MADA YA 2 MSAMIATI KUHUSU MAZINGIRA YA NYUMBANI
Uwezo mahususi wa mada: Kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na
kuandika matini fupifupi kwa kutumia msamiati unaofaa katika mazingira ya
nyumbani.
Malengo ya ujifunzaji:
• Kutumia msamiati uhusuo mazingira ya nyumbani, mifugo na vifaa vya nyumbani,
• Kuainisha watu wa nyumbani na uhusiano wa familia,
• Kutumia majina ya ngeli ya LI- YA na vivumishi kwa ufasaha.
Kidokezo
1. Taja watu wote wanawopatikana nyumbani kwenu.
2. Taja sehemu kuu za nyumba.
3. Orodhesha vifaa na mifugo wanawopatikana nyumbani.
SOMO LA 5: MAZINGIRA YA NYUMBANI
Kazi ya 1:
Tazama mchoro hapo juu kisha jibu maswali yanayofuata:
a. Unaona nini kwenye picha hii? Eleza.
b. Kuna uhusiano gani kati ya mchoro huo na kichwa cha habari cha
hapa chini?
5.1. Kusoma na ufahamu: Makao ya Gakuba
Mimi na rafiki yangu Rurangwa tunazoea kutembea baada ya masomo ya
jioni. Siku moja tulipata gari na kuelekea kijijini.Tulipofika kijiji ambapo mzee
Gakuba anaishi tuliona nyumba yake na familia yake. Mzee Gakuba, mke
wake na watoto wao wawili walikuwa wanasimama mbele ya nyumba yao
katika bustani.Walikuwa wakizungumza.
Tulipigwa na bumbuazi kwa sababu kabla ya kuenda likizoni hapo palikuwa
na nyumba ya msonge. Mapendekezo ya serikali ya Rwanda ni kuishi katika
nyumba za kisasa. Nyumba hii ina sehemu kuu zifuatazo: sebule,vyumba
vya kulala, chumba cha wageni, chumba cha vyombo, na jikoni. Nyumba hii
inajengwa kwa mchanga, saruji, vyuma, nondo, milango, madirisha, mawe,
matofali na mabati. Vifaa vyote hivi vinapatikana nchini Rwanda. Kwa kujenga
nyumba hii kuna: msingi, kuta, zege, paa, madirisha, milango, sakafu, dari,
bomba na kadhalika. Nyumba hii ina bustani na miti ya aina tofauti kama vile
mti wa machungwa na mti wa maembe. Tulitazama nyumba hiyo kwa makinina kujiuliza mengi kuhusu mabadiliko ya muda mfupi.
Tulichunguza gharama za ujenzi wa nyumba yake! Na kujiuliza Je, gharama
hizi zimetoka wapi? Gakuba na bibi yake, kwa ushirikiano wao walitumia
fedha za mkopo kutoka benki. Gharama za nyumba ni thamani ambayo
unapaswa kuilipa ili uweze kuipata nyumba hiyo unayoitaka! Sasa thamani
unaweza kuilipa kwa njia ya pesa, nguvu ya kazi yako, nguvu ya akili na
pesa. Ina maana kwamba bila kulipa gharama stahiki huwezi kupata thamani
ya nyumba ile unayoitaka. Gharama hizi unaweza kuwalipa watu wengine
wanaokufanyia kazi au wanaokuuzia bidhaa, lakini pia unaweza kuzilipa
wewe mwenyewe kama muda na nguvu zako. Bila kulipa gharama stahiki
huwezi kupata nyumba hiyo.
Mara moja, Rurangwa alianza kuniuliza: “ je, unaona tofauti kati ya nyumba
za jadi na nyumba za kisasa?” Jibu langu lilikuwa hivi: “ kwanza ni vibaya
kwa maisha ya mtu anayeishi katika nyumba za msonge kwa sababu usafi
wa nyumba hizi si kazi rahisi. Nyingi zinajengwa kwa majani. Tena ni hatari
sana kuishi katika nyumba ya msonge: Nyumba hii inaweza kuangukia watu,
inaweza kuungua kwa sababu kunatumiwa majani kwa ujenzi wa nyumba
hii, na kadhalika. Tunahifadhi mazingira wakati tunapojenga nyumba
za kisasa kuliko ujenzi wa nyumba za jadi. Je, Rurangwa, unafahamu
umuhimu wa kuhifadhi mazingira wakati tunapojenga nyumba?” Rurangwa
anatoa jibu: “Hatuwezi kuorodhesha umuhimu wa mazingira kwa sababu
bila mazingira viumbe vyote haviwezi kuishi. Kuna mashirika mengi nchini
Rwanda yanayotetea uhifadhi wa mazingira. Bila mazingira hakuna maisha.
Binadamu na wanyama hupumua hewa nzuri kutoka kwenye mazingira.
Tunapata mvua kwa sababu mazingira yanahifadhiwa na kadhalika.”
Tulipomaliza matembezi yetu, tuliamua kuelezea wazazi wetu umuhimu wa
kuishi katika nyumba nzuri kwa kutumia vifaa ambavyo vinapatikana nchini
mwetu na kutumia fedha kutoka benki kwa njia ya mkopo. Na sisi kama
wanafunzi tutaunda klabu zitakazofundisha watu umuhimu wa kuishi mahalipazuri na kuhifadhi mazingira.
Kazi ya 2 :
Maswali ya ufahamu
1. Taja majina ya watu wote wanaotajwa katika kifungu hiki.
2. Familia ya Gakuba ina watu wangapi? Orodhesha watu hao.
3. Kwa kujenga nyumba yao, walitumia vifaa gani? Kutoka wapi?
4. Nyumba hii ilijengwa na nani? Toa maelezo.
5. Je, Mtu mwenye uwezo mdogo wa kiuchumi anaweza kuishi katika
nyumba ya kisasa? Eleza.
6. Kwa sababu gani tunatakiwa kuheshimu mazingira wakati
tunapojenga nyumba?
7. Kama mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, msaada wako ni upi
kwa kuhifadhi mazingira unamoishi?5.2. Matumizi ya msamiati
Kazi ya 3:
Tumia maneno yafuatayo katika sentensi zako ukizingatia namna
yalivyotumiwa katika kifungu cha habari ulichosoma
1. Busitani
2. Bumbuazi
3. Mkopo
4. Kuhifadhi
5. Shirika
6. Kupumua
7. Kutetea
8. KlabuKazi ya 4:
Oanisha maneno yaliyomo katika sehemu A na yale yaliyomo katikasehemu B.
5.3. Sarufi: Matumizi ya ngeli ya LI-YA.
Kazi ya 5:
Chunguza sentensi zifuatazo na kuandika viambishi nafsi
vinavyopatikana katika vitenzi
1. Kundi la wanamuziki liliwatumbuiza watu jana.
2. Mashirika haya yaliundwa na vijana mbalimbali.
3. Koti hilo limeshonwa na mshonaji hodari.
4. Makabati yalitengenezwa na maseremala.5. Gari zuri lile lilitengenezwa nchini Rwanda
Maelezo muhimu
• Vitenzi vilivyomo katika sentensi hapo juu, vinatumia viambishi nafsi LI-YA
• Matumizi ya viambishi hivi LI-YA yanategemea nomino zilizotumiwa katika sentensi hizo.
• Nomino hizo zikiwa katika umoja kitenzi huchukua LI; zikiwa katika wingi kitenzi huchukua YA.
• Nomino zilizopendekezwa katika umoja huchukua wingi wake kwa kuongeza ma- kwa jina hilo:
Mfano:
1. Kundi makundi
2. Shirika mashirika
3. Jani majani
4. Gari magari
5. Darasa madarasa
Tanbihi: Kuna majina ya ngeli hii yasiyokuwa na umoja.
Maji, mate, maziwa (ya kunywewa), mateso, mavi, manukato, mazishi,
matumizi, manufaa, masafa. Katika sentensi, majina ya ngeli hii hufuatwana kitenzi chenye kiambishi awali li- katika umoja na ya- katika wingi
Mfano:
Umoja Wingi
1. Shirika liliundwa. Mashirika yaliundwa.
2. Koti lingesafishwa. Makoti yangesafishwa.
3. Chungwa liliangushwa. Machungwa yaliangushwa.
5.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 6:
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia nomino hizi katika umuja na
wingi kisha ueleze kile ulichokigundua
Umoja Wingi
1. Kabati ..........................................................
2. Koti ..............................................................
3. Bega ............................................................
4. Goti .............................................................
5. Panga .........................................................
6. Janga ..........................................................
7. Jangwa .......................................................
8. Jina .............................................................
9. Jibu .............................................................10. Jembe…………………………………………
Kazi ya 7:
Andika sentensi zifuatazo katika umoja au wingi.
1. Mimi nina lengo la kupambana na jangwa.
2. Wewe utaondoa jani kavu hilo.
3. Majani yalikauka.
4. Shavu linaniuma.
5. Kijana mrefu alibeba kasha kwenye bega.
6. Debe hilo linavuja kwa sababu limetoboka.
7. Watoto watano walilazwa hospitalini kwa sababu ya matatizo ya mapafu.
8. Madaftari yanapaswa kuhifadhiwa vizuri.
9. Tarumbeta lilitumiwa wakati wa burudani.10. Shirika la reli liliagiza garimoshi kubwa.
5.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 8:
Simulia mbele ya darasa muhtasari wa kifungu “ Makao ya Gakuba.”
5.6. Kuandika
Kazi ya 9:
Tunga kifungu cha mistari 12 kuhusu ujenzi wa nyumba ya wazazi
wako.
SOMO LA 6: MSAMIATI KUHUSU WATU WANAOPATIKANA
NYUMBANI
Kazi ya 1:
Chunguza michoro hii kisha ujadili unachoona kwenye michoro hii.
6.1. Kusoma na ufahamu: Watu wa nyumbani
Familia ni jamaa ya watu wanaoishi pamoja yenye baba , mama na watoto.
Katika utamaduni wetu kama Wanyarwanda, watu hawa wana majukumu
tofauti katika familia.
Baba pamoja na mama wana majukumu ya kutafuta maendeleo ya familia
yao. Baba kwa ushirikiano na mama wana wajibu wa kufanya juu chini ili
familia yao iweze kupiga hatua kimaendeleo na kujitegemea kikamilifu.
Kulinda usalama wa nyumbani ni mojawapo wa wajibu huo. Hapa mama na
baba ndio walinzi wa kwanza wa utaratibu nyumbani ili familia yao iwe na
amani kila wakati.
Kuwalea watoto wao, wazazi wana majukumu makubwa sana kwa watoto
wao kama vile: kuwapenda, kuheshimu haki zote za mtoto na kukidhi mahitaji
yao yote kama vile kuwalisha, kuwasomesha, kuwalipia karo za shule na
kuwapeleka hospitalini wakati wanapoumwa, n.k.
Wazazi huwapa mawaidha mema na kuwafundisha mila na desturi za
Wanyarwanda kama vile: uzalendo, ushirikiano, kuheshimiana, n.k. Wazazi
pia huwasihi kuepukana na tabia za: ukatili, uongo, uovu, ulevi, uzembe,
kupiga marufuku itikadi ya mauaji ya kimbari, na mienendo yote isiyofaa.
Kwa upande wa watoto, nao wana majukumu ya kuwaheshimu wazazi wao,
kutimiza mipango ya wazazi kama ilivyopendekezwa na kutoa mchango
mwafaka wa maendeleo ya familia yao.
Nyumbani, wageni wa aina yote hukaribishwa. Miongoni mwa wageni hao
ni kama babu, bibi, mjomba, shangazi, mpwa na shemeji. Wageni hawa
wanalakiwa vizuri.Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Kwa maoni yako, eleza maana ya familia.
2. Kwa kawaida familia hujengwa namna gani?
3. Katika utamaduni wetu kama Wanyarwanda, baba na mama
wanashirikiana vipi?
4. Je, mchango wa watoto ni upi katika familia?5. Eleza mila na desturi ambazo wazazi wanafundisha watoto wao.
6.2. Msamiati kuhusu watu wa nyumbani
Kazi ya 3:
Baada ya kusoma kifungu cha habari, toa maana ya msamiati
unaofuata, kisha utunge sentensi zenye maana kamili kwa kutumia
msamiati huo.
1. Majukumu
2. Ushirikiano
3. Usalama
4. Uzalendo5. Mienendo
Kazi ya 4:Oanisha maneno kutoka sehemu A na maana yake katika B
6.3. Sarufi: Matumizi ya vivumishi vya idadi katika ngeli ya
LI-YA
Kazi ya 5:
Chunguza sentensi zifuatazo, kisha ueleze muundo wa vivumishi
vilivyotumiwa
1. Jibu moja limepatikana.
2. Mawe sita yameanguka chini.
3. Matunda saba yameiva.
4. Madarasa tisa yanasafishwa.
5. Makoti kumi yatashonwa.
Maelezo muhimu
Katika matumizi ya ngeli ya li-ya na vivumishi vya idadi, idadi mbili ambayo
hugeuka -wili, tatu, nne, tano pamoja na nane huchukua kiambishi makatika wingi. Vivumishi hivyo huwa mawili, matatu, manne, matano na
manane.
Kinyume na matumizi ya ngeli ya li-ya na vivumishi vya idadi tulivyoona
hapo juu, idadi, sita, saba, tisa na kumi havichukui kiambishi ma- katika
wingi. Vivumishi hivyo hubaki vile vilivyo yaani, sita, saba, tisa, na kumi.
Nomino za ngeli ya “li-ya” huweza kutumiwa na vivumishi vya idadi ya jumla
/isiyo kamili / isiyo dhahiri:
Kwa mfano:
Matendo mengi mazuri yamefanywa na watu hawa.Kazi ya 6:
Andika sentensi zifuatazo kwa kutumia vivumishi vilivyomo ndani
ya mabano.
1. Mawe .................... yamewekwa kando ya barabara (tatu).
2. Madirisha ........................... yamefunguliwa (tano).
3. Meno ...................... yameng’oka (mbili).
4. Matunda ....................... yameiva (nane).
5. Makundi ................................. ya wanafunzi yameshiriki vilivyo (nne).
6. Madarasa .............................. yamejengwa (tatu).
7. Taja mambo .............. yanayozingatiwa katika kazi ya fasihi (tatu).8. Makoti ...................... yameuzwa na mfanyabiashara huyu (tano).
Kazi ya 7:
Chunguza vivumishi vya idadi isiyo dhahiri vya ngeli ya “li-ya”
vifuatavyo kisha utunge sentensi zenye vivumshi hivyo.
1. Machache
2. Mengi
3. Kadhaa
4. Tele5. Kidogo
6.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 8:
Kamilisha tungo zifuatazo kwa kutumia vivumishi vya idadi: toka
moja hadi arubaini (Andika kwa maneno)
1. Kanuni za Mungu ni ........................
2. Mwaka una miezi .............................
3. Ni rahisi kujua kwamba wiki moja ina siku .....................
4. Watu wa zamani walipika kwa kuweka chungu juu ya mafiga
...........................
5. Wanyarwanda huwapa majina watoto wao kwenye siku ya ..........
.........................
6. Nchi ya Rwanda ina majimbo/ mikoa................. na mji wa Kigali.
7. Nchi yetu inapakana na nchi........................
8. Dunia ina mabara............................
9. Rwanda ina milima ya volkano..................
10. Katika mchezo wa soka, timu moja huwa na wachezaji...................
uwanjani.
