• MADA YA 1 MATUMIZI YA KISWAHILI SHULENI

    Uwezo mahususi wa mada: Kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na kuandika matini fupifupi kwa kusisitizia msamiati maalum unaotumiwa katika 
    mazingira ya shuleni.

    Malengo ya ujifunzaji:

    • Kutumia kwa ufasaha msamiati unaotumiwa katika mazingira ya shule;
    • Kueleza kuhusu wafanyakazi wanaopatikana shuleni;
    • Kueleza kuhusu msamiati unaohusiana na shughuli zifanyikazo shuleni; 
    • Kutunga sentensi kwa kuzingatia matumizi ya umoja na wingi wa 

    majina ya ngeli ya LI-YA.

    Kidokezo

    cc

    Tazama mchoro huu na kueleza kinachofanyika hapa juu.

    SOMO LA 1: TARATIBU ZA SHULENI

    1.1. Kusoma na ufahamu: Shule ya Icyerekezo

    Soma kifungu cha habari hapa chini kisha ujibu maswali yanayofuata
    Shule yetu inaitwa Shule ya Sekondari ya Icyerekezo.

    Shule hii inapatikana 

    katika wilaya ya Kicukiro makao yake makuu yapo mjini Kigali. Shule hii 
    ya Ikerekezo ina walimu ishirini na madarasa kumi na mawili pamoja na 
    wafanyakazi wengine kumi ambao siyo walimu.

    Inapokuwa kipindi cha muhula kuanza, jumuiya nzima ya shule huchukua 
    muda wa saa mbili za mazungumzo kuelezea kuhusu taratibu za shule 
    kwa ujumla kabla ya kuanza shughuli yoyote shuleni.
    Mazungumzo haya huanzishwa na mkuu wa shule ambaye huanza kwa 

    kuelezea kama ifuatavyo: 
    Shughuli za shule huanza saa mbili kila siku, inapofika saa nne huwa kuna 
    mapumziko ya dakika ishirini. Baada ya hapo masomo huendelea hadi 
    saa sita,ambapo kunakuwepo mapumziko ya saa moja kwa chakula cha 
    mchana. Saa saba masomo yanaendelea hadi saa kumi.

    Baada ya masomo, wanafunzi hufanya usafi binafsi kwa muda wa saa 
    moja, kisha hujitayarisha kwa chakula cha jioni ambacho hupatikana saa 
    moja na baadaye huendelea na masomo binafsi darasani hadi saa tatu 
    ambao ni muda wa kwenda kulala.

    Saa moja asubuhi ni muda wa kupata kifunguakinywa (staftahi) hadi saa 
    moja na nusu huku wakijiandaa kuanza masomo. Utaratibu huu unaanzia 
    Jumatatu hadi Ijumaa.

    Shule hii ina madarasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Ina mikondo 
    miwili yaani mchepuo wa lugha na mchepuo wa sayansi.
    Shule hii ina maabara mbili. Maabara ya kidato cha kwanza hadi cha tatu na 
    maabara ya kidato cha nne hadi cha sita kwa kufanyia mazoezi ya vitendo 
    kwenye masomo ya lugha na sayansi.

    Idadi ya wanafunzi wote ni mia tano. Kuna ofisi ya naibu mkuu wa shule, 
    mkuu wa taaluma ambaye anashughulika na taratibu za mafunzo ya 
    wanafunzi ya kila siku, mkuu wa nidhamu na ofisi ya walimu kwa ujumla.
    Baada ya maelezo haya, mkuu wa shule alichukua fursa ya kuwatambulisha 
    walimu na wafanya kazi wengine.

    Mara baada ya mkuu wa shule kumaliza kuwatambulisha wafanyakazi wote 
    wa shule, alitoa fursa kwa wanafunzi kuuliza maswali huku akianzia kidato 

    cha kwanza ambao ndio waliokuwa wageni muhula huo.

