MADA YA 5 KISWAHILI KATIKA SHUGHULI ZA KIBIASHARA
Uwezo mahususi wa mada: Kuzungumza na kuandika kwa ufasaha matinifupifupi kwa kutumia msamiati unaofaa katika shughuli za kibiashara.Malengo ya ujifunzaji:• Kufanya mazungumzo kati ya mfanyabiashara na mteja,• Kutumia kwa ufasaha mizani au vipimo katika hesabu,• Kuainisha pesa zitumiwazo katika shughuli za kibiashara,• Kuainisha bidhaa mbalimbali zipatikazo sokoni,• Kutumia kwa ufasaha ngeli ya I-ZI katika sentensi sahihi,KidokezoTaja baadhi ya msamiati maalumu unaotumiwa katika mazingira yabiashara
SOMO LA 19: MAWASILIANO SOKONI
Kazi ya 1:Tazama mchoro hapa juu na kueleza kinachofanyika hapo.19.1. Kusoma na ufahamu: Safari ya Niwemwiza na Kayigi sokoni
Siku moja nilitembea sokoni na kaka yangu Kayigi ili kununua vifaa vya
shule. Soko hilo linaloitwa Gatare lilikuwa katika kilomita kumi na tano kutoka
kwetu. Mama alitupatia pesa za nauli na nyingine za kununua vifaa tofauti
vya shule na bidhaa nyingine za kutumia nyumbani.
Tulitoka nyumbani saa tatu za asubuhi na kufika sokoni saa nne. Tulipokuwa
garini, Kayigi aliniuliza kama ninakumbuka vifaa ambavyo mama alituambia
kununua. Nilimkumbusha kwamba alituambia kununua vifaa vifuatavyo:
shati, jaketi, jozi ya viatu, sidiria, madaftari kumi, kalamu nane, soksi mbili
na sabuni vilevile.
Kayigi aliniuliza kama hakuna vitu vingine amabavyo nimesahau ili
anikumbushe tusije tukasahau na vile vilivyokuwa vinahusu matumizi ya
nyumbani. Kwa kusema hayo nilianza kuangalia kulia na kushoto, mbele
na nyuma kwa ajili ya kuchunguza aina mbalimbali za bidhaa tofauti ili nisije
nikasahau chochote nilichoambiwa na mama.
Nilikumbuka kuwa, mama alikuwa ameniambia kununua nyama, viazi vitamu, maharagwe na sukari. Tulipofika sokoni, tulishangaa kuona watu wengi wa marika tofauti wakijaa sehemu zote. Kelele nyingi za watu sokoni zilikuwa zimehanikiza si huku si kule.
Kayigi alinishika mkono na kunielekeza pahali panapouzwa bidhaa tofauti. Sauti hizo zilikuwa za wauzaji wakisema: Mia bei! Mia bei! ….karibu mteja… bei rahisi…..chagua….chagua…..kaptula hii ni mia tatu, jaketi hii ni mia tano. Karibu mteja wangu. Karibu katika kibanda changu. Bidhaa ni nyingi utachagua zile utakazo. Tulianzia sehemu panapouzwa nguo.
Kayigi nami tulifika mbele ya kibanda cha nguo tukaanza kuuliza bei ya vile tulivyokuwa tunataka. Kwanza niliuliza bei ya jaketi niliyokuwa nimechagua. Muuzaji alinijibu kuwa jaketi ilikuwa elfu moja. Nilimwambia apunguze kidogo kwa kuwa bei ilikuwa ghali. Tulijadiliana bei mpaka akakubali mia tisa.
Baada ya kununua nguo, tuliendelea kutembea sokoni tukanunua vifaa vya shule. Kwenye kibanda cha vifaa vya shule, tulinunua madaftari na kalamu. Bei za kila bidhaa zilikuwa ni bei nafuu. Daftari moja tulilinunua kwa mia moja na hamsini na kalamu kwa mia tu.
Kabla ya kurudi nyumbani, tulikumbuka kuwa mama alitutuma kununua nyama kwenye bucha. Nilichunguza mfukoni mwangu pesa nilizokuwa nabaki nazo nikaona mnabaki dola mia tano za Marekani tu. Niliuliza dada yangu jambo la kufanya akanishauri kwenda kwenye duka la kubadilisha pesa za kigeni. Tulikwenda mbio na kufika kwenye nyumba ya ghorofa kubwa ambapo pamekuwa maduka mengi ya kubadilisha pesa.
Tuliingia duka moja ambamo tulikaribishwa na kijana mmoja aliyetubadilishia pesa zetu katika pesa za Rwanda tukarudi sokoni.
Kwenye bucha, bei ilikuwa ghali pia kwani kilo moja ya nyama ilikuwa mbili elfu mia tano. Kayigi alijaribu kupunguzisha bei. Muuza nyama alikataa kuipunguza akisema kuwa hawezi kupata faida akipunguza. Je, mnataka nipate hasara? Muuza nyama aliuliza. Nilimwomba kupunguza bei kidogo kufika mbili elfu mia tatu.
Aidha, tulinunua kifungu kimoja cha mboga za sukumawiki, vifungu viwili vya nyanya na kilo moja ya chumvi.
Ilipofika saa saba za mchana tulichukua basi tukarudi nyumbani. Tulipofika nyumbani mama alitushukuru kwa kuwa hatukukawia kurudi na kuwa
tulitumia pesa vizuri. Kila mmoja alimwahidi kumpa tuzo ya peremende mbili.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
a. Taja aina mbili za bidhaa ambazo mama aliwatuma wanawe sokoni.
b. Ni kwenye sehemu gani ya soko ambapo Kayigi na Niwemwiza walinunua madaftari na kalamu?
c. Nini kilichosababisha Kayigi na Niwemwiza kushangaa walipofika sokoni?
d. Kwa sababu gani mchinjaji alikataa kupunguza bei ya kilo moja ya nyama?
e. Ni kwa sababu gani mama aliwapongeza wanawe walipotoka sokoni?
19.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3: Toa maana ya msamiati ufuatao:
a. Faida
b. Bei ghali
c. Kununua
d. Kuuza
e. Bucha
f. Hasara19.3. Sarufi: Matumizi ya ngeli ya I-ZI
Kazi ya 4:
Tazama sentensi zifuatazo na kujadili mabadiliko ya kisarufi yanayojitokeza.
a. Biashara imetajirisha watu wengi duniani na kuendeleza hali yao ya
maisha (Umoja).
• Biashara zimetajirisha watu wengi duniani na kuendeleza hali yao
ya maisha (Wingi).
b. Nguo ambayo imechafuka imemuambukiza magonjwa (Umoja).
• Nguo ambazo zimechafuka zimewaambukiza magonjwa (Wingi).
Maelezo muhimu
Ngeli hii ya I-ZI inajumuisha nomino za vitu visivyo na uhai. Nomino hizi
umoja na wingi wake huwa ni sawa. Isitoshe, nomino hizi ni za vitu ambavyo
vinaweza kuhesabika k.m kalamu, meza, sahani, rafu, linga, saa, rula, soksi,
nyumba, karatasi, kamusi, wiki, siku, chaki, chupa, ndizi, kamba, bawaba,
pete, n.k.
Majina ya ngeli hii hutumia kiambishi nafsi “I” katika umoja na kiambishi nafsi
“ZI” katika wingi kufuatana na upatanisho wa kisarufi.
Matumizi ya majina ya ngeli ya I-ZI na vivumishi vya sifa
• Vivumishi “-baya” na”-pya” huchukua kiambishi “m-“ badala ya “n-“.
Mfano:
Umoja: Barabara mpya ilijengwa Kiramuruzi na kurahisisha
mawasiliano baina ya raia huko.
Wingi: Barabara mpya zilijengwa Kiramuruzi na kurahisisha
mawasiliano baina ya raia huko.
Umoja:Tabia mbaya inakemewa na wengi
Wingi: Tabia mbaya zinakemewa na wengi
Vivumishi vinavyoanza na “r” herufi hiyo hugeuka “nd” inapotanguliwa na
kiambishi “n”.
Mfano:
Umoja: Ndoo ndefu imewekwa bafuni ili kuogea mikono.
Wingi: Ndoo ndefu zimewekwa bafuni ili kuogea mikono.
• Vivumishi vinavyoanza na “ch, f, p, k, t” havipachikwi viambishi katika
umoja wala wingi.
Mfano:
Umoja: Meza chafu imetupwa nje.
Wingi: Meza chafu zimetupwa nje.
Umoja: Nyumba kubwa na ya kisasa inahitajika mjini.
Wingi: Nyumba kubwa na za kisasa zinahitajika mjini.
Umoja: Sketi fupi inakatazwa shuleni.
Wingi: Sketi fupi zinakatazwa shuleni.
Umoja: Meza kubwa imewatosha watu wengi harusini.
Wingi: Meza kubwa zimewatosha watu wengi harusini.
Umoja: Ndizi tamu imenunuliwa sana sokoni.
Wingi: Ndizi tamu zimenunuliwa sana sokoni.
Umoja: Nyumba pana iliwatosha wageni wote wakati wa mkutano wa
kimataifa.
Wingi: Nyumba pana ziliwatosha wageni wote wakati wa mkutano wa
kimataifa.Kazi ya 5:
Chagua neno linalofaa na kuliandika katika nafasi iliyoachwa wazi.
1. Barabara hii ni ……….lakini imepasuka kwa sababu haikujengwa
vizuri. (Zipya, kipya, mpya)
2. Tafadhari nipe Kamusi ya Kiswahili ……… kuna msamiati mgumu
ninaotaka kuchunguza ( kisanifu, jisanifu, sanifu)
3. Karatasi …………zimetupwa jalalani ( mchafu, wachafu, chafu).
4. Meza …………imewekewa bidhaa nyingi sokoni (vipana, pana,
kipana)
5. Pombe ………iliwalevya watoto na kusababisha kutohudhuria
masomo (mtamu, litamu, tamu)
Kazi ya 6:
Kwa kutumia vivumishi vya sifa, tunga sentensi sahihi kwa kutumia
maneno yafuatayo:
a. Nyumba
b. Shule
c. Karatasi
d. Baiskeli
e. Nyumba
19.4. Matumizi ya lugha: Msamiati maalumu katika uwanja
wa kibiashara
Kazi ya 7:
Taja istilahi tano zitumiwazo katika shughuli za kibiashara na kueleza
maana yake.
Maelezo muhimu kuhusu msamiati unaotumiwa katika shughuli za
kibiashara.
• Biashara: ununuzi na uuzaji wa bidhaa na/au huduma.
• Faida/tijara/kivuno/chumo/ziada - Pato libakialo baada ya kuondoa
gharama za kufanya biashara k.v. ununuzi na usafirishaji.
• Hasara: Ukosefu wa faida; hali ya kupoteza pato au mali katika biashara.
• Bei: Kiwango cha pesa kununulia au kuuzia bidhaa au huduma fulani.
• Bei: Kiwango cha pesa kununulia au kuuzia bidhaa au huduma fulani.
• Uuzaji wa rejareja: Uuzaji wa kiasi kidogo kidogo.
• Uuzaji wa jumla: Uuzaji wa kwa pamoja
• Bei rafi: Bei ambayo haipunguzwi.
• Kipimo rafi: Kipimo ambacho hakipunguzwi.
• Bei ya kuruka: Bei isiyokubalika kisheria/haramu.
• Rasilimali: Jumla ya mali inayomilikiwa na mtu au nchi.
• Malighafi: Mali inayotumika kutengeneza vitu vingine k.m. pamba ni
malighafi ya kutengenezea nguo.
• Maliasili: Utajiri kama vile madini, misitu, maziwa, mito, anga
vinavyopatikana katika mazingira.
• Uwekezaji: Kutumia pesa / mali ili kuzalisha fedha/mali zaidi (ilikupata
faida).
• Kitegauchumi: Rasilimali k.v. kiwanda inayotumika kuzalisha mali.
• Ujasiriamali: Uwekezaji mtaji katika biashara.
• Mtaji: Mali ya kuanzisha biashara au kuipanulia.
• Ulanguzi: Ufichaji wa bidhaa ili bei yake iruke.