11. Siku moja ina saa...........................6.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 9:
Soma kifungu cha habari hapo juu “watu wa nyumbani” baadaye
utoe muhtasari kimazungumzo.
Kazi ya 10:
Kwa njia ya mazungumzo, zungumzia wanafunzi wenzako ushirikiano
uliopo baina ya watu wa familia yenu.
6.6. Kuandika
Kazi ya 11:
Buni, kwa kuandika, mazungumzo ya watu nyumbani wakishirikiana
katika kazi fulani unayoitaka.
SOMO LA 7: UHUSIANO WA KIFAMILIA
Kazi ya 1:
Tazama mchoro huu. Unaona nini kwenye mchoro huu?
Bi. Nyiranzage aliolewa na Bw. Rutebuka. Sasa, Bi Nyiranzage
anaitwa bibi Rutebuka. Wengine humwita Bi. Nyiranzage. Bwana
Rutebuka ni mume wa bibi Nyiranzage. Bibi Nyiranzage na
bwana Rutebuka, ni mke na mume. Bwana na bibi Rutebuka
walizaa watoto wawili tu. Kifunguamimba wao ni mwanamume.
Jina lake ni Matabaro. Mtoto wa pili ni mwanamke. Yeye anaitwa
Nyiratabaro. Kwa upande mwingine Rutabagisha ambaye ni jirani
yao amemuoa Nyiramavugo; hivyo wote huitana mume na mke.
Bw. Rutabagisha na Nyiramavugo nao walizaa watoto wawili
tu, mmoja wa kike anayeitwa Mukabutera ndiye aliyetangulia
kuzaliwa na mwingine wa kiume Butera alifuata baadaye. Wototo
wa familia hizi mbili husomea kwenye Chuo cha Ualimu cha
Gacuba II.
Watoto wote ni wanafunzi wa shule za sekondari. Vifunguamimba
husoma katika mwaka wa tatu katika chuo cha Ualimu cha Gacuba II.
Ilhali vifungamimba husoma katika mwaka wa pili.
Baada ya muda mfupi, majirani hawa walikata shauri ya
kushirikiana kimasomo. Vifunguamimba walitangulia kushirikiana
na kusaidiana kati yao na hata kuwasaidia wadogo wao kimasomo
na kuwahimiza kuwaiga. Walikuwa wakishika nafasi ya kwanza
kwa kila muhula wa masomo. Baada ya kuona matunda ya
kushirikiana kimasomo, wote waliamua kuwasaidia wanafunzi
wenzao waliokuwa wakishindwa shuleni wakifanya marudio nao.
Jambo hili lilishamiri sana na kujulikana shuleni kote. Ilitokea
Mkurugenzi wa shule akapata habari hii na kuwakabidhi zawadi
ya kusoma mwaka mzima bila kulipa ada ya shule.
Jambo hili liliwafurahisha wazazi na kuwapongeza watoto wao
kwa zawadi nono. Shuleni, walimu wote walikuwa wanatumia
mfano wao ili kuwahimiza wanafunzi wengine kuwaiga.
Mwishowe, wanafunzi hawa walimaliza masomo yao na kuachia
shule yao makumbusho ya milele. Walianza maisha mapya
wakawa walimu mashuhuri. Baada ya miaka miwili, Matabaro na
Mukabutera walifunga ndoa na kuzaa mtoto anayeitwa Rubangura.
Punde si punde, Butera na Nyiratabaro walioana wakazaa mtoto
anayeitwa Rubaduka. Familia hizi ziliendelea kuishi pamoja na
kushirikiana katika shughuli zote za nyumbani.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu:
1. Taja uhusiano uliopo baina ya Butera na Mukabutera.
2. Bi. Nyiramavugo atamwitaje Mukabutera?
3. Bw. Rutebuka atamwitaje Matabaro?
4. Jaza mapengo kwa neno faafu:
a. Bw. Rutebuka ni …………… wa Bi. Nyiranzage.
b. Mukagatera ni ………….. yake Butera.
c. Rutebuka ni ………….. yao Matabaro na Nyiratabaro.5. Nyiramavugo atamwitaje mke wa Butera?
Kazi ya 3:
Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia msamiati wa uhusiano wa
kifamilia unaofaa.
1. Mama ya mama yangu anaitwa……………………….
2. Ndugu wa kike wa baba yangu anaitwa ……………….
3. Baba ya mume wangu anaitwa …………………………
4. Mtoto wa mtoto wangu anaitwa…………………………
5. Baba ya baba yangu anaitwa ……………………………..
6. Mtoto wa mjukuu wako anaitwa ………………………….
7. Mama ya mke wako anaitwa ……………………………..
8. Mwanamke aliyeolewa na babako, na ambaye si mama yako wa
damu anaitwa …………………………………………………….
9. Mtoto wa kwanza kuzaliwa anaitwa …………………………….
10. Mtoto wa mwisho kuzaliwa anaitwa…………………………
Maelezo muhimu kuhusu uhusiano wa kifamilia
• Mjomba: Mvulana aliyezaliwa na dada yako au kaka ya mama yako.
