MADA YA 7 TANZU ZA FASIHI ANDISHI
Malengo ya Ujifunzaji
-- Kueleza kwa ufasaha maana ya fasihi andishi,
-- Kubainisha na kueleza tanzu za fasihi andishi,
-- Kutetea dhima au umuhimu wa fasihi andishi katika jamii,
-- Kutofautisha fasihi simulizi na fasihi andishi,-- Kutunga sentensi sahihi za Kiswahili kwa kuzingatia muundo wa sentensi.
14.1. Kusoma na Ufahamu: Mwangaza wa Maisha
Belinda na Didier ni wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Malezi Bora. Katika
mawasiliano yao wametetea umuhimu wa fasihi andishi katika kuimarisha
ushirikiano, umoja na maridhiano katika kijiji chao.
Belinda: Didy, hapa nimekufumbia fumbo aina ya chemshabongo. Tunu ya
kupendeza kwako utakapolifumbua wazi.
Didier: Tunu gani hiyo? Niambie Beli! Udadisi umeniingia mwilini kote! Maana
yake nimesumbuka sana!
Belinda: Didy umenaswa! Wewe hupenda kulipwa kabla ya kazi! Fumbua
kwanza zawadi baadaye.
Didier: Samahani dada! Sasa nimetega sikio. Lakini tafadhali usiniangushemtegoni wa kushindwa.
Belinda: Punguza wasiwasi kakangu! Fumbo ni hili: Ni kitu gani cha maajabu
kilichochangia kuleta umoja na maridhiano katika kijiji chetu cha
Ushujaa miaka miwili iliyopita?
Didier: Fumbo kali sana! Jambo ninalokumbuka ni kwamba kabla ya miaka miwili
iliyopita, hali ya umoja na maridhiano katika kijiji chetu ilikuwa imezorota
mno. Iliboreshwa baadaye na mchango wa maigizo ya tamthilia kutoka
Shirika la Burudani katika Jamii. Wachezaji waliigusia migogoro kadhaa
inayoiangamiza jamii yetu na kuitolea suluhisho ambalo matokeo yake
yalitufikisha kwenye ushirikiano, umoja na maridhiano.
Belinda: Hongera Didy kwa fumbuo hili! Fumbo la pili sasa: Maigizo hayo ya
tamthilia ni aina ya fasihi andishi. Kwa maoni yako, fasihi andishi ina
lengo gani katika jamii kwa ujumla?
Didier: Sitaki Beli, usininyang’anye! Kwanza kumbuka kuwa ahadi ni deni.
Zawadi yangu vipi?
Belinda: Hahaaaa! Bado fumbo halijafumbuliwa kikamilifu. Usikate tamaa,
tunaelekea mwishoni mwake.
Didier: Haidhuru! Fursa ninayo. Kwa maoni yangu, dhima ya fasihi yoyote ni
kuielimisha na kuionya jamii kwa ajili ya kurekebisha mienendo ambayo
si mizuri ndani ya wanajamii.
Belinda: Vizuri sana Didy! Je, ni hayo tu? Hukumbuki jinsi raia walivyofurahia
mdundo wa ngoma pamoja na sauti nyororo za wachezaji wa tamthilia
hiyo?
Didier: Kweli sana! Tamthilia ile ilikuwa na lengo jingine la kukuza lugha pamoja
na kuiburudisha jamii.
Belinda: Asante sana Didy kwa nia yako ya kuchunguza maendeleo ya jamii
yetu.
Didier: Inayofuata ni fursa ya kupewa zawadi yangu.
Belinda: Umeishapewa! Kuelewa umuhimu wa fasihi andishi katika maendeleo
ya jamii ni zawadi yenye thamani kubwa kuliko pesa au kitu kingine.
Didier: Jambo hilo naliunga mkono. Matokeo ya fasihi ile yalikuwa mwangaza
wa maisha katika jamii yetu.Maswali ya ufahamu
Maelezo muhimu
Tungo ni neno au nomino inayotokana na kitenzi “tunga.” Kutunga ni kuweka/
kushikamanisha vitu pamoja kwa kutumia kitu kama kamba au uzi kwa kupitishia
ndani yake. Tunaposhikamanisha vitu pamoja tunapata kitu kinachoitwa utungo
(katika umoja) au tungo (katika wingi). Kwa maana nyingine, utungo au sentensi
ni kundi la neno moja au maneno zaidi yenye kiima na kiarifa na inayofuata kanuni
za sarufi. Tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani
ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.
Muundo wa tungo
Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima huwa na vipengele vifuatavyo:
• Kiima: Ni sehemu katika sentensi ambayo hujaza sehemu ya mtenda au
mtendwa wa jambo linaloelezwa. Katika tungo kiima hutokea kushoto
mwa kitenzi.
• Kiarifa: Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayoarifu
tendo lililofanywa, linapofanywa au litakapofanywa. Kiarifa ndiyo
sehemu muhimu zaidi katika sentensi ambayo wakati mwingine huweza
kusimama pekee, kwani wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima.
Sentensi huwa na vifungu mbalimbali. Baadhi ya vifungu hivi ni vishazi na virai.
i) Virai
Kirai ni fungu la maneno lisilokuwa na kitenzi.
Kuna aina nne za virai:
• Kirai Nomino: ni fungu la maneno katika sentensi lenye nomino
(Kikundi Nomino/Kiima)
Mfano:
Wanafunzi wanapaswa kushirikiana darasani na nje ya darasa.
Walimu na wazazi wanaombwa kushughulikia pamoja maadili ya wanafunzi.
Elimu kuhusu usawa wa jinsia inatakiwa kwa watu wa marika yote.
• Kirai Kiwakilishi: ni fungu la maneno linalowakilisha nomino katikasentensi
Mfano:
Wenyewe watajenga nchi yao.
Atakayetumia dawa za kulevya atahatarisha maisha yake.
Wao walipanda miti mingi kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
• Kirai Kivumishi: ni fungu la maneno katika sentensi linalotupa habari
zaidi kuhusu nomino.
Mfano:
Matunda tuliyokuwa tunatarajia yatapatikana.
Mahali penye kutupwa taka ovyo panaambukiza magonjwa.
Mtu mkatili kuliko shetani hataleta mchango wowote katika jamii.
• Kirai Kielezi: ni fungu la maneno linaloelezea zaidi kuhusu kitenzi au
kivumishi.
Mfano:
Raia wanakatazwa kuponda mali yao ovyo ovyo.
Wanawake na wanaume wakishirikiana wataishi kwa amani na furaha milele na
milele
b) Vishazi
Kishazi ni sehemu ya sentensi yenye kitenzi. Kuna aina mbili za vishazi:
1. Kishazi huru: huwa na maana kamili na kinaweza kujisimamia chenyewe
kama sentensi.
Mfano:
Wanafunzi wote wa mwaka wa nne wamefanikiwa.
Anayeingia katika mambo ya uzinifu anaweza kuambukizwa ugonjwa wa ukimwi.
Tutafungua akaunti benkini kwa ajili ya kukuza kazi za kibiashara.
2. Kishazi Tegemezi: huhitaji kuunganishwa na kishazi kingine ili kuleta
maana iliyokusudiwa. Aghalabu huwa na kirejeshi k.v amba-, -enye, n.k
Mfano:
Kila mtu atapewa zawadi baada ya kuonyesha mwenendo mwema.Yeyote aliyehusika na vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi atahukumiwa.
Maelezo muhimu
Fasihi andishi ni sanaa itumiayo maandishi kufikisha ujumbe kwa hadhira
iliyokusudiwa.
Kwa maana nyingine, fasihi andishi ni aina ya sanaa ambayo hutumia maneno
yaliyoandikwa kupitisha ujumbe.Ni sanaa inayopitishwa kwa njia ya maandishi.
Maelezo ya kuzingatia
• Kuburudisha jamii. Takribani vipera vyote vya fasihi huwa na kusudi la
kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.
• Kuelimisha. Fasihi hukusudia kuelimisha hadhira kuhusu jamii, mazingira,
n.k
• Kudumisha maadili katika jamii kwa kuelekeza, kuonya na kunasihi
hadhira jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
• Kuunganisha jamii. Fasihi huleta pamoja watu katika jamii. Kwa mfano,
katika nyimbo, miviga, vichekesho.
• Kukuza lugha. Aghalabu tungo zote za fasihi hutumia lugha. Isitoshe,
fasihi hutumia mbinu nyingi za lugha. Wasimulizi na wandishi wa fasihi
huhitaji kuwa na ukwasi wa lugha.
• Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Aghalabu kazi za fasihi
(hasahasa Fasihi Simulizi) huambatanishwa na desturi mbalimbali za
jamii husika.
• Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhirakufikiri sana ili kupata suluhisho. k.m vitendawili, ngano za mtanziko, n.k
15.1. Kusoma na Ufahamu: Akili ni Mali
Dhana ya utajiri inaendelea kuwa mada tata kati ya matajiri na watu duni. Kuna
wanaoshuku kuwa utajiri ni mali iliyorithiwa na vizazi vikongwe kwa vizazi vichanga.
Watu wanaotetea msimamo huu hukubali kwamba unapozaliwa na kulelewa
katika familia fukara hivyo utafariki katika hali ya wasiwasi na ya masumbuko.
Wengine huamini kuwa utajiri hushughulikiwa na hufikiwa kwa njia tofauti. Hivyo
utawasikia watu wakitoa madai kama ifuatavyo:
“Utajiri wa jamaa yule ulipatikana kwa matumizi ya hila za hali ya juu.”
“ Bwana yule hakuwa na nguo ya kujikinga dhidi ya upepo wala chumba cha
kulala. Lakini leo ameishajenga ghorofa tele. Ametajirika hivi majuzi baada ya
kutoka kuzimuni.”
“ Unamuona bibi yule katika gari lenye thamani kubwa sana! Habari zilizosambaa
zinasema kwamba alipandishwa vyeo miongoni mwa matajiri wanaojulikana
kwa ngazi ya kimataifa baada ya kuwadhulumu urithi watoto yatima aliokuwa
anawalea”.
Licha ya madai haya yote, mimi nina ushahidi wangu nilioshuhudia mimi
mwenyewe kwa macho yangu kuhusu familia moja ambayo ilipata utajiri
kwa kutegemea akili za kielimu. Familia ya bwana Bahati na bibie Fifi ilikuwa
haijulikani kamwe katika kijiji chao. Bahati alikuwa na kibarua katika kampuni
moja ya utangazaji habari wakati ambapo mkewe Fifi alikuwa anaajiriwa katika
duka la mavazi mjini. Ingawa wafanyakazi hawa walikuwa wanapata mshahara
kila mwezi, mahitaji ya kimaisha yalikuwa yanaendelea kuwasumbua. Siku moja,
bwana Bahati alijadiliana na mkewe juu ya njia mwafaka wangelipitia ili waridhike
na masharti ya kimaisha. Makubaliano yao yaliichagua shughuli ya kutumia akili
kama watu waliokuwa wasomi. Shughuli ya kuendeleza kazi za fasihi andishi
ilipewa alama asilimia tisini na tano. Baada ya mpango kuiva, Bahati na mkewe
waliunda kampuni yenye jina la Maisha ni Bora Ltd. Waliwaajiri wataalamu wa
kutunga hadithi fupi, riwaya, tamthila pamoja na mashairi. Miezi minane baadaye,
matunda ya kampuni yalikuwa yameanza kujitokeza. Matini za riwaya, hadithi fupi
pamoja na mashairi yalichapwa na kununuliwa kwa wingi wakati ambapo kundi
la wachezaji wa tamthilia lilikuwa likizunguka sehemu mbalimbali za nchi. Raiawalifurahia sana maadili kutoka tanzu hizo kwa sababu zilichangia sana kuijenga
Baadhi ya mada zilizokuwa zimegusiwa mno katika kazi hizo za fasihi andishi
ni kama vile umoja wa jamii, mapenzi, uhifadhi wa utamaduni, amani na utulivu
katika jamii pamoja na vita dhidi ya umaskini. Mafanikio kutoka kazi hizi zote
yaliiwezesha familia hii kununua magari ya kazi na ya ziara, kujenga nyumba ya
kisasa, kuishi kwa raha na kuwalipia karo watoto wao katika shule siyo tu za humu
Rwanda bali pia Marekani na Ulaya. Leo, familia ya bwana Bahati na mkewe Fifiimekuwa kielelezo kwa wasomi wote kuwa akili ni nywele, kila mtu ana zake.
15.3. Sarufi: Aina za tungo katika Kiswahili
Maelezo ya kuzingatia
Kimuundo na kimaana, tungo hujigawa katika aina tatu kuu kama ifuatavyo:
1. Tungo Sahili : Ni sentensi zenye kishazi kimoja na huwakilisha wazo
moja tu.
Mfano:
Tumeelewa faida za fasihi andishi.
Wanaume na wanawake huwa na haki sawa.
2. Tungo ambatano: Ni sentensi zenye zaidi ya kishazi huru kimoja na
huwakilisha mawazo mawili au zaidi. Aghalabu sentensi hizi hutumia
viunganishi (U) au alama za uakifishaji kama vile kituo (.) na nukta-nusu (;)
ili kubainisha wazo moja toka jingine.
Mifano:
Tulipanda miti kwa ajili ya kupigana dhidi ya mporomoko wa ardhi. Ardhi yetu
iliporomoka.
• Ingawa tulipanda miti kwa ajili ya kupigana dhidi ya mporomoko wa
ardhi, ardhi yetu iliporomoka.
Bwana Bahati na mkewe Fifi waliunda kampuni ya uandishi wa riwaya. Bwana
Bahati na mkewe Fifi waliwaajiri wafanyakazi wengi.
• Bwana Bahati na mkewe Fifi waliunda kampuni ya uandishi wa riwaya
na kuwaajiri wafanyakazi wengi.
Familia ya Bwana Bahati na mkewe Fifi ilijitafutia ajira. Familia ya Bwana Bahati
na mkewe Fifi ilitajirika.
• Familia ya Bwana Bahati na mkewe Fifi ilijitafutia ajira ikatajirika.
3. Tungo Changamano: Ni sentensi zinazoundwa kwa kuunganisha
kishazi huru pamoja na kishazi tegemezi au sentensi mbili kwa kutumia
o-rejeshi ili kuleta zaidi ya wazo moja.
Mifano:
- Tumepata maelezo ya kutosha kuhusu elimu ya usanifishaji. Tulikuwa tunaomba
maelezo hayo toka mwezi uliopita.
• Tumepata maelezo ya kutosha kuhusu elimu ya usanifishaji ambayo
tulikuwa tunayaomba toka mwezi uliopita.
- Shirika jipya lilitunga tamthilia hii. Ni tamthilia inayovutia sana.• Shirika jipya ndilo lililotunga tamthilia hii inayovutia sana.
Zingatia yafuatayo
Kuna tanzu nne kuu za fasihi andishi ambazo ni zifuatazo:
1. Hadithi fupi
2. Riwaya
3. Tamthilia
4. Mashairi yaliyoandikwa
A. HADITHI FUPI
Hadithi Fupi ni aina ya kazi andishi ambayo huwa fupi; na huangazia wazo mojakwa kurejelea kisa kimoja.
Hadithi fupi huwa na wahusika wachache na huchukua muda mfupi. Masuala
mbalimbali huzingatiwa katika hadithi fupi kama vile masuala ya kijamii, kisiasa,
kidini, kielimu, kiutamaduni, kiuchumi, n.k.
Mfano: Hadithi fupi za Alley Yusufu Mugenzi
Mifano mingine ya hadithi fupi za Kiswahili:
-- Kachukua Hatua Nyingine
-- Mayai Waziri wa Maradhi
-- Siku ya Mganga
-- Ngome ya Nafsi
B. RIWAYA
Riwaya ni kazi ya fasihi andishi ambayo huwa ndefu na aghalabu riwaya moja
hujaza kitabu kizima. Riwaya huwa na wahusika wengi na huangazia mawazo
kadhaa. Aidha, riwaya hufanyika katika mazingira mbalimbali na aghalabu
huchukua muda mrefu ikilinganishwa na hadithi fupi. Kazi hii huhusisha
binadamu,wanyama ama vitu vingine vinavyopewa uhai kama vile mizimu.
Kunazo aina nyingi za Riwaya katika Fasihi Andishi. Ifuatayo ni baadhi ya mifano:
Riwaya sahili: Ni aina ya riwaya ambayo visa vyake husimuliwa moja kwa moja
na huwa rahisi kueleweka.
Riwaya changamano: Hii ni riwaya ambayo huhitaji kusomwa kwa makini
ili kueleweka. Aghalabu huwa na maudhui mengi na wahusika wengi ambao
wanachangia katika tatizo kuu katika riwaya hiyo. Hujengwa kwa taharuki ili
kuwavutia hadhira kutazamia jinsi tatizo kuu litakavyotatuliwa. Hutumia mbinu za
taharuki na visengere nyuma/mbele.
Riwaya ya kibarua: Ni riwaya ambayo hutumia muundo wa barua kuwasilishaujumbe wake.
Riwaya kiambo: Ni riwaya ambayo huhusisha masuala ya kawaida katika jamii.
Mfano wa riwaya:
Adili na Nduguze
Utengano
Siku Njema
Mwisho wa KosaKiu
C. TAMTHILIA
Tamthilia ni sanaa ambayo huwasilisha mchezo wa kuigiza kwa njia ya
maandishi. Majina ya wahusika huandikwa katika upande wa kushoto,
kisha koloni, halafu hufuatiwa na maneno halisi yaliyotamkwa na mhusika
huyo. Kwa maana nyingine,tamthilia ni mchezo wa kuigiza ulioandikwa
ili uigizwe jukwaani kwa kuwasilisha ujumbe kwa jamii.
Aina za jukwaa
Kuna aina mbili za jukwaa:
-- Jukwaa la akilini kama hali ya kujiundia akilini k.v. mchezo unaoigizwa
redioni.
-- Jukwaa la hadharani, yaani mahali ambapo maonyesho ya tamthilia
yanaigiziwa mbele ya watazamaji au wasikilizaji.
Aina za tamthilia
Tamthilia au mchezo wa kuigiza huwa na aina mbalimbali kulingana na dhamira
kuu inayoendelezwa. Utaipata tamthilia ya mapenzi, ya kihistoria, ya kisiasa, ya
kidini, ya kiuchumi, n.k. Tamthilia hizi zote huangukia baadhi ya makundi makuu
yafuatayo:
Tanzia
Ni aina ya tamthilia iliyojaa, huzuni ndani yake, mikasa, matokeo ya vifo na mateso
makali. Mwisho wa tamthilia za aina hii huwa ni wa masikitiko, maanguko na
hasara kubwa kwa mhusika mkuu au jamii inayoibushwa. Wengine huita aina hiitamthilia simanzi au trejedia.
Ramsa
Tamthilia zenye kuchekesha kutokana na utani, mzaha, kejeli, maneno
yaonyeshayo ujinga, n.k. Iwapo tamthilia hizi huwa na dhana ya uchekeshaji,
lengo lake ni kukosoa jamii, watawala na tabia mbaya na watu binafsi. Aina hii
huitwa tena Tamthilia cheshi au komedia.
Tanzia – ramsa
Tanzia – ramsa au simanzi – cheshi ni mchezo wenye sifa za ramsa, lakini ndani
ya uchekeshaji wake na tanzia kama vile kifo cha mhusika mkuu au kuanguka
kwa jamii. Pengine huitwa Trejikomedia.
