MADA YA 8 UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Malengo ya Ujifunzaji:
-- Kueleza uhakiki wa kazi za fasihi na umuhimu wake,
-- Kubainisha vipengele muhimu katika uhakiki wa kazi za fasihi andishi,
-- Kutofautisha fani na maudhui,
-- Kuhakiki kazi za tanzu mbalimbali za fasihi andishi,-- Kutumia kwa ufasaha viambishi rejeshi katika ngeli za majina mbalimbali.
16.1. Kusoma na Ufahamu: Uhakiki kama Kazi ya
Kitaalamu
Jinsi binadamu alivyo, na anavyomudu maisha yake ya kila siku, hutokana na
maarifa ya kielimu aliyoyapata darasani au katika tajiriba yake ya kimaisha. Aidha,
watu hujishughulisha na kazi mbalimbali. Kutokana na tofauti za kazi, utawakuta
mafundi katika kazi za ujenzi wa nyumba, mabingwa katika uwanja wa kiteknolojia,
wabobezi katika uchumi na wataalamu katika mambo ya fasihi au lugha kwa
ujumla. Hali kadhalika, jinsi dereva anavyojiamini katika uendeshaji wa gari,
ndivyo mhakiki wa kazi za fasihi anavyotawala katika uchambuzi au uchanganuzi
wa kazi za kifasihi zilizotungwa na wasanii.
Jambo hili linatupeleka kwenye maswali yafuatayo: Je, uhakiki unamaanisha nini?Kwa nini uhakiki? Ni jukumu gani mhakiki wa kazi za kifasihi anastahili kutimiza?
Kimsingi, kazi ya fasihi andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno
yaliyoandikwa kupitisha ujumbe, au ni sanaa inayowasilisha ujumbe kwa njia ya
maandishi. Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na hadithi fupi, tamthiliya, riwaya
pamoja na ushairi.
Kwa hiyo, msanii hatungi kwa kutunga tu ila huongozwa na kutawaliwa na misingi
ya kisanii katika ufundi wake. Katika mwelekeo huu, mhakiki hustahili kushiriki
katika uchunguzi wa kazi ya msanii iliyotolewa ili kuichunguza au kuitathmini.
Kwa hivyo, uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni
juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalumu. Hali kadhalika,
uhakiki wa kazi za fasihi ni kitendo cha kuchambua, kutathmini na kuainisha kazi
ya fasihi ili kuona ubora na udhaifu wa kazi hiyo kwa kutumia kaida au vigezo
husika vya fani na maudhui.
Kutokana na maelezo haya, inaeleweka wazi kuwa mhakiki wa kazi za fasihi bila
shaka huwa ni mtaalamu au mwerevu katika uwanja wa kifasihi ambaye huwa na
uwezo au stadi za kuzisoma, kuzitafakari, na kuzitolea tathmini kazi za fasihi kwa
kujiegemeza katika mwelekeo wa kaida maalum zinazotakiwa kuzingatiwa katika
utunzi wa kazi hizo.
Hivyo basi hatuna budi kukubali kuwa mhakiki wa kazi za fasihi huwa na jukumu
au nafasi kubwa katika kazi za fasihi kama ifuatavyo:
Kwanza, mhakaki ndiye anayefafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kuelewa
vizuri kazi hiyo. Vilevile mhakiki huwaonyesha watunzi au wasanii wa kifasihi
ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hayo mhakiki huwawezesha watunzi
kutoa kazi bora zaidi.
Pengine, inambidi mhakiki huyo awe na habari kamili juu ya mwandishi au msanii
wa kazi inayohakikiwa. Maana yake, inambidi mhakiki kuelewa hali pamoja na
mazingira aliyokuwemo msanii kama kielelezo cha hisia zake au hoja zake. Hivi
mhakiki hufanikiwa kutambua sababu za hisia au dhamira zilizoendelezwa na
msanii katika kazi yake.
Hali kadhalika, mhakiki hutafakari kikamilifu kazi ya msanii na kuichambua
kimawazo au kimalengo kwa kudhihirisha au kutambua maudhui pamoja na
dhamira kuu au ndogondogo ambazo ni kiini cha kazi kamili ya msanii. Ili kulikabili
jukumu hili, mhakiki hutoa majibu kwa maswali yafuatayo:
Msanii anatufahamisha nini? Kazi ya msanii inamlenga nani? Anazungumzia nini
na ni suluhisho gani analotutolea kwa shida alizozitaja? Mwandishi ametungakatika kipindi gani cha historia na katika mazingira gani?
Mwisho, mhakiki huwa na jukumu la kurahisisha mawasiliano au kiungo kati
ya hadhira na mtunzi. Jukumu hili hujidhihirisha kwa njia ya uchunguzi wa jinsi
msanii alivyojenga sanaa yake ili ujumbe wake uwafikie walengwa husika, yaani
uhakiki wa lugha iliyotumiwa na msanii pamoja na jinsi alivyowajenga wahusika
katika kazi yake ya kifasihi. Kwa upande mwingine, uhakiki wa kazi mbalimbali
za kifasihi humsaidia msomaji wa kazi husika ya kifasihi kuielewa au kupatamwangaza fulani juu ya kazi husika aisomayo.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi –ye- ni kiambishi kinachotumika katika tungo kwa kurejelea
mawazo, nomino au mambo yaliyokwisha tajwa au yanayojulikana. Kiambishi hiki
hujihusisha tu na majina ya ngeli ya A-WA- katika umoja, yaani majina ya watu,
Mwenyezi Mungu, pamoja na wanyama. Matumizi ya kiambishi rejeshi – ye –
hutumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
Mfano: Aliyeshiriki
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-
Mfano: Mwanafunzi ambaye
Binadamu ndiye
• Mwishoni mwa kitenzi
Mfano: Mnyama alindaye
Tanbihi: Kiambishi rejeshi –ye- hugeuka – o - katika wingi.
Mfano:
i) Watu walioshiriki katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda
wamekamatwa na kupelekwa mahakamani.
ii) Wanafunzi ambao hufanya bidii hushinda mitihani bila tatitizo.iii) Mbwa ni wanyama walindao nyumba za watu.
MAELEZO MUHIMU YA KUZINGATIA
DHIMA ZA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa
msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo:
• Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi:
Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi ya lugha na taswira, hivyo
mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia msomaji kuelewa vipengele hivikwa kuvifafanua kwa lugha rahisi.
• Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi:
Mhakiki anapoonyesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi fulani, watunzi
wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora zaidi.
• Hukuza uelewa wa mhakiki:
Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki hujiongezea maarifa ya lugha
pamoja na mambo yanayotokea katika jamii.
NAFASI YA MHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Mhahiki kama mtaalamu wa kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni
juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum, huwa na nafasi
kubwa katika kazi za fasihi. Mhakiki ndiye anayefafanua kazi ya fasihi ili hadhira
iweze kumwelewa vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo, hapa mhakiki anasaidia
kurahisisha mawasiliano kati ya hadhira na mtunzi. Vilevile mtunzi huwaonyesha
watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo, huwawezesha watunzikufanya kazi bora zaidi.
SOMO LA 17: TARATIBU ZA UHAKIKI WA KAZI ZAFASIHI ANDISHI
17.1. Kusoma na Ufahamu: Uhakiki wa Fani na Maudhui
Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha ujibu maswali ya ufahamu
hapo chini
Wahenga walisema kuwa maneno huwa na utamu zaidi yanaporudiwa. Kwa hiyo,
hatuna budi kukumbusha kuwa uhakiki ni kitendo cha kuchambua, kutathmini na
kuainisha kazi ya fasihi ili kuona ubora na udhaifu wa kazi hiyo kwa kutumia kaida
husika. Ili kazi yake itimizwe kwa hali mwafaka, mhakiki anastahili kupitia hatuatatu zifuatazo:
Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi; hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya
fasihi kwa kina na kuielewa vizuri.
Pili ni kuainisha na kuchambua mambo muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo
kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui.
Tatu ni kutoa tathmini au kuelezea ubora na udhaifu wa kazi inayohusika. Je,
tunapozungumzia vipengele vya fani na maudhui tunagusia nini?
Tuchukue mfano wa barua pepe ambayo imeandikwa ovyo ovyo bila kuzingatia
mitindo ya kisarufi, aya pamoja na alama za vituo. Mambo haya yote huchukuliwa
kama umbo la barua pepe hii. Kama umbo hili halivutii basi msomaji hatakuwa na
nia ya kuisoma barua pepe hii. Mfano wa pili ni wa nyumba inayong’aa kwa rangi
na mapambo mbalimbali yaliyoko kwenye nyumba hiyo. Atakayeiona nyumba
hii, atakuwa ameingiwa na udadisi wa kuingia ndani kwa sababu uzuri wake
umemvutia mtazamaji. Umbo hilo ndilo linalolinganishwa na fani katika kazi za
kifasihi.
Hivyo, baada ya kuvutiwa na umbo la barua pepe, hamu au hiari ya kusoma
ujumbe unaowasilishwa ndani yake itaongezeka. Ujumbe huo utatiliwa maanani
na kupokewa kwa urahisi. Vilevile, mtazamaji aliyeridhika na umbo la nyumba
hatasita kuingia ndani ili ashuhudie jinsi vifaa vya nyumbani vilivyo kama vile
mpangilio wake, vyumba, milango, n.k. Atatafakari yeye mwenyewe ujumbe
kuhusu uwezo mkubwa wa fundi aliyeijenga na kuipamba nyumba hiyo. Ujumbe
huu au yaliyomo hufananishwa wazi na maudhui katika kazi za fasihi.
Mifano ni wa msichana mrembo ambaye maumbile yake ni mithili ya malkia. Ah!
Utapatwa na bumbwazi utakapomtathmini kimwenendo au kitabia. Mfano huu
ungelikwenda sambamba na mtu ambaye unamkuta amevaa nguo za bei ghali
iwapo mwili wake unatoa harufu mbaya; maana yake mwezi mzima umemalizika
bila mtu huyo kuoga.
Kwa hiyo, kazi ya msanii wa fasihi yoyote huwekwa mikononi mwa mhakiki ili
kuitathmini na kutoa maoni yake kuhusu kufanikiwa au kutofanikiwa kwa msanii.
Kwa upande mmoja, kufaulu au kutofaulu kwa msanii hutokana na jinsi umbo au
fani ya kazi yake inavyowavutia walengwa wake.
Kwa upande mwingine, kufaulu au kutofaulu kwa msanii huelezwa na jinsi ujumbeuliokusudiwa kuwasilishwa ulivyopangwa toka mwanzoni hadi mwishoni.
17.2. Matumizi ya Msamiati
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi husika ni – o - . Kirejeshi hiki hujihusisha na ngeli za majina
kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi -
• Mwishoni mwa kitenzi
Mifano mbalimbali kuhusu ngeli za majina husika.
Ngeli ya majina Matumizi ya kirejeshi – o –
LI-YA- : Swali ambalo litaulizwa na wengi ndilo litakalojadiliwa.
zaidi – Maswali ambayo yataulizwa na wengi ndiyo yatakayojadiliwa zaidi.
KI-VI- : Kikulacho kinguoni mwako – Vikulavyo vingoni mwako.
MWELEKEO WA MAELEZOi) UHAKIKI WA HADITHI FUPI NA RIWAYA
Kwa kawaida, uhakiki wa kazi za fasihi andishi hutegemea FANI na MAUDHUI.
A. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA UHAKIKI WA FANI
Kama sura ya nje ya hadithi fupi au riwaya, fani hufanyiwa uhakiki kwa kuzingatia
vipengele fifuatavyo:
–– Wahusika
–– Muundo
–– Lugha
–– Mtindo
–– Mandhari
a) WAHUSIKA: Ni watu au viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu
katika kazi za fasihi.
Aina za wahusika: Wahusika wa hadithi fupi au riwaya hujigawa katika
makundi makuu mawili:
Wahusika wakuu: Mhusika mkuu ni mhusika mmoja au wawili ambao hujitokeza
kutoka mwanzo hadi mwisho wa hadithi fupi.
Wahusika wadogo: Ni aina ya wahusika muhimu sana ambao humsaidia
mhusika mkuu kuipa hadithi au riwaya mwelekeo wa kisanaa na kimaudhui.
Tabia za wahusika: Kutokana na majukumu yao, wahusika huonyesha tabia
za aina tatu:
Wahusika bapa: Ni aina ya wahusika ambao hawabadiliki kitabia kutoka
mwanzoni mpaka mwishoni mwa hadithi fupi.
Wahusika duara: Ni wahusika ambao wanabadilika kitabia kutokana na
mabadiliko ya mazingira.
Wahusika foili: Ni wahusika wenye tabia zinazobadilika kinusu. Wako kati ya
wahusika bapa na wahusika duara.
b) MUUNDO: Ni namna msanii anavyopanga visa vyake au fikra zake katika
hadithi fupi, yaani mtiririko wa visa na matukio. Kinachozingatiwa hapa ni jinsi
mwandishi alivyopanga kazi yake; mfano sura na sura, kisa na kisa au tukio
na tukio.
c) LUGHA: Kipengele cha lugha ni muhimu sana katika fasihi kwani ndicho
hutenganisha fasihi na sanaa nyinginezo. Matumizi ya lugha katika fasihi yapo
ya aina mbalimbali: kuna tamathaili za semi, misemo, nahau, methali, lahaja za
wahusika, uchaguzi wa msamiati, miundo ya sentensi.
Mifano ya tamathali za semi:
• Tanakali za Sauti: Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au
hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
Mfano: anguka pa!
• Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti
kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’.
• Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye
uhai (sifa za kibinadamu).
• Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili
kusisitiza ujumbe fulani.
• Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha
maneno ya kinyume au yanayokinzana.
• Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutotumia
viunganishi ambapo kitu kimoja hufanywa kuwa sawa kabisa na kitu
kingine.
• Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au
jambo fulani kwa msomaji.
• Taashira: Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina
au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na
kile kilichotumiwa.
• Majazi: Majazi ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina
yao halisi.
• Lakabu: Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika
wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa
zake.
Chuku: Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe
fulani au kusifia kitu, kutilia chumvi.
d) MTINDO: Mtindo ni namna ambavyo mwandishi huipa hadithi yake sura ya
kifani na kimaudhui.
Mtindo ndio unaotofautisha wasanii. Katika mtindo tunachunguza sana
matumizi ya lugha.
e) MANDHARI: Mandhari ni mazingira au mahali tukio la hadithi fupi lilipotokea.
Kuna mandhari ya kubuni na mandhari ya kweli.
B. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA MAUDHUI
Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi.
Hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi
akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Mawazo na mafunzo haya hayazuki
hivihivi tu. Kwa hiyo wakati wa kuyachambua na kuyajadili ni lazima yahusishwe
na hali halisi ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi zilizopo katika jamii, hali hizi
ndizo zilimzaa, zilimlea na kumkuza msanii.
Wakati wa kuchambua kazi za kifasihi mhakiki ni lazima ajiulize amaswali
yafuatayo:
-- Je, msanii anatueleza nini?
-- Je, msanii kamtungia mtu wa tabaka gani?
-- Anamtukuza nani?
-- Anambeza nani?
-- Msanii anataka tuchukue hatua gani katika utatuzi wa matatizo
ayashughulikiayo katika kazi yake?
Maudhui hujengwa na vipengele muhimu vifuatavyo: Dhamira, ujumbe,
migogoro, msimamo wa msanii pamoja na falsafa yake.
a) Dhamira: Ni mawazo yanayojitokeza sana katika kazi ya fasihi. Ni jumla
ya maana anayoivumbua mwandishi aandikapo, na jumla ya maana
anayoitambua msomaji katika usomaji wake.
Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo
Dhamira kuu ni kiini cha kazi ya fasihi, ni wazo kuu.
Dhamira ndogondogo ni mawazo madogomadogo ambayo hujenga dhamira
kuu.
b) Migogoro: Ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu,
mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake. Migogoro ni mivutano na
misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati
ya wahusika, familia zao au matabaka yao. Migogoro hii inaweza kuwa ya
kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kifalsafa, n.k.
c) Ujumbe: Ni funzo na maadili yaliyokusudiwa na mtunzi yaifikie jamii
aliyoilenga kufikisha kazi yake ya fasihi.
d) Falsafa: Ni imani na mwelekeo wa mwandishi kuhusu maisha katika jamii.
e) Msimamo wa msanii: Msimamo wa msanii kuhusu masuala mbalilmbaili
ya kijamii hubainishwa na mawazo, mafunzo, lengo na falsafa. Msimamo
ndio uwezao kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaotunga kazi
za fasihi zilizo na kiini na chimbuko moja. Kwa hiyo, msanii huweza
kuchukua msimamo wa kimapinduzi au wa kiyakinifu kulingana na jinsi
anavyoyazingatia maisha ya jamii inayozungumziwa.
C. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA TAMTHILIA
Tamthilia au mchezo wa kuigiza huweza kuhakikiwa jukwaani au kupitia maandishi.
a) Uhakiki wa Kifani
Wahusika: Wahusika katika tamthilia huwa wengi pamoja na tabia zao
mbalimbali.Tamthilia huwa na wahusika halisi ambao wanajitetea jukwaani
kimatendo na kitabia wakati.
Muundo: Tamthilia huwa na sehemu tatu: Mwanzo, Katikati na Mwisho.
Sehemu zake zinatazamiwa kuingiliana, kujengana na kukamilishana. Muundo
katika tamthilia huangaliwa kwa kuzingatia idadi ya vitendo/ sehemu na idadi ya
maonyesho.
Mtindo: Tamthilia huwa na mgawiko wazi wa matendo na matukio kwa mujibu
wa sehemu na sura mbalimbali. Majina ya wahusika huandikwa katika upande
wa kushoto, kisha koloni, halafu hufuatiwa na maneno halisi yaliyotamkwa na
mhusika huyo.
Lugha: Tamthilia inatawaliwa na lugha ya mazungumzo katika majibizano au
hata mazungumzo pweke. Ucheshi, porojo au mizaha, tamathali za usemi na
onomatopia hutumiwa sana.
D. UHAKIKI WA MASHAIRI
Sawa na kazi nyingine za fasihi, uhakiki wa mashairi huzingatia fani na maudhui.a) Fani
Uhakiki wa fani ya shairi huzingatia muundo wake, yaani jinsi shairi lilivyoundwa
kwa kuangazia mizani, vina, mishororo n.k Aidha, ni muhimu kutaja aina na bahari
za shairi zinazohusiana na kila sifa uliyoitaja.
Idadi ya mishororo katika kila ubeti - Tumia idadi ya mishororo kubainisha
aina ya shairi hilo.
Kwa mfano: Shairi lina mishororo minne katika kila ubeti, kwa hivyo ni Tarbia.
Idadi ya mizani katika kila mshororo na katika kila kipande cha
mshororo.
Kwa mfano: Kila mshororo una mizani kumi na sita: nane katika utao na nane
katika ukwapi.
Idadi ya vipande katika kila mshororo - Taja ikiwa shairi lina kipande
kimoja, viwili, vitatu au vinne kisha utaje bahari yake.
Kituo, kiishio au kibwagizo - Ikiwa mstari wa mwisho umerudiwa rudiwa,
basi shairi lina kibwagizo au kiitikio, la sivyo lina kiishio.
Vina - Zingatia vina vya kati na vya mwisho kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
Kisha utaje ikiwa ni Mtiririko, Ukara au Ukaraguni.
Matumizi ya lugha: Mtindo wa lugha hurejelea namna mbalimbali ambazo
mshairi anatumia mbinu za lugha. Mshairi anaweza kutumia mbinu za lugha.
kama vile: Tanakali za sauti, Tamathali za semi, n.k.
Katika mtindo wa lugha mhakiki huchunguza uhuru wa msanii, yaani mshairi
hafungwi na kanuni za kisarufi za lugha katika utunzi wa shairi. Anaweza kufanya
makosa ya kisarufi kimakusudi ili shairi lizingatie umbo fulani.
b) Maudhui
Uhakiki wa maudhui ya shairi huzingatia vipengele vikuu ambavyo ni Dhamira(Dhamira kuu na dhamira ndogondogo) pamoja na Ujumbe.
SOMO LA 18: MFANO WA UHAKIKI WA TAMTHILIA
18.1. Kusoma na Ufahamu: Muhtasari wa Hawala ya Fedha
Familia ya Mzee Ibrahim CHANDE imetumiwa hawala ya fedha na mpwaye
anayesomea mjini London. Thamani ya hawala hiyo ni shilingi elfu mbili. Ibrahim
CHANDE anapaswa kuchukua kiasi cha shilingi mia tatu, kiasi kingine cha
shilingi miatano ampatie mama yake Abdul, mia tano zinazobakia amwekee
mpwa wake.
Hawala hii inaleta matumaini katika familia ya Ibrahim CHANDE. Familia
nzima wanafikiri kwamba umaskini na njaa vimemalizika. Kwa kuwa wake zake
CHANDE walitafuta mtu wa kuwasomea hawala ya fedha (kwa kuwa wao
hawakujua kusoma wala kuandika), habari inazagaa mahali pote na majirani zote
wanaarifiwa.
Watu kadha wa kadha wanakuja kukopa fedha na chakula kwenye familia
hiyo. Wengine wanamfuata Ibrahim CHANDE kila anapokwenda ili awasaidie
kutokana na fedha hizo.
Inambidi Ibrahim CHANDE aende kubadilisha hawala ya fedha posta. Anapofika
anaombwa kuwa na kitambulisho lakini anakikosa. Hana kitambulisho chochote
kile ila kadi ya chama isiyo na picha. Hivyo analazimika aende kwenye kituo chapolisi.
Anapofika, anaelezwa kuwa hawezi kuwa na kitambulisho kama hana picha.
Ibrahim CHANDE anamwendea AMBROZI ambaye ni mpigapicha. Anampiga
picha na kumwambia kurudi kesho yake baada ya kulipa shilingi thelathini. Kwa
bahati mbaya, anaporudi AMBROZI huyu anamnyang’anya picha pamoja na
pesa zake.
Siyo hayo tu, bali anamfanyia mabaya zaidi. MBAYE anajitolea kumsaidia
CHANDE kutoa fedha kwenye posta. Kwa upande mwingine, dada yake
CHANDE, yaani Mama Abdul, anakuja kudai pesa zake zilizoelezwa kwenye
barua iliyokuja pamoja na hawala hiyo.
Mzee huyo inambidi auze hereni za dhahabu za mkewe ili dada yake asiende
mikono mitupu. Ibrahim CHANDE hapumziki hata kidogo. Mwishowe, MBAYE
aliyejidai kumsaidia anamwambia kuwa fedha alizichukua kutoka posta lakini
akanyang’anywa na wezi akiwa njiani.
Matumaini yote ya Ibrahim CHANDE pamoja na wake zake yakafifia. Amne mke
wake wa pili akaamua kwenda zake na Mama Dogo, mke wake wa kwanzaakaenda kijijini kulima shamba.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi – o – kimehusishwa na majina ya ngeli za majina ya U-I na
U-ZI. Kimetumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-• Mwishoni wa kitenzi
Mifano mbalimbali kuhusu ngeli za majina husika
U-I- : Mti ulioanguka umefunga njia – Miti iliyonguka imefunga njia.
Mti ulioanguka ndio uliofunga njia – Miti iliyoanguka ndiyo iliyofunga njia.
U-ZI- : Tumenunua uzi unaoonekana vizuri - Tumenunua nyuzi zinazoonekana
vizuri.
MWELEKEO MUHIMU
UHAKIKI WA FANI
1. Wahusika na tabia zao
a) Wahusika wakuu
Ibrahim CHANDE ndiye mhusika mkuu katika tamthiliya “Hawala ya fedha”. Ana
wake wawili: MAMA DOGO na AMNE. Habadiliki kitabia tangu mwanzo hadi
mwisho wa mchezo, yeye ni mhusika bapa. Ubapa wake unadhihirishwa na
ujinga wake anaokumbana nao katika habari yote. Mhusika huyu hajui kusoma
wala kuandika. Isitoshe, hataki pia wake zake wawe na kisomo (uk. 4). Kwa kuwa
inaruhusiwa katika dini ya Uislam, Ibrahim CHANDE ana wake wawili. Katika
usemi wake wote kuna rejesta ya dini. Pengine anaonekana akitoa sadaka kwamaskini, wengine anakataa kuwapa.
Isipokuwa ujinga wake wa kutojua kusoma na kuandika, mzee huyu anaonyesha
moyo wa kusikiliza shida za watu wengine hasa hasa wale wanaotaka msaada
kutoka kwake.
b) Wahusika wadogowadogo au wasaidizi
i) Mama Dogo: Huyu ni mke wa kwanza wa Ibrahim CHANDE. Yeye na Amne
ni wake wenza. Hali yao ya uke wenza haiwatenganishi wala kuwafanya
wachukiane. Wanaonyesha ushirikiano tangu mwanzo hadi mwisho wa
mchezo. Mama Dogo anaonyesha busara katika maneno yake. Mfano
bayana ni usemi wake (uk. 41), pale ambapo anasema:”Afugaye punda
lazima ampendelee mlimaji nyasi. ” Katika usemi huu alitaka kuonyesha
namna ambavyo hakuna mtu pekee anayeweza kujitosheleza. Kama mtu
ana duka, anategemea wale ambao wanakuja kununua vitu katika duka hilo.
Kwa sababu hiyo, mtu yeyote anapaswa kutodharau mwenzake. Kila wakati,
Mama Dogo anaonekana akimtetea mumewe. Anaonekana akihangaishwa
na usalama wa mumewe. Ili watu wasiendelee kumfuata Ibrahim CHANDE
kwa ajili ya fedha, yeye alibuni kisingizio na kuwaambia watu kuwa mume
amenyang’anywa fedha hizo (uk. 36-38). “Alipopata pesa watu wakamvamia
(uk. 36).” “Majangili ndugu yakamvamia. Hata senti moja si yake. Mungu na
Mtume, sasa pesa zimekwenda na heshima yetu pia imekwenda.” Pengine
Mama Dogo anaonyesha imani katika Mungu. Anaamini kuwa Mwenyezi
Mungu hasahau waamini wake (uk. 1). Yeye ndiye anaweza kunusuru maisha
ya mtu aliye hatarini (uk. 37).
ii) AMNE: Huyu ni mke wa pili wa Ibrahim CHANDE, yaani mke mwenza
wa Mama Dogo. Tabia yake inaonyeshwa na ushirikiano anaokuwa nao
kati yake na Mama Dogo mbele ya mume wao. Amne ana tamaa ya kuwa
na kisomo. Anamwona mumewe kama mjinga wakati wowote anapomzuia
kwenda kusoma. Mwishoni mwa mchezo, anaonyesha tabia ya kutoweza
kuvumilia hali ya umaskini na njaa inayojitokeza katika familia yake. Alipokata
tamaa ya kupata fedha zilizokuwa kwenye hawala iliyotumwa na Abdul,
yeye aliamua kumtoroka mumewe.
iii) Mbarka: Ni mwenye duka. Kutokana na mazingira au hali mbalimbali,
yeye anabadilika kitabia. Wakati alipojua kuwa Ibrahim alikuwa na hawala
ya fedha, alifurahi sana na kumkopa mchele bila wasiwasi. Lakini alipopata
habari kuwa pesa za Ibrahim zimeibiwa, alikasirika na kuanza kumdai kwa
fadhaa. Mbarka anaonyesha tabia za uduara.
iv) Issa: Huyu ni rafiki yake Ibrahim CHANDE. Urafiki wao unatokana na
kuwa Issa anataka sehemu ya fedha alizonazo Ibrahim. Yeye anaonyesha
tabia ya unyonyaji. Kila alipoongozana na Ibrahim wakienda mjini, alitaka
Ibrahim amlipie basi. Unyonyaji wake unaonyeshwa pia na kunyang’anya
watu akitumia ujanja (uk. 16). Yeye alikuwa anaganda kwenye Ibrahimkama rubu ama kupe wagandavyo kwenye ng’ombe.
v) Ambrozi: Ni mwenye studio. Yeye anaonyesha tabia ya kunyanyasa watu
duni. Yeye ni mjangili: anachukua pesa za watu kwa bure na kuwadhulumu
ili wasije wakamdai fedha zao. Lugha anayoitumia ni ya matusi. Amandina
Lihamba alitumia katika mchezo wake wahusika wengine wa aina mbalimbali
ili kuonyesha hali halisi ya maisha. Mojawapo wa wahusika hao ni bapa
vielelezo. Majina yao yanaonyesha shughuli au tabia zao. Hao ni kama
mchuuzi, polisi, karani, maskini na kadhalika. Mhusika Abdul anasimamia
kundi la watu waliopata kisomo. Yeye anajua umuhimu wa kusoma, ndiyo
sababu alienda Landon. Vilevile, anajua wazazi wanahitaji msaada kutoka
kwa watoto wao wakati wakiwa na uwezo. Kwa sababu hiyo, alitumia
mjomba wake pamoja na mama yake hawala ya fedha.
2. Mtindo
Mtindo ni kiwango cha lugha alichotumia mwandishi katika Hawala ya fedha.
Lugha inayotumiwa ni ya mazungumzo kwani kitabu hiki ni cha mchezo wa
kuigiza, yaani tamthiliya. Vipengele vya lugha vilivyotumiwa na msanii ni tamathali
za usemi, nahau, methali, misemo na rejesta. Pengine alitumia lugha ya kawaida,
lugha inayoeleweka kwa wazungumzaji wengi wa lugha hiyo.
Tamathali za usemi
a) Sitiari: mifano, - Umaskini bila nyumba ni kifo - Madeni yatushika mpaka
pwani - Ndiye shetani mkubwa. b) Tashibiha - Kukusanyika kama sisimizi,
(uk. 3) - Asiponilipa haraka nitamganda kama rubu, (uk. 16)
ii) Methali - Kutoa ni moyo si utajiri, (uk. 13) - Ulimi hauna mfupa: ulimi
husema yote, yaani mazuri na mabaya. - Dawa ya moto ni moto: kwa tatizo
nzito lazima kauli nzito.
iii) Nahau - Kutia chumvi, - Chungu nzima, - Kukata kauli, - Kuwa na mkono
mrefu (kuwa na huruma kwa kila mtu), - Kuwa na mkono wa birika (kinyume
na kuwa na mkono mrefu), - Kukata tamaa, - Kufariki dunia/kuaga dunia.
3. Muundo
Msanii alitumia muundo wa moja kwa moja, yaani hakufanya mazungumzo
yanayoweza kutatanisha msomaji. Visa na matukio muhimu vya kuzingatia
katika Hawala ya fedha ni hivi vifuatavyo: - Taarifa inayomfikia Ibrahim CHANDE
yenye ujumbe wa kupelekewa hawala ya fedha na kuwa postani. - Tumaini la
kuwa hawala ya fedha ingemwokoa toka hali yake ya umaskini, - Kupanda kwa
madeni, - Harakati za kubadilisha hawala hiyo, - Kupanda kwa tumaini la Ibrahim,
- Matumaini ya kupata vitambulisho, - Kupatikana kwa fedha na kuibiwa kwake
(Upeo wa habari), - Kushuka chini kwa tumaini. Msanii amefaulu kujenga kiinikimoja kutokana na mchanganyiko wa matukio mbalimbali.
4. Mandhari
Mandhari inayozungumziwa mchezoni ni halisi. Kama tulivyoelezwa na mwandishi,
habari hii inatokea katika mji mdogo pwani mwa Afrika Mashariki.
UHAKIKI WA MAUDHUI
Katika uchunguzi wa maudhui ya mchezo wa Hawala ya fedha tunachambua
dhamira kuu pamoja na dhamira ndogo.
Dhamira kuu
a) Unyonyaji na kuharibika kwa urasimu
Unyonyaji ni hali ya kutegemea wengine bila ya kufanya kazi; ni hali ya kuishi kwa
jasho la mwingine. Katika tamthiliya Hawala ya fedha, unyonyaji unadhihirishwa
na hasa hasa na majirani wa Ibrahim CHANDE wanaotaka awasaidie kwa kila
hali baada ya kupata habari kuwa ametumiwa hawala ya fedha. Kuna wanaotaka
awakopeshe mchele na wengine fedha kiasi kwamba angetimiza hoja zao angebaki
mikono mitupu. Mhusika anayeonekana kuwa mnyonyaji kuliko wengine ni ISSA.
Huyu anamsindikiza Ibrahim CHANDE katika harakati za kubadilisha hawala ya
fedha ili apate fedha. Kila wanapoenda, ISSA anataka Ibrahim amlipie basi. Si
hayo tu, anataka ampatie fedha za kutumia katika shughuli mbalimbali. Watu
wengine wanaodhihirisha unyonyaji ni msichana aliyekutana na Ibrahim CHANDE
akimuomba msaada kwa mara nyingi. Pengine ni Ambrozi, aliyemnyang’anya
pesa zake alipoenda kujipigisha picha. Mhusika mwingine ni MBAYE aliyefaidi
hawala isiyokuwa yake. Kwa upande mwingine kuna katika mchezo huu, hali ya
kuharibika kwa urasimu. Ijulikane kuwa urasimu ni utaratibu wa kuendesha kazi
za kiofisi kulingana na kanuni za kiutawala. Katika mchezo (tamthiliya) Hawala ya
fedha kuharibika kwa urasimu kunatambulika kutokana na viongozi (makarani).
Hawa hawafanyi kazi yao kama ilivyo. Hawakutaka kuendesha haraka mambo ya
hawala ya fedha ya Ibrahim ili yeye awapatie rushwa.
b) Ujinga
Ujinga unatokana na tabia ya Ibrahim: kutojua kusoma, kukosa vitambulisho
ambavyo ni mambo muhimu ya raia. Kwa ajili ya kutojua, ilimbidi Ibrahim
kusomesha barua yake iliyohusu Hawala ya fedha. Habari hiyo ilipaswa kuwasiri lakini ilisambaa katika kijiji kizima kutokana na kuwa barua imesomeshwa.
Dhamira ndogo
-- Mvutano baina ya vizazi (vijana mbele ya wazazi)
Mvutano huu unaelezwa na msichana mmoja aliyetukana Ibrahim baada ya
kujionyesha mbele yake akitaka msaada na kunyimwa. Matusi yake yalienda
pamoja na kumsingizia kuwa alitaka kumtongoza. Mvutano unaonekana pia
kutokana na tabia ya Ambrozi aliyempiga Ibrahim badala ya kumpa picha zake.
Alionyesha dharau kubwa mbele yake mzee.
-- Nafasi ya mwanamke katika jamii
Katika nchi nyingi za Afrika, mwanamke huonekana kama kiumbe duni. Mambo
yanayokuwa vilevile katika Hawala ya fedha. Ibrahim anaonyesha dharau lakini
wanawake hawa wanaonekana kuwa washauri wa nafasi ya kwanza wa mume
wao.
AMNE anaonekana kujikomboa kutoka dharau hiyo. Katika kitabu hiki, wanawake
wengine huonekana wakitaka kusitisha mambo ya rushwa.
-- Nafasi ya fedha katika maisha ya kila siku
Dhamira hii inajidhihirisha katika matukio mengi ya habari hii. Kusomesha barua
lazima fedha, kutafuta vitambulisho ni fedha, picha, chakula, safari katika basi ni
mambo hayo hayo. Inadhihirika kuwa watu wote wametekwa na tamaa ya fedha
ili waweze kufanya shughuli zao mbalimbali. Mfano wa watu wanaotamani fedha
kuliko wengine ni ISSA. Huyu anatumia hila ili aweze kuzipata.
Migogoro
Tamathiliya hii ina migogoro kadhaa ambayo inajitokeza katika jamii.
Mgogoro wa kiuchumi ni wa kwanza kuonyeshwa. Mgogoro huu unaiathiri jamii
kwa kiwango kikubwa. Wenye nacho wameonyeshwa kuwa ndio wanyanyasaji
wakubwa wa watu wa chini. Mwandishi anaelekea kueleza kwamba si sawa
kuwa na matabaka ya wafanyakazi na wafanyiwa kazi, yaani, mabwana na
watwana (uk.38).
Mgogoro mwingine unatokana na hali ya mazingira kati ya ukale na
usasa. Mwandishi anaelezea athari za kutojua kusoma na kuandika katika jamii.Kwa upande mmoja kuna watu wangependa kusoma, wengine hawataki.
Ujumbe
Tamthiliya ya Hawala ya Fedha ina ujumbe ufuatao:
-- Ni vema kuwa na busara katika utekelezaji wa mambo.
-- Elimu ni ufunguo wa maisha. Ni vema kuwa na tahadhari wakati wa
matumizi ya fedha.
-- Uvivu ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya jamii.
Falsafa
Hawala ya Fedha ni tamthiliya inayoonyesha falsafa ya mapambano dhidi ya
unyonge. Msimamo wa mwandishi na falsafa yake juu ya maisha ni kuwa watu
wasikate tamaa wanapokutana na matatizo. Utatuzi wa matatizo si wa siku moja,unachukua muda na hatimaye ushindi lazima upatikane.
19.1. Kusoma na Ufahamu: Kila Mtoto na Koja Lake
Rubyogo lilikuwa jina la kupanga la bwana Ndizihiwe. Wengine walikuwa
wanamwita Nyangufi. Majina haya aliyapewa utotoni mwake alipokuwa na umri
wa miaka mitatu. Asili ya jina hili ilielezwa na kimo chake: Ndizihiwe alikuwa
mfupi sana na mwembamba. Aliyekuwa amemwona hakuwa anaamini kwamba
siku moja mtoto huyu atafikia kuwa mtu mzima. Wazazi wake walikuwa wakiishi
kwa mnung’uniko na fedheha katika kijiji cha Shengerero, Jimbo la Kusini nchini
Rwanda.
Ntawiheba (kifupi cha Ntawihebagihumeka) na mkewe Bazubagira walikuwa
wazazi wa Rubyogo. Huyu alikuwa mtoto wa pekee. Familia ya Rubyogo
ilikuwa inaishi kwa kutegemea kilimo tu. Wakati mmoja wazazi wake walikuwa
wakifurahia mavuno ya kilimo chao na wakati mwingine kulalamikia hali ya hewa.
Mathalan, hali hii ya malalamiko ilikuwa ikijitokeza hususan wakati wa maafa.
Ntawiheba na mkewe walifanya bidii kwa kumlea ipasavyo mtoto wao. Walimpatia
maadili toka utotoni hadi alipoanza elimu ya msingi. Ntawiheba na Bazubagira
walikuwa wanapendana sana na kushirikiana katika kazi zote za kijamii. Majirani
zao walikuwa wakiitamani familia yao. Aidha, Ntawiheba na mkewe walikuwakielelezo cha familia yenye kuishi kwa amani na masikilizano.
Siku moja alipokuwa katika kazi ya kupalilia migomba, Ntawiheba alipata fursa
ya kuwaza juu ya maisha ya familia yake kwa siku za baadaye. “Je, ni jambo
la busara kweli kumzaa mtoto mmoja tu na tena mwenye ulemavu wa kimo?”
Alijinung’unikia. Wazo la ukewenza lilimtawala sana na kumsumbua kupita
kipimo.
Alipofika nyumbani jioni, mkewe alimkaribisha kwa chakula cha mchana lakini
yeye alikipokea kwa shingo upande. Mkewe alipomtupia maneno ya utani,
mumewe hakumwonyesha jino. Aliendelea kuonyesha hali ya kukasirika na
kukosa furaha moyoni mwake. Hali hii ilimkera mkewe na kumsogelea, “Mume
wangu mpendwa, mbona hali yako leo imenitisha? Ni balaa ipi iliyokufikia siku ya
leo?”, mkewe alimbembeleza.
Ntawiheba alishindwa kuficha sababu za huzuni yake. “Mke wangu, miaka kumi na
miwili imemalizika tangu siku yetu ya kufunga ndoa. Maisha tuliyo nayo leo unajua
wazi haturidhiki nayo. Zaidi ya hayo, unaona jinsi mtoto wetu alivyo kimaumbile:
mfupi mithili ya kinu! Unadhani kuwa Rubyogo atatufuta machozi kweli? Mimi
ningependekeza nimwoe....” Anguka pa! Kabla hajakamilisha sentensi hii, mkewe
alipatwa na mshituko na kuanguka chini kama mtu aliyepoteza fahamu. Mumewe
huruma ilimwingia na kumhudumia kwa haraka. Alimwimbia wimbo mzuri sana
wa kimapenzi, ule ule ulioimbwa siku ya ndoa yao. Punde si punde, Bazubagira
alizinduka na kumwangalia mumewe machoni. Alimkumbatia na kuweka kichwa
chake kifuani pa mumewe. “Mume wangu, ni shetani yupi aliyekutembelea leo?
Kwa nini unataka nijitoe uhai kweli? Ni kosa gani nililokutendea kusudi uchukue
uamuzi huo wa kuniletea mkemwenza wa kunitesa? Kwa nini hukubali kwamba
mtoto ni sawa na mwingine hata akiwa na kasoro fulani? Mume wangu, kila
mtoto na koja lake!”, Bazubagira aliongea kwa huzuni mno machozi yakimtoka
machoni.
Ntawiheba alipigwa na bumbuwazi kisha akaangua kilio. Hali hii ilirudisha
kumbukumbu ya ahadi aliyoitoa siku ya ndoa yao mbele ya mkuu wa wilaya
pamoja na mbele ya kasisi kanisani. Hivyo, alimwomba mkewe msamaha na
kumwahidi kutofikiria tena hata siku moja mpango mbaya ule.
Ndizihiwe alipoingia shule za sekondari alionyesha maarifa yasiyo ya kawaida.
Toka mwaka wa kwanza hadi wa mwisho alikuwa akishika nafasi ya kwanza.
Vilevile, alichaguliwa kuendelea na elimu katika chuo kikuuu huko Huye. Hapo
alifanya maajabu zaidi! Mwishoni mwa masomo yake ilitangazwa nchini kote
kuwa ndiye aliyejinyakulia shahada yenye alama za juu katika Kitivo cha Uhasibu.
Miaka michache baadaye aliajiriwa kama meneja mkuu katika kampuni moja
ya kuagiza bidhaa kutoka nje za nchi. Ndizihiwe alionyesha ubingwa sana
katika kazi yake na kuongezewa mshahara wa kuridhisha. Aliwajengea wazaziwake nyumba ya kisasa na akawanunulia gari zuri la kutembelea. Leo wazazi
wake Ndizihiwe wanaishi kwa kheri na fanaka wakifurahia kuwasimulia hadithi
wajukuu wao wanne: Fany, Fils, Fiyette pamoja na Fisto. Katika masimulizi yao
hawakusahau kusisitiza kuwa “Akiba haiozi” pamoja na “Mtoto umleavyo ndivyo
akuavyo”.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi – o – kimehusishwa na majina ya ngeli za majina ya U- na PAM-
KU. Kimetumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-
• Mwishoni mwa kitenzi
a) Uzalendo ambao una maana ni ule kutoka nchi asili.
b) Ushirikiano unaotakiwa kati ya mume na mke ndio utakaoimarisha uchumi
wa nchi yetu.
c) Mahali paliposafishwa ndipo pazuri.
d) Chumbani mnamoingia ndimo mnamolala.
e) Nchini tunamoishi ndimo tutakamofanikiwa.f) Mezani ambako kumewekwa vitabu kumesafishwa.
MWELEKEO MUHIMU
UHAKIKI WA FANI
1. Wahusika na tabia zao
a) Wahusika wakuu
Ntawiheba pamoja na Bazubagira ndio wahusika wakuu katika hadithi fupi
“Kila Mtoto na Koja Lake.” Ntawiheba ni mume wa Bazubagira. Ametawaliwa na
tabia ya ufoili: mwanzoni alikuwa amevumilia hali ya familia yake hivi akisikilizana
na mkewe. Baadaye amebadilisha mawazo na kutaka kumwoa mwanamke wa
pili. Mwishoni amekubali kushawishiwa na mkewe na kutulia. Ni mwanamume
mwenye huruma, mapenzi na msanii pia. Ameonyesha sanaa yake wakati
alipomwiimbia mkewe wimbo wa mapenzi ili asiendelee kupoteza akili.
Bazubagira ni mkewe. Yeye ameongozwa na tabia ya ubapa: habadiliki kimawazo
na msimamo wake ni kumlea mtoto wao Ndizihiwe ingawa kimo chake kilikuwa
kinaonekana kama kasoro. Ni mwanamke mwenye huruma na mapenzi: anatimiza
ahadi la ndoa yake na mumewe.
b) Wahusika wadogowadogo au wasaidizi
Ndizihiwe ndiye mhusika msaidizi. Mtoto wa pekee wa bwana Ntawiheba na
mkewe Bazubagira, Ndizihiwe ametumiwa na mwandishi kuendeleza mtiririko
wa visa au matokeo. Iwapo kimo chake kinazusha dukuduku au fedheha katika
familia yake, Ndizihiwe ni mtoto mwenye akili. Amemudu masomo yake na
kupewa vyeo. Ni mtoto mwenye mawazo ya kimaendeleo na ya kijamii.
2. Mtindo
Mwandishi ametumia mtindo wa nathari, yaani aya. Lugha iliyotumiwa ni ya
kawaida, rahisi kueleweka. Baadhi ya vipengele vya lugha vilivyotumiwa na
msanii kuna tanakali za sauti tamathali za usemi, nahau, methali.
Tanakali za sauti
Mfano: Anguka pa !
Konsonansi (mbinu ya kusawazisha konsonanti mwanzoni mwa neno) - Fils,Fiyette pamoja na Fisto.
