina sukari. Sukari ni ____________.
5. Yeye ana kole la ndizi. Kole ni __________.
6. Wewe una muhogo. Muhogo ni _____________.
Kazi ya wanafunzi wawili wawili
Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Someni kifungu kifuatacho huku mkitambua jinsi
vivumishi vilivyotumiwa.
Mimi ni mwanafunzi mwenye bidii. Nia yangu kuu maishani mwangu ni kuridhika
na shughuli za kilimo cha kisasa kama mojawapo ya njia nzuri za kupigana dhidi
ya umaskini. Lengo langu kuu la kwenda shuleni hasa ni kupata maarifa mema ya
kuniwezesha kuishi maisha ya kitajiri. Maarifa hayo yataniwezesha kuwa mkulima
bora.
Nitaendelea na masomo hadi chuo kikuu. Nitafanya somo la Kilimo katika chuo
kikuu. Hata hivyo, hilo pekee halitatosha. Nitafanya kazi ndogo ndogo kwa muda
ili kutafuta pesa za kuanzisha kilimo. Kufikia hapo, nitakuwa nimepiga hatua lakini
bado sitakuwa nimefikia lengo langu.
Kuanzisha kilimo cha kisasa kutakuwa ni hatua kubwa lakini bado kutakuwa
na kazi kubwa ya kufanywa. Ni sharti niupige vita vikali umaskini kupitia kilimo
hicho. Umaskini ni adui mbaya ambaye lazima niangamize. Njia moja ya kumaliza
umaskini ni kuweka uvivu kando.
Mbali na kulima, nitafuga mifugo wengi. Nitahakikisha ya kuwa nina vifaa vyote
vinavyohitajika kwa kufanyia kazi hizo mbili. Kutakuwa na trekta kubwa kubwa
na mashine za kukamua. Nitanunua magari mazuri ya kusafirisha mazao mengi
nitakayovuna. Nitawapa vijana wenzangu kazi ili nao wawe na kipato kizuri. Kwa
jumla, nitahakikisha kuwa vitu vyote anavyohitaji mkulima wa kisasa vipo.
Mwisho, nitatafuta masoko mazuri na ya kuaminika. Nia yangu hapa ni kuuza
bidhaa zangu katika masoko yaya haya ya hapa kwetu. Baadaye nitaziuza katika
masoko, nje ya nchi yetu. Hizi zote zitakuwa ni juhudi za kuendeleza vita vikali dhidi
ya umaskini au uchochole.
Zoezi
1. Orodhesheni vivumishi vyote vilivyomo kifunguni humu kwa kuzingatia aina
ya kila kivumishi husika.
2. Tunga sentensi fupi fupi na sahihi ukitumia vivumishi mlivyoorodhesha hapo juu.
Viwakilishi
Viwakilishi ama vibadala ni maneno ama viambata (sehemu za maneno)
vinavyosimama badala ya majina. Kundi hili la maneno huweza kugawika katika
sehemu mbalimbali ifuatavyo.
a) Viwakilishi nafsi
Husimamia nafsi za nomino inayozungumziwa katika umoja au wingi. Kuna aina
mbili kuu za viwakilishi vya nafsi:
i) Viwakilishi nafsi huru
Huwakilisha nafsi iliyo huru, yaani isiyounganishwa na kitenzi katika umoja na
wingi kwenye sentensi.
Mfano: nafsi ya kwanza (mimi, sisi), nafsi ya pili (wewe, nyinyi), nafsi ya tatu (yeye, wao).
Zoezi
Umoja Wingi
1. Mimi ninalima. Sisi tunalima.
2. Wewe unavuna. Nyinyi mnavuna.
3. Yeye anafyeka. Wao wanafyeka.
ii) Viwakilishi nafsi viambata
Viwakilishi hivi huambatanishwa na vitenzi.
Mfano: nafsi ya kwanza (ni-, tu-), nafsi ya pili (u-, m-) nafsi ya tatu (a-, wa-)
ii) Pia, vipo viwakilishi ambata vya ngeli. Navyo ni:
b) Viwakilishi vitokanavyo na vivumishi
Je, unakumbuka vivumishi ulivyosoma hapo juu? Endapo kivumishi husika
kimetumika badala ya nomino, kivumishi hicho kinakuwa kiwakilishi. Nacho
kiwakilishi hicho huchukua jina la kivumishi hicho. Mfano:
i) Viwakilishi vionyeshi
Hutokana na vivumishi vionyeshi. Tazama vivumishi vionyeshi. Unapoondoa
nomino katika vivumishi hivyo, unapata viwakilisihi vionyeshi.
Kumbuka kwamba hufai kutumia nomino na kiwakilishi katika sentensi moja.
ii) Viwakilishi viulizi
Viwakilishi hivi vinatokana na vivumishi viulizi.
iii) Viwakilishi vimilikishi
Viwakilishi hivi hutokana na vivumishi vimilikishi. Tazama mifano hapa chini.
Zoezi A
Tunga sentensi ukitumia viwakilishi mbalimbali.
Zoezi A
Soma kifungu kifungu kifuatacho huku ukitambua jinsi viwakilishi vilivyotumiwa.
Zama hizo, fisi alikuwa jirani ya binadamu aliyependa kulima. Binadamu alimiliki
shamba kubwa la mihogo. Naye Fisi alikuwa mvivu aliyependa kumtembelea
binadamu kwake. Alidhani kuwa huyo binadamu naye alimpendana sana. Hata
hivyo, binadamu hakumpenda sana fisi. Fisi hakupenda kulima bali alipenda sana
kula.
Siku moja jioni, fisi alimuaga binadamu na kusema, “Kesho nitaamkia huku kwako ili uniandalie kiamshakinywa! ”Kwa roho ya ndani, mwanadamu alijisemea, ‘Huyu hapendi kufanya kazi, anapenda tu kula. Kwa nini haoni kuwa simpendi?’Akamwambia fisi, “Labda utanipata, labda utanikosa.”
Fisi kuona kuwa anaweza kukosa mlo alisema, “Basi nitajaribu nije hata mapema zaidi. Kwa namna hiyo tunaweza kula halafu wewe uende shambani. Napenda sana namna unavyopika nyama.” Bila kungoja jawabu, alitoka na kujiendea zake.
Keshoye, mwendo wa saa kumi na moja asubuhi, fisi alibisha hodi kwa mwanadamu. Naye mwanadamu hakusita kumfungulia mlango. Mwanadamu aliazimia kumfunza fisi adabu.
“Karibu, karibu kwangu rafiki yangu,” mwanadamu alijibu.
Naye fisi kwa kusukumwa na njaa yake ya asubuhi pamoja na ulafi wake, alimpita
tu na kuingia ndani. Harufu ya nyama mle ndani ilimfanya fisi ameze mafunda ya mate.
“Karibu, karibu kaa,” mwanadamu alimlaki fisi. “Nipe dakika chache tu na chakula
kitamu na kingi kitakuwa mezani hapa.”
“Basi fanya haraka. Ninakufa kwa njaa,” fisi alisema.
Baada ya muda usiokuwa mrefu vile, mwanadamu alikuwa ameandika meza
kwa kila namna ya nyama ya mifupa. Ohoo! Fisi kuona hivyo, nusura kuirukia
lakini mwanadamu akamzuia kwa kusema, “Bwana fisi, ili leo ushibe vya kutosha,
tumbukiza kila sahani mdomoni mwako na umeze tu bila kutafuna.
”Hata kabla ya mwanadamu kumaliza usemi wake, fisi alikuwa ametumbukiza
sahani mbili kinywani mwake!
“Mbona hiki cha leo ni kikali jinsi hii? Lo! Kinawasha sana! Loooooooooo!”
Fisi alilalamika.
Kumbe mwanadamu alijaza pilipili kwenye nyama. Tangu siku hiyo, fisi hakurudi
tena kwa mwanadamu.
Maswali
1. Je, fisi alikuwa mnyama wa aina gani?
2. Ni kwa nini mwanadamu hakumpenda fisi?
3. Mwanadamu aliikomeshaje tabia mbaya ya fisi?
4. Unadhani ni yapi yaliyompata fisi?
5. Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Bainisheni viwakilishi vyote vilivyomo
katika kifungu mlichosoma hapo juu. Tungeni sentensi sahihi mkitumia
vivumishi hivyo.
Vielezi
Vielezi pia huitwa viarifa. Ni maneno yafafanuayo vitenzi, vivumishi au vielezi
vingine. Mathalan, ukisema Anatembea haraka, neno 'haraka' linaeleza jinsi
anavyotembea mhusika. Kwa hivyo, neno hilo linalokuarifu mengi kuhusu
kutembea ni kielezi.
Maneno haya hujigawa katika vikundi mbalimbali kama ifuatavyo:
a) Vielezi vya namna au jinsi
Haya ni maneno ambayo huarifu jinsi ya kutendeka mambo.
Mfano: sana, bure, kitoto, vizuri, upesi, kwa miguu, kwa bidii, bwe!
b) Vielezi vya wakati
Nayo haya ni maneno yanayofafanua ama kueleza wakati wa kutokea tendo.
Mathalan, ukisema Mgeni alifika jioni neno jioni ni kielezi cha wakati.
Vipo vielezi vya wakati vya aina mbili:
i) Vielezi vya wakati maalumu.
