MADA YA 6 UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI
Malengo ya Ujifunzaji:
-- Kueleza maana ya uhakiki,
-- Kubainisha taratibu au mbinu za uhakiki wa kazi za fasihi simulizi,
-- Kuonyesha umuhimu wa kuhakiki kazi za fasihi,
-- Kujadili maana ya uhakiki na mwongozo wake,
-- Kuhakiki hadithi za masimulizi mbalimbali,
-- Kutoa mapendekezo juu ya kazi za fasihi zilizohakikiwa,
-- Kukuza falsafa tofauti zinazojidhihirisha kutoka ujumbe wa kazi za fasihi
simulizi,-- Kuainisha aina za maneno katika Kiswahili.
SOMO LA 12: MAANA YA UHAKIKI
12.1. Kusoma na Ufahamu: Siku Njema Huonekana
Asubuhi
Soma kifungu kifuatacho, kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo
chini.
Ilikuwa Jumatatu asubuhi wakati mwalimu wetu wa Kiswahili Bibi Amina
alipotuchekesha sana. Mwalimu huyu kwa kawaida yake alikuwa mcheshi
na mwenye kupenda utani. Ilikuwa ni ajabu mno kumwona amekunja uso.
Wanafunzi wote walikuwa wakimpenda na hata wagonjwa walikuwa wakijikaza
kiume ili wawahi somo lake. Alikuwa mnene kiasi, macho mazuri kama gololi
yaliyokuwa yakicheza katika vidimbwi vya machozi. Alipokuwa akicheka, vishimo
vidogovidogo vilikuwa vikionekana kwenye mashavu yake. Sauti yake ilikuwa
ikituvutia sana. Alikuwa akifundisha na wanafunzi sote tukatoka tukisema kuwa
tumetosheka.
Asubuhi hiyo, tulipofika shuleni tuliulizana habari mbalimbali. Kuna wale
waliokuwa na habari za michezo na wengine walikuwa na habari zinazohusu
maisha ya nchi yetu: uchumi, elimu, siasa, ufugaji, kilimo na kadhalika. Habari
hizo zote tulikuwa tumezipata kutoka kwenye redio na nyingine kutoka kwenye
runinga. Kwa kuwa nami nilikuwa sogora kwa kutia chumvi katika mazungumzo,
kila siku wanafunzi walikuwa wakinizunguka kama nyuki wazengeavyo maua.
Kengele ya kwanza ilipolia, sote tulikusanyika karibu na mlingoti wenye bendera
ya taifa na kuanza kuimba wimbo wa taifa. Tulipomaliza, Joni, mwalimu wa somo
la ujasiriamali, alipanda jukwaani na kuanza kutuhutubia kuhusu mada ya “Ndi
Umunyarwanda.” Siku hiyo yeye alitilia mkazo kwenye umoja na maridhiano kati
ya Wanyarwanda, uzalendo na mshikamano kama njia bora za kuendeleza nchi
yetu. Alipomaliza, tuliingia madarasani na kuwasubiri walimu wetu.
Kengele ya pili ilipolia mwalimu wetu wa Kiswahili alijtokeza na kutuamkia kama
kawaida yake. Alikuwa na mkoba begani na vitabu pamoja na boksi la chaki
mikononi. Sisi sote tulikuwa na hamu ya kusikia mchapo aliokuwa ametuletea
asubuhi ile. Bila ya kusema neno lolote aliweka vifaa vyake mezani akaangaza
macho kama aliyekuwa akishuku jambo baya fulani darasani. Sisi sote tulitulia
tuli kama maji mtungini. Hayawi hayawi huwa. Alipomaliza ukaguzi wake
alituuliza majina ya wale ambao hawakuhudhuria shule lakini sote tulikuwa hapo.
Alitabasamu na kuanza somo lake.
Kwanza alituuliza maswali kuhusu somo lililopita. Somo hilo lilikuwa vipengele
vya fasihi simulizi. Tuliposonga mbele alituomba kumwonyesha kazi ya nyumbani
aliyotupatia. Kazi hiyo ilikuwa uchambuzi wa hadithi. Sote tulikuwa tumejaribu
kwa uwezo wetu. Alituuliza mbinu tulizotumia katika uchambuzi wetu, kila mtu
akataja zake. Alitukagua kitambo kidogo, akatupongeza na kusema kuwa “Kweli
siku njema huonekana asubuhi.” Mara hii alichukua chaki na kuandika neno
“UHAKIKI” ubaoni. Nasi tukaanza kunong’onezana kwa kuwa ilikuwa mara ya
kwanza kuona neno hilo. Tulishangaa sana kwa kuona kuwa hakuandika jaribio
kama desturi yake ya kutuuliza kila alipokuwa akiingia darasani. Alipotangaza
kuwa neno hilo lilikuwa somo la siku ile sote tulitega masikio.
Pili, alitugawa katika makundi. Kila kundi lilikuwa limeundwa na wavulana na
wasichana, na wanafunzi wenye matatizo maalum ya kielimu. Kila kundi lilipewa
kitabu. Kabla hatujafungua vitabu, alituomba kukagua vema kama kila kundi
lilipewa vitabu vya Kiswahili. Alituonya hivi huku akitwambia kuwa kulikuwa
na mtu mmoja aliyeingia mgahawani bila kuuliza habari wala kusoma, akatia
pilipili hoho nyingi kwenye chakula akidhani kwamba ni supu. Alipokula chakula
hicho, aliwashwa na machozi yalimlemgalenga. Katika kujaribu kupoza koo lake,
akashika na kunywa sabuni ya kunawia mikono akifikiri kwamba ni juisi. Sisi sote
tulishika mbavu. Alituagiza kufungua vitabu na kuzungumzia kuhusu uhakiki wa
kazi za fasihi simulizi. Tulipomaliza kuzungumza, kila kundi liliwasilisha.
Tuliona kwamba uhakiki ni kazi ya kutathmini, kufasili na kuainisha kazi za fasihi.
Ni kazi ya kusoma maandishi au kusikiliza mambo fulani kwa kuyachambua na
kuyafafanua ili kupata ukweli wa mambo hayo.
Zaidi ya hayo, tulisoma kuwa kwa kuhakiki maandishi au masimulizi,
tunachunguza na kufafanua vipengele vya fani na maudhui. Katika fani kama sura
ya nje ya maandishi au masimulizi, tunachunguza wahusika, muundo, mtindo
na mengineyo. Kimaudhui, tunachunguza dhamira, ujumbe, migogoro, itikadi,
falsafa na hata mtazamo. Wakati huu, mambo yaliyokuwa yakitushinda, mwalimu
alikuwa akitusaidia ili tuyaelewe zaidi.
Isitoshe, baada ya kuona maana ya uhakiki, mwalimu alituomba kueleza
umuhimu wa uhakiki tukagundua kwamba uhakiki una umuhimu wa kumwezesha
mhakiki kuchambua na kuelewa kazi ya fasihi au sanaa kwa ujumla, kuwezeshakulinganisha kazi tofauti na mengine mengi.
Lakini katika uchambuzi wetu, tuligundua kuwa uhakiki una matatizo fulani kwa
sababu ni sayansi ngumu inayoomba bidii, ukakamavu wa mhakiki, uwezo wake na
mienendo ya jamii. Hili linatulazimisha tufanye mazoezi mengi ili tuweze kupevuka
katika kazi hii. Tena tuliona kuwa, wakati mwingine, wahakiki hawakubaliani kwa
kuwa kila mmoja ana namna yake ya kuona na kuelewa mambo.
Somo lilipokaribia kutia nanga, sote tulikuwa tumeelewa kwamba uhakiki lilikuwa
si somo geni kwa kuwa kila siku tunajaribu kuchambua yale tunayosoma au
tunayoambiwa. Kutokana na weredi wa haraka tuliokuwa nao ndipo nilipokumbuka
kuwa “Siku njema huonekana asubuhi.” Kabla ya kutuaga mwalimu alitupa kaziya nyumbani ya kuhakiki hadithi.
• Nomino/ jina
a) Maana ya nomino
Nomino au jina ni neno linaloita kitu chenye uhai au kisicho na uhai kwa
kukitofautisha na vingine.
b) Aina za nonino
-- Nomino za pekee: Butare, Rusizi, Kamana, Ibilisi, Mukungwa, Akanyaru,
-- Nomino za kawaida: barabara, gari, kuku, kiongozi, nchi, …
-- Nomino za dhana au za dhahania: maridhiano, uzalendo, utoto, utu,
upendo, …
-- Nomino za jamii/ za makundi: jamii, jamaa, baraza, genge, kikosi, …
-- Nomino za wingi: mawese, maji, mafuta, mamlaka, madaraka, …
-- Nomino za kitenzi-jina: kuishi kwa amani kunapendeza. Kuimba ni
kuzuri. Kufurahi kwako kunatutuliza. (kuishi, kuimba na kufurahi ni vitenzijina
katika sentensi hizi)
• Vivumishi
a) Maana ya Kivumishi
Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu
vivumishi hutanguliwa na nomino.
b) Aina za vivumishi
• Vivumishi vya sifa
Mifano:
-- Mke mrefu yule ni mtulivu.
-- Tunapaswa kujenga jamii nzuri.
-- Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni.
• Vivumishi vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha umiliki wa nomino. Mizizi ya vivumishi hivi
huundwa kulingana na nafsi mbalimbali. Mizizi hiyo ni : -angu, -ako, -ake, -etu,
-enu, -ao.
Mifano :
-- Nyumba yangu haina mlango.
-- Familia yake inaishi vizuri.
• Vivumishi vya idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi
vya idadi.
a) Idadi kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
Mifano:
-- Mmomonyoko wa ardhi ulibomoa nyumba kumi katika vijiji viwili.
-- Ili kupunguza uhasama unaotokana na ukewenza mume mmoja
analazimishwa kuoa mke mmoja.
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano: Chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani.
Mifano:
-- Watoto kadhaa waligeuka mayatima wakati wa mauaji ya kimbari dhidi ya
Watusi yaliyotokea mnamo mwaka wa 1994.
-- Mvua nyingi ilinyesha na kusababisha mafuriko.
• Vivumishi viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
-ngapi?, -pi? wapi?, gani?
Mifano:
-- Mtu mzima ana meno mangapi?
-- Ni mbuga gani inayohifadhi sokwe nchini Rwanda?
• Vivumishi viashiria / vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Karibu: hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale.
Mbali kidogo: hapo, huyo, hiyo, hicho.
Mbali zaidi: pale, lile, kile.
Mifano:
-- Safisha mahali hapa.
-- Mwanafunzi yule ni mchezaji kabumbu.
• Vivumishi visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria
Mifano:
-- Anaishi pahali papa hapa.
-- Mtu yuyu huyu anatuongoza vizuri.
• Vivumishi virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa
vivumishi vya O-/-ye rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea
nomino.
Mifano:
-- Mwanafunzi ambaye ataenda nje ya shule bila ruhusa ataadhibiwa.
-- Wanyama ambao wametoroka mbuga hawapaswi kuuawa.
• Vivumishi vya A-unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki
nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na
kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino.
Mfano: cha, la, kwa, za, ya.
-- Dawa ya moto si moto.
• Viwakilishi
a) Maana ya viwakilishi
Viwakilishi vya nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi
hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.
b) Aina za viwakilishi
• Viwakilishi vya nafsi
-- Viwakilishi nafsi huru: Mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao.
-- Viwakilishi nafsi viambata : Ni-, u-, a-, tu-, m-, wa-, mi-, li-, ya-, ki-, vi-,
i-, zi-, ku-, pa-
• Viwakilishi viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kuonyesha
nomino inayorejelewa bila kuitaja.
-- Hiki ni chanzo cha maradhi.
-- Hao wanataka maridhiano.
• Viwakilishi visisitizi
Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia kiashiria chake mara mbili mfululizo.
Kwa mfano: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, zizi hizi,
- Kiki hiki ndicho kinachonifurahisha,
- Yuyu huyu alitueleza matumizi ya viwakilishi visisitizi
• Viwakilishi vya sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
Kwa mfano: -chungu, -eupe, -dogo, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, -gumu,
-kali, ekundu.
• Viwakilishi vya idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
a) Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino
-- Wawili hugeuka mmoja.
-- Alizaa watatu tu.
b) Idadi isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano:
-- Tutasikiliza maoni ya wengi kabla ya kuanzisha mradi huu.
-- Vichache viliandikwa kuhusu maradhi ya UKIMWI.
• Viwakilishi viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli.
Mifano:
-- Unaenda wapi?
-- Ulinunua mangapi?
• Viwakilishi vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
-- Kwao hakuna maji safi.
-- Yao yameharibika tena kutokana na mvua kali.
• Viwakilishi virejeshi
Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino.
Kwa mfano: ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule.
-- Ambao walizaliwa mwaka huu watachanjwa.
-- Ambacho kinahitajika kitatafutwa.
• Viwakilishi vya A-unganifu
Huwakilisha nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa
kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha
a-unganifu.
Kwa mfano: cha, la, kwa, za, ya
-- Cha mlevi huliwa na mgema.
-- La kuvunja halina rubani.
• Kitenzi
a) Maana ya kitenzi
Kitenzi ni neno linaloeleza jambo linalotendwa au kufanywa na nomino au
kiwakilishi chake.
b) Aina za vitenzi
• Kitenzi halisi: ni kitenzi kimoja kinachotumiwa katika sentensi.
Mifano:
-- Wanafunzi walipanda miti michache.
-- Rais atafika kesho.
• Vitenzi vikuu na vitenzi visaidizi: Wakati vitenzi viwili hutumika
pamoja kueleza kitendo kimoja, kitenzi cha kwanza huitwa kisaidizi na
cha pili ndicho kitenzi kikuu.
Mifano:
-- Yeye alikuwa akisoma.
-- Wao wanahitaji kuishi vizuri.
• Vitenzi vishirikishi: Vitenzi vishirikishi vina dhana ya kitenzi kuwa au
kuwa na.
Vitenzi vishirikishi huwa vya aina mbili kuu:
• Vitenzi vishirikishi vikamilifu: hivi huchukua viambishi vya wakati na
viambishi nafsi.
Mifano:
-- Watoto wangali kitandani.
-- Wao wamekuwa na uzembe.
• Vitenzi vishirikishi vipungufu: hivi huchukua viambishi nafsi lakini
havichukui viambishi wakati.
-- Wezi si wazuri.
-- Yeye yu mkweli.
-- Sisi ni walimu.
Ukakiki wa Tanzu za Fasihi Simulizi
• Maana ya Uhakiki
Uhakiki ni utathmini, ufasili na uainishaji wa kazi ya fasihi. Ni uchambuzi wa ndani
kabisa wa kitu au jambo ulioambatana na fikra za mchambuzi. Uhakiki ni kazi ya
kusoma maandishi au kusikiliza mambo fulani kwa kuyachambua na kuyafafanua
ili kupata ukweli wa mambo hayo.
Uhakiki ni sayansi maalum ya kuchambua na kudadisi au kupima ubora au
udhaifu wa kazi ya kisanaa hasa fasihi. Uhakiki wa tanzu za fasihi huzingatia
mambo mawili muhimu yaani fani na maudhui. Fani na maudhui ni mambo mawiliambayo hayawezi kutengana kwa sababu moja hutegemea jingine.
i) Fani
Fani ni namna msanii anavyowasilisha maudhui yake kwa hadhira. Fani pia
huweza kutazamwa kama umbo la nje la kazi ya sanaa yaani sura yake ya nje.
Kuchunguza fani ni kuchunguza kiundani vipengele mbalimbali vya kifani na
namna vilivyotumika ili kuwasilisha maudhui. Uchunguzi wa fani unazingatia
vipengele vifuatavyo: wahusika, muundo, mtindo, mandhari, matumizi ya lugha.
• Wahusika
Wahusika ni watu, wanyama, vitu, hata viumbe vya kufikirika ambavyo msanii
wa kazi ya fasihi hutumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika kazi
za fasihi msanii huwagawa wahusika katika makundi mawili: wahusika wakuu
na wahusika wadogo. Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia
mwanzo mpaka mwisho na ndio huwa msingi wa kazi ya fasihi hasa hadithi.
Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza mara chache au sehemu
mbalimbali katika kazi ya fasihi na huwasaidia wahusika wakuu katika kubeba
maudhui. Wahusika wadogo hawa wanaweza kuwa watetezi (wakimsaidia
mhusika mkuu) au wakawa wapinzani (wakimzuia mhusika mkuu).
Wahusika wa kazi za fasihi wana tabia mbalimbali. Tabia ya kwanza ni ubapa
yaani tabia ya kutobadilika kwa mhusika toka mwanzo hadi mwisho. Tabia ya pili
ni uduara yaani tabia ya kubadilika kihulka, kimawazo na kisaikolojia kufuatana
na mazingira mapya, wakati, hali, na kadhalika. Tabia ya tatu ni ufoili. Ni tabia
inayojidhihirisha kati ya ubapa na uduara. Wahusika wenye tabia hii hawaonyeshi
msimamo wao kama wanaweza kubadilika au kutobadilika.
Mtindo
Ni namna ambavyo msanii huipa kazi yake sura ya kifani na kimaudhui kwa njia
ambayo msanii mwingine hawezi kuipa hivyo hata kama jambo lizungumziwalo
na wasanii hawa wawili ni lile moja. Mtindo ndio unaomwezesha msomaji,
msikilizaji au mtazamaji wa kazi ya fasihi amtambue msanii wa kazi hiyo bila
kuelezwa au kusoma jina la msanii huyo. Kuchunguza mtindo wa kazi ya fasihi
ni kuangalia matumizi ya lugha katika kazi hiyo. Wakati wa kufanya kazi hiyotunajiuliza maswali yafuatayo:
-- Msanii anatumia lugha namna gani? Je kuna tamathali za usemi, mafumbo,
methali, nahau,…
-- Picha alizochora msanii zinaeleweka au zimesaidia kurahisisha katika
maelezo yake?
-- Msanii anatumia mbinu zipi? Mazungumzo, mijadala, hadithi ndani ya
hadithi,… ?
• Muundo
Ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia msanii katika kupanga kazi yake. Pia ni
mpangilio na mtiririko wa visa na matukio. Katika muundo tunaangalia vipengele
kama ploti. Ploti ni mtiririko wa kiusababishi wa visa na matukio. Aidha, katika
muundo tunajiuliza mtiririko huu wa visa na matukio ni wa moja kwa moja au ni
wa kiurejeshi? Kama ni wa moja kwa moja ni muundo wa msago. Kama unaenda
mbele na kurudi nyuma ni muundo rejeshi.
• Mandhari
Mandhari ni sura ya mahali popote palipotumiwa na msanii kwa kukisimika
anachokisimulia katika kazi ya fasihi. Kuna Mandhari halisi yaani mahali
panapoweza kuonekana, panapojulikana waziwazi, panapopatikana (nchi fulani,
wilaya, mkoa, mlima,…) na Mandhari pakubuni yaani mahali pa kujiundia, pa
kindoto pasipopatikana (mbinguni, jahanamu, ahera, ujinini, ...)
• Muktadha
Muktadha ni mazingira au hali ambamo tukio au jambo fulani hutendeka. Ni
kusema kuwa msanii huishi katika jamii na jamii huzungukwa na mazingira
mbalimbali. Mazingira haya yanaweza kuonekana katika kazi ya fasihi. Mazingira
haya yanaweza kuonekana kulingana na lugha iliyotumiwa, msamiati uliotumiwa,
mawazo fulani ya msanii yanayolingana na wakati fulani. Kwa mfano kazi za fasihi
simulizi za enzi za ufalme ni tofauti na kazi zilizopatikana baada ya uhuru wa
Rwanda.
ii) Maudhui
maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa na masanii katika kazi ya
kifasihi. Haya ndiyo huwa yamemsukuma msaniii kuisana kazi yake hii. Maudhui
hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi
akatunga na kusanii kazi yake ya kifasihi. Uchambuzi wa maudhui huzingatia
vipengele kama vile dhamira, ujumbe, migogoro, falsafa na hata mtazamo.
• Dhamira
Dhamira ni wazo lililomo katika kazi za sanaa. Kwa kawaida, dhamira zinagawika
katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
a) Dhamira kuu: ni kiini cha wazo kuu la msanii ambalo linaongoza
ujumbe autakao msanii kufikisha kwa jamii. Dhamira kuu huweza kuhusu
jamii, magonjwa ya zinaa, siasa, uzalendo, uchumi, ushirikiano, umoja na
maridhiano, usawa wa jinsia, malezi bora, mapenzi, mazingira na maendeleoendelevu, n.k.
b) Dhamira ndogondogo: ni dhamira zile mbalimbali zinazogusiwa na
msanii ili kuendeleza dhamira kuu. Dhamira hizi husaidia dhamira kuu katika
kujidhihirisha.
• Ujumbe /Mafunzo
Mafunzo ni masomo yanayopatikana katika kazi ya fasihi. Kila kazi ya sanaa huwa
na ujumbe maalumu ambao msanii anataka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe
katika kazi za kifasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana ndani ya kazi
hiyo. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi wakati ambapo
dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito
zaidi ujumbe wa msingi.
• Migogoro
Ni hali ya kutokubaliana kimawazo, kimatendo kati ya wahusika. Migogoro
hii inaweza kuwa kati ya wahusika binafsi na kizazi kimoja au kati ya kizazi na
kingine. Pia inaweza kuwa kati ya watawala na watawaliwa, jamii na misukosuko
(misukumano) ya kijamii au kimazingira iliyomo katika eneo fulani.
• Falsafa
Kimsingi, falsafa ni elimu ya asili; busara au hekima. Falsafa ya msanii hugusiwa
kutokana na jinsi anavyoelewa matatizo ya jamii na jinsi anavyoyatolea suluhisho
kwa njia ya busara, amani na utulivu. Katika kazi za fasihi simulizi hususani hadithi
zile za paukwa pakawa, falsafa inayojitokeza ni ile isemayo kuwa maisha ni
mapambano ya wema dhidi ya ubaya na daima wema huushinda ubaya.
TANBIHI
Katika kuhakiki kazi za fasihi simulizi, kila kazi ina mbinu mahususi katika
kuichambua. Kwa mfano uchambuzi wa nahau, methali na misemo unatofautiana
sana na uchambuzi wa hadithi au mashairi.
• Umuhimu wa Uhakiki
Mara nyingi fasihi huwa ngumu kuielewa. Kuna wakati mtu anaweza kusoma au
kusikiliza kazi ya fasihi akashindwa kuelewa alichojaribu kueleza msanii. Hapa
ndipo uhakiki unahitajika ili kumwongoza katika kuelewa kazi hiyo.
Kwa hiyo, uhakiki wa kazi za fasihi simulizi una umuhimu mkubwa. Baadhi ya
umuhimu huo ni kama vile:
a) Kuwezesha kuelewa kazi ya fasihi na kuchunguza kama inatimiza sifa zote.
Kila kazi ya fasihi ina sifa zake. Kwa hiyo uhakiki unatusaidia kugundua
kwamba kazi ya fasihi inajaza sifa zake zote.
b) Kuwezesha kulinganisha kazi tofauti za fasihi. Hapa uhakiki unatuwezeshakupima uzito na ulegevu wa utunzi wa msanii.
c) Kuwezesha kupanua lugha yetu kwa sababu katika kazi ya sanaa kunatumika
msamiati, mifumo, semi na mambo mengine mengi yanayokuza lugha yetu.
d) Kuwezesha kuchambua na kumulika mafunzo na maonyo yanayopatikana
katika kazi za fasihi. Maonyo na mafunzo hayo yanaweza kutumiwa kwakujirekebisha au kuirekebisha jamii.
• Matatizo ya uhakiki
Hakuna jambo lisilokuwa na ila. Matatizo ya uhakiki ni mengi sana. Kwanza ni
vigumu kwa wahakiki kukubaliana kuwa hivi ndivyo ilivyo maana ya kazi ya sanaa
husika. Kila mhakiki huweza kusoma na kuelewa kazi hiyo kwa namna yake.
Pili, uhakiki wenyewe ni taaluma ngumu ambayo inahitaji kutumia bidii kubwa
ya kuweza kuitawala. Wahakiki wengi wanafanya uchambuzi na uchambuzi huo
ukichambuliwa ukaonekana bado una dosari. Jambo hili hutokana na mhakikikuwa na changamoto mbalimbali. Changamoto hizo zinaweza kuwa :
-- Kutokuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu sifa za utanzu unaohakikiwa,
-- Kutawaliwa kwa mhakiki na hisia zake zinazoweza kuleta upendeleo fulani,
-- Kutofuata misingi inayozingatiwa katika uhakiki.
Jibu maswali yafuatayo:
1. Ni ipi maana ya uhakiki?
2. Ni mambo gani tunayochunguza kwa kuhakiki kazi ya fasihi?
3. Taja na ueleze tabia za wahusika.
4. Ni tofauti gani iliyoko baina ya mandhali na muktadha?
12.5. Kusikiliza na Kuzungumza
13.1. Kusoma na Ufahamu: Kobe na Kijumbamshale
Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini
Hapo zamani za kale palikuwa na Kobe na Kijumbamshale. Kobe alikuwa
mnyamavu, mshindani pamoja na mpole. Kila wakati alikuwa hafanyi jambo lolote
ovyo ovyo wala kwa pupa. Kwake, kila jambo lilikuwa na mpango wake kabla ya
kulishughulikia kimatendo.
Kwa upande mwingine, Kijumbamshale alikuwa ndege mpinzani, mjuba, mpuuzi
na mwenye majivuno. Mara nyingi alikuwa anafanya kazi bila mpango.
Siku moja Kobe na Kijumbamshale walikutana njiani wote wakipunga upepo
huku wakielekea kwa kasri ya Malkia Tembo. Walisalimiana na kukaa chini kabla
hawajaendelea na safari. Kwa hiyo, walipata fursa ya kuongea sana. Maongezi yao
yalipokuwa yakiendelea, Kobe alishangaa sana kumwona Fisi amekuja akikimbia
mno. Alikuwa amechelewa kuhudhuria sherehe ya mtoto wa Malkia Tembo. Kobe
hakuamini macho yake na kumwonyesha Kijumbamshale, “Angalia pale jinsi Fisi
anavyokimbia kwa mwendo wa kasi. Anakimbia mbio kama umeme. Bila shaka
hakuna mnyama hata ndege yeyote anayeweza kumshinda katika mashindano
ya riadha.” Fisi aliwapitia bila kuwasalimia wakashangazwa na adabu yake.
Kijumbamshale hakuridhishwa hata kamwe na maoni ya Kobe kuhusu Fisi. Mara
moja alimgeukia na kumuuliza kwa dharau, “Je, una hakika kwa hayo yote ambayo
umeyatamka? Nani aliyekuambia kuwa Fisi yule anaweza kuthubutu kunishinda
mimi? Kama wewe ni mlemavu wa miguu na mabawa, usidhani kuwa sisi sote
ni sawa nawe.”
Kobe alijaribu kumsihi akisema, “Samahani rafiki yangu! Hii siyo sababu ya
kukasirika kwa bure! Ukweli mtupu ni kwamba mimi ninaamini kwamba Fisi
anaweza kunishinda katika zoezi la mashindano ya kukimbia. Lakini, wewe sahau
hilo! Huwezi, huwezi na huwezi hata kamwe! Maishani mwangu wanyama wawili
pamoja na ndege mmoja tu ndio niwaogopao katika mashindano ya namna hii.
Hao ni Fisi, Sungura pamoja na Tai. Wengine hapana!”
Kijumbamshale alikunja uso na kumwambia mwenzake, “Huna haya kuhakikisha
hayo mbele yangu? Kobe hakutaka jambo hili lipambe moto. Hivyo, aliamua
kutoa suluhu la kimatendo. “Acha tukubaliane kwenye mashindano ya kukimbia
kilomita mbili wakati wa dakika sitini. Atakayeibuka mshindi ndiye atakayekuwa
mheshimiwa kati yetu.” Kobe alipendekeza.
Bila kusita, Kijumbamshale alikubaliana na Kobe hivi wakiamua siku, mahali
pamoja, na wakati wa mashindano. Baada ya kutoka katika sherehe, Kobe
hakupata tena utulivu. Alianza kufikiria juu ya mbinu angetumia kujinyakulia
ushindi dhidi ya Kijumbamshale.
Siku moja kabla ya mashindano kuwadia, Kobe alikaa peke yake na kufikiri.
“Wazazi wangu kabla ya kuaga dunia, walinitolea maonyo ambayo sitayasahau
hata siku moja. Wakati mmoja waliniambia ‘Chelewa chelewa utamkuta mtoto
si wako’ na wakati mwingine ‘bandubandu humaliza gogo.” Kobe aliyakumbuka
mashauri ya wazazi. Kutokana na haya, alijisemea kimoyomoyo, “Linalowezekana
leo lisingoje kesho.” Papo hapo, aliamua kuandaa safari na kuelekea kwenye
uwanja wa mashindano asubuhi na mapema. Aliahidiana na jogoo kwamba
angemwamsha.
Jogoo alipowika alfajiri, Kobe alikuwa ameishatoka nyumbani kwake kuelekea
mahali pa mashindano. Njiani aliwakuta wanyama wengi waliokuwa wakisafisha
mbuga yao na kuwasalimu. Walipomuuliza sababu ya safari yake, aliwaeleza
kwamba alikuwa katika shindano la kukimbia. Isipokuwa nyani aliyempa motisha
kwa kumpa ndizi, wanyama wengine walishika mbavu kwa vicheko kwa kuwa
walikuwa wakijua uwezo wake wa kukimbia. Lakini yeye hakukata tamaaakaendelea na safari yake.
Kobe alitembea, akatembea na kutembea. Saa nane mchana, Kobe alikuwa
amesogelea mti mkubwa ambapo alikuwa amekubaliana na Kijumbamshale
kuwa kikomo cha mashindano. Wakati huo ndipo Kijumbamshale alikumbuka
kuwa siku hiyo ilistahili kuwa siku ya mashindano kati yake na Kobe. Alishtuka
kwa ghafla na kuruka haraka kwa mwendo usio wa kawaida. Aliruka na kuruka!
Lahaula! Alipokuwa umbali wa mita karibu mbili, Kobe alikuwa amejinyakulia
ushindi, hivi akishangilia kwa furaha tele.
Kijumbamshale alipomwona Kobe alipoteza nguvu za kuendelea kuruka na
kuanguka chini. Kobe alisikia huruma moyoni na kumsogelea Kijumbamshale,
“Pole sana ndugu yangu. Katika mashindano ni lazima kuwepo mshindi na
anayeshindwa. Lakini siyo mwisho wa dunia. Somo kubwa kutokana na
mashindano haya ni kwamba uwezo mkubwa wa kuruka pekee hautoshi, jambo
muhimu zaidi ni maandalizi, akili na maarifa ya kufanikisha lengo lolote”.
Kijumbamshale aliona haya na kufunga mdomo wake. Baada ya dakika chache,
alizinduka na kumwambia Kobe, “Leo nimeona kuwa kila kitu kinawezekana
maishani. Sina budi kukubali ushindi wako kwa sababu asiyekubali kushindwa
si mshindani. Nimepiga saluti kwa heshima zako mheshimiwa.” Na huu ndiomwisho wa hadithi.
Maelezo Muhimu kuhusu Aina za Maneno
Katika lugha ya Kiswahili kuna aina nane za maneno. Aina hizo ni kama vile
nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kihusishi, kielezi, kiunganishi na kihisishi.
Katika somo letu tutagusia aina nne yaani kihusishi, kihisishi, kiunganishi na
kielezi.
• Viunganishi
Viunganishi ni maneno yanayofanya kazi ya kuunganisha. Huonyesha uhusiano
baina ya neno na neno, fungu moja la maneno na fungu jingine au sentensi na
sentensi.
Mifano:
-- Unataka maji au juisi?
-- Anasoma kitabu badala ya kupiga ubwana.
-- Kufanikiwa maishani si bahati bali ni kujishughulisha na kujitolea.
-- Alishinda mtihani ijapokuwa alipatwa na ugonjwa mkali.
-- Alienda shuleni bila kupata chakula.
• Vihisishi
Vihisishi ni maneno ambayo yanaonyesha hisia za mtu za ndani kwa mujibu wa
hali na muktadha. Yanaonyesha hangaiko la moyo ama kudokeza mguso wa
moyo ama hata wa akili. Mifano:
-- Mtume! Umefika asubuhi hii!
-- Lo! Mvua imenyesha!
-- Salaa! Inawezekana mtu kunywa chupa ishirini za juisi!
• Vielezi
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi
hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi na vielezi vingine.
Kuna vielezi vya namna, vielezi vya wakati, vielezi vya mahali na vielezi vya kiasi.
Mifano:
-- Mwanafunzi yule ameshinda mtihani vizuri.
-- Mvua itanyesha kesho.
-- Wanyama huishi misituni.
-- Mvua ilinyesha mara mbili kwa mwezi.
• Vihusishi
Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano baina ya watu au vitu viwili au
zaidi. Kuna vihusishi vya mahali na vya wakati.
Mifano:
-- Nitakutembelea baada ya masomo .
-- Alisafiri nje ya nchi.
-- Ng’ombe hulala ndani ya zizi.
-- Amefika hapa kabla ya mvua kunyesha.
-- Wao wanaishi pamoja kwa amani.
Uhakiki wa hadithi za masimulizi
Uhakiki wa hadithi za masimulizi ni kazi au kitendo cha kuchambua na kufafanua
vipenge vya fani na maudhui katika hadithi hizo. Vipengele vya fani na maudhui
ni pamoja na wahusika, muundo, mtindo, dhamira, migogoro na ujumbe.
• Fani katika Hadithi za Masimulizi
Ikumbukwe kuwa fani ni ufundi au mbinu anayoitumia msanii wa fasihi ili kutoa au
kufikisha maudhui kwa watu aliowakusudia. Tunapohakiki hadithi ya masimulizi
kifani, tunachunguza wahusika, mtindo, muundo, mandhari, na mengineyo.
1. Wahusika
Wahusika ni watu, wanyama, vitu, hata viumbe vya kufikirika ambavyo msanii
wa hadithi hutumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika hadithi msanii
huwagawa wahusika katika makundi mawili: wahusika wakuu na wahusika
wadogo. Wahusika wadogo wanaweza kuwa watetezi au wakawa wapinzani.
Wahusika katika hadithi za masimulizi hutegemea aina ya hadithi simulizi. Kwa
mfano:
• Ngano: Hadithi ambayo wahusika wake ni mchanganyiko wa wanyama,
wadudu, mizimu, miungu, miti, watu, na viumbe visivyo na uhai kama
mawe, miamba, n.k.
• Hekaya: Hadithi ambayo wahusika wake kwa kawaida ni binadamu tu.
• Hurafa: Hadithi ambazo wahusika wake huwa ni wanyama wanaopewa
tabia na vitendo vya kibinadamu.
• Visasili: Hadithi hizi zinazohusu asili ya mambo fulani.
• Soga: Hizi ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Wahusika wake ni
watu wa kubuni lakini wanapewa majina ya watu walio katika mazingira
hayo.
• Visakale au Mighani: Ni hadithi ambazo wahusika wake ni watuwaliotenda matendo ya kishujaa na wanaosifiwa katika jamii fulani.
Tabia za wahusika katika hadithi za masimulizi
Wahusika katika hadithi simulizi hupewa tabia za aina mbalimbali. Hawa
wanaweza kuwa na tabia ya:
• Ubapa: tabia ya kutobadilika
• Uduara: tabia ya kubadilika
• Ufoili: tabia ya kutoonyesha msimamo
Kwa upande mwingine, katika hadithi za masimulizi tunatumia wanyana kwa
mara nyingi. Wanyama hawa huwakilisha binadamu katika jamii waishimo. Hili
ni kwa sababu utumiaji wa majina halisi ya watu unaweza kuzua ugomvi katika
jamii. Wanyama wanaotumiwa sana katika hadithi za masimulizi ni kama:
• Sungura: Mara nyingi Sungura hupewa tabia za ujanja, ndiyo sababu
huonekana mahali pengi kama Sungura-mjanja. Kwa hiyo, Sungura
huwakilisha watu wenye ujanja kwa madhumuni ya kula jasho la
wengine, kuwaangamiza adui zao au kuwaangusha mtegoni pamoja na
kuwategua wanyama wakubwa kama vile simba.
• Simba: Mnyama huyu hutumika mara nyingi kama kiongozi au mfalme.
Katika jamii ya wanadamu huwakilisha watu wenye ukali ambao
wakiongea husikika na huogopewa sana.
• Fisi: Mnyama huyu huonekana kama mhusika mwenye tamaa na ulafi
ambaye fikra zake zimetawaliwa na tamaa yake. Pia fisi hupewa tabia ya
uchoyo, woga pamoja na ujinga. Fisi hutumika kuwakilisha wanadamu
waroho, woga, wazembe na wajinga, wasiopenda kufikiria sana kwani
mawazo yao yametawaliwa na tamaa zao.
• Nyani: Katika hadithi, nyani hudhihirisha hekima na uwezo wa kufanya
uamuzi wa busara. Hutumika sana kama hakimu na huwakilisha viongozi
wenye hekima katika jamii.
• Nyoka: Mnyama huyu hupewa tabia ya hila na huwakilisha watu wenye
hila/ udanganyifu katika jamii.
• Kobe: Huwakilisha watu wanyamavu, ambao japo wanajua kufanya
kitu, hawapendi kuchangia, lakini mwisho huibuka washindi; watu
wasiokimbilia kufanya mambo.
• Ndovu: Huwakilisha watu wenye kimbelembele, ambao hujisifu na
kujitafutia umaarufu. Watu wa aina hii hupenda kuwa katika mstari wa
mbele japo huenda hawana ujuzi wa kutosha katika jambo hilo.
• Chui: Chui ni mnyama mkatili sana. Katika hadithi yeye huwakilisha
tabia ya uharifu.
• Kinyonga: Huyu huwakilisha tabia ya ugeugeu. Watu wenye tabia ya
aina hii hawaonyeshi msimamo mmoja.
• Kunguru: Huyu ni ndege mwoga sana. Katika hadithi yeye huwakilishawatu ambao ni waoga.
2. Mtindo
Mtindo ni mbinu ya kipekee kwa kila msanii katika ufundi wake wa kifasihi. Kwa
mfano, namna msanii anavyotumia lugha (nahau, misemo, methali, tamathali
za usemi) na anavyoteua msamiati wa msingi. Hii ni kwa sababu lugha ndiyo
wenzo mkubwa wa msanii katika kazi za fasihi. Isitoshe kwa kuchunguza mtindo
tunachunguza namna msanii anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi
ya kwanza, ya pili au ya tatu, anaweza kutumia nyimbo kwa ajili ya burudani, n.k.).
Kwa kutunga hadithi ya masimulizi msanii anaweza kutumia majina ya watu au
akatumia wanyama, wadudu, ndege, miungu na kadhalika.
3. Muundo
Ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia msanii katika kupangilia zoezi lake, mpangilio
na mtiririko wa hadithi, kwa upande wa visa na matukio. Msimuliaji anaweza
kufuatanisha matukio moja kwa moja (Msago) au akasimulia kwa kurukaruka
hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na
mwanzo (urejeshi).
Isitoshe, hadithi za masimulizi au za paukwa pakawa huwa na mipangilio maalum.Hadithi hizi huwa na fomula yake katika utangulizi na mwisho wake.
• Mianzo ya hadithi za kimapokeo
i) Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Kaondokea chanjagaa
Kajenga nyumba kakaa
Mwanangu mwana siti
Vijino kama chikichi
Cha kujengea kikuta
Na vilango vya kupitia
Atokeani!
Hadhira: Naam twaibu!
Mtambaji:Hapo zamani za kale………………….
ii) Mtambaji: Paukwa!
Hadhira: Pakawa!
Mtambaji: Sahaniǃ
Hadhira: Ya mcheleǃ
Mtambaji: Giza!
Hadhira: La mwizi!
Mtambaji: Baiskeli!
Hadhira: Ya mwalimuǃ n.k.
Mtambaji: Hadithi hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Mtambaji: Hadithi hadithi!
Hadhira: Hadithi njoo!
Mtambaji: Hapo zamani za kale palikuwepo na …………………………
iii) Msimulizi: Atokaeni!
Hadhira: Naam Twaibu!
Msimulizi: Kaondokea chanjagaa, n.k.
• Hadithi huwa pia na miisho yake
Hadithi ikimalizika tunasema: “Huu ndio mwisho wa hadithi” au “Hadithi
inakomea hapa.”
1. Mandhari
Ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza
kuwa halisi kama vile nyumbani, baharini, njiani, msituni, kijijini, mjini lakini
vyote vinavyojulikana au ya kufikirika kama vile kuzimuni, mbinguni, peponi na
kadhalika. Katika hadithi nyingi za masimulizi wanatumia mandhali pa kubuni kwasababu mandhari hayo huwa ni ya kujiundia.
2. Muktadha
Muktadha ni mazingira au hali ambamo tukio au jambo fulani hutendeka. Ni
kusema kuwa msanii huishi katika jamii na jamii huzungukwa na mazingira
mbalimbali. Mazingira haya yanaweza kuonekana katika hadithi. Ukichambua
hadithi za masimulizi utagundua mazingira yaliyokuwa yakiwazunguka wasanii.
Haya yote huonekana kulingana na msamiati na dhamira msanii alizotia ndani yahadithi.
Mbali na vipengele vilivyotajwa hapo juu, tunapochambua hadithi
tunaanzia kwa kutaja kichwa na mtunzi kama anajulikana. Lakini mara nyingi
watunzi wa kazi za masimulizi hawajulikani. Kazi za masimulizi ni mali ya jamii.