    Mwanafunzi wa kidato cha kwanza alipewa fursa ya kuuliza swali na kuanza 
    kama ifuatavyo: Mimi naitwa Revocatus Kabayiza; mwanafunzi wa kidato 
    cha kwanza. Swali langu ni hili: “Mmetuelezea kuwa kufanya usafi binafsi 
    shuleni ni kuanzia saa kumi. Je, mbona hamkutuelezea shughuli za siku ya 

    Jumamosi na Jumapili ?”
    Mkuu wa shule alimshukuru kwa swali zuri, kisha akaendelea kuwaelezea 
    kuwa siku ya Jumamosi ni utawala binafsi, yaani wanafunzi hupata staftahi 
    kama kawaida baada ya hapo ni kufanya usafi wa mazingira kwa muda wa 
    saa moja. Wanafunzi hujigawa katika makundi ya kufanya usafi darasani, 
    kwenye mabweni na kwenye mazingira ya shule.

    Chakula cha mchana hupatikana saa za kawaida na siku ya Jumapili ni 
    utawala binafsi shuleni, pale ambapo itaonekana kuwa kuna mwanafunzi 
    mwenye matatizo siku za Jumamosi na Jumapili, ataweza kumwona 
    mwalimu wa zamu kupitia viranja wenu pamoja na viongozi wa madarasa.

    Baada ya maelezo mazuri haya, mkuu wa shule aliwatakia kila la heri na 
    fanaka kwa kuanza muhula mpya wa masomo. Wanafunzi walionyesha 
    furaha yao kwa kumpigia makofi mkuu wa shule wakionyesha walivyofurahia 
    mazumgumzo yake. Baadaye, mkutano ulimalizika na shughuli za shule 

    ziliendelea kama kawaida. 

    Kazi ya 1

    Maswali ya Ufahamu
    1. Ni wahusika gani wanaozungumziwa katika kifungu hiki?
    2. Mkuu wa shule alikuwa na lengo lipi kwa kufanya mkutano na 
    wanafunzi?
    3. Wanafunzi hao walikuwa katika kiwango gani cha elimu? 
    4. Nini maana ya mkuu wa taaluma?
    5. Unadhani wanafunzi hawa wamefurahia mazungumzo 
    waliyopewa na mkuu wa shule ? Eleza maoni yako. 
    6. Kifungu hiki cha habari kinazungumzia kuhusu:
    a. Maabara ya shule ya Icyerekezo.
    b. Utaratibu wa shule ya sekondari ya Icyerekezo.
    c. Ziara ya wanafunzi wa Shule jirani. 

    d. Masomo ya Shule.

    7. Ofisi ya Taaluma hujishughulisha na:
    a. Wafanyakazi wote shuleni.
    b. Wapishi shuleni.
    c. Masomo na kumbukumbu za kila siku za wanafunzi.
    d. Mwalimu wa zamu, viranja na viongozi wa madaras.
    8. Maabara ni sehemu ambayo walimu na wanafunzi hufanyia:
    a. Mchezo wa mpira wa miguu.
    b. Mazoezi ya chemshabongo.
    c. Sehemu ya kufanyia mazoezi ya sayansi kwa vitendo.
    d. Sehemu ya kufanyia mikutano.
    9. Ofisi ya walimu ni:
    a. Eneo la burudani na starehe.
    b. Mahali pa kuzungumzia na kupigia porojo.
    c. Sehemu ya kufanyia kazi na kutayarisha masomo ya wanafunzi.

    d. Hakuna shughuli yoyote ifanyikayo huko.

    1.2. Msamiati kuhusu mazingira ya shule

    Kazi ya 2

    Baada ya kusoma kifungu cha habari cha hapo juu,oanisha 

    msamiati ulio katika sehemu A na maelezo yake katika sehemu B.

    ff

    bb

    1.3. Sarufi: Matumizi ya umoja na wingi wa majina ya ngeli 

    ya LI-YA

    vv

    Mifano ya maneno yaliyomo katika ngeli ya LI-YA katika umoja na wingi: 

     Umoja wingi

    1. Kundi                    Makundi
    2. Shirika                  Mashirika
    3. Jani                       Majani
    4. Gari                       Magari
    5. Darasa                Madarasa

    Tanbihi : Kuna majina ya ngeli hii yasiyokuwa na umoja yaani hubaki katika 
    wingi kama vile:

    Maji, mate, maziwa (ya kunywewa), mateso, manukato, mazishi, matumizi, 

    manufaa, masafa.
    Katika sentensi, majina ya ngeli hii hufuatwa na kitenzi chenye kiambishi 

    awali li- katika umoja na ya- katika wingi.

    Mfano: 

     Umoja                                                                 Wingi
    1. Shirika liliundwa.                                    Mashirika yaliundwa.
    2. Koti lingesafishwa.                                 Makoti yangesafishwa.
    3. Chungwa liliangushwa.                        Machungwa yaliangushwa.

    Majina mengi ya ngeli ya li-ya hufanya wingi wake kwa kiambishi awali makama inavyoonekana kwenye mifano iliyotolewa hapa chini.

    bb

    Kazi ya 4:

    Tunga sentensi za umoja na za wingi kwa kutumia maneno haya: 

    jaribio, swali, jino, jembe, juma, jengo

    1.4. Matumizi ya lugha: Shughuli za Wafanyakazi Shuleni

    Kazi ya 5:

    Zungumzia kuhusu viongozi wote wa shule na wajibu wao.

    Kazi ya 6.

    cc

    1.5. Kusikiliza na kuzungumza
    Kazi ya 7:
    Itambulishe shule uliposomea katika kidato cha tatu
    1.6. Kuandika
    Kazi ya 8:
    Buni mazungumzo kati ya Mkuu wa Shule na wanafunzi wawili.
    Kazi ya 9:

    Iangalie ratiba hii kisha panga vipindi vyako inavyostahili kulingana 

    na ratiba yako ya kila siku.

    dd
    dd
    ddd

    SOMO LA 2: USAFI SHULENI

    Kidokezo

    ff

    Kazi ya 1:

    Tazama mchoro hapo juu kisha uzungumzie unayoyaona. 

    dd

    Soma kifungu cha habari hapa chini kisha ujibu maswali yanayofuata

    Usafi shuleni ni shughuli au kazi moja muhimu inayofanyika shuleni. 
    Usafi wa shule na vifaa vya shule ni njia ya kuendeleza afya kwa kuzuia 
    mawasiliano ya binadamu na athari za taka. Athari hizo zinaweza kuhusu 
    mwili wa binadamu.

    Uchafu unachangia pakubwa kuharibu maisha ya binadamu. Usafi shuleni 
    ni jambo ambalo linafaa kutiliwa maanani na wanafunzi, walimu, viongozi 
    wa shule na wafanyakazi wengine wa shule. Watu wa shuleni wachache 
    wanafikiri kuwa usafi unahusu miili na sare tu wakisahau kuwa usafi 
    huhusu kila kitu kinachopatikana na sehemu zote katika mazingira ya shule.

    Wanafunzi ni lazima wawe safi. Sare humfanya mwanafunzi aonekane 
    maridadi na apendeze. Mavazi ni hifadhi ya staha ya utu wa mtu. Mavazi 
    hukusudia pia kuficha utupu wa mtu. Wanaposafisha sare zao, wanajiepusha 
    na magonjwa yanayotokana na wadudu wanaoweza kuishi katika nguo chafu. 
    Wadudu hawa ni kama chawa, viroboto na kadhalika. Isitoshe, usafi wa sare 
    lazima uende sambamba na usafi wa mwili. Usafi wa mwili unahusiana na 
    kuoga, kunyoa nywele, kupiga mswaki na kukata kucha.

    Sehemu za shule zinazoshughulikiwa kusafishwa ni kama vile: darasani, 
    nje ya darasa, bweni, bwalo, vyoo, chumba cha wasichana, ofisi za walimu 
    na wakuu wa shule, viwanja vya michezo, n.k. Wanafunzi wanaposafisha 
    sehemu zote hizo wanatumia vifaa kama vile: ndoo ya maji, sabuni za 
    kawaida au sabuni za kemikali au dawa za kuulia wadudu wenye kuambukiza 
    watu, deke, n.k. 

    Wanafunzi au wafanyakazi wengine wanakata nyasi zinazozunguka 
    madarasa ili kuwafukuza mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria. Ni 
    lazima kuhifadhi mazingira. Katika bustani, wanatumia jembe kwa kupalilia 
    na panga kwa kukata nyasi. Wanafunzi au watu wengine wasitupe uchafu 
    ovyoovyo. Taka zote zinazotokana na vitu vyote vilivyotumiwa zinafaa 
    kutupwa mahali panapofaa kama vile pipa la taka au jalalani.

    Wanafunzi wasisahau usafi wa vifaa vya shule kama vile: vitabu, madaftari, 
    kalamu, kifutio, dawati, meza ya mwalimu, n.k. Wanafunzi wanaombwa 
    kuwa na vitabu na madaftari yenye vifuniko safi. Inakatazwa kuharibu vifaa 
    vya shule kwa kila mtu.

    Shuleni, maji yote ya kunywa na ya matumizi mengine yatoke kwenye vyanzo 
    salama au yachemshwe. Vyombo vya kubebea na kuhifadhi maji viwekwe 
    safi ndani na nje na kufunikwa ili kuepuka uchafuzi wa maji. Wanafunzi wawe 
    na tabia ya kunawa mikono kwa maji na sabuni kabla na baada ya chakula 

    na baada ya kutoka chooni.

    Kazi ya 2:
    Maswali ya Ufahamu
    1. Usafi shuleni unasadia nini binadamu?
    2. Usafi shuleni ni jambo ambalo linafaa kutiliwa maanani. Eleza. 
    3. Usafi shuleni unawahusu watu gani?
    4. Watu wachache wa shule wanafikiri nini kuhusu usafi?
    5. Kwa sababu gani wanafunzi wanaombwa kuvaa sare safi?
    6. Faida gani ya kusafisha sare za wanafunzi?
    7. Kuna umuhimu gani wa kukata nyasi zinazozunguka madarasa?
    8. Tunatumiaje pipa za taka na jalala?
    9. Wanafunzi wanatumia nini kusafisha bustani ?

    2.2. Matumizi ya msamiati

    Toa maana ya msamiati ufuatao na kuutumia katika sentensi sahihi
    1. Usafi
    2. Uchafu
    3. Athari 
    4. Maanani
    5. Bweni 
    6. Bwalo

    7. Mbu

    Kazi ya 4:
    Jaza sentensi kwa kutumia maneno yafuatayo kutoka kifungu cha 
    hapo juu: (yachemshwe, kunawa, jalalani, kunyoa, mswaki, hifadhi, 
    maridadi, unahusu, usafi, kuharibu)
    1. ……… ni jambo ambalo linafaa kutiliwa maanani shuleni.
    2. Watu wachache wa shuleni wanafikiri kuwa usafi ni…….mikono, 
    kuoga na kuvaa sare safi. 
    3. Sare humfanya mwanafunzi aonekane ……………..na apendeze.
    4. Mavazi ni …………..ya staha ya utu wa mtu.
    5. Usafi wa mwili unahusiana na kuoga, …….. nywele, kupiga ………. 
    na kukata kucha.
    6. Taka zote zinazotokana na vitu vyote vilivyotumiwa, zinafaa 
    kutupwa mahali panapofaa kama vile pipa la taka au..................... 
    7. Wanafunzi wana tabia ya……….. mikono kwa maji na sabuni 
    kabla na baada ya chakula.
    8. Maji yote ya kunywa na ya matumizi mengine lazima yatoke 
    kwenye vyanzo salama au ………………

    2.3. Sarufi: Ngeli ya LI – YA na vivumishi vya kumiliki
    Kazi ya 5:
    Chunguza mifano ya sentensi hapa chini na ueleze aina za maneno 
    yaliyopigiwa mstari.
    a. Jino langu linaniuma.
    b. Gazeti letu lina habari nyingi.
    c. Shamba lako limelimwa vizuri.
    d. Dawati lenu linavunjika.
    e. Soko lao linajaa watu
    Maelezo muhimu
    Vivumishi vya kumiliki ni -angu, -ako, -ake, -etu, -enu na -ao. Vivumishi 
    hivi katika ngeli ya Li-Ya huchukua kiambishi konsonanti l- katika umoja na 

    y- katika wingi.

    Kazi ya 6:

    Andika sentensi zifuatazo katika umoja au wingi
    1. Jiji letu linapata wageni kutoka Kigali.
    2. Ua langu linapamba mazingira.
    3. Dirisha lao linafunguliwa ili hewa iingie.
    4. Sikio langu lina shida ya kusikia.
    5. Gari lenu linatereza siku hii.
    6. Jino langu linaniuma.
    7. Gazeti letu lina habari nyingi.
    8. Shamba lako limelimwa vizuri.
    9. Dawati lenu limevunjika.
    10. Soko lao linajaa watu.

    2.4. Matumizi ya lugha
    Kazi ya 7:
    Mwambie mwenzako namna mnavyofanya usafi shuleni kwako.
    2.5. Kusikiliza na kuzungumza 
    Kazi ya 8:
    Jadili kuhusu “Uhifadhi wa vifaa vya shule” 
    2.6. Kuandika
    Kazi ya 7:
    Tunga kifungu cha habari kwa kutumia kichwa kifuatacho (maneno 
    yasiyopungua mia moja): “Uchafu shuleni ni asili ya maradhi mengi”

    SOMO LA 3: VIONGOZI WETU SHULENI

    fff

    Kazi ya 1:
    Tazama mchoro hapo juu kisha uzungumzie yale unayoyaona.
    3.1. Kusoma na ufahamu: Viongozi wa shule na wajibu wao
    Soma kifungu cha habari hapo chini kisha jibu maswali yanayofuata
    Mimi ninaitwa Kwizera. Ninasoma kidato cha nne. Shule yetu inaitwa shule 

    ya Sekondari ya Gikondo.

    Kayitare ni kiranja wa darasa letu. Yeye hutuwakilisha katika mikutano mingi 
    ya shule. Katika mikutano na mkuu wa shule, yeye huuliza maswali mazuri 
    kwa sababu yeye ni mwanafunzi hodari sana. Mimi ninaelewa vizuri masomo 
    yote; Kiswahili, Kinyarwanda, Kiingereza, Hisabati, Jiografia, Historia na 
    mengine kwani shule yetu ina viongozi wazuri. 

    Mkutubi hufanya kazi maktabani ambapo vitabu vyetu huhifadhiwa kwani. 
    Shule yetu ina vitabu vingi. Mwalimu wa taaluma kila asubuhi, hutukagua 
    ikiwa tumevaa sare. Yeye pia hutushauri kupenda masomo yetu, kusaidiana 
    na kufanya kazi kwa bidii. Yeye hupanga masomo ya kila muhula. Mwishoni 
    mwa kila muhula, sisi hufanya mitihani. Mhasibu wa shule hupokea karo 
    za wanafunzi. Mwalimu wa nidhamu huwaadhibu wanafunzi wanaofanya 
    makosa: wanafunzi watukutu, wanafunzi wanaotoroka shule na wale 
    wanaopiga kelele darasani. 

    Mwalimu mshauri wa wasichana, huchunguza nidhamu ya wasichana. 
    Yeye hutatua shida zao shuleni, hutushauri kuwa na mwenendo mzuri, 
    huchunguza wakati wa kuingia mabwenini na kadhalika. Mwalimu mshauri 
    wa wavulana huchunguza nidhamu ya wavulana na kupanga michezo 
    shuleni kwa kushirikiana na mwalimu mshauri wa wasichana. 
    Wakati wa chakula cha mchana na chakula cha jioni, walimu wa zamu 
    huingia bwaloni kuchunguza chakula chetu na kutushauri kuheshimiana 
    wakati wa kula. Mimi nawapenda sana viongozi wetu shuleni. 

    Kazi ya 2:
    Maswali ya ufahamu
    1. Kwizera anasomea wapi? 
    2. Yeye anasoma kidato gani?
    3. Fafanua umuhimu wa maktaba kwa mwanafunzi.
    4. Je, Kwizera anaelewa vizuri masomo yake? Eleza.
    5. Viongozi wao ni wepi?
    6. Eleza kazi zinazofanywa na mhasibu.
    7. Mwishoni mwa kila muhula wanafunzi hufanya nini?
    8. Nini wajibu wa kiranja?
    9. Mkuu wa shule anaitwa nani na ana majukumu gani?
    10. Walimu wa zamu huingia bwaloni kufanya nini?

    3.2. Msamiati kuhusu mazingira ya shule

    Kazi ya 3:xx

    3.3. Sarufi: Matumizi ya umoja na wingi wa majina ya ngeli 

    ya li-ya

    Kazi ya 4:

    Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia mabadiliko yanayojitokeza 
    kutoka sehemu A kwenda sehemu B
    xx

    TNBH: Kuna majina ya ngeli hii yasiyokuwa na umoja kama vile :
    Maji, mate, maziwa (ya kunywewa), mateso, manukato, mazishi, matumizi, 
    manufaa, masafa.
    Katika sentensi, majina ya ngeli hii hufuatwa na kitenzi chenye kiambishi 
    awali li- katika umoja na ya- katika wingi.
    Mfano: 
     Umoja                                                Wingi
    1. Shirika liliundwa.                       Mashirika yaliundwa.
    2. Koti lingesafishwa.                    Makoti yangesafishwa.
    3. Chungwa liliangushwa.          Machungwa yaliangushwa.
    Maelezo muhimu 
    Majina mengi ya ngeli ya li-ya hufanya wingi wake kwa kuongeza kiambishi 
    awali ma- mwanzoni mwa neno. 

    Kazi ya 5:
    Weka sentensi hizi kati wingi au umoja:
    a. Zoezi hili halieleweki.
    b. Shamba la mjomba ni jipya.
    c. Yai lililoharibika halifai kwa afya ya mwanadamu.
    d. Gari lililoharibika halipendezi.
    e. Matope yamechafua nguo zangu.
    f. Jeshi limemshinda adui.
    g. Juma la kazi limemalizika.
    h. Magurudumu ya gari yanaviringika kasi.
    i. Hekalu limejengwa vizuri.

    j. Majamvi yaliliwa na panya.

    Kazi ya 6:

    Chunguza sentensi hizi kutoka sehemu A na sehemu B uziunganishe 

    ili ziwe sentensi kamili

    dd

    3.4. Matumizi ya lugha: Vyeo vya viongozi shuleni

    Kazi ya 7:

    Husisha maneno kutoka sehemu A kwenda sehemu B

    dd

    3.5. Kusikiliza na Kuzungumza
    Kazi ya 8:
    Zungumzia kuhusu shule uliposomea kidako cha tatu.
    3.6. Kuandika
    Kazi ya 9:
    Andika kuhusu umuhimu wa kuwa na viongozi katika jumuia zetu

    SOMO LA 4 : RATIBA YA WIKI YA MWANAFUNZI

    rr

    Kazi ya 1:
    Tazama michoro hapo juu, tambua kazi zinazofanywa na utaje 

    umuhimu wa kazi hizo

    4.1. Kusoma na ufahamu: Ratiba ya shughuli za kila siku 
    katika Shule ya Gasozi
    Soma kifungu cha habari hapo chini kisha jibu maswali yanayofuata
    Gasimba ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza kwenye shule ya Gasozi. 
    Yeye ni mwanafunzi mwenye bidii na hachelewi shuleni. Jumatatu, Gasimba 
    huamka saa kumi na moja na nusu alfajiri na kuanza kujiandaa kwenda 
    shuleni. Baadaye, yeye hupiga meno yake mswaki, huchana nywele na 
    kuvaa sare yake.

    Mamake Gasimba huamka mapema zaidi ili kumwandalia mwanawe 
    kifunguakinywa. Gasimba hunywa chai kwa mkate kisha hubeba mkoba 
    wake wenye madaftari na vitabu vyake kuelekea shuleni. Gasimba humuaga 
    mamake na kuondoka. Gasimba hufika shuleni saa kumi na mbili na nusu na 
    kuingia darasani na kuanza kusoma. Yeye huwatangulia wanafunzi wengine.
    Saa mbili kasorobo kengele hulia na wanafunzi wote huenda kwenye gwaride 
    ambapo wao husali na baadaye wakaimba wimbo wa taifa la Rwanda. 
    Mwalimu mkuu huwahutubia wanafunzi kisha humpisha mwalimu wa zamu 
    kuwapa wanafunzi matangazo muhimu.

    Saa mbili kamili, somo la kwanza huanza. Baada ya vipindi viwili wanafunzi 
    hupewa dakika ishirini za mapumziko. Chakula cha mchana huliwa saa saba 
    kamili. Masomo huendelea kuanzia saa nane alasiri. Saa kumi na dakika 
    ishirini masomo ya siku huwa yamekamilika. Wanafunzi wote huenda 

    uwanjani kwa michezo mbalimbali kama kandanda, voliboli na kuruka kamba. 
    Ifikapo saa kumi na moja na nusu wanafunzi wote huelekea nyumbani.

    Gasimba afikapo nyumbani, yeye humsaidia mamake kufanya kazi za 
    nyumbani. Baadaye, yeye hufanya kazi zake za ziada na za shuleni. Saa 
    tatu na nusu usiku zifikapo huenda kulala. 

    Kila siku ya wiki huhusika na matukio haya ila siku ya Alhamisi jioni ambapo 
    Gasimba hufanya mazoezi ya kuogelea katika bwawa la kuogelea nyumbani 
    kwao. Ijumaa jioni, wanafunzi hushiriki katika mjadala kuhusu mada ambazo 
    walimu wao huwa wamewachagulia. Jumamosi, Gasimba humsaidia 
    mamake kufanya kazi za nyumbani. Jumapili, Gasimba huendelea na 
    mapumziko kama kawaida. Baada ya kupumzika, Gasimba hujitayarisha 
    kwa ajili ya kwenda shuleni Jumatatu.

    Kazi ya 2:
    Maswali ya Ufahamu

    1. Gasimba anasomea katika shule gani?
    2. Je, Gasimba yuko katika kidato kipi?
    3. Gasimba hufanya nini anapoamka kabla ya kustaftahi?
    4. Baina ya Gasimba na mamake, nani huamka mapema zaidi?
    5. Gasimba hufanya nini afikapo shuleni kabla wanafunzi wengine 
    wafike?
    6. Gasimba na wanafunzi wenzake hufanya nini Alhamisi na Ijumaa 
    jioni baada ya masomo yao?
    7. Gasimba hufanya nini Jumamosi?

    8. Taja shughuli za Gasimba za siku ya Jumapili?

    4.2. Matumizi ya msamiati
    Kazi ya 3:
    Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo: (ratiba, 
    kuogelea, mjadala, huchana nywele na mapumziko)
    4.3. Sarufi: Matumizi ya vivumishi vya kuonyesha vya 

    ngeli ya LI-YA

    Kazi ya 4:

    Tazama sentensi zifuatazo na kuzungumzia mabadiliko 
    yanayojitokeza kutoka sehemu A kwenda sehemu B

    Sehemu A                                                                                    Sehemu B

    1. Bega hili limepambwa nyota za kijeshi.                 a. Mabega haya yamepambwa nyota za kijeshi.
    2. Gari hili ni jipya.                                                                b. Magari haya ni mapya.
    3. Jengo hili ni la hospitali.                                               c. Majengo haya ni ya hospitali.

    4. Pazia hili ni Safi .                                                              d. Mapazia haya ni safi.

    4.4. Matumizi ya lugha: Shughuli za kila siku za mwanafunzi

    Kazi ya 5:

    rr

    4.5. Kusikiliza na Kuzungumza
    Kazi ya 6:

    Eleza kwa ufupi kuhusu shughuli uzifanyazo shuleni unakosomea.

    4.6. Kuandika
    Kazi ya 7:
    Andika kwa ufupi kuhusu maendeleo ya shule yako.

    Tathmini ya mada

    Jibu maswali yafuatayo:

    1. Taja vitu angalau vitano ambavyo hupatikana katika mazingira ya 
    shule yenu.
    2. Zungumzia kuhusu shughuli tatu zinazofanyika shuleni kwenu. 
    3. Eleza majukumu ya wafanyakazi wanne wapatikanao shuleni. 
    4. Tunga sentensi kumi kwa kutumia ngeli ya LI-YA katika umoja 
    na uwingi.
    5. Eleza nafasi ya kila mwanafunzi katika harakati za kuzuia 
    ueneaji wa magonjwa shuleni.



    MADA YA 2 MSAMIATI KUHUSU MAZINGIRA YA NYUMBANI