MADA YA 3 MSAMIATI KATIKA MAZINGIRA YA HOSPITALI
Uwezo mahususi katika mada hii:
Kuzungumza na kuandika kwa ufasaha matini fupifupi kwa kutumia msamiati
unaofaa katika mazingira ya hospitalini.
Malengo ya Ujifunzaji:
• Kutumia kwa ufasaha msamiati maalum wa mazingira ya hospitali katika mawasiliano;
• Kueleza vifaa vya hospitalini na umuhimu wake,
• Kubainisha wafanyakazi wa hospitalini na majukumu yao,
• Kusikiliza kwa makini na kusoma kwa ufasaha kifungu cha habari kinachohusika,• Kunyambua vitenzi kwa kuzingatia kauli mbalimbali.
Kidokezo
1. Hospitali ni nini?
2. Orodhesha angalau hospitali tatu muhimu zinazojulikana nchini Rwanda.
3. Taja vifaa vitano vinavyotumiwa hospitalini na kueleza umuhimu wake.
4. Bainisha wafanyakazi angalau wanne wapatikanao hospitalini na kuainisha kazi au majukumu yao.SOMO LA 10: SEHEMU ZA HOSPITALI
Tazama kwa makini mchoro hapa juu. Zungumzia vitu muhimu
unavyoona vyenye uhusiano na hospitali.10.1. Kusoma na ufahamu: Ziara yetu hospitalini
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maadili wamefanya ziara kwenye hospitali
moja wilayani Huye. Shabaha yao ni kuielewa vyema hospitali. Wamekaribishwana mpokezi wageni ambaye amewaongoza kwa Daktari Mkuu.
Daktari: Hamjambo vijana!
Vijana: Hatujambo Daktari!
Aminata: Jina langu ni Aminata na mimi ndimi kiranja wa darasa letu. Hawa
ni wanafunzi wenzangu.
Tumefurahia fursa hii ya kuitembelea hospitali yenu kwa ajili ya kuyaelewa
vyema mazingira ya hospitali.
Daktari: Asante sana kwa nia yenu. Kwa hiyo, karibuni nyote!
Mimi ni Birashoboka, Daktari Mkuu wa hospitali hii. Na huyu ni muuguzi
wetu, jina lake Veneranda.
Nifuateni sasa niwatembeze sehemu mbalimbali za hospitali.
Muuguzi: Tuanzie kwenye sehemu ambapo mmekaribishiwa na kupata kiti.
Sehemu hiyo huitwa pambajio. Ni sehemu ya kuwapokelea wagonjwa.
Pascal: Samahani Daktari! Sisi siyo wagonjwa, msije mkatudunga sindano!
Daktari: Hahaaaa! Usiwe na wasiwasi kijana! Tafadhali tuendelee. Sehemu
hii ni chumba cha matibabu ya dharura, yaani chumba cha kuwatibia
wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka sana kama vile majeruhi wa ajali.
Muuguzi: Samahani Daktari! Ni vizuri kuelewa kwamba chumba cha
dharura ni tofauti na wodi kwani wodi ni chumba cha kushughulikia maradhi
ambayo si ya kawaida kama vile maradhi ambayo yamezuka ghafla na bado
hayaeleweki vizuri.
Daktari: Asante sana Muuguzi! Kama nyongeza, kuna wodi nyingine
ambayo ni sehemu ya kuwalaza wagonjwa wanaoendelea na matibabu.
Samilla: Samahani Daktari! Kwenye mlango ule nimesoma neno maabara.
Je, nini maana ya neno hili?
Daktari: Vizuri sana! Maabara ni chumba cha kufanyia uchunguzi wa
magonjwa. Kwa kuwa hatuna muda wa kutosha wa kuizunguka hospitali
yote, inafaa kusimamia hapa na kumwomba Muuguzi awaelezee sehemu
nyingine za hospitali.
Muuguzi: Asante sana Daktari! Kuna chumba cha kuhifadhia dawa;
kuna kungawi, yaani chumba cha kujifungulia kwa kina mama wajawazito;
chumba cha upasuaji; chumba cha uangalizi maalum ambacho ni chumba
cha matibabu ya kiwango cha juu sana. Hususan chumba hiki hutumiwakwa wagonjwa walio katika hali mahututi.
Daktari: Chumba hiki huwa na mitambo na mashine za hali ya juu sana za kumsaidia mgonjwa.
Muuguzi: Chumba cha mwisho ni ufuoni au makafani ambacho hutumiwa kuhifadhia maiti.
Jado: Asante sana kwa maelezo haya. Ningependa sasa mtuelezee kuhusu vifaa muhimu vinavyotumiwa humu.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
a. Soma kifungu cha habari hapa juu na kujibu maswali ya ufahamu yafuatayo:
1. Habari hii imetokea wapi?
2. Ni lengo gani la wanafunzi kuitembelea hospitali?
3. Ni watu gani wanaozungumziwa katika kifungu cha habari hiki?
4. Ni sehemu zipi za hospitali zilizotajwa?
5. Aminata alikuwa na wajibu gani?
b. Chagua jibu lililo sahihi kuliko mengine
1. Kifungu hiki cha habari kinazungumzia:
a. Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Maadili na Daktari.
b. Vifaa na wafanyakazi wa hospitali wilayani Huye.
c. Ziara ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maadili kwenye hospitali moja wilayani Huye.
d. Mazungumzo kati ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maadili kuhusu uchaguzi wa mchepuo wa udaktari.2. Walipofika hospitalini, wanafunzi walikaribishwa na
a. Muuguzi.
b. daktari mkuu.
c. nesi.
d. mpokeaji.
3. wanafunzi walitembezwa sehemu za hospitali na
a. daktari mkuu.
b. muuguzi pamoja na daktari mkuu.
c. mpokezi.
d. majibu yote ni sahihi.
4. Wanafunzi walielezewa vyumba vingapi ?
a. vyumba tisa.
b. vyumba vitatu.
c. vyumba kumi.
d. vyumba vitano.
e. hakuna jibu sahihi.
5. Kungawi ni chumba cha:
a. kuwapasulia wajawazito.
b. kuzalia wajawazito.
c. kununulia dawa.
d. kulalia wagonjwa.10.2. Matumizi ya msamiati kuhusu mazingira ya hospitali
Kazi ya 3:
Kwa kutumia Kamusi ya Kiswahili Sanifu au njia nyingine tofauti, toa
maana ya msamiati ufuatao na kuutungia sentensi sahihi.
1. Kudunga 6. Kuhifadhi
2. Matibabu 7. Uchafu
3. Mgonjwa 8. Mjamzito
4. Hali mahututi 9. Kujifungua
5. Kupenyeza 10. DharuraKazi ya 4:
Oanisha maneno katika sehemu A na maana zake kutoka sehemu B.
10.3. Sarufi: Matumizi ya kauli za vitenzi
Kazi ya 5:
Soma sentensi zifuatazo na kutofautisha viambishi vilivyokolea
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Maadili walikuwa wanapendana sana.
Waliandaa mpango wa kumwandikia Daktari Mkuu wa Hospitali kwa ajiliya kuitembelea hospitali yake.
Maelezo muhimu
Viambishi vilivyokolea ni viambishi vya mnyambuliko wa vitenzi.
Mnyambuliko wa vitenzi ni jinsi vitenzi vinavyobadilika kulingana na kauli/hali mbalimbali.
Hapo juu, kauli za vitenzi zilizotumiwa ni tatu kama ifuatavyo:
i. Kauli ya kutenda.
ii. Kauli ya kutendana.
iii. Kauli ya kutendea.
Yafuatayo ni maelezo kwa kila aina ya kauli:
1. Kauli ya Kutenda - kitendo katika hali yake ya kawaida (bila kunyambuliwa).
2. Kauli ya Kutendana - unamfanya mtu kitendo, naye anakufanya vivyo hivyo.
3. Kauli ya Kutendea - kufanya kitendo kwa niaba (au kwa ajili) ya mtu mwingine.Kazi ya 6:
Onyesha mnyambuliko wa vitenzi ulivyochagua kisha uviweke katika
hali ya kutendea na kutendeana.
Kazi ya 7:
Tunga sentensi ambazo vitenzi vyake vinabeba kauli ya kutenda,
kutendea na kutendana
Kazi ya 8:
Andika vitenzi vifuatavyo katika hali ya kutendea kwa kuzingatia
mabadiliko ya kimaana.
1. Tumeandika barua kwa ajili ya rafiki zetu.
2. Wazazi walifanya mema kwa niaba ya watoto wao
3. Baba yake ameweka pesa kwenye akaunti kwa manufaa ya mtoto wake.
10.4. Matumizi ya lugha: Sehemu muhimu za hospitali
Maelezo muhimu kuhusu sehemu muhimu za hospitali
Hospitali ni mahali pa kutibia wagonjwa. Kuna hospitali kubwa na nyinginendogo. Hospitali ndogo huitwa dispensali au zahanati.
Hospitali ina sehemu muhimu zifuatazo:
1. Pambajio: Sehemu ya kuwapokelea wagonjwa.
2. Wodi: Sehemu ya kuwalaza wagonjwa wanapoendelea kupokea
matibabu.
3. Kungawi: Chumba cha kujifungulia kwa waja wazito.
4. Chumba cha upasuaji: Chumba cha kufanyiwa upasuaji wa wagonjwa.
5. Wodi wa matibabu maalum: Chumba cha kushughulikia maradhi ambayo si ya kawaida k.m. maradhi ambayo yamezuka ghafla na bado hayaeleweki vizuri.
6. Chumba cha matibabu ya dharura: Chumba cha kuwatibia wale wanaohitaji matibabu ya haraka sana k.m. waathiriwa wa ajali.
7. Chumba cha matibabu ya kina: Chumba cha matibabu ya kiwango cha juu sana. Hususan hutumiwa kwa wale walio katika hali
mahututi. Chumba hiki huwa na mitambo na mashine za hali ya juu za kumsaidia mgonjwa.
8. Maabara: Chumba cha kufanyia utafiti.
9. Chumba cha dawa: Chumba cha kuhifadhia dawa zitolewazo kwa wagonjwa.
10. Ufuoni/makafani: Mahali pa kuhifadhia maiti.10.5. Kusikiliza na Kuzungumza
Kazi ya 10:
Sikiliza taarifa ya habari moja kutoka redio au runinga juu ya mambo
ya afya. Isimulie mbele ya darasa.
Kazi ya 11:
Kwa ushirikiano na wenzako, igiza mazungumzo hapo juu
Kazi ya 12:
Fikiria zahanati au hospitali moja uliyoitembelea, kisha zungumziachumba kimoja ambamo uliingia na sababu za kuitembelea.
10.6. Kuandika
Kazi ya 13:
Chora hospitali moja na kuonyesha sehemu zake angalau nne nakueleza umuhimu wake
Kazi ya 1:
Tazama kwa makini mchoro hapa juu. Zungumzia vitu muhimu unavyoonavyenye uhusiano na hospitali.
11.1. Kusoma na ufahamu: Vifaa vya hospitalini
Daktari: Kabla ya kutembelea vyumba vyote ambamo mmepatikana vifaa
mbalimbali, tazameni picha hizi za vifaa vipatikanavyo hospitalini. Picha hii ni ya
eksrei au uyoka ambayo ni mashine ya kutazamia viungo vya ndani ya mwili.
Muuguzi: Hii ni machela, yaani kigari au kitanda cha kubebea wagonjwa.
Aminata: Tafadhali Muuguzi. Je, naweza kuwasaidia? Picha inayofuata
ninajua jina lake.
Muuguzi: Vizuri sana! Kushirikiana katika kazi zote ni jambo muhimu sana.
Fursa ni yako kiongozi wa darasa.
Aminata: Ile ni mikroskopu au hadubini. Inatumiwa kuangalia vijidudu
vidogo sana ambavyo haviwezi kuonekana kwa macho tu.
Daktari: Hongera Aminata! Tuendelee. Hii ni dipfriza ambayo ni chombo
cha kuhifadhia dawa katika kipimo cha baridi kali sana.
Muuguzi: Jiko lile hutumiwa kuchemshia vyombo ili kuulia vijidudu na bakteria.
Kifaa hiki chenye umbo sawa na soksi kinaitwa glovu. Kinavaliwa mkononi
kumkinga muuguzi dhidi ya uchafu au kuambukizwa na maradhi.
Daktari: Vifaa hivi ninadhani vinafahamika kwa kila mtu. Vijana, nani ambaye anaweza kutuelezea?
Bugingo: Hizi ni sindano. Zinatumiwa kupenyezea dawa mwilini. Pembeni
kuna makasi ambazo hutumiwa kwa kukatia vitu mbalimbali.
Muuguzi: Vijana, mpigieni makofi! Bendeji hii ni kitambaa cha kufungia
jeraha au kidonda kisichafuliwe.
Na hii ni plasta ambayo ni kitambaa kigumu sana cha kufungia sehemu ya
mwili iliyovunjika.
Daktari: Mwishoni, koleo hii husaidia kama kifaa cha kushikia vitu
vinavyotumiwa na daktari.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
a. Soma kifungu cha habari hapa juu na kujibu maswali ya
ufahamu yafuatayo:
1. Mazungumzo haya yametokea wapi?
2. Ni madhumuni gani ya wanafunzi kuitembelea sehemu hii?
3. Ni wahusika gani waliowasiliana?
4. Baadhi ya vifaa vilivyoonyeshwa, ni kifaa kipi ambacho kingeweza kuwatia hofu wanafunzi?
5. Daktari ametumia mbinu gani ya kuonyesha na kuelezea vifaa?
b. Chagua jibu lililo sahihi kuliko mengine
1. Kifungu hiki cha habari kinazungumzia:
a. Vifaa vitumiwavyo hospitalini
b. Daktari na wanafunzi
c. Ziara ya wanafunzi hospitalini
d. Hakuna jibu sahihi2. Katika maelezo yake, Daktari ameungwa mkono na
a. muuguzi
b. kiongozi wa darasa
c. wanafunzi
d. muuguzi pamoja na wanafunzi wawili.
3. Dipfriza ni mojawapo ya:
a. Wafanyakazi wa hospitalini
b. Dawa za hospitalini
c. Sehemu za hospitali
d. Vifaa vya hospitalini.
4. Machela inatumiwa kubeba
a. Dawa za wagonjwa
b. Walemavu
c. Vifaa vya hospitalini
d. Wagonjwa hospitalini.
5. Daktari au Muuguzi anatumia bendeji
a. Kumfunga kamba mgonjwa
b. Kufungia kidonda
c. Kufungia sehemu iliyovunjika
d. Kumwezesha mgonjwa kutembeatembea.11.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Kwa kutumia Kamusi ya Kiswahili Sanifu au njia nyingine tofauti, toa
maana ya msamiati ufuatao na kuutungia sentensi sahihi.
i. Vidudu
ii. Bakteria
iii. Kuhifadhi
iv. Jerahav. Kidonda
Kazi ya 4:
Jaza nafasi iliyoachwa wazi kwa kutafuta msamiati unaofaa kwenyeupande wa maneno na maana kwenye upande wa maelezo
Kazi ya 5:
Kamilisha sentensi zifuatazo ili zilete maana kamili kwa kutumia
msamiati huu: eksirei, plasta, sindano, kuhifadhia baadhi ya dawa.
1. Kitambaa kigumu sana cha kufungia sehemu iliyovunjika
huitwa.......................................................
2. Dipfriza ni chombo...................................
3. .......................ni kifaa cha kupenyezea dawa mwilini.
4. ..................ni mashine ya kuonea viungo vya ndani ya mwili.
11.3. Sarufi: Matumizi ya kauli za vitenzi
Kazi ya 6:
Soma sentensi zifuatazo na kutofautisha viambishi vilivyokolea
Baada ya mpango kukamilika, walifikisha hoja zao kwa Mkuu wa shule
ambaye aliridhika na nia hiyo ya wanafunzi wake.
Baadaye, walitumiwa barua na Daktari Mkuu wa hospitali ya kuwakubalia
ziara yao.
Maelezo muhimu
Kauli za vitenzi zilizotumiwa katika sentensi hapo juu ni zifuatazo:
i. Kauli ya kutendeka
ii. Kauli ya kutendesha
iii. Kauli ya kutendewa
Yafuatayo ni maelezo kwa kila aina ya kauli:
1. Kauli ya Kutendeka - kitendo kukamilika au kuwa katika hali timilifu.
2. Kauli ya Kutendewa - kitendo kufanywa kwa niaba yako au kwa ajili yako.3. Kauli ya Kutendesha - kumfanya mtu atende jambo fulani.
Kazi ya 7:
Onyesha mnyambuliko wa vitenzi vifuatavyo katika hali ya kutendeka
na kutendewa
Vitenzi ni kunywa, kuzaa, kupenda, kutaja na kujenga.
Kazi ya 8:
Tunga sentensi 3 ambazo vitenzi vyake vinabeba kauli ya kutendeka,
kutendesha na kutendewa
Kazi ya 9:
Soma kisa kifuatacho na kuweka vitenzi husika katika hali ya
kutendewa
Baba alimpatia mtoto wake elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira,
uzalishajimali pamoja na usawa wa kijinsia. Alimwelezea pia faida za
kupiga marufuku uvivu, ulevi pamoja na ukatili. Alimtungia hadithi za
kumwongoza na kumwelekeza katika njia nzuri za kimaisha. Baadaye,
alimpelekea wajibu wa kuzitetea haki za binadamu na kuishi kwa amani na
watu wote mahali popote atakapokuwepo.
11.4. Matumizi ya lugha: Vifaa vya hospitalini
Kazi ya 10:Taja majina ya vifaa vifuatavyo na kueleza umuhimu wa kila kifaa.