Mfano: Januari, Disemba, Jumamosi, saa tatu, kesho, leo, mtondo na kadhalika.
ii) Vielezi vinavyotaja wakati kwa jumla
Mfano: baadaye, zamani, daima, milele, awali, punde, karibuni, zama hizo.
c) Vielezi vya kiasi/idadi
Vielezi vya kiasi ni namna ya maneno ambayo hufafanua vitenzi kwa kujulisha
limetokea mara ngapi tendo linalotajwa.
d) Vielezi vya mahali
Haya nayo ni maneno ama mafungu ya maneno yanayofafanua panapotokea kitendo.
Mara nyingi, maneno haya huwa ni majina ya mahali.
Zoezi
Jiunge na wenzako watatu na mworodheshe vielezi vyote vilivyomo kifunguni humu
huku mkivitungia sentensi fupi na sahihi.
Gakwerere alikuwa mfugaji mwenye bidii nyingi sana tangu zamani. Mwanzoni,
Gakwerere alikuwa akifuga ng’ombe wa kienyeji. Aliwalisha ng’ombe hao uwanjani
na pembeni mwa mashamba. Hata hivyo, ng’ombe hao hawakuwa wakimpa kiasi
cha maziwa alichotarajia. Angewakamua mara moja tu kwa siku. Alikata shauri
kuanzisha ufugaji wa ng’ombe bora wa maziwa.
Mfugaji huyu aliwapeleka ng’ombe wake wa kienyeji sokoni na kuwauza mnamo
Novemba. Baada ya kuwauza, aliamka alfajiri na kufunga safari ya kuzuru shamba
la kisasa la Nyinawumuntu. Bi. Nyinawumuntu alikuwa mfugaji na mkulima
mashuhuri sana katika eneo hilo alilokaa Gakwerere. Alipofika huko, alimpata
bibiye yupo na wakaanza kupiga bei. Baada ya kukubaliana bei, alinunua mitamba
wawili kwa bei nafuu. Alilipa papo hapo kwa sababu hakutaka kuwa na deni.
Kumaliza hivi tu, yule bibi alimpa Gakwerere gari lake ili alitumie kuwasafirisha
ng’ombe wake. Gakwere alimshukuru kwa wema wake na akawasafirisha hao
mitamba wake hadi kwake.
Alipofika nyumbani kwake, mfugaji huyo alianza kuwalisha ng’ombe wake kwa njia
za kisasa. Kwa kuwa walikuwa wakilishwa kwa lishe bora ya ng’ombe, haukuchukua
muda mrefu kuwapandisha. Muda ulipowadia, walizaa ndama wawili wenye afya
nzuri.
Baada ya muda usio mrefu, Gakwerere alianza kuvuna matokeo ya jasho lake la kila
siku. Hakuamini kiasi cha maziwa alichokuwa akikama kila asubuhi na jioni.
Aliweka akiba kwa muda. Hatimaye, mfugaji huyu alinunua gari. Alitumia gari hilo
kuwatafutia na kuwabebea chakula ng’ombe hao wake wa gredi.
E . Matumizi ya wakati uliopo na uliopita na vitenzi vya silabi moja
i) Matumizi ya wakati uliopo (-na-) na vitenzi vya silabi moja
Wakati uliopo -na-unaweza kuwa katika hali mbili: Hali hizo ni hali yakinishi na hali
kanushi. Hali yakinishi ni ya ukubali na hali kanushi ni ya ukatavu.
Soma sentensi hizi.
Hali yakinishi
Hali yakinishi ni hali ya kukubali. Tazama tena mifano iliyopo hapo juu. Vitenzi
unakufa, anakula, anakunywa, anakuja, anampa na inanyesha vimo katika hali
yakinishi, yaani hali ya kukubali.
Hali kanushi
Nayo hali kanushi ni hali ya kukataa. Itazame tena mifano hapo juu. Vitenzi haufi,
hali, hanywi, haji, hampi na hainyeshi vipo katika hali kanushi, yaani hali ya kukataa.
Unaweza kutunga sentensi zaidi za namna hii kama ifuatavyo:
Kazi ya wanafunzi wawili wawili
Jiunge na mwenzako. Tafuteni vitenzi zaidi vyenye silabi moja katika kamusi huku
mkijadiliana mabadilko ambayo hutokea vitenzi hivyo vinapotumiwa katika hali
kanushi na yakinishi.
ii) Matumizi ya wakati uliopita -li- na vitenzi vya silabi moja
Wakati uliopita huonyesha kuwa kitendo kilifanyika muda mrefu uliopita. Wakati
huu huwakilishwa na -li-. Vitendo husika vinaweza kuwa katika hali yakinishi au
kanushi. Kama ujuavyo, hali yakinishi ni ya kukubali na hali kanushi ni kukataa.