• Magendo: Upigaji biashara kwa njia haramu/isiyo halali.
• Chenji: pesa inayobaki baada ya kununua kitu
• Maduhuli: Bidhaa ambazo hununuliwa kutoka nchi za nje.
• Mahuruji: Bidhaa zinazouzwa nchi za nje.
• Ushuru: Kodi ya kuingiza bidhaa nchini au kuziuza/Ada ya forodha.
• Ruzuku: Pesa inayotolewa na serikali kwa idara mbalimbali ili
kujiendeleza.
• Mshitiri: Mnunuzi.
• Mteja: Mtu aendaye kununua bidhaa au huduma.• Wakala: Ajenti
• Utandawazi: Utaratibu wa mataifa kushirikiana katika nyanja mbalimbali
k.v. biashara.
• Ubinafsishaji: Hali ya kusababisha mali ya umma imilikiwe na watu
binafsi.
• Ubia: Ushirikiano wa watu wawili au zaidi katika shughuli k.v. ya
biashara.
• Hawala: Hundi/ cheki yaani cheti maalumu cha benki kinachotumiwa
kuidhinisha aliyetajwa kwenye cheti hicho apewe fedha za mwenye
hesabu.
• Amana: Kitu unachomwekea mwenzako hadi atakapokihitaji.
• Turuhani: Kiwango kinachotolewa kutoka katika bei iliyotangazwa.
• Iktisadi: Uangalifu katika kutumia fedha/mali.
• Ubepari: Mfumo wa uchumi ambao unawawezesha watu wachache
kumiliki rasilimali na vitegauchumi.
• Ukiritimba: Hali ya kuzuia wengine kufanya biashara au kushindana
katika biashara.
• Dukakuu: Duka kubwa ambapo wateja hujichukulia bidhaa watakazo
kutoka rafuni.• Hisa: Sehemu ya mtaji katika biashara.
Kazi ya 8:
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo
a. Hundi
b. Mteja
c. Ruzuku
d. Magendo
e. Rasilimali
19.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 9:
Tega sikio habari inayosimuliwa na mwanafunzi mwenzako kuhusu
safari yake sokoni na kusimulia hali ya safari hiyo mbele ya darasa.
19. 6. Kuandika
Kazi ya 10:
Tunga kifungu cha habari chenye aya tatu kuhusu safari yako sokoni.
SOMO LA 20: MAJADILIANO DUKANI
Kazi ya 1:
Taja mahali fulani panapofanyiwa biashara na huduma zinazotolewa hapo.20.1. Kusoma na ufahamu: Muuzaji na mteja
Mazungumzo yafuatayo yanahusu Kalisa ambaye ni mteja na Uwera ambayeni muuzaji. Wanajadiliana bei dukani.
Kalisa : Habari za asubuhi bibi !
Uwera : Nzuri. Nikusaidie nini ?
Kalisa : Nataka kununua bidhaa tofauti tofauti katika duka lako. Naona duka
lako lina bidhaa mbali mbali zinazovutia macho.
Uwera : Ndiyo. Mimi ninaagiza bidhaa kufuatana na mahitaji ya wateja ili
waweze kufaidika na kile wanachokinunua.
Kalisa : Mimi nahitaji sabuni, kilo moja ya chumvi, kilo mbili za sukari, nusu
ya vitunguu, lita ya mafuta ya kupikia na sufuria moja.
Uwera : Vyote hapa Kalisa.
Kalisa :Kila bidhaa ambayo nimekutajia inauzwa kwa bei gani ?
Uwera : Bidhaa hizi zote zinauzwa kwa bei nafuu. Sabuni moja ni faranga
mia moja, kilo moja ya chumvi ni faranga mia tatu, nusu ya vitunguu ni
faranga mia moja hamsini, lita ya mafuta ya kupikia ni mia tano na sufuria
hii ni moja elfu.
Kalisa : Mbona sufuria ni bei ghali ? Je, unaweza kupunguza kidogo ?
Uwera : Hiyo ni bei rafi bwana. Ungenunua sufuria mbili ningekupunguzia.
Kalisa : Nipunguzie faranga mia moja nitaendelea kununulia hapa.
Uwera : Ninakupunguzia faranga hamsini tu kwa sababu sufuria hii ni kubwa.
Kalisa : Asante. lakini chukua mizani unipimie kilo ya chumvi na nusu ya
vitunguu.
Uwera : Ndiyo. Angalia hapa vipimo vinaenea. Kwa uhakika mizani yangu
ni mpya sikunyang’anyi.
Kalisa : Hakuna nyongeza bibi ?
Uwera : Nitakupatia nyongeza ya kutosha siku ijayo.
Kalisa : Ni pesa ngapi ya kulipa kwa jumla?
Uwera : Mbili elfu kwa jumla.
Kalisa : Ahsante sana bibi.
Uwera : Asante kwa kushukuru. Karibu tena.Kalisa :Kwaheri !
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Taja bidhaa zinazozungumziwa katika mazungumzo haya.
2. Kalisa alinunua nini dukani ?
3. Nini umuhimu wa mizani ?
4. Ni kwa sababu gani Uwera huuza bidhaa zinazovutia macho ya watu ?5. Uwera alimwahidi Kalisa kumfanyia nini siku ijayo ?
20.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Toa maelezo ya bidhaa zifuatazo:
a. Kekee
b. Patasi
c. Chungu
d. Jiko la mkaa
e. Almasi
f. Dhahabu
g. Maziwa
h. Kuku
i. Maparachichij. Tikitimaji
20.3. Sarufi: Matumizi ya ngeli ya I-ZI na vivumishi vya a-unganifu
Kazi ya 4:
Tazama sentensi katika sehemu A na sentensi katika sehemu B nakueleza mabadiliko ya kisarufi yanayojitokeza.
Maelezo muhimu kuhusu matumizi ya vivumishi vya a-unganifu
Majina ya ngeli ya I-ZI yakitumiwa pamoja na vivumishi vya a-Unganifu,
umoja wake huchukua ya na wingi huchukua za.
Mfano:
Umoja: Runinga ya Gakire ilinipasha habari kuhusu nanma ya kuleta umoja na maridhiano kwetu
Wingi: Runinga za Gakire zilinipasha habari kuhusu nanma ya kuleta umoja na maridhiano kwetu.
Umoja: Rafu ya mama inajaa bidha nyingi.
Wingi: Rafu za mama zinajaa bidha nyingi.
Kazi ya 5:
Tunga sentensi 5 kwa kutumia majina ya ngeli ya I-ZI na kiambishi
cha -a unganifu
20.4. Matumizi ya lugha: Aina za bidhaa zinazopatikana
sokoni
Kazi ya 6
Bainisha aina kumi za bidhaa zinazopatikana sokoni.
Maelezo muhimu
Kuna aina mbalimbali za bidhaa zinazouzwa na kununuliwa sokoni. Baadhi
ya bidhaa hizo hutokana na kilimo, ufugaji, vifaa vya ufundi na vile ambavyo
hutengenezewa viwandani.
Kazi ya 7:
Toa mifano miwili miwili ya bidhaa zinazoweza kupatikana katika mazingira
ya sokoni (Bidhaa zitokanazo na viwanda, mazao, ufugaji, madini)
20.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 8:
Buni mazungumzo kati yako na mwenzako kuhusu majadiliano
kati ya muuzaji na mnunuzi. Majadiliano haya yafanyike sokoni na
yaonyeshe kutokubaliana kwenye bei ya bidhaa zinazouzwa.
20.6. Kuandika
Kazi ya 9:
Tunga mazungumzo yasiyopungua ukurasa mmoja kuhusumajadiliano ya bei dukani.
Kazi ya 1:
Tazama mchoro hapo juu na kueleza kinachofanyika.21.1. Kusoma na ufahamu: Matumizi bora ya mizani
Bwana Muhire ni mfanyabiashara katika soko linaloitwa Maridadi. Biashara
yake inahusu uuzaji wa matunda, bidha za kula, na mafuta ya kupikia. Mara
nyingi raia humlalamikia wakisema kuwa yeye hatumii vipimo sahihi.
Siku moja, Amina alikwenda sokoni kununua bidhaa tofauti za matumizi
ya nyumbani. Soko hilo lilikuwa kwenye umbali wa kilomita mbili kutoka
kwake. Alipofika sokoni, alikaribishwa na muuzaji aitwae Muhire. Muhire
anajulikana sana katika soko hili la Maridadi. Muhire alimwomba kutaja vitu
vyote alivyokuwa anataka kununua.
Baadhi ya bidhaa alizokuwa anahitaji kulikuwa kilo kumi za maharage,
kilo moja na nusu ya chumvi, lita tano za mafuta ya kupikia, gramu mia
mbili hamsini ya nyama za kupikia ndugu yake mdogo, mafungu mawili ya
sukumawiki na fungu moja la nyanya.Baada ya kuorodhesha bidhaa hizo zote, aliomba Muhire kuchukua mizani
na kupima ili kuhakikisha kwamba hamnyang’anyi. Muhire alichukua
mizani na kuanza kupima maharagwe. Alipomaliza kupima, Amina aliona
kuwa maharagwe yaliyokuwa yamepimwa yalikuwa machache akaanza
kumlalamikia. Mbona unanipa maharagwe kidogo? “Mizani yako si sahihi,”
Amina alisema. Amina alienda nyuma ya kibanda akapigia simu mfanyakazi
katika Bodi ya Mapato Rwanda.
Katika dakika thelathini viongozi wanaohusika na ushuru nchini walitembelea
soko hilo na kuwakagua wafanyabiashara halamu. Walitembelea watu
ishirini na kukagua jumla ya mizani ishirini na miwili. Baadhi ya mizani hiyo,
iliyokutwa sahihi ni ishirini na jumla ya mizani miwili ilikutwa na kasoro.
Tokea hapo, mizani hii haikuruhusiwa katika biashara mpaka itengenezwe
na mafundi na kuhakikiwa upya na wakala wa Vipimo ili iweze kuruhusiwa
kutumiwa katika biashara.
Wafanyabiashara waliotuhumiwa ni Muhire na Kazimoto ambao walikubali
kosa lao la kutaka faida nyingi mno kwa njia isiyo halali. Bila kusita , viongozi
waliwashawishi raia na wafanyabiashara kutumia mizani iliyopimwa tu yaani
iliyo sahihi.
Katika hatua nyingine, kiongozi mkuu aliwaonya wafanyabiashara
wanaolalamikiwa kuweka mawe, kokoto pamoja na mchanga,vipande vya
vyuma na aina nyingine za vitu kwenye mizani kwa ajili ya kuongeza uzito
waache tabia mbaya hiyo mara moja kwani wakikamatwa watapata hasara.
Alieleza kwamba sheria ya vipimo ipo na inafanyakazi kwa pande zote mbili
yaani kwa muuzaji na mnunuzi.
Wote hawatakiwi kufanya udanganyifu wowote katika biashara. Alisisitiza
kuwa wale watakaobainika kuchezea mizani kwa ajili ya kuwaiba wananchi
adhabu ni kubwa sana kwawo kama vile kifungo au kutozwa faini au vyote
kwa pamoja ; shabaha ikiwa ni kumlinda mlaji ili apate faida na thamani ya
kile alichozalisha ama kukinunua na siyo tu kupunjwa na wafanyabiashara
wajanjawajanja.
Baada ya mkutano, mbele ya watu wote waliokuwa wamekusanyika hapo
sokoni, viongozi walitoa tuzo ya mizani nne kwa wafanyabiashara ambao
hawakuwa na makosa yoyote katika shughuli zao za kibiashara. Hii ilikuwa
ni kutoa mfano kwa watu wote ili kusipatikane tena kosa lile la kuiba watu.
Watu waliokuwepo walifurahi na kuwapigia makofi viongozi wao. Viongozi
nao waliwapongeza kwa kuwa waliwajulisha hali ya makosa yanayofanywa
na wafanyabiashara wakiwanyonya raia.Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Nani ambaye alilalamikiwa kuwa na matumizi ya mizani isiyo sahihi?
2. Bainisha aina mbili za adhabu ambazo hupewa mtuhumiwa anayehusika na matumizi ya mizani isiyo sahihi.
3. Ni onyo gani lililotolewa na kiongozi mkuu kwa wafanyabiashara wanaotumia mizani kinyume na sheria?
4. Eleza lengo la ziara ya viongozi wanaohusika na ushuru katika soko la Maridadi.
5. Afanyaye vizuri hutuzwa. Eleza kauli hii kwa kutoa mfano kutoka katika kifungu hiki cha habari.
21.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:Oanisha maneno katika sehemu A na maana yake katika sehemu B.
21.3. Sarufi: Matumizi ya ngeli ya I-ZI na vivumishi vya kurejesha
Kazi ya 4
Soma sentensi katika sehemu A na kujadili mabadiliko ya kisarufiyanayojitokeza katika sehemu B:
Maelezo muhimu
Majina ya ngeli ya I-ZI, katika sentensi hutumia kirejeshi -yo katika umoja
na kirejeshi -zo katika wingi. Vivumishi hivi kuwa vinarejelea nomino.
Mfano:
Umoja: Pikipiki ambayo amenunua imemtajirisha.
Wingi: Pikipiki ambazo wamenunua zimewatajirisha.
Kazi ya 5
Kwa kutumia kirejeshi amba-, tunga sentensi katika umoja na wingi
kwa kutumia maneno yafuatayo:
a. Klabu
b. Chupa
c. Redio
d. kaptula
e. suruali
21.4. Matumizi ya lugha: Matumizi ya mizani katika hesabu na aina za pesa
Kazi ya 6
Taja aina za mizani au vipimo unavyovijua
Maelezo muhimu
A. Matumizi ya mizani au vipimo
Kipimo ni kiasi au kadiri. Kuna vipimo vya aina tofauti.
Jedwali lifuatalo linaonyesha aina mbalimbali za vipimo.
B. HesabuMifano ya hesabu kwa tarakimu na kwa maneno kutoka 1-1,000,000
Kazi ya 7:
Andika kwa tarakimu
a. Kumi na sita
b. Thelathini na moja
c. Sabini na saba
d. Mia tatu hamsini
e. Moja elfu mia mbili na saba
f. Laki tano
g. Moja elfu mia mbili ishirini na sita
C. Alama za hesabu
Alama ni mchoro wa kutambulisha kitu (Ishara)Jedwali lifuatalo linaonyesha alama za hesabu na maana zake.
Kazi ya 8:
Andika kwa tarakimu
a. Sitini jumlisha kumi ni sawa na sabini.
b. Mia moja arobaini toa ishirini na saba ni sawa na mia moja na kumi na tatu.
c. Mia nane na themanini gawanya kwa nane ni sawa na mia moja na kumi.
d. Sabini na moja ni kubwa kuliko kumi na nne.
e. Mia moja ni ndogo kuliko laki moja.
f. Tisini mara tatu ni sawa na mia mbili na sabini.
D. Aina za pesa zitumiwazo katika shughuli za kibiashara
Kazi ya 9:Tazama mchoro ufuatao na kueleza shughuli zinazofanyiwa hapo.
Maelezo muhimu
Pesa ni nini?
Pesa ni chombo cha kubadilishana bidhaa na huduma kati ya watu. Pesa
zenyewe hazina faida na hazitoshelezi mahitaji ya binadamu ila zimekubalika
katika jamii kama njia ya kujipatia mahitaji mengine. Kuna majina mengine
ya pesa katika Kiswahili, kama kwa mfano: hela, fedha, dirhamu, darahima,
fulusi au sarafu, n.k.
Pesa hutolewa na serikali ya nchi au na taasisi kama vile benki kuu inayofanya
kazi hii kwa niaba ya serikali.
Kuna aina nyingi za pesa zinazotumiwa duniani katika biashara. Jedwali
lifuatalo linatuonyesha baadi ya aina tofauti za pesa na nchi au bara
zinakotumiwa.
Kazi ya 10:
Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia aina ya pesa zinazotumiwa
katika nchi au bara husika.
a. Wanyarwanda wengi hutumia …………………..katika shughuli
nyingi za biashara ya ndani.
b. Mjomba wangu alikwenda kumtembelea rafiki yake anayeishi
Uganda. Kabla ya kuvuka mpaka alikwenda kwenye duka la
kubadilisha pesa ili wampe ………..za Uganda.
c. Mama aliniahidi kwamba nikishika nafasi ya kwanza katika kidato
cha kwanza atanitembeza Marekani. Katika safari yetu tutatumia
………………… mia nne za kimarekani.
d. Shughuli za biashara anazozifanya mama yangu huhusisha
uagizaji wa bidhaa kutoka Japani. Kila wiki hulipa ……..elfu tano.
e. Je, uliwahi kufika katika duka la kubadilisha pesa? Mimi nilifikapo
nikaona faranga za Rwanda, Shilingi za Kenya, Dola za Marekani
na Kanada na ………..za Uingereza.
Kazi ya 11:
Tafuta aina tofauti za pesa zinazotumiwa katika nchi nyingine ambazo
hazikushughulikiwa katika somo hili.
21.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 12:
Katika jozi, simulia mwenzako sifa za soko fulani uliyoitembelea na
kueleza bidhaa ulizoziona.
21.6. Kuandika
Kazi ya 13:
Tunga kifungu cha habari kifupi kuhusu umuhimu wa biashara
Tathmini ya mada
1. Taja angalau vifaa kumi vinavyouzwa sokoni.
2. Chagua neno linalofaa katika mabano na kukamilisha sentensi
zifuatazo:
a. Mwalimu wetu huvaa suti nzuri sana. Wanafunzi wote hufikiri
kwamba suti zake hununuliwa kwa bei ………. (ghali, rahisi, rafi).
b. Dada yangu amekwenda sokoni …………………….sare ya shule ili arudi
shuleni kesho kuanza masomo ya muhula wa tatu( kununua, kuuza).
c. Uwantege anauza matunda katika soko la Nyagasambu. Kwenye kibanda
chake kuna ,………….,………,……… na ………….( maembe, ndizi
mbivu, machungwa, viazi vitamu, tikitimaji, mchele, madaftari, mananasi).
d. Mwenye duka la vitabu alitoa ………………………………. ya kitabu
kimoja cha hadithi za Kiswahili kwa wateja wote ambao hununua kwake
kila wiki (nyongeza, mtaji).
e. Wakati wa uhaba wa …………… sokoni, bei hupanda sana (wateja,
wanunuzi, bidhaa).
3. Kwa kuzingatia matumizi ya ngeli ya I-ZI, tunga sentensi sahihi kwa
kutumia maneno yafuatayo:
a. Nchi
b. Tarafa
c. Serikali
d. Barabara
e. Shule
4. Kamilisha kifungu cha habari hiki kwa kutumia maneno sahihi.
Mama Mutoni ni mfanyabiashara katika soko la Nyarugenge. Mara nyingi
huagiza bidhaa kutoka nchi zinazopakana na Rwanda. Anapoagiza
bidhaa kutoka Uganda inambidi abadilishe …………za Rwanda katika
……………..za Uganda. Ni sawa na kuagiza bidhaa kutoka Tanzania na
Kenya.
Ikiwa Mama anahitaji bidhaa zinazotengenezewa katika nchi za Ulaya
kama Vile Uingereza, inambidi kutumia ………………Mwezi uliopita
rafiki yake ambaye anaishi Marekani alimwambia kuwa kuna bidhaa
nzuri zinazoweza kumletea faida nyingi anapoziuza kwa Wanyarwanda.
Mama aliamua kumtumia ………….elfu tatu za Marekani ili amnunulie
bidhaa hizo.
Kazi ya biashara naipenda sana. Kuna wakati amabapo naenda pamoja
na mama yangu Zambia na Libya kufanya biashara huko nikaona namna
anavyobadilisha faranga zake katika …………….. Libya au ……….za
Zambia nikawa na motisha ya kufanya biashara ya kubadilisha pesa siku
moja. Mimi nafikiri kwamba aina hii ya biashara itachangia kuongeza
mapato yetu nyumbani.
5. Buni mazungumzo yenye ukurasa mmoja kati ya muuzaji na
mnunuzi katika duka la vitabu.