Kazi ya 11:
Tafuta vifaa vingine vinavyotumiwa hospitalini na kueleza umuhimu wake.
Maelezo muhimu
Hospitali hutumia vifaa mbalimbali wakati wa kuhudumia wagonjwa. Baadhi
ya vifaa hivyo ni hivi vifuatavyo:
1. Eksrei/uyoka: mashine ya kuonea viungo vya ndani ya mwili.
2. Machela: kigari au kitanda cha kubebea wagonjwa.
3. Mikroskopu/hadubini: kifaa kitumiwacho kuangalia vitu vidogo.
4. Dipfriza: chombo cha kuhifadhia baadhi ya dawa zinazohitaji kuhifadhiwa katika kiwango cha baridi sana.
5. Jiko: chombo cha kuchemshia vyombo ili kuulia viini na bakteria.
6. Glovu: kitu kama soksi kitengenezwacho kwa mpira na huwekwa mkononi kukingia uchafu.
7. Sindano: kifaa cha kupenyezea dawa mwilini.
8. Sirinji: kifaa chenye umbo la bomba ambapo madaktari na wauguzi huchopeka sindano ili kumdunga mgonjwa au kufyonza sampuli ya damu.
9. Makasi: kifaa ambacho hutumiwa kwa kukatia
10. Bendeji: kitambaa cha kufungia jeraha au kidonda
11. Plasta: kitambaa kigumu sana cha kufungia sehemu iliyovunjika
12. Koleo: kifaa cha kushikia vitu vinavyotumiwa na daktari.11.5. Kusikiliza na Kuzungumza
Kazi ya 12:
Kwa ushirikiano na wenzako, igiza mazungumzo yanayohusu vifaa
vya hospitalini.
Kazi ya 13:
Itembelee zahanati au hospitali moja, kisha uzungumzie vifaaulivyowahi kuviona.
Kazi ya 14:
Simulia hisia ulizokuwa nazo au ulizosikia kutoka mtu mwingine
kuhusu siku yako au yake ya kwanza kudungwa sindano hospitalini.
11.6. Kuandika
Kazi ya 15:
Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kuongozwa na muktadha wa vifaa vya hospitalini
a. Nilipokuwa bado mtoto nilikuwa na woga wa kuenda hospitalini kwa sababu....................................
b. Inasemekana leo kuwa Hospitali ya Roi Faisal ni maarufu sana kwa sababu....................................
c. Hospitali au zahanati nyingi hushindwa kutoa huduma bora kwa sababu ya..................................
d. Sindano hospitalini hutumiwa mara moja kwa mgonjwa kwa ajili ya.............................................SOMO LA 12: WAFANYAKAZI WA HOSPITALINI
Kazi ya 1:
Tazama kwa makini mchoro hapo juu kisha uzungumzie vitu muhimuunavyoviona
12.1. Kusoma na ufahamu: Kazi nzuri ya udaktari
Wanafunzi wameendelea na matembezi yao hospitalini. Sasa ni wakati
wa kuongea na wafanyakazi.
Muuguzi: Shukrani Daktari, ningependa tuelekee sehemu ambapo
tutawapata wafanyakazi mbalimbali ili niwaelezee kazi zao. Daktari au
tabibu mnayemwona hapa ndiye anayewatibu wagonjwa. Mimi ni Muuguzi
au nesi. Kazi yangu ni kumsaidia daktari katika kazi yake.
Mkunga: Jina langu ni Liberata. Mimi ni Mkunga. Kazi yangu ni kutoa
huduma kwa wajawazito wakati wa kujifungua.
Mhazigi: Ninaitwa Jean Paul. Mimi ni mhazigi. Wajibu wangu ni
kuwashughulikia waliovunjika viungo kama vile miguu au mikono.
Msaidizi: Ninaitwa Francoise, Msaidizi katika maabara. Mimi hutoa huduma
kwa wagonjwa.
Karani: Jina langu ni Shema, Karani wa hospitali. Jukumu langu ni kufanya
rekodi za wagonjwa.
Mfamasia: Mimi ni mfamasia na jina langu Pascasie. Kazi yangu ni kuziweka
dawa na kuzitoa kwa wagonjwa.
Daktari wa meno: Byiringiro Charles, daktari wa meno. Jukumu langu ni
kuwashughulikia wagonjwa walio na matatizo ya meno.Aminata: Kwa mujibu wa wanafunzi wenzangu, tumenufaika zaidi kutokana
na safari hii. Kwa kweli, tungeliitembelea hospitali hii mwaka jana, tungelijua
haya yote tayari. Wahenga walisema kwamba asiyefika kwa mfalme
hudanganywa mengi. Tumebahatika kufika hapa na mengi tumeyaelewa.
Mireille: Sisi sote tumeridhika na maelezo tuliyopewa. Kwa upande wetu,
tunaahidi kuwaunga mkono kama iwezekanavyo kwa kuchagua mchepuo
wa udaktari ili kuwahudumia wagonjwa hospitalini.
Daktari: Asanteni sana vijana. Kwa heri ya kuonana, tunawatakia kila la kheri!
Aminata: Asante sana Daktari pamoja na Muuguzi, na sisi tunawatakia kazi
njema!
Kazi ya 2:
Soma kifungu cha habari hapo juu na kujibu maswali ya ufahamu
yafuatayo:
1. Ni watu gani wanaozungumziwa katika mazungumzo haya?
2. Matembezi haya yamekuwa na lengo lipi?
3. Jadili faida pamoja na hasara kutoka ziara ya wanafunzi iliyozungumziwa.
4. Wanafunzi wameridhika na ziara yao. Je, unakubaliana na ukweli huu? Eleza msimamo wako.
12.2. Matumizi ya msamiati kuhusu mazingira ya hospitali
Kazi ya 3:
Kwa kutumia Kamusi ya Kiswahili Sanifu au njia nyingine tofauti,
toa maana ya msamiati ufuatao na kutungia sanifu sentensi sahihi.
a. Kutibu
b. Jukumu
c. Mujibu
d. Wahenga
e. kuahidi
Kazi ya 4:
Kazi ya 5:Husisha wafanyakazi wafuatao na vifaa wanavyotumia
12.3. Sarufi: Matumizi ya kauli za vitenzi
Kazi ya 6:
Soma sentensi zifuatazo na kutofautisha viambishi vilivyokolea
Walipowasili hospitalini walikaribishwa na kupokelewa vizuri. Walielezewa
mambo mengi sana na kuongezewa ujasiri wa kuchagua mchepuo waudaktari. Waliahidi kwamba kazi yao itafanywa kwa bidii.
Maelezo muhimu
Viambishi vilivyopigiwa mstari vinaonyesha kauli ya kutendwa ambayo
huathirika moja kwa moja na kitendo
Kazi ya 7:
Andika vitenzi vifuatavyo katika hali ya kutendewa kwa kuzingatia
mabadiliko ya kimaana.
1. Wezi wameniiba pesa zangu.
2. Tulimzaa mtoto wa kike miaka sita iliyopita.
3. Dawa imewaua nzi wengi kutoka chooni.
4. Kampuni ilimfikisha meneja wake mahakamani kwa sababu ya
uporaji mali.
5. Tumekula chakula kitamu kwa wingi.
6. Tulivua samaki wengi kutoka ziwa Kivu.
7. Si vizuri kunywea pombe hospitalini.
8. Wilaya itatengeneza barabara za lami nyingi.
9. Dobi amefua nguo za aina mbalimbali.
12.4. Matumizi ya lugha: Aina za kazi
Kazi ya 8:
Katika jozi, jadilini kuhusu kazi za watu mbalimbali mnazozijua.
Maelezo muhimu
Zipo kazi za aina nyingi duniani. Kazi hizi hutofautiana kulingana na ujuzi,
elimu na tajiriba ya kiwango cha juu.
Ifuatayo ni baadhi ya mifano mbalimbali ya kazi:
Mhasibu: Mtaalamu wa kuweka hesabu ya fedha.
Mhandisi/injinia: Mjuzi wa kutengeneza, kuhudumia na kuunda mitambo.
Tarishi/Katikiro: Anayehudumu ofisini kwa kutumwa kupeleka habari au ujumbe.
Bawabu: Alindaye mlangoni.
Topasi/chura: Asafishaye choo.
Tabibu/daktari/mganga: Mwenye ujuzi wa kutibu.
Muuguzi/mualisaji: Ahudumiaye wagonjwa.
Msarifu: Anayesimamia na kuidhinisha matumizi mazuri ya fedha katika
shirika.
Dereva: Aendeshaye vyombo vya nchi kavu k.v. gari.
Nahodha: Aendeshaye na kuongoza vyombo vya majini k.v. meli.
Rubani/Mwanahewa: Aendeshaye na kuongoza vyombo vya angani
k.v.ndege.
Utingo/taniboi: Mpakiaji na mpakuaji wa mizigo katika gari.
Hamali/mpagazi/mchukuzi: Abebaye mizigo kwa malipo.
Malenga: Mtunzi stadi wa mashairi na nyimbo.
Manju: Stadi wa kutunga na kuimba nyimbo katika ngoma.
Kuli: Apakiaye na kupakua shehena za forodhani.
Dobi: Afuaye na kupiga nguo za watu pasi kwa malipo
Sogora: Fundi wa kupiga ngoma
Saisi: Atunzaye wanyama wanaopandwa k.v. punda na farasi.
Msajili: Awekaye orodha ya kazi, vitu au viumbe.
Mkalimani/mtarijumani: Afasiriaye lugha moja hadi nyingine.
Sonara: Atengenezaye mapambo kwa kutumia madini.
Kinyozi: Anyoaye nywele.
Msusi/msosi: Asukaye watu nywele.
Ngariba: Mtu anayefanya kazi ya kutahiri katika jando.
Mkunga: Awasaidiaye wajawazito kujifungua.
Kungwi: Afundishaye mwari wa kike au kiume.
Mshenga: Atumwaye kupeleka habari za ndoa (posa).
Refa: Mwamuzi katika mchezo k.v. soka
Kasisi: Kiongozi wa kidini katika madhehebu fulani ya kikristo
Imamu: Kiongozi wa kidini katika madhehebu fulani ya kiislamu.
Hakimu: Aamuaye kesi katika mahakama.
Kadhi: Hakimu wa kiislamu
Mwekezaji: Anayeweka mali au pesa katika mradi au biashara.
Meneja: Msimamizi au kiongozi katika kampuni au shirika.
Karani: Afanyaye kazi ya kuandika k.m. barua na majarida.
Kocha: Mwalimu wa mchezo k.v. soka, voliboli, n.k.
Mkutubi: Ahifadhiye vitabu maktabani na kuviazima kwa wasomaji.
Mnajimu: Mwenye elimu ya nyota. Hutabiri mambo.
Mpigaramli: Abashiriaye kwa kupiga bao.
Mwajiri: Aandikaye mtu kwa kazi ya malipo au mshahara.
Mzegazega: Achotaye maji na kuyauza.
Dalali: Auzaye bidhaa katika mnada (soko la kushindania bei)
Manamba: Mfanyakazi wa muda katika shamba kubwa.
Mnyapara: Msimamizi wa kazi.
Mhazili: Sekretari - Atunzaye barua na majarida na kuandika kwa mashine ofisini.
Mhadhiri: Mwalimu katika chuo kikuu.
Mwashi: Fundi wa kujenga nyumba.
Mhunzi: Afuaye vitu vya madini ya chuma au bati.
Seremala : Atengenezaye samani za mbao au miti.
Mfinyanzi: Atengenezaye vyombo vya udongo k.m. vyungu.
Mvuvi: Afanyaye kazi ya kuvua samaki.
Mwanaanga: Afanyaye utafiti wa hali ya anga.
Mkabidhi: Mtu atunzaye mali kwa ajili ya mwingine
Diwani: Anayewakilisha watu wake katika serikali za wilaya
Mzoataka: Anayeokota takataka
Kaimu: Anayeshikilia cheo au wadhifa fulani kwa muda.
12.5. Kusikiliza na Kuzungumza
Kazi ya 9:
Kwa kushirikiana na wenzako,buni na uigize mazungumzo kuhusu
kazi za ufundi mbalimbali.
Kazi ya 10:
Itembelee zahanati au hospitali moja, kisha zungumzia wafanyakazi
uliowaona hapo.
Kazi ya 11:
“Daktari ni muhimu sana kuliko mwalimu”. Jadili na wenzako kauli hii.
12.6. Kuandika
Kazi ya 12:
Kamilisha sentensi hizi kulingana na ujuzi wako
a. Ili uwe na cheti cha udaktari, unapaswa kuwa na weledi katika
mchepuo wa...............................
b. Baada ya kuhitimu masomo ya................................ mtu huweza
kupatiwa cheti cha urubani
c. Hakimu ni mfanyakazi ambaye alihitimu masomo ya...................
d. Kasisi huwa ameyazingatia masomo ya ........................
e. Keshia huteuliwa baada ya masomo ya.....................................
f. Katibu ni lazima awe na stadi katika elimu ya.........................
Kazi ya 1:Tazama mchoro huu kwa makini na kuzungumzia unachoona.
Daktari Mkuu pamoja na Muuguzi kutoka hospitali moja wilayani Gatsibo
wamepata fursa ya kuwatolea wagonjwa maonyo kuhusu umuhimu wa usafi
katika maeneo ya hospitali na mahali pengine.
Daktari: Hamjambo wote!
Wagonjwa: Hatujambo Daktari!
Daktari: Haya! Kabla ya kuwatolea huduma mbalimbali, ningetaka tuongee
kidogo kuhusu usafi hapa hospitalini.
Nani anayeweza kutuelezea kwa nini usafi hospitalini ni muhimu sana?
Mgonjwa wa 1: Usafi hospitalini ni lazima utiliwe maanani kwa sababu
pasipokuwa na usafi afya ya wagonjwa pamoja na
wafanyakazi wa hospitalini huwa katika hali mbaya sana.
Daktari: Vizuri sana! Nani mwingine ambaye anaweza kutaja mahali ambapo
usafi unastahili kuliko pengine?
Mgonjwa wa 2: Mahali muhimu pakushughulikia mno ni kama vile vyooni,
vyumbani pamoja na nje ya hospitali.
Muuguzi: Asante sana! Je, mnafikiri nini kwa mtu ambaye anakuja
hospitalini bila usafi wa mwili pamoja na mavazi yake?
Mgonjwa wa 3: Kwa ukweli, watu kama hao wapo lakini tabia hiyo ni ya
kuepuka sana.
Daktari: Ndiyo. Lakini ni lazima kujua kwamba usafi hospitalini
huchunguzwa kupitia vifaa vyote vinavyotumiwa, dawa
zinazotunzwa na kupewa wagonjwa, mahali pa kutolea
huduma tofauti bila kusahau usafi wa mwili na nguo kwa
wafanyakazi wa hospitalini.
Muuguzi :Sasa, nani ambaye anaweza kueleza hasara inayotokana
na ukosefu wa usafi kwa ujumla?
Mgonjwa wa 4 : Si hospitalini tu, ukosefu wa usafi mahali popote huweza
kuambukiza magonjwa kadhaa kama vile ugonjwa wa
kipindupindu, kuhara, minyoo, n.k.
Daktari : Asante sana! Basi, nani wa kueleza njia au jinsi magonjwa hayo yanavyosambazwa?
Mgonjwa wa 5 : Kwa mfano, kama vyoo havisafishwi vizuri, nzi huweza
kujitafutia makazi humo. Wadudu hawa wanapogusa
kinyesi cha mgonjwa na kutua kwenye chakula cha watu
wazima vilelevile huwaambukiza ugonjwa wa kipindupindu
au kuhara. Lakini na matumizi ya maji machafu huweza
kuwa chanzo cha magonjwa haya.
Muuguzi: Je, hakuna ugonjwa mwingine unaosababishwa na ukosefu
wa usafi kwenu nyumbani?
Mgonjwa wa 6: Taka zikitupwa mahali pasipofaa, madimbwi pamoja na
vichaka karibu na nyumba huwakaribisha mbu ambao
husababisha ugonjwa wa malaria.
Daktari: Asante sana kwa mchango wenu. Kumbukeni kwamba
usafi ni ufunguo wa afya njema. Inatubidi kuushughulikia
mahali popote kwa ajili ya kuboresha maisha yetu mema.Kazi ya 2:
Maswali ya Ufahamu
Chagua jibu sahihi kuliko mengine
1. Tunatakiwa kuwa na usafi mahali popote kwa sababu
a. usafi ni mzuri
b. usafi wa mwili hulinda magonjwa
c. penye ukosefu wa usafi maisha ya binadamu pamoja na ya
mazingira yake huathirika vibaya.
d. Mbu huweza kujificha katika vichaka na kuambukiza ugonjwa wa
malaria.
2. Ugonjwa wa kipindupindu au kuhara husababishwa na
a. nzi
b. uchafu kutoka kinyesi unaosambazwa na nzi pamoja na matumizi
ya maji machafu
c. chakula kichafu na ambacho hakikuiva vizuri
d. ukosefu wa vyoo safi na vya kutosha.3. Taka zote ni lazima
a. zichomwe
b. zitupwe shambani
c. zitupwe jalalani baada ya kutofautisha zinazooza na zisizooza
d. zihifadhiwe katika mashimo mbali na nyumba.
4. Inastahili kuvaa glovu na bwelasuti wakati wa
a. kula
b. kupiga deki
c. kuingia hospitalini
d. kufanya usafi kwa ajili ya kujikinga na uchafu.
5. Usafi hospitalini ni jukumu la
a. wagonjwa
b. wagonjwa, wafanyakazi wa hospitali pamoja na yeyote anayekwenda hapo
c. wafanyakazi wa hospitalid. hakuna jibu sahihi.
13.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Eleza maana ya maneno yafuatayo:
1. Madimbwi
2. Kupiga deki
3. Huduma
4. Kuambukiza
5. Kipindupindu
6. Kichaka
7. Minyoo8. Bwelasuti
Kazi ya 4:
Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia choo, kuhara, deki,
kutiliwa maanani, taka.
1. .....................ni kifaa chenye majimaji kinachotumiwa kuosha
sakafu ili kuondoa uchafu.
2. Baada ya kujisaidia ni lazima umwage maji
katika........................................................................................
3. Matumizi ya maji machafu yanaweza kuwa chanzo cha
kuambukizwa ugonjwa wa......................................
4. Kila jamii inalazimishwa kuwa na jalala la
kutupia......................................................
5. Usafi ni jambo la...........................mahali popote.
13.3. Sarufi: Matumizi ya kauli ya kutendeshana
Kazi ya 5:
Soma sentensi zifuatazo na kueleza maana ya kitenzi baada ya
kuongezewa viambishi vilivyopigiwa mstari.
1. Martha na Peter wanaelimishana mambo ya kujitegemea.
2. Walikaribishana na kutoa hoja zao.3. Si vuzuri kugombanishana watu.
Maelezo muhimu
Kauli ya Kutendeshana - mtu anakufanya utende jambo fulani, nawe
unamfanya atende jambo hilo hilo.
Kazi ya 6:
Weka vitenzi vifuatavyo katika hali ya kutendeshana
a. Wamepikiana chakula kitamu.
b. Tumefanyana mambo mema ya kuieleza jamii yetu.
c. Wamelimiana shamba la maharage.d. Mmechora michoro inayoeleza wazi usawa wa kijinsia
13.4. Matumizi ya lugha: Msamiati kuhusu aina za magonjwa
Kazi ya 7:
Zungumzia aina mbalimbali za magonjwa yanayoweza kuhatarisha
maisha ya binadamu
Maelezo ya kuzingatia
a. Maana ya ugonjwa
Ugonjwa ni hali au kitu kinachomfanya mtu, mnyama au mmea kuwa katika
afya duni. Pia ugunjwa huitwa maradhi, uele, ukongo. Kuna maradhi chungu
nzima yanayoweza kumwathiri mtu. Mengine yana tiba mengine hayana.
Mengine yanaambukizwa.
Maradhi ya kuambukiza ni yale yanayoenea kutoka kwa mtu mmoja hadi
mwingine.
b. Aina za maradhi
Kuna aina mbalimbali za ugonjwa au maradhi. Ifuatayo ni miongoni mwa mifano.
Saratani/kansa: ugonjwa usio na tiba kwa sasa. Ni ukuaji usio wa kawaida wa seli katika mwili.
Malale: ugonjwa wa usingizi unaoambukizwa na mbung’o.
Homa ya matumbo: taifodi
Kwashakoo/ukosandisha: uele wa watoto unaosababishwa na uhaba wa chakula hususan protini.
Surua/shurua/firangi/ukambi: ugonjwa wa watoto unaofanya ngozi kuwa na vipele. Hatua za kwanza huwa ni homa kali.
Mafua/bombo: maradhi ya kuambukiza yanayosababisha mgonjwa kuumwa na koo na kichwa. Mgonjwa hutokwa na kamasi na kuwa na homa.
Kaputula: uele wa kuhara. Tumbo la kuendesha.
Baridi yabisi: maumivu ya mifupa au viungo yanayosababishwa na baridi
shadidi.
Ukoma: uele wa kuambukiza wa mabatomabato ambao unaharibu mishipa
ya fahamu na kukata viungo vya mwili.
Matumbwitumbwi / machibwichibwi: ugonjwa wa kuvimba mashavu hadi chini ya taya hususan kwa watoto
Kisunzi/kizunguzungu / masua / gumbizi: uele wa kuhisi kichwa kikizunguka.
Kipwepwe: ugonjwa wa ngozi unaosababisha madoa mekundu unaodaiwa kuletwa na chawa.
Ndui: ugonjwa unaosababisha pele nyingi zenye majimaji na usaha.
Kororo: uele wa kuvimba kooni.
Ngiri: ugonjwa wa kukazana kwa mishipa iliyo sehemu za chini ya kitovu.
Zongo: ugonjwa wa kuvimba tumbo kwa watoto wadogo.
Vimbizi: hali ya kutoweza kupata pumzi kutokana na chakula kutosagika tumboni.
Mbalanga / barasi: uele unaobadilisha rangi ya ngozi na kuwa na mabaka au matone.
Rovu: ugonjwa wa kuvimba tezi kwenye shingo.
Tetekuwanga / galagala / tetemaji: ugonjwa wa pele na homa kali wa kuambukizwa13.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 8:
Igiza mazungumzo hapo juu kati ya Daktari na wagonjwa.
Kazi ya 9:
“Usafi ni ufunguo wa afya njema.” Jadili kauli hii.
13.6. Kuandika
Kazi ya 10:
Tunga sentensi nne kwa kutumia vitenzi kama vile kuondoa, safisha,
kunawa, kuambukiza.
SOMO LA 14: ADABU HOSPITALINI
Kazi ya 1:
Eleza adabu inayotakiwa hospitalini na utoe sababu za adabu hiyo.
14.1. Kusoma na ufahamu: Utaratibu hospitalini
Yafuatayo ni mazungumzo mbele ya darasa ya wanafunzi walioitembelea
hospitali ya Girubuzima
Mwalimu: Hamjambo vijana!
Wanafunzi: Hatujambo mwalimu!
Mwalimu: Kuna kundi la wanafunzi waliopewa kazi ya nyumbani kwenda
kuitembelea hospitali moja.
Nawaomba wafike mbele ya darasa na kutusimulia juu ya ziara
yao.