• Maudhui katika hadithi za masimulizi
Maana ya maudhui
Katika somo la kwanza katika mada hii tuliona kuwa, katika kazi ya fasihi, maudhui
ni jumla ya mambo yote yanayozungumzwa au yaliyomsukuma msanii kuisana
kazi yake.
Katika uhakiki wa hadithi za masimulizi kimaudhui, vipengele vifuatavyo ni lazima
vizingatiwe: dhamira, migogoro, mitazamo falsafa, ujumbe pamoja na msimamo
wa msanii.
1. Dhamira
Dhamira huelezwa kama wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika
kazi ya fasihi. Kwa kawaida, dhamira zinagawika katika makundi mawili, kuna
dhamira kuu na dhamira ndogondogo. Dhamira zinazozungumziwa sana katika
hadithi za masimulizi ni uongozi, amani na maendeleo, mauaji, uroho, ujanja, hila,
uchoyo, upendo, uzalendo, ushirikiano, ujinga, uhaini, usaliti, wivu na kadhalika.
2. Migogoro
Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro
inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa
mbalimbali.Vilevile, migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, migogoro ya
nafsi, migogoro ya kisiasa, n.k. Katika hadithi za masimulizi nyingi tunakuta
migogoro kati ya wahusika wenye nguvu na wale wasio na nguvu na kwa mara
zote wenye nguvu huishia kwa kuanguka.
3. Falsafa
Kimsingi, falsafa ni elimu ya asili; busara au hekima. Falsafa ya msanii hugusiwa
kutokana na jinsi anavyoelewa matatizo ya jamii na jinsi anavyoyatolea suluhisho
kwa njia ya busara, amani na utulivu. Falsafa ya msanii wa hadithi za masimulizi
hugundulika unaposoma hadithi zake nyingi. Hapo ndipo utagundua mawazo au
saikolojia yake.
4. Ujumbe
Kila kazi ya sanaa huwa na ujumbe maalumu ambao msanii anataka uifikie jamii
aliyoikusudia. Ujumbe katika hadithi za masimulizi ni mafunzo mbalimbali ambayo
hupatikana ndani yake. Kwa kuwa hadithi zina umuhimu wa kuelimisha jamii
ndiyo maana kila unapomaliza kusoma au kusikiliza hadithi unaombwa kuelezasomo ambalo umepata.
Jibu maswali yafuatayo
1. Katika uhakiki wa fani ya hadithi tunachunguza nini ?
2. Taja na ueleze aina tano za hadithi.
3. Falsafa ya masanii ni nini?
4. Kwa sababu gani kuelewa usuli ni jambo muhimu?
• Mfano wa uhakiki wa hadithi ya masimulizi
1. Fani
• Kichwa cha hadithi: Kobe na Kijumbamshale
• Mtunzi: hajulikani.
• Wahusika
• Wahusika wakuu: Kijumbamshale, Kobe
• Wahusika wadogo: Jogoo, Fisi na Nyani na wanyama waliokuwa
wakisafisha mbuga.
• Watetezi: Jogoo (Alimwamsha Kobe) na Nyani (alimpatia ndizi)
• Wapinzani: Wanyama waliokuwa wakisafisha mbuga (walimcheka
Kobe).
• Tabia za wahusika: Kobe ni mhusika bapa kwa sababu hakubadilika
na Kijumbamshale ni mhusika duara kwa sababu alibadilika kimawazo
(alianzia kwa kupinga uwezo wa Kobe lakini mwishowe alikubali).
• Aina ya hadithi: Hurafa (wahusika ni wanyama na ndege).
• Mtindo: Katika hadithi hii masanii alitumia lugha ya kawaida. Hadithi
imeandikwa kwa lugha ya nathari (katika aya). Msanii alitia mazungumzo
katikati. Msanii alitumia:
-- Nahau: kunyakua ushindi (kushinda), kupunga hewa (kupumuzika), kukunja
uso (kukasirika)
-- Methali: Chelewachelewa utamkuta mtoto si wako, bandubandu huisha
gogo, linalowezekana leo lisingoje kesho.
-- Tamathali za usemi: kukimbia mbio kama umeme (tashbiha), takriri
(chelewachelewa, bandubandu).
• Muundo
-- Mwanzo wa hadithi ni “Hapo zamani za kale”. Na mwisho wake ni “Na huu
ndio mwisho wa hadithi.”
-- Msanii alitumia msago kwa sababu alisimulia moja kwa moja bila
kuchanganya matukio.
-- Msanii alitumia nafsi ya tatu kwa kusimulia hadithi yake. Lakini pia alitumia
nafsi ya kwanza na ya pili alipotumia mazungumzo kati ya Kijumbamshalena Kobe.
• Mandhari
Mahali panaposimuliwa hadithini ni njiani, kasri ya Malkia Tembo, Mbuga ya
wanyama: mandhari haya ni halisi kwa sababu ni mahali panapoweza kuonekana.
• Muktadha
Mtunzi alikuwa akiishi katika mazingira yenye dharau, bezo na upinzani kati ya
watu.
2. Maudhui
• Dhamira
• Dhamira kuu: kupingana kati ya kobe na Kijumbamshale
• Dhamira ndogo: usafi, harusi, michezo, dharau
• Migogoro
Migogoro inayopatikana katika hadithi hii ni migogoro kati ya wahusika
Kijumbamshale na Kobe (kutokubaliana kwa yule anayeweza kushinda mwingine
katika mbio).
• Falsafa
Falsafa ya mtunzi inatazamwa kwa kuangalia ni kipi ambacho mtunzi anaangalia
kuwa huo ndio ukweli katika maisha. Katika hadithi hii, inaonekana mtunzi
anaamini kwamba mafanikio katika maisha yanaletwa na uthubutu na maandalizi
ya kina.
• Ujumbe/ funzo
-- Kutodharauliana
-- Kukubali matokeo ya shindano-- Kuwa na adabu njema (Fisi alipitia wenzake bila kuwasalimu)