Tazama mifano ifuatayo:
Vitenzi hivyo vipo katika wakati uliopo. Tunaweza kuvigeuza viwe katika wakati
uliopita kwa kuweka ‘-li-‘ mahali pa ‘-na-‘. Tunapofanya hivyo, tunamaanisha kuwa
vitendo hivyo vilifanyika muda au wakati uliopita. Tazama jedwali hili.
Tazama mifano ifuatayo:
Katika jedwali lililopo hapo juu, vitenzi ulikufa, alikula, alikunywa, alikuja, alimpa,
na ilimnyeshea vimo katika hali yakinishi au kukubali kwa wakati uliopita. Navyo
vitenzi haukufa, hakula, hakunywa, hakumpa, haikumnyeshea vimo katika hali ya
kukataa yaani hali kanushi.
Mazoezi ya ziada
Zoezi A
Jiunge na mwanafunzi mwenzako na mworodheshe vitenzi vinane vya silabi moja
huku mkivitungia sentensi sahihi katika wakati uliopita. Sentensi zenu zihusiane na
kilimo na ufugaji. Someaneni vitenzi na sentensi huku mkisahihishiana.
Zoezi B
Jiunge na wanafunzi wenzako katika kikundi. Msomeane tungo au hadithi
mbalimbali zilizopo katika kitabu hiki na vitabu vingine. Mbainishe na kuainisha aina
za maneno katika tungo hizo (vivumishi, viwakilishi na vielezi) kama vinavyotokea
katika umoja na wingi pamoja na matumizi ya wakati uliopo na wakati uliopita.
Maswali ya marudio
li kujikumbusha mengi ya yale uliyojifunza katika sehemu hii, yajibu vilivyo maswali
haya yafuatayo yote.
1. Bila ya kuangalia popote, taja maneno kumi yanayohusu mazao na kumi
yanayohusu ufugaji huku ukiyaeleza.
2. Ipo misimu mingapi hapa Rwanda? Ieleze huku ukirejelea upanzi na uvunaji
wa mimea.
3. Tazama picha zifuatazo. Eleza misimu kulingana na kila mchoro.
4. Tunga sentensi sahihi ukitumia msamiati ufuatao:
a) mahindi
b) ndizi
c) kahawa
d) viazi mviringo
e) maharagwe
f ) njugu
5. a) Jaza kila pengo kwa jina sahihi la kifaa cha kilimo.
i) Ndoli anafyeka shamba kwa ______________.
ii) Mkulima yule anatumia _________ la mkono kulimia shamba lake.
iii) Shamba kubwa hulimwa kwa _______________.
iv) __________ hutumiwa kukata matawi ya miti shambani.
6. Tunga sentensi tano fupi ukitumia vifaa mbalimbali vya kilimo ambavyo vinatumiwa katika eneo utokako.
7. Eleza jinsi unavyopanga kupiga vita uchochole kwa kilimo cha kisasa.
8. Taja majina kumi ya mifugo nchini Rwanda na uyatungie sentensi sahihi.
9. Taja chuo cha kilimo hapa nchini ambacho ungependa kukiingia baada ya
masomo yako huku ukieleza ni kwa nini unakistahi chuo hicho.
10. Eleza umuhimu wa ufugaji katika jamii unapotoka.
11. Zipo tamaduni zozote za kikwenu zihusuzo kilimo na ufugaji? Zitaje
huku ukieleza huo uhusiano.
12. Taja wanyama kumi wa porini wanaopatikana nchini Rwanda.
13. Andika majina na sifa za wanyama wafuatao wa porini:
14. Eleza faida za wanyama wanaoishi porini.
15. Pendekeza njia zinazoweza kutumiwa kuwavutia watalii wanaozuru mbuga
zetu za wanyama wa porini.
16. Eleza maana ya:
a) nomino
b) vivumishi
c) vielezi
d) viwakilishi
17. Huku ukitoa mifano, eleza aina nne nne za:
a) nomino
b) vivumishi
c) vielezi
18. a) Je, vitenzi vya silabi moja ni maneno ya aina gani?
b) Andika mifano minne ya maneno yenye silabi moja na uyatungie sentensi sahihi.
19. a) Huku ukitoa mifano, eleza tofauti zilizopo kati ya:
i) wakati uliopo na wakati uliopita
ii) hali kanushi na yakinishi
b) Andika sentensi zifuatazo katika hali yakinishi au kanushi.
i) Baba anakula mahindi.
ii) Mahindi hayafi wakati wa kiangazi.
iii) Ng’ombe hakunywa maji jana.
iv) Mkulima alimpa ndizi nyingi.
c) Andika sentensi zifuatazo katika wakati uliopo au uliopita.
i) Ndoli anakula mihogo.
ii) Mimi sinywi maziwa.
iii) Mama alinipa jembe.
iv) Kuku hao hawakufa.
20. Kwa ufupi, elezea mambo muhimu uliyojifunza katika sura hii na useme jinsi
yatakavyokufaidi na jamii.