Kiongozi wa kundi: Asante sana mwalimu kwa fursa hii. Kazi
tuliyoshughulikia ilikuwa inahusu mwenendo
hospitalini.
Tuliitembelea hospitali moja inayoitwa Girubuzima.
Ningetaka niwashirikishe wenzangu katika
masimulizi haya.
Mwanafunzi wa kwanza: Tulipoingia katika maeneo ya hospitali, tuliwakuta
watu wamekaa kimya mbele ya ofisi tofauti
kwa ajili ya kutaka kuhudumiwa.
Mwanafunzi wa pili: Kwenye ukuta wa hospitali palikuwa pameandikwa
maonyo au maadili mbalimbali kuhusu utaratibu
unaofaa hospitalini kama ifuatavyo:
Mwanafunzi wa tatu: Hapa ni eneo la Hospitali. Inakatazwa kutenda
yafuatayo:Kuvuta sigara.
Mwanafunzi wa nne: Kuchafua majengo ya hospitali na mazingira yake.
Mwanafunzi wa tano: Kujisaidia pasipofaa.
Mwanafunzi wa sita: Kutema mate hadharani.
Mwanafunzi wa saba: Kupiga kelele.
Mwanafunzi wa nane: Kuharibu vifaa vya hospitalini kama vile kuvunja vioo, viti, mlango, n.k.
Mwanafunzi wa tisa: Kutumia pombe pamoja na dawa za kulevya.
Mwanafunzi wa kumi: Kuonyesha tabia ya ukatili, ugomvi, chuki pamoja
na ubaguzi.
Kiongozi wa kundi: Hii ndiyo miiko ya kupiga marufuku ndani ya hospitali tuliyoorodheshewa.
Mwalimu: Asante sana kwa kazi hii! Darasa, pigieni makofi kundi hili.Maswali ya Ufahamu
Kazi ya 2:
Jibu maswali yafuatayo
1. Habari hii imetokea wapi?
2. Ni mbinu gani ya ufundishaji na ujifunzaji inayozungumziwa?
3. Kwa nini maonyo yale yalitolewa hospitalini?
4. Ni wahusika wangapi wanaojitokeza?5. Unadhani maonyo yale yalitolewa na nani?
14.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:Oanisha msamiati kutoka sehemu A na maana yake katika sehemu B
14.3. Sarufi: Matumizi ya kauli za vitenzi
Kazi ya 4:
Soma sentensi zifuatazo na kueleza maana ya kitenzi baada ya
kuongezewa viambishi
1. Mama na shangazi wamepikiana chakula kitamu sana.
2. Kagina na Amina waliimbiana nyimbo za kuvutia.
3. Mimi na binamu yangu tulitembeleana mwishoni mwa mwaka uliopita.
Maelezo muhimu
Viambishi vilivyopigiwa mstari vinaonyesha kauli ya kutendeana yaani
unafanya kitendo kwa niaba ya mtu, naye anafanya kitendo hicho kwa niaba yako.
14.4. Matumizi ya lugha: Muhtasari kuhusu kauli za vitenzi
Kazi ya 5:
Unganisha kauli za vitenzi vifuatavyo: fanya, lima, piga, cheza, lipa,
penda, omba, dunga katika jedwali moja na kutoa mifano husika kwa
kila kauli.
1. Kauli ya Kutenda: Kitendo katika hali yake ya kawaida (bila
kunyambuliwa)
2. Kauli ya Kutendea: Kufanya kitendo kwa niaba(au kwa ajili) ya
mtu mwingine
3. Kauli ya Kutendana: Unamfanya mtu kitendo, naye anakufanya
vivyo hivyo
4. Kauli ya Kutendeana: Unafanya kitendo kwa niaba ya mtu, naye
anafanya kitendo hicho kwa niaba yako.
5. Kauli ya Kutendwa: Kuathirika moja kwa moja na kitendo
6. Kauli ya Kutendewa : Kitendo kufanywa kwa niaba yako au kwa
ajili yako.
7. Kauli ya Kutendeka: Kitendo kukamilika au kuwa katika hali timilifu
8. Kauli ya Kutendesha : Kumfanya mtu atende jambo fulani
9. Kauli ya Kutendeshana: Mtu anakufanya utende jambo fulani,
nawe unamfanya atende jambo lilo hilo
14.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 6:
Simulia mbele ya darasa muhtasari wa mazungumzo hapo juu baina
ya mwalimu na wanafunzi
Kazi ya 7:
Kwa ushirikiano na wenzako, igiza mazungumzo hayo.
14.6. Kuandika
Kazi ya 8:
Buni mazungumzo mafupimafupi baina ya mwanafunzi na mzazi wake
kuhusu umuhimu wa usafi na uandike maneno yasiyopungua 100.Tathmini ya mada
1. Taja vifaa angalau vinne vya hospitalini na kueleza umuhimu wake
2. Baadhi ya sehemu muhimu za hospitali, chagua tatu na kueleza umuhimu wake.
3. Kamilisha sentensi zifuatazo:
i. Kazi ya muuguzi ni..................................................................
ii. Karani hospitalini hushughulikia...............................................
iii. Tabibu ni mfanyakazi wa hospitalini anaye..................................
iv. Mfanyakazi wa hospitalini anayeshughulikia waliovunjika viungo vya mwili huitwa................
v. Anayetoa huduma kwa wajawazito wakati wa kujifungua huitwa..............................................
4. Jadili hasara zinazoweza kujitokeza kwa sababu ya ukosefu wa usafi.
5. Zungumzia kasoro angalau tano ambazo zinachukuliwa kama mwiko hospitalini.
6. Weka vitenzi vinavyopatikana katika sentensi zifuatazo katika hali ya kutendwa.
a. Tumesafisha vyumba, vyoo pamoja na jikoni kwa ajili ya kujilinda uchafu.
b. Jana wageni walikula chakula kwa wingi.
c. Si vizuri kupiga kelele hospitalini.
d. Tunakunywa maji baada ya kuchemka.
e. Sisi huvaa tai shingoni.