Mfano wa tamthilia
Hawala ya Fedha
Kifo Kisimani
Shamba la Wanyama
Mstahiki Meya
D. MASHAIRI YALIYOANDIKWA
Ushairi ni utungo wa kisanaa unaotumia maneno ya mkato na lugha yenye
kuvutia (lugha teule na mpangilio fulani wa maneno badala ya kutumia lugha
natharia) na ambayo yamepangwa kwa urari wa mizani na vina maalum. Ushairi
unaweza kuwa kipera cha fasihi simulizi (nyimbo) na pia katika fasihi andishi kwa
sababu mashairi yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya kukariri na pia kwa njia ya
maandishi. Mashairi yanayoghaniwa badala ya kusomwa huitwa maghani.
Kuna aina kuu tatu za ushairi: Mashairi, Ngonjera, Tendi au Tenzi.
Mashairi:
Shairi ni mtungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum na kutumia lugha ya
mkato na mnato kwa kuelezea hisi na mawazo ya jamii husika na kuwasilisha
ujumbe fulani. Mashairi hugawika katika makundi mawili: mashairi ya kimapokeo
au mashairi arudhi na mashairi huru. Mashairi arudhi hutungwa kwa kufuata au
kuzingatia sheria na kanuni au kaida za utunzi kama vile kuzingatia vina, idadi
fulani ya mizani, mishororo na vipande vya mishororo. Kulingana na idadi ya
mishororo katika kila ubeti, mashairi huweza kugawika tena katika aina mbalimbalikama ifuatavyo:
1. Tamonitha ni shairi lenye mshororo mmoja kwa kila ubeti.
2. Tathnia ni shairi lenye mishororo miwili kwa kila ubeti.
3. Tathlitha ni shairi lenye mishororo mitatu kwa kila ubeti.
4. Tarbia ni shairi lenye mishoro minne kwa kila ubeti.
5. Takhmisa ni shairi lenye mishororo mitano kwa kila ubeti.
6. Tasdisa shairi lenye mishororo sita.
Ngonjera:
Ngonjera ni shairi lenye malumbano na majibizano kati ya watu wawili au zaidi.
Tenzi
Tenzi ni aina ya shairi ambayo ni mtungo mrefu wa kishairi unaoelezea habari au
masuala mbalimbali kishairi. Utenzi huwa hauna vina vya kati katika mistari yake
bali kila ubeti una vina vya namna moja katika mistari yake isipokuwa mstari wa
mwisho wa ubeti.
Kuna mambo mengine muhimu kuhusu shairi. Mishororo ya shairi huwa na
majina maalum.
Mwanzo huwa ni mshororo wa kwanza wa ubeti.
Mloto huwa ni mshororo wa pili wa ubeti.
Mlea huwa ni mshororo wa tatu wa ubeti
Kituo huwa ni mshororo wa mwisho wa ubeti.
Kuna aina mbili za vituo ambazo ni kituo kimalizio na kituo kibwagizo. Kituo
kimalizio ni kituo ambacho hakirudiwi mwishoni mwa kila ubeti katika shairi. Kituo
kibwagizo ni kituo kinachorudiwarudiwa mwishoni mwa kila ubeti.
Vipande au sehemu za mishororo ni zifuatazo:
Ukwapi: Ni kipande cha kwanza cha mshororo.
Utao: Ni kipande cha pili cha mshororo.Mwandamizi: Ni kipande cha tatu cha mshororo.
Dhima ya ushairi
Kama mtungaji wa kazi nyingine za fasihi, mshairi huwa na madhumuni yafuatayokwa jamii:
-- Kuburudisha
-- Kuhamasisha jamii
-- Kukuza sanaa na ukwasi wa lugha
-- Kuliwaza
-- Kuelimisha
-- Kuonya, kutahadharisha, kunasihi na kuelekeza
-- Kupitisha ujumbe fulani
-- Kusifia mtu au kitu
-- Kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii.