MADA YA HOTUBA 4 HOTUBA
• Malengo ya ujifunzaji
-- Kubainisha sehemu kuu za hotuba,
-- Kueleza mwongozo wa kutunga hotuba nzuri,
-- Kuonyesha tofauti iliyopo kati ya hotuba na aina mbalimbali za insha,
-- Kueleza tofauti kati ya usemi wa asili na usemi wa taarifa.
SOMO LA 8: MAANA YA HOTUBA
8.1. Kusoma na Ufahamu: Hotuba ya Afisa wa Umoja na
Maridhiano wilayani kwa Wananchi
Soma hotuba ifuatayo kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini:
Ndugu zangu wananchi, ndugu zangu wazalendo na ndugu zangu wazawa.
Hamjambo!
Ninasimama mbele zenu leo hii ili tuzungumzie kuhusu umoja wa Wanyarwanda.
Hebu tujitazame leo tunaishi vipi? Je, tunaishi kwa umoja kama Wanyarwanda?
Kabla sijasonga mbele, ningependa tukumbushane historia ya nchi yetu kuhusu
umoja. Hapo zamani za kale, katika enzi za ufalme, Wanyarwanda walikuwa
na umoja thabiti. Wote walikuwa wakimheshimu mfalme kwa pamoja bila ya
ubaguzi wowote. Mizozo midogo midogo ilipokuwa ikitokota ilikuwa ikitatuliwa
kidugu katika familia au katika vikao vya waungwana. Matatizo hayo yalikuwa
yakihusiana na kama vile mifugo au mashamba. Matatizo magumu yalikuwa
yakitatuliwa na viongozi na hata mfalme mwenyewe.
Wakati huu, umoja wetu ulikuwa ukirutubishwa na sherehe au hafla mbalimbali.
Mtu alipokuwa akitaka kujenga nyumba, majirani walikuwa wakimpa msaada
“umuganda” kwa Kinyarwanda. Aliyekuwa na harusi, majirani walikuwa wakimpa
msaada kama vile kazi za nyumbani zihusuzo matayarisho ya shughuli za harusi,
pombe, n.k. Kwa kuonyesha urafiki wa hali ya juu, Wanyarwanda walikuwa
wakichanganya damu na kuzawadