MADA YA 8 DHIMA YA LUGHA YA KISWAHILI KATIKA JAMII
Uwezo mahususi katika mada hii:
Kuonyesha dhima ya lugha ya Kiswahili kwa jamii ya nchi zinazozungumza
lugha hii.
Malengo ya ujifunzaji:
• Kutoa maana na umuhimu wa lugha,
• Kusoma na kuelewa kifungu kuhusu lugha kama chombo cha
mawasiliano,
• Kusikiliza kwa makini na kusimulia kwa ufasaha kifungu cha habari
kinachohusika,
• Kujadili namna ya kuitunza lugha na mwenendo unaofaa.
Kidokezo
1. Taja lugha zote zinazozungumzwa nchini Rwanda.2. Andika dhima nne za lugha ya Kiswahili.
SOMO LA 29: TUONGEE KISWAHILI SANIFU
Kazi ya 1:
Tazama mchoro hapa juu na kujadili kazi mbalimbali zinazoendelea.
29.1. Kusoma na ufahamu: Kiswahili nchini Rwanda
Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha ujibu maswali
yanayoambatana nacho:
Lugha ya Kiswahili ni mojawapo ya lugha nne zinazozungumzwa nchini
Rwanda. Hizi ni Kinyarwanda, Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili vilevile.
Hapo mwanzo, lugha ya Kiswahili ilikuwa lugha ya kibiashara lakini polepole
mambo yalibadilika kutokana na ushirikiano wa Rwanda pamoja na nchi
jirani zake ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo na Burundi zinazotumia lugha ya Kiswahili katika shughuli
mbalimbali.
Lugha ya Kiswahili ambayo ni chombo cha mawasiliano kwa kupashana
habari, nchini Rwanda, imeshamiri na kupata nguvu nyingi baada ya Rwanda
kuwa mwanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, Kiswahili
kikiwemo lugha rasmi.
Lugha ya Kiswahili hufundishwa nchini katika shule za sekondari na vyuo
vikuu. Vituo vya utangazaji habari kama vile redio na vituo vya televisheni
pia hutumia Kiswahili katika baadhi ya matangazo vinavyorusha.
Aidha, lugha ya Kiswahili hutunza, hukuza, na huendelezautamaduniwajamii,
bila ya kusahau kwamba ni alama ya utambulisho wa jamii au taifa fulani.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Ni lugha gani zinazozungumzwa nchini Rwanda ?
2. Kwa sababu gani, nchini Rwanda, lugha ya Kiswahili imekua
sana siku hizi?
3. Onyesha dhima mbili za Kiswahili.
4. Taja shule zinazofundisha Kiswahili nchini Rwanda .
5. Je, lugha ya Kiswahili ni lugha ya mawasiliano nchini? Eleza jibu
lako kwa kutumia mifano sahihi kutoka kifungu.
29.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Toa maana ya maneno yafuatayo:
1. Dhima
2. Ushirikiano
3. Kupashana
4. Maarifa
5. Utamaduni
6. Jamii7. Mzawa
29.3. Sarufi: Matumizi ya hali ya kuamuru
Kazi ya 4:
Tazama michoro hapo juu na kueleza kinachofanyika pale.
Kazi ya 5:
Tunga sentensi tano kwa kutumia hali ya kuamuru.
Maelezo muhimu
• Katika hali ya kuamuru au ya kushurutisha, vitenzi vya silabi zaidi
ya moja na vyenye kiambishi tamati -a, huondolewa tu kiambishi
cha kitenzi ku- katika umoja hali yakinishi. Katika wingi, vitenzi hivi
huondolewa kiambishi ku- pamoja na kiambishi tamati-a, halafu
vikachukua kiambishi -eni badala ya kiambishi -a cha mwishoni.
Mfano:Kitenzi: kusimama
Umoja: (Wewe) Simama!
Wingi: (Nyinyi/ Ninyi) Simameni!
Kazi ya 6:
Zikamilishe sentensi zifuatazo kwa kutumia hali ya kushurutisha
kwa vitenzi ambavyo vimo katika mabano.
Kwa mfano: Swali: Mwalimu aliwaambia wanafunzi: “…….madaftari
yenu”. (kuchukua)
Jibu: Mwalimu aliwaambia wanafunzi: “Chukueni madaftari yenu.”
1. “…………… kazi yako ya shule kuhusu dhima ya Kiswahili.” Mama
alimwamrisha mtoto wake. (fanya)
2. Mwalimu alimwomba mwanafunzi akisema: “…………… ubao
tufanye mazoezi!”(Kufuta)
3. Baada ya kujiunga na nchi nyingine za Afrika Mashariki viongozi
wa Rwanda walituambia: “……… Kiswahili!” (kuzungumza).
4. Kwa kuwa wewe ni mkazi wa nchi ya Rwanda …………. vizuri
lugha ya Kinyarwanda! (ongea)
5. Mwalimu ameniambia kuwa mtafanya jaribio la Kiswahili kesho;
kwa hiyo……… (kurudia) masomo yenu.
6. Mwalimu aliwaambia wanafunzi: “…………..runinga kuna mchezo
wa kuigiza uhusuo uhifadhi wa mazingira!” (kutazama).
7. Katibu aliombwa na mwenyekiti: “……………….mawazo yote
yatakayotolewa mkutanoni!” (kuandika).
8. Kama unataka kukuza stadi zako za kuzungumza na kusikiliza
lugha ya Kiswahili, ……………..matangazo ya redioni na utazame
runinga! (kusikiliza)
29.4. Matumizi ya Lugha: Maana na umuhimu wa lugha
katika jamii
Kazi ya 7:
Panga maneno yafuatayo kwa utaratibu unaofaa ili yaweze kuleta
maana kamili
1. ni -ya -Kiswahili- Mashariki- muhimu -lugha -Jumuia -ya -Afrika
-katika -sana
2. Kiswahili -mwanzoni -kama- lugha -ilikuwa -ya- hapo- biasharalugha-ikitumiwa -ya.
3. Walifurahi- rasmi- Wanyarwanda- kusikia- sana- mojawapo- lugha
ya- nchini- Kiswahili- kwamba- ni- Rwanda- ya- lugha.
Kazi ya 8:
Tunga sentensi kwa kutumia maneno yafuatayo:
1. Jumuiya
2. Utamaduni
3. Matangazo
4. Jamii
29.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Umuhimu wa lugha ya
Kiswahili katika jamii
Kazi ya 9:Jadili kuhusu dhima za lugha ya Kiswahili
29.6 Kuandika: Utungaji wa kifungu cha habari
Kazi ya 10:
Tunga kifungu kifupi (mistari kumi) ukionyesha faida ya Rwanda
kutumia lugha ya KiswahiliSOMO LA 30: MAWASILIANO YETU.
Kazi ya 1:
Eleza kinachofanyika kwenye mchoro wa hapo juu.
30.1. Kusoma na ufahamu: Ziara ya mjini
Soma kifungu cha habari hiki na kujibu maswali yanayokifuata:
Siku moja Bwana Mugisha aliondoka zake kijijini Kirenge kuelekea mjini.
Alichukua mkoba wake mweusi na kuujaza kila kitu cha kumsadia njiani na
mjini vilevile. Alipofika mjini, aliwakuta jamaa wawili mmoja aitwaye Rukundo
na mwingine Ruhara.Walisalimiana kwa hamu kubwa kwani siku zilikuwa
nyingi bila ya kuonana.
Wakati huo huo wasichana watatu Ange, Lidia na Isimbi walipita karibu nao
wakiwa wametoka kabisa. Lugha waliyokuwa wanaongea ilimshangaza
Mugisha sana kwani ilikuwa mara yake ya kwanza kuisikia. « Mbona watu
hawa siwaelewi hata kidogo, wametoka wapi ? » Alitamka haya akiwa
na mshangao mkubwa sana. Ruhara ambaye alizoea maisha ya mjini
alimwambia, ‘’hii ni lugha ya Kiswahili, lugha nzuri yenye asili ya upwa
wote wa Afrika Mashariki.’’ Aliendelea kumsimulia yaliyompata alipokwenda
sehemu za Arusha huko Tanzania. ‘’Miaka miwili iliyopita, nilikwenda mjini
Arusha katika mkutano wa waumini wa dini moja huko, nilipoingia mjini
lugha ilikuwa hiyo, mitaani na migahawani, misikitini na makanisani, kweli
sikuwa na tamko lolote isipokuwa kimya tu na kutumia ishara. Kwa bahati
nzuri, nilipata usaidizi kutoka kwa raia wa huko kwani baadhi yao walijua
lugha nyingi ikiwemo yangu. Baada ya wiki moja, tulirudi kwetu nikiwa na
fikra moja kichwani mwangu ya kujifunza Kiswahili na kukizungumza vizuri.
Leo nina hatua nzuri. ’’
Kuyasikia hayo, Mugisha aliunga mkono Ruhara na kusema kuwa naye
angepata mwalimu angejifunza Kiswahili. Wote waliendelea na safari zao
kwa makubaliano ya kujua lugha zaidi ya moja, msingi wa maendeleo na
ushirikiano na wengine.
Punde si punde mabinti wale Ange, Lidia na Isimbi walimwita Mugisha
ambaye alionekana kuwa mgeni mjini. Walisema ‘’ Mzee njoo hapa, tunahitaji
kuongea na wewe.’’ Mugisha bila kusita alianza mbio kinyumenyume
akihofia kuibiwa au usumbufu mwingine. Yeye aliona wasichana hao kama
wakware ambao wanataka awape pesa zake alizokuwa ameficha mkobani
chini ya nguo. Ange alimfuata kwa hatua ndefu na maneno ya upole, jambo
lililopunguza wasiwasi wake Mugisha na kusimama.
Mazungumzo yalianza katika lugha ya Kinyarwanda Ange na wenzake
wakimwonyesha umuhimu wa lugha kama chombo cha mawasiliano kati
ya jamii fulani. Bwana Mugisha aliwajulisha uamuzi wake ili mara ijayo
asije akakabiliana na shida hiyo tena. Walimfundisha maneno machache
na kumshauri aendelee kuvifuata vipindi vya redio na televisheni katika
Kiswahili. Mugisha aliwaomba namba zao za simu ili kila mara atakapopata
shida au atahitaji msaada awapigie simu. Wasichana walimnunulia chakula
na chai akala na kushiba. Baadaye, kundi la watatu lilimuaga Mugisha. Tangu
siku hiyo, Mugisha hawezi kuidharau lugha na umuhimu wa mawasiliano.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Toa majina ya wahusika katika kifungu cha habari hiki.
2. Mgeni huyu alishangazwa na nini alipofika mjini?
3. Kwa sababu gani Ruhara alikuwa kimya na kutumia ishara tu
alipokuwa mjini Arusha ? Alisaidiwa na nini ?
4. Je, mabinti waliokutana na Mugisha walizungumza lugha zaidi ya
moja ? Fafanua jibu lako.
5. Kwa nini Mugisha alianza kukimbia alipoitwa na wasichana ?
6. Nini kilimridhisha Mugisha katika ziara yake mjini ?
7. Ingekuwa wewe ungefanya nini baada ya kupata shida ya
kimawasiliano ? Jadili.
30.2. Matumizi ya msamiati kuhusu mawasiliano yetu
Kazi ya 3:
Toa kinyume cha maneno haya:
1. Mzee
2. Mji
3. Haraka
4. Lugha nzuri
5. Karibu
Kazi ya 4:
Jaza sentensi hizi kwa kutumia msamiati unaofaa ulioko katika
kifungu
1. Bwana Mugisha alisaidiwa na……………………….wawili
waliomnunulia ………….akala akashiba.
2. Miaka miwili iliyopita ……………..alikwenda mjini……………..
katika …….wa waumini.
3. Ange na ……..waliongea lugha ya………….na lugha ya.....
4. Mugisha alidhani wasichana walikuwa ……………..na kukimbia.
Kazi ya 5:
Eleza maana ya maneno yanayofuata:
a. Mkoba
b. Jamaa
c. Mkutano
d. Kutoka
e. Fikra
f. Binti
g. Mbio
h. Kuaga
Kazi ya 6:
Kamilisha sentensi zifuatazo ili zilete maana kamili kwa kutumia
msamiati huu: lugha, jumuia, televisheni, simu, ishara.
1. Kiswahili ni................................ambayo inatumiwa katika
………………….ya afrika Mashariki.
2. Jamila hufuata vipindi vya………………………kila siku.
3. Wasichana watapigiwa …………………….. na mzee Karinda.
4. Mtu asiye na ujuzi wa lugha lazima atumie……..……………….
30.3. Sarufi: Hali ya kuamuru
Kazi ya 7:
Soma mazungumzo yafuatayo na kubainisha vitenzi vilivyotumiwa
katika hali ya kuamuru
Baba: Waambaje, Nikuze?
Nikuze: Salama babangu. Naona umechoka leo! Tafadhali nenda bafuni.
Baba: Ehee! Leo nimefanya kazi nyingi bila kupumuzika. Nenda ukaniletee
maji na sabuni ya kuogea.
Nikuze: Ndiyo. Jitayarishe, uchukue taulo na kandambili halafu uende
bafuni.
Baba: Asante sana binti yangu. Niandalie chakula haraka iwezekanavyo
nina njaa.
Nikuze: Chakula kimeiva na ninakaribia kukiweka mezani. Nimekupikia
ugali na kitoweo kitamu sana bila shaka utakifurahia. Karibu ndani mama.
Mama: Asante binti yangu. Habari za nyumbani?
Nikuze: Nzuri mama. Baba amekuja akiwa amechoka na hivi sasa yumo
bafuni.
Mama: Ni kweli kabisa. Leo amefanya kazi isiyo rahisi.
Nikuze : Namwona baba anatoka bafuni usisahau kumpa pole kwa
uchovu alio nao.
Mama: Wewe mwekee chakula na kinywaji mezani, mengine ni yangu.
Fanya haraka binti yangu.Nikuze: Barabara kabisa.
Kazi ya 8:
Tunga sentensi tatu kwa kutumia hali ya kuamuru tungo yakinishi.
Kazi ya 9:
Tunga sentensi tatu zenye vitenzi vilivyoko katika hali ya kuamuru
tungo kanushi.
Maelezo muhimu kuhusu hali ya kuamuru / hali ya amri
Hali ya kuamuru ni ya vitenzi ambavyo vimo katika hali shurutishi au ya
kulazimisha yaani mtendaji wa tendo halitendi kwa hiari yake bali ni kwa
sharti ya mtu mwingine.
Huonyesha kuwa mtu analazimishwa kufanya jambo fulani. Hutumiwa kwa
nafsi ya pili tu (umoja na wingi).
Tunafuata kanuni zifuatazo :
• Vitenzi vyenye silabi nyingi, hupoteza ku- ya kitenzi. Kwa wingi, kitenzi
huongezwa «-ni» mwishoni, katika hali yakinishi.
Mfano: Nyamaza! (Umoja)
Nyamazeni! (Wingi)
shukuru! (umoja)
shukuruni! (wingi)
• Katika hali kanushi, vitenzi huishia na «-e» isipokuwa vitenzi vya asili
ya kigeni.
Mfano: Usinyamaze! (Umoja)
msinyamaze! (Wingi)
• Usirudi! (umoja)
• Msirudi! (wingi)
• Vitenzi vyenye silabi moja hubaki na «ku-» ya kitenzi (katika hali
yakinishi) na huongezwa «-ni», kwa wingi.
Mfano: - Kunywa! (umoja)
• Usinywe!
• Kunyweni! (wingi)
• Msinywe!
• Vitenzi: kuja, kwenda (kuenda) na kuleta, havifuati kanuni hizi.
Mifano:
a. Kuja:
Njoo! (umoja hali yakinishi)
Usije! (hali yakinishi)
Njooni! (wingi hali yakinishi)
Msije! (wingi hali kanushi)
b. Kwenda/kuenda :
Nenda! (Umoja hali yakinishi)
Usiende! (Umujo hali kanushi)
Nendeni! (Wingi hali yakinishi)
Msiende! (Wingi hali kanushi)
c. Kuleta:
Lete! (Umoja hali yakinishi)
Usilete! (Umoja hali kamushi)
Leteni! (Wingi hali yakinishi)
Msilete! (Wingi hali kanushi)
d. Kupa:
Nipe! (Umoja hali yakinishi)
usinipe! (Umoja hali kanushi)
Nipeni! (Wingi hali yakinishi)
Msinipe! (Wingi hari kanushi)
Kazi ya 10:
Badilisha sentensi zifuatazo ziwe katika hali ya kuamuru katika wingi.
1. Njoo hapa utusalimu!
2. Kimbia ili usichelewe shuleni!
30.4. Matumizi ya lugha: Mawasiliano yetu
Kazi ya 11:
Jadili maswali yafuatayo:
Mawasiliano ni nini?
Je,ndege na wanyama huwasiliana kwa njia gani?
Mawasiliano yana umuhimu gani ?
Maelezo muhimu
Mawasiliano ni mchakato wa kuhawilisha taarifa kwa njia ya ubadilishanaji wa
mawazo, hisia, malengo, tabia, matarajio, mitazamo kupitia mazungumzo,
ishara na maandishi. Ni ubadilishanaji wa taarifa unaoleta maana baina ya
pande mbili au zaidi ambazo zinaweza kuwa viumbe hai au kinyume chake.
Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na
kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo
wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za
lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule
isipokuwa mwanadamu.
Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana, mawasiliano
yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa
yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa.
Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuzitumia katika
mazingira yake na kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano,
ukimchukua paka wa Uchina na kumleta Rwanda atatoa sauti ile ile sawa
na paka wa Rwanda kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.
Ulishawahi kujiuliza kwamba mawasiliano yangekuwaje pasipokuwepo
lugha? Mwalimu angekuwa anatumia mtindo gani kukufundisha darasani au
wewe ungemwombaje kalamu rafiki yako? (Unasema ungewasiliana kama
wanavyowasiliana watu wasiosikia au kuzungumza?) Hao pia wanawasiliana
hivyo kwa sababu wana maarifa ya lugha. Watu wasiosikia au kuzungumza
wanawasiliana kwa lugha ya ishara, lugha ambayo inafundishwa katika
baadhi ya shule za sekondari na vyuo vikuu nchini Rwanda.
Ufumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia usingewezekana pasipo kuitumia
lugha, usingeweza kusogoa na marafiki zako kwenye fesibuku, usingeweza
kumwandikia ujumbe rafiki yako kupitia simu yako na kadhalika. Kiswahili
kinatarajiwa kutumika kama chombo cha mawasiliano katika taaluma
mbalimbali kama vile utawala na taasisi mbalimbali kama vile bungeni,
mahakamani na penginepo.
Kazi ya 12:
Jibu maswali yafuatayo:
1. watu wasiosikia au kuzungumza huwasiliana kwa njia ipi?
2. Ni tofauti gani kati ya mawasiliano ya binadamu na yale ya viumbe
wengine?
3. Andika njia nne ambamo Kiswahili kinaweza kutumiwa na
kurahisisha mawasiliano.
Kazi ya 13:
Pamoja na picha hizi, sema ikiwa kuna mawasiliano ya lugha, yaishara au ya sauti na kujaza jedwali hapo chini:
30.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
Kazi ya 14:
”Mawasiliano ya lugha ni bora kuliko mawasiliano ya ishara na
sauti.” jadili kauli hii.
30.6. Kuandika: Utangaji wa insha
Kazi ya 15:
Tunga insha fupifupi ukionyesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili
nchini Rwanda.
Kazi ya 16:Andika aya mbili kuhusu “umuhimu wa mawasiliano.”
SOMO LA 31: UMUHIMU WA LUGHA
Kazi ya 1:
Eleza yale unayoyaona kwenye mchoro huu.
31.1. Kusoma na ufahamu: Umuhimu wa lugha
Soma kifungu kifuatacho kuhusu “Umuhimu wa lugha” kisha, jibu
maswali uliyopewa hapo chini.
Familia ya mzee Yakobo inaishi katika kijiji cha Nyamugari. Kila mara Mzee
Yakobo huwahimiza watoto wake Maria na Maria kujifunza lugha mbalimbali
kwa madhumuni ya maisha yao ya usoni. Yeye anajua kwamba lugha, kama
mfumo wa ishara au sauti nasibu zinazowezesha jamii kuwasiliana, ina
umuhimu sana katika maisha ya kila siku. Tangu Maria alipoyasikia maneno
ya baba yake aliyazingatia sana mawaidha aliyopewa na kujifunza vizuri
lugha zote zilizopatikana kwenye ratiba yake ya masomo. Kwa sasa, yeye ni
mkuu wa kitengo cha utalii katika taasisi inayoshughulikia masuala ya utalii na
mazingira. Petro ni tofauti na ndugu yake Petro aliyeonyesha mtazamo hasi
kuhusu ujifunzaji wa lugha. Yeye alipenda kusema: « Siwezi kupoteza muda
wangu kujifunza lugha za watu wengine, lugha ninayozungumza inanitosha».
Kwa kweli, alikuwa mtoto mtukutu asiyejali maonyo na mawaidha ya wazazi
wake. Kwake, kujisomea hata sentensi fupi za Kiswahili lilikuwa jambo la
ajabu! Alikuwa amesitisha masomo yake alipomaliza darasa la pili katika
shule ya Sekondari ya Nyamugari ingawa baba yake hakuacha kumuonya
kuhusu umuhimu wa elimu na nafasi ya lugha katika maisha ya binadamu.
Siku moja, Mzee Yakobo aliamua kwenda kumtembelea binti yake aliyeishi
katika nchi jirani. Petro alimsihi waende pamoja kuwasalimia binamu zake
ambao ni Kamugisha na Kana. Mzee Yakobo aliposikia maneno ya mtoto
wake, hakusita kukubali wazo lake. Alifikiria kwamba mtoto wake angekutana
na binamu zake wangemuuliza mengi kuhusiana na masomo yake. Kwa
hivyo, Mzee Yakobo alimwomba mtoto wake Petro ajiandae kwa safari.
Gari lao lilitoka Nyabugogo saa kumi na moja alfajiri. Walipofika njiani, Petro
alishindwa kuvumilia njaa iliyokuwa ikimuuma kutokana na safari ndefu. Kwa
bahati nzuri, walipofika katika mji mmoja, dereva aliamua kusimamisha gari
ili wasafiri waweze kwenda haja na wengine waweze kujinunulia chakula na
kinywaji kabla hawajaendelea na safari yao. Baba yake Yakobo alimwonea
huruma mtoto wake na kumpa shilingi mia mbili ili aweze kwenda kujinunulia
chakula. Petro alifurahi sana. Alikuwa na hamu ya kula mkate na kunywa
juisi ya matunda iliyotengenezewa katika nchi jirani. Alienda haraka na
kuingia dukani. Dukani alimkuta Bi Hassani aliyemkaribisha na kumuuliza
alichotaka kununua dukani humo.
Lo ! Petro alikosa neno. Alisimama akimkodolea macho kama aliyejiingiza
baharini bila kujua kuogelea. Kweli alishindwa kuulizia kile kilichomleta
pale. Alijitahidi kutumia ishara kumwonyesha sehemu palipowekwa mikate
na vyakula vingine lakini mfanyabiashara hakuelewa alichokuwa anahitaji
miongoni mwa vyakula vilivyokuwemo dukani. Petro aliposhindwa kusema
alichukua shilingi zote alizokuwa nazo na kumkabidhi Bi. Hassani. Hapo
ndipo alipewa mkate na maji. Petro alipokea kwa shingo upande alichopewa
na mwenye duka na kurudi haraka na kuziacha shilingi mia moja zilizobaki
kwenye jumla ya bei ya mkate na maji. Kama angekwenda shuleni
asingefanyiwa hayo.
Mara moja, dereva alianza kugeuza gari ili waendelee na safari. Petro
alikuwa ameketi kwenye kiti chake karibu na baba yake. “Salaalaa!” Yakobo
alishikwa na bumbuazi alipoona mtoto wake ameleta chakula kilichokuwa
kimepitisha tarehe ya kukila mwaka uliopita. “Wewe hujui kusoma wala
kuhesabu! Tazama tarehe iliyoandikwa hapa! Huoni kuwa chakula hiki
kingepaswa kuliwa kabla ya mwezi uliopita?” Kwa kweli, alianza kujiuliza
mengi kuhusu maisha ya mtoto wake. Alisikitika sana na kumwomba
asithubutu kula chakula hicho kwani kingeweza kuharibu afya yake. Petro
alikunywa maji tu aliyoleta na kuvumilia njaa iliyokuwa ikimbana wakati huo.
Alianza kujuta kwa kutofuata mawaidha aliyopewa na wazazi wake. Alifikiri,
“Nisingepuuza mawaidha ya baba yangu, nisingekutana na matatizo haya”.
Walipofika Dar-es-salaam, walifurahi kuonana na shangazi na binamu zake.
Walipokelewa vizuri na kupata muda wa kutembelea mazingira mazuri ya jiji
hilo. Tangu alipofika, Petro alifuatana na binamu zake kila wakati walipotoka
kununua vitu ili asikilize walivyoweza kuwasiliana na watu wengine katika
lugha ya Kiswahili. Hapo, aliweza kuelewa umuhimu wa kujifunza lugha na
aliamua kwamba angeanza kujifunza kwa bidii mara wakirudi nyumbani. Kwa
sasa, Petro amemaliza kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Museta
ambapo walimu wake wanampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha
ya Kiswahili na lugha nyingine anazojifunza.
Kazi ya 2:
Maswali ya Ufahamu
1. Taja majina ya watu wanaozungumziwa katika kifungu hiki.
2. Ni mawaidha gani mzee Yakobo aliyokuwa anawapa watoto
wake ?
3. Maria amefaidika vipi kutokana na ujuzi wake wa lugha
mbalimbali ?
4. Safari ya mzee Yakobo ilikuwa na lengo gani ?
5. Ni hasara gani aliyoipata Petro aliposhindwa kuwasiliana na
mfanyabiashara ?
6. Eleza tabia za mfanyabiashara Bi Hassani mbele ya mteja wake.
7. Ni jambo lipi lingetokea ikiwa mzee Yakobo hakumkataza mtoto
wake Petro kula chakula alichokinunua ?
8. Petro alikuwa na majuto gani? Kwa nini alijuta?
9. Aliporudi nyumbani alifanya nini?
10. Unajifunza nini kutokana na kifungu hiki cha habari?
31.2. Msamiati kuhusu umuhimu wa lugha
Kazi ya 3:
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo huku ukizingatia
matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu.
1. Kuhimiza
2. Madhumuni
3. Mawaidha
4. Mtazamo
5. Mtukutu
6. Utalii
7. Kwenda haja
8. Kwa shingo upande
9. Bidii10. Bumbuazi
Kazi ya 4:
Oanisha maneno katika sehemu A na maana zake zilizopo katika sehemu B.
Kazi ya 5:
Jaza nafasi kwa kutumia maneno mwafaka yafuatayo: bidii,
madhumuni, kupuuza, maarufu, mawaidha, mtazamo, bumbuazi,
ratiba, kwenda haja, shingo upande.
1. Nilianzisha mradi huu kwa ...................................ya kuhifadhi
mazingira yetu.
2. Kila mwanafunzi analazimishwa kuwa na .........................ya
masomo yake ya kila siku.
3. Usipojifunza kwa............................. basi hutafaulu mitihani yako.
4. Aliposikia habari hiyo alipigwa na ............................... na kukosa
la kufanya.
5. Anaanza kujuta kwa kutofuata ....................................ya baba
yake.
6. Baada ya kufanya safari ndefu, wasafiri wamesimamisha dereva
ili waweze ....................
7. Sikubaliani na ...............................wako kuhusu uhifadhi mwafaka
wa mazingira.
8. Alipokea zawadi hiyo kwa.................................................
9. Amekuwa mchezaji.....................................kutokana na ustadi
wake wa kusakata mpira.
10. Si vizuri ...............................fikra za mwenzako kabla hujamsikiliza.
31.3. Sarufi: Matumizi ya hali ya kuamuru
Kazi ya 6:
Soma kifungu cha habari kifuatacho na kubainisha vitenzi
vilivyotumiwa katika hali ya kuamrisha
Ona kwenye gazeti hili viongozi wa mataifa mbalimbali wamekusanyika
mjini Kigali. Lengo lao ni maendeleo ya lugha yetu. Soma habari yote
uelewe vizuri yanayoendelea pale na usiendelee kusimama kwenye
barabara. Kimbia nyumbani uwashe runinga yako ili uweze kuwaona
na uandike matangazo hayo kwa ufupi. Lakini jaribu kujifunza Kiswahili
kitakuwezesha kushirikiana na jamii, nchi zote za kanda hii hasa hasa
Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kwani Kiswahili ni lugha rasmi.
Kazi ya 7:
Tunga sentensi tano zenye vitenzi mbalimbali katika hali ya kuamuru.
Kazi ya 8:
Tazama picha hizi kisha utunge sentensi katika hali ya kuamurukulingana na vitendo vinavyoendelea kwenye picha hizi:
Kazi ya 9:
Andika vitenzi vilivyopigiwa msitari katika hali ya kuamuru tungo
yakinishi na kanushi:
Nchi yetu ni nzuri sana,ina milima na mabonde,viongozi bora na sehemu
mbalimbali za utalii. Mutesi hutembelea maziwa mengi naye Bugingo
husafisha kwake akipanda maua na miti ili kuhifadhi mazingira. Yeye
huwazuru wenzake akiwashawishi watende mema kila siku. Benita
aliamua kujenga nchi yake kwa kufanya kazi za umuganda, vilevileakiwajengea wasiojiweza na kutengeneza barabara.
Kazi ya 10:
Weka sentensi zifuatazo katika hali ya kuamuru katika umoja na
kuzingatia mabadiliko ya kisintaksia katika sentensi.
a. Sauti ya pili,ingieni tuimbie Bwana.
b. Teteeni maendeleo ya lugha ya kiswahili.
c. Kuleni nyama yote pia osheni vyombo.
d. Lieni kwa sauti ndogo majambazi yasituvamie.
31.4. Matumizi ya lugha: Umuhimu wa lugha
Kazi ya 11:
Soma maelezo yafuatayo, kisha ujibu maswali hapo chini.
Maelezo muhimu: Umuhimu wa lugha
Lugha ni mojawapo ya vipengele vya utamaduni wa jamii na tena ni chombo
cha utamaduni. Hili ni kwa sababu chombo hiki hutumiwa kuwasilisha amali,
mila na desturi zote za jamii. Lugha ndio uti wa mgongo wa utamaduni.
Lengo kuu la lugha katika jamii ni pamoja na kuwafanya watu wawasiliane
kwa kupashana habari. Kujua lugha fulani kunamwezesha mtu kujipatia
marafiki, kukuza ujuzi kwa kusoma maandishi mbalimbali au kwa kufuata
vipindi mbalimbali kwenye redio, runinga na tovuti
Kutumia lugha moja katika jamii kunaweza kuwa na faida pamoja na
hasara mbalimbali kutokana na mazingira ya jamii. Rwanda kama nchi
inayozungukwa na nchi zinazotumia Kiswahili, itanufaika kwa kutumia
lugha ya Kiswahili. Vilevile, lugha ya Kiswahili ina umuhimu mkubwa sana
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ndiyo lugha rasmi
inayotumiwa katika Jumuiya hii.
Maswali:
1. “Lugha ndio uti wa mgongo wa utamaduni.” Eleza.
2. Lipi ni lengo kuu la kuijua lugha?
3. Jadili: “Kutumia lugha moja katika jamii kunaweza kuwa na faida
pamoja na hasara mbalimbali”.
31.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
Kazi ya 12:
Jadili kuhusu mambo yafuatayo:
1. Matatizo yawezayo kujitokeza baina ya watu wawili wanaposhindwa
kusikilizana kimawasiliano
2. Umuhimu wa lugha katika jamii
3. Mambo mbalimbali yanayoweza kukwamisha mawasiliano yenye
kutumia lugha
31.6. Kuandika: Utungaji wa kifungu cha habari
Kazi ya 13:
Kwa kutoa hoja zenye mifano, tunga kifungu chako kwa kutumia
mada ifuatayo:
“Lugha inapotumiwa vizuri hujenga jamii na ikitumiwa vibaya huangamiza
jamii”.
Kazi ya 14:
Chagua mada moja kati ya hizi zifuatazo na kuzitungia insha
isiyopungua maneno 100.
• Lugha ni kitambulisho cha jamii
• Lugha hurahisisha mawasiliano katika jamii
• Lugha hukuza utamaduni
• Lugha huburudisha
Tathmini ya mada
Jibu maswali yote.
1. Je, ushirikiano wa Rwanda pamoja na nchi nyingine za kikanda
ulisaidia nini Kiswahili?
2. Toa lugha rasmi nchini Rwanda.
3. Ni vituo gani vya utangazaji habari vinavyotumia Kiswahili katika
baadhi ya matangazo vinavyorusha?
4. Fafanua maneno haya: - Malighafi, chatu, mawaidha.
5. Jaza sentensi zifuatazo kwa kutumia neno lililo mabanoni:
i. “…………… kazi yako ya shule kuhusu dhima ya kiswahili!”.
Mama alimuamrisha mtoto wake (kurekebisha).
ii. Mwalimu alimwomba mwanafunzi akisema: “…………… kurasa
mbili za kifungu!”(Kuandika).
iii. Baada ya kujiunga na nchi nyingine za Afrika Mashariki viongozi
wa Rwanda walituambia: “……… Kiswahili!” (jifunza)6. Onyesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika jamii.
MAREJEO
1. Ntawiyanga, S. na Wenzake (2016). Kiswahili kwa Shule za Rwanda,
Kidato cha Kwanza. Longhorn Publishers (K) Ltd.
2. Ndalu, A. E. (2016). Masomo ya Kiswahili Sanifu, Kidato cha 2. Moran
(E.A.) Publishers Ltd.
3. Rwanda Education Board (2019). Kiswahili kwa Shule za Rwanda,
Mchepuo wa Lugha, Kidato cha 4. Rwanda Education Board.
4. Rwanda Education Board (2019). Kiswahili kwa Shule za Rwanda,
Michepuo Mingine, Kidato cha 6. Rwanda Education Board.
5. TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Pili. Oxford University
Press.
6. NKWERA, F.M.V. (1979). Sarufi na Fasihi, Sekondari na Vyuo. Tanzania
Publishing House Dar-es-salaam, Tanzania.
7. https://sw.wikipedia.org/wiki/Kito_(madini)
8.;
9.;
10. http://swa.gafkosoft.com/maigizo11. https://www.facebook.com/1416762588414463/posts/hali-yakuamuru-hali-hii-ilichambuliwa-kwenye-tawi-la-mutanga-jumapili-hiikidat/1823486384408746