Topic outline
MADA YA 1 UFAHAMU NA UFUPISHO
Uwezo mahususi
Kufupisha matini zenye urefu wowote kulingana na kanuni zinazohusika.
Malengo ya ujifunzaji:
-- Kueleza mbinu za kufahamu kifungu cha habari fulani,
-- Kuonyesha dhamira kuu au kiini cha habari kinachozungumziwa,
-- Kupanga mawazo muhimu yaliyozungumziwa katika matini,
-- Kubainisha mbinu au taratibu za ufupisho,
-- Kubainisha sifa za ufupisho,
-- Kuonyesha umuhimu wa ufupisho,
-- Kufupisha matini mbalimbali za Kiswahili kulingana na taratibu au mbinu
za ufupisho,-- Kuambisha maneno ya Kiswahili.
SOMO LA 1: UFAHAMU
1.1. Kusoma na Ufahamu: Miti
Soma kifungu kifuatacho, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini
Miti ina faida nyingi. Si kwa binadamu tu bali hata kwa wanyama, ndege, wadudu
na viumbe wa baharini. Kuna miti inayotoa vyakula kwa watu na kwa wanyama.
Miti hiyo ni kama michungwa, mipapai, milimau, mipea, mikanju, miwa, fito na
kadhalika. Miti mingine hutupatia vifaa vya kukidhi mahitaji yetu. Vifaa hivyo ni
kama samani yaani meza, makabati, viti, madawati na vifaa vingine kama vinu,
michi, mipini ya majembe na mashoka, mivure na kadhalika. Miti hiyo ni kama
mivule, mikalitusi, misonobari na mikangazi. Baadhi ya miti hutupa dawa za
kutibu magonjwa mbalimbali.
Halikadhalika, miti hutupa mvua na kutuepusha na jangwa. Miti pia ni kuni na
makaa ya kupikia vyakula. Na miti hutumiwa kwa kujengea mapaa ya nyumba.
Vilevile, miti ni mapambo ya mazingira.
Kwa kuona faida na umuhimu wa miti, watu duniani walitenga siku maalum,
kila mwaka, ya kupanda miti. Nchi yetu nayo haikubaki nyuma kama mkia bali
nayo hushiriki kikamilifu katika shughuli ya upandaji wa miti. Mbali na siku hiyo
maalum, serikali yetu inahamasisha raia kupanda miti. Jambo hili, hufanyika katika
misaragambo au katika hafla mbalimbali. Kulingana na jambo hili Wanyarwanda
wana msemo usemao “Ukikata mmoja (mti), panda miwili.” Isitoshe, serikali ya
Rwanda ilitunga sheria za kuzuia uharibifu wa misitu. Uharibifu huu unahusiana
na ukataji wa miti kwa kutafuta kuni, kuchoma makaa na hata kuchoma misitu na
vichaka kwa utafutaji wa malisho ya mifugo. Ikumbukwe kuwa misitu ni makazi
ya ndege na wanyama wa porini. Misitu hii ikiharibika kutokana na ukataji wa miti
ndege na wanyama hawa watakosa vyakula na mahali pa kuishi.
Miti ikiendelea kukatwa ovyo bila ya kupanda mingine ama misitu ikiendela
kuharibiwa, mazingira yetu hayatakuwa safi. Nchi yetu Itakosa mvua na hata
dunia nzima itageuka jangwa. Ni wajibu wetu wa kulinda mazingira kwa kupanda
miti na kutoikata ovyo ili tusikumbane na madhara yatakayotokana na kuchafuka
kwa hali ya hewa. Sababu ni kwamba miti ina umuhimu mkubwa katika maishaya hapa duniani.
1.2. Msamiati kuhusu Kifungu
1.3. Sarufi: Uambishaji wa Maneno
Maelezo muhimu kuhusu uambishaji
Uambishaji ni mbinu ya kuzalisha maneno mapya kutoka maneno mengine. Mbinu
hii hufanyika kwa kuongeza kwenye sehemu fulani (viini, mizizi au mashina) za
maneno hayo viambishi mbalimbali mwanzoni au mwishoni. Mbinu hii huitwa
tena mnyambuliko. Katika sarufi ya lugha ya Kiswahili kuna :
-- Uambishaji wa vitenzi
-- Uambishaji wa nomino
-- Uambishaji wa vielezi
• Uambishaji wa vitenzi
Uambishaji wa vitenzi ni uundaji wa vitenzi vipya kutoka maneno mengine. Kuna :
-- Uambishaji wa vitenzi kutoka vitenzi vingine
-- Uambishaji wa vitenzi kutoka majina
-- Uambishaji wa vitenzi kutoka vivumishi-- Uambishaji wa vitenzi kutoka vielezi
i) Uambishi wa vitenzi kutoka vitenzi vingine
Uundaji huu wa vitenzi vipya hufanyika kwa kuongezea mzizi wa kitenzi viambishi
tamati vya kauli au vya hali. Ni kusema kuwa tunachukua kitenzi katika kauli yakutenda na kukitia katika kauli nyingine.
Mifano:
ii) Uambishaji wa vitenzi kutoka majina
Uundaji wa vitenzi kutoka majina hufanyika kwa kuongeza kwenye shina la jina
kiambishi awali ku- na viambishi tamati (viambishi vya kauli na viishio).Mifano:
iii) Uambishaji wa Vitenzi kutoka Vivumishi
Uundaji wa vitenzi kutoka vivumishi hufanyika kwa kuongezea shina la kivumishikiambishi awali ku- na viambishi tamati (vya kauli na viishio).
i) Uambishaji wa vitenzi kutoka vielezi
Uambishaji wa aina hii hufanyika kwa kuongeza kwenye kielezi au sehemu yakielezi kiambishi awali ku- na viambishi tamati (viambishi vya kauli na viishio).
1.4. Matumizi ya Lugha: Maelezo Muhimu kuhusu Ufahamu
Ufahamu ni neno ambalo linatokana na kitenzi “kufahamu.” Yaani kujua, kutambua
na kuelewa unachosoma au unachoambiwa. Ufahamu ni dhana inayolenga
kujua na kulielewa jambo kwa usahihi ili kuweza kulieleza upya bila kupotosha
maana yake ya awali. Ufahamu ni somo la kupata mbinu zote za kuelewa mambo
tunayosikia au tunayosoma.
Ufahamu unaweza kufanyika kwa kusikiliza yanayosemwa au kwa kusoma
yaliyoandikwa. Kwa hiyo, kuna aina kadhaa za ufahamu: ufahamu wa kusoma,
ufahamu wa kusikiliza, ufahamu wa kutazama na kusikiliza (runinga au filamu) na
ufahamu wa kutazama tu (picha za filamu au video ambazo hazina sauti).
Tunapozungumza au tunaposoma maandishi fulani ni lazima tuelewe na
kuelewana. Kuelewa mambo yanayosemwa na mtu mwingine ni hatua ya kwanza.
Hatua ya pili ni kuweza kupata ukweli wa yale yanayosemwa na kuyakubali au
kuyakana. Hatua ya tatu ni kujenga uhusiano na uelewano kati ya hao wawili
wanaozungumza.
Ili mtu aweze kufahamu anayoambiwa au anayoyasoma, au tunayoyatazama
kuna mbinu anazopaswa kutumia. Mbinu hizo ni hizi zifuatazo:
a) Kujua ujumbe wa maandiko mazima au mazungumzo. Hili hufanyika kwa
kusoma vizuri kwa kuzingatia matumizi ya alama za vituo. Katika mazungumzo
msikilizaji anapaswa kusikiliza vizuri kwa kuzingatia matamshi ya msemaji.
b) Kuelewa maana za maneno na misemo tofauti: msomaji au msikilizaji anatakiwa
kubaini maana ya maneno hayo ili kuelewa vema maana ya maneno aliyoyatumia
mwandishi au msimuliaji.
c) Kuchunguza mawazo makuu na yale madogo madogo katika maandiko
hayo au masimulizi hayo kwa kujenga ujumbe.
d) Kuelewa utanzu anaousoma au anaousikiliza: Anapokuwa na makini kuhusu
utanzu anaousoma au anaousikiliza, ndipo msomaji au msikilizaji anaelewa vizuri
jambo analolisoma au analolisikiliza.
Ufahamu una umuhimu mkubwa kwa kuwa ni fursa njema ya kupanua msamiati.
Kutokana na kuwa mwandishi au msemaji hutumia hasa maneno na misemo
mbalimbali ambayo hutuongezea ujuzi wa lugha.
Jibu maswali yafuatayo:
1. Ufahamu ni nini?
2. Kuna aina gani za ufahamu?
3. Ni hatua zipi zinazofuatiliwa katika kufahamu?
4. Taja mbinu za kutumia ili uweze kufahamu unayoyasoma au unayoyasikiliza.5. Ni nini umuhimu wa ufahamu?
SOMO LA 2: UFUPISHO
2.1. Kusoma na Ufahamu: Hotuba
Soma hotuba ifuatayo, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini.
Hotuba: Jifya Moja Haliinjiki Chungu
Mheshimiwa Mkurugenzi wa Masomo hapa shuleni,
Mheshimiwa Mkuu wa Nidhamu hapa shuleni,
Waheshimiwa Walimu,Na wanafunzi wote hamjambo?
Tumekutana sote hivi leo, viongozi, walimu na wanafunzi wa shule yetu
ya Mwangaza ili tuzungumze kwa kawaida yetu kuhusu mada ya “Ndi
Umunyarwanda.” Asubuhi hii ningependa tuzungumzie waziwazi juu ya umuhimu
wa ushirikiano baina yetu sote iwapo tunataka maendeleo mazuri ya shule yetu.
Wahenga walisema: “Ngozi ivute ingali mbichi”. Tupo mwanzoni mwa mwaka.
Ndiyo maana nimewaita hapa ili tuanze safari ya mwaka huu. Hii ni safari ndefu
na ngumu na msafiri ni aliye bandarini.
Madhumuni ya kuwataka viongozi, walimu na wanafunzi kushirikiana ni kwa
sababu matokeo mazuri yanategemea ushirikiano wetu sisi sote pamoja. Jifya
moja haliinjiki chungu. Kitu ambacho ningependa kusisitiza ni kwamba wanafunzi
wote ni sawa. Wawe wavulana, wawe wasichana. Hatuwezi kusema wanafunzi
wa aina fulani huzaliwa wajinga na wengine wa aina nyingine huzaliwa werevu.
Mungu hakupanga hivyo kwani hana moyo wa kupendelea jinsia hii wala kuonea
jinsia nyingine. Suala tunalokumbana nalo ni hili lifuatalo: «Kwa nini shule fulani
tu ndizo zenye matokeo na maendeleo mazuri kila kukicha? » Ukaona kuwa
wanafunzi wao hushinda vizuri, shule ina usafi na mengineyo. Jibu ni kwamba
wanafunzi wote wa shule hizo huungana pamoja wavulana kwa wasichana.
Mtanisamehe, leo, hakuna kufichana. Wahenga walisema “Mficha uchi hazai.”
Tuambiane ukweli ili tuweze kuyatatua matatizo tunayokumbana nayo. Katika
shule hii unaona kuwa wavulana wameanza kujenga makundi yao na wasichana
wakajenga yao. Ati hamwezi kusoma pamoja, msichana hawezi kuwa kiranja,
mvulana hawezi kupiga deki au kufagia na mambo mengine mengi ya utovu wa
nidhamu. Leo ninawahamasisha walimu kufuatilia karibu mambo hayo ili tuweze
kwenda pamoja. “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.” Kazi anayoweza
mvulana na msichana anaweza kuifanya au mvulana akafanya kazi zinazodhaniwa
kuwa za kisichana. Mshikamano huu ndio utakaotuwezesha kuwa Wanyarwanda
kindakindaki.
Kwa upande wa masomo wanafunzi nawakumbusha kwamba, “Mtaka cha
uvunguni sharti ainame.” Matokeo mazuri yatatokana na ustahamilivu, jitihada,
mshikamano na kujitolea. Na wenzenu kutoka shule nyingine ndivyo wafanyavyo.
“Ukiona vyaelea, vimeundwa.” Shule yetu ina vifaa vya kutosha na walimu wazuri.
Mimi nina imani kwenu na ninatumaini kwamba mtaweza kwa kuwa uwezo mnao
na nguvu mnazo. Kuanzia asubuhi hii tupate uamuzi mmoja wa kushikamana
sote vilivyo na sisi wenyewe tutavuna matunda yatakayotufurahisha. Na shule
yetu na hata nchi yetu zitazidi kusonga mbele.
Nawashukuru kwa kunisikiliza na ninadhani kuwa maneno yangu hayajapita sikiohadi sikio. Asanteni.
• Kulima ni kitenzi
• Mkulima, kilimo: nomino zinazotoka kwenye kitenzi kulima.
• Mtoto ni jina.
• Kitoto, toto, utoto: ni majina yanayotoka kwenye jina mtoto.
• Usafi: ni jina linalotoka kwenye kivumishi safi.
• Kitoto: ni kielezi kinachotoka kwenye jina mtoto.
Maelezo muhimu kuhusu uambishaji wa maneno
Katika somo la kwanza tulizungumzia kwa kina uambishaji kama mbinu ya
kuzalisha maneno mapya kutoka maneno mengine. Mbinu hii hufanyika kwa
kuongeza kwenye sehemu fulani (viini, mizizi au mashina) za maneno hayo
viambishi mbalimbali mwanzoni au mwishoni. Katika somo hilo tuliona uambishaji
wa vitenzi yaani uzalishaji wa vitenzi kutoka maneno mengine.
Katika somo hili tutaona:
-- Uambishaji wa majina-- Uambishaji wa vielezi
• Uambishaji wa majina
Uambishaji wa majina ni uundaji wa majina kutoka maneno mengine. Kuna:
-- Uambishaji wa majina kutoka majina mengine
-- Uambishaji wa majina kutoka vitenzi
-- Uambishaji wa majina kutoka vivumishi
-- Uambishaji wa majina kutoka vielezi
i) Uambishaji wa majina kutoka majina mengine
Uambishaji wa majina kutoka majina mengine hufanyika kwa kuweka katika hali/
dhana fulani. Hali/dhana hizo ni umoja, wingi, udogo, ukubwa na dhahania.
Kwa kawaida jina huundwa na sehemu mbili: kiambishi ngeli na shina. Kiambishi
ngeli ni mofimu inayoonyesha ngeli ya jina. Viambishi ngeli vya majina ni mu-
(vitu vyenye uhai), wa-, mu- (vitu visivyo na uhai), mi-,ji-/Ø-, ma-, ki-,
vi-, n-, n-, u-, u-, ku-, pa-, mu-, ku-.Mifano:
TANBIHI: Hakuna majina kwenye ngeli ya mu- na ku-. Kwa hiyo, katika lugha
ya Kiswahili tunapachika kiambishi –ni nyuma ya majina ya kawaida.
Mifano:
-- Mezani kuna usafi.
-- Chumbani mna usafi.
a) Hali ya umoja na wingi
• Katika umoja viambishi ngeli ni mu-, mu-, ji-/Ø-, ki-, n-, u-, u-, ku-,
pa-, mu-, ku-.• Katika wingi viambishi ngeli ni wa-, mi,-ma-, vi-, n-/Ø, ku-, pa-.
Mifano:
b) Hali ya udogo (Kudunisha)
Uundaji wa majina ya hali ya udogo hufanyika kwa kupachika viambishi ki- navi- mbele ya mashina ya majina ya kawaida.
TANBIHI:
• Majina yenye mashina ya silabi moja huchukua ji- nyuma ya
ki- na vi-.
Mifano:
Mtu: kijitu- vijitu
Mto: Kijito- vijito
• Mashina yanayoanzwa na irabu huchukua ji- nyuma ya ki- na
vi-.
Mifano:
Mwana: Kijana- vijana
Mume: kijiume- vijiume
• Majina ya ngeli ya Ki-/Vi- huchukua ji- nyuma ya ki- na vi-.
Mifano:
Kitabu: Kijitabu- vijitabu
Kiboko: kijiboko- vijiboko
c) Hali ya ukubwa (Kukuza)
Uundaji wa majina ya hali ya ukubwa hufanyika kwa kupachika viambishi ji-/Øna
ma- mbele ya mashina ya majina ya kawaida.
TANBIHI:
• Kwa majina yenye mashina ya silabi moja ji- hurudi katika
wingi.Mifano:
• Majina yenye silabi mbili au zaidi huchukua kiambishi Ømbeleya shina katika umoja na ma- katika wingi.
Mifano:
• Majina ya ngeli ya Li-/Ya- huchukua ji- katika umoja na wingi.
Mifano:
• Majina yenye mashina yanayoanzwa na irabu huchukua jikatikaumoja na ji- hii ikarudi katika wingi.
Mifano:
Tahadhari: Wanafuzi wawe makini na matumizi ya dhana za udogo au ukubwa
katika mawasiliano rasmi. Kwani ukubwa au udogo unaojitokeza hapa mara
nyingine huwa sio wa kupendeza.
d) Hali ya dhahania
Uundaji wa majina ya hali ya dhahania hufanyika kwa kupachika kiambishi umbele
ya mashina ya majina ya kawaida. Majina haya hayana wingiMifano:
ii) Uambishaji wa majina kutoka vitenzi
Uundaji wa majina kutoka vitenzi hufanyika kwa kupachika viambishi ngeli mbele
ya mizizi au mashina ya vitenzi na viishio nyuma ya mizizi au nyuma ya mashina.
Viishio vinavyotumiwa ni aji-, u-, e-, i-, o- na a-
Mifano:
-- Kufuga: mfugaji, ufugaji
-- Kutenda: tendo, utendaji
-- Kusoma: msomi, somo, msomaji
-- Kufa: kifo, mfu-- Kupinda: pindo, upinde
iii) Uambishaji wa majina kutoka vivumishi
Uundaji wa majina kutoka vivumishi hufanyika kwa kupachika viambishi ngelimbele ya mashina ya vivumishi.
Mifano:
-- safi: usafi
-- refu: mrefu, urefu
-- pana: upana
-- nene: unene, mnene-- zuri: uzuri
iv) Uambishaji wa majina kutoka vielezi
Uundaji wa majina kutoka vielezi hufanyika kwa kupachika viambishi ngeli mbele
ya vielezi.
Mifano:
-- Sawa: usawa-- Mbali: umbali
• Uambishaji wa vielezi
Uambishaji wa vielezi ni uzalishaji wa vielezi kutoka maneno mengine. Kuna:
-- Uambishaji wa vielezi kutoka majina
-- Uambishaji wa vielezi kutoka vivumishi.
i) Uambishaji wa vielezi kutoka majina
Uambishaji wa vielezi kutoka majina hufanyika kwa kupachika kiambishi ki- mbeleya shina la jina. Vielezi vinavyoundwa kwa namna hii ni vielezi vya namna.
Mifano:
ii) Uambishaji wa vielezi kutoka vivumishi
Uambishaji wa vielezi kutoka vivumishi hufanyika kwa kupachika viambishi ki- na
vi- mbele ya shina la kivumishi. Vielezi vinavyoundwa kwa namna hii ni vielezi vya
namna na vile vya kiasi.Mifano:
Maelezo muhimu: Maana ya ufupisho
Ufupisho ni taaluma ya kufanya muhtasari wa habari iliyoandikwa au iliyosimuliwa
bila kupotosha wazo au mawazo ya awali ya msemaji au mwandishi. Ufupisho ni
hali ya kufanya muhtasari au kupunguza urefu.
Ili mtu aweze kufanya ufupisho vizuri anapaswa kuzingatia taratibu zifuatazo:
-- Kusoma habari au kusikiliza habari husika zaidi ya mara moja ili kuweza
kuielewa.
-- Ni lazima kuzingatia mawazo makuu na kuyaandika.
-- Kuchagua au kuteua mambo muhimu au kiini cha habari huku tukijiepusha
na maelezo ya ziada, mifano, vielezi au tamathali za usemi.
-- Hakikisha kwamba maneno yote ya maana yaliyokusudiwa na makala au
habari ya awali yamebaki.
-- Hakikisha pia kwamba ufupisho wako una urari au mfuatano mzuri wa
mawazo.
-- Zingatia urefu wa muhtasari unaohitajika.
-- Kuandika kwa mtiririko mambo muhimu uliyoyateua.
-- Usiige lugha ya mwandishi au msimuliaji. Ni kusema kuwa unapaswa
kutumia maneno yako unapofanya ufupisho.
Ufupisho mzuri hauna budi kuwa na sifa zifuatazo:
-- Unapaswa kuwa na mawazo makuu yanayoeleweka.
-- Unapaswa kuwa si zaidi ya theluthi moja ya kifungu cha habari chote au
habari uliyosikia.
-- Lugha inayotumiwa ni lazima iwe lugha fasaha.
-- Unaweza kuwa katika aya moja au nyingi.
-- Unapaswa kumwezesha msikilizaji au msomaji kupanua msamiati.
Jibu maswali haya :
1. Unadhani ni kwa sababu gani ufupisho hutegemea sana mbinu za
ufahamu?2. Ni nini umuhimu wa ufupisho?
MADA YA 2 UTUNGAJI WA BARUA RASMI
• Malengo ya ujifunzaji:
-- Kueleza maana ya barua rasmi,
-- Kutaja sehemu kuu za barua rasmi,
-- Kubainisha mahali tofauti pa kutumia barua rasmi,
-- Kuonyesha umuhimu wa barua rasmi,-- Kutambua nafasi ya kiwakilishi rejeshi -po- katika kitenzi.
SOMO LA 3: MWONGOZO WA KUTUNGA BARUA
RASMI/KIKAZI3.1. Kusoma na Ufahamu: Baruaya Kuomba Kazi
Tovuti:Tovuti: www.gisagara.gov.rwBarua pepe: gisagaradistrict@minaloc.gov.rw
Ndugu,
KUH. OMBI LA KAZI YA KUFUNDISHA
Napenda kutuma ombi langu la kazi ambayo nimeitaja kwenye kichwa cha habari
cha hapo juu.
Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka kumi na nane. Nimemaliza masomo yangu
mwaka 2019 katika chuo cha Ualimu cha Save na kupewa cheti cha ualimu wa
ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari.
Barua pepe: gisagaradistrict@minaloc.gov.rw
Ndugu,
KUH. OMBI LA KAZI YA KUFUNDISHA
Napenda kutuma ombi langu la kazi ambayo nimeitaja kwenye kichwa cha habari
cha hapo juu.
Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka kumi na nane. Nimemaliza masomo yangu
mwaka 2019 katika chuo cha Ualimu cha Save na kupewa cheti cha ualimu wa
ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika shule za sekondari.
Natuma ombi langu la kazi ya kufundisha kwako ili niwe mmoja kati ya wale
watakaofikiriwa kupewa kazi ya kufundisha katika Wilaya ya Gisagara.
Nyaraka zote zinazohitajika nimeziambatisha kwenye barua hii kama viambatisho.
Ni matumaini yangu kuwa ombi langu litakubaliwa.
Wako mtiifu,
UwamwizaUWAMWIZA Zawadi
Maelezo muhimu kuhusu matumizi ya kiambishi –po-
Kiambishi rejeshi –po- kinaweza kutumiwa kwa njia mbili. Njia ya kwanza –poinarejelea
mahali. Kwa njia ya pili –po- huonyesha wakati.
• Matumizi ya –po- ya mahali
Kiambishi -po- kikisimamia mahali kinakuwa –o rejeshi iliyotumiwa katika ngeli
ya PA-M-KU. Kinapotumiwa ndani ya kitenzi kinasimamia maneno “mahali
ambapo.” Ni kusema kuwa –po- hii inapatikana tunapoondoa “amba” katika
sentensi.
Mifano:
-- Mahali ambapo anaishi ni pazuri: Mahali anapoishi ni pazuri.
-- Pale (Mahali) ambapo palijengwa panatisha: Pale palipojengwa
panatisha.
-- Mahali ambapo tutapanda miti ile ni pale milimani: Mahali tutakapopanda
miti ile ni pale milimani.
• Matumizi ya –po- ya wakati
Kiambishi –po- kikionyesha wakati hutumiwa kwa kuonyesha tendo hutendeka,
lilitendeka au litatendeka na kufuatwa na jingine.
Mifano:
-- Mvua iliponyesha tulikimbia.
-- Mvua nyingi inaponyesha watu wengi huogopa.
Tanbihi:
• Katika wakati ujao kiambishi –po- huenda pamoja na kiambishi –ka-.
Mifano:
-- Atakapofika tutampokea vizuri.
-- Nitakapopewa kazi ya kufundisha nitafundisha ipasavyo.
• Kuna kiambisi –po- kinachotumiwa pamoja na –si- tukikanusha vitenzi
vyenye kiambishi ki- na –takapo-.Mifano:
i) Maana ya Barua
Barua au waraka ni maandishi yaliyopangwa kwa utaratibu na mtiririko maalum
kwa minajili ya kuwasilisha ujumbe fulani. Barua ni risala au mjumbe mwepesi
anayemwakilisha mtungaji wake kwa mtu mwingine na kuwasilisha taarifa yake
kwa mtu huyo.
Barua huandikwa kwa madhumuni mbalimbali kama kuarifu, kuomba kitu kama
vile kazi, ruhusa; kuagiza bidhaa, n.k.
ii) Aina za barua
-- Barua za kirafiki: ni zile ambazo huandikiwa na mtu au watumbalimbali
walio na uhusiano wa karibu na anayeandika; k.v. rafiki, mzami, ndugu, n.k.
-- Barua za mwaliko zenye lengo la kumwalika mtu katika sherehe au
sikukuu fulani
-- Barua rasmi/ za kikazi zenye madhumuni ya kazi. Kwa kawaida
barua rasmi huandikwa kwa makusudi mbalimbali kama vile, kutoa
taarifa za tukio fulani, kuomba kazi, kuagiza vifaa au vitu, kumwalika
kiongozi katika shughuli maalumu, kutoa taarifa ya kushindwa kufika
mkutanoni na kadhalika. Barua hizi zina utaratibu wa kuziandika.
iii) Sehemu za barua rasmi
Sehemu za baruwa rasmi zinakaribia kufanana na zile za barua ya kirafiki lakini
kuna tofauti kidogo. Ifuatayo ni mifano wa mipangilio ya barua za kuomba kazi.*Barua ya kuomba kazi kwa mara ya kwanza
iv) Maelezo
1. Anwani ya ya mwandishi na tarehe
Anwani hii huandikwa upande wa juu mkono wa kulia wa barua na chini yake
kunawekwa tarehe.
2. Anwani ya mwandikiwa
Anwani hii inaandikwa upande wa kushoto wa karatasi chini kidogo ya anwani
ya mwandishi. Katika sehemu hii jina la mwandikiwa haliandikwi isipokuwa cheo
chake; hata ikiwa mnazoeana kwa kiasi fulani ni lazima kuandika cheo chake.
3. Kichwa cha habari
Hili ni kusudi la barua. Kichwa cha habari huwa chini ya anwani ya mwandikiwa.
Kichwa hicho huandikwa kwa herufi kubwa na kupigiwa mstari chini.
4. Ujumbe wa barua
Ujumbe wa barua huandikwa chini ya kichwa cha barua. Katika barua za kikazi
ni mambo muhimu yanayoandikwa tu. Ujumbe huu unatanguliwa na sentensi
inayorejerea kwenye kichwa cha habari.
Tanbihi:
-- Uandishi wa barua za kikazi unahitaji uangalifu sana na lugha iliyo wazi kwa
sababu kama kuna matatizo barua hiyo huwa ni shahidi wako na inaweza
kukuokoa au kukuponza.
-- Hakuna sehemu ya salamu kwa mwandikiwa katika barua hizi. Mambo
hayo ya salamu ni ya barua za kirafiki.
5. Hitimisho la barua
Hitimisho/Mwisho wa barua huwa ni tamko la heshima la kumalizia barua. Mara
nyingi mwisho unaotumika katika barua rasmi ni kama vile :
-- Wako mtiifu,
-- Wako mwaminifu,
-- Wako katika ujenzi wa taifa,
-- Wako katika kazi,
-- Na kadhalika.
6. Sahihi na jina la mwandikaji
Jina la mwandishi huandikwa likifuata sahihi yake. Jina huwekwa chini ya sahihisi juu yake.
TANBIHI:
Kama barua rasmi inatoka ofisi ikienda nje au inatoka nje ikingia ofisini, kuwa
sehemu nyingine zinazoweza kuonekana kwenye barua hiyo. Sehemu hizo ni
kama kumbukumbu namba, kupitia kwa na nakala.
1. Kumbukumbu namba
Kumbukumbu namba zinaandikwa mara nyingi kwenye upande wa kushoto wa
karatasi. Kumbukumbu hii husaidia kurahisisha kutafuta barua katika majalada.
Kwa hiyo ni muhimu kutaja kumbukumbu namba ya barua unapojibu na kuandika
barua iliyo na uhusiano nayo. Zaidi ya kumbukumbu namba, barua nyingine
zinakuwa na namba ya simu chini yake.
2. Kupitishwa kwa (kwa kifupi: KK)
Kuna wakati mwandishi wa barua hupitisha barua yake kwa kiongozi mwingine
kabla ya kuifikisha kwa mwandikiwa. Inapojitokeza haja hiyo, huandika KK
chini kidogo ya anwani ya mwandikiwa na chini yake cheo cha huyo kiongozi,
ukitarajia kwamba atatia saini yake kuhakikisha kwamba amekuwa wa kwanza
kujua maombi yako.
Kwa mfano, iwapo mwandishi wa barua ameajiriwa na anaandika barua binafsi
kwa mkuu mwingine wa kazi ili kuomba kazi, kuuliza mambo ya kikazi na kadhalika,
inambidi apitishe barua hiyo kwa mkuu wake wa kazi mahali anapofanyia kazi.
3. Nakala mbalimbali
-- Iwapo kuna watu zaidi ya yule unayempelekea barua ambao unataka
wapashwe habari ya jambo uliloandika, basi ni lazima kuwatumia nakala
ya barua hiyo unayoandika. Jambo hilo pia litamjulisha mwandikiwa kuwa
barua hiyo inasambazwa kwa watu wengi.
-- Orodha ya watu wanaopelekewa nakala ya barua huonyeshwa upande wa
kushoto wa karatasi. Kichwa cha nakala hulingana na sahihi ya mwandikaji.
Jibu maswali yafuatayo:
1. Barua rasmi huandikwa kwa minajili ipi ?
2. Barua rasmi hutofautiana vipi na barua ya kirafiki ?3. Taja sehemu muhimu ziundazo barua rasmi
KUH: KUOMBA RUHUSA YA KUPUMZIKA
Kichwa cha habari cha hapo juu chahusika. Ninaandika barua hii ili kuomba
ruhusa ya kukosa kuhudhuria masomo yote ya leo.
Jana sikuweza kuja chuoni kwa sababu niliamka nikijihisi mgonjwa. Mama
alinipeleka hospitalini ambapo nilipata matibabu. Walipopata vipimo waligundua
kuwa ninaugua malaria. Nilipata dawa lakini bado sijapata nafuu. Ninaomba
uniruhusu siku tatu nimalize dawa kisha nikipata nafuu nitarejea shuleni.Samahani sana kwa kutosema hili mapema.
Ninaambatisha na ripoti ya daktari.
Ninatumai ombi langu litakubaliwa.
Asante.
Wako mwaminifu,
marymMary Mutoni
Barua rasmi zipo za aina nyingi, lakini zote zinapatikana kulingana na minajili
yake. Barua hizo zinaweza kuwa:
-- Barua ya kuomba kazi
-- Barua ya kutoa taarifa
-- Barua ya kuomba ruhusa
-- Barua ya huduma
-- Barua ya kuomba nafasi katika shule fulani
-- Barua ya kuomba msamaha
-- Barua ya shukrani
-- Barua ya malalamiko
-- Barua kwa mhariri
-- Barua ya mapendekezo
-- Barua ya uteuzi
-- Barua za kuagiza au kupokea bidhaa/vitu
-- Barua ya kusimamisha kazi-- Barua ya kusimamishwa au kufutwa kazi
YAH: NAFASI YA MASOMO
Kichwa cha habari cha hapo juu chahusika. Ninakuandikia barua hii kuomba
nafasi ya kujiunga na Chuo kikuu cha Rwanda chenye sifa na umaarufu mwaka
wa masomo ujao.
Kwa mintarafu ya masomo yangu, mimi nilisoma katika Chuo cha Ualimu cha
Byumba, wilayani Gicumbi. Nilimaliza masomo yangu mwaka jana na nikafaulu
vizuri sababu kiasi kwamba nilipewa zawadi na serikali ya kuchagua chuo
chochote kile nipendacho ili niendeleze masomo yangu.
Ni matumaini yangu kwamba utanipa fursa ya kusajiliwa ili nithibitishe uwezo na
ukakamavu wangu.
Vitambulisho vyangu pamoja na matokeo ya mtihani wa taifa utayasoma kwenye
stashahada yangu iliyoambatishwa kwenye barua hii.
Asante sana !
Wako mwaminifu,
karemjon
KAREMERA Joni
Nakala:
-- Waziri wa Elimu
-- Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Elimu
Jibu maswali yafuatayo:
1. Ni madhumuni gani yanayoweza kumfanya mtu aandike barua rasmi.
2. Ni nini tofauti, katika mpangilio, iliyoko baina ya barua ya kuomba ruhusana barua ya kuomba nafasi ya masomo.
4.5. Kusikiliza na Kuzungumza
MADA YA 3 UTUNGAJI WA INSHA
• Malengo ya Ujifunzaji
-- Kueleza maana ya insha na aina zake,
-- Kubainisha mbinu au taratibu za kutunga insha,
-- Kutaja aina za insha,
-- Kubainisha sifa za insha ya masimulizi na ya kubuni,
-- Kuchunguza sifa za sehemu kuu za insha,
-- Kupanga mawazo kwa mfuatano mzuri,
-- Kutumia kwa ufasaha alama za vituo kulingana na kanuni za matumizi kwa
kila alama,
-- Kutunga aina mbalimbali za insha,
-- Kutoa maana ya mnyambuliko na mnyumbuliko,
-- Kueleza tofauti iliyopo kati ya mnyambuliko na mnyumbuliko wa maneno,-- Kunyambua na kunyumbua maneno ya Kiswahili.
SOMO LA 5: MAANA YA INSHA
5.1. Kusoma na Ufahamu: Asiyesikia la Mkuu Huvunjika
Guu
Soma kifungu kifuatacho, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini
Kanuma ni kijana ambaye alikuwa na tabia ya uvivu hasahasa darasani. Kila wakati
mwalimu alikuwa akimuadhibu kwa vuruguvurugu na kuwa na tabia ya kusinzia
darasani. Isitoshe, Kanuma hakuandika maandishi darasani na kila mwalimu
alipokuwa akiacha kazi za nyumbani za kufanya alikuta Kanuma hajaanza wala
kuandika maswali. Wakati wa mitihani na majaribio, Kanuma alikuwa na tabia
ya kunakili na kumuuliza aliyekuwa akikaa karibu naye. Mara nyingine alikuwa
akileta vikaratasi alivyotumia kwa kuandika majibu na alikuwa akivificha dawatini
ili vimsaidie kunakili.
Wazazi wake walijaribu kumfunza tabia ya kuwa na bidii kwani siku zote bidii
huzaa matunda. Walipenda kumuonya ili aweze kuweka njia za kuepukana na
tabia hizo mbaya za kotopenda kufanya kazi lakini yeye hakusikia. Wazazi wake
walijaribu kushirikiana na walimu wake kumfanya awe mtu mwenye kujitegemea
katika siku za baadaye kwa kumpa mfano wa ndugu yake mdogo aliyempita na
ambaye alikuwa chuoni wakati huo. Kilichokuwa kinaaibisha ni kuwa Kanuma
alikuwa angali katika kidato cha pili shule za sekondari kwa miaka yake kumi nasita.
Kanuma aliendelea na tabia zake mbaya na kutia pamba masikioni kwa kukataa
mashauri ya wazazi wake. Wakati wa kufanya mtihani wa taifa alitaka kunakili.
Alipokamatwa na walimu, polisi waliitwa na hivyo akakamatwa na kupelekwa
katika kituo cha kurekebisha maadili. Walimu na wanafunzi wenzake walipomuona
na kukumbuka maonyo aliyopewa kutoka kwa wazazi wake na hata kwa walimu;
walisema kuwa, “asiyesikia la mkuu huvunjika guu.”
Kanuma alipofika katika kituo cha kurekebishia maadili alikutana na vijana wengine
waliofanya makosa mengi kama ubakaji, uvutaji wa bangi, utumiaji wa dawa za
kulevya, wizi, mauaji na kadhalika. Hapo alipolinganisha kosa lake na makosa ya
wenzake, alianza kujutia matendo aliyoyafanya. Kituoni alikutana na rafiki mmoja
aliyeitwa Kimasa. Kila siku Kimasa alikuwa akimsimulia namna ambavyo alitiwa
nguvuni kwa kosa la ubakaji. Wakati wote, Kimasa alikuwa akimwambia kuwa
alionewa. Siku moja Kimasa alitaka kumlawiti Kanuma lakini Kanuma akakataa
kwa sababu alikumbuka kuwa tendo hilo ni tendo la aibu. Alipowazia makosa ya
Kimasa, alikumbuka kwamba mwalimu wake alimfundisha kwamba ulawiti ni njia
nyofu ya kuambukizana magonjwa ya zinaa hasa UKIMWI. Hapo aliona kwamba
ilikuwa lazima atengane na Kimasa.
Mbali na kurekebishwa kimaadili, Kanuma alifundishwa mambo mengi sana
kituoni. Kwanza alifundishwa kucharaza gitaa akageuka mwimbaji hodari. Na
wakati wa usiku yeye pamoja na vijana wenzake walikuwa wakiwaliwaza wenzao
kwa nyimbo.
Alipotoka kituoni aliwakuta wanafunzi wenzake wakiwa na kazi nzuri; wengine
walikuwa katika vyuo vikuu, akajuta. Wakati huu, mdogo wake alikuwa daktari.
Mtegemea cha nduguye hufa maskini. Kanuma aliona kuwa ilikuwa lazima
ajitegemee ili asije akawa mzigo kwa mdogo wake. Ndipo alianza kazi ya kuimba
vilabuni, hotelini, harusini na katika hafla nyingine. Kuanzia wakati huo pesa
zilianza kumiminika, akaajiri waimbaji wengine wakaunda bendi kubwa iliyovuma
nchini mwao na kuvuka mipaka. Nyimbo nyingi za bendi hii zilikuwa zikiwahimiza
vijana kuwa na mienendo mizuri. Bendi hii inasifika sana kwa kuwa imeundwa navijana chipukizi waliokuwa na mienendo mibaya hapo kabla.
• Alama zilizopigiwa mstari chini huitwa alama za vituo au alama za
uakifishaji.
Maelezo muhimu kuhusu matumizi ya alama za vituo/ uakifishaji
Binadamu wanapozungumza, tunaweza kutambua jinsi wanavyopandisha
sauti au kuishusha kwa ajili ya kutoa ujumbe fulani (kuuliza, kushangaa,
kushtuka, n.k). Vilevile, wanapomaliza usemi wao mtu huweza kutambua
kuwa usemi umefikia kikomo kwa kusikia sauti zao tu. Lakini katika
uandishi, hakuna sauti. Badala ya sauti, zipo alama za vituo ambazo hutumiwa
kuwakilisha sauti katika uandishi. Kutokana na alama hizo, tunatambua kama
usemi umekwisha, kuulizwa swali, kushangaa na kadhalika. Pia, tunaposoma,
tunajua wapi tunafaa kupumua kidogo, kushusha au kupandisha sauti na
kadhalika.
Alama hizi huitwa p i a viakifishi. Hivyo basi, viakifishi ni alama zinazotumiwa
katika maandishi ili kuleta maana ikusudiwayo katika matini mbalimbali
kama vile sentensi, aya, mtungo, barua, mialiko, matangazo, ilani na kadhalika.
Mifano zaidi ya alama za vituo au viakifishi
1. Nukta (.)
i) Huwekwa mwishoni mwa sentensi.
Mifano:
-- Amechoka.
-- Rais wetu hapendi wachokozi.
ii) Hutumiwa kuonyesha ufupisho wa maneno.
Mfano:
-- S.L.P. ( Sanduku la Posta )
iii) Hutumika kubainisha saa na dakika au tarehe.
Mifano:
-- 9.20: saa tisa na dakika ishirini
-- 14.11.2019: tarehe kumi na nne, Novemba, mwaka wa elfu mbili na kumi
na tisa.
2. Kistari kifupi (-)
i) Hutumiwa kuonyesha kuwa neno linakatwa kwa vile limefika ukingoni mwa
mstari husika na bado linaendelea katika mstari unaofuatia.
ii) Hutumiwa kuunga maneno yanayojenga neno moja. Mtindo huu aghalabu
hujitokeza katika maneno yenye asili ya kigeni.
Mfano:
-- Idd-el-Fitri
-- Dar-es-Salaam
iv) Huweza kutumiwa badala ya koma.
Mfano: Nyimbo za asili-hasa Rumba-zinapendwa na wengi.
v) Hutumiwa kutenga silabi au mofimu zinazojenga neno.
Mifano:
u-ku-li-ma
ha-zi-na
ku-end-a
ku-li-a
Hutumiwa pamoja na nukta mbili kabla ya orodha.
Mfano:Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi hizi:
-- Rwanda
-- Tanzania
-- Uganda
-- Kenya-- Burundi
3. Kistari kirefu(—)
i) Hutumiwa wakati panapotokea badiliko la ghafla katika sentensi. Hapo
kinachukua nafasi ya mkato au mabano.
Mfano: Wewe—nina hakika—hutaki kutusaidia.
i) Hutumiwa baada ya orodha tangulizi / kauli tangulizi, labda kuifafanua zaidi.
Mfano: Kiingereza, Historia, Kinyarwanda—haya ndiyo masomo yanayowavutia
wengi—hayamo katika ratiba.
ii) Hutumiwa kabla ya maneno ambayo ni msisitizo wa dhana iliyotajwa.
Mfano: Uharibifu wa mazingira—mnaona jinsi ulivyozidi—unatia wasiwasi.
iii) Hutumiwa kuonyesha kauli isiyomalizika au kukatizwa kwa kauli.
Mfano: Kalisa alisema, “nita —”
iv) Hutumiwa badala ya neno mpaka au hadi.
Mifano: Hesabu kutoka 20—50.
Alianzia hapa—pale.
4. Alama ya mshangao (!)
i) Hutumiwa kuashiria mahangaiko ya moyo kama vile hasira, hofu,
mshangao na kadhalika.
Mifano:
-- Lo! Mwanafunzi ameangusha kitabu cha mwalimu matopeni!
-- Wamefungwa mabao kumi kwa nunge!
5. Alama ya kuulizia/kiulizi (?)
i) Hutumiwa mwishoni mwa sentensi kuonyesha kuwa sentensi hiyo ni swali.
Mfano: Unaitwa nani?
ii) Hutumiwa kuonyesha ukosefu wa uhakika kuhusu jambo kama vile mwaka.
Mfano: Shule hii ya Kigali ilianzishwa 1992?
6. Mabano/parandesi
i) Hutumiwa kufunga maneno ya ziada katika sentensi.
Mfano: Nyamata (makao makuu ya Bugesera) inakua kwa kasi.
ii) Hutumiwa na mwandishi anapotaka kutoa ufafanuzi kwa lugha nyinginetofauti na ile anayoitumia.
3. Kistari kirefu(—)
i) Hutumiwa wakati panapotokea badiliko la ghafla katika sentensi. Hapo
kinachukua nafasi ya mkato au mabano.
Mfano: Wewe—nina hakika—hutaki kutusaidia.
i) Hutumiwa baada ya orodha tangulizi / kauli tangulizi, labda kuifafanua zaidi.
Mfano: Kiingereza, Historia, Kinyarwanda—haya ndiyo masomo yanayowavutia
wengi—hayamo katika ratiba.
ii) Hutumiwa kabla ya maneno ambayo ni msisitizo wa dhana iliyotajwa.
Mfano: Uharibifu wa mazingira—mnaona jinsi ulivyozidi—unatia wasiwasi.
iii) Hutumiwa kuonyesha kauli isiyomalizika au kukatizwa kwa kauli.
Mfano: Kalisa alisema, “nita —”
iv) Hutumiwa badala ya neno mpaka au hadi.
Mifano: Hesabu kutoka 20—50.
Alianzia hapa—pale.
4. Alama ya mshangao (!)
i) Hutumiwa kuashiria mahangaiko ya moyo kama vile hasira, hofu,
mshangao na kadhalika.
Mifano:
-- Lo! Mwanafunzi ameangusha kitabu cha mwalimu matopeni!
-- Wamefungwa mabao kumi kwa nunge!
5. Alama ya kuulizia/kiulizi (?)
i) Hutumiwa mwishoni mwa sentensi kuonyesha kuwa sentensi hiyo ni swali.
Mfano: Unaitwa nani?
ii) Hutumiwa kuonyesha ukosefu wa uhakika kuhusu jambo kama vile mwaka.
Mfano: Shule hii ya Kigali ilianzishwa 1992?
6. Mabano/parandesi
i) Hutumiwa kufunga maneno ya ziada katika sentensi.
Mfano: Nyamata (makao makuu ya Bugesera) inakua kwa kasi.
ii) Hutumiwa na mwandishi anapotaka kutoa ufafanuzi kwa lugha nyingine
tofauti na ile anayoitumia.
Mfano: Wandishi (editors) waalikwa.
iii) Hutumiwa kufungia herufi za kuorodhesha.
Mifano:
(a) huelimisha, (b) huburudisha, (c) huonya.
7. Mkwaju (/)
i) Hutumiwa kwa kuandika kumbukumbu namba za barua.
Mifano: Kumb. Na 002/001/0012/KGL/002
Kumb. Na 112/012/0099/NY/012
Hutumiwa kwa kuandika tarehe.
Mfano: Leo ni terehe 12/07/2019
Hutumiwa badala ya neno « au », « ama ».
Mifano: Mbweha/mbwamwitu ni mkali sana.
Beberu / mbuzi dume yule ni mkongwe.
Hutumiwa kwa kuandika akisami.
Mifano:
2/3
3/4
4/9
8. Mtajo: (“ ” au ‘ ’)
i) Hutumiwa kuonyesha maneno halisi ya mzungumzaji.
Kwa mfano: “Nitafika kesho jioni,” alisema mdogo wake.
ii) Hutumiwa kwa kuonyesha maneno yaliyonukuliwa katika kitabu au
maandishi mengine.
Mfano: Kama Kamusi ya Kiswahili Sanifu inasema, “boi ni mwanamume
aliyeajiriwa kufanya kazi za nyumbani” (Uk30).
i) Hutumiwa kwa kurejerea anwani za makala mbalimbali katika maelezo.
Mfano: Kitabu cha “Darubini ya Sarufi” ni kizuri sana.
ii) Hutumia kuonyesha neno geni katika lugha au lenye maana au kazi maalum.
Mifano: Mimi sipendi “matoke”.
Tulikwenda mjini tukaona ma “lorries”mengi.
iii) Hutumiwa kuandika jina la gazeti.
Mfano: Mnapaswa kusoma « Imvaho Nshya » ili mjue habari za ulimwengu.
9. Mkato
i) Hutumika kwa kutenganisha sehemu mbili za tungo
Mfano: Mtoto anasoma Kiswahili, wazazi wanamtafutia karo.
ii) Hutumika kwa kutenganisha maneno yanayofuatana.
Mfano: Wao hufuga kuku, mbuzi, kondoo na ng’ombe.
10. Ritifaa (’)
i) Hutumiwa kwa kuonyesha sauti/ herufi fulani imeachwa.
Mifano:
’likukanya (nilikukanya)
’kawa (ukawa)
’siniudhi (usiniudhi)
’19 (2019)
ii) Hutumiwa kwa kuonyesha sauti za ving’ong’o.
Mifano:
Ng’ombe
kung’aa
Kung’oa
11. Nukta za dukuduku (…)
Hutumiwa:
i) Badala ya neno na kadhalika.
Mifano: Alinunua viazi vitamu, nyama, nyanya, …
ii) Kuonyesha mambo yasiyotajika katika sentensi.
Mfano: Niliamshwa alfajiri na mapema…
iii) Kuonyesha kukatizwa kwa kauli/ usemi.
Mfano: La …ki …kini una …unani … ni …penda.
• Maana ya utungaji wa insha
Utungaji ni neno linalotokana na kitenzi “kutunga”. Kitenzi hiki kinamaanisha
“kutoa mawazo kutoka ubongoni na kuyakusanya, kisha kuyadhihirisha kwa
maandishi, kwa kusimulia, kwa kuyaimba au kwa muziki. Kwa hiyo tunaweza
kusema kuwa, utungaji ni utoaji wa mawazo binafsi kutoka akilini mwa mtu
kuhusiana na mambo mbalimbali katika jamii, kisha kuyaweka wazi kwa njia ya
mdomo au maandishi. Insha ni mtungo wa maneno kwa mtindo wa nathari juuya jambo fulani.
• Sehemu za insha
Insha huwa na sehemu kuu tatu ambazo ni:
• Utangulizi (Mwanzo)
Katika sehemu hii inampasa mwandishi atoe maelezo mafupi na maana ya habari
aliyopewa.
• Kiini cha insha (Kati/insha yenyewe)
Sehemu hii ni insha yenyewe. Katika sehemu hii inamlazimu mwandishi afafanue
kwa mapana mada anayoishughulikia huku akitoa mifano hai inayoendana na
hali halisi. Kwa kawaida, sehemu hii hueleza kwa ukamilifu kila hoja iliyodokezwa
katika utangulizi.
• Hitimisho (Mwisho)
Hii ni sehemu ya mwisho. Katika sehemu hii inampasa mwandishi kutoa
mapendekezo (maoni) ya msingi au kusisitiza kwa ufupi yale aliyoyaelezea katika
habari yenyewe. Mwisho wa insha huonyesha uhusiano uliopo kati ya utangulizi
na maelezo yaliyomo katika mwili.
• Taratibu za kutunga insha
Kwa kuweza kutunga insha vilivyo, huna budi kufuata taratibu zifuatazo:
-- Kusoma kwa makini mada/kichwa/anwani uliyopewa zaidi ya mara moja, ili
uielewe vizuri.
-- Kufikiria mada/kichwa/anwani kwa muda.
-- Kuandika mambo muhimu yatakayokuongoza katika kuiandika insha.
-- Maelezo yote yatolewe kwa undani na kwa njia ya kuvutia.
-- Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.
-- Kutumia msamiati mwafaka wa kutosha kwa kutegemea mada
(kutorudiarudia maneno).
-- Kutumia sentensi fupi.
-- Kutumia vizuri alama za uakifishaji.
-- Kutumia lugha safi na yenye adabu.
-- Kuandika methali, misemo na nahau ambazo unadhania zinaweza kukufaa
katika utungaji.
• Aina za insha
Insha ni za aina nyingi kulingana na namna zilivyoandikwa au kulingana na kusudi
lake. Katika utungaji wa insha kuna insha za wasifu, insha za picha, insha za
mdokezo, insha za maelezo, insha za masimulizi, insha za methali, insha za hoja
na insha za kubuni.
Jibu maswali haya
1. Kwa maoni yako nini maana ya insha ?
2. Kwa sababu gani katika utungaji wa insha ni lazima kuheshimu sehemu
za insha ?
3. Andika sifa kuu tano za insha.
6.1. Kusoma na Ufahamu: Mafanikio ya Kudumu
Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini
Masengesho ni, kijana aliyezaliwa mwanapekee katika familia yake. Hakubahatika
kulelewa na wazazi wake kwani walifariki angali mdogo kutokana na ugonjwa wa
UKIMWI. Baada ya wazazi wake kufariki, alichukuliwa na kulelewa na shangazi
yake. Wakati huo, alikuwa katika shule za sekondari. Alipomaliza masomo yake
katika shule za sekondari, alipata cheti cha kuhitimu masomo hayo akiwa na
alama nzuri. Jambo hili liliwafurahisha watu wengi wakiwemo walimu na majirani
zake. Ndiyo maana ilikuwa tafrija ya kijiji kizima. Hii ni siku tuliposherehekea
kupata tuzo kwa kijana hodari ambaye aliyamudu maisha yake kiasi cha kuigwa
na vijana wengine.
Wengi waliompongeza siku hiyo walimletea zawadi nyingi. Alikuwa mwanafunzi
mwenye bidii tangu shule ya chekechea hadi kiwango alichofikia. Muda mfupi
baadaye, alijiunga na vijana wenzake kufuata masomo ya muda mfupi yaliyokuwayakitolewa kijijini hapo.
Masomo hayo yaliwalenga vijana wote waliokuwa wamemaliza masomo yao ya
shule za sekondari na yalilenga kuwawezesha kuandaa miradi midogo midogo
ya kujiendeleza na jinsi ya kuifanikisha. Masomo hayo yaliwafurahisha vijana
wengi na Masengesho aliyasoma kwa makini; jambo lililokuwa desturi yake.
Masengesho alikuwa msichana mwenye mawazo na mtazamo imara wa maisha
kiasi kwamba watu walishangaa kutokana na tabia na mienendo yake. Mafunzo
yalifanyika kwa muda wa mwaka mzima akapewa cheti katika fani ya maandalizi
na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo. Mwezi mmoja uliofuata, Taasisi ya
Maendeleo ya Rwanda ilihitaji kuajiri vijana waliokuwa wamemaliza masomo yao
ili wasaidie katika kazi za ukalimani na uongozaji wa watalii kwenye vivutio vya
utalii. Masengesho alipeleka ombi lake na baada ya muda mfupi akaitwa kwa
mtihani na kuufaulu. Kazi ilipoanza, aliifanya kwa bidii kiasi kwamba watalii wengi
walifurahia huduma yake, wakampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha
tofauti na bidii aliyokuwa akionyesha kazini.
Alifungua akaunti kwenye benki moja na kuanza kuhifadhi sehemu ya mshahara
wake. Alipoona akaunti yake ilikuwa na pesa za kutosha, aliamua kuomba mkopo
ili aweze kuzalisha mali katika shamba lake kubwa ambalo mpaka wakati huo
lilikuwa halijatumiwa vizuri. Shamba hili lilikuwa kwenye mwinuko wa mlima na
lilikuwa likiharibiwa na mmomonyoko wa ardhi. Kwa kupambana na tatizo hili,
alitengeneza mifereji ya maji na kupanda miti mbalimbali karibu na shamba hilo.
Aliandaa vizuri mradi wa kilimo na ufugaji, akajenga vibanda vya mifugo yake,
akawaajiri baadhi ya vijana waliokuwa pamoja katika mafunzo ya muda ule mfupi,
kila mmoja akapewa jukumu lake. Pamoja na kazi yake ya ukalimani, Masengesho
alifuata vizuri mradi wake akanunua vifaa vilivyohitajika pamoja na gari lililokuwa
likitumia umeme. Alinunua gari hili ili apunguze moshi unaochafua mazingira.
Mwaka mmoja baadaye, alikuwa ameishapata mali nyingi na kuanza kujulikana
nchini kote kwa uwezo wake wa kufanya mambo mengi kwa muda mfupi na kwa
ukamilifu.
Serikali ya Rwanda ilipotoa tuzo kwa watu waliochangia kubadilisha maisha
ya watu wengine, Masengesho alikuwa miongoni mwa watu waliochangia
kuyaboresha maisha ya majirani zao. Kila mtu katika kijiji chetu aliitikia mwaliko
wake na wengi tulikuwa tunajivunia kuwa na kijana mwerevu kama yeye. Kwa
sasa ameanza kuendelea na masomo yake katika Chuo kikuu cha Rwanda
ambapo anatarajia kupata shahada yake ya kwanza katika uwanja wa Ukalimani.
Masengesho amekuwa mfano mzuri kwa vijana wengine wengi ambao
wanapoyakumbuka maisha yake, huyaamini yaliyosemwa na wahenga kwamba”
Mchumia juani hulia kivulini” na “mvumilivu hula mbivu”. Wema kwa kila mtu,
utulivu na upendo ni baadhi ya sifa zinazomtambulisha kijana huyu ambayeamewashangaza wengi wanaofahamu alipotoka.
Maelezo muhimu kuhusu mnyambuliko wa maneno
Katika mada ya kwanza tuliona kuwa mnyambuliko au uambishaji ni mbinu ya
kuzalisha maneno mapya kutoka maneno mengine. Mbinu hii hufanyika kwa
kuongeza kwenye sehemu fulani (viini, mizizi au mashina) za maneno hayo
viambishi mbalimbali mwanzoni au mwishoni. Katika sarufi ya lugha ya Kiswahili
kuna:
-- Mnyambuliko wa vitenzi
-- Mnyambuliko wa nomino
-- Mnyambuliko wa vielezi
• Mnyambuliko wa vitenzi
Mnyambuliko wa vitenzi ni uundaji wa vitenzi kutoka maneno mengine. Tunaweza
kupata :
-- Vitenzi kutoka vitenzi
-- Vitenzi kutoka majina
-- Vitenzi kutoka vivumishi
-- Vitenzi kutoka vielezi
• Vitenzi kutoka vitenzi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kuongezea viambishi mbalimbali katika mzizi
wa kitenzi. Viambishi hivi vinaweza kuja mwanzoni au mwishoni mwa mzizi huu.
Mifano: Kucheza: wanacheza- mtachezea-ulichezwa-litachezeshwa
Kupenda: wanapendana-unapendwa-zilipendwa-yanapendeza
• Vitenzi kutoka majina
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kuongezea viambishi mbalimbali katika shina la
jina. Viambishi hivi vinaweza kuja mwanzoni au mwishoni mwa shina hilo.
Mifano: Haya: kutahayari-wametahayarishwa-tulitahayaria-vilitahayarika
Dhuluma: kudhulumu-walidhulumiwa-hawakudhulumiwawatadhulumiana
• Vitenzi kutoka vivumishi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kuongezea viambishi mbalimbali vya shina la
kivumishi. Viambishi hivi vinaweza kuja mwanzoni au mwishoni mwa shina hilo.
Mifano: Laini: kulainisha-vililainishwa-mtalainisha-yamelainika
Pana: kupanua-vilipanuka-mlipanua-yalipanuliwa-pamepanuliwa
• Vitenzi kutoka vielezi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kuongezea kielezi au sehemu ya kielezi viambishi
mbalimbali. Viambishi hivi vinaweza kuja mwanzoni au mwishoni mwa mzizi huu.
Mifano: Sawa: kusawazishwa-kumesawazishwa-watasawazishianahayakusawazishika
Karibu: Kukaribiana-watakapokaribishwa-tulipokaribishwa-yanavyokaribiana
• Mnyambuliko wa majina
Mnyambuliko wa majina/nomino ni uzalishaji wa majina mapya kutoka maneno
mengine. Tunaweza kupata :
-- Majina kutoka majina mengine
-- Majina kutoka vivumishi
-- Majina kutoka vitenzi
-- Majina kutoka vielezi
• Majina kutoka majina
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kubadilisha ngeli za kawaida za majina. Jambo
hili linaweza kufanyika kwa kutia jina katika umoja au wingi, kwa kulidunisha,
kulikuza au kulitia katika dhana ya dhahania.
Mifano:
• Majina kutoka vivumishi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kupachika kiambishi ngeli mbele ya shina lakivumishi.
Mifano: -embamba : wembamba
-- rembo: urembo
-- ovu: ovu, maovu, uovu
-- hodari: uhodari
• Majina kutoka vitenzi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kutia viambishi ngeli vya majina mbele ya mzizi
wa kitenzi na viambishi tamati (viambishi vya kauli, viishio) nyuma ya mzizi huo.
Viishio vinavyotumiwa ni –a, -e, -o, -i, -u na -aji
Mifano: - dunda: mdundo
-- lima: mkulima-kilimo-kilimio
-- pika: mpishi-upishi
-- andika: mwandishi-wandikaji- uandishi
• Majina kutoka vielezi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kupachika kiambishi ngeli mbele ya kielezi.
Mifano: Sawa: usawa
Mbali: umbali
Karibu: ukaribu
• Mnyambuliko wa vielezi
Mnyambuliko wa vielezi ni uzalishaji wa vielezi kutoka maneno mengine. Tunaweza
kuwa na :
-- Vielezi kutoka majina
-- Vielezi kutoka vivumishi
• Vielezi kutoka majina
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kupachika kiambishi ki- mbele ya shina la
nomino. Vielezi hivi ni vya namna.
Mifano: Mume: kiume (Ijapokuwa alipata shida alijikaza kiume.)
Mke: kike (Kabarisa anapenda kuvaa nguo za kike.)
Upuuzi: kipuuzi (Usitamke mambo ya kipuuzi mbele ya watu wazima.)
Marekani:kimarekani (Vitabu hivi vilinunuliwa kwa dola hamsini za
kimarekani)
• Vielezi kutoka vivumishi
Mnyambuliko huu hufanyika kwa kupachika viambishi ki- na vi- mbele ya shina la
kivumishi. Vielezi hivi ni vya namna au vya kiasi.
Mifano: - dog: kidogo- Kutokana na homa anatamka kidogo (namna).
Mwaka huu tumepata mvua kidogo (kiasi).
-- zuri: vizuri- Amefanya vizuri katika mtihani.
-- vyake: kivyake - Kila mtu anaelewa mambo kivyake.
-- gumu: vigumu – Kwa kuwa ana masikio mazito yeye anasikia vigumu.
SOMO LA 7: INSHA ZA KUBUNI
7.1. Kusoma na Ufahamu: Kioja katika Mbuga ya
Mwangaza
Soma kifungu kifuatacho, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini
Siku ya mazishi ya Mzee Ngedere ilikuwa siku tukufu kwa wanyamapori wote wa
Mbuga ya Mwangaza. Waliamua asindikizwe kwa sherehe maalum kwa sababu
mbili. Kwanza, alikuwa mpatanishi wao mwenye busara. Mizozo ilipokuwa ikizuka
mbugani alikuwa akiitatua bila kupendelea upande wowote. Pili, Mzee Ngedere
alikuwa muuguzi bingwa wa kienyeji aliyeheshimika sana.
Baada ya kifo cha Mzee Ngedere, umoja wa Wanyama ulivunjika. Baadhi yao
walikuwa wakipendekeza mganga huyu arithiwe na Bwana Chui na wenginewengi wakimpendekeza Bi Tembo. Siku hii ya mazishi, Mfalme Simba aliamua
kulifumbia jicho jambo hili la urithi wa uganga ili Marehemu asisindikizwe kwa
zogo na vurumai.
Waombolezaji walimiminika kwa wingi: wafalme na raia kutoka mbuga jirani,
viongozi wa kidini na raia wa Mbuga ya Mwangaza kwa ujumla. Wanyama walijaa
uwanjani hata pasipatikane nafasi ya kuweka sindano. Kila raia wa Mwangaza
alijiandaa kila iwezekanavyo kuifanikisha siku hiyo. Lakini wote walifanya hivi
nyoyo zikisumbuka kwa majonzi ya kumpoteza mshauri na mganga wao.
Kabla ya sala ya wafu kuanza, waombolezaji walijipanga kwa mstari mrefu
na kumuaga mpatanishi na tabibu wao kitamaduni kwa kuimba nyimbo za
kuomboleza na kubeba mikoba yake ya utabibu pamoja na mgwisho wake wa
uungwana. Gunia lenye maiti lilibebwa kutoka nyumba ya Mzee Ngedere hadi
kaburi lililokuwa karibu na kasri la Mfalme Simba.
Baada ya msafara huo, mpanga ratiba, ambaye ni Binti Sungura alimkaribisha
Kasisi Nyati kuongoza sala. Wasemaji wote waliopewa fursa walikariri sifa za
marehemu. Kipindi cha sifa kilipomalizika, jua lilikuwa likiwaka sana. Kila kiumbe
kilikuwa kikitokwa na jasho. Wakati wa kufundisha Neno la Bwana ulipofika,
kasisi wa Mbuga ya Mwangaza, Mzee Nyati, alichukua fursa akamsifu Mungu na
kuwaomba wanyama wamshukuru Mungu wao. Yeye alisimama, akivaa miwani
sawasawa na kufungua jarida la karatasi. Baada ya kusafisha koo lake alianza
kuzungumza. Alizungumza na kuzungumza hadi wanyama wengine waanze kuota
mizizi kwa sababu ya kukaa na wengine kusimama kwa muda mrefu. Bwana Chui
alimwamrisha Kasisi Nyati kumaliza maneno yake wakamzike Mzee Ngedere.
Bwana Chui alisema haya huku akipanga kumrithi Mzee Ngedere kwa sababu
alikuwa makamu wake. Aliposikia hayo, Bi Simba alilia kwa kwikwi huku
akimwomba Mungu amrudishe mpatanishi wao kwa sababu Bwana Chui
alikuwa akiogopwa na wanyama wengi kwa ukatili wake. Alikuwa hawapokei
vizuri walipokuwa wakimpelekea malalamiko yao.
Kimya kizito kilitawala kati ya wanyamapori. Kitambo, wingu jeusi lilipita na
kuwatisha wote waliokuwa hapo. Kunguru moyo ulimdundadunda na kujitayarisha
kukimbia akisema kuwa shetani kapita. Kusikia hayo Mfalme Simba alimshauri
kutowatisha kwa kusema mambo ya kishenzi.
Mara gunia lilianza kutikisika na kuonyesha dalili ya kuwa ndani mlikuwamo
kiumbe hai. Kasisi Nyati alipoona hayo alianza kutokwa na jasho kubwa hadi mwili
mzima ukalowa maji. Lo! Wanyama wengi walitimuka na kutawanyikia vichakani
na porini. Kasisi Nyati naye hakuweza kuhimili kioja hicho. Bila ya kuvua joho lake
naye alitimka mbio na kufuata wafuasi wake. Mfalme Simba na Bwana Chui
walijizatiti na kubaki pale ili wajionee kilichokuwa kikijili hapo huku wakiwashauriwenzao kutokimbia.
Baada ya muda mfupi walimwona Mzee Fuko, mke na watoto wake wawili
wakijitokeza chini ya gunia wakidai kuja kumzika Mzee Ngedere. Bi Fuko
alipotaka kujua sababu iliyowafanya wanyama kutimuka, alielezwa kwamba
labda walidhani kwamba Mzee Ngedere amefufuka. Bada ya hapo, Bwana
Chui alitumwa kuwarudisha wanyama kwa sababu kulikuwa hakuna jambo la
kuwafanya wakimbie.
Baada ya kupata taarifa, wanyama walirudi na kumzika mganga na mpatanishi
wao mpendwa. Mazishi yalipomalizika, Bi Tembo alichaguliwa kuwa mpatanishi.
Nafasi ya makamu akapewa Binti Sungura. Bwana Chui alipotaka kuzusha ghasia
alionywa kuwa angefunguliwa mashtaka kwa kosa la uchochezi wa ghasia. Kwa
kusikia hayo, aliomba msamaha, akaahidi kugeuka mzalendo mwema. Aliwaambia
wafuasi wake kutimiza masharti ya Mfalme Simba. Tangu siku hiyo hali ya utulivuilirudi. Upendo na amani ikatawala katika Mbuga ya Mwangaza.
Maelezo muhimu kuhusu mnyumbuliko
Soma maelezo yafuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini
Mnyumbuliko wa kitenzi ni mbinu ya kurefusha kitenzi. Mbinu hii hufanyika kwa
kuongezea mzizi wa kitenzi viambishi tamati. Kiambishi tamati ni mofimu yoyote
inayokuja baada ya mzizi wa kitenzi. Viambishi tamati vinavyotumiwa katika
mnyambuliko ni viambishi tamati vya kauli. Viambishi tamati vya kauli ni viambishi
vinavyoongezea mzizi wa kitenzi maana mpya yenye kauli fulani. Kuna:
• Kauli ya kutendea: -il-
Maelezo Muhimu kuhusu Insha za Kubuni
Insha za kubuni ni aina ya insha ambazo hutungwa kuhusu mawazo yanayozuliwa
na ambayo si matukio ya kawaida.
Kama insha nyingine, insha ya kubuni huwa na kichwa cha habari cha insha
ambacho ni maneno machache, takribani matano, ambayo ndiyo jina la insha.
Kichwa cha habari huandikwa juu, sehemu ya katikati kwenye ukurasa wa kwanza
wa insha. Mara nyingi, huandikwa kwa herufi kubwa na hubeba wazo kuu la
insha. Insha ya kubuni huwa na utangulizi ambao ni sehemu ya mwanzo yenye
urefu usiozidi aya moja. Utangulizi hudondoa kwa ufupi kabisa kile kinachoelezwa
kwenye insha.
Kiini cha insha ya kubuni ni sehemu tunayoweza kusema kwamba ni insha
yenyewe. Kwenye kiini ndipo ufafanuzi wote hutolewa. Ufafanuzi huu hupangwa
katika aya moja au zaidi. Hapa ndipo mwandishi hubainisha mawazo yake,
huthibitisha, hushawishi, huhimiza na hufafanua. Baada ya kiini, huja hitimisho,
yaani sehemu ya mwisho wa insha ya kubuni ambayo haizidi aya moja. Katika
sehemu hii, mwandishi anaweza kurejea kwa ufupi sana yale aliyozungumzia
kwenye insha yake. Anaweza kuonyesha msimamo wake, anaweza kutoamapendekezo, au kuwahimiza walengwa wake kuchukua hatua fulani.
Insha za namna hii humhitaji mwandishi kujiweka kimawazo katika hali fulani ya
kubuni na kutunga insha katika hali hiyo. Kwa hivyo, ili mwandishi afaulu katika
uandishi wake, ni sharti awe na uwezo wa kubuni mawazo kwa undani na pia
kuweza kuyaeleza mawazo hayo kwa njia ya kuaminika kwa wasomaji.
Tanbihi: Kuwepo kwa insha za kubuni hakuondoi ukweli unaosema kwamba
insha zote hutokana na ubunifu wa mwandishi. Hivi ni kwa sababu aina zote
za insha huwa zinaandikwa kwa mawazo yanayobuniwa na akili ya mwandishi.
Jibu maswli yafuatayo:
1. Kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu Kioja katika Mbuga ya
Mwangaza ni aina gani ya insha? Kwa sababu gani?
2. Ni jambo gani mwandishi wa insha ya kubuni anapaswa kuzingatia kabla
ya kuandika?3. Ni mambo gani yanayojitokeza katika insha ya kubuni na insha nyingine?
MADA YA HOTUBA 4 HOTUBA
• Malengo ya ujifunzaji
-- Kubainisha sehemu kuu za hotuba,
-- Kueleza mwongozo wa kutunga hotuba nzuri,
-- Kuonyesha tofauti iliyopo kati ya hotuba na aina mbalimbali za insha,
-- Kueleza tofauti kati ya usemi wa asili na usemi wa taarifa.
SOMO LA 8: MAANA YA HOTUBA
8.1. Kusoma na Ufahamu: Hotuba ya Afisa wa Umoja na
Maridhiano wilayani kwa Wananchi
Soma hotuba ifuatayo kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini:
Ndugu zangu wananchi, ndugu zangu wazalendo na ndugu zangu wazawa.
Hamjambo!
Ninasimama mbele zenu leo hii ili tuzungumzie kuhusu umoja wa Wanyarwanda.
Hebu tujitazame leo tunaishi vipi? Je, tunaishi kwa umoja kama Wanyarwanda?
Kabla sijasonga mbele, ningependa tukumbushane historia ya nchi yetu kuhusu
umoja. Hapo zamani za kale, katika enzi za ufalme, Wanyarwanda walikuwa
na umoja thabiti. Wote walikuwa wakimheshimu mfalme kwa pamoja bila ya
ubaguzi wowote. Mizozo midogo midogo ilipokuwa ikitokota ilikuwa ikitatuliwa
kidugu katika familia au katika vikao vya waungwana. Matatizo hayo yalikuwa
yakihusiana na kama vile mifugo au mashamba. Matatizo magumu yalikuwa
yakitatuliwa na viongozi na hata mfalme mwenyewe.
Wakati huu, umoja wetu ulikuwa ukirutubishwa na sherehe au hafla mbalimbali.
Mtu alipokuwa akitaka kujenga nyumba, majirani walikuwa wakimpa msaada
“umuganda” kwa Kinyarwanda. Aliyekuwa na harusi, majirani walikuwa wakimpa
msaada kama vile kazi za nyumbani zihusuzo matayarisho ya shughuli za harusi,
pombe, n.k. Kwa kuonyesha urafiki wa hali ya juu, Wanyarwanda walikuwa
wakichanganya damu na kuzawadiana mifugo hasa ng’ombe. Wakati wa vita,
Wanyarwanda walikuwa wakipigania usalama wa nchi yao kwa pamoja bila
ubaguzi wowote. Kwa upande wa malezi, mtoto alikuwa akikanywa na mtu
mzima yeyote yule katika jamii.
Ndugu zangu wananchi, wakati wa enzi za ukoloni, umoja wa Wanyarwanda
ulivunjika. Kwanza, wakoloni hawa walidunisha ufalme na watu wengi wakaanza
kugoma. Walivunja nguzo zote zilizokuwa zikishikilia umoja wa Wanyarwanda.
Kitu kibaya mno walichotufanyia na ambacho hatuwezi kukisahau, walituletea
makabila. Makabila haya yalipofika yalitenganisha watu: ndugu, mzazi na mtoto,mke na mume, walianza kuangaliana kwa kijicho na husuda.
Baada ya uhuru, mambo yaligeuka balaa zaidi. Wanyarwanda wengi walianza
kuuawa na Wanyarwanda wenzao. Hawa wa nyuma waligawana mashamba
yao na mifugo yao, walichoma nyumba zao na kuwakimbiza hadi nchi jirani.
Uvunjikaji huu wa umoja wetu ndio uliotufikisha kwenye mauwaji ya kimbari dhidi
ya Watutsi yaliyotokea nchini mwetu mnano mwaka wa 1994.
Afisa: Umoja oyee!
Wasikilizaji: Oyee! Oyee!
Afisa: Amani oyee!
Wasikilizaji: Oyee! Oyee!
Afisa: Utengano zuu!
Wasikilizaji: Zuu!
Ndugu wananchi wenzangu, wahenga walisema yaliyopita si ndwele, tugange
yajayo. Yaliyopita yalipita lakini yalituachia kovu kubwa. Yawe somo kwetu. Siku
hizi tunapaswa kusimama kidete na kuendelea na safari yetu ya kuendeleza
nchi. Safari hii si ya mtu mmoja pekee bali ni safari ya sisi sote Wanyarwanda.
Kwa hiyo, ninawaomba tuungane mikono. Serikali yetu ilipewa jina zuri “Serikali
ya Umoja wa Wanyarwanda.” Umoja huu unapaswa kuwa uti wa mgongo wa
maisha yetu kama Wanyarwanda. Tuishi kwa umoja, tusaidiane vilivyo kwa lolote
lile. Haya yatakapotendeka, nchi yetu inakuwa paradiso ya Afrika na majirani zetu
watatumezea mate.
Ninawashukuru kwa kunitegea masikio na nina imani kuwa kuanzia leo
mnakwenda kuimarisha umoja wetu zaidi ya sasa.Asanteni!
Maelezo muhimu: Maana ya usemi wa asili na usemi wa taarifa
• Usemi wa asili
Ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza .
• Usemi wa taarifa
Iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa
na mtu mwingine bila kupotosha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo
analotaka kulitolea maelezo, basi maneno hayo anayoyasema ni ``usemi wa
Taarifa.``
• Mambo muhimu katika usemi wa taarifa
Wakati wa kuandika usemi wa taarifa kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa ili
usemi huo uwe wa taarifa sahihi.
Maelezo muhimu: Maana ya usemi wa asili na usemi wa taarifa
• Usemi wa asili
Ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza .
• Usemi wa taarifa
Iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa
na mtu mwingine bila kupotosha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo
analotaka kulitolea maelezo, basi maneno hayo anayoyasema ni ``usemi wa
Taarifa.``
• Mambo muhimu katika usemi wa taarifa
Wakati wa kuandika usemi wa taarifa kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa ili
usemi huo uwe wa taarifa sahihi.
1. Nafsi ya kwanza hubadilika na kuwa nafsi ya tatu
Mimi hugeuka kuwa yeye
Sisi hugeuka kuwa wao
Mfano:
-- “Mimi ninasoma kwa bidi,” mtoto alisema.
• Mtoto alisema kuwa yeye alisoma kwa bidi.
-- “Sisi tulisoma kwa bidi,” watoto walisema.
• Watoto walisema kuwa wao walisoma kwa bidi.
2. Badala ya kutumia wakati uliopo, wakati uliopita –li- ndio hutumika.
Mfano: Nina kazi nyingi ofisini.
• Alisema kwamba alikuwa na kazi nyingi ofisini.
3. Alama za kufunga na kufungua maneno hazitumiki kwenye usemi wa
taarifa .
4. Alama za kuuliza na kushangaa hazitumiki kwenye usemi wa taarifa
5. Katika usemi wa taarifa mahali penye wakati ujao -ta- kwenye usemi
wa asili hugeuka kuwa -nge-
Mfano: “Nitaondoka kuelekea Kigali,” shangazi alisema.
• Shangazi alisema kuwa angeondoka kuelekea Kigali.
6. Baadhi ya maneno hubadilisha nyakati yanapotumika katika usemi wa
taarifa .
kama :
Hapa huwa hapo
leo huwa ---siku hiyo/ile
wakati huu ------------wakati huo
kwetu -------kwao
kwangu ------kwake
sasa -----wakati huo/ule
Mfano:
-- “Nitaondoka sasa,” mgeni alisema.
• Mgeni alisema kuwa angeondoka wakati huo/ule.
“Tutacheza leo uwanjani,” wanafunzi walisema.
• Wanafunzi walisema kuwa wangecheza siku hiyo/ile uwanjani.
7. Mojawapo ya maneno yafuatayo hutumika katika usemi wa taarifa
Kuwa----kama ----kwamba
Mfano: -” Utanikuta mjini jioni hii, “Juma alimweleza rafiki yake.
• Juma alimweleza rafiki yake kuwa angemkuta mjini jioni ile.
Hotuba
i) Maana ya hotuba
Hotuba ni maelezo maalumu yanayotolewa na mtu mmoja mbele ya kundi la
watu. Hotuba inaweza kutolewa kwa madhumuni ya kutaka kuhimiza kazi, kufanya
kampeni fulani, kutoa taarifa fulani kwa watu.
ii) Aina za hotuba
a) Mahubiri: Ni hotuba za mafundisho ya kidini, zinazotolewa makanisani,
misikitini, n.k.
b) Hotuba za kisiasa: Ni hotuba zihusuzo taarifa ya serikali kama vile
kuwahimiza watu na kuwaalika kutenda jambo fulani, n.k.
c) Mihadhara: Ni hotuba au mafundisho ya mwalimu shuleni anapofundisha
kundi la wanafunzi na hasa wanafunzi wa vyuo vikuu.
iii) Sifa za hotuba
-- Ukweli wa habari na taarifa
-- Kujua vizuri aina ya watu unaowatolea hotuba, umri wao, kazi zao, n.k.
-- Ufasaha wa lugha ili iweze kupendeza na kueleweka vizuri
-- Nidhamu au adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo mbele
ya watu
-- Mantiki nzuri au mfuatano mzuri wa mawazo
-- Sauti ya kusikika vizuri
-- Kuvaa vizuri.
iv) Tofauti kati ya hotuba na insha
A) HOTUBA
• Hotuba hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/hatibu/kiongozi
anapozungumzia hadhira kuhusu jambo fulani.
• Mwandishi wa hotuba hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza
hotuba yake
• Mara nyingi hotuba huwa katika nafsi ya pili
• Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi,
shirika fulani, daktari, n.k
• Hotuba huanza kwa kutambua hadhira (waliohudhuria mkutano)
• Waliohudhuria mkutano hutajwa kwa vyeo vyao kuanza kwa yule wa
cheo cha juu hadi wa chini k.m: Waziri wa Elimu, Mkuu wa Wilaya,
mabibi na mabwana,……..
• Hatibu akiwa anawazungumzia hadhira isiyomjua, lazima ajitambulishe
• Katika hotuba, hatibu hutoa mapendekezo
• Mwisho wa hotuba humalizika kwa shukurani.
B) INSHA
• Mwandishi wa insha anaweza kunukuu yaliyosemwa na wengine
• Insha inaweza kuwa na mada ambayo mwandishi anatakiwa kutetea au
kupinga
• Katika insha mwandishi hataji vyeo vya hadhira
• Katika insha nyingi, mwandishi hatoi mapendekezo
• Mwisho wa insha hupangwa katika aya na haumaliziki kwa shukurani
Maswali
1. Eleza maana ya hotuba
2. Hotuba hutolewa kwa lengo gani?
3. Taja aina za hotuba
4. Eleza sifa muhimu za hotuba
9.1. Kusoma na Ufahamu: Kazi ni Kazi
Soma hotuba ya Katibu mtendaji wa wilaya katika harakati za uzinduzi
wa elimu ya kujitegemea kwa vijana « Kazi ni Kazi » katika Tarafa yaAmani wilaya ya Tujitegemee
Katibu: Kazi oyee !
Vijana: oyee ! Oyee ! Oyee !
Katibu: Uzembe zii !
Vijana: Zii !
Mheshimiwa Katibu Mtendaji wa Tarafa ya Amani,
Waheshimiwa wakurugenzi wa shule na vyuo
Waheshimiwa vijana,
Mabwana na mabibi mliokusanyika hapa,
Hamjambo?
Vijana ni nani ambaye hapendi kuishi? Sote tunapenda kuishi tena bila shaka
kwa raha. Licha ya hivyo, ili tuishi maisha ya raha mstarehe tunahitaji kufanya kazi.
Kazi ndio msingi wa uhai wa binadamu. Mtu asipofanya kazi hawezi kuyapata
mahitaji yake ya kila siku.
Kazi siyo adhabu kwani binadamu ameumbwa ili afanye kazi; ndiyo maana ana
akili, mikono, miguu, na viungo, vingine vya mwili. Viungo vyote hivi lazima vifanye
kazi ili maisha yawe mazuri. Mtu anahitaji kula, kuvaa na kuishi mahali pazuri. Lakini
ili kuyapata mahitaji yote, ni lazima afanye kazi. Hivyo basi, tunalazimika kufanya
kazi kwa kuwa kazi ni kitendo cha maendeleo. Maendeleo ya mtu huletwa na
kazi. Binadamu hupiga hatua za kwenda mbele kimaendeleo akifanya kazi kwa
bidii. Bila kufanya kazi, maendeleo ya nchi husimama ama hurudi nyuma.
Kazi ni za aina nyingi. Kuna kazi zinazotolewa na serikali au makampuni fulani na
kazi za kujitegemea. Kazi zote hizo ni kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, uchukuzi,
ulindaji wa usalama, ufanyabiasha na kadhalika. Kazi hizi zote zipo ili kujenga
nchi yetu. Hii ni kwa sababu nchi yetu itajengwa na mikono ya wananchi wake.
Siku hizi kuna wale wanaochagua kazi na kupuuza nyingine ati si kazi za heshima.
Msemo wa Kinyarwanda unasema « Hakuna kazi mbaya isipokuwa kuiba na
kuroga. » na Waswahili husema « Kazi mbi si mchezo mwema.»
Siku hizi kuna ongezeko la wasomi. Ongezeko hili halilingani na kazi zinazotolewa
na serikali yetu au makampuni na mashirika ya kibinafsi. Ndiyo maana tunahimizwa
sisi wenyewe kujitengenezea kazi za kibinafsi (kujiajiri). Sote hatuwezi kukaa
ofisini. Tuna mikono na akili, tengeneza kazi na usitegemee wengine kwani
« Mtegemea cha nduguye hufa maskini. »
Kazi ni wajibu wa kila mtu. Kila mtu analazimika kufanya kazi ili atoe mchango
wake katika maendeleo ya jamii. Mtu ni sehemu ya jamii. Kama mtu hafanyi kazi
hulegeza maendeleo ya jamii na matokeo yake ni kwamba jamii hukumbwa na
umaskini. Vijana, mnataka nchi yetu iendelee kuitwa maskini? Hapana! Nchi yetu
inapaswa kusonga mbele kama nchi nyingine zilizoendelea. « Mkiona vyaelea
vimeundwa. » Nchi zile zilizoendelea zilifikia kwenye kiwango kile kutokana
na juhudi, uzalendo na bidii ya raia wao. Kwa hiyo fukuzeni uvivu, ugoigoi nauzembe. Saidieni serikali yetu katika kazi za « umuganda.»
Vijana kumbukeni kuwa kazi ni bakora ya kuondosha umasikini maishani. Ili kuwa
na maisha bora, ni lazima kufanya kazi. Kumbuka kuwa hakuna mtu mwingine
atakayekufanyia kazi. Aidha, kumbuka kuwa jamii isiyofanya kazi ni jamii yenye
watu waliokufa. Kwa hiyo, kila mmoja akumbuke kutimiza wajibu wake. Msemo
wa Kinyarwanda unasema « Asiyefanya kazi hapaswi kula. »
Leo ningependa nitie nanga hapa. Ninawashukuru kwa kunitegea masikio.
Kuanzia leo tuzidi kuchapa kazi ipasavyo. Hii ni kwa kuwa “Kazi ni kazi, la muhimu
mtu amudu maisha.”Asanteni!
Maelezo Muhimu
Usemi wa asili ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza lakini
usemi wa taarifa ni kurudia maneno yaliyosemwa na mtu kwa njia nyingi bila
kupotosha maana ya kwanza. Usemi wa asili hutumia alama za mtajo, kuuliza
na kushangaa lakini usemi wa taarifa huishia kwa nukta. Katika usemi wa taarifanyakati na nafsi za vitenzi vilivyotumiwa katika usemi wa asili hubadilika.
9.4. Matumizi ya Lugha: Maelezo muhimu Kuhusu Muundo
wa Hotuba
Soma maelezo yafuatayo kisha ujibu maswali hapo chini.
• Muundo wa hotuba
Hotuba ina sehemu zifuatazo:
1. Anwani: Anwani, mada au kichwa cha hotuba huchukua mada ya hotuba.
Hiki ndicho kichwa chake hotuba.
Mfano: Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda katika Sikukuu ya Mashujaa.
2. Utangulizi: Mazungumzo katika utangulizi yanatoa mwangaza ama
picha ya habari inayokusudiwa kuzungumzwa. Anza hotuba yako kwa
kuwatambua waliohudhuria mkutano. Wataje kwa majina au vyeo vyao
kuanzia kwa yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana.
Kumbuka kwamba huhitaji kuwasalimia. Kuwatambua kwa vyeo vyao vya
pekee kunatosha.
Mfano: Waziri wa Elimu, Gavana wa Jimbo la Kusini, Mkuu wa Wilaya ya Nyanza,
Wanachama wa kikundi hiki cha Elimu Bora, mabibi na mabwana. Ni matumaini
yangu kwamba nyote mna afya nzuri.
3. Mwili/Kiini: Hakikisha kuwa kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi
mwisho. Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisi wala si
wa taarifa. Panga mawazo kufuatana na uzito ama umuhimu wake. Wazo
muhimu lazima lianze kuzungumziwa kwa ukamilifu halafu lifuatiwe na
mawazo mengine, nayo kwa kikamilifu.
4. Mwisho: Hapa mazungumzo yajumlishe mawazo yote yaliyozungumziwa
kwa maelezo fasaha. Ni vizuri kwa hotuba kufungwa kwa picha inayofanana
na ile ya utangulizi ili kumbukumbu ya habari ibaki katika mawazo ya
wasikilizaji.
• Sifa za hotuba
Hotuba safi huzingatia mambo haya:
• Ukweli wa habari na taarifa: Ni lazima mhutubi ahakikishe kuwa yale
anayozungumzia yana uhusiano na ukweli.
• Ufasaha wa lugha: lazima mhutubi kutumia lugha fasaha, nzuri, safi
na yenye kusikika vizuri kwa kila msikilizaji. Si vizuri kutumia lugha ya
mafumbo.
• Mantiki nzuri: Ni lazima kuweka kwa mfuatano mzuri wa mawazo au
fikra.
• Nidhamu: Yaani adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo
mbele ya watu.
• Sauti ya kusikia wazi pamoja na ishara zinazoeleweka na zinazohusianana yasemwayo. -Ishara hizo si za lazima iwapo hotuba inatolewa kwa
njia ya redio.
• Umuhimu wa hotuba
Hotuba huwa na umuhimu kwa mhutubu na kwa wanaohutubiwa.
Umuhimu huo ni kama vile:
• Kujenga ushirikiano
• Kuheshimiana
• Huondoaa ubaguzi wa kijinsia
• Huhamasisha watu kuwa viongozi walio bora
• Huwahamasisha watu kukuza vipawa na kushiriki katika kuonyesha
vipaji mbalimbali kama michezo ya kuigiza n,k kwa kusikiliza hotuba
zitolewazo.
Maswali
1. Hotuba inatarajiwa kuwa na sehemu zipi?
2. Katika kuanza hotuba yake, mhutubi hufanya nini?
3. Habari yenyewe hutolewa katika sehemu gani? Kwa nini?
4. Mwisho wa hotuba una maumbile gani?
MADA YA 5 UANDISHI WA RIPOTI
Malengo ya ujifunzaji
-- Kutaja aina za ripoti na sifa zake muhimu,
-- Kuonyesha mbinu na taratibu za kutunga ripoti za aina mbalimbali,
-- Kubainisha mazingira mbalimbali ya kutolea ripoti,
-- Kuonyesha vipashio vya tungo za Kiswahili.
SOMO LA 10: MAANA YA RIPOTI
10.1. Kusoma na Ufahamu: Ziara ya Kielimu
Soma ripoti ifuatayo hapo kisha ujibu maswali ya hapo chini.
Ripoti ya Ziara ya Kielimu Iliyofanywa na Wanachuo wa Mwaka wa 3
Chuo cha Ualimu Busara katika Majumba ya Makumbusho mnamo
Tarehe 10/7/2019 hadi 12/7/2019.
Katika mchakato wa ukufunzi na ujifunzaji, wakufunzi na wanafunzi huhitaji kufanya
ziara za kielimu ili kunoa ujuzi wao. Ndiyo maana kuanzia tarehe 10/7/2019
hadi 12/7/2019 wanachuo wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Ualimu Busara
walifanya ziara ya kielimu katika majumba ya makumbusho yanayopatikana
hapa nchini Rwanda. Lengo kuu la ziara hizi lilikuwa kuelewa zaidi historia na
utamaduni wa Wanyarwanda. Ziara hizi ziliongozwa na Mkufunzi Steven Kabera.
Majumba ya Makumbusho Yaliyotembelewa
i) Jumba la Makumbusho la Rukali-Nyanza
ii) Jumba la Makumbusho la Huye
iii) Jumbala Makumbusho la Nyarugenge
Tarehe ya 10/7/2019 ndipo walianza ziara zao. Wanachuo na mkufunzi wao
walianzia katika wilaya ya Nyanza, wakatembelea Jumba la Makumbusho
linaloonyesha maisha ya wafalme. Katika jumba hilo, wanachuo walielezwa
mengi kuhusu maisha ya wafalme walioongoza Rwanda. Hapo walionyeshwa
vifaa tofauti vilivyokuwa vikitumiwa na wafalme hawa na Wanyarwanda kwa
ujumla kabla ya ukoloni. Zaidi ya hayo, jumba hili la Rukali huhifadhi ng’ombe wa
kupendeza macho “Inyambo” kwa Kinyarwanda na nyumba za kifalme.
Walipopewa fursa ya kuuliza, wanachuo waliuliza maswali mbalimbali yaliyopata
majibu kutoka kwa wahudumu wa Jumba hili.
Kwenye tarehe ya 11/7/2019 ziara ya wanachuo ilielekezwa katika Wilaya ya
Huye, katika jumba la makumbusho linalohusu maisha ya Wanyarwanda kwa
ujumla. Katika jumba hili, wanachuo walitembezwa katika vyumba mbalimbali
vinavyounda jumba hili na kuonyeshwa vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na
Wanyarwanda. Mahali hapa, wanachuo walipewa maelezo ya kina kuhusu
historia ya Wanyarwanda toka enzi za wafalme hadi utawala wa jamhuri.
Kwenye tarehe ya 12/7/2019 usukani ulielekezwa jijini Kigali katika Jumba la
Makumbusho la Nyarugenge. Katika jumba hili, wanachuo walielezwa namma
ambavyo wakoloni walikuwa wakiongoza nchi ya Rwanda. Zaidi ya hayo,
wanachuo hawa walielezwa kuwa jumba hili lilikuwa ofisi ya kiongozi wa kwanza
wa kikoloni Dkt. Richard Kandt. Pia, waliambiwa kuwa huyu ndiye aliyefanya
Kigali kuwa mji mkuu wa Rwanda. Vilevile, wanachuo walionyeshwa nyoka
mbalimbali na mamba wanaohifadhiwa katika jumba hili.
Ziara hizi zilipomalizika, wanachuo walikaa pamoja katika ukumbi wa chuo
na kujadiliana kuhusu yale yote waliyoyaona. Kwa pamoja, waliamua kuwa
wametosheka kabisa. Lakini walitoa mapendekezo yafuatayo:
-- Wanaomba chuo kuandaa ziara za kielimu nyingine katika majumba mengine
yaliyobakia kama Jumba la Makumbusho la Karongi (linahifadhi mambo
ya kimazingira), Jumba la makumbusho la mapambano ya kujikomboa la
Kimihurura, Handaki ya Mulindi wa Mashujaa (ku Mulindi w’Intwari), Jumba
la Makumbusho la Mambo ya kisanaa la Kanombe, na kadhalika.
-- Wanaiomba Serikali ya Rwanda, kupitia Bodi ya Maendeleo ya Rwanda(RDB) kutafuta mbinu thabiti za kulinda majumba haya ya makumbusho na
kuhifadhi vitu na vifaa vyote vilivyomo humo.
-- Wanawashauri Wanyarwanda kutembelea katika majumba haya ili kujua
historia na utamaduni wao.
Imetayarishwa na.
Jina: Steven Kabera
Cheo: Mkufunzi wa Kiswahili
Saini: Stevkabera
Tarehe: 13/7/2019
Maelezo muhimu kuhusu sehemu za tungo
i) Maana ya tungo
Tungo ni fungu la maneno ambayo yanawakilisha nafsi, kitu kinachotendwa
au jambo linalopasha habari kamili. Pengine tungo ni kipashio cha kimuundo
kinachotokana na uwekaji pamoja wa vipashio sahili ili kujenga kipashio kikubwa
zaidi. Kipashio ni kipande cha tungo ambacho huweza kujenga au kujengwa
na tungo nyingine.
ii) Aina za tungo
Kiswahili kina tungo nyingi sana; nyingine ni fupi sana, nyingine ni ndefu sana.
Ziko tungo zilizojengwa kwa neno moja tu, na nyingine kwa maneno mengi.
Kwa mfano :
-- Tunasoma.
-- Masika yanakaribia.
-- Mwana wao wa pekee aliwasaidia.
Tungo za Kiswahili ni nyingi, lakini zinaweza kuwekwa katika makundi ya idadi
ndogondogo kwa kufuata misingi fulani fulani ya kisarufi. Angalia mfano huu :
a) Msingi wa muundo wa tungo
b) Msingi wa maana za tungo
Kwa msingi wa muundo wa tungo, tungo hugawanyika katika aina kuu tano :
1. Tungo sahili (Mwanafunzi anafagia.)
2. Tungo tegemezi (Aliyefika)
3. Tungo changamano (Mwanafunzi aliyefika anafagia.)
4. Tungo ambatano (Kijana amekuja na ameondoka.)
5. Tungo shurtia (Mvua ingenyesha mapema tungepanda mahindi.)
Kwa msingi wa wa maana za tungo, tungo hugawanyika pia katikaaina nne
1. Tungo sahili (Mwanafunzi amefika.)
2. Tungo tegemezi (Aliyefika)
3. Tungo nyofu: yenye maana moja tu. (Sipendi kunywa pombe)
4. Tungo tata: yenye maana zaidi ya moja (Sipendi kunywa bia [ tanbihi:bia
humaanisha pombe au ‘pamoja; kwa kushirikiana na mtu mwingine])
iii) Sehemu za tungo
Kwa kawaida tungo ya Kiswahili inaundwa na sehemu mbili kubwa. Sehemu hizo
ni kiima na kiarifu/ kiarifa au prediketa.
Kiima ni sehemu ya tungo inayoonyesha nafsi ya mtenda au mtendwa wa jambo
linaloelezwa yaani kuarifiwa. Kiima huandikwa kushoto mwa kitenzi. Kiima ndiyo
sehemu ambayo hutoa upatanisho wa kiambishi awali cha kitenzi.
Kiarifu /kiarifa/prediketa ni sehemu katika tungo ambayo huzungumza
juu ya kiima. Ni kusema sehemu ya sentensi yenye kitenzi na vipashio vyake
(shamirisho na chagizo).
i) Maana ya Ripoti
Ripoti ni maelezo ya kuhusu mtu, kitu au jambo fulani lililotokea. Ni aina ya
kumbukumbu ambazo huandikwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Ripoti
inaweza kuwa ya uchunguzi wa utafiti kuhusu jambo fulani, inaweza kuwa yapolisi, daktari au ya tume fulani.
ii) Namna ya Kuandika Ripoti
Kabla ya kuandika ripoti, lazima kuwe na ushahidi unaohusu suala au jambo
linaloandikiwa ripoti hiyo. Kwa hiyo, ni lazima mtunzi afanye uchunguzi
kwanza. Pia mtunzi anapaswa kufahamu kiwango cha elimu na uwanja wa mtu
anayemwandikia ripoti hiyo. Kwa mfano kama ni polisi, daktari, mwanasheria,
mfanyabiashara, n.k. Lugha atakayoitumia mwandishi au mtunzi izingatiemuktadha wa matumizi. Lugha itegemee aina ya ripoti.
i) Sehemu za ripoti
a) Kichwa cha ripoti
Kichwa cha ripoti hutambulisha kiini cha ripoti. Yaani ripoti inahusu nini, tarehe
ya tukio au jambo linaloandikiwa ripoti na mahali palipotokea jambo hilo.
b) Utangulizi wa ripoti
Katika hatua hii mwandishi hueleza kwa muhtasari madhumuni ya ripoti.
c) Kiini cha ripoti
Katika sehemu hii mwandishi hueleza mambo aliyoyaona, chanzo chake na
madhara au faida yake.
d) Hitimisho
Katika kuhitimisha ripoti mwandishi anaonyesha msimamo na mapendekezo
yake. Baada ya hitimisho, mwandishi huandika au huonyesha aliyeandika ripoti,
cheo chake (nafasi yake hasa katika ripoti hiyo) na tarehe ripoti hiyo ilipoandikiwa.Ikumbukwe kuwa aghalabu ripoti huandaliwa ili kutaka mageuzo fulani ya jambo.
v) Aina za Ripoti
Ripoti ni za aina nyingi:
-- Za kielimu
-- Za mikutano
-- Kiuchumi
-- Kijamii
-- Kisiasa
-- Kiusalama
vi) Sifa za Ripoti
Ripoti ni lazima iwe na mpangilio mzuri wenye mada zinazozungumziwa na labda
hata mada ndogo ndogo zenye kuzingatia utaratibu wa nambari. Matumizi ya
nambari husaidia kuipa ripoti mpangilio mzuri na wenye kueleweka kwa urahisi.
Ripoti hazipaswi kuwa ndefu sana na zinapaswa kuwasilisha mambo muhimu
kwa ufupi. Mwandishi wa ripoti hutumia mbinu za kufupisha lakini anahakikisha
kuwa kila kitu kimezungumziwa. Ripoti hutumia sentensi fupi fupi zinazowasilisha
mambo muhimu kwa uwazi. Ni vyema lugha inayotumiwa katika ripoti iteuliwe
kwa uangalifu na isiwe na hisia au sifa ya kuathiri vibaya wanaoisoma.Jibu maswali yafuatayo :
1. Ripoti ni nini?
2. Taja angalau mambo matatu ya kuzingatia wakati wa kuandika ripoti.
3. Taja sehemu za ripoti
10.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
11.1. Kusoma na Ufahamu: Ripoti ya Maandalizi ya
Mafunzo ya Elimu Jumuishi
Soma ripoti ifuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini:
Ripoti ya Maandalizi ya Mafunzo ya Elimu Jumuishi Yaliyofanyika
tarehe 2/11-15/11/2019 katika chuo cha TUENDELEZE ELIMU.
Mnamo tarehe 2/11/2019 hadi 15/11/2019 yalifanyika mafunzo kuhusu elimu
jumuishi. Mafunzo haya ili yaweze kufanikiwa, yalihitaji ufasaha wenye maandalizi
ya kutosha yaliyochukua wiki mbili. Ilifanyika hivi ili wakufunzi waweze
kufanikisha kuandaa mada husika . Kufanikiwa kwa maandalizi hayo ni kutokana
na juhudi za wakufunzi wenyewe kuwa na moyo wa kujituma, na ushirikiano
mkubwa ulioonyeshwa na jopo la uongozi wa chuo cha Ualimu“TUENDELEZE
ELIMU” kilichopo wilayani ya Matumaini.
Wakufunzi tulifurahia ushirikiano kutoka chuo “TUENDELEZE ELIMU” kwani
kila kitu tulichohitaji ili kufanikisha mafunzo yetu kilitolewa na uongozi wa chuo
bila tatizo lolote. Ushirikiano wao ulikuwa katika vifaa vya maandalizi, chakula na
malazi, posho kwa ajili ya kujikimu na usafiri. Hayo yote yalikuwa changamoto
kwa wahadhiri na washiriki wa mafunzo.
Utoaji wa mafunzo
Mafunzo yalifanyika kwa muda wa siku tano saa nane zilitumika kwenye mafunzo
na saa mbili zilitumiwa kwenye majadiliano, kwa ajili ya chakula na mapumziko
kwa wakufunzi, walengwa na uongozi.
Zifuatazo ni mada mbalimbali zilizotolewa kwenye mafunzo haya:
1. Njia Shirikishi katika Ujifunzaji
Njia shirikishi katika kujifunza ilipewa kipaumbele katika muda wote wa mafunzo.
Njia hii ilihamasisha wanachuo kushiriki zaidi katika mazoezi na kwa kiwango
fulani iliwasaidia pia kushiriki katika kujifunza. Njia hii ilileta msukumo katika
kutafuta majibu na kuunganisha pamoja taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, badala
ya kumtegemea tu mkufunzi kuongoza vipindi vyote vya masomo. Kwa sababu
elimujumuishi si dhana rahisi ambayo inaweza kutumika kwa namna moja, katika
sehemu zote, wanachuo katika mafunzo ya elimujumuishi wanapaswa kupewa
mwongozo wa kutafuta na kupata habari sahihi na kutafuta njia bora ya kusonga
mbele kwa kuanzia sehemu walizopo. Zaidi ya mazoezi yaliyokuwa yamepangwa
kwenye ratiba, ushirikishwaji katika kujifunza ulifanywa pia katika majadiliano ya
nje wakati wa mapumziko, na katika maktaba ndogo ambamo washiriki huwezakupata nafasi ya kujisomea katika muda wa ziada.
2. Umuhimu na sifa za mafunzo haya
Mafunzo yalilenga kuendeleza dhana kwamba hupaswi kujifanya mjuaji zaidi wa
elimu jumuishi kwa kufanya peke yako matendo ambayo unadhani yanaifanya
elimu iwe jumuishi zaidi. Kila mmoja ana mawazo na uzoefu wake ambapo yote
ni muhimu katika kuendeleza mfumo wa elimu jumuishi na jamii nzima.
3. Stadi za mawasiliano
Ingawa kulitumiwa uwasilishaji wa mada au kazi za vikundi, tulihitaji stadi maalum
za mawasiliano. Tunapaswa kuwaelezea watu kuhusu sisi wenyewe, kazi zetu,
uzoefu wetu au mawazo yetu, na mara kwa mara tunahitaji uwezo wa kufanya
hivi kwa muda mfupi. Ni kawaida kwa wanachuo kukosa ujuzi na/au kutojiamini
katika mawasiliano. Hii inaweza kuathiri maendeleo na matokeo ya mafunzo
hasa ukizingatia kwamba wanachuo wanatarajiwa kuchangia hoja na uzoefu
na siyo kuwa wasikilizaji.
4) Hitimisho
Katika kuhitimisha ripoti waandaaji wa mafunzo walitoa shukrani zao kwa jopo
zima la chuo na uongozi na watendaji wake kwa ushirikiano wao mzuri
waliouonyesha kwa mijadala yao mizuri iliyowawezesha kujua tatizo lipo wapi
na pia kuibua uzoefu uliopo na hatimaye kwa pamoja kuweza kutambua udhaifu
upo wapi. Hatua hii itasaidia kutoa uzoefu wa namna ya kurekebisha ambapohapakwendeka vizuri.
Kipashio
Kipashio ni neno moja au kifungu cha maneno chenye kazi maalum katika
tungo. Vipashio hivi ndivyo ambavyo huungana pamoja na kujenga sehemu kuu
za tungo yaani kiima na kiarifu.
• Vipashio vya kiima
Kiima kinaweza kuundwa na vipashio vya aina mbili: neno moja au fungu la
maneno.
a) Neno moja katika kiima
i) Nomino (N): Kazi ni uhai.
ii) Kiwakilishi (W): Yeye hapendi kushiriki ngono.
-- Huyu ni kiranja wetu.
iii) Kitenzi-jina: Kuimba kunapendeza.
iv) Kishazi: Atakayevuta bangi ataadhibiwa.
b) Fungu la maneno katika kiima
i) Nomimo mbili (N+N): Baba na Mama wanafanya kazi za Umuganda.
ii) Bwana Kagabo ni mcheshi.
iii) Nomino na kivumishi (N+V): Mwanafunzi hodari hana wasiwasi.
iv) Kiwakilishi na kivumishi (W+V): Huyu hodari hana wasiwasi.
v) Nomino na kishazi: Mwanafunzi atakayevuta bangi ataadhibiwa.
• Vipashio vya kiarifu
Kiarifu kinaweza kuundwa na vipashio vya aina mbili: neno moja na fungu la
maneno
a) Neno moja katika kiarifu
i) Kitenzi (T): Mama analima.
b) Fungu la maneno katika kiarifu
i) Kitenzi na Kitenzi (TS+T): Yeye anapenda kucheza.
ii) Kitenzi na shamirisho (T+SH (N)): Yeye anacheza mpira.
(T+SH(W)): yeye anapenda yule.
iii) Kitenzi na chagizo (T+CH (E)): Yeye anacheza vizuri.
(T+CH(HU)): Yeye alienda kwa mganga.
iv) Kitenzi na kishazi: Yeye anacheza tunapolala.
• Taratibu za kufuatilia wakati wa kuandaa ripoti
Unapoandika ripoti unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:
• Hakikisha kuwa umeelewa shughuli inayohusika
• Hakikisha unajua urefu unaohitajika na masuala unayopaswa kuyagusia
• Kusanya maelezo yote unayohitaji kuhusiana na ripoti hiyo.
• Yapange maelezo yako vizuri. Zipitie hoja zako ili uondoe mawazo
ambayo yanaweza kuwa yamerudufishwa au yamerudiwa.
• Yaangalie mawazo yako ili kubainisha ni yapi ambayo yanapaswa
kutangulia na yanafuatwa na yapi.
• Unapoandika ripoti yako hakikisha kuwa unaitumia lugha yako. Usiridhike
tu na maneno unayoyapata wakati wa uchunguzi wako. Kuandika ripoti
kwa lugha na maneno yako huonyesha kuwa umeielewa.
• Unaweza kuuboresha uwezo wako wa kuandika ripoti kwa kujitahidi
kuyaelewa maelezo yanayohusika na kujitahidi kuyaeleza kivyako.
• Baada ya kuandika nakala ya kwanza ya ripoti unaweza kuiboresha kwa
kupunguza mambo ambayo siyo muhimu katika ripoti hiyo.
• Lugha inayotumiwa katika uandishi wa ripoti lazima izingatie wasomaji
wa ripoti inayohusika. Kwa mfano, ikiwa wasomaji ni wanafunzi wa shule
lugha yake haipaswi kuwa na ugumu au utata wa kisayansi.
• Mifano ya mazingira ya kutolea ripoti
• Kila jambo mtu analofanya kila mara nyingi huomba kutolewa ripoti. Kwa
mifano:
-- Mwanafunzi anaweza kutumwa kuwakilisha chuo chake katika kongamano
la vilabu mbalimbali akatoa ripoti baadaye.
-- Mwanfunzi anaweza kuenda kujizoeza kufundisha katika chuo fulani,
anapomaliza akaombwa kutoa kuripoti kwa chuo chake.
-- Mtangazaji wa habari anaweza kufanya utafiti kuhusu jambo fulani kisha
akatoa ripoti kwa yale aliyoyaona.
-- Mtafiti fulani anaweza kutumwa kuchunguza mambo fulani (ukiukaji wa
haki za kibinadamu, kuenea kwa ugonjwa fulani, kiwango cha hongo, n.k)
kisha akatoa ripoti.
-- Maafisa wa kiserikali wanaweza kufanya utafiti kuhusu maisha ya jamii
(uchumi, kilimo, ufugaji, …) wakatoa ripoti kwa serikali.
• Mazingira ya kutolea ripoti ni mengi mno, ripoti zinaweza kutolewa katika
mikutano, darasani, kwenye televisheni, redioni, katika hafla, katika vikao
vya dharura, katika makongamano na kadhalika.
Jibu maswali yafuatayo
1. Uboreshaji wa ripoti hufanyika namna gani?
2. Kwa sababu gani mwandishi wa ripoti analazimishwa kuzingatia vizuri
lugha anayoitumia?
3. Taja mazingira matatu ya kutolea ripoti.
MADA YA 6 UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Malengo ya Ujifunzaji:
-- Kueleza maana ya uhakiki,
-- Kubainisha taratibu au mbinu za uhakiki wa kazi za fasihi simulizi,
-- Kuonyesha umuhimu wa kuhakiki kazi za fasihi,
-- Kujadili maana ya uhakiki na mwongozo wake,
-- Kuhakiki hadithi za masimulizi mbalimbali,
-- Kutoa mapendekezo juu ya kazi za fasihi zilizohakikiwa,
-- Kukuza falsafa tofauti zinazojidhihirisha kutoka ujumbe wa kazi za fasihi
simulizi,-- Kuainisha aina za maneno katika Kiswahili.
SOMO LA 12: MAANA YA UHAKIKI
12.1. Kusoma na Ufahamu: Siku Njema Huonekana
Asubuhi
Soma kifungu kifuatacho, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo
chini.
Ilikuwa Jumatatu asubuhi wakati mwalimu wetu wa Kiswahili Bibi Amina
alipotuchekesha sana. Mwalimu huyu kwa kawaida yake alikuwa mcheshi
na mwenye kupenda utani. Ilikuwa ni ajabu mno kumwona amekunja uso.
Wanafunzi wote walikuwa wakimpenda na hata wagonjwa walikuwa wakijikaza
kiume ili wawahi somo lake. Alikuwa mnene kiasi, macho mazuri kama gololi
yaliyokuwa yakicheza katika vidimbwi vya machozi. Alipokuwa akicheka, vishimo
vidogovidogo vilikuwa vikionekana kwenye mashavu yake. Sauti yake ilikuwa
ikituvutia sana. Alikuwa akifundisha na wanafunzi sote tukatoka tukisema kuwa
tumetosheka.
Asubuhi hiyo, tulipofika shuleni tuliulizana habari mbalimbali. Kuna wale
waliokuwa na habari za michezo na wengine walikuwa na habari zinazohusu
maisha ya nchi yetu: uchumi, elimu, siasa, ufugaji, kilimo na kadhalika. Habari
hizo zote tulikuwa tumezipata kutoka kwenye redio na nyingine kutoka kwenye
runinga. Kwa kuwa nami nilikuwa sogora kwa kutia chumvi katika mazungumzo,
kila siku wanafunzi walikuwa wakinizunguka kama nyuki wazengeavyo maua.
Kengele ya kwanza ilipolia, sote tulikusanyika karibu na mlingoti wenye bendera
ya taifa na kuanza kuimba wimbo wa taifa. Tulipomaliza, Joni, mwalimu wa somo
la ujasiriamali, alipanda jukwaani na kuanza kutuhutubia kuhusu mada ya “Ndi
Umunyarwanda.” Siku hiyo yeye alitilia mkazo kwenye umoja na maridhiano kati
ya Wanyarwanda, uzalendo na mshikamano kama njia bora za kuendeleza nchi
yetu. Alipomaliza, tuliingia madarasani na kuwasubiri walimu wetu.
Kengele ya pili ilipolia mwalimu wetu wa Kiswahili alijtokeza na kutuamkia kama
kawaida yake. Alikuwa na mkoba begani na vitabu pamoja na boksi la chaki
mikononi. Sisi sote tulikuwa na hamu ya kusikia mchapo aliokuwa ametuletea
asubuhi ile. Bila ya kusema neno lolote aliweka vifaa vyake mezani akaangaza
macho kama aliyekuwa akishuku jambo baya fulani darasani. Sisi sote tulitulia
tuli kama maji mtungini. Hayawi hayawi huwa. Alipomaliza ukaguzi wake
alituuliza majina ya wale ambao hawakuhudhuria shule lakini sote tulikuwa hapo.
Alitabasamu na kuanza somo lake.
Kwanza alituuliza maswali kuhusu somo lililopita. Somo hilo lilikuwa vipengele
vya fasihi simulizi. Tuliposonga mbele alituomba kumwonyesha kazi ya nyumbani
aliyotupatia. Kazi hiyo ilikuwa uchambuzi wa hadithi. Sote tulikuwa tumejaribu
kwa uwezo wetu. Alituuliza mbinu tulizotumia katika uchambuzi wetu, kila mtu
akataja zake. Alitukagua kitambo kidogo, akatupongeza na kusema kuwa “Kweli
siku njema huonekana asubuhi.” Mara hii alichukua chaki na kuandika neno
“UHAKIKI” ubaoni. Nasi tukaanza kunong’onezana kwa kuwa ilikuwa mara ya
kwanza kuona neno hilo. Tulishangaa sana kwa kuona kuwa hakuandika jaribio
kama desturi yake ya kutuuliza kila alipokuwa akiingia darasani. Alipotangaza
kuwa neno hilo lilikuwa somo la siku ile sote tulitega masikio.
Pili, alitugawa katika makundi. Kila kundi lilikuwa limeundwa na wavulana na
wasichana, na wanafunzi wenye matatizo maalum ya kielimu. Kila kundi lilipewa
kitabu. Kabla hatujafungua vitabu, alituomba kukagua vema kama kila kundi
lilipewa vitabu vya Kiswahili. Alituonya hivi huku akitwambia kuwa kulikuwa
na mtu mmoja aliyeingia mgahawani bila kuuliza habari wala kusoma, akatia
pilipili hoho nyingi kwenye chakula akidhani kwamba ni supu. Alipokula chakula
hicho, aliwashwa na machozi yalimlemgalenga. Katika kujaribu kupoza koo lake,
akashika na kunywa sabuni ya kunawia mikono akifikiri kwamba ni juisi. Sisi sote
tulishika mbavu. Alituagiza kufungua vitabu na kuzungumzia kuhusu uhakiki wa
kazi za fasihi simulizi. Tulipomaliza kuzungumza, kila kundi liliwasilisha.
Tuliona kwamba uhakiki ni kazi ya kutathmini, kufasili na kuainisha kazi za fasihi.
Ni kazi ya kusoma maandishi au kusikiliza mambo fulani kwa kuyachambua na
kuyafafanua ili kupata ukweli wa mambo hayo.
Zaidi ya hayo, tulisoma kuwa kwa kuhakiki maandishi au masimulizi,
tunachunguza na kufafanua vipengele vya fani na maudhui. Katika fani kama sura
ya nje ya maandishi au masimulizi, tunachunguza wahusika, muundo, mtindo
na mengineyo. Kimaudhui, tunachunguza dhamira, ujumbe, migogoro, itikadi,
falsafa na hata mtazamo. Wakati huu, mambo yaliyokuwa yakitushinda, mwalimu
alikuwa akitusaidia ili tuyaelewe zaidi.
Isitoshe, baada ya kuona maana ya uhakiki, mwalimu alituomba kueleza
umuhimu wa uhakiki tukagundua kwamba uhakiki una umuhimu wa kumwezesha
mhakiki kuchambua na kuelewa kazi ya fasihi au sanaa kwa ujumla, kuwezeshakulinganisha kazi tofauti na mengine mengi.
Lakini katika uchambuzi wetu, tuligundua kuwa uhakiki una matatizo fulani kwa
sababu ni sayansi ngumu inayoomba bidii, ukakamavu wa mhakiki, uwezo wake na
mienendo ya jamii. Hili linatulazimisha tufanye mazoezi mengi ili tuweze kupevuka
katika kazi hii. Tena tuliona kuwa, wakati mwingine, wahakiki hawakubaliani kwa
kuwa kila mmoja ana namna yake ya kuona na kuelewa mambo.
Somo lilipokaribia kutia nanga, sote tulikuwa tumeelewa kwamba uhakiki lilikuwa
si somo geni kwa kuwa kila siku tunajaribu kuchambua yale tunayosoma au
tunayoambiwa. Kutokana na weredi wa haraka tuliokuwa nao ndipo nilipokumbuka
kuwa “Siku njema huonekana asubuhi.” Kabla ya kutuaga mwalimu alitupa kaziya nyumbani ya kuhakiki hadithi.
• Nomino/ jina
a) Maana ya nomino
Nomino au jina ni neno linaloita kitu chenye uhai au kisicho na uhai kwa
kukitofautisha na vingine.
b) Aina za nonino
-- Nomino za pekee: Butare, Rusizi, Kamana, Ibilisi, Mukungwa, Akanyaru,
-- Nomino za kawaida: barabara, gari, kuku, kiongozi, nchi, …
-- Nomino za dhana au za dhahania: maridhiano, uzalendo, utoto, utu,
upendo, …
-- Nomino za jamii/ za makundi: jamii, jamaa, baraza, genge, kikosi, …
-- Nomino za wingi: mawese, maji, mafuta, mamlaka, madaraka, …
-- Nomino za kitenzi-jina: kuishi kwa amani kunapendeza. Kuimba ni
kuzuri. Kufurahi kwako kunatutuliza. (kuishi, kuimba na kufurahi ni vitenzijina
katika sentensi hizi)
• Vivumishi
a) Maana ya Kivumishi
Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu
vivumishi hutanguliwa na nomino.
b) Aina za vivumishi
• Vivumishi vya sifa
Mifano:
-- Mke mrefu yule ni mtulivu.
-- Tunapaswa kujenga jamii nzuri.
-- Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni.
• Vivumishi vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha umiliki wa nomino. Mizizi ya vivumishi hivi
huundwa kulingana na nafsi mbalimbali. Mizizi hiyo ni : -angu, -ako, -ake, -etu,
-enu, -ao.
Mifano :
-- Nyumba yangu haina mlango.
-- Familia yake inaishi vizuri.
• Vivumishi vya idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi
vya idadi.
a) Idadi kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
Mifano:
-- Mmomonyoko wa ardhi ulibomoa nyumba kumi katika vijiji viwili.
-- Ili kupunguza uhasama unaotokana na ukewenza mume mmoja
analazimishwa kuoa mke mmoja.
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano: Chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani.
Mifano:
-- Watoto kadhaa waligeuka mayatima wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya
Watusi yaliyotokea mnamo mwaka wa 1994.
-- Mvua nyingi ilinyesha na kusababisha mafuriko.
• Vivumishi viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
-ngapi?, -pi? wapi?, gani?
Mifano:
-- Mtu mzima ana meno mangapi?
-- Ni mbuga gani inayohifadhi sokwe nchini Rwanda?
• Vivumishi viashiria / vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Karibu: hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale.
Mbali kidogo: hapo, huyo, hiyo, hicho.
Mbali zaidi: pale, lile, kile.
Mifano:
-- Safisha mahali hapa.
-- Mwanafunzi yule ni mchezaji kabumbu.
• Vivumishi visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria
Mifano:
-- Anaishi pahali papa hapa.
-- Mtu yuyu huyu anatuongoza vizuri.
• Vivumishi virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa
vivumishi vya O-/-ye rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea
nomino.
Mifano:
-- Mwanafunzi ambaye ataenda nje ya shule bila ruhusa ataadhibiwa.
-- Wanyama ambao wametoroka mbuga hawapaswi kuuawa.
• Vivumishi vya A-unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki
nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na
kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino.
Mfano: cha, la, kwa, za, ya.
-- Dawa ya moto si moto.
• Viwakilishi
a) Maana ya viwakilishi
Viwakilishi vya nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi
hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.
b) Aina za viwakilishi
• Viwakilishi vya nafsi
-- Viwakilishi nafsi huru: Mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao.
-- Viwakilishi nafsi viambata : Ni-, u-, a-, tu-, m-, wa-, mi-, li-, ya-, ki-, vi-,
i-, zi-, ku-, pa-
• Viwakilishi viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kuonyesha
nomino inayorejelewa bila kuitaja.
-- Hiki ni chanzo cha maradhi.
-- Hao wanataka maridhiano.
• Viwakilishi visisitizi
Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia kiashiria chake mara mbili mfululizo.
Kwa mfano: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, zizi hizi,
- Kiki hiki ndicho kinachonifurahisha,
- Yuyu huyu alitueleza matumizi ya viwakilishi visisitizi
• Viwakilishi vya sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
Kwa mfano: -chungu, -eupe, -dogo, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, -gumu,
-kali, ekundu.
• Viwakilishi vya idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
a) Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino
-- Wawili hugeuka mmoja.
-- Alizaa watatu tu.
b) Idadi isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano:
-- Tutasikiliza maoni ya wengi kabla ya kuanzisha mradi huu.
-- Vichache viliandikwa kuhusu maradhi ya UKIMWI.
• Viwakilishi viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli.
Mifano:
-- Unaenda wapi?
-- Ulinunua mangapi?
• Viwakilishi vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
-- Kwao hakuna maji safi.
-- Yao yameharibika tena kutokana na mvua kali.
• Viwakilishi virejeshi
Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino.
Kwa mfano: ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule.
-- Ambao walizaliwa mwaka huu watachanjwa.
-- Ambacho kinahitajika kitatafutwa.
• Viwakilishi vya A-unganifu
Huwakilisha nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa
kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha
a-unganifu.
Kwa mfano: cha, la, kwa, za, ya
-- Cha mlevi huliwa na mgema.
-- La kuvunja halina rubani.
• Kitenzi
a) Maana ya kitenzi
Kitenzi ni neno linaloeleza jambo linalotendwa au kufanywa na nomino au
kiwakilishi chake.
b) Aina za vitenzi
• Kitenzi halisi: ni kitenzi kimoja kinachotumiwa katika sentensi.
Mifano:
-- Wanafunzi walipanda miti michache.
-- Rais atafika kesho.
• Vitenzi vikuu na vitenzi visaidizi: Wakati vitenzi viwili hutumika
pamoja kueleza kitendo kimoja, kitenzi cha kwanza huitwa kisaidizi na
cha pili ndicho kitenzi kikuu.
Mifano:
-- Yeye alikuwa akisoma.
-- Wao wanahitaji kuishi vizuri.
• Vitenzi vishirikishi: Vitenzi vishirikishi vina dhana ya kitenzi kuwa au
kuwa na.
Vitenzi vishirikishi huwa vya aina mbili kuu:
• Vitenzi vishirikishi vikamilifu: hivi huchukua viambishi vya wakati na
viambishi nafsi.
Mifano:
-- Watoto wangali kitandani.
-- Wao wamekuwa na uzembe.
• Vitenzi vishirikishi vipungufu: hivi huchukua viambishi nafsi lakini
havichukui viambishi wakati.
-- Wezi si wazuri.
-- Yeye yu mkweli.
-- Sisi ni walimu.
Ukakiki wa Tanzu za Fasihi Simulizi
• Maana ya Uhakiki
Uhakiki ni utathmini, ufasili na uainishaji wa kazi ya fasihi. Ni uchambuzi wa ndani
kabisa wa kitu au jambo ulioambatana na fikra za mchambuzi. Uhakiki ni kazi ya
kusoma maandishi au kusikiliza mambo fulani kwa kuyachambua na kuyafafanua
ili kupata ukweli wa mambo hayo.
Uhakiki ni sayansi maalum ya kuchambua na kudadisi au kupima ubora au
udhaifu wa kazi ya kisanaa hasa fasihi. Uhakiki wa tanzu za fasihi huzingatia
mambo mawili muhimu yaani fani na maudhui. Fani na maudhui ni mambo mawiliambayo hayawezi kutengana kwa sababu moja hutegemea jingine.
i) Fani
Fani ni namna msanii anavyowasilisha maudhui yake kwa hadhira. Fani pia
huweza kutazamwa kama umbo la nje la kazi ya sanaa yaani sura yake ya nje.
Kuchunguza fani ni kuchunguza kiundani vipengele mbalimbali vya kifani na
namna vilivyotumika ili kuwasilisha maudhui. Uchunguzi wa fani unazingatia
vipengele vifuatavyo: wahusika, muundo, mtindo, mandhari, matumizi ya lugha.
• Wahusika
Wahusika ni watu, wanyama, vitu, hata viumbe vya kufikirika ambavyo msanii
wa kazi ya fasihi hutumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi
za fasihi msanii huwagawa wahusika katika makundi mawili: wahusika wakuu
na wahusika wadogo. Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia
mwanzo mpaka mwisho na ndio huwa msingi wa kazi ya fasihi hasa hadithi.
Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza mara chache au sehemu
mbalimbali katika kazi ya fasihi na huwasaidia wahusika wakuu katika kubeba
maudhui. Wahusika wadogo hawa wanaweza kuwa watetezi (wakimsaidia
mhusika mkuu) au wakawa wapinzani (wakimzuia mhusika mkuu).
Wahusika wa kazi za fasihi wana tabia mbalimbali. Tabia ya kwanza ni ubapa
yaani tabia ya kutobadilika kwa mhusika toka mwanzo hadi mwisho. Tabia ya pili
ni uduara yaani tabia ya kubadilika kihulka, kimawazo na kisaikolojia kufuatana
na mazingira mapya, wakati, hali, na kadhalika. Tabia ya tatu ni ufoili. Ni tabia
inayojidhihirisha kati ya ubapa na uduara. Wahusika wenye tabia hii hawaonyeshi
msimamo wao kama wanaweza kubadilika au kutobadilika.
Mtindo
Ni namna ambavyo msanii huipa kazi yake sura ya kifani na kimaudhui kwa njia
ambayo msanii mwingine hawezi kuipa hivyo hata kama jambo lizungumziwalo
na wasanii hawa wawili ni lile moja. Mtindo ndio unaomwezesha msomaji,
msikilizaji au mtazamaji wa kazi ya fasihi amtambue msanii wa kazi hiyo bila
kuelezwa au kusoma jina la msanii huyo. Kuchunguza mtindo wa kazi ya fasihi
ni kuangalia matumizi ya lugha katika kazi hiyo. Wakati wa kufanya kazi hiyotunajiuliza maswali yafuatayo:
-- Msanii anatumia lugha namna gani? Je kuna tamathali za usemi, mafumbo,
methali, nahau,…
-- Picha alizochora msanii zinaeleweka au zimesaidia kurahisisha katika
maelezo yake?
-- Msanii anatumia mbinu zipi? Mazungumzo, mijadala, hadithi ndani ya
hadithi,… ?
• Muundo
Ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia msanii katika kupanga kazi yake. Pia ni
mpangilio na mtiririko wa visa na matukio. Katika muundo tunaangalia vipengele
kama ploti. Ploti ni mtiririko wa kiusababishi wa visa na matukio. Aidha, katika
muundo tunajiuliza mtiririko huu wa visa na matukio ni wa moja kwa moja au ni
wa kiurejeshi? Kama ni wa moja kwa moja ni muundo wa msago. Kama unaenda
mbele na kurudi nyuma ni muundo rejeshi.
• Mandhari
Mandhari ni sura ya mahali popote palipotumiwa na msanii kwa kukisimika
anachokisimulia katika kazi ya fasihi. Kuna Mandhari halisi yaani mahali
panapoweza kuonekana, panapojulikana waziwazi, panapopatikana (nchi fulani,
wilaya, mkoa, mlima,…) na Mandhari pakubuni yaani mahali pa kujiundia, pa
kindoto pasipopatikana (mbinguni, jahanamu, ahera, ujinini, ...)
• Muktadha
Muktadha ni mazingira au hali ambamo tukio au jambo fulani hutendeka. Ni
kusema kuwa msanii huishi katika jamii na jamii huzungukwa na mazingira
mbalimbali. Mazingira haya yanaweza kuonekana katika kazi ya fasihi. Mazingira
haya yanaweza kuonekana kulingana na lugha iliyotumiwa, msamiati uliotumiwa,
mawazo fulani ya msanii yanayolingana na wakati fulani. Kwa mfano kazi za fasihi
simulizi za enzi za ufalme ni tofauti na kazi zilizopatikana baada ya uhuru wa
Rwanda.
ii) Maudhui
maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa na masanii katika kazi ya
kifasihi. Haya ndiyo huwa yamemsukuma msaniii kuisana kazi yake hii. Maudhui
hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi
akatunga na kusanii kazi yake ya kifasihi. Uchambuzi wa maudhui huzingatia
vipengele kama vile dhamira, ujumbe, migogoro, falsafa na hata mtazamo.
• Dhamira
Dhamira ni wazo lililomo katika kazi za sanaa. Kwa kawaida, dhamira zinagawika
katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
a) Dhamira kuu: ni kiini cha wazo kuu la msanii ambalo linaongoza
ujumbe autakao msanii kufikisha kwa jamii. Dhamira kuu huweza kuhusu
jamii, magonjwa ya zinaa, siasa, uzalendo, uchumi, ushirikiano, umoja na
maridhiano, usawa wa jinsia, malezi bora, mapenzi, mazingira na maendeleoendelevu, n.k.
b) Dhamira ndogondogo: ni dhamira zile mbalimbali zinazogusiwa na
msanii ili kuendeleza dhamira kuu. Dhamira hizi husaidia dhamira kuu katika
kujidhihirisha.
• Ujumbe /Mafunzo
Mafunzo ni masomo yanayopatikana katika kazi ya fasihi. Kila kazi ya sanaa huwa
na ujumbe maalumu ambao msanii anataka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe
katika kazi za kifasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana ndani ya kazi
hiyo. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi wakati ambapo
dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito
zaidi ujumbe wa msingi.
• Migogoro
Ni hali ya kutokubaliana kimawazo, kimatendo kati ya wahusika. Migogoro
hii inaweza kuwa kati ya wahusika binafsi na kizazi kimoja au kati ya kizazi na
kingine. Pia inaweza kuwa kati ya watawala na watawaliwa, jamii na misukosuko
(misukumano) ya kijamii au kimazingira iliyomo katika eneo fulani.
• Falsafa
Kimsingi, falsafa ni elimu ya asili; busara au hekima. Falsafa ya msanii hugusiwa
kutokana na jinsi anavyoelewa matatizo ya jamii na jinsi anavyoyatolea suluhisho
kwa njia ya busara, amani na utulivu. Katika kazi za fasihi simulizi hususani hadithi
zile za paukwa pakawa, falsafa inayojitokeza ni ile isemayo kuwa maisha ni
mapambano ya wema dhidi ya ubaya na daima wema huushinda ubaya.
TANBIHI
Katika kuhakiki kazi za fasihi simulizi, kila kazi ina mbinu mahususi katika
kuichambua. Kwa mfano uchambuzi wa nahau, methali na misemo unatofautiana
sana na uchambuzi wa hadithi au mashairi.
• Umuhimu wa Uhakiki
Mara nyingi fasihi huwa ngumu kuielewa. Kuna wakati mtu anaweza kusoma au
kusikiliza kazi ya fasihi akashindwa kuelewa alichojaribu kueleza msanii. Hapa
ndipo uhakiki unahitajika ili kumwongoza katika kuelewa kazi hiyo.
Kwa hiyo, uhakiki wa kazi za fasihi simulizi una umuhimu mkubwa. Baadhi ya
umuhimu huo ni kama vile:
a) Kuwezesha kuelewa kazi ya fasihi na kuchunguza kama inatimiza sifa zote.
Kila kazi ya fasihi ina sifa zake. Kwa hiyo uhakiki unatusaidia kugundua
kwamba kazi ya fasihi inajaza sifa zake zote.
b) Kuwezesha kulinganisha kazi tofauti za fasihi. Hapa uhakiki unatuwezeshakupima uzito na ulegevu wa utunzi wa msanii.
c) Kuwezesha kupanua lugha yetu kwa sababu katika kazi ya sanaa kunatumika
msamiati, mifumo, semi na mambo mengine mengi yanayokuza lugha yetu.
d) Kuwezesha kuchambua na kumulika mafunzo na maonyo yanayopatikana
katika kazi za fasihi. Maonyo na mafunzo hayo yanaweza kutumiwa kwakujirekebisha au kuirekebisha jamii.
• Matatizo ya uhakiki
Hakuna jambo lisilokuwa na ila. Matatizo ya uhakiki ni mengi sana. Kwanza ni
vigumu kwa wahakiki kukubaliana kuwa hivi ndivyo ilivyo maana ya kazi ya sanaa
husika. Kila mhakiki huweza kusoma na kuelewa kazi hiyo kwa namna yake.
Pili, uhakiki wenyewe ni taaluma ngumu ambayo inahitaji kutumia bidii kubwa
ya kuweza kuitawala. Wahakiki wengi wanafanya uchambuzi na uchambuzi huo
ukichambuliwa ukaonekana bado una dosari. Jambo hili hutokana na mhakikikuwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo zinaweza kuwa :
-- Kutokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu sifa za utanzu unaohakikiwa,
-- Kutawaliwa kwa mhakiki na hisia zake zinazoweza kuleta upendeleo fulani,
-- Kutofuata misingi inayozingatiwa katika uhakiki.
Jibu maswali yafuatayo:
1. Ni ipi maana ya uhakiki?
2. Ni mambo gani tunayochunguza kwa kuhakiki kazi ya fasihi?
3. Taja na ueleze tabia za wahusika.
4. Ni tofauti gani iliyoko baina ya mandhali na muktadha?
12.5. Kusikiliza na Kuzungumza
13.1. Kusoma na Ufahamu: Kobe na Kijumbamshale
Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini
Hapo zamani za kale palikuwa na Kobe na Kijumbamshale. Kobe alikuwa
mnyamavu, mshindani pamoja na mpole. Kila wakati alikuwa hafanyi jambo lolote
ovyo ovyo wala kwa pupa. Kwake, kila jambo lilikuwa na mpango wake kabla ya
kulishughulikia kimatendo.
Kwa upande mwingine, Kijumbamshale alikuwa ndege mpinzani, mjuba, mpuuzi
na mwenye majivuno. Mara nyingi alikuwa anafanya kazi bila mpango.
Siku moja Kobe na Kijumbamshale walikutana njiani wote wakipunga upepo
huku wakielekea kwa kasri ya Malkia Tembo. Walisalimiana na kukaa chini kabla
hawajaendelea na safari. Kwa hiyo, walipata fursa ya kuongea sana. Maongezi yao
yalipokuwa yakiendelea, Kobe alishangaa sana kumwona Fisi amekuja akikimbia
mno. Alikuwa amechelewa kuhudhuria sherehe ya mtoto wa Malkia Tembo. Kobe
hakuamini macho yake na kumwonyesha Kijumbamshale, “Angalia pale jinsi Fisi
anavyokimbia kwa mwendo wa kasi. Anakimbia mbio kama umeme. Bila shaka
hakuna mnyama hata ndege yeyote anayeweza kumshinda katika mashindano
ya riadha.” Fisi aliwapitia bila kuwasalimia wakashangazwa na adabu yake.
Kijumbamshale hakuridhishwa hata kamwe na maoni ya Kobe kuhusu Fisi. Mara
moja alimgeukia na kumuuliza kwa dharau, “Je, una hakika kwa hayo yote ambayo
umeyatamka? Nani aliyekuambia kuwa Fisi yule anaweza kuthubutu kunishinda
mimi? Kama wewe ni mlemavu wa miguu na mabawa, usidhani kuwa sisi sote
ni sawa nawe.”
Kobe alijaribu kumsihi akisema, “Samahani rafiki yangu! Hii siyo sababu ya
kukasirika kwa bure! Ukweli mtupu ni kwamba mimi ninaamini kwamba Fisi
anaweza kunishinda katika zoezi la mashindano ya kukimbia. Lakini, wewe sahau
hilo! Huwezi, huwezi na huwezi hata kamwe! Maishani mwangu wanyama wawili
pamoja na ndege mmoja tu ndio niwaogopao katika mashindano ya namna hii.
Hao ni Fisi, Sungura pamoja na Tai. Wengine hapana!”
Kijumbamshale alikunja uso na kumwambia mwenzake, “Huna haya kuhakikisha
hayo mbele yangu? Kobe hakutaka jambo hili lipambe moto. Hivyo, aliamua
kutoa suluhu la kimatendo. “Acha tukubaliane kwenye mashindano ya kukimbia
kilomita mbili wakati wa dakika sitini. Atakayeibuka mshindi ndiye atakayekuwa
mheshimiwa kati yetu.” Kobe alipendekeza.
Bila kusita, Kijumbamshale alikubaliana na Kobe hivi wakiamua siku, mahali
pamoja, na wakati wa mashindano. Baada ya kutoka katika sherehe, Kobe
hakupata tena utulivu. Alianza kufikiria juu ya mbinu angetumia kujinyakulia
ushindi dhidi ya Kijumbamshale.
Siku moja kabla ya mashindano kuwadia, Kobe alikaa peke yake na kufikiri.
“Wazazi wangu kabla ya kuaga dunia, walinitolea maonyo ambayo sitayasahau
hata siku moja. Wakati mmoja waliniambia ‘Chelewa chelewa utamkuta mtoto
si wako’ na wakati mwingine ‘bandubandu humaliza gogo.” Kobe aliyakumbuka
mashauri ya wazazi. Kutokana na haya, alijisemea kimoyomoyo, “Linalowezekana
leo lisingoje kesho.” Papo hapo, aliamua kuandaa safari na kuelekea kwenye
uwanja wa mashindano asubuhi na mapema. Aliahidiana na jogoo kwamba
angemwamsha.
Jogoo alipowika alfajiri, Kobe alikuwa ameishatoka nyumbani kwake kuelekea
mahali pa mashindano. Njiani aliwakuta wanyama wengi waliokuwa wakisafisha
mbuga yao na kuwasalimu. Walipomuuliza sababu ya safari yake, aliwaeleza
kwamba alikuwa katika shindano la kukimbia. Isipokuwa nyani aliyempa motisha
kwa kumpa ndizi, wanyama wengine walishika mbavu kwa vicheko kwa kuwa
walikuwa wakijua uwezo wake wa kukimbia. Lakini yeye hakukata tamaaakaendelea na safari yake.
Kobe alitembea, akatembea na kutembea. Saa nane mchana, Kobe alikuwa
amesogelea mti mkubwa ambapo alikuwa amekubaliana na Kijumbamshale
kuwa kikomo cha mashindano. Wakati huo ndipo Kijumbamshale alikumbuka
kuwa siku hiyo ilistahili kuwa siku ya mashindano kati yake na Kobe. Alishtuka
kwa ghafla na kuruka haraka kwa mwendo usio wa kawaida. Aliruka na kuruka!
Lahaula! Alipokuwa umbali wa mita karibu mbili, Kobe alikuwa amejinyakulia
ushindi, hivi akishangilia kwa furaha tele.
Kijumbamshale alipomwona Kobe alipoteza nguvu za kuendelea kuruka na
kuanguka chini. Kobe alisikia huruma moyoni na kumsogelea Kijumbamshale,
“Pole sana ndugu yangu. Katika mashindano ni lazima kuwepo mshindi na
anayeshindwa. Lakini siyo mwisho wa dunia. Somo kubwa kutokana na
mashindano haya ni kwamba uwezo mkubwa wa kuruka pekee hautoshi, jambo
muhimu zaidi ni maandalizi, akili na maarifa ya kufanikisha lengo lolote”.
Kijumbamshale aliona haya na kufunga mdomo wake. Baada ya dakika chache,
alizinduka na kumwambia Kobe, “Leo nimeona kuwa kila kitu kinawezekana
maishani. Sina budi kukubali ushindi wako kwa sababu asiyekubali kushindwa
si mshindani. Nimepiga saluti kwa heshima zako mheshimiwa.” Na huu ndiomwisho wa hadithi.
Maelezo Muhimu kuhusu Aina za Maneno
Katika lugha ya Kiswahili kuna aina nane za maneno. Aina hizo ni kama vile
nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kihusishi, kielezi, kiunganishi na kihisishi.
Katika somo letu tutagusia aina nne yaani kihusishi, kihisishi, kiunganishi na
kielezi.
• Viunganishi
Viunganishi ni maneno yanayofanya kazi ya kuunganisha. Huonyesha uhusiano
baina ya neno na neno, fungu moja la maneno na fungu jingine au sentensi na
sentensi.
Mifano:
-- Unataka maji au juisi?
-- Anasoma kitabu badala ya kupiga ubwana.
-- Kufanikiwa maishani si bahati bali ni kujishughulisha na kujitolea.
-- Alishinda mtihani ijapokuwa alipatwa na ugonjwa mkali.
-- Alienda shuleni bila kupata chakula.
• Vihisishi
Vihisishi ni maneno ambayo yanaonyesha hisia za mtu za ndani kwa mujibu wa
hali na muktadha. Yanaonyesha hangaiko la moyo ama kudokeza mguso wa
moyo ama hata wa akili. Mifano:
-- Mtume! Umefika asubuhi hii!
-- Lo! Mvua imenyesha!
-- Salaa! Inawezekana mtu kunywa chupa ishirini za juisi!
• Vielezi
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi
hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi na vielezi vingine.
Kuna vielezi vya namna, vielezi vya wakati, vielezi vya mahali na vielezi vya kiasi.
Mifano:
-- Mwanafunzi yule ameshinda mtihani vizuri.
-- Mvua itanyesha kesho.
-- Wanyama huishi misituni.
-- Mvua ilinyesha mara mbili kwa mwezi.
• Vihusishi
Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano baina ya watu au vitu viwili au
zaidi. Kuna vihusishi vya mahali na vya wakati.
Mifano:
-- Nitakutembelea baada ya masomo .
-- Alisafiri nje ya nchi.
-- Ng’ombe hulala ndani ya zizi.
-- Amefika hapa kabla ya mvua kunyesha.
-- Wao wanaishi pamoja kwa amani.
Uhakiki wa hadithi za masimulizi
Uhakiki wa hadithi za masimulizi ni kazi au kitendo cha kuchambua na kufafanua
vipenge vya fani na maudhui katika hadithi hizo. Vipengele vya fani na maudhui
ni pamoja na wahusika, muundo, mtindo, dhamira, migogoro na ujumbe.
• Fani katika Hadithi za Masimulizi
Ikumbukwe kuwa fani ni ufundi au mbinu anayoitumia msanii wa fasihi ili kutoa au
kufikisha maudhui kwa watu aliowakusudia. Tunapohakiki hadithi ya masimulizi
kifani, tunachunguza wahusika, mtindo, muundo, mandhari, na mengineyo.
1. Wahusika
Wahusika ni watu, wanyama, vitu, hata viumbe vya kufikirika ambavyo msanii
wa hadithi hutumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika hadithi msanii
huwagawa wahusika katika makundi mawili: wahusika wakuu na wahusika
wadogo. Wahusika wadogo wanaweza kuwa watetezi au wakawa wapinzani.
Wahusika katika hadithi za masimulizi hutegemea aina ya hadithi simulizi. Kwa
mfano:
• Ngano: Hadithi ambayo wahusika wake ni mchanganyiko wa wanyama,
wadudu, mizimu, miungu, miti, watu, na viumbe visivyo na uhai kama
mawe, miamba, n.k.
• Hekaya: Hadithi ambayo wahusika wake kwa kawaida ni binadamu tu.
• Hurafa: Hadithi ambazo wahusika wake huwa ni wanyama wanaopewa
tabia na vitendo vya kibinadamu.
• Visasili: Hadithi hizi zinazohusu asili ya mambo fulani.
• Soga: Hizi ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Wahusika wake ni
watu wa kubuni lakini wanapewa majina ya watu walio katika mazingira
hayo.
• Visakale au Mighani: Ni hadithi ambazo wahusika wake ni watuwaliotenda matendo ya kishujaa na wanaosifiwa katika jamii fulani.
Tabia za wahusika katika hadithi za masimulizi
Wahusika katika hadithi simulizi hupewa tabia za aina mbalimbali. Hawa
wanaweza kuwa na tabia ya:
• Ubapa: tabia ya kutobadilika
• Uduara: tabia ya kubadilika
• Ufoili: tabia ya kutoonyesha msimamo
Kwa upande mwingine, katika hadithi za masimulizi tunatumia wanyana kwa
mara nyingi. Wanyama hawa huwakilisha binadamu katika jamii waishimo. Hili
ni kwa sababu utumiaji wa majina halisi ya watu unaweza kuzua ugomvi katika
jamii. Wanyama wanaotumiwa sana katika hadithi za masimulizi ni kama:
• Sungura: Mara nyingi Sungura hupewa tabia za ujanja, ndiyo sababu
huonekana mahali pengi kama Sungura-mjanja. Kwa hiyo, Sungura
huwakilisha watu wenye ujanja kwa madhumuni ya kula jasho la
wengine, kuwaangamiza adui zao au kuwaangusha mtegoni pamoja na
kuwategua wanyama wakubwa kama vile simba.
• Simba: Mnyama huyu hutumika mara nyingi kama kiongozi au mfalme.
Katika jamii ya wanadamu huwakilisha watu wenye ukali ambao
wakiongea husikika na huogopewa sana.
• Fisi: Mnyama huyu huonekana kama mhusika mwenye tamaa na ulafi
ambaye fikra zake zimetawaliwa na tamaa yake. Pia fisi hupewa tabia ya
uchoyo, woga pamoja na ujinga. Fisi hutumika kuwakilisha wanadamu
waroho, woga, wazembe na wajinga, wasiopenda kufikiria sana kwani
mawazo yao yametawaliwa na tamaa zao.
• Nyani: Katika hadithi, nyani hudhihirisha hekima na uwezo wa kufanya
uamuzi wa busara. Hutumika sana kama hakimu na huwakilisha viongozi
wenye hekima katika jamii.
• Nyoka: Mnyama huyu hupewa tabia ya hila na huwakilisha watu wenye
hila/ udanganyifu katika jamii.
• Kobe: Huwakilisha watu wanyamavu, ambao japo wanajua kufanya
kitu, hawapendi kuchangia, lakini mwisho huibuka washindi; watu
wasiokimbilia kufanya mambo.
• Ndovu: Huwakilisha watu wenye kimbelembele, ambao hujisifu na
kujitafutia umaarufu. Watu wa aina hii hupenda kuwa katika mstari wa
mbele japo huenda hawana ujuzi wa kutosha katika jambo hilo.
• Chui: Chui ni mnyama mkatili sana. Katika hadithi yeye huwakilisha
tabia ya uharifu.
• Kinyonga: Huyu huwakilisha tabia ya ugeugeu. Watu wenye tabia ya
aina hii hawaonyeshi msimamo mmoja.
• Kunguru: Huyu ni ndege mwoga sana. Katika hadithi yeye huwakilishawatu ambao ni waoga.
2. Mtindo
Mtindo ni mbinu ya kipekee kwa kila msanii katika ufundi wake wa kifasihi. Kwa
mfano, namna msanii anavyotumia lugha (nahau, misemo, methali, tamathali
za usemi) na anavyoteua msamiati wa msingi. Hii ni kwa sababu lugha ndiyo
wenzo mkubwa wa msanii katika kazi za fasihi. Isitoshe kwa kuchunguza mtindo
tunachunguza namna msanii anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi
ya kwanza, ya pili au ya tatu, anaweza kutumia nyimbo kwa ajili ya burudani, n.k.).
Kwa kutunga hadithi ya masimulizi msanii anaweza kutumia majina ya watu au
akatumia wanyama, wadudu, ndege, miungu na kadhalika.
3. Muundo
Ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia msanii katika kupangilia zoezi lake, mpangilio
na mtiririko wa hadithi, kwa upande wa visa na matukio. Msimuliaji anaweza
kufuatanisha matukio moja kwa moja (Msago) au akasimulia kwa kurukaruka
hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na
mwanzo (urejeshi).
Isitoshe, hadithi za masimulizi au za paukwa pakawa huwa na mipangilio maalum.Hadithi hizi huwa na fomula yake katika utangulizi na mwisho wake.
• Mianzo ya hadithi za kimapokeo
i) Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Kaondokea chanjagaa
Kajenga nyumba kakaa
Mwanangu mwana siti
Vijino kama chikichi
Cha kujengea kikuta
Na vilango vya kupitia
Atokeani!
Hadhira: Naam twaibu!
Mtambaji:Hapo zamani za kale………………….
ii) Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Sahaniǃ
Hadhira: Ya mcheleǃ
Mtambaji: Giza!
Hadhira: La mwizi!
Mtambaji: Baiskeli!
Hadhira: Ya mwalimuǃ n.k.
Mtambaji: Hadithi hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Mtambaji: Hadithi hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Mtambaji: Hapo zamani za kale palikuwepo na …………………………
iii) Msimulizi: Atokaeni!
Hadhira: Naam Twaibu!
Msimulizi: Kaondokea chanjagaa, n.k.
• Hadithi huwa pia na miisho yake
Hadithi ikimalizika tunasema: “Huu ndio mwisho wa hadithi” au “Hadithi
inakomea hapa.”
1. Mandhari
Ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza
kuwa halisi kama vile nyumbani, baharini, njiani, msituni, kijijini, mjini lakini
vyote vinavyojulikana au ya kufikirika kama vile kuzimuni, mbinguni, peponi na
kadhalika. Katika hadithi nyingi za masimulizi wanatumia mandhali pa kubuni kwasababu mandhari hayo huwa ni ya kujiundia.
2. Muktadha
Muktadha ni mazingira au hali ambamo tukio au jambo fulani hutendeka. Ni
kusema kuwa msanii huishi katika jamii na jamii huzungukwa na mazingira
mbalimbali. Mazingira haya yanaweza kuonekana katika hadithi. Ukichambua
hadithi za masimulizi utagundua mazingira yaliyokuwa yakiwazunguka wasanii.
Haya yote huonekana kulingana na msamiati na dhamira msanii alizotia ndani yahadithi.
Mbali na vipengele vilivyotajwa hapo juu, tunapochambua hadithi
tunaanzia kwa kutaja kichwa na mtunzi kama anajulikana. Lakini mara nyingi
watunzi wa kazi za masimulizi hawajulikani. Kazi za masimulizi ni mali ya jamii.
• Maudhui katika hadithi za masimulizi
Maana ya maudhui
Katika somo la kwanza katika mada hii tuliona kuwa, katika kazi ya fasihi, maudhui
ni jumla ya mambo yote yanayozungumzwa au yaliyomsukuma msanii kuisana
kazi yake.
Katika uhakiki wa hadithi za masimulizi kimaudhui, vipengele vifuatavyo ni lazima
vizingatiwe: dhamira, migogoro, mitazamo falsafa, ujumbe pamoja na msimamo
wa msanii.
1. Dhamira
Dhamira huelezwa kama wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika
kazi ya fasihi. Kwa kawaida, dhamira zinagawika katika makundi mawili, kuna
dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira zinazozungumziwa sana katika
hadithi za masimulizi ni uongozi, amani na maendeleo, mauaji, uroho, ujanja, hila,
uchoyo, upendo, uzalendo, ushirikiano, ujinga, uhaini, usaliti, wivu na kadhalika.
2. Migogoro
Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro
inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa
mbalimbali.Vilevile, migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, migogoro ya
nafsi, migogoro ya kisiasa, n.k. Katika hadithi za masimulizi nyingi tunakuta
migogoro kati ya wahusika wenye nguvu na wale wasio na nguvu na kwa mara
zote wenye nguvu huishia kwa kuanguka.
3. Falsafa
Kimsingi, falsafa ni elimu ya asili; busara au hekima. Falsafa ya msanii hugusiwa
kutokana na jinsi anavyoelewa matatizo ya jamii na jinsi anavyoyatolea suluhisho
kwa njia ya busara, amani na utulivu. Falsafa ya msanii wa hadithi za masimulizi
hugundulika unaposoma hadithi zake nyingi. Hapo ndipo utagundua mawazo au
saikolojia yake.
4. Ujumbe
Kila kazi ya sanaa huwa na ujumbe maalumu ambao msanii anataka uifikie jamii
aliyoikusudia. Ujumbe katika hadithi za masimulizi ni mafunzo mbalimbali ambayo
hupatikana ndani yake. Kwa kuwa hadithi zina umuhimu wa kuelimisha jamii
ndiyo maana kila unapomaliza kusoma au kusikiliza hadithi unaombwa kuelezasomo ambalo umepata.
Jibu maswali yafuatayo
1. Katika uhakiki wa fani ya hadithi tunachunguza nini ?
2. Taja na ueleze aina tano za hadithi.
3. Falsafa ya masanii ni nini?
4. Kwa sababu gani kuelewa usuli ni jambo muhimu?
• Mfano wa uhakiki wa hadithi ya masimulizi
1. Fani
• Kichwa cha hadithi: Kobe na Kijumbamshale
• Mtunzi: hajulikani.
• Wahusika
• Wahusika wakuu: Kijumbamshale, Kobe
• Wahusika wadogo: Jogoo, Fisi na Nyani na wanyama waliokuwa
wakisafisha mbuga.
• Watetezi: Jogoo (Alimwamsha Kobe) na Nyani (alimpatia ndizi)
• Wapinzani: Wanyama waliokuwa wakisafisha mbuga (walimcheka
Kobe).
• Tabia za wahusika: Kobe ni mhusika bapa kwa sababu hakubadilika
na Kijumbamshale ni mhusika duara kwa sababu alibadilika kimawazo
(alianzia kwa kupinga uwezo wa Kobe lakini mwishowe alikubali).
• Aina ya hadithi: Hurafa (wahusika ni wanyama na ndege).
• Mtindo: Katika hadithi hii masanii alitumia lugha ya kawaida. Hadithi
imeandikwa kwa lugha ya nathari (katika aya). Msanii alitia mazungumzo
katikati. Msanii alitumia:
-- Nahau: kunyakua ushindi (kushinda), kupunga hewa (kupumuzika), kukunja
uso (kukasirika)
-- Methali: Chelewachelewa utamkuta mtoto si wako, bandubandu huisha
gogo, linalowezekana leo lisingoje kesho.
-- Tamathali za usemi: kukimbia mbio kama umeme (tashbiha), takriri
(chelewachelewa, bandubandu).
• Muundo
-- Mwanzo wa hadithi ni “Hapo zamani za kale”. Na mwisho wake ni “Na huu
ndio mwisho wa hadithi.”
-- Msanii alitumia msago kwa sababu alisimulia moja kwa moja bila
kuchanganya matukio.
-- Msanii alitumia nafsi ya tatu kwa kusimulia hadithi yake. Lakini pia alitumia
nafsi ya kwanza na ya pili alipotumia mazungumzo kati ya Kijumbamshalena Kobe.
• Mandhari
Mahali panaposimuliwa hadithini ni njiani, kasri ya Malkia Tembo, Mbuga ya
wanyama: mandhari haya ni halisi kwa sababu ni mahali panapoweza kuonekana.
• Muktadha
Mtunzi alikuwa akiishi katika mazingira yenye dharau, bezo na upinzani kati ya
watu.
2. Maudhui
• Dhamira
• Dhamira kuu: kupingana kati ya kobe na Kijumbamshale
• Dhamira ndogo: usafi, harusi, michezo, dharau
• Migogoro
Migogoro inayopatikana katika hadithi hii ni migogoro kati ya wahusika
Kijumbamshale na Kobe (kutokubaliana kwa yule anayeweza kushinda mwingine
katika mbio).
• Falsafa
Falsafa ya mtunzi inatazamwa kwa kuangalia ni kipi ambacho mtunzi anaangalia
kuwa huo ndio ukweli katika maisha. Katika hadithi hii, inaonekana mtunzi
anaamini kwamba mafanikio katika maisha yanaletwa na uthubutu na maandalizi
ya kina.
• Ujumbe/ funzo
-- Kutodharauliana
-- Kukubali matokeo ya shindano-- Kuwa na adabu njema (Fisi alipitia wenzake bila kuwasalimu)
MADA YA 7 TANZU ZA FASIHI ANDISHI
Malengo ya Ujifunzaji
-- Kueleza kwa ufasaha maana ya fasihi andishi,
-- Kubainisha na kueleza tanzu za fasihi andishi,
-- Kutetea dhima au umuhimu wa fasihi andishi katika jamii,
-- Kutofautisha fasihi simulizi na fasihi andishi,-- Kutunga sentensi sahihi za Kiswahili kwa kuzingatia muundo wa sentensi.
14.1. Kusoma na Ufahamu: Mwangaza wa Maisha
Belinda na Didier ni wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Malezi Bora. Katika
mawasiliano yao wametetea umuhimu wa fasihi andishi katika kuimarisha
ushirikiano, umoja na maridhiano katika kijiji chao.
Belinda: Didy, hapa nimekufumbia fumbo aina ya chemshabongo. Tunu ya
kupendeza kwako utakapolifumbua wazi.
Didier: Tunu gani hiyo? Niambie Beli! Udadisi umeniingia mwilini kote! Maana
yake nimesumbuka sana!
Belinda: Didy umenaswa! Wewe hupenda kulipwa kabla ya kazi! Fumbua
kwanza zawadi baadaye.
Didier: Samahani dada! Sasa nimetega sikio. Lakini tafadhali usiniangushemtegoni wa kushindwa.
Belinda: Punguza wasiwasi kakangu! Fumbo ni hili: Ni kitu gani cha maajabu
kilichochangia kuleta umoja na maridhiano katika kijiji chetu cha
Ushujaa miaka miwili iliyopita?
Didier: Fumbo kali sana! Jambo ninalokumbuka ni kwamba kabla ya miaka miwili
iliyopita, hali ya umoja na maridhiano katika kijiji chetu ilikuwa imezorota
mno. Iliboreshwa baadaye na mchango wa maigizo ya tamthilia kutoka
Shirika la Burudani katika Jamii. Wachezaji waliigusia migogoro kadhaa
inayoiangamiza jamii yetu na kuitolea suluhisho ambalo matokeo yake
yalitufikisha kwenye ushirikiano, umoja na maridhiano.
Belinda: Hongera Didy kwa fumbuo hili! Fumbo la pili sasa: Maigizo hayo ya
tamthilia ni aina ya fasihi andishi. Kwa maoni yako, fasihi andishi ina
lengo gani katika jamii kwa ujumla?
Didier: Sitaki Beli, usininyang’anye! Kwanza kumbuka kuwa ahadi ni deni.
Zawadi yangu vipi?
Belinda: Hahaaaa! Bado fumbo halijafumbuliwa kikamilifu. Usikate tamaa,
tunaelekea mwishoni mwake.
Didier: Haidhuru! Fursa ninayo. Kwa maoni yangu, dhima ya fasihi yoyote ni
kuielimisha na kuionya jamii kwa ajili ya kurekebisha mienendo ambayo
si mizuri ndani ya wanajamii.
Belinda: Vizuri sana Didy! Je, ni hayo tu? Hukumbuki jinsi raia walivyofurahia
mdundo wa ngoma pamoja na sauti nyororo za wachezaji wa tamthilia
hiyo?
Didier: Kweli sana! Tamthilia ile ilikuwa na lengo jingine la kukuza lugha pamoja
na kuiburudisha jamii.
Belinda: Asante sana Didy kwa nia yako ya kuchunguza maendeleo ya jamii
yetu.
Didier: Inayofuata ni fursa ya kupewa zawadi yangu.
Belinda: Umeishapewa! Kuelewa umuhimu wa fasihi andishi katika maendeleo
ya jamii ni zawadi yenye thamani kubwa kuliko pesa au kitu kingine.
Didier: Jambo hilo naliunga mkono. Matokeo ya fasihi ile yalikuwa mwangaza
wa maisha katika jamii yetu.Maswali ya ufahamu
Maelezo muhimu
Tungo ni neno au nomino inayotokana na kitenzi “tunga.” Kutunga ni kuweka/
kushikamanisha vitu pamoja kwa kutumia kitu kama kamba au uzi kwa kupitishia
ndani yake. Tunaposhikamanisha vitu pamoja tunapata kitu kinachoitwa utungo
(katika umoja) au tungo (katika wingi). Kwa maana nyingine, utungo au sentensi
ni kundi la neno moja au maneno zaidi yenye kiima na kiarifa na inayofuata kanuni
za sarufi. Tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani
ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.
Muundo wa tungo
Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima huwa na vipengele vifuatavyo:
• Kiima: Ni sehemu katika sentensi ambayo hujaza sehemu ya mtenda au
mtendwa wa jambo linaloelezwa. Katika tungo kiima hutokea kushoto
mwa kitenzi.
• Kiarifa: Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayoarifu
tendo lililofanywa, linapofanywa au litakapofanywa. Kiarifa ndiyo
sehemu muhimu zaidi katika sentensi ambayo wakati mwingine huweza
kusimama pekee, kwani wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima.
Sentensi huwa na vifungu mbalimbali. Baadhi ya vifungu hivi ni vishazi na virai.
i) Virai
Kirai ni fungu la maneno lisilokuwa na kitenzi.
Kuna aina nne za virai:
• Kirai Nomino: ni fungu la maneno katika sentensi lenye nomino
(Kikundi Nomino/Kiima)
Mfano:
Wanafunzi wanapaswa kushirikiana darasani na nje ya darasa.
Walimu na wazazi wanaombwa kushughulikia pamoja maadili ya wanafunzi.
Elimu kuhusu usawa wa jinsia inatakiwa kwa watu wa marika yote.
• Kirai Kiwakilishi: ni fungu la maneno linalowakilisha nomino katikasentensi
Mfano:
Wenyewe watajenga nchi yao.
Atakayetumia dawa za kulevya atahatarisha maisha yake.
Wao walipanda miti mingi kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
• Kirai Kivumishi: ni fungu la maneno katika sentensi linalotupa habari
zaidi kuhusu nomino.
Mfano:
Matunda tuliyokuwa tunatarajia yatapatikana.
Mahali penye kutupwa taka ovyo panaambukiza magonjwa.
Mtu mkatili kuliko shetani hataleta mchango wowote katika jamii.
• Kirai Kielezi: ni fungu la maneno linaloelezea zaidi kuhusu kitenzi au
kivumishi.
Mfano:
Raia wanakatazwa kuponda mali yao ovyo ovyo.
Wanawake na wanaume wakishirikiana wataishi kwa amani na furaha milele na
milele
b) Vishazi
Kishazi ni sehemu ya sentensi yenye kitenzi. Kuna aina mbili za vishazi:
1. Kishazi huru: huwa na maana kamili na kinaweza kujisimamia chenyewe
kama sentensi.
Mfano:
Wanafunzi wote wa mwaka wa nne wamefanikiwa.
Anayeingia katika mambo ya uzinifu anaweza kuambukizwa ugonjwa wa ukimwi.
Tutafungua akaunti benkini kwa ajili ya kukuza kazi za kibiashara.
2. Kishazi Tegemezi: huhitaji kuunganishwa na kishazi kingine ili kuleta
maana iliyokusudiwa. Aghalabu huwa na kirejeshi k.v amba-, -enye, n.k
Mfano:
Kila mtu atapewa zawadi baada ya kuonyesha mwenendo mwema.Yeyote aliyehusika na vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi atahukumiwa.
Maelezo muhimu
Fasihi andishi ni sanaa itumiayo maandishi kufikisha ujumbe kwa hadhira
iliyokusudiwa.
Kwa maana nyingine, fasihi andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno
yaliyoandikwa kupitisha ujumbe.Ni sanaa inayopitishwa kwa njia ya maandishi.
Maelezo ya kuzingatia
• Kuburudisha jamii. Takribani vipera vyote vya fasihi huwa na kusudi la
kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.
• Kuelimisha. Fasihi hukusudia kuelimisha hadhira kuhusu jamii, mazingira,
n.k
• Kudumisha maadili katika jamii kwa kuelekeza, kuonya na kunasihi
hadhira jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
• Kuunganisha jamii. Fasihi huleta pamoja watu katika jamii. Kwa mfano,
katika nyimbo, miviga, vichekesho.
• Kukuza lugha. Aghalabu tungo zote za fasihi hutumia lugha. Isitoshe,
fasihi hutumia mbinu nyingi za lugha. Wasimulizi na wandishi wa fasihi
huhitaji kuwa na ukwasi wa lugha.
• Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Aghalabu kazi za fasihi
(hasahasa Fasihi Simulizi) huambatanishwa na desturi mbalimbali za
jamii husika.
• Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhirakufikiri sana ili kupata suluhisho. k.m vitendawili, ngano za mtanziko, n.k
15.1. Kusoma na Ufahamu: Akili ni Mali
Dhana ya utajiri inaendelea kuwa mada tata kati ya matajiri na watu duni. Kuna
wanaoshuku kuwa utajiri ni mali iliyorithiwa na vizazi vikongwe kwa vizazi vichanga.
Watu wanaotetea msimamo huu hukubali kwamba unapozaliwa na kulelewa
katika familia fukara hivyo utafariki katika hali ya wasiwasi na ya masumbuko.
Wengine huamini kuwa utajiri hushughulikiwa na hufikiwa kwa njia tofauti. Hivyo
utawasikia watu wakitoa madai kama ifuatavyo:
“Utajiri wa jamaa yule ulipatikana kwa matumizi ya hila za hali ya juu.”
“ Bwana yule hakuwa na nguo ya kujikinga dhidi ya upepo wala chumba cha
kulala. Lakini leo ameishajenga ghorofa tele. Ametajirika hivi majuzi baada ya
kutoka kuzimuni.”
“ Unamuona bibi yule katika gari lenye thamani kubwa sana! Habari zilizosambaa
zinasema kwamba alipandishwa vyeo miongoni mwa matajiri wanaojulikana
kwa ngazi ya kimataifa baada ya kuwadhulumu urithi watoto yatima aliokuwa
anawalea”.
Licha ya madai haya yote, mimi nina ushahidi wangu nilioshuhudia mimi
mwenyewe kwa macho yangu kuhusu familia moja ambayo ilipata utajiri
kwa kutegemea akili za kielimu. Familia ya bwana Bahati na bibie Fifi ilikuwa
haijulikani kamwe katika kijiji chao. Bahati alikuwa na kibarua katika kampuni
moja ya utangazaji habari wakati ambapo mkewe Fifi alikuwa anaajiriwa katika
duka la mavazi mjini. Ingawa wafanyakazi hawa walikuwa wanapata mshahara
kila mwezi, mahitaji ya kimaisha yalikuwa yanaendelea kuwasumbua. Siku moja,
bwana Bahati alijadiliana na mkewe juu ya njia mwafaka wangelipitia ili waridhike
na masharti ya kimaisha. Makubaliano yao yaliichagua shughuli ya kutumia akili
kama watu waliokuwa wasomi. Shughuli ya kuendeleza kazi za fasihi andishi
ilipewa alama asilimia tisini na tano. Baada ya mpango kuiva, Bahati na mkewe
waliunda kampuni yenye jina la Maisha ni Bora Ltd. Waliwaajiri wataalamu wa
kutunga hadithi fupi, riwaya, tamthila pamoja na mashairi. Miezi minane baadaye,
matunda ya kampuni yalikuwa yameanza kujitokeza. Matini za riwaya, hadithi fupi
pamoja na mashairi yalichapwa na kununuliwa kwa wingi wakati ambapo kundi
la wachezaji wa tamthilia lilikuwa likizunguka sehemu mbalimbali za nchi. Raiawalifurahia sana maadili kutoka tanzu hizo kwa sababu zilichangia sana kuijenga
Baadhi ya mada zilizokuwa zimegusiwa mno katika kazi hizo za fasihi andishi
ni kama vile umoja wa jamii, mapenzi, uhifadhi wa utamaduni, amani na utulivu
katika jamii pamoja na vita dhidi ya umaskini. Mafanikio kutoka kazi hizi zote
yaliiwezesha familia hii kununua magari ya kazi na ya ziara, kujenga nyumba ya
kisasa, kuishi kwa raha na kuwalipia karo watoto wao katika shule siyo tu za humu
Rwanda bali pia Marekani na Ulaya. Leo, familia ya bwana Bahati na mkewe Fifiimekuwa kielelezo kwa wasomi wote kuwa akili ni nywele, kila mtu ana zake.
15.3. Sarufi: Aina za tungo katika Kiswahili
Maelezo ya kuzingatia
Kimuundo na kimaana, tungo hujigawa katika aina tatu kuu kama ifuatavyo:
1. Tungo Sahili : Ni sentensi zenye kishazi kimoja na huwakilisha wazo
moja tu.
Mfano:
Tumeelewa faida za fasihi andishi.
Wanaume na wanawake huwa na haki sawa.
2. Tungo ambatano: Ni sentensi zenye zaidi ya kishazi huru kimoja na
huwakilisha mawazo mawili au zaidi. Aghalabu sentensi hizi hutumia
viunganishi (U) au alama za uakifishaji kama vile kituo (.) na nukta-nusu (;)
ili kubainisha wazo moja toka jingine.
Mifano:
Tulipanda miti kwa ajili ya kupigana dhidi ya mporomoko wa ardhi. Ardhi yetu
iliporomoka.
• Ingawa tulipanda miti kwa ajili ya kupigana dhidi ya mporomoko wa
ardhi, ardhi yetu iliporomoka.
Bwana Bahati na mkewe Fifi waliunda kampuni ya uandishi wa riwaya. Bwana
Bahati na mkewe Fifi waliwaajiri wafanyakazi wengi.
• Bwana Bahati na mkewe Fifi waliunda kampuni ya uandishi wa riwaya
na kuwaajiri wafanyakazi wengi.
Familia ya Bwana Bahati na mkewe Fifi ilijitafutia ajira. Familia ya Bwana Bahati
na mkewe Fifi ilitajirika.
• Familia ya Bwana Bahati na mkewe Fifi ilijitafutia ajira ikatajirika.
3. Tungo Changamano: Ni sentensi zinazoundwa kwa kuunganisha
kishazi huru pamoja na kishazi tegemezi au sentensi mbili kwa kutumia
o-rejeshi ili kuleta zaidi ya wazo moja.
Mifano:
- Tumepata maelezo ya kutosha kuhusu elimu ya usanifishaji. Tulikuwa tunaomba
maelezo hayo toka mwezi uliopita.
• Tumepata maelezo ya kutosha kuhusu elimu ya usanifishaji ambayo
tulikuwa tunayaomba toka mwezi uliopita.
- Shirika jipya lilitunga tamthilia hii. Ni tamthilia inayovutia sana.• Shirika jipya ndilo lililotunga tamthilia hii inayovutia sana.
Zingatia yafuatayo
Kuna tanzu nne kuu za fasihi andishi ambazo ni zifuatazo:
1. Hadithi fupi
2. Riwaya
3. Tamthilia
4. Mashairi yaliyoandikwa
A. HADITHI FUPI
Hadithi Fupi ni aina ya kazi andishi ambayo huwa fupi; na huangazia wazo mojakwa kurejelea kisa kimoja.
Hadithi fupi huwa na wahusika wachache na huchukua muda mfupi. Masuala
mbalimbali huzingatiwa katika hadithi fupi kama vile masuala ya kijamii, kisiasa,
kidini, kielimu, kiutamaduni, kiuchumi, n.k.
Mfano: Hadithi fupi za Alley Yusufu Mugenzi
Mifano mingine ya hadithi fupi za Kiswahili:
-- Kachukua Hatua Nyingine
-- Mayai Waziri wa Maradhi
-- Siku ya Mganga
-- Ngome ya Nafsi
B. RIWAYA
Riwaya ni kazi ya fasihi andishi ambayo huwa ndefu na aghalabu riwaya moja
hujaza kitabu kizima. Riwaya huwa na wahusika wengi na huangazia mawazo
kadhaa. Aidha, riwaya hufanyika katika mazingira mbalimbali na aghalabu
huchukua muda mrefu ikilinganishwa na hadithi fupi. Kazi hii huhusisha
binadamu,wanyama ama vitu vingine vinavyopewa uhai kama vile mizimu.
Kunazo aina nyingi za Riwaya katika Fasihi Andishi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano:
Riwaya sahili: Ni aina ya riwaya ambayo visa vyake husimuliwa moja kwa moja
na huwa rahisi kueleweka.
Riwaya changamano: Hii ni riwaya ambayo huhitaji kusomwa kwa makini
ili kueleweka. Aghalabu huwa na maudhui mengi na wahusika wengi ambao
wanachangia katika tatizo kuu katika riwaya hiyo. Hujengwa kwa taharuki ili
kuwavutia hadhira kutazamia jinsi tatizo kuu litakavyotatuliwa. Hutumia mbinu za
taharuki na visengere nyuma/mbele.
Riwaya ya kibarua: Ni riwaya ambayo hutumia muundo wa barua kuwasilishaujumbe wake.
Riwaya kiambo: Ni riwaya ambayo huhusisha masuala ya kawaida katika jamii.
Mfano wa riwaya:
Adili na Nduguze
Utengano
Siku Njema
Mwisho wa KosaKiu
C. TAMTHILIA
Tamthilia ni sanaa ambayo huwasilisha mchezo wa kuigiza kwa njia ya
maandishi. Majina ya wahusika huandikwa katika upande wa kushoto,
kisha koloni, halafu hufuatiwa na maneno halisi yaliyotamkwa na mhusika
huyo. Kwa maana nyingine,tamthilia ni mchezo wa kuigiza ulioandikwa
ili uigizwe jukwaani kwa kuwasilisha ujumbe kwa jamii.
Aina za jukwaa
Kuna aina mbili za jukwaa:
-- Jukwaa la akilini kama hali ya kujiundia akilini k.v. mchezo unaoigizwa
redioni.
-- Jukwaa la hadharani, yaani mahali ambapo maonyesho ya tamthilia
yanaigiziwa mbele ya watazamaji au wasikilizaji.
Aina za tamthilia
Tamthilia au mchezo wa kuigiza huwa na aina mbalimbali kulingana na dhamira
kuu inayoendelezwa. Utaipata tamthilia ya mapenzi, ya kihistoria, ya kisiasa, ya
kidini, ya kiuchumi, n.k. Tamthilia hizi zote huangukia baadhi ya makundi makuu
yafuatayo:
Tanzia
Ni aina ya tamthilia iliyojaa, huzuni ndani yake, mikasa, matokeo ya vifo na mateso
makali. Mwisho wa tamthilia za aina hii huwa ni wa masikitiko, maanguko na
hasara kubwa kwa mhusika mkuu au jamii inayoibushwa. Wengine huita aina hiitamthilia simanzi au trejedia.
Ramsa
Tamthilia zenye kuchekesha kutokana na utani, mzaha, kejeli, maneno
yaonyeshayo ujinga, n.k. Iwapo tamthilia hizi huwa na dhana ya uchekeshaji,
lengo lake ni kukosoa jamii, watawala na tabia mbaya na watu binafsi. Aina hii
huitwa tena Tamthilia cheshi au komedia.
Tanzia – ramsa
Tanzia – ramsa au simanzi – cheshi ni mchezo wenye sifa za ramsa, lakini ndani
ya uchekeshaji wake na tanzia kama vile kifo cha mhusika mkuu au kuanguka
kwa jamii. Pengine huitwa Trejikomedia.
Mfano wa tamthilia
Hawala ya Fedha
Kifo Kisimani
Shamba la Wanyama
Mstahiki Meya
D. MASHAIRI YALIYOANDIKWA
Ushairi ni utungo wa kisanaa unaotumia maneno ya mkato na lugha yenye
kuvutia (lugha teule na mpangilio fulani wa maneno badala ya kutumia lugha
natharia) na ambayo yamepangwa kwa urari wa mizani na vina maalum. Ushairi
unaweza kuwa kipera cha fasihi simulizi (nyimbo) na pia katika fasihi andishi kwa
sababu mashairi yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya kukariri na pia kwa njia ya
maandishi. Mashairi yanayoghaniwa badala ya kusomwa huitwa maghani.
Kuna aina kuu tatu za ushairi: Mashairi, Ngonjera, Tendi au Tenzi.
Mashairi:
Shairi ni mtungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum na kutumia lugha ya
mkato na mnato kwa kuelezea hisi na mawazo ya jamii husika na kuwasilisha
ujumbe fulani. Mashairi hugawika katika makundi mawili: mashairi ya kimapokeo
au mashairi arudhi na mashairi huru. Mashairi arudhi hutungwa kwa kufuata au
kuzingatia sheria na kanuni au kaida za utunzi kama vile kuzingatia vina, idadi
fulani ya mizani, mishororo na vipande vya mishororo. Kulingana na idadi ya
mishororo katika kila ubeti, mashairi huweza kugawika tena katika aina mbalimbalikama ifuatavyo:
1. Tamonitha ni shairi lenye mshororo mmoja kwa kila ubeti.
2. Tathnia ni shairi lenye mishororo miwili kwa kila ubeti.
3. Tathlitha ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti.
4. Tarbia ni shairi lenye mishoro minne kwa kila ubeti.
5. Takhmisa ni shairi lenye mishororo mitano kwa kila ubeti.
6. Tasdisa shairi lenye mishororo sita.
Ngonjera:
Ngonjera ni shairi lenye malumbano na majibizano kati ya watu wawili au zaidi.
Tenzi
Tenzi ni aina ya shairi ambayo ni mtungo mrefu wa kishairi unaoelezea habari au
masuala mbalimbali kishairi. Utenzi huwa hauna vina vya kati katika mistari yake
bali kila ubeti una vina vya namna moja katika mistari yake isipokuwa mstari wa
mwisho wa ubeti.
Kuna mambo mengine muhimu kuhusu shairi. Mishororo ya shairi huwa na
majina maalum.
Mwanzo huwa ni mshororo wa kwanza wa ubeti.
Mloto huwa ni mshororo wa pili wa ubeti.
Mlea huwa ni mshororo wa tatu wa ubeti
Kituo huwa ni mshororo wa mwisho wa ubeti.
Kuna aina mbili za vituo ambazo ni kituo kimalizio na kituo kibwagizo. Kituo
kimalizio ni kituo ambacho hakirudiwi mwishoni mwa kila ubeti katika shairi. Kituo
kibwagizo ni kituo kinachorudiwarudiwa mwishoni mwa kila ubeti.
Vipande au sehemu za mishororo ni zifuatazo:
Ukwapi: Ni kipande cha kwanza cha mshororo.
Utao: Ni kipande cha pili cha mshororo.Mwandamizi: Ni kipande cha tatu cha mshororo.
Dhima ya ushairi
Kama mtungaji wa kazi nyingine za fasihi, mshairi huwa na madhumuni yafuatayokwa jamii:
-- Kuburudisha
-- Kuhamasisha jamii
-- Kukuza sanaa na ukwasi wa lugha
-- Kuliwaza
-- Kuelimisha
-- Kuonya, kutahadharisha, kunasihi na kuelekeza
-- Kupitisha ujumbe fulani
-- Kusifia mtu au kitu
-- Kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii.
MADA YA 8 UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Malengo ya Ujifunzaji:
-- Kueleza uhakiki wa kazi za fasihi na umuhimu wake,
-- Kubainisha vipengele muhimu katika uhakiki wa kazi za fasihi andishi,
-- Kutofautisha fani na maudhui,
-- Kuhakiki kazi za tanzu mbalimbali za fasihi andishi,-- Kutumia kwa ufasaha viambishi rejeshi katika ngeli za majina mbalimbali.
16.1. Kusoma na Ufahamu: Uhakiki kama Kazi ya
Kitaalamu
Jinsi binadamu alivyo, na anavyomudu maisha yake ya kila siku, hutokana na
maarifa ya kielimu aliyoyapata darasani au katika tajiriba yake ya kimaisha. Aidha,
watu hujishughulisha na kazi mbalimbali. Kutokana na tofauti za kazi, utawakuta
mafundi katika kazi za ujenzi wa nyumba, mabingwa katika uwanja wa kiteknolojia,
wabobezi katika uchumi na wataalamu katika mambo ya fasihi au lugha kwa
ujumla. Hali kadhalika, jinsi dereva anavyojiamini katika uendeshaji wa gari,
ndivyo mhakiki wa kazi za fasihi anavyotawala katika uchambuzi au uchanganuzi
wa kazi za kifasihi zilizotungwa na wasanii.
Jambo hili linatupeleka kwenye maswali yafuatayo: Je, uhakiki unamaanisha nini?Kwa nini uhakiki? Ni jukumu gani mhakiki wa kazi za kifasihi anastahili kutimiza?
Kimsingi, kazi ya fasihi andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno
yaliyoandikwa kupitisha ujumbe, au ni sanaa inayowasilisha ujumbe kwa njia ya
maandishi. Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na hadithi fupi, tamthiliya, riwaya
pamoja na ushairi.
Kwa hiyo, msanii hatungi kwa kutunga tu ila huongozwa na kutawaliwa na misingi
ya kisanii katika ufundi wake. Katika mwelekeo huu, mhakiki hustahili kushiriki
katika uchunguzi wa kazi ya msanii iliyotolewa ili kuichunguza au kuitathmini.
Kwa hivyo, uhakiki ni kitendo cha kutathimini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni
juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalumu. Hali kadhalika,
uhakiki wa kazi za fasihi ni kitendo cha kuchambua, kutathmini na kuainisha kazi
ya fasihi ili kuona ubora na udhaifu wa kazi hiyo kwa kutumia kaida au vigezo
husika vya fani na maudhui.
Kutokana na maelezo haya, inaeleweka wazi kuwa mhakiki wa kazi za fasihi bila
shaka huwa ni mtaalamu au mwerevu katika uwanja wa kifasihi ambaye huwa na
uwezo au stadi za kuzisoma, kuzitafakari, na kuzitolea tathmini kazi za fasihi kwa
kujiegemeza katika mwelekeo wa kaida maalum zinazotakiwa kuzingatiwa katika
utunzi wa kazi hizo.
Hivyo basi hatuna budi kukubali kuwa mhakiki wa kazi za fasihi huwa na jukumu
au nafasi kubwa katika kazi za fasihi kama ifuatavyo:
Kwanza, mhakaki ndiye anayefafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kuelewa
vizuri kazi hiyo. Vilevile mhakiki huwaonyesha watunzi au wasanii wa kifasihi
ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hayo mhakiki huwawezesha watunzi
kutoa kazi bora zaidi.
Pengine, inambidi mhakiki huyo awe na habari kamili juu ya mwandishi au msanii
wa kazi inayohakikiwa. Maana yake, inambidi mhakiki kuelewa hali pamoja na
mazingira aliyokuwemo msanii kama kielelezo cha hisia zake au hoja zake. Hivi
mhakiki hufanikiwa kutambua sababu za hisia au dhamira zilizoendelezwa na
msanii katika kazi yake.
Hali kadhalika, mhakiki hutafakari kikamilifu kazi ya msanii na kuichambua
kimawazo au kimalengo kwa kudhihirisha au kutambua maudhui pamoja na
dhamira kuu au ndogondogo ambazo ni kiini cha kazi kamili ya msanii. Ili kulikabili
jukumu hili, mhakiki hutoa majibu kwa maswali yafuatayo:
Msanii anatufahamisha nini? Kazi ya msanii inamlenga nani? Anazungumzia nini
na ni suluhisho gani analotutolea kwa shida alizozitaja? Mwandishi ametungakatika kipindi gani cha historia na katika mazingira gani?
Mwisho, mhakiki huwa na jukumu la kurahisisha mawasiliano au kiungo kati
ya hadhira na mtunzi. Jukumu hili hujidhihirisha kwa njia ya uchunguzi wa jinsi
msanii alivyojenga sanaa yake ili ujumbe wake uwafikie walengwa husika, yaani
uhakiki wa lugha iliyotumiwa na msanii pamoja na jinsi alivyowajenga wahusika
katika kazi yake ya kifasihi. Kwa upande mwingine, uhakiki wa kazi mbalimbali
za kifasihi humsaidia msomaji wa kazi husika ya kifasihi kuielewa au kupatamwangaza fulani juu ya kazi husika aisomayo.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi –ye- ni kiambishi kinachotumika katika tungo kwa kurejelea
mawazo, nomino au mambo yaliyokwisha tajwa au yanayojulikana. Kiambishi hiki
hujihusisha tu na majina ya ngeli ya A-WA- katika umoja, yaani majina ya watu,
Mwenyezi Mungu, pamoja na wanyama. Matumizi ya kiambishi rejeshi – ye –
hutumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
Mfano: Aliyeshiriki
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-
Mfano: Mwanafunzi ambaye
Binadamu ndiye
• Mwishoni mwa kitenzi
Mfano: Mnyama alindaye
Tanbihi: Kiambishi rejeshi –ye- hugeuka – o - katika wingi.
Mfano:
i) Watu walioshiriki katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda
wamekamatwa na kupelekwa mahakamani.
ii) Wanafunzi ambao hufanya bidii hushinda mitihani bila tatitizo.iii) Mbwa ni wanyama walindao nyumba za watu.
MAELEZO MUHIMU YA KUZINGATIA
DHIMA ZA UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa
msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo:
• Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi:
Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi ya lugha na taswira, hivyo
mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia msomaji kuelewa vipengele hivikwa kuvifafanua kwa lugha rahisi.
• Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi:
Mhakiki anapoonyesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi fulani, watunzi
wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora zaidi.
• Hukuza uelewa wa mhakiki:
Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki hujiongezea maarifa ya lugha
pamoja na mambo yanayotokea katika jamii.
NAFASI YA MHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Mhahiki kama mtaalamu wa kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni
juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum, huwa na nafasi
kubwa katika kazi za fasihi. Mhakiki ndiye anayefafanua kazi ya fasihi ili hadhira
iweze kumwelewa vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo, hapa mhakiki anasaidia
kurahisisha mawasiliano kati ya hadhira na mtunzi. Vilevile mtunzi huwaonyesha
watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo, huwawezesha watunzikufanya kazi bora zaidi.
SOMO LA 17: TARATIBU ZA UHAKIKI WA KAZI ZAFASIHI ANDISHI
17.1. Kusoma na Ufahamu: Uhakiki wa Fani na Maudhui
Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha ujibu maswali ya ufahamu
hapo chini
Wahenga walisema kuwa maneno huwa na utamu zaidi yanaporudiwa. Kwa hiyo,
hatuna budi kukumbusha kuwa uhakiki ni kitendo cha kuchambua, kutathmini na
kuainisha kazi ya fasihi ili kuona ubora na udhaifu wa kazi hiyo kwa kutumia kaida
husika. Ili kazi yake itimizwe kwa hali mwafaka, mhakiki anastahili kupitia hatuatatu zifuatazo:
Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi; hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya
fasihi kwa kina na kuielewa vizuri.
Pili ni kuainisha na kuchambua mambo muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo
kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui.
Tatu ni kutoa tathmini au kuelezea ubora na udhaifu wa kazi inayohusika. Je,
tunapozungumzia vipengele vya fani na maudhui tunagusia nini?
Tuchukue mfano wa barua pepe ambayo imeandikwa ovyo ovyo bila kuzingatia
mitindo ya kisarufi, aya pamoja na alama za vituo. Mambo haya yote huchukuliwa
kama umbo la barua pepe hii. Kama umbo hili halivutii basi msomaji hatakuwa na
nia ya kuisoma barua pepe hii. Mfano wa pili ni wa nyumba inayong’aa kwa rangi
na mapambo mbalimbali yaliyoko kwenye nyumba hiyo. Atakayeiona nyumba
hii, atakuwa ameingiwa na udadisi wa kuingia ndani kwa sababu uzuri wake
umemvutia mtazamaji. Umbo hilo ndilo linalolinganishwa na fani katika kazi za
kifasihi.
Hivyo, baada ya kuvutiwa na umbo la barua pepe, hamu au hiari ya kusoma
ujumbe unaowasilishwa ndani yake itaongezeka. Ujumbe huo utatiliwa maanani
na kupokewa kwa urahisi. Vilevile, mtazamaji aliyeridhika na umbo la nyumba
hatasita kuingia ndani ili ashuhudie jinsi vifaa vya nyumbani vilivyo kama vile
mpangilio wake, vyumba, milango, n.k. Atatafakari yeye mwenyewe ujumbe
kuhusu uwezo mkubwa wa fundi aliyeijenga na kuipamba nyumba hiyo. Ujumbe
huu au yaliyomo hufananishwa wazi na maudhui katika kazi za fasihi.
Mifano ni wa msichana mrembo ambaye maumbile yake ni mithili ya malkia. Ah!
Utapatwa na bumbwazi utakapomtathmini kimwenendo au kitabia. Mfano huu
ungelikwenda sambamba na mtu ambaye unamkuta amevaa nguo za bei ghali
iwapo mwili wake unatoa harufu mbaya; maana yake mwezi mzima umemalizika
bila mtu huyo kuoga.
Kwa hiyo, kazi ya msanii wa fasihi yoyote huwekwa mikononi mwa mhakiki ili
kuitathmini na kutoa maoni yake kuhusu kufanikiwa au kutofanikiwa kwa msanii.
Kwa upande mmoja, kufaulu au kutofaulu kwa msanii hutokana na jinsi umbo au
fani ya kazi yake inavyowavutia walengwa wake.
Kwa upande mwingine, kufaulu au kutofaulu kwa msanii huelezwa na jinsi ujumbeuliokusudiwa kuwasilishwa ulivyopangwa toka mwanzoni hadi mwishoni.
17.2. Matumizi ya Msamiati
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi husika ni – o - . Kirejeshi hiki hujihusisha na ngeli za majina
kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi -
• Mwishoni mwa kitenzi
Mifano mbalimbali kuhusu ngeli za majina husika.
Ngeli ya majina Matumizi ya kirejeshi – o –
LI-YA- : Swali ambalo litaulizwa na wengi ndilo litakalojadiliwa.
zaidi – Maswali ambayo yataulizwa na wengi ndiyo yatakayojadiliwa zaidi.
KI-VI- : Kikulacho kinguoni mwako – Vikulavyo vingoni mwako.
MWELEKEO WA MAELEZOi) UHAKIKI WA HADITHI FUPI NA RIWAYA
Kwa kawaida, uhakiki wa kazi za fasihi andishi hutegemea FANI na MAUDHUI.
A. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA UHAKIKI WA FANI
Kama sura ya nje ya hadithi fupi au riwaya, fani hufanyiwa uhakiki kwa kuzingatia
vipengele fifuatavyo:
–– Wahusika
–– Muundo
–– Lugha
–– Mtindo
–– Mandhari
a) WAHUSIKA: Ni watu au viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu
katika kazi za fasihi.
Aina za wahusika: Wahusika wa hadithi fupi au riwaya hujigawa katika
makundi makuu mawili:
Wahusika wakuu: Mhusika mkuu ni mhusika mmoja au wawili ambao hujitokeza
kutoka mwanzo hadi mwisho wa hadithi fupi.
Wahusika wadogo: Ni aina ya wahusika muhimu sana ambao humsaidia
mhusika mkuu kuipa hadithi au riwaya mwelekeo wa kisanaa na kimaudhui.
Tabia za wahusika: Kutokana na majukumu yao, wahusika huonyesha tabia
za aina tatu:
Wahusika bapa: Ni aina ya wahusika ambao hawabadiliki kitabia kutoka
mwanzoni mpaka mwishoni mwa hadithi fupi.
Wahusika duara: Ni wahusika ambao wanabadilika kitabia kutokana na
mabadiliko ya mazingira.
Wahusika foili: Ni wahusika wenye tabia zinazobadilika kinusu. Wako kati ya
wahusika bapa na wahusika duara.
b) MUUNDO: Ni namna msanii anavyopanga visa vyake au fikra zake katika
hadithi fupi, yaani mtiririko wa visa na matukio. Kinachozingatiwa hapa ni jinsi
mwandishi alivyopanga kazi yake; mfano sura na sura, kisa na kisa au tukio
na tukio.
c) LUGHA: Kipengele cha lugha ni muhimu sana katika fasihi kwani ndicho
hutenganisha fasihi na sanaa nyinginezo. Matumizi ya lugha katika fasihi yapo
ya aina mbalimbali: kuna tamathaili za semi, misemo, nahau, methali, lahaja za
wahusika, uchaguzi wa msamiati, miundo ya sentensi.
Mifano ya tamathali za semi:
• Tanakali za Sauti: Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au
hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika.
Mfano: anguka pa!
• Tashbiha: Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti
kwa kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’.
• Tashihisi: Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye
uhai (sifa za kibinadamu).
• Takriri: Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili
kusisitiza ujumbe fulani.
• Ukinzani: Ukinzani ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha
maneno ya kinyume au yanayokinzana.
• Sitiari: Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutotumia
viunganishi ambapo kitu kimoja hufanywa kuwa sawa kabisa na kitu
kingine.
• Taswira: Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au
jambo fulani kwa msomaji.
• Taashira: Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina
au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na
kile kilichotumiwa.
• Majazi: Majazi ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina
yao halisi.
• Lakabu: Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubandikwa jina na wahusika
wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa
zake.
Chuku: Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe
fulani au kusifia kitu, kutilia chumvi.
d) MTINDO: Mtindo ni namna ambavyo mwandishi huipa hadithi yake sura ya
kifani na kimaudhui.
Mtindo ndio unaotofautisha wasanii. Katika mtindo tunachunguza sana
matumizi ya lugha.
e) MANDHARI: Mandhari ni mazingira au mahali tukio la hadithi fupi lilipotokea.
Kuna mandhari ya kubuni na mandhari ya kweli.
B. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA MAUDHUI
Maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa katika kazi ya fasihi.
Hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi
akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Mawazo na mafunzo haya hayazuki
hivihivi tu. Kwa hiyo wakati wa kuyachambua na kuyajadili ni lazima yahusishwe
na hali halisi ya kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi zilizopo katika jamii, hali hizi
ndizo zilimzaa, zilimlea na kumkuza msanii.
Wakati wa kuchambua kazi za kifasihi mhakiki ni lazima ajiulize amaswali
yafuatayo:
-- Je, msanii anatueleza nini?
-- Je, msanii kamtungia mtu wa tabaka gani?
-- Anamtukuza nani?
-- Anambeza nani?
-- Msanii anataka tuchukue hatua gani katika utatuzi wa matatizo
ayashughulikiayo katika kazi yake?
Maudhui hujengwa na vipengele muhimu vifuatavyo: Dhamira, ujumbe,
migogoro, msimamo wa msanii pamoja na falsafa yake.
a) Dhamira: Ni mawazo yanayojitokeza sana katika kazi ya fasihi. Ni jumla
ya maana anayoivumbua mwandishi aandikapo, na jumla ya maana
anayoitambua msomaji katika usomaji wake.
Kifasihi kuna aina mbili za dhamira yaani dhamira kuu na dhamira ndogondogo
Dhamira kuu ni kiini cha kazi ya fasihi, ni wazo kuu.
Dhamira ndogondogo ni mawazo madogomadogo ambayo hujenga dhamira
kuu.
b) Migogoro: Ni hali ya kutoelewana baina ya pande mbili yaani mtu na mtu,
mtu na kikundi au mtu mwenyewe na nafsi yake. Migogoro ni mivutano na
misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati
ya wahusika, familia zao au matabaka yao. Migogoro hii inaweza kuwa ya
kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni, kifalsafa, n.k.
c) Ujumbe: Ni funzo na maadili yaliyokusudiwa na mtunzi yaifikie jamii
aliyoilenga kufikisha kazi yake ya fasihi.
d) Falsafa: Ni imani na mwelekeo wa mwandishi kuhusu maisha katika jamii.
e) Msimamo wa msanii: Msimamo wa msanii kuhusu masuala mbalilmbaili
ya kijamii hubainishwa na mawazo, mafunzo, lengo na falsafa. Msimamo
ndio uwezao kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaotunga kazi
za fasihi zilizo na kiini na chimbuko moja. Kwa hiyo, msanii huweza
kuchukua msimamo wa kimapinduzi au wa kiyakinifu kulingana na jinsi
anavyoyazingatia maisha ya jamii inayozungumziwa.
C. MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA TAMTHILIA
Tamthilia au mchezo wa kuigiza huweza kuhakikiwa jukwaani au kupitia maandishi.
a) Uhakiki wa Kifani
Wahusika: Wahusika katika tamthilia huwa wengi pamoja na tabia zao
mbalimbali.Tamthilia huwa na wahusika halisi ambao wanajitetea jukwaani
kimatendo na kitabia wakati.
Muundo: Tamthilia huwa na sehemu tatu: Mwanzo, Katikati na Mwisho.
Sehemu zake zinatazamiwa kuingiliana, kujengana na kukamilishana. Muundo
katika tamthilia huangaliwa kwa kuzingatia idadi ya vitendo/ sehemu na idadi ya
maonyesho.
Mtindo: Tamthilia huwa na mgawiko wazi wa matendo na matukio kwa mujibu
wa sehemu na sura mbalimbali. Majina ya wahusika huandikwa katika upande
wa kushoto, kisha koloni, halafu hufuatiwa na maneno halisi yaliyotamkwa na
mhusika huyo.
Lugha: Tamthilia inatawaliwa na lugha ya mazungumzo katika majibizano au
hata mazungumzo pweke. Ucheshi, porojo au mizaha, tamathali za usemi na
onomatopia hutumiwa sana.
D. UHAKIKI WA MASHAIRI
Sawa na kazi nyingine za fasihi, uhakiki wa mashairi huzingatia fani na maudhui.a) Fani
Uhakiki wa fani ya shairi huzingatia muundo wake, yaani jinsi shairi lilivyoundwa
kwa kuangazia mizani, vina, mishororo n.k Aidha, ni muhimu kutaja aina na bahari
za shairi zinazohusiana na kila sifa uliyoitaja.
Idadi ya mishororo katika kila ubeti - Tumia idadi ya mishororo kubainisha
aina ya shairi hilo.
Kwa mfano: Shairi lina mishororo minne katika kila ubeti, kwa hivyo ni Tarbia.
Idadi ya mizani katika kila mshororo na katika kila kipande cha
mshororo.
Kwa mfano: Kila mshororo una mizani kumi na sita: nane katika utao na nane
katika ukwapi.
Idadi ya vipande katika kila mshororo - Taja ikiwa shairi lina kipande
kimoja, viwili, vitatu au vinne kisha utaje bahari yake.
Kituo, kiishio au kibwagizo - Ikiwa mstari wa mwisho umerudiwa rudiwa,
basi shairi lina kibwagizo au kiitikio, la sivyo lina kiishio.
Vina - Zingatia vina vya kati na vya mwisho kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
Kisha utaje ikiwa ni Mtiririko, Ukara au Ukaraguni.
Matumizi ya lugha: Mtindo wa lugha hurejelea namna mbalimbali ambazo
mshairi anatumia mbinu za lugha. Mshairi anaweza kutumia mbinu za lugha.
kama vile: Tanakali za sauti, Tamathali za semi, n.k.
Katika mtindo wa lugha mhakiki huchunguza uhuru wa msanii, yaani mshairi
hafungwi na kanuni za kisarufi za lugha katika utunzi wa shairi. Anaweza kufanya
makosa ya kisarufi kimakusudi ili shairi lizingatie umbo fulani.
b) Maudhui
Uhakiki wa maudhui ya shairi huzingatia vipengele vikuu ambavyo ni Dhamira(Dhamira kuu na dhamira ndogondogo) pamoja na Ujumbe.
SOMO LA 18: MFANO WA UHAKIKI WA TAMTHILIA
18.1. Kusoma na Ufahamu: Muhtasari wa Hawala ya Fedha
Familia ya Mzee Ibrahim CHANDE imetumiwa hawala ya fedha na mpwaye
anayesomea mjini London. Thamani ya hawala hiyo ni shilingi elfu mbili. Ibrahim
CHANDE anapaswa kuchukua kiasi cha shilingi mia tatu, kiasi kingine cha
shilingi miatano ampatie mama yake Abdul, mia tano zinazobakia amwekee
mpwa wake.
Hawala hii inaleta matumaini katika familia ya Ibrahim CHANDE. Familia
nzima wanafikiri kwamba umaskini na njaa vimemalizika. Kwa kuwa wake zake
CHANDE walitafuta mtu wa kuwasomea hawala ya fedha (kwa kuwa wao
hawakujua kusoma wala kuandika), habari inazagaa mahali pote na majirani zote
wanaarifiwa.
Watu kadha wa kadha wanakuja kukopa fedha na chakula kwenye familia
hiyo. Wengine wanamfuata Ibrahim CHANDE kila anapokwenda ili awasaidie
kutokana na fedha hizo.
Inambidi Ibrahim CHANDE aende kubadilisha hawala ya fedha posta. Anapofika
anaombwa kuwa na kitambulisho lakini anakikosa. Hana kitambulisho chochote
kile ila kadi ya chama isiyo na picha. Hivyo analazimika aende kwenye kituo chapolisi.
Anapofika, anaelezwa kuwa hawezi kuwa na kitambulisho kama hana picha.
Ibrahim CHANDE anamwendea AMBROZI ambaye ni mpigapicha. Anampiga
picha na kumwambia kurudi kesho yake baada ya kulipa shilingi thelathini. Kwa
bahati mbaya, anaporudi AMBROZI huyu anamnyang’anya picha pamoja na
pesa zake.
Siyo hayo tu, bali anamfanyia mabaya zaidi. MBAYE anajitolea kumsaidia
CHANDE kutoa fedha kwenye posta. Kwa upande mwingine, dada yake
CHANDE, yaani Mama Abdul, anakuja kudai pesa zake zilizoelezwa kwenye
barua iliyokuja pamoja na hawala hiyo.
Mzee huyo inambidi auze hereni za dhahabu za mkewe ili dada yake asiende
mikono mitupu. Ibrahim CHANDE hapumziki hata kidogo. Mwishowe, MBAYE
aliyejidai kumsaidia anamwambia kuwa fedha alizichukua kutoka posta lakini
akanyang’anywa na wezi akiwa njiani.
Matumaini yote ya Ibrahim CHANDE pamoja na wake zake yakafifia. Amne mke
wake wa pili akaamua kwenda zake na Mama Dogo, mke wake wa kwanzaakaenda kijijini kulima shamba.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi – o – kimehusishwa na majina ya ngeli za majina ya U-I na
U-ZI. Kimetumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-• Mwishoni wa kitenzi
Mifano mbalimbali kuhusu ngeli za majina husika
U-I- : Mti ulioanguka umefunga njia – Miti iliyonguka imefunga njia.
Mti ulioanguka ndio uliofunga njia – Miti iliyoanguka ndiyo iliyofunga njia.
U-ZI- : Tumenunua uzi unaoonekana vizuri - Tumenunua nyuzi zinazoonekana
vizuri.
MWELEKEO MUHIMU
UHAKIKI WA FANI
1. Wahusika na tabia zao
a) Wahusika wakuu
Ibrahim CHANDE ndiye mhusika mkuu katika tamthiliya “Hawala ya fedha”. Ana
wake wawili: MAMA DOGO na AMNE. Habadiliki kitabia tangu mwanzo hadi
mwisho wa mchezo, yeye ni mhusika bapa. Ubapa wake unadhihirishwa na
ujinga wake anaokumbana nao katika habari yote. Mhusika huyu hajui kusoma
wala kuandika. Isitoshe, hataki pia wake zake wawe na kisomo (uk. 4). Kwa kuwa
inaruhusiwa katika dini ya Uislam, Ibrahim CHANDE ana wake wawili. Katika
usemi wake wote kuna rejesta ya dini. Pengine anaonekana akitoa sadaka kwamaskini, wengine anakataa kuwapa.
Isipokuwa ujinga wake wa kutojua kusoma na kuandika, mzee huyu anaonyesha
moyo wa kusikiliza shida za watu wengine hasa hasa wale wanaotaka msaada
kutoka kwake.
b) Wahusika wadogowadogo au wasaidizi
i) Mama Dogo: Huyu ni mke wa kwanza wa Ibrahim CHANDE. Yeye na Amne
ni wake wenza. Hali yao ya uke wenza haiwatenganishi wala kuwafanya
wachukiane. Wanaonyesha ushirikiano tangu mwanzo hadi mwisho wa
mchezo. Mama Dogo anaonyesha busara katika maneno yake. Mfano
bayana ni usemi wake (uk. 41), pale ambapo anasema:”Afugaye punda
lazima ampendelee mlimaji nyasi. ” Katika usemi huu alitaka kuonyesha
namna ambavyo hakuna mtu pekee anayeweza kujitosheleza. Kama mtu
ana duka, anategemea wale ambao wanakuja kununua vitu katika duka hilo.
Kwa sababu hiyo, mtu yeyote anapaswa kutodharau mwenzake. Kila wakati,
Mama Dogo anaonekana akimtetea mumewe. Anaonekana akihangaishwa
na usalama wa mumewe. Ili watu wasiendelee kumfuata Ibrahim CHANDE
kwa ajili ya fedha, yeye alibuni kisingizio na kuwaambia watu kuwa mume
amenyang’anywa fedha hizo (uk. 36-38). “Alipopata pesa watu wakamvamia
(uk. 36).” “Majangili ndugu yakamvamia. Hata senti moja si yake. Mungu na
Mtume, sasa pesa zimekwenda na heshima yetu pia imekwenda.” Pengine
Mama Dogo anaonyesha imani katika Mungu. Anaamini kuwa Mwenyezi
Mungu hasahau waamini wake (uk. 1). Yeye ndiye anaweza kunusuru maisha
ya mtu aliye hatarini (uk. 37).
ii) AMNE: Huyu ni mke wa pili wa Ibrahim CHANDE, yaani mke mwenza
wa Mama Dogo. Tabia yake inaonyeshwa na ushirikiano anaokuwa nao
kati yake na Mama Dogo mbele ya mume wao. Amne ana tamaa ya kuwa
na kisomo. Anamwona mumewe kama mjinga wakati wowote anapomzuia
kwenda kusoma. Mwishoni mwa mchezo, anaonyesha tabia ya kutoweza
kuvumilia hali ya umaskini na njaa inayojitokeza katika familia yake. Alipokata
tamaa ya kupata fedha zilizokuwa kwenye hawala iliyotumwa na Abdul,
yeye aliamua kumtoroka mumewe.
iii) Mbarka: Ni mwenye duka. Kutokana na mazingira au hali mbalimbali,
yeye anabadilika kitabia. Wakati alipojua kuwa Ibrahim alikuwa na hawala
ya fedha, alifurahi sana na kumkopa mchele bila wasiwasi. Lakini alipopata
habari kuwa pesa za Ibrahim zimeibiwa, alikasirika na kuanza kumdai kwa
fadhaa. Mbarka anaonyesha tabia za uduara.
iv) Issa: Huyu ni rafiki yake Ibrahim CHANDE. Urafiki wao unatokana na
kuwa Issa anataka sehemu ya fedha alizonazo Ibrahim. Yeye anaonyesha
tabia ya unyonyaji. Kila alipoongozana na Ibrahim wakienda mjini, alitaka
Ibrahim amlipie basi. Unyonyaji wake unaonyeshwa pia na kunyang’anya
watu akitumia ujanja (uk. 16). Yeye alikuwa anaganda kwenye Ibrahimkama rubu ama kupe wagandavyo kwenye ng’ombe.
v) Ambrozi: Ni mwenye studio. Yeye anaonyesha tabia ya kunyanyasa watu
duni. Yeye ni mjangili: anachukua pesa za watu kwa bure na kuwadhulumu
ili wasije wakamdai fedha zao. Lugha anayoitumia ni ya matusi. Amandina
Lihamba alitumia katika mchezo wake wahusika wengine wa aina mbalimbali
ili kuonyesha hali halisi ya maisha. Mojawapo wa wahusika hao ni bapa
vielelezo. Majina yao yanaonyesha shughuli au tabia zao. Hao ni kama
mchuuzi, polisi, karani, maskini na kadhalika. Mhusika Abdul anasimamia
kundi la watu waliopata kisomo. Yeye anajua umuhimu wa kusoma, ndiyo
sababu alienda Landon. Vilevile, anajua wazazi wanahitaji msaada kutoka
kwa watoto wao wakati wakiwa na uwezo. Kwa sababu hiyo, alitumia
mjomba wake pamoja na mama yake hawala ya fedha.
2. Mtindo
Mtindo ni kiwango cha lugha alichotumia mwandishi katika Hawala ya fedha.
Lugha inayotumiwa ni ya mazungumzo kwani kitabu hiki ni cha mchezo wa
kuigiza, yaani tamthiliya. Vipengele vya lugha vilivyotumiwa na msanii ni tamathali
za usemi, nahau, methali, misemo na rejesta. Pengine alitumia lugha ya kawaida,
lugha inayoeleweka kwa wazungumzaji wengi wa lugha hiyo.
Tamathali za usemi
a) Sitiari: mifano, - Umaskini bila nyumba ni kifo - Madeni yatushika mpaka
pwani - Ndiye shetani mkubwa. b) Tashibiha - Kukusanyika kama sisimizi,
(uk. 3) - Asiponilipa haraka nitamganda kama rubu, (uk. 16)
ii) Methali - Kutoa ni moyo si utajiri, (uk. 13) - Ulimi hauna mfupa: ulimi
husema yote, yaani mazuri na mabaya. - Dawa ya moto ni moto: kwa tatizo
nzito lazima kauli nzito.
iii) Nahau - Kutia chumvi, - Chungu nzima, - Kukata kauli, - Kuwa na mkono
mrefu (kuwa na huruma kwa kila mtu), - Kuwa na mkono wa birika (kinyume
na kuwa na mkono mrefu), - Kukata tamaa, - Kufariki dunia/kuaga dunia.
3. Muundo
Msanii alitumia muundo wa moja kwa moja, yaani hakufanya mazungumzo
yanayoweza kutatanisha msomaji. Visa na matukio muhimu vya kuzingatia
katika Hawala ya fedha ni hivi vifuatavyo: - Taarifa inayomfikia Ibrahim CHANDE
yenye ujumbe wa kupelekewa hawala ya fedha na kuwa postani. - Tumaini la
kuwa hawala ya fedha ingemwokoa toka hali yake ya umaskini, - Kupanda kwa
madeni, - Harakati za kubadilisha hawala hiyo, - Kupanda kwa tumaini la Ibrahim,
- Matumaini ya kupata vitambulisho, - Kupatikana kwa fedha na kuibiwa kwake
(Upeo wa habari), - Kushuka chini kwa tumaini. Msanii amefaulu kujenga kiinikimoja kutokana na mchanganyiko wa matukio mbalimbali.
4. Mandhari
Mandhari inayozungumziwa mchezoni ni halisi. Kama tulivyoelezwa na mwandishi,
habari hii inatokea katika mji mdogo pwani mwa Afrika Mashariki.
UHAKIKI WA MAUDHUI
Katika uchunguzi wa maudhui ya mchezo wa Hawala ya fedha tunachambua
dhamira kuu pamoja na dhamira ndogo.
Dhamira kuu
a) Unyonyaji na kuharibika kwa urasimu
Unyonyaji ni hali ya kutegemea wengine bila ya kufanya kazi; ni hali ya kuishi kwa
jasho la mwingine. Katika tamthiliya Hawala ya fedha, unyonyaji unadhihirishwa
na hasa hasa na majirani wa Ibrahim CHANDE wanaotaka awasaidie kwa kila
hali baada ya kupata habari kuwa ametumiwa hawala ya fedha. Kuna wanaotaka
awakopeshe mchele na wengine fedha kiasi kwamba angetimiza hoja zao angebaki
mikono mitupu. Mhusika anayeonekana kuwa mnyonyaji kuliko wengine ni ISSA.
Huyu anamsindikiza Ibrahim CHANDE katika harakati za kubadilisha hawala ya
fedha ili apate fedha. Kila wanapoenda, ISSA anataka Ibrahim amlipie basi. Si
hayo tu, anataka ampatie fedha za kutumia katika shughuli mbalimbali. Watu
wengine wanaodhihirisha unyonyaji ni msichana aliyekutana na Ibrahim CHANDE
akimuomba msaada kwa mara nyingi. Pengine ni Ambrozi, aliyemnyang’anya
pesa zake alipoenda kujipigisha picha. Mhusika mwingine ni MBAYE aliyefaidi
hawala isiyokuwa yake. Kwa upande mwingine kuna katika mchezo huu, hali ya
kuharibika kwa urasimu. Ijulikane kuwa urasimu ni utaratibu wa kuendesha kazi
za kiofisi kulingana na kanuni za kiutawala. Katika mchezo (tamthiliya) Hawala ya
fedha kuharibika kwa urasimu kunatambulika kutokana na viongozi (makarani).
Hawa hawafanyi kazi yao kama ilivyo. Hawakutaka kuendesha haraka mambo ya
hawala ya fedha ya Ibrahim ili yeye awapatie rushwa.
b) Ujinga
Ujinga unatokana na tabia ya Ibrahim: kutojua kusoma, kukosa vitambulisho
ambavyo ni mambo muhimu ya raia. Kwa ajili ya kutojua, ilimbidi Ibrahim
kusomesha barua yake iliyohusu Hawala ya fedha. Habari hiyo ilipaswa kuwasiri lakini ilisambaa katika kijiji kizima kutokana na kuwa barua imesomeshwa.
Dhamira ndogo
-- Mvutano baina ya vizazi (vijana mbele ya wazazi)
Mvutano huu unaelezwa na msichana mmoja aliyetukana Ibrahim baada ya
kujionyesha mbele yake akitaka msaada na kunyimwa. Matusi yake yalienda
pamoja na kumsingizia kuwa alitaka kumtongoza. Mvutano unaonekana pia
kutokana na tabia ya Ambrozi aliyempiga Ibrahim badala ya kumpa picha zake.
Alionyesha dharau kubwa mbele yake mzee.
-- Nafasi ya mwanamke katika jamii
Katika nchi nyingi za Afrika, mwanamke huonekana kama kiumbe duni. Mambo
yanayokuwa vilevile katika Hawala ya fedha. Ibrahim anaonyesha dharau lakini
wanawake hawa wanaonekana kuwa washauri wa nafasi ya kwanza wa mume
wao.
AMNE anaonekana kujikomboa kutoka dharau hiyo. Katika kitabu hiki, wanawake
wengine huonekana wakitaka kusitisha mambo ya rushwa.
-- Nafasi ya fedha katika maisha ya kila siku
Dhamira hii inajidhihirisha katika matukio mengi ya habari hii. Kusomesha barua
lazima fedha, kutafuta vitambulisho ni fedha, picha, chakula, safari katika basi ni
mambo hayo hayo. Inadhihirika kuwa watu wote wametekwa na tamaa ya fedha
ili waweze kufanya shughuli zao mbalimbali. Mfano wa watu wanaotamani fedha
kuliko wengine ni ISSA. Huyu anatumia hila ili aweze kuzipata.
Migogoro
Tamathiliya hii ina migogoro kadhaa ambayo inajitokeza katika jamii.
Mgogoro wa kiuchumi ni wa kwanza kuonyeshwa. Mgogoro huu unaiathiri jamii
kwa kiwango kikubwa. Wenye nacho wameonyeshwa kuwa ndio wanyanyasaji
wakubwa wa watu wa chini. Mwandishi anaelekea kueleza kwamba si sawa
kuwa na matabaka ya wafanyakazi na wafanyiwa kazi, yaani, mabwana na
watwana (uk.38).
Mgogoro mwingine unatokana na hali ya mazingira kati ya ukale na
usasa. Mwandishi anaelezea athari za kutojua kusoma na kuandika katika jamii.Kwa upande mmoja kuna watu wangependa kusoma, wengine hawataki.
Ujumbe
Tamthiliya ya Hawala ya Fedha ina ujumbe ufuatao:
-- Ni vema kuwa na busara katika utekelezaji wa mambo.
-- Elimu ni ufunguo wa maisha. Ni vema kuwa na tahadhari wakati wa
matumizi ya fedha.
-- Uvivu ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya jamii.
Falsafa
Hawala ya Fedha ni tamthiliya inayoonyesha falsafa ya mapambano dhidi ya
unyonge. Msimamo wa mwandishi na falsafa yake juu ya maisha ni kuwa watu
wasikate tamaa wanapokutana na matatizo. Utatuzi wa matatizo si wa siku moja,unachukua muda na hatimaye ushindi lazima upatikane.
19.1. Kusoma na Ufahamu: Kila Mtoto na Koja Lake
Rubyogo lilikuwa jina la kupanga la bwana Ndizihiwe. Wengine walikuwa
wanamwita Nyangufi. Majina haya aliyapewa utotoni mwake alipokuwa na umri
wa miaka mitatu. Asili ya jina hili ilielezwa na kimo chake: Ndizihiwe alikuwa
mfupi sana na mwembamba. Aliyekuwa amemwona hakuwa anaamini kwamba
siku moja mtoto huyu atafikia kuwa mtu mzima. Wazazi wake walikuwa wakiishi
kwa mnung’uniko na fedheha katika kijiji cha Shengerero, Jimbo la Kusini nchini
Rwanda.
Ntawiheba (kifupi cha Ntawihebagihumeka) na mkewe Bazubagira walikuwa
wazazi wa Rubyogo. Huyu alikuwa mtoto wa pekee. Familia ya Rubyogo
ilikuwa inaishi kwa kutegemea kilimo tu. Wakati mmoja wazazi wake walikuwa
wakifurahia mavuno ya kilimo chao na wakati mwingine kulalamikia hali ya hewa.
Mathalan, hali hii ya malalamiko ilikuwa ikijitokeza hususan wakati wa maafa.
Ntawiheba na mkewe walifanya bidii kwa kumlea ipasavyo mtoto wao. Walimpatia
maadili toka utotoni hadi alipoanza elimu ya msingi. Ntawiheba na Bazubagira
walikuwa wanapendana sana na kushirikiana katika kazi zote za kijamii. Majirani
zao walikuwa wakiitamani familia yao. Aidha, Ntawiheba na mkewe walikuwakielelezo cha familia yenye kuishi kwa amani na masikilizano.
Siku moja alipokuwa katika kazi ya kupalilia migomba, Ntawiheba alipata fursa
ya kuwaza juu ya maisha ya familia yake kwa siku za baadaye. “Je, ni jambo
la busara kweli kumzaa mtoto mmoja tu na tena mwenye ulemavu wa kimo?”
Alijinung’unikia. Wazo la ukewenza lilimtawala sana na kumsumbua kupita
kipimo.
Alipofika nyumbani jioni, mkewe alimkaribisha kwa chakula cha mchana lakini
yeye alikipokea kwa shingo upande. Mkewe alipomtupia maneno ya utani,
mumewe hakumwonyesha jino. Aliendelea kuonyesha hali ya kukasirika na
kukosa furaha moyoni mwake. Hali hii ilimkera mkewe na kumsogelea, “Mume
wangu mpendwa, mbona hali yako leo imenitisha? Ni balaa ipi iliyokufikia siku ya
leo?”, mkewe alimbembeleza.
Ntawiheba alishindwa kuficha sababu za huzuni yake. “Mke wangu, miaka kumi na
miwili imemalizika tangu siku yetu ya kufunga ndoa. Maisha tuliyo nayo leo unajua
wazi haturidhiki nayo. Zaidi ya hayo, unaona jinsi mtoto wetu alivyo kimaumbile:
mfupi mithili ya kinu! Unadhani kuwa Rubyogo atatufuta machozi kweli? Mimi
ningependekeza nimwoe....” Anguka pa! Kabla hajakamilisha sentensi hii, mkewe
alipatwa na mshituko na kuanguka chini kama mtu aliyepoteza fahamu. Mumewe
huruma ilimwingia na kumhudumia kwa haraka. Alimwimbia wimbo mzuri sana
wa kimapenzi, ule ule ulioimbwa siku ya ndoa yao. Punde si punde, Bazubagira
alizinduka na kumwangalia mumewe machoni. Alimkumbatia na kuweka kichwa
chake kifuani pa mumewe. “Mume wangu, ni shetani yupi aliyekutembelea leo?
Kwa nini unataka nijitoe uhai kweli? Ni kosa gani nililokutendea kusudi uchukue
uamuzi huo wa kuniletea mkemwenza wa kunitesa? Kwa nini hukubali kwamba
mtoto ni sawa na mwingine hata akiwa na kasoro fulani? Mume wangu, kila
mtoto na koja lake!”, Bazubagira aliongea kwa huzuni mno machozi yakimtoka
machoni.
Ntawiheba alipigwa na bumbuwazi kisha akaangua kilio. Hali hii ilirudisha
kumbukumbu ya ahadi aliyoitoa siku ya ndoa yao mbele ya mkuu wa wilaya
pamoja na mbele ya kasisi kanisani. Hivyo, alimwomba mkewe msamaha na
kumwahidi kutofikiria tena hata siku moja mpango mbaya ule.
Ndizihiwe alipoingia shule za sekondari alionyesha maarifa yasiyo ya kawaida.
Toka mwaka wa kwanza hadi wa mwisho alikuwa akishika nafasi ya kwanza.
Vilevile, alichaguliwa kuendelea na elimu katika chuo kikuuu huko Huye. Hapo
alifanya maajabu zaidi! Mwishoni mwa masomo yake ilitangazwa nchini kote
kuwa ndiye aliyejinyakulia shahada yenye alama za juu katika Kitivo cha Uhasibu.
Miaka michache baadaye aliajiriwa kama meneja mkuu katika kampuni moja
ya kuagiza bidhaa kutoka nje za nchi. Ndizihiwe alionyesha ubingwa sana
katika kazi yake na kuongezewa mshahara wa kuridhisha. Aliwajengea wazaziwake nyumba ya kisasa na akawanunulia gari zuri la kutembelea. Leo wazazi
wake Ndizihiwe wanaishi kwa kheri na fanaka wakifurahia kuwasimulia hadithi
wajukuu wao wanne: Fany, Fils, Fiyette pamoja na Fisto. Katika masimulizi yao
hawakusahau kusisitiza kuwa “Akiba haiozi” pamoja na “Mtoto umleavyo ndivyo
akuavyo”.
Maelezo muhimu ya kuzingatia
Kiambishi rejeshi – o – kimehusishwa na majina ya ngeli za majina ya U- na PAM-
KU. Kimetumiwa kama ifuatavyo:
• Katikati ya kiambishi nafsi cha kitenzi na mzizi wa kitenzi.
• Kwenye mzizi wa amba- na ndi-
• Mwishoni mwa kitenzi
a) Uzalendo ambao una maana ni ule kutoka nchi asili.
b) Ushirikiano unaotakiwa kati ya mume na mke ndio utakaoimarisha uchumi
wa nchi yetu.
c) Mahali paliposafishwa ndipo pazuri.
d) Chumbani mnamoingia ndimo mnamolala.
e) Nchini tunamoishi ndimo tutakamofanikiwa.f) Mezani ambako kumewekwa vitabu kumesafishwa.
MWELEKEO MUHIMU
UHAKIKI WA FANI
1. Wahusika na tabia zao
a) Wahusika wakuu
Ntawiheba pamoja na Bazubagira ndio wahusika wakuu katika hadithi fupi
“Kila Mtoto na Koja Lake.” Ntawiheba ni mume wa Bazubagira. Ametawaliwa na
tabia ya ufoili: mwanzoni alikuwa amevumilia hali ya familia yake hivi akisikilizana
na mkewe. Baadaye amebadilisha mawazo na kutaka kumwoa mwanamke wa
pili. Mwishoni amekubali kushawishiwa na mkewe na kutulia. Ni mwanamume
mwenye huruma, mapenzi na msanii pia. Ameonyesha sanaa yake wakati
alipomwiimbia mkewe wimbo wa mapenzi ili asiendelee kupoteza akili.
Bazubagira ni mkewe. Yeye ameongozwa na tabia ya ubapa: habadiliki kimawazo
na msimamo wake ni kumlea mtoto wao Ndizihiwe ingawa kimo chake kilikuwa
kinaonekana kama kasoro. Ni mwanamke mwenye huruma na mapenzi: anatimiza
ahadi la ndoa yake na mumewe.
b) Wahusika wadogowadogo au wasaidizi
Ndizihiwe ndiye mhusika msaidizi. Mtoto wa pekee wa bwana Ntawiheba na
mkewe Bazubagira, Ndizihiwe ametumiwa na mwandishi kuendeleza mtiririko
wa visa au matokeo. Iwapo kimo chake kinazusha dukuduku au fedheha katika
familia yake, Ndizihiwe ni mtoto mwenye akili. Amemudu masomo yake na
kupewa vyeo. Ni mtoto mwenye mawazo ya kimaendeleo na ya kijamii.
2. Mtindo
Mwandishi ametumia mtindo wa nathari, yaani aya. Lugha iliyotumiwa ni ya
kawaida, rahisi kueleweka. Baadhi ya vipengele vya lugha vilivyotumiwa na
msanii kuna tanakali za sauti tamathali za usemi, nahau, methali.
Tanakali za sauti
Mfano: Anguka pa !
Konsonansi (mbinu ya kusawazisha konsonanti mwanzoni mwa neno) - Fils,Fiyette pamoja na Fisto.
Tamathali za usemi
a) Tashihisi (mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai
(sifa za kibinadamu) - ni shetani yupi aliyekutembelea leo?
b) Tashibiha (mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa
kutumia maneno ya kulinganisha; ‘kama’, ‘mithili ya’, ‘sawa na’) - mfupi
mithili ya kinu.
i) Methali – Kila mtoto na koja lake; Akiba haiozi; Mtoto umleavyo ndivyo
akuavyo.
ii) Nahau – kufanya bidii, kupokea kwa shingo upande, kuonyesha jino,
kufunga ndoa, kufuta machozi, kujitoa mhanga, kupatwa na bumbwazi.
3. Muundo
Msanii ametumia muundo wa moja kwa moja, yaani hakufanya mazungumzo
yanayoweza kutatanisha msomaji. Mtiririko wa visa na matukio muhimu
umejitokeza kama ifuatavyo :
-- Asili ya jina la Rubyogo
-- Maisha ya familia ya Ntawiheba na mkewe Bazubagira
-- Elimu na mafanikio ya Ndizihiwe
-- Upeo: Hali ya kheri na furaha katika familia ya Ndizihiwe na wazazi wake.
4. Mandhari
Hadithi fupi imetokea katika kijiji cha Shengerero, jimbo la kusini nchini Rwanda.
UHAKIKI WA MAUDHUI
Dhamira kuu
a) Haki za Watoto
Mtoto yeyote anastahili kupewa haki zake zote za kimaisha hata akiwa na ulemavu.
Ingawa Ndizihiwe alikuwa na ulemavu wa kimo alijiamini katika masomo yake
pamoja na kazi zake na kufurahia baadaye matokeo mazuri.
b) Maadili Mema
Malezi bora kwa watoto huchangia kukuza akili na mienendo mizuri. Ndizihiwealipata manufaa kutokana na maadili aliyopewa na wazazi wake.
Dhamira Ndogo
-- Mapenzi ya ndoa
Ntawigira na mkewe wasingelikuwa na mapenzi ya ndoa hawangelisikilizana
baada ya Ntawigira kubadilisha mawazo yake ya kutaka kumwoa mke wa pili.
Wimbo wa mapenzi aliomwimbia Bazubagira na kumfanya apate nafuu.
-- Uwazi
Mume na mke wanapaswa kuwa wazi katika mawasiliano yao ya kila siku. Jambo
la Ntawiheba kutoboa siri la mpango wake kwa mkewe lilichangia kupata suluhu
la mzozo uliokuwa umezuka.
-- Ukewenza
Dai la Ntawiheba kwamba kumwoa mke wa pili kutakuwa suluhisho la matatizo
katika jamii yake lilibanwa na pingamizi ya sheria. Hivyo sheria katika Jamhuri ya
Rwanda haikubali utamaduni wa ukewenza.
-- Umuhimu wa elimu
Baadaya ya kuhitimu masomo ya uhasibu katika chuo kikuu, Ndizihwe alipata
kazi katika kampuni ya kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi. Alipewa mshahara wa
kuridhisha akawajengea wazazi wake nyumba ya kisasa na akawanunulia gari la
kutembelea
Migogoro
Hadithi fupi imeizingatia migogoro mbalimbali:
Mgogoro wa kijamii: Kimo cha Ndizihiwe kilileta hali ya manung’uniko na
fedheha katika jamii yake;
Hali ya maisha ilimfanya Ntawiheba akimbilie kwenye suluhu ya ukewenza.
Mgogoro wa kisheria na kidini : Ahadi ya ndoa serikalini na kanisani ilikuwa
kizuizi kwa uamuzi wa Ntawiheba kumwoa mke wa pili.
Mgogoro wa kielimu : Mafanikio katika familia nyingi hutokana na kiwango
cha elimu wanajamii walicho nacho. Mathalan, Ndizihiwe alifaidika katika maishayake kutokana na elimu yake.
Ujumbe
-- Watoto wote wanapaswa kuwa na haki sawa hata walemavu
-- Wazazi wana jukumu la kuwapatia watoto wao maadili
-- Elimu ni msingi wa maendeleo ya jamii.
-- Mvumilivu hula mbivu.
Falsafa
Msimamo wa mwandishi na falsafa yake ni kwamba mtu yeyote, apende asipende,
huwa na nguvu kama sifa pamoja na udhaifu kama kasoro. Kwa hiyo, litakuwa
jambo la aibu kumnyima au kumnyanyasa mtu haki zake kwa kupitia vigezo vya
kimaumbile, kiafya, kikabila, kidini, kijamii, n.k. Hakuna mtu anayeweza kuthubutu
kudai kuwa huyu au yule atakuwa nini wakati ujao au atafaulu hiki na kushindwa
kile. Pengine, si vizuri kuzubaika mno kwa maisha uliyonayo leo kwa sababuhujui kitakochotokea kesho au kesho kutwa.
MAREJEO
Bakhressa,S.K. na Wenzake (2008). Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi.
Darasa la Saba. Oxford University Press, East Africa Ltd, Elgon Road, Upper
Hill, Nairobi, Kenya.
Bakhressa, S.K. na Wenzake (2008). Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi.
Darasa la 8. Oxford University Press, East Africa Ltd, Elgon Road, Upper Hill,
Nairobi, Kenya.
Hererimana, F. (2017). Tujivunie Lugha Yetu. Kitabu cha Mwanafunzi, Kidato
cha 5. MK Publishers (R) Ltd. Kigali, Rwanda.
Kenya Literature Bureau (2006). Kiswahili kwa Darasa la nane. Kitabu cha
Wanafunzi. Kenya Literature Bureau, Nairobi, Kenya.
Kihore, Y.M. na Wenzake (2012). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu, Sekondari
na Vyuo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Tanzania.
Massamba, D.P.B. na Wenzake (2009). Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu,
Sekondari na Vyuo. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Tanzania.
Ndalu, A.E. (2016). Masomo ya Kiswahili Sanifu. Kitabu cha mwanafunzi.
Kidato cha 2. Moran (E.A) Publishers Limited.
Niyirora, E. & Ndayambaje, L. (2012). Kiswahili Sanifu kwa Shule za Sekondari.
Kitabu cha Mwanafunzi kidato cha tano, Tan Prints (India) Pvt. Ltd.
Nkwera, F.M.V (1979). Sarufi na Fasihi, Sekondari na Vyuo.Tanzania Publishing
House, Dar es Salaam,Tanzania.
Ntawiyanga, S. na Wenzake (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo
wa Lugha, Kidato cha 5. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
Ntawiyanga, S. na Wenzake (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo
wa Lugha, Kidato cha 6. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
Waititu, F. na Wenzake (2008). Kiswahili Fasaha. Kitabu cha Mwanafunzi.
Kidato cha tatu. Oxford University Press, East Africa Ltd, Nairobi, Kenya.TUKI (2004): Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la pili. Oxford University Press.