• Shangazi: Msichana aliyezaliwa pamoja na baba yako au ndugu wa kike wa baba yako.• Mpwa: Mtoto wa dada yako.
• Binamu: Mtoto wa mjomba wako au wa shangazi yako.
• Shemeji: Ni ndugu zote wa mkeo au ndugu za kiume wa mumeo.
• Wifi: Jina wanaloitana dada zako na mkeo.
• Mkaza mjomba: Mke wa mjomba wako.
• Mkaza mwana: Mke wa mtoto wako.
• Mavyaa: Jina linalotumiwa katika kuitana baina ya mke na mama mkwe wake.
• Kifunguamimba: Mtoto wa kwanza kuzaliwa.
• Kitindamimba:Mtoto wa mwisho kuzaliwa.
• Mapacha: Watoto wawili waliozaliwa siku moja kutokana na mimba moja.
• Baba wa kambo: Mwanaume aliyeoa mamako na ambaye si baba yako wa damu.
• Mama wa kambo: Mwanamke aliyeolewa na babako, na ambaye si mama yako wa damu.
• Kitukuu: Mtoto wa mjukuu.
• Kilembwe: Mtoto wa kitukuu.
• Kilembwekeza/Kinying’inya: Mtoto wa kilembwe.
• Kitojo: Mtoto wa kilembwekeza.
7.2. Msamiati kuhusu uhusiano wa kifamilia
Kazi ya 4:
Eleza maneno yalopigiwa mistari katika sentensi hizi:
1. Watoto wanaheshimu wazazi wao.
2. Tunampokea nyanya yetu nyumbani.
3. Kifunguamimba kutoka familia ya mjomba wetu anahifadhi mazingira.
4. Baba wa kambo wa Juma anamsadia mtoto mwenzake mwenye matatizo ya kutembea.
5. Binamu yenu anaunda shirika la kutetea watoto wenye matatizo.7.3. Sarufi: Matumizi ya vivumishi vya kuuliza katika ngeli ya LI-YA
Kazi ya 5:
Chunguza sentensi zifuatazo kisha ueleze muundo wa vivumishi
vilivyotumiwa.
1. Jengo lipi ni kubwa?
2. Mapapai yapi yameiva?
3. Tukupe magunia mangapi?
4. Mashirika gani yanasaidia wakulima?
5. Wewe unataka nikupe jembe lipi?
Maelezo muhimu kuhusu vivumishi viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali kuhusu nomino. Vivumishi hivi
vinapotumiwa katika sentensi ni sharti sentensi hiyo ikamilishwe kwa alama
ya kiulizi. Vivumishi viulizi ni vitatui?, -ngapi? na -gani? Vivumishi viulizi
-ngapi? na -pi? huchukua viambishi vya ngeli lakini kiulizi “gani” hakichukui
kiambishi chochote cha ngeli.
Kwa mfano:
1. Gari lipi linatembea?
2. Magari yapi yanatembea?
3. Je, nyumba yako ina madirisha mangapi?
4. Unapenda shirika gani? –
5. Unapenda mashirika gani?
Kazi ya 6:
Tumia vivumishi viulizi vilivyomo mabanoni ili kujaza sentensi
zifuatazo:
1. Jibu .............. limeishapatikana? (-pi)
2. Mawe ................. yamewekwa kando ya barabara? (-ngapi)
3. Madirisha .............. yamefunguliwa? (gani)
4. Meno ................ yameng’oka? (-pi)
5. Tunda ................ limeiva? (gani)Kazi ya 7:
Andika sentensi zifuatazo katika umoja ama wingi.
1. Jengo lipi ni kubwa?
2. Mapapai yapi yameiva?
3. Tukupe magunia yapi?
4. Mashirika gani yanasaidia wakulima?
5. Wewe unataka nikupe jembe lipi?
7.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 8:
Soma maelezo hapo juu kuhusu uhusiano wa kifamilia kisha umwambie
mwenzako hali halisi ya kila mtu katika familia yako binafsi.
7.5. Kusikiliza na Kuzungumza
Kazi ya 9:
Baada ya kusoma maelezo kuhusu uhusiano wa kifamilia, zungumzia
darasa ukoo wako.
7.6. Kuandika
Kazi ya 10:
Tunga mazungumzo kuhusu
“ uhusiano wa kifamilia” ( angalau misitari 15)SOMO LA 8: VIFAA VYA NYUMBANI NA USAFI WAKE
Kazi ya 1:
Orodhesha vifaa mnavyotumia nyumbani kwenu mnapofanya usafi.
8.1. Kusoma na ufahamu: Vifaa vya nyumbani na usafi wake
Usafi wa nyumbani na vifaa vyake ni njia ya kuendeleza afya kwa kuzuia
maradhi yanayotokana na athari za taka kwa binadamu. Athari hizo zinaweza
kuhusu miili yetu.
Usafi wa nyumbani ni jambo ambalo linafaa kutiliwa maanani na kila mtu,
kwani uchafu unachangia pakubwa kuharibu maisha ya binadamu. Jambo
la kushangaza ni kwamba watu wengi wanafikiri kuwa usafi unahusu miili na
mavazi tu, wakisahau kuwa usafi huhusu kila kitu kinachopatikana katika
mazingira wanamoishi.
Tunapozungumzia usafi wa nyumbani, watu wengi huelewa shughuli
muhimu zinazostahili kufanywa katika kusafisha vyumba vya nyumbani na
kutengeneza bustani zinazozunguka nyumba hiyo. Lakini, ni lazima kujua
kwamba usafi huchunguzwa kupitia vifaa vya nyumbani vinavyotumiwa
kama vile: sahani, vikombe, vijiko, sufuria,vijiko, nguo, meza, kabati,
runinga, redio,na kadhalika. Tena inafaa kusafisha sehemu zote za nyumba
kama vile vyumba vya kula, sebule, jikoni, chooni, bila ya kusahau bustani.
Kabla ya kufanya usafi wa vifaa na sehemu za nyumba, sisi wenyewe
tunaombwa kuwa na usafi ipasavyo. Kama vile: Kunawa mikono kwa maji
na sabuni hupunguza kwa kiasi kikubwa maambukizo ya ugonjwa wa
kuhara. Wazazi na walezi wengine wanapaswa kunawa mikono kwa sabuni
kila baada ya kumhudumia mtoto mchanga au mtoto mdogo aliyejisaidia,
kumpeleka mtoto msalani, kutoka msalani wao wenyewe, kabla ya kuandaa
chakula, kabla ya kulisha watoto wadogo na baada ya kuondoa takataka.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kuwajengea watoto tabia ya kunawa
mikono kwa maji safi na sabuni kabla ya chakula na baada ya kutoka
msalani. Kinyesi cha wanyama na binadamu kisiruhusiwe kukaa ndani ya
nyumba, njiani, kwenye vyanzo vya maji na katika maeneo ya kuchezea
watoto. Matumizi ya vyoo pamoja na tabia ya usafi, hasa unawaji wa mikono
kwa sabuni ni mambo muhimu kwa afya ya jamii. Hutoa kinga kwa watoto
na kwa kaya kwa gharama nafuu pamoja na kuwapatia watoto haki yao ya
kuwa na afya njema na lishe bora.
Tunaposafisha nyumba tunatumia maji, sabuni za kawaida, na sabuni za
majimaji au dawa za kuulia wadudu wenye kuambukiza watu magonjwa
mbalimbali.Tunawaonya watu wasitupe uchafu ovyoovyo. Taka ambazo
zinaweza kusababisha matatizo ya afya ni kinyesi cha binadamu na cha
wanyama, taka ngumu, maji machafu, taka za viwandani, na za kilimo, n.k.
Taka zote zinazotokana na vitu vyote vilivyotumiwa zinafaa kutupwa mahali
panapofaa kama vile jalalani au zikachomwa kupitia njia zinazokubaliwa.
Nyasi nazo zinazozunguka nyumba zetu zinafaa kufyekwa ili kuwafukuza
mbu wanaosambaza ugonjwa wa malaria.
Maji yote ya kunywa na ya matumizi mengine yatoke kwenye vyanzo salama
na yachemshwe baadaye au yanyunyiziwe dawa ya kuulia vijidudu. Vyombo
vya kuwekea na kuhifadhia maji vitunzwe vizuri ndani na nje na kufunikwa ili
kuepukana na uchafu wa maji. Ni lazima iwepo mikakati rahisi ya kusafisha
maji yawe safi nyumbani kama vile kuyachemsha, kunyunyizia dawa ya maji
(klorini) ili kuua vijidudu. Vyakula vibichi au mabaki ya vyakula vilivyopikwa
yanaweza kuwa hatari. Vyakula vibichi visafishwe kwa maji safi kabla ya
kupikwa. Chakula kilichopikwa kiliwe kikiwa moto na kiporo kipashwe moto
vizuri kabla ya kuliwa. Chakula, vyombo na eneo la kutayarishia chakula
halina budi kuwa safi na mbali na wanyama.
Chakula kihifadhiwe kwenye vyombo vilivyofunikwa.
Upungufu wa usafi wa mazingira ni sababu kuu ya maradhi kote duniani.
Uboreshaji wa mazingira una manufaa makubwa kwa afya ya watu katika
kaya na katika jamii.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Ni sehemu zipi za nyumba ambazo huhitaji usafi?
2. Taja vifaa vya nyumbani vilivyotajwa katika kifungu hiki.
3. Kwa sababu gani watoto wanapaswa kuepukana na uchafu?
4. Tunatumia nini katika kufanya usafi wa nyumbani?
5. Wazazi au walezi wengine wanafundisha watoto wao nini kuhusu
usafi?
6. Ni umuhimu gani wa kuwa na maji safi?
7. Ni dosari zipi za upungufu wa usafi kwa binadamu?
8.2. Msamiati
Kazi ya 3:
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo:
1. Athari
2. Maanani
3. Kuhara
4. Kinga
5. Takataka
6. Kaya
Kazi ya 4:
Baada ya kusoma kifungu cha habari hapo juu, kamilisha sentensi
zifuatazo kwa kutumia maneno yafuatayo: runinga, redio, kijiko,
sufuria, meza, malaria, usafi, tabia, sabuni, linafaa, vifaa.
1. Mama anapika chakula ndani ya……………….
2. Tunaposoma kiswahili nyumbani tunaandikia kwenye………..
3. Nyanya yangu anatumia………….. wakati mimi ninatumia uma.
4. Tunasikiliza habari za mpira kwenye………………
5. Wanafunzi hupenda kutazama filamu kwenye…………
6. Usafi nyumbani ni jambo ambalo ………..kutiliwa maanani.
7. Watu wengi wanafikiri kuwa ……..unahusu miili na mavazi tu.
8. Usafi nyumbani huonekana kupitia ………. vinavyotumiwa nyumbani.
9. Kunawa mikono kwa maji na …………hupunguza kwa kiasi kikubwa
magonjwa.
10. Wazazi na walezi wengine wanapaswa kuwazoeza watoto ……….
ya kunawa mikono kwa maji safi.
11. Nyasi nazo zinazozunguka nyumba zetu zinafaa kukatwa ilikuwafukuza mbu wanaosababisha ugonjwa wa…………..
8.3. Sarufi: Nomino za ngeli ya LI-YA na vivumishi vya
kumiliki
Kazi ya 5:
Chunguza mifano ya sentensi hapa chini, kisha ueleze aina za
maneno yaliyopigiwa mstari.
1. Koti langu limechafuka.
2. Shirika lako linajulikana sana.
3. Gari lake ni la kifahari.
4. Jumba letu linapendeza
Maelezo muhimu kuhusu matumizi ya nomino za ngeli ya LI-Ya na
vivumishi vya kumiliki
Vivumishi vya kumiliki ni -angu, -ako, -ake, -etu, -enu na -ao. Vivumishi
hivi katika ngeli ya Li-Ya huchukua kiambishi konsonanti l- katika umoja na
y- katika wingi.
Kazi ya 6:
Andika wingi wa sentensi za hapa chini.
Umoja Wingi
1. Jembe langu limepotea. -------------------------------------------
2. Janga kubwa limesababisha maafa. ----------------------------------
3. Jaribio la leo limesahihishwa. -------------------------------------------
4. Jeshi lao lina askari wengi. -------------------------------------------
5. Jeraha lake lina uchafu sana. -------------------------------------------
6. Jambo hili liliwafurahisha wengi. ----------------------------------------
7. Jicho lake linaona mbali sana. ------------------------------------------
8. Jiwe langu lina thamani kubwa. -----------------------------------------
9. Jino lako limeng’oka? -------------------------------------------
10. Jiko langu limeharibika. -------------------------------------------
8.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 7:
Katika makundi ya wanafunzi wawili wawili jadilini kuhusu “Umuhimu
wa usafi na madhara ya kutokuwa na usafi.”
Kazi ya 8:
Eleza umuhimu wa vifaa hivi vya usafi:
1. Bafu
2. Sabuni
3. Deki
4. Ufagio
5. Taulo
8.5. Kusikiliza na Kuzungumza
Kazi ya 9:
Mwambie mwenzako namna mnavyofanya usafi nyumbani kwenu
na usafi wa vifaa vya nyumbani.
8.6. Kuandika
Kazi ya 10:
Tunga kifungu cha habari kwa kutumia kichwa kifuatacho (maneno
yasiyopungua mia moja): “Uchafu ni asili ya maradhi mengi.”SOMO LA 9: MSAMIATI KUHUSU MIFUGO
Kazi ya 1:
Jiunge na mwanafunzi mwenzako. Kumbushaneni majina ya mifugombalimbali mnayoyajua.
9.1. Kusoma na ufahamu: Kazi nzuri ya ufugaji.
Huyu ni Ikirezi. Ikirezi ni mfugaji wa nyuki. Ikirezi anarina asali. Baada ya
kurina, yeye husafisha asali yake na kuiuza. Asali hiyo hutumiwa kamachakula au hutengenezewa dawa.
Huyu ni Ituze. Ituze anakama ng’ombe. Kabla ya kukama, aliosha chuchu
kwa maji vuguvugu na kuzikausha kwa kitambaa safi. Anatumia mkebe safikuwekea maziwa. Ituze huwapandisha madume kwa mitamba au mpira.
Hili ni josho. Ng’ombe hawa wanaogeshwa kwa dawa ndani ya josho.
Wafugaji huosha mifugo katika josho ili kuwakinga dhidi ya kupe. Dawahuua viroboto wanaoishi kwenye ngozi za mifugo.
Hawa ni Mudenge na Gatera. Mudenge anawalisha kuku kwa mahindi. Pia,
huwapa kuku mtama, ugali, wadudu na vyakula vinavyopatikana kwa urahisi.
Wakati mwingine, yeye huwapa kuku chakula maalumu kilichotengenezewa
katika viwanda. Mudenge anawafuga kuku wa mayai na wa nyama. Yeye
huuza baadhi ya mayai ili kujipatia riziki. Mudenge, pia, huwaatamisha
baadhi ya kuku wake ili apate vifaranga wa kuuza na kufuga.
Gatera, naye, anawalisha ng’ombe kwa nyasi. Gatera anawafuga ng’ombe
wake ndani kwa ndani. Anawapa lishe, maji na dawa humo humo zizini.
Gatera hukata pembe za ng’ombe wake. Ng’ombe hukatwa pembe ilikumzuia kumdhuru mtu au kuharibu vitu.
Huyu ni Kaliza. Kaliza anapenda kuchunga farasi. Anawachunga farasi
penye maji safi na nyasi nyingi. Kulisha mifugo ni shughuli muhimu ya
ufugaji. Mifugo wanapolishwa vizuri hukua kwa haraka, huwa na afya nzurina hutupatia mapato mazuri.
Kaliza anafagia zizi la ng’ombe. Mfugaji bora husafisha makao ya mifugo na
vyombo vyao vya kulia, kunywea na kulalia. Mifugo wanaolala katika mahalisafi na kulia katika vyombo safi huwa na afya njema.
Daktari wa mifugo anamtibu kuku kwa kumdunga sindano. Kutibu mifugo
ni muhimu kwa mfugaji. Ni vizuri kutambua dalili ya ugonjwa ili watibiwe
mapema.
Kazi ya 2:
Maswali ya ufahamu
1. Andika majina yote ya mifugo yaliyotajwa hapo juu.
2. Asali ina umuhimu gani kwa maisha ya binadamu?
3. Kwa sababu gani tunakata sufu ya kondoo?
4. Kabla ya kukama ng’ombe, tunaombwa kufanya nini kwanza?
5. Chagua mifugo watano katika vifungu vya habari hapo juu kisha
utaje umuhimu wao kwa binadamu.
6. Kwa maoni yako, ufugaji unaleta matunda gani kwa maendeleo
ya nchi?
9.2. Msamiati kuhusu mifugo
Kazi ya 3:
Baada ya kusoma kifungu cha habari hiki, toa maana ya msamiati
unaofuata:
• kurina
• kukata sufu
• kukama
• kupandisha madume kwa mtamba
• kufuga ng’ombe ndani kwa ndani
• kuwapeleka ng’ombe katika josho
• kuatamisha kuku
• kuchunga• kukata pembe
9.3. Sarufi: Ngeli ya LI –YA na Vivumishi vya kuonyesha.
Kazi ya 5:Tazama sentensi zifuatazo na kujadili mabadiliko ya kisarufi yanayojitokeza.
Maelezo muhimu
Vivumshi vya kuonyesha hili, hilo, lile hufuata nomino katika umoja.Vivumishi vya kuonyesha haya, hayo, yale hufuata nomino katika wingi.
Kazi ya 6:
Chagua neno sahihi katika mabano na kujaza pengo.
1. Debe ………….. lilitoboka (hii, haya, hili, hiyi).
2. Jambazi ……….liliadhibiwa (yule, hii, lile, hiyo).
3. Tafadhali kunja majamvi………..(ayo, hizo, hayo, halo).
4. Anakuomba umnunulie machungwa ………….(hizo, hayo, yayo).
5. Jahazi …….ni kubwa (lili, hile, jile, lile).
Kazi ya 7:
Sahihisha sentensi zifuatazo:
1. Kabati kale kalivunjwa na wezi.
2. Maji haya alimwagwa ovyo sakafuni.
3. Alipotaka kujenga nyumba alitafuta majiwe makubwa.
4. Mafuta haya haamwagwi ziwani kwa sababu anaweza kuua samaki.5. Maboga haya yana manufaa nyingi kwa mwili wako.
9.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 8:
Husisha majina haya na mifugo wanaopatikana hapo chini: mbuzi,mbwa, kuku, paka, na sungura.
9.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
Kazi ya 9:
Zungumzia wanafunzi jinsi mnavyofanya ufugaji wengine namna
gani nyumbani kwenu au kwa babu yako mnavyofanya ufugaji.
9.6. Kuandika
Kazi ya 10:
Tunga kifungu kifupi cha maneno yasiyozidi 100 kuhusu “Umuhimu
wa ufugaji nchini Rwanda.”
Tathmini ya mada
1. Tumia maneno yafuatayo ya ngeli ya LI-YA na vivumishi vya
kumiliki au vya kuonyesha katika sentensi sahihi katika
umoja.
a. Azimio
b. Ini
c. Jiko
d. Ua
e. Shamba
2. Tumia sentensi za hapo juu katika wingi.
3. Jaza sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno: baba, wifi,
mama, shangazi, mjomba, mjukuu, binamu, mpwa, mapacha,
baba wa kambo.
a. Mke wa baba yako ni ……………………………….. yako.
b. Mume wa mama yako utamuita……………………… yako.
c. Mtoto wa mjomba au shangazi yako ni……………..
d. Mtoto wa mtoto wako utamuita…………..
e. Bwana ya mama yako ambaye si baba yako utamuita……..
f. Dada ya baba yako utamuita……………………………….
g. Kaka ya mama yako utamuita………………………………..
h. Mke wa ndugu yako utamuita…………………………….
i. Watoto wawili waliozaliwa siku moja na mama mmoja
tutawaita……..
j. Mtoto wa dada yako utamuita……….4. Andika umuhimu wa vifaa vya nyumbani vifuatavyo:
5. Tunga insha ndogo ya maneno yasiyozidi 100 kuhusu “Umuhimuwa kuishi katika nyumba ya kisiasa kwa maisha ya binadamu”