Tamathali za usemi
a) Tashihisi (mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai
(sifa za kibinadamu) - ni shetani yupi aliyekutembelea leo?
b) Tashibiha (mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa
kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’) - mfupi
mithili ya kinu.
i) Methali – Kila mtoto na koja lake; Akiba haiozi; Mtoto umleavyo ndivyo
akuavyo.
ii) Nahau – kufanya bidii, kupokea kwa shingo upande, kuonyesha jino,
kufunga ndoa, kufuta machozi, kujitoa mhanga, kupatwa na bumbwazi.
3. Muundo
Msanii ametumia muundo wa moja kwa moja, yaani hakufanya mazungumzo
yanayoweza kutatanisha msomaji. Mtiririko wa visa na matukio muhimu
umejitokeza kama ifuatavyo :
-- Asili ya jina la Rubyogo
-- Maisha ya familia ya Ntawiheba na mkewe Bazubagira
-- Elimu na mafanikio ya Ndizihiwe
-- Upeo: Hali ya kheri na furaha katika familia ya Ndizihiwe na wazazi wake.
4. Mandhari
Hadithi fupi imetokea katika kijiji cha Shengerero, jimbo la kusini nchini Rwanda.
UHAKIKI WA MAUDHUI
Dhamira kuu
a) Haki za Watoto
Mtoto yeyote anastahili kupewa haki zake zote za kimaisha hata akiwa na ulemavu.
Ingawa Ndizihiwe alikuwa na ulemavu wa kimo alijiamini katika masomo yake
pamoja na kazi zake na kufurahia baadaye matokeo mazuri.
b) Maadili Mema
Malezi bora kwa watoto huchangia kukuza akili na mienendo mizuri. Ndizihiwealipata manufaa kutokana na maadili aliyopewa na wazazi wake.
Dhamira Ndogo
-- Mapenzi ya ndoa
Ntawigira na mkewe wasingelikuwa na mapenzi ya ndoa hawangelisikilizana
baada ya Ntawigira kubadilisha mawazo yake ya kutaka kumwoa mke wa pili.
Wimbo wa mapenzi aliomwimbia Bazubagira na kumfanya apate nafuu.
-- Uwazi
Mume na mke wanapaswa kuwa wazi katika mawasiliano yao ya kila siku. Jambo
la Ntawiheba kutoboa siri la mpango wake kwa mkewe lilichangia kupata suluhu
la mzozo uliokuwa umezuka.
-- Ukewenza
Dai la Ntawiheba kwamba kumwoa mke wa pili kutakuwa suluhisho la matatizo
katika jamii yake lilibanwa na pingamizi ya sheria. Hivyo sheria katika Jamhuri ya
Rwanda haikubali utamaduni wa ukewenza.
-- Umuhimu wa elimu
Baadaya ya kuhitimu masomo ya uhasibu katika chuo kikuu, Ndizihwe alipata
kazi katika kampuni ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Alipewa mshahara wa
kuridhisha akawajengea wazazi wake nyumba ya kisasa na akawanunulia gari la
kutembelea
Migogoro
Hadithi fupi imeizingatia migogoro mbalimbali:
Mgogoro wa kijamii: Kimo cha Ndizihiwe kilileta hali ya manung’uniko na
fedheha katika jamii yake;
Hali ya maisha ilimfanya Ntawiheba akimbilie kwenye suluhu ya ukewenza.
Mgogoro wa kisheria na kidini : Ahadi ya ndoa serikalini na kanisani ilikuwa
kizuizi kwa uamuzi wa Ntawiheba kumwoa mke wa pili.
Mgogoro wa kielimu : Mafanikio katika familia nyingi hutokana na kiwango
cha elimu wanajamii walicho nacho. Mathalan, Ndizihiwe alifaidika katika maishayake kutokana na elimu yake.
Ujumbe
-- Watoto wote wanapaswa kuwa na haki sawa hata walemavu
-- Wazazi wana jukumu la kuwapatia watoto wao maadili
-- Elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii.
-- Mvumilivu hula mbivu.
Falsafa
Msimamo wa mwandishi na falsafa yake ni kwamba mtu yeyote, apende asipende,
huwa na nguvu kama sifa pamoja na udhaifu kama kasoro. Kwa hiyo, litakuwa
jambo la aibu kumnyima au kumnyanyasa mtu haki zake kwa kupitia vigezo vya
kimaumbile, kiafya, kikabila, kidini, kijamii, n.k. Hakuna mtu anayeweza kuthubutu
kudai kuwa huyu au yule atakuwa nini wakati ujao au atafaulu hiki na kushindwa
kile. Pengine, si vizuri kuzubaika mno kwa maisha uliyonayo leo kwa sababuhujui kitakochotokea kesho au kesho kutwa.
MAREJEO
Bakhressa,S.K. na Wenzake (2008). Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi.
Darasa la Saba. Oxford University Press, East Africa Ltd, Elgon Road, Upper
Hill, Nairobi, Kenya.
Bakhressa, S.K. na Wenzake (2008). Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi.
Darasa la 8. Oxford University Press, East Africa Ltd, Elgon Road, Upper Hill,
Nairobi, Kenya.
Hererimana, F. (2017). Tujivunie Lugha Yetu. Kitabu cha Mwanafunzi, Kidato
cha 5. MK Publishers (R) Ltd. Kigali, Rwanda.
Kenya Literature Bureau (2006). Kiswahili kwa Darasa la nane. Kitabu cha
Wanafunzi. Kenya Literature Bureau, Nairobi, Kenya.
Kihore, Y.M. na Wenzake (2012). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu, Sekondari
na Vyuo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Tanzania.
Massamba, D.P.B. na Wenzake (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu,
Sekondari na Vyuo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Tanzania.
Ndalu, A.E. (2016). Masomo ya Kiswahili Sanifu. Kitabu cha mwanafunzi.
Kidato cha 2. Moran (E.A) Publishers Limited.
Niyirora, E. & Ndayambaje, L. (2012). Kiswahili Sanifu kwa Shule za Sekondari.
Kitabu cha Mwanafunzi kidato cha tano, Tan Prints (India) Pvt. Ltd.
Nkwera, F.M.V (1979). Sarufi na Fasihi, Sekondari na Vyuo.Tanzania Publishing
House, Dar es Salaam,Tanzania.
Ntawiyanga, S. na Wenzake (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo
wa Lugha, Kidato cha 5. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
Ntawiyanga, S. na Wenzake (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo
wa Lugha, Kidato cha 6. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
Waititu, F. na Wenzake (2008). Kiswahili Fasaha. Kitabu cha Mwanafunzi.
Kidato cha tatu. Oxford University Press, East Africa Ltd, Nairobi, Kenya.TUKI (2004): Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la pili. Oxford University Press.