MADA YA 6 UIGIZAJI WA MAZUNGUMZO
Uwezo mahususi katika mada hii: Kuigiza mazungumzo mbalimbali kwa
kutumia Kiswahili sanifu.
Malengo ya ujifunzaji:
• Kuzungumza Kiswahili Sanifu kwa ufasaha;
• Kujiamini katika mazungumzo ya hadharani au jukwaani;
• Kukuza stadi za kusikiliza, kukariri na kuzungumza hadharani;
• Kuendeleza weledi wa kubuni mazungumzo mbalimbali.
Kidokezo
1. Nini maana ya mazungumzo?
2. Ni faida gani zinazopatikana kutoka mazungumzo?
3. Mazungumzo hujadili mada gani?
4. Katika mazungumzo, inawabidi wahusika kuwa na sifa gani?5. Mazungumzo huweza kutokea wapi?
SOMO LA 22: KUIGIZA MAZUNGUMZO
Kazi ya 1:
Unaona nini kwenye mchoro huu?
22.1. Kusoma na ufahamu: Mazungumzo kati ya mwalimumkuu wa shule na mzazi
Mwalimu mkuu wa shule: Karibu bibi! Habari za asubuhi?
Bibi: Si nzuri hedimasta! Ahsante sana kwa kunikaribisha.
Mwalimu mkuu wa shule: Shida gani bibi? Nikusaidieje?
Bibi: Labda ni makosa ya mwanangu kutumwa mzazi.
Mwalimu mkuu wa shule: Jina lake ni nani?
Bibi: Gasagara Peter, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza.
Mwalimu mkuu wa shule: Kwa nini umeitwa na shule?
Bibi: Kwa sababu ya utovu wa nidhamu wa mtoto wangu. Sababu hii
niliisoma kwenye barua aliyopewa na shule ya kuniita mimi mzazi wake nije
hapa shuleni haraka.
Mwalimu mkuu wa shule: Ndiyo! Mtoto huyo namkumbuka. Ni yapi
yaliyomsibu? Je, alikuelezea kilichotokea?
Bibi: Alikuwa na makosa! Aliyakiri makosa matatu hivi: Kosa la kuchelewa
shuleni, kuja shuleni bila vifaa vya shule na kukosa usafi mwilini.
Mwalimu mkuu wa shule: Ni kweli. Ilitubidi tumwite mzazi wake aje shuleni
kwa sababu ya mwenendo wa mtoto wako ulikuwa unaendelea kuzorota
sana. Bibi, unaweza kunielezea kwa nini mtoto wako hufanya kinyume na
wenzake?
Bibi: Ushahidi ni kwamba sisi wazazi ndisi tuliokuwa chanzo cha matatizo
haya yote. Kulingana na shughuli za kimaisha, tulidharau fursa ya kumchunga
mwanetu na kuongea naye kila siku. Maana yake tulisahau jukumu letu
kama wazazi. Kwa hiyo, naomba msamaha. Toka leo nimeahidi kurekebisha
mienendo yetu na ya mtoto ili kuimarisha sura ya familia yetu.
Mwalimu mkuu wa shule: Ahsante sana kwa uamuzi mzuri huu. Kwa
mujibu wa shule, tutashirikiana bega kwa bega kwa njia ya mawasiliano ya
kila siku.
Bibi: Asante sana kwa makubaliano haya.
Mwalimu mkuu wa shule: Kumbuka kuwa ahadi ni deni.
Bibi: Ndiyo, usijali yote yatatimizwa.
Kazi ya 2:
Jibu maswali ya ufahamu yafuatayo:
1. Kifungu cha habari cha hapo juu kinazungumzia nini?
2. Habari hii imetokea wapi?
3. Kwa nini mzazi ameitwa shuleni?
4. Ni makosa yapi yanayojitokeza katika kifungu cha habari?
5. Ni makubaliano gani yaliyofikiwa kati ya wahusika wawili?
6. “Harakati za maisha ya leo ni changamoto kubwa kwa elimu ya
watoto katika jamii.” Husisha maoni haya na kifungu cha habari.
22.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Kwa kutumia Kamusi ya Kiswahili Sanifu au njia nyingine tofauti, toa
maana ya msamiati ufuatao na kuutungia sentensi sahihi.
a. Utovu wa nidhamu
b. Kuja
c. Kukiri
d. Kuzorota
e. Chanzo
f. Kuahidi
g. Kurekebisha
h. Kuimarisha
i. Uamuzi
j. Kushirikiana bega kwa bega
Kazi ya 4:
Jaza nafasi iliyoachwa wazi kwa kutumia msamiati unaofaa kutoka
kifungu cha habari
i. ............. kosa ni njia ya kusamehewa.
ii. Ukosefu wa mwenendo mzuri ni ..........................cha kushindwa
masomo shuleni.
iii. Ni lazima kuepuka vita kwa sababu bila usalama amani na utulivu
..................................
iv. Tunaombwa .....................tabia mbaya ili tujenge jamii nzuri.
v. Tumechukua ................huu shuleni kwa ajili ya kugombana dhidi
ya uvivu miongoni mwa wanafunziKazi ya 5:
Toa kinyume cha msamiati ufuatao
a. Kumkaribisha mtu
b. Utovu wa nidhamu
c. Kushirikiana bega kwa bega
d. Kuzungumza
e. Kuheshimu
22.3. Sarufi: Matumizi ya “nini”, “nani” na “lini’ katika
kuuliza maswali
Kazi ya 6:
Soma sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya maneno
yaliyopigiwa mstari
i. Jina lako ni nani?
ii. Kifungu cha habari kinazungumzia nini?
iii. Nchi yetu ilijinyakulia uhuru lini?
Maelezo muhimu
Maneno yaliyopigiwa mstari huitwa viulizi, yaani maneno yanayotumiwa
kuulizia swali.
Viulizi huweza kutumiwa mwanzoni mwa sentensi au mwishoni mwake.
Kwa mfano:
• Nani amepiga hodi?
• Umesema bwana huyo anaitwa nani?
Matumizi maalum ya viulizi
a. Nani
Neno hili hutumiwa kuulizia mtu, Mwenyezi Mungu, mnyama, ndege au
wadudu.Mfano:
• Nani amezungumziwa hapa?
• Jina lake ni nani?
• Nani aliyeumba binadamu?
• Baadhi ya sungura na fisi, nani mjanja kuliko mwingine?
b. Nini
Hutumiwa kwa kuulizia kitu.
Mfano: Mmejifunza nini leo?
c. Lini
Neno hili hutumiwa kuuliza majira, kipindi cha muda (tarehe au mwaka)
Mfano: Ulizaliwa lini?
Wageni wako waliwasili nyumbani lini?
Kazi ya 7:
Uliza swali linalofaa kwa kila sentensi kulingana na maneno
yaliyopigiwa mstari
a. Shule yetu ilijengwa miaka thelathini iliyopita.
b. Ukosefu wa usafi huweza kusababisha magonjwa.c. Mgeni amewasili nyumbani.
22.4. Matumizi ya lugha: Mazungumzo na uigizaji wake
Kazi ya 8:
Kwa kuzingatia mfano wa mazungumzo hapo juu, eleza maana ya
neno ‘mazungumzo’ pamoja na aina zake.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Maana ya mazungumzo
Mazungumzo au dayolojia ni utanzu mojawapo wa fasihi simulizi. Ni utaratibu
wa kuongea baina ya watu wawili au miongoni mwa watu zaidi ya mmoja au
pande mbili tofauti kuhusu mada mbalimbali zinazobadilikabadilika.
Baadhi ya vipera vya mazungumzo, vipera vitatu vifuatavyo ndivyo
vinavyojulikana na kutumiwa sana.
Malumbano ya utani: Ni mashindano ya kuongea jukwaani baina ya watu
wa makundi au jamii mbili ambayo hutumia kejeli na chuku kukejeli tabia
mbaya katika jamii au kundi fulani. Watu husimama jukwaani na kushindana
kwa maneno. Mazungumzo haya hutumia mzaha na vichekesho pamoja na
kejeli ili kuangazia ukweli fulani katika jamii.
Ulumbi: Ni uwezo wa kipekee wa kuzungumza mbele ya hadhira. Mtu
mwenye uwezo huo wa kipekee wa kuzungumza jukwaani huitwa mlumbi.
Walumbi husifika sana kwa kuzungumzia mambo yanayoathiri jamii.
Soga: Ni mazungumzo baina ya watu wawili au zaidi ambayo aghalabu huwa
hayana mada maalum. Aghalabu soga huwa na vichekesho vingi, mzaha
na kejeli. Nia yake huwa kuburudisha na kupitisha wakati. Soga huwa na
vichekesho na mzaha mwingi. Mada hubadilikabadilika kutoka wakati mmoja
hadi mwingine. Haihitaji taaluma yoyote ya kisanaa na inaweza kufanyika
pahali popote - njiani, sebuleni, katika vyumba vya burudani, n.k.
22.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 9
Sikiliza mazungumzo kutoka video zifuatazo na kusimulia mbele ya
darasa mambo yafuatayo:
https=//
https=//
a. Dhamira kuu iliyozungumziwa
b. Maudhui
Kazi ya 10
Kwa kushirikiana na wenzako, igiza mazungumzo kati ya mwalimu
mkuu wa shule na mzazi wa mwanafunzi
22.6. Kuandika
Kazi ya11:
Buni mazungumzo (yenye ukurasa mmoja) kati ya mwalimu na mwanafunzi.Kazi ya12:
Kazi ya1:Tunga sentensi sita kwa kuzingatia viulizi “nani” na “nini”.
SOMO LA 23: UMUHIMU WA UIGIZAJI WA MAZUNGUMZO
Unaona nini kwenye mchoro huu?
23.1. Kusoma na ufahamu: Tujivunie lugha yetu
Kamana na Zaninka ni wanafunzi wanaosomea darasa moja kwenye Shule
ya Sekondari ya Tarubwenge. Wanazungumzia faida za kujizoeza uigizaji
wa mazungumzo kama mojawapo ya njia za kupata weledi na umahiri wa
lugha fulani.
Kamana: Dada, unakumbuka jinsi tulivyokuwa miaka mitatu iliyopita?
Zaninka: Unataka kumaanisha nini? Unadhani nilihifadhi matukio yote
katika miezi thelathini na sita yote?
Kamana: Nimetaka kuzungumzia mchakato wa kukuza ujuzi wetu katika
stadi nne za lugha ya Kiswahili.Zaninka: Aa! Kuna mambo tele ya kuongea kuhusu mafanikio tuliyonayo
Kamana: Kiwango cha matumizi ya Kiswahili leo ni cha juu mithili ya
Waswahili wenyewe.
Zaninka: Acha! Haya ni majivuno! Nakubali tumepiga hatua kubwa lakini
hatujashindana na wale wakazi wa pwani.
Kamana: Mimi nina ushahidi mkubwa sana.
Zaninka: Ushahidi wako unautoa wapi?
Kamana: Weledi wangu katika kuizungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili
ulitokana na mazoezi darasani kwa kuigiza mazungumzo mbalimbali.
Zaninka: Si hayo tu. Kwa nini huzungumzii faida nyingine?
Kamana: Kwa mfano?
Zaninka: Kama kujiamini katika masimulizi hadharani.
Kamana: Huo ni ukweli mtupu. Wiki iliyopita niliingia katika mashindano ya
mdahalo pamoja na wanafunzi kutoka shule tofauti za mjini ambao nilikuwa
ninawaogopa kulingana na tajriba yao ya kuitumia lugha ya Kiswahili kwa
ufasaha.
Zaninka: Matokeo ya mashindano yalikuwaje?
Kamana:Bila shaka nilijinyakulia ushindi na kutunukiwa kombe la almasi!
Zaninka: Mimi nimeishafanya maajabu kijijini kwetu! Wakati wa sherehe
mbalimbali watu hunialika kwa ajili ya kuwaburudisha kupitia uigizaji wa
mazungumzo. Mwishowe hunipatia zawadi ya pesa zaidi ya elfu kumi.
Kamana: Hatuwezi kuorodhesha faida zote, ndiyo sababu tunapaswakujivunia lugha yetu tukufu.
Kazi ya 2:
Jibu maswali ya ufahamu yafuatayo:
1. Kifungu cha habari kinazungumzia nini?
2. Ni wahusika gani wanaozungumziwa kifunguni?
3. Mafanikio ya wanafunzi hawa yalisababishwa na nini?
4. Je, majivuno ya wanafunzi hawa yana sababu ya kuwepo? Eleza.23.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya3:
Kwa kutumia kamusi ya Kiswahili sanifu au njia nyingine uzipendazo,
toa maana ya msamiati ufuatao:
a. Kujivunia
b. Mchakato
c. Tele
d. Mafanikio
e. Kujiamini
Kazi ya4:
Jaza nafasi iliyoachwa wazi kwa kutumia msamiati huu: majivuno, pwani, ushahidi, tajriba, kujinyakulia
i. Zaninka na Kamana wametoa..............................kwamba uigizaji
wa mazungumzo ulikuwa chanzo cha mafanikio yao.
ii. Inahakikishwa kuwa asili ya Kiswali ni sehemu za................... au
mwambao wote wa Afrika Mashariki.
iii. .......................ni tabia ya kujisikia bora kuliko wengine; maringo.
iv. Baada ya kuishambulia timu B, timu A iliweza .........................ushindi wa mabao mawili kwa nunge.
23.3. Sarufi: Matumizi ya “nini”, “wapi” na “kwa nini’ katika kuuliza maswali
Kazi ya 5:
Soma sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya maneno yaliyopigiwa mstari
i. Je, miti itapandwa wapi?
ii. Kwa nini vijana hawajaelewa hasara ya kutumia dawa za kulevya?Maelezo muhimu
a. Wapi
Tunatumia neno hili kuulizia mahali au sehemu fulani
Mfano: Unaishi wapi? ; Umesema uliniona juzi. Je, uliniona wapi?
Tanbihi: Matumizi ya neno ‘pahali’, kiulizi ‘wapi’ hugeuka ‘papi’
Mfano: Pahali papi panapotembelewa sana nchini humu?
b. Kwa nini/ mbona
Kiulizi hiki hutumiwa kuulizia sababu.
Mfano: Kwa nini/ mbona mmechelewa kufika shuleni?
c. Namna gani
Neno hili hutumiwa kuulizia namna au jinsi jambo lilivyotendeka
Kwa mfano:
Mlifanya kazi hii namna gani?
Kazi ya 6:
Toa swali sahihi kutegemea maneno au kundi la maneno yaliyopigiwa mstari
i. Sokwe mtu hupatikana katika mbuga ya wanyama iliyoko kaskazini
mwa Rwanda.
ii. Taka zote hutupwa jalalani.
iii. Hali ya hewa ilikuwa nzuri mwaka huu kwani raia walipanda miti
pahali pengi.
iv. Mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliwezekana nchini Rwanda
kwa sababu ya itikadi ya ubaguzi wa kikabila iliyofundishwa miaka mingi.
23.4. Matumizi ya lugha: Mazungumzo na uigizaji wake
Kazi ya 7:
Jadili maswali yafuatayo:
a. Nini maana ya uigizaji wa mazungumzo?
b. Uigizaji wa mazungumzo una umuhimu gani?
Maelezo muhimu
a. Kuigiza mazungumzo ni nini?
Ni kuyakariri mazungumzo yaliyosimuliwa na mtu mwingine na kuyarudia
kwa kumwiga mtu huyo kimatendo kwa njia au namna ya mchezo; yaani
kuvaa uhalisia wa mtu huyo. Ni karibu na maigizo au michezo ya kuigiza.
b. Umuhimu wa kuigiza mazungumzo
• Huunganisha watu katika jamii
• Hutumiwa kama chombo cha kuburudisha katika jamii.
• Vilevile huelimisha kuhusu mambo fulani
• Pia huleta umoja na utangamano
• Hutumiwa kuonya dhidi ya matendo mabaya.
• Hutumiwa kupitisha wakati.
• Hukuza stadi za kuzungumza lugha kwa ufasaha
23.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 8:
Kwa ushirikiano na wenzako, igiza mazungumzo kati ya Zaninka na
Kamana.
23.6. Kuandika
Kazi ya 9:
Buni kifungu cha habari kwa kutilia mkazo juu ya umuhimu wa
uigizaji wa mazungumzo
Kazi ya 10:
Tunga sentensi nne kwa kutumia viulizi ‘’wapi’’ na ‘’kwa nini’’.SOMO LA 24: VIFAA KATIKA UIGIZAJI WA MAZUNGUMZO
Kazi ya 1:
Unaona nini kwenye mchoro huu?
24.1. Kusoma na ufahamu: Majukumu yetu katika uigizaji wa mazungumzo
Egide na Liliane ni wanafunzi wanaosomea kidato kimoja kwenye Shule
ya Sekondari ya Mazungumzo. Wanazungumzia vifaa vinavyowasaidiakatika uigizaji wa mazungumzo pamoja na sifa za mwigizaji bora
Egide: Liliane, unayakumbuka mashindano tutakayoshuhudia wiki ijayo?
Liliane: Bila shaka nayakumbuka na nilazima tuanze maandalizi yake
Egide: Hayo ni kweli. Je, ni vifaa gani tutakavyohitaji ili tuliambulie kombe?
Liliane: Baadhi ya vifaa muhimu ni lazima kuwepo na simu ya mkononi,
kofia, aina tofauti za pesa, chupa, tarumbeta, n.k.
Egide: Usisahau aina za mavazi mbalimbali kama suti, kimono, tarubushi
pamoja na bombo.
Liliane: Aa! Hatukutaja vuvuzela, barakoa za ucheshi, mkongojo pamoja na
miwani.
Egide: Asante sana kwa nyongeza. Sasa ni wakati wa kuzungumzia sifa
zinazofaa kwa kila mwigizaji wa mazungumzo.
Liliane: Hizo ni mboga! Kwanza, mwigizaji bora ni lazima ajiamini katika
mazungumzo yake.
Pili, anapaswa kutumia lugha ya ishara kama vile kusugua mikono, kutikisa
kichwa, kugusa pua, kupiga vidole, kuinua nyushi, n.k.
Tatu, kuwa na ucheshi wa kutosha
Nne, kutumia vihisishi ili kufanya mazungumzo yawe ya kusisimua.
Egide: Si hayo tu, sifa zifuatazo sharti zizingatiwe pia:
Kutumia matamshi au lafudhi bora
Kuzungumza kwa ufasaha Kuonyesha moyo wenye huruma
Kuwa na mazungumzo ya mkato na yasiyozidiana sana kati ya
wahusika. Mhusika mmoja asitawale mazungumzo kupita wengine.
Liliane: Naam! Egide, tujipigie makofi kabisa! Ushindi ni wetu bila shaka.
Egide: Lakini kumbuka lililosemwa na wahenga kwamba chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.
Liliane: Usijali kaka yangu! Nimekupata wazi, ni lazima maandalizi yaanze leo bila kungoja kesho.
Egide: Naam, liwezekanalo leo lisingoje kesho.Maswali ya ufahamu
Kazi ya 2:
Jibu maswali ya ufahamu yafuatayo:
1. Kifungu cha habari kinazungumzia nini?
2. Ni wahusika gani wanaozungumza?
3. Ni vifaa gani vilivyotajwa?
4. Onyesha angalau sifa tatu muhimu anazostahili mwigizaji bora.
5. Bila shaka wanafunzi hawa watajinyakulia ushindi. Tetea ukweli
huu kulingana na ushahidi kutoka mazungumzo.
24.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Kwa kutumia Kamusi ya Kiswahili Sanifu au njia nyingine tofauti, toa
maana ya msamiati ufuatao na kuutungia sentensi sahihi.
a. Kombe
b. Kujali
c. Maandalizi
d. Mkongojo
e. Ucheshi
f. Kimono
g. Tarubushi
h. Bombo
i. Barakoa
Kazi ya 4:
Oanisha michoro hii na majina yake, kisha eleza umuhimu wa kila
aina: tarumbeta, vuvuzela, suti, miwani, barakoa.
24.3. Sarufi: Matumizi ya “gani” na “-ngapi’ katika kuuliza maswali
Kazi ya 5:
Soma sentensi zifuatazo na kuzungumzia matumizi ya maneno yaliyopigiwa mstari
i. Swali gani ambalo halikutolewa jibu?
ii. Miti mingapi mliyoipanda nyumbani kwenu?
Maelezo muhimu
a. Gani
Neno hili hutumiwa kuulizia aina ya mtu au vitu.
Mfano: Tatizo gani linalojitokeza hapa?
Tanbihi:
1. Kiulizi gani huweza kuwakilishwa na kiwakilishi -pi
Mfano:
• Tatizo lipi ambalo halijatatuliwa?
• Vitambulisho vipi vinavyotakiwa kwa kila mwanafunzi?
• Darasani mpi mnapatikana uchafu?
2. Viulizi mbalimbali huweza kuchukua nafasi ya viwakilishi viulizi.
Mfano:
• Zipi zimenunuliwa?
• Papi pamesafishwa?
• Mpi mmesafishwa?
b. -ngapi
Hiki ni kiulizi cha kuulizia idadi ya watu au vitu.
Kwa mfano:
• Ng’ombe wangapi walitolewa kwa raia kwa ajili ya kujitegemea?
• Ni wanafunzi wangapi wanaoomba mahitaji maalum ya ujifunzaji?
Tanbihi: Kiulizi hiki huweza kuchukua nafasi ya viwakilishi viulizi.Mfano: Vingapi vinahitajika?
Kazi ya 6:
Toa swali sahihi kulingana na maneno au kundi la maneno
linalopigiwa mstari
i. Tumetumia vifaa vya aina nyingi katika maigizo yetu
ii. Sabuni kadhaa zimewekwa nje ya choo kwa ajili ya usafi.
iii. Wanafunzi kumi wamezawadiwa kwa sababu ya kuimarisha amani
na umoja darasani mwao.
iv. Mwigizaji bora anapaswa kuwa na sifa kama vile kujiamini,
kuzungumza kwa ufasaha, kuzungumza kwa kutoa sauti, n.k.
24.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 7:
Jadili mada zifuatazo:
a. Umuhimu wa uigizaji wa mazungumzo
b. Wahusika wanaoshiriki katika uigizaji wa mazungumzo
c. Maigizo na aina zake
Maelezo muhimu
a. Kuigiza mazungumzo ni nini?
Ni kuyakariri mazungumzo yaliyosimuliwa na mtu mwingine na kuyarudia
kwa kumwiga mtu huyo kimatendo kwa njia au namna ya mchezo; yaani,
kuvaa uhalisia wa mtu huyo. Ni karibu sawa na maigizo au michezo ya
kuigiza
b. Wahusika katika uigizaji wa mazungumzo
Kwa kawaida wahusika huwa ni binadamu. Wahusika ndio wanaozungumza
katika sehemu zao mbalimbali. Kulingana na aina ya mazungumzo, wahusika
wanaweza kuwa wawili au zaidi. Katika uigizaji wa mazungumzo, majukumu
ya watu wa marika au viwango mbalimbali huigizwa kama vile wazee, rais,
waziri, askari jeshi, mbunge, mwalimu, mfanyabiashara, mfalme, daktari,
hakimu, n.k.
Maigizo ni sanaa katika fasihi simulizi ambayo watendaji huwa ndio wahusika.
Maigizo hayasimuliwi kama mbinu nyingine za fasihi. Wahusika ndio
huzungumza katika sehemu zao mbalimbali. Ifuatayo ni mifano ya maigizo.
1. Michezo ya kuigiza ( agh. huletwa jukwaani): Haya ni maigizo ya
jukwaani ambapo watendaji huiga maneno na matendo ya wahusika
mbele ya hadhira.
2. Miviga: Sherehe mbalimbali katika jamii fulani. Watu hujumuika na
sherehe hizi kulingana na tamaduni zao
3. Ngomezi: Ni sanaa ya ngoma. Midundo mbalimbali ya ngoma
hutumika kuwasilisha jumbe mbalimbali.
4. Malumbano ya utani: Mashindano ya kuongea jukwaani baina ya
watu wa makundi au jamii mbili ambayo hutumia kejeli na chuku
kukejeli tabia mbaya katika jamii au kundi fulani
5. Ulumbi: Uwezo wa kipekee wa kuzungumza mbele ya hadhira. Mtu
mwenye uwezo huo wa kipekee wa kuzungumza jukwaani huitwa
mlumbi.
6. Soga : Mazungumzo baina ya watu wawili au zaidi ambayo aghalabu
huwa hayana mada maalum.
7. Vichekesho: Aina ya sanaa ya fasihi simulizi ambayo watu hutoa
vihadithi vifupi au sentensi zenye uwezo wa kuwafanya wasikilizaji
wacheke.
8. Maonyesho ya sanaa: Maonyesho huhusisha watu wa jamii au kundi
fulani wanaoonesha taaluma, ujuzi au sanaa yao kwa watazamaji.
24.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 8:
Kwa ushirikiano na wenzako, igiza mazungumzo kati ya Egide na Liliane.
24.6. Kuandika
Kazi ya 9:
Buni kifungu cha habari ambapo vifaa tofauti pamoja na sifa
mbalimbali zimeonekana kwa wahusika wanaoigiza mazungumzo.
Kazi ya 10:
Tunga sentensi nne kwa kutumia viulizi “gani” na “-ngapi”.
Tathmini ya mada
1. Taja aina tatu za mazungumzo na kuzieleza
2. Nini umuhimu wa uigizaji wa mazungumzo?
3. Mwigizaji wa mazunguzo anastahili kuwa na sifa gani? Toa angalau tano
4. Kwa kutegemea mifano mitatu, onyesha mandhari au pahali panapoweza kuigiziwa mazungumzo.
5. Toa maswali sahihi kwa sentensi zifuatazo:
i. Barabara hii ilijengwa kabla ya Wazungu kufika nchini humu.
ii. Mtoto wangu hakuweza kufika shuleni jana kwani alikuwa mgonjwa.
iii. Tunakuja shuleni kwa miguu.
iv. Maswali kumi yametolewa na washiriki.
v. Wazazi pamoja na walimu ndio watu muhimu katika jitihada za kuimarisha elimu bora.
vi. Mgeni amepiga hodi.