MADA YA 7 UTUNGAJI WA INSHA
Uwezo mahususi wa mada : Kutunga insha fupifupi kwa kuzingatia kanuni
za utungaji na masimulizi.
Malengo ya ujifunzaji:
• Kueleza maana ya insha,
• Kutofautisha aina za insha,
• Kujadili umuhimu wa insha,
• Kutunga insha kwa kuzingatia kanuni za utungaji wa insha,• Kutumia kwa usahihi alama za vituo husika.
Kidokezo
Zungumzia aina mbalimbali za maandishi au masimulizi unazozijua.
SOMO LA 25: DHANA YA INSHA25.1. Kusoma na ufahamu: Mchuano wa fainali
Wiki iliyopita nilibahatika kutazama mchuano wa fainali ya kuwania kombe
la Agaciro kati ya shule ya wasichana ya Elimu Bora na Tusonge Mbelekwenye uwanja wa michezo Amahoro.
Nilipofika nyumbani, wazazi wangu waliniuliza kwa mapana na marefu
kuhusu mchezo huo kwa sababu mmoja kati ya wachezaji ni dada yangu,
jina lake Umutesi Marie Alice.
Nilianza kuelezea wazazi kwanza historia ya timu hizo. Timu hizi mbili ni
wapinzani sugu tangu jadi na jadi. Elimu Bora inajivunia historia nzuri kwa
kushinda kombe hili mara kumi. Wao ndio mabingwa watetezi. Tusonge
Mbele imeshinda kombe hili mara tatu. Mwaka jana walitimuliwa katika nusu
fainali. Katika awamu hii, wana rekodi ya kutoshindwa katika mechi zote
hadi kufikia fainali.
Timu zote mbili ziliingia uwanjani tayari kwa mapambano. Kwa ufupi, kila timu
ilikuwa na golikipa mmoja. Elimu Bora waliweka wachezaji watatu katika safu
ya ulinzi wao Wakati ambapo tusone mbele walichezesha wachezaji wanne
katika safu hiyo hiyo. Timu ya Elimu Bora walitia wachezaji watano katika
kiungo cha kati nao Tusonge Mbele waliwachezesha wachezaji watatu.
Elimu Bora walikuwa na washambulizi wawili nao wakati ambapo tusonge
mbere walikuwa na washambulizi watatu katika safu ya mashambulizi.
Timu zote mbili zilikuwa na wachezaji wa akiba watano. Refa mkuu alipuliza
kipenga nao wasaidizi wake wawili walikimbia pembeni mwa uwanja kuinua
kijibendera. Mmoja alikimbia kushoto naye mwingine alikimbia kulia.
Manahodha wa timu zote mbili walisimama katikati ya uwanja kurusha sarafu
ili kuamua timu inayoanzisha mpira. Mashabiki wa timu zote mbili walikuwa
wanaimba nyimbo za kushangilia timu zao. Makochi wao walikaa pembeni
mwa uwanja kushuhudia wasichana wao wakimenyana.
Naam, refa alipuliza kipenga. Mpira ulianzishwa pale na Ikirezi na Umutesi
Marie Alice wa timu ya Elimu Bora. Elimu Bora walianza mchuano huo
kwa kasi mno. Walitafuta bao la mapema. Tusonge Mbele nao walifanya
shambulizi la kujibu. Kipindi cha kwanza kilimalizika bila goli kwa timu zote.
Katika kipindi cha pili, kila timu ilicheza vizuri. Kwenye dakika ya sabini
kulikuwa hatari katika lango la Tusonge Mbele. Kayitesi alinawa mpira.
Naam, kipenga kilipulizwa. Refa aliwapa Elimu Bora penalti. Shangwe na
vifijo vikahanikiza huku na huko kutoka kwa mashabiki wa Elimu Bora.
Kayitesi alionyeshwa kadi ya manjano. Ikirezi alisimama nyuma ya mpira
ule tayari kufyatua mkwaju wa penalti. Kabatesi akaruka na kuupiga mpira
ule ukapitia juu ya mtambaapanya wa goli hadi nje. Ilikuwa konakiki.
Konakiki hiyo ilipigwa na Umulisa. Uwamwiza alikimbilia mpira ule. Alipiga
kichwa! Hatimaye Elimu Bora walipata goli la kwanza. Mashabiki wote wa
Elimu Bora na makochi wao waliacha viti vyao huku wakijirusharusha kwanderemo kama kulungu. Mashabiki wa Tusonge Mbele waliviinamisha vichwa
vyao mithili ya kondoo. Wachezaji wa Tusonge Mbele walipandwa na mori
kwa goli walilofungwa. Walimzingira refa mkuu. Walidai kuwa Uwamwiza
alikuwa ameotea. Nahodha wao, Mutoni, ambaye ni beki wa kupanda na
kushuka alimiminia refa maneno makali. Refa alitia mkono katika mfuko wa
nyuma ya kaptula na kuchomoa kadi nyekundu. Mutoni alionyeshwa kadi
nyekundu kwa kukosa adabu. Alisindikizwa nje ya uwanja. Timu ya Tusonge
Mbele walibaki na wachezaji kumi pekee.Mchezo ulimalizika ikiwa ni goli moja la Elimu Bora kwa bila.
Kazi ya 1:
Maswali ya ufahamu
1. Timu hizi mbili ni zipi?
2. Timu hizo mbili zinagombania kombe gani?
3. Timu hizo zilikuwa marafiki? Eleza.
4. Historia ya timu hizo ilikuwa namna gani katika mchezo wa
kandanda?
5. Mchezo ulimalizika vyema? Eleza.
6. Kwa sababu gani wazazi walitaka kusikiliza matokeo ya mchezo huo?
7. Kwa sababu gani Mutoni alipewa kadi nyekundu?
8. Kwa maoni yako, michezo ina umuhimu gani?
9. Ni vizuri kwa wasichana kucheza mchezo wa kandanda?
25.2. Matumizi ya msamiati kuhusu kifungu cha habari
Kazi ya 2:
Eleza maana ya maneno yafuatayo kutoka katika kifungu cha habari
ulichokisoma hapo juu kuhusu “Mchuano wa fainali”
Kabumbu
Mchuano
Fainali
Kuwania kombe
Wapinzani
Bingwa tetezi
Nusu fainali
Safu ya ulinzi
Kiungo cha kati
Washambulizi
Kazi ya 3:
Kamilisha sentensi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya
yafuatayo: kabumbu, mchuano, fainali, kuwania kombe, washambulizi,
kuinua kijibendela, mabingwa watetezi, refa, mashabiki, penalti.
1. Elimu Bora ndiyo …………… kwa sababu walishinda mara
nyingi.
2. ………anachomoa kadi nyekundu na kumuonyesha Mutoni.
3. Kulikuwepo mashabiki wengi katika mchezo wa …………..la
Agaciro nchini Rwanda
4. ………….. ndio wanaofungia timu yao magoli mengi.
5. Mara nyingi …………husababisha goli.
6. Wasaidizi wa refa wanamsaidia katika mchezo kwa………………..
7. Timu ya Arsenal ina ……….. wengi nchini Rwanda.
8. Siku hizi wachezaji wa ………….hulipwa hela nyingi.
9. Nchini Rwanda, …………wa APR FC na Rayon Sport unatazamwa
na watu wengi sana.
10. Katika mchezo wa ………….kila timu hutakiwa kuwa bingwa.
25.3. Sarufi: Matumizi ya herufi kubwa
Kazi ya 4:
Tazama herufi zinazopigiwa mstari na kueleza sababu ya kutumia
herufi kubwa
a. Mjini Kigali panajulikana kuwa na usalama pamoja na usafi.
b. Shule ya Mtakatifu Yohana inawapokea wasichana na wavulana.
c. Jina lako ni nani? Ninaitwa Peter. Jina jingine ?
Maelezo ya matumizi ya herufi kubwa
a. Hutumiwa kuanzishia sentensi: Tazama mfano ufuatao:
Nilikuona jana.
b. Herufi kubwa hutumiwa mwanzoni mwa majina au nomino pekee
kama vile: majina ya watu, mahali, milima, mito, maziwa, nchi,
mabara, siku za wiki, miezi ya kalenda, sikukuu, dini mbalimali,
barabara, majina ya vitabu, visiwa, n.k.
c. Hutumiwa kuandikia anwani:
Mfano:
JINSI YA KUPANDA MITI
Kazi ya 5:
Chunguza makosa ya kisarufi katika sentensi zifuatazo na
kuyasahihisha.
1. musanze ni mji mkubwa.
2. kalisa na uwineza ni wanafunzi wenye bidii.
3. miti hutupatia kivuli cha kupumzikia.
4. mwalimu anafundisha.
5. berwa anacheza mpira.
25.4. Matumizi ya Lugha: Dhana ya insha na utungaji wake
Kazi ya 6:
Jadili maswali yafuatayo:
a. Insha ni nini?
b. Toa umuhimu wa kujifunza insha.
c. Insha nzuri inastahili kuwa na sifa gani?
d. Kifungu hiki cha habari ni cha aina gani ya insha ?
Maelezo muhimu kuhusu insha.
Maana ya insha:
Insha ni mtungo wa kinathari unaozungumzia suala au kusimulia kisa
fulani. Utungo huu huwa na urefu wa wastani. Kisa hicho au suala hilo
ndilo mada ya utungo huo. Insha hutumiwa kueleza maoni ya mwandishi
kuhusu masuala au mambo tofauti. Utungaji ni neno linalotokana na kitenzi
“tunga”. Kitenzi hiki kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004: 414)
kinamaanisha “Kutoa mawazo kutoka ubongoni na kuyakusanya, kisha
kuyadhihirisha kwa maandishi, kwa kusimulia, kwa kuyaimba au kwa
muziki.»
Kwa hiyo, tunaweza kusema kuwa utungaji ni utoaji wa mawazo binafsi
kutoka akilini mwa mtu kuhusiana na mambo mbalimbali katika jamii, kisha
kuyaweka wazi kwa njia ya mdomo au maandishi.
Sehemu kuu za insha: Insha hugawika katika sehemu kuu tatu ambazo ni
pamoja na:
• Utangulizi (mwanzo)
Katika sehemu hii inampasa mwandishi/ mtungaji atoe maelezo mafupimafupi
na maana ya habari aliyopewa.
• Kiini cha insha (Kati au mwili)
Inamlazimu mwandishi afafanue kwa mapana na marefu mada
anayoishughulikia huku akitoa mifano hai inayoendana na hali halisi ya
maisha ya mtu kijamii. Kwa kawaida sehemu hii hueleza kwa ukamilifu kila
hoja iliyodokezwa katika utangulizi.
• Hitimisho na mwisho
Inampasa mwandishi kutoa mapendekezo (maoni) ya msingi au kusisitiza
kwa ufupi yale aliyoyaeleza katika habari yenyewe. Mwisho wa insha
huonesha uhusiano uliopo kati ya utangulizi na maelezo yaliyomo katika
mwili.
25.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 7:
Fikiria juu ya insha moja uliyoisikiliza au kusoma na kuisimulia
mbele ya darasa
176
25.6. Kuandika: Utungaji wa insha
Kazi ya 8:
Kutokana na mfano wa insha uliotolewa hapo juu, andika insha
kuhusu mada ifuatayo:
“Umoja wa Afrika ni Msingi Muhimu kwa Maendeleo ya Afrika”SOMO LA 26: AINA ZA INSHA
Jadili michoro hii kwa kuelekea kwenye insha26.1. Kusoma na ufahamu: Usafi wa mavazi yetu
Vazi ni nguo ya aina yoyote inayovaliwa mwilini. Binadamu huhitaji mavazi
kujikinga dhidi ya hali ya hewa ya aina mbalimbali. Wakati wa joto huhitaji
vazi jepesi na wakati wa baridi huhitaji vazi linaloweza kumtilia joto mwilini.
Hii ndiyo sababu wakati wa baridi watu hujifunika mavazi kama migolole,
makoti, makabuti, kaniki, vikoi, na sweta .
Mavazi ni pambo kwa binadamu. Vazi humfanya mtu aonekane maridadi na
apendeze zaidi. Labda, hii ndiyo sababu ya kuwepo kwa aina mbalimbali za
mavazi na mitindo tofauti inayomfanya mtu avutie.
Mavazi huonesha utamaduni wa watu. Kusema kwamba mtu akivaa nguo
ya mtindo fulani mara nyingi utamaduni wake au asili yake hutambulika
waziwazi. Hata mtu awe mweupe anayetoka Ulaya au Marekani, akivaa
mgolole, kanga, kitenge, atakuwa akiiga vazi la utamaduni wa Afrika kwa
ujumla. Hadi leo, kuna mavazi unayoweza kusema kuwa ni ya Kichina,
Kihindi, Kiarabu, Kizungu, Kinyarwanda, Kiganda, Kimasai na kadhalika.
Tena mtu anaweza kuvaa nguo kwa mtindo wa aina fulani akafikiriwa kuwa ni
Mkongomani, Mganda, Mmasai, raia kutoka Afrika Magharibi na kadhalika.
Mavazi ni ya aina nyingi na mitindo tofauti. Lakini mavazi hayo yote huweza
kupangwa katika aina kuu tatu: mavazi ya kike, ya kiume na mavazi mahususi.Kwa upande wa kwanza, mavazi ya kike ni mavazi ambayo kwa kawaida
huvaliwa na watu wa jinsia ya kike. Kuna mavazi au nguo za ndani, ambazo
huvaliwa na wanawake na hazipaswi kuonekana ovyo. Na hizo ni kama
chupi, fulana, sidiria na shimizi.
Tena, kuna nguo za nje ambazo ndizo zionekanazo mara nyingi. Hizo ni
kama sketi, blauzi, shati, jaketi, gauni, kanga, kaniki, kitenge, kaptula, suruali
na kadhalika.
Kwa upande mwingine, wanaume nao huwa na nguo za staha yaani nguo
za ndani kama chupi na fulana. Pia, wana nguo zinazoonekana nje kama
kaptula, suruali, shati, koti, tai, suti, kanzu na kadhalika.
Zaidi ya hayo, kuna mavazi mahususi ambayo ni mavazi rasmi kwa ajili ya
shughuli maalum au kazi maalum. Mfano wa mavazi haya ni kama mavazi
ya viongozi wa kidini, masista, makasisi, mapadri na mashehe. Kundi la
aina hii huwa na nguo zao maalum kwa ajili ya kazi zao na pia huwasaidia
kujitambulisha kwa urahisi kwa umma au jamii. Baadhi ya nguo hizo ni kama
kasiki, joho, kanzu, kilemba na nguo zinazofanana na hizo.
Mfano mwingine ni mavazi rasmi kama ya askari jeshi, askari polisi, askari
magereza, wafanyakazi wa forodha, walinda usalama wa mashirika ya
kujitegemea, waganga na wauguzi, wafanyakazi wa mashirika ya ndege,
wachezaji na hata wanafunzi. Hawa wote wana mavazi yao rasmi kwa ajili
ya shughuli zao. Mtu akivaa nguo ya aina fulani, hujitokeza kuwa yeye ni
mtu wa namna fulani au kazi fulani.
Mavazi yetu yote ni lazima yawe na usafi. Usafi wa mavazi yetu ni muhimu
sana kwa sababu jambo hili husaidia mambo mengi maishani mwetu.
Kwanza tunaposafisha nguo zetu, tunajiepusha na magonjwa yanayotokana
na wadudu wanaoweza kuishi katika nguo chafu.
Wadudu hawa ni kama chawa, viroboto na kadhalika.
Nguo chafu hasa zile za ndani huweza kusababisha madhara katika sehemu
za uzazi na kuleta magonjwa mbalimbali kutokana na vidudu ambavyo
vinaweza kusababishwa na uchafu.
Pili, mtu akiwa na nguo chafu hutoa harufu mbaya ambayo husumbua
wenzake wanapomsogelea.
Kwa ujumla, mavazi yetu ni ya aina nyingi na mitindo tofauti. Mavazi
haya yana umuhimu sana katika maisha yetu. Ndiyo maana tunalazimika
kuyatunza vizuri na kuyasafisha ili tuwe na usafi wa kutosha. Usafi huu
lazima uende bega kwa bega na usafi wa miili yetu.
(Kifungu hiki msingi wake ni kutoka: Ndalu A. (1997) Mwangaza wa Kiswahili,East African Educational Publishers Ltd, Nairobi, Kenya.
Kazi ya 2:
Maswali ya Ufahamu:
1. Vazi ni nini ?
2. Kwa sababu gani vazi ni kifaa muhimu sana kwa binadamu?
3. Taja aina kuu tatu za mavazi.
4. Ni kwa namna gani vazi linavyoweza kutambulisha utamaduni wa
anayevaa vazi hilo? Eleza kwa kutoa mifano ya kutosha.
5. Taja mifano mitatu ya nguo mahususi.
6. Veli linaweza kutambulika kama vazi la aina gani miongoni mwa
aina za mavazi tulizotaja hapo juu?
7. Eleza jinsi ambavyo mavazi hutegemea sana utamaduni wa jamii husika?
8. Taja majina ya wadudu wanaoishi ndani ya mavazi machafu.
9. Kwa sababu gani nguo zilizofuliwa ni lazima zipigwe pasi baada
ya kukaushwa na jua?
10. Ni ushauri gani unaoweza kutoa kulingana na kifungu hiki?
26.2. Msamiati kuhusu kifungu cha hatari
Kazi ya 3:
Tazama kwa makini jedwali hili. Bainisha msamiati mbalimbali nakueleza maana yake.
26.3. Sarufi: Matumizi ya alama za vituoKazi ya 4:
Unganisha msamiati kutoka sehemu A na maana yake kutoka sehemu B.
a. Matumizi ya nukta ( . )
Kazi ya 5:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
yanayojitokeza.
i. Usafi ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu.
ii. Kalisa alienda sokoni. Alikutana na rafiki yake sokoni.
iii. Tunasoma ili tupate elimu.
Maelezo muhimu
Nukta
a. Huwekwa mwishoni mwa sentensi sahili sahihi. Kwa mfano
i. Tunakula mboga kwa ajili ya afya nzuri
ii. Inatubidi kusafisha mahali tunapoishi.
b. .Hutumiwa kuonyesha ufupisho wa maneno. Kwa mfano:
i. S.L.P. – Sanduku la Posta
ii. Bi. – Bibi
182
c. Hutumika kubainisha saa na dakika au tarehe. Kwa mfano:
i. 3.20 – saa tisa na dakika ishirini
ii. 14.5.2016- tarehe kumi na nne, mwezi wa tano, mwaka wa mbili elfu
kumi na sita
d. Hutumiwa kuonyesha vipashio vya pesa. Kwa mfano:
sh.10.50- shilingi kumi na thumuni hamsini
e. Zikitumiwa mara tatu mfululizo (…) huonyesha kutokamilika kwa
sehemu husika
Kwa mfano: Nitakupa lakini ni sharti...
Kazi ya 6:
Chunguza sentensi hizi na kusahihisha makosa ya kisarufi.
1. mwalimu anaandika ubaoni
2. mifano ya ndege ni kv kuku, mwewe na bata
3. tulianza mitihani yetu tarehe 12122017
4. bi mutoni anaendesha gari
5. wanafunzi wanasoma darasani
b. Matumizi ya koma / mkato ( , )
Kazi ya 7:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
yanayojitokeza.
1. Nimemkuta mzee, nikamwuliza shida zake, nikamsaidia kupata
gari la kumpeleka nyumbani.
2. Tumekuja kwa ajili ya akili, si kwa ajili ya pesa.
3. Baadhi ya maadili na thamani Mnyarwanda anatakiwa kuwa na zo
ni kama vile utu, unyarwanda, ushirikiano na ushujaa.
Maelezo muhimu
Mkato / koma
a. Hutumiwa kuonyesha pa kutua kwa muda mfupi katika sentensi.
Kwa mfano:
ii. Nilipowasili nyumbani, nilienda kuteka maji kisimani.
iii. Kwa kuwa tulijiandaa vilivyo kwa mtihani wa kitaifa, tulipita.
b. Hutumiwa kutenga maneno yaliyo katika orodha:
i. Nenda sokoni ununue mboga, nyama, mafuta, na unga.
ii. Mwanafunzi huyu ni mtiifu, mwerevu, mtanashati, na mwenye bidii.
c. Hutumiwa kubainisha sehemu mbili za sentensi zilizo kinyume:
i. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.
ii. Aliniambia atakuja, hakuja.
d. Hutumiwa kabla ya alama za mtajo.
Kwa mfano:
Mama akasema, “Niletee chumvi.”
e. Hutumiwa wakati sentensi inapoanza kwa kiunganishi.
Kwa mfano:
Kweli, alikuwa mtu mwovu.
f. Hutumiwa unapoita mtu ili kupata usikivu wake kabla hujamwambia
chochote. Kwa mfano:
Nkusi, niletee kalamu.
g.Hutumiwa unapokubali au unapokataa kitu. Mfano:
i. Ndiyo, nitakuja.ii. Hapana, sitakulipa.
Kazi ya 8:
Sahihisha makosa ya kisarufi katika sentensi zifuatazo
1. Baba alinunua daftari kalamu rula na kifutio
2. Mama alipofika sokoni alinunua nanasi mkate chungwa na
parachichi
3. Familia yetu ina watoto wafuatao: Kabanda Kabalisa na Mukandoli
4. Mwalimu wetu anatufundisha masomo ya Kiswahili Kiingereza na
Historia
5. Katika lugha ya Kiswahili kuna alama za uandishi kama vile: nukta
mkato alama ya kuuliza ….
26.4. Matumizi ya lugha: Ainaza insha
Kazi ya 9:
Jibu maswali yafuatayo:
1. Kifungu “ Usafi wa mavazi” ni aina gani ya insha?
2. Kifungu “Mchuano wa fainali” ni aina gani ya insha?
Maelezo muhimu kuhusu aina za insha
Insha ni za aina nyingi kulingana na namna zilivyoandikwa au kufuatana na
kusudi lake. Katika utungaji wa insha kuna :
1. Insha za wasifu
Insha za wasifu ni aina ya utungaji ambao huchora picha ya kitu
kinachozungumziwa. Huonyesha waziwazi hisia za msanii. Aghalabu, kuna
vitu vingi ambavyo tunaviona kila siku kama vya kawaida lakini mtungaji
anaweza akavitungia insha za wasifu na tukaviona katika mtazamo tofauti
kabisa. Katika insha za wasifu kuna usanii wa kueleza sifa za mtu, mahali
au kitu fulani.
2. Insha ya mjadala au ya mdahalo
Inalenga mara nyingi kulieleza jambo na vile vile kuhimiza mtazamo fulani.
Hata hivyo, jambo lililo muhimu zaidi si kueleza bali ni kujibidiisha kushawishi.
Katika mdahalo shawishi, mwandishi hulenga katika kuathiri hisia na maoni
ya msomaji kwa njia ya kumfanya achukue hatua. Insha hii huhusisha mada
ambayo mwanafunzi anapaswa kuitetea au kuipinga katika kisa chake. Hoja
nyingi na nzito hutolewa kwenye upande anaounga mkono.
3. Insha fafanuzi
Katika aina hii ya insha, mwandishi hutumia mifano kufafanua au kutilia
mkazo hoja yake. Anaweza kutumia mfano mmoja wenye uzito au mifano
mingi yenye kuhusiana.
Mfano: Rushwa imepigwa marufuku nchini Rwanda.
4. Insha ya methali
Insha ya methali ni utungo unaoandikwa kwa kuzingatia methali. Kisa au
maelezo yatolewayo huwa yanaongozwa na maana iliyomo katika methali
husika. Kabla ya kuanza kuandika insha, ni bora kwanza kuielewa vyema
maana ya methali au maudhui yake. Mbali na kufahamu maana ya kijuujuu
ya methali, inambidi mtunzi wa insha kuelewa mazingira (miktadha mingine
ambapo methali husika inaweza kutumiwa). Kwa mfano: Akili ni nywele kila
mtu ana zake. Hapa, anayetunga insha hii lazima aeleze maana ya juu na
ya ndani ya methali. Pia, msamiati uliotumiwa hufafanuliwa.
5. Insha ya mdokezo
Insha ya mdokezo ni aina ya utungo ambao huandikwa kwa kuongozwa
na maneno aliyopewa mtunzi wake. Maneno hayo yaliyotolewa ndiyo
mwongozo wa kumwelekeza mwandishi kuhusu maudhui atakayoandika.
Lililo muhimu ni kuhakikisha kuwa mtungo utakaoandikwa unaoana vizuri na
maneno yaliyotolewa kama mwongozo.
Mfano: Nilipofika katika eneo la tukio hilo, sikuamini niliyoyaona ………………
Hapa, unaweza kuendeleza kidokezi hiki kwa kukitungia kisa mwafaka.
6. Insha za picha
Insha za picha ni zile ambazo msingi wake wa kuzitunga ni picha ambazo
huwa zimechorwa na ambazo humwongoza mwandishi kubuni hadithi au
kisa kinachooana na picha hizo. Kimsingi, huhitaji ufasiri wa picha zilizo
kwenye ukurasa na kuibuni hadithi kuzihusu.
Hivyo basi huwa ni insha za kusimulia.
7. Insha ya mawazo au ya kubuni
Insha hizi zinahusu jambo la kufikiriwa. Jambo linalojadiliwa katika aina hii ya
insha huwa halitokani na hali au tukio halisi katika maisha. Vipengele vyote
vinavyoijenga hubuniwa na mtunzi wake. Maudhui, wahusika, mandhari vya
mtungo wa aina hii vyote hubuniwa katika fikra ya mtunzi.
8. Insha ya kitawasifu (Insha elezi/ ya maelezo)
Insha hii huwasilisha sifa za vitu, watu, hali, matendo, mahali au hata
sherehe uliyohudhuria. Inalenga kutoa picha ya kitu katika akili zetu jinsi
ambavyo kinamdhihirikia anayekiona. Ili kuandika insha ya maelezo,
mwandishi wake anahitaji kwanza kabisa kukusanya habari za kina kuhusu
jambo analoliandikia. Hategemei tu yale ambayo yanaonekana kwa macho
bali pia aina nyingine za hisi kama vile kugusa, kuonja, kunusa, kusikia na
kadhalika. Hali hii humwezesha msomaji kupata taswira kamilifu kuhusu
jambo linaloelezewa kupitia viungo vya kuona, kuonja, kugusa na kusikia.
9. Insha ya masimulizi
Insha ya masimulizi ni insha yenye kuhadhiria tukio au hali fulani. Ni utungo
ambao husimulia au kueleza kisa. Dhima yake ni kuburudisha au kuteka
umakini wa msomaji. Kwa kuwa inalenga hadhira ni muhimu kufahamu na
kuitambua hadhira yako kabla ya kuandika utungo wako
26.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 10:
Jadili mada zifuatazo
1. Mavazi ya kigeni yana athari kubwa katika utamaduni wa
Wanyarwanda
2. Matumizi ya mtumba (mavazi) huleta hasara kwa Wanyarwanda.
26.6. Kuandika
Kazi ya 11:
Tunga insha ya wasifu unayotaka yenye ukurasa mmoja.SOMO LA 27: INSHA YA MASIMULIZI
Kazi ya 1:
Unaona nini kwenye mchoro hapa juu?
27.1. Kusoma na ufahamu: Mafanikio ya kudumu
Ilikuwa tafrija ya kijiji kizima, tuliposherehekea siku ya kupata tuzo kwa kijana
hodari ambaye aliyamudu maisha yake kiasi cha kuigwa na vijana wengine.
Kabatesi, kijana aliyezaliwa mwanapekee katika familia yake hakubahatika
kulelewa na wazazi wake kwani walifariki angali mdogo akachukuliwa na
kulelewa na shangazi yake.
Alipomaliza masomo yake katika shule za sekondari, Kabatesi alipata cheti
cha kuhitimu masomo ya sekondari huku akiwa na alama nzuri. Jambo hili
liliwafurahisha watu wengi: walimu na majirani zake. Alikuwa mwanafunzi
mwenye bidii tangu shule za chekechea hadi kiwango alichofikia. Muda mfupi
baadaye, alijiunga na vijana wenzake kufuata masomo ya muda mfupi yaliyokuwa
yakitolewa kijijini mwake. Masomo hayo ni kuandaa miradi midogo midogo ya
kujiendeleza na jinsi ya kuifanikisha.
Alipokubaliwa kufuata mafunzo pamoja na vijana wengine alielewa kwamba hiyo
ilikuwa njia nzuri ya kupata suluhisho na ufumbuzi wa tatizo lililokuwa likimkera
kwa muda mrefu. Mafunzo yalifanyika kwa muda wa mwaka mzima, akapewa
cheti katika fani ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.
Mwezi mmoja uliofuata, Bodi ya Maendeleo Rwanda ilihitaji kuajiri vijana
waliokuwa wamemaliza masomo yao katika mkondo wa lugha ili wasaidie katika
kazi za ukalimani na uongozaji wa watalii kwenye vivutio vya utalii.
Kabatesi alipeleka ombi lake na baada ya muda mfupi akaitwa kwa mtihani. Hili
lilikuwa jambo jepesi kwake kwani aliufaulu vizuri mtihani na hivyo akaajiriwa na
bodi hiyo. Alifanya kazi yake kwa bidii kiasi kwamba watalii wengi walifurahia
huduma yake, wakampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha nyingi
tofauti na bidii aliyoonesha kazini.
Kabatesi alifungua akaunti kwenye benki moja na kuanza kuhifadhi sehemu
ya mshahara wake. Kwa kweli, alikuwa msichana asiyekata tamaa na kila
aliposhikilia jambo alilifuatilia mpaka lilipokamilika. Kwa hivyo, alipoona akaunti
yake imeshakua na pesa za kutosha, aliamua kuomba mkopo ili aweze
kutekeleza mengi aliyokuwa amejifunza katika maandalizi na utekelezaji wa
miradi ya kimaendeleo. Mawazo yake yalikuwa kwenye shamba lake kubwa
aliloachiwa na wazazi ambalo mpaka wakati huo lilikuwa halijatumiwa vizuri.
Aliandaa vizuri mradi wa kilimo na ufugaji, akajenga vibanda vya mifugo yake,
akawaajiri baadhi ya vijana waliokuwa pamoja katika mafunzo ya muda ule
mfupi, kila mmoja akapewa jukumu lake.
Pamoja na kazi yake ya ukalimani, Kabatesi alifuata vizuri mradi wake
akanunua vifaa vilivyohitajika. Ninakumbuka kuwa mwaka jana, serikali yetu
ilipotoa tuzo kwa watu waliochangia kubadilisha maisha ya watu wengine,
Kabatesi alikuwa miongoni mwa watu waliochangia kuyaboresha maisha ya
majirani zake. Kwa sasa ameanza kuendelea na masomo yake katika Chuo
kikuu cha Rwanda.
Kabatesi amekuwa mfano mzuri kwa vijana wengine wengi ambao
wanayakumbuka maisha yake, huyaamini yaliyosemwa na wahenga
kwamba” Mchumia juani hulia kivulini” na “mvumilivu hula mbivu”.
Wema kwa kila mtu, utulivu na upendo ni baadhi ya sifa zinazomtambulisha
kijana huyu ambaye amewashangaza wengi wanaofahamu alipotoka.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Eleza hali ya maisha ya Kabatesi alipokuwa mtoto mdogo.
2. Kwa nini Kabatesi alipewa zawadi nyingi baada ya kumaliza
masomo yake ya shule za Sekondari?
3. Masomo ya muda mfupi aliyoyafuata yalikuwa yanahusu nini?
4. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kufaidika kutokana na
masomo ya muda mfupi.
5. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kufaidika kutokana na
masomo yake ya Sekondari.
6. Ni mambo gani yanayokudhihirishia kwamba Kabatesi alikuwa
kijana asiyekata tamaa?
7. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kuboresha maisha ya watu
wengine.
8. Kwa nini Kabatesi alipewa tuzo?
9. Kwa kifupi, eleza tabia na mienendo ya Kabatesi.
10. Kwa nini Kabatesi anachukuliwa kuwa mfano kwa vijana wengine?
11. Umepata funzo gani kutokana na kifungu hiki?
12. .Kulingana na kifungu hiki, eleza maana ya methali hizi:
a. Mvumilivu hula mbivu.
b. Mchumia juani hulia kivulini.
27.2. Matumizi ya msamiati kuhusu kifungu
Kazi ya 3:
Tunga sentensi kwa kutumia maneno yafuatayo:
1. Kuandaa
2. Karo
3. Tafrija
4. Ajira
5. Hodari
6. Kukata tamaa
7. Akaunti
8. Tuzo
9. Mradi
Kazi ya 4:
Husisha maneno kutoka sehemu A na maana yake kwenye sehemu B.
Kazi ya 5:
Kamilisha sentensi kwa kutumia maneno unayoona yanafaa kati ya
yafuatayo: Bidii, inawapongeza, utulivu, majukumu, vibanda, shule za
chekechea, ukalimani
1. Nchini Rwanda watoto wengi wanaanzia masomo yao katika……
2. Wanafunzi wanalazimishwa kusoma kwa ............ ili waweze
kufaulu mtihani wa taifa.
3. Kuna uhusiano wa karibu wa kazi ya ………. na tafsiri.
4. Wanafunzi wenye tabia ya …….. wanapata alama nzuri katika
masomo yao.
5. Serikali ya Rwanda ………. na kuwahimiza wasichana wanaosoma
sayansi na teknolojia.
6. Wazazi wana ……. ya kuwalisha na kulipa karo za watoto wao.
7. Mjomba wangu alijenga ……… vitatu vya kuku wake
27.3. Sarufi: Matumizi ya alama za vituo
a. Matumizi ya alama ya kuuliza/ ulizo ( ? )
Kazi ya 6:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
inayojitokeza.
i. Unasema nini?
ii. Mnafanya nini hapa ?
iii. Je, jina lako nani ?
iv. Kwa sababu gani wototo wanapaswa kuheshimu wazazi wao ?
Maelezo muhimu
Alama ya kuuliza au ulizo hutumiwa mwishoni mwa sentensi kuonyesha
kuwa sentensi hiyo ni swali.
Kwa mfano: Unaitwa nani?
Kazi ya 7:
Sahihisha sentensi zifuatazo:
1. Unasoma kitabu kipi
2. Mwalimu wako wa Kiswahili anaitwa nani
3. Je, unakunywa chai
4. Kwa nini unapiga kelele darasani
5. Unachora nini
b. Matumizi ya alama ya mshangao ( ! )
Kazi ya 8:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
inayojitokeza.
i. O lalala! Baba yako amekufa!
ii. Gooooo ! Amefunga goli!
Maelezo muhimu
Alama ya mshangao hutumiwa kuashiria mahangaiko ya moyo kama vile
hasira, hofu, mshangao na kadhalika.
i. Lo! Mwanafunzi ameangusha kitabu cha mwalimu matopeni.
ii. Wamefungwa mabao kumi kwa nunge!
Kazi ya 9:
Chunguza sentensi zifuatazo na kuzisahihisha
1. Ala umebeba mzigo huo pekee yako
2. Hoyee wanariadha wametunzwa medali
3. Pesa zangu zimeibiwa
4. Nimepita mtihani wangu wa kitaifa
5. Lo Akimana ameanguka chini
27.4. Matumizi ya lugha: Sifa za inshe ya masimulizi
Kazi ya 10:
Je, kifungu “Mafanikio ya kudumu” ni aina gani ya insha? Toa maelezo.
Maelezo muhimu
Sifa kuu za aina hii ya insha:
• Matamshi na lafudhi ni lazima yawe sahihi.
• Ni lazima mazungumzo haya yagawanyike katika sehemu kuu tatu:
mwanzo, kati, na mwisho.
• Utungaji wa masimulizi ni lazima uzungumzie ukweli wa jambo
linalozungumziwa.
• Uwasilishaji wa hali, matukio, na mazingira yanayodhihirika waziwazi.
• Mtiririko wa mawazo wenye mshikamano.
• Msimuliaji ni lazima azungumze kwa nidhamu na kwa lugha sanifu
inayoeleweka kwa watu wote.
Mfululizo wa matukio ya haraka haraka.
• Masimulizi yawe ya kupendeza sana, pengine ya kuchekesha na yenye
kuteka hisia kwa maelezo ya kushangaza au yenye kujaa taharuki.
• Kutoa funzo maalumu kutokana na hadithi yenyewe, yaani maadili
fulani kuhusu maisha kwa ujumla.
27.5. Kusikiliza na kuzungumza: Majadiliano
Kazi ya 11:
Serikali ya Rwanda inawahimiza wananchi kujitafutia ajira kutokana
na uhaba wa kazi. Jadili kuhusu namna ya kujitafutia kazi.
27.6. Kuandika: Utangazaji wa insha ya masimulizi
Kazi ya 12:
Baada ya kusoma kifungu kuhusu insha za masimulizi “Mafanikio
ya kudumu,” tunga insha ya masimulizi kuhusu tukio fulani, kisa au
tukio la kweli au la kubuni kwa kuheshimu vipengele muhimu vya
insha ya msimulizi na taratibu zake.SOMO LA 28: MWONGOZO WA KUTUNGA INSHA
Kazi ya 1:
Unaona nini kwenye mchoro hapa juu?
28.1. Kusoma na kufahamu: Siku yangu ya kwanza katikashule za mabweni
Mwanzo wa masomo yetu ulipokaribia kufika, wazazi wote walianza
kujiandaa kwa kutimiza wajibu wao wa kuwanunulia watoto wao mahitaji
kwa ajili ya masomo yao katika shule za sekondari. Wazazi wangu nao
waliwajibika kuninunulia mahitaji yote muhimu yaliyohitajika.
Ulikuwa wakati wa mwanzo wa mwaka, shule za msingi na za sekondari
zilifungua tayari kwa kuanza masomo. Mimi niliamka asubuhi na mapema
nikatoka nyumbani saa kumi na mbili kamili. Baba, mama, dada na kaka
zangu wawili walinisindikiza umbali wa takribani kilomita mbili toka nyumbani
kabla ya wengine kurudi nyumbani isipokuwa baba. Baba yangu alichukua
begi langu lililokuwa zito nami nikachukua ndoo na godoro langu tukaendelea
mpaka kituo cha basi.
Tulipofika njiani, baba yangu aliniambia kwa sauti ya upole akisema:
“Mwanangu, nenda ukasome kwa bidii. Wakati ni mali, kamwe usiuatili.
Kumbuka kuwa tumewauza mbuzi wetu wawili ili tuweze kukutafutia vifaa
vyote unavyohitaji. Huko shuleni utakutana na vijana wengi wenye tabia
tofauti. Tafadhali, usishabihiane na wanafunzi wabaya ambao hawazingatii
maonyo na mawaidha ya wazazi wao na walimu”. Nami nilifikiria kidogo ili
niweze kumpa baba yangu jibu kutokana na yale aliyoniambia. Hatimaye
nilipata cha kumuambia baba. “Baba! Sitakusaliti kamwe! Malezi uliyonipa
tangu utotoni mwangu nitayatilia maanani; nitajifunza kwa bidii kama
unavyonitakia. Sitalandana na vijana hao wasio na maadlili mema.” Baada
ya kusikia hayo, baba yangu alitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana nami
kuhusu mwelekeo wangu wa maisha katika mazingira niliyokuwa natarajia
kuingia.
Tuliendelea na safari mpaka tulipofika kwenye kituo cha basi. Huo ulikuwa
mwendo wa saa moja tu kwa miguu.
Kwenye kituo cha basi, kulikuwa na wanafunzi wengi lakini mabasi yalikuwa
machache. Baada ya dakika thelathini, basi lilikuja tukaingia sote. Mimi
nilikaa upande wa dirisha na baba alikaa karibu nami.Tuliendelea na safari
yetu mpaka shuleni. Kufika hapo, tulielekea kwenye ofisi ya mwalimu mkuu
wa shule ili tujitambulishe na kujisajilisha. Hapo nje palikuwa na umati wa
wanafunzi waliokuwa wakielekezwa kwenye mabweni yao na wengine
wakifanya shughuli za usafi. Labda hao walikuwa wenyeji wa shule hiyo
kwani walikuwa wakizungumza na kucheka kwa furaha kubwa pasipo
wasiwasi wowote
Tulipiga hodi ofisini tukapokelewa vyema. Hedimasta alituuliza habari kamili,
tukamwelezea yote halafu nilielekezwa kwa katibu ambaye alinisajili baada
ya kuonyesha stakabadhi ya malipo ya karo ya shule. Mfanyakazi huyu
alimwita afisa wa nidhamu ili anipeleke bwenini na kunionyesha kitanda
changu. Hapo hapo nilimuaga baba yangu, naye akarudi nyumbani baada
ya kunitakia kila heri na fanaka katika masomo yangu.
Nilipofika bwenini nilishangaa sana kuona vitanda vingi katika ukumbi
mkubwa ambapo kila kitanda kilikuwa na sehemu mbili za kulala, moja chini
na nyingine juu yake. Nilitandika godoro langu kwenye sehemu ya chini ya
kitanda. Hata hivyo, nilikuwa na hofu kubwa moyoni kuwa yule atakayelala
juu yangu siku moja anaweza kuniangukia. Lakini nilijikaza kiume nikafikiria
kwamba hayo yalikuwa mazoea yao na kwamba shule haingekubali
kuendeleza hali hiyo kama kungetokea tatizo kama hilo.
Baadaye, kengele ililia kuwaita wanafunzi wote kuingia bwaloni kupata
chakula cha jioni. Chakula kilikuwa kizuri. Siku hiyo tulikula wali, maharagwe,
mboga na matunda.
Tulipomaliza kula tuliambiwa kuingia madarasani mwetu kwa masomo ya
kibinafsi. Sisi sote tuliingia darasani, kila mwanafunzi alichukua daftari fulani
alilotaka na kuanza kujikumbusha yale tuliyokuwa tumesoma hapo awali.
Mimi nilichukua daftari langu la somo la Kiswahili nikaanza kupitia masomo
yote tuliyojifunza katika kidato cha tatu. Shughuli hii iliendelea mpaka saa
tatu za jioni ambapo kengele ililia tena kuashiria kuenda mabwenini kulala.
Mumo humo, tulilala kwa utulivu mpaka asubuhi tulipoamka kuanza masomo
yetu.
Kwa hakika, siku hiyo ya kwanza ya masomo yangu katika shule za mabweni
ilikuwa siku ya furaha na ugunduzi wa mambo mengi yanayohusu mazingira
ya shule hizo ambayo sikuyajua. Nilifurahia maonyo niliyopewa na wazazi
wangu na jinsi nilivyopokelewa na kuelekezwa na kila mmoja niliyemkutakatika shule yangu.
Kazi ya 2:
Maswali ya Ufahamu
1. Eleza shughuli za wazazi kila wanapokaribia mwanzo wa masomo
ya watoto wao.
2. Mwanafunzi anayezungumziwa katika kifungu hiki anakwenda
kujifunza katika aina gani ya shule?
3. Nani ambaye alimsindikiza mwanafunzi hadi shuleni?
4. Ni mawaidha gani aliyompatia baba yake walipokuwa njiani?
5. Eleza sifa za mwanafunzi anayezungumziwa katika kifungu hiki.
6. Ni nini kinachokuonyesha kwamba mwanafunzi huyu alipokelewa
vizuri mara tu alipofika shuleni?
7. Kwa nini alishangaa alipofika bwenini?
8. Wanafunzi walipewa chakula gani wakati wa jioni?
9. Walipoingia darasani mwanafunzi huyu alifanya nini?
10. Wanafunzi walitakiwa kulala saa ngapi?
28.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Tunga sentensi fupi kwa kutumia maneno yafuatayo kama
yalivyotumiwa katika kifungu ulichokisoma hapo juu.
1. kujiandaa 6. maadili
2. kusaliti 7. heri na fanaka
3. kuuza 8. ukumbi
4. bidii 9. kusajili5. tabia 10. kuashiria
Kazi ya 4:
Tumia mshale kwa kuonyesha maana ya maneno yafuatayo:
28.3. Sarufi: matumizi ya alama za vituo
a. Nuktambili / koloni ( : )
Kazi ya 5:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
nuktambili inayojitokeza.
i. Tunaenda sokoni kununua vitu vifuatavyo: nyanya, mahindi,…
ii. Katika familia yetu kuna watoto kama: Karangwa, Mukamurenzi…
iii. Jimbo la kusini kuna wilaya kama: Ruhango, Kamonyi, HuyeMaelezo muhimu
Nukta mbili
a. Hutumiwa kutanguliza maneno yaliyo katika orodha.
Kwa mfano:
i. Nenda ukaniletee: kalamu, karatasi na kifutio.
ii. Amenunua: machungwa, sukari, na ndizi.
b. Hutumiwa kuashiria maneno ya msemaji badala ya alama za mtajo
hasa katika uandishi wa mazungumzo au tamthilia.
i. Mama: Lazima uniambie ulikokuwa tangu jana.
ii. Mwalimu alisema: Ingieni darasani.
c. Hutenganisha nambari za saa (saa na dakika).
Kwa mfano:
4: 10 – saa kumi na dakika kumi
Kazi ya 6:
Sahihisha sentensi zifuatazo
1. Mifano ya ndege wanaofugwa ni kuku, bata, na njiwa
2. Baba yangu hutengeneza meza, kiti, kitanda na kabati.
3. Familia huwa na baba, mama, nyanya, babu na watoto
4. Mimi huamka saa 2: 00 asubuhi kila siku
5. Mchezo wa kandanda ulianza saa10: 00 jioni
b. Nuktamkato / nukta na kituo / semikoloni ( ; )
Kazi ya 7:
Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya alama
nuktamkato inayojitokeza.
a. Sikwenda Kayonza; nilienda Kirehe.
b. Usiwe na wasiwasi; nitakuwa pamoja nawe siku zote.
c. Harusi hiyo ilihudhuriwa na watu wengi: wanawake kwa wanaume;
wadogo kwa wakubwa; wazee kwa vijana.
Maelezo muhimu
Nukta na kituo
a. Hutumiwa kuunganisha vishazi vikuu bila kutumia kiunganishi.
Kwa mfano:
• Tuliwasili darasani tukiwa tumechelewa; mwalimu alitukaribisha kwa
kutuuliza tulipokuwepo.
b. Hutumiwa kumpumzisha msomaji katika sentensi iliyo ndefu ili
apumzike zaidi kuliko pale inapotumiwa koma.
Kwa mfano:
Alipofikiri sana, alitanabahi kuwa hakikuwepo cha kutorokwa; yeye angeweza
kuondoka nyumbani au kumwacha mumewe, aende popote kufanya lolote.
c. Kuorodhesha vitu hasa vinapokuwa na zaidi ya neno moja
Mfano:
Wakati wa likizo tulitembelea sehemu kadhaa: Mombasa, Kenya; Dodoma,
Tanzania; Kampala, Uganda na tukamalizia hapa Nairobi, Kenya.
Kazi ya 8:
Sahihisha sentensi zifuatazo:
1. Kabla ya kupata chakula ni lazima kunawa mikono hii ni tabia nzuri
2. Akili ni mali kila mtu ana zake.
28.4. Matumizi ya lugha: Taratibu za kutunga insha
Kazi ya 9:
Jibu maswali yafuatayo:
1. Kwa sababu gani utangulizi mzuri ni muhimu katika insha?
2. Jadili sehemu kuu za insha.
3. Jadili mambo ya kuzingatia katika uandishi wa insha.
Maelezo muhimu: Taratibu za kutunga insha:
• Soma kwa makini mada/ kichwa/ anwani uliyopewa zaidi ya mara moja,
ili uielewe vizuri.
• Ifikirie mada/ kichwa/ anwani kwa muda.
• Yaandike mambo muhimu yatakayokuongoza katika kuiandika insha .
• Maelezo yote yatolewe kwa undani na kwa njia ya kuvutia.
• Kutumia vizuri alama za uakifishaji.
• Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.
• Kutumia msamiati mwafaka kwa kutegemea mada.
• Lugha iwe ya adabu na isiyo ya matusi.
• Andika methali, misemo na nahau ambazo unadhania zinaweza
kukufaa katika utungaji.
Mambo ya kuzingatia katika uandishi wa insha
Bila kujali ni aina gani ya insha mtu anayoiandika, yapo mambo kadhaa ya
kuzingatia wakati wa uandishi wa insha. Mambo hayo ni pamoja na:
1. Kubaini ni mada gani ya kuandikia insha na kuielewa vyema,
2. Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki,
3. Kutumia mtindo unaoendana na kusudi la insha.
Kwa mfano: Mtindo wa masimulizi unafaa kwa hadithi au insha nyingine za
kisanaa.
4. Kutumia lugha fasaha na inayoeleweka,
5. Kufuata kanuni za uandishi.
Kwa mfano:
Matumizi ya alama za uandishi, aya, herufi kubwa na herufi ndogo.
Kupanga insha katika muundo wake, yaani kichwa, utangulizi, kiini na
hitimisho.
1. Kichwa cha habari
Kichwa cha habari cha insha ni maneno machache, takribani matano,
ambayo ndiyo jina la insha. Kichwa cha habari huandikwa juu, katikati
kwenye ukurasa wa kwanza wa insha. Mara nyingi, huandikwa kwa herufi
kubwa na hubeba wazo kuu la insha.
2. Utangulizi wa insha
Utangulizi wa insha ni sehemu ya mwanzo yenye urefu usiozidi aya moja.
Utangulizi hudondoa kwa ufupi kabisa kile kinachoelezwa kwenye insha.
3. Kiini cha insha / mwili
Hii ni sehemu tunayoweza kusema ndiyo insha yenyewe. Kwenye kiini ndipo
ufafanuzi wote hutolewa. Ufafanuzi huu hupangwa katika aya moja au zaidi.
Hapa ndipo mwandishi hubainisha mawazo yake, huthibitisha, hushawishi,
huhimiza na hufafanua kiundani kabisa.
4. Hitimisho la insha
Hii ni sehemu ya mwisho ya insha ambayo nayo haizidi aya moja.
Katika sehemu hii, mwandishi anaweza kurejelea kwa ufupi sana yale
aliyozungumzia kwenye insha yake, anaweza kuonyesha msimamo wake,
anaweza kutoa mapendekezo, au kuwahimiza walengwa wake kuchukua
hatua fulani.
28.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 10:
Chagua mada moja kati ya hizi, kisha uizungumzie kwa mapana na
marefu na kuiwasilisha mbele ya darasa.
1. Harusi uliyoihudhuria
2. Mchezo uliohudhuria
28.6. Kuandika: Utungaji wa insha
Kazi ya 11:
Andika insha ya ukurasa mmoja kuhusu “Siku yangu ya kwanza shuleni.”
Tathmini ya mada
A. Sahihisha makosa ya kimaandishi katika mazungumzo hapa chini
Mgonjwa: hujambo daktari
Daktari: sijambo Karibu uketi.
Mgonjwa: asante daktari
Daktari: nikusaidie vipi
Mgonjwa: Jina langu ni kayitesi ninaumwa na tumbo sana.
Daktari: pole sana kayitesi tumbo lilianza kukuuma lini
Mgonjwa: Tangu jana usiku hata sijalala ninaendesha na kutapika sana
Daktari: pole sana Ulikula nini jana usiku
Mgonjwa: Nilikula wali kwa kitoweo cha samaki
Daktari Mmmmhh!Wewe hunywa maji yaliyochemshwa
Mgonjwa Si kila siku daktari Mimi hunywa maji yoyote bora yanaonekana
kuwa safi.
B. Andika insha ya masimulizi kuhusu mada zifuatazo:
i. Siku ya kuadhimisha mwaka mpya.
ii. Safari yangu mjini Kigali.
iii. Utoto wangu.
iv. Likizo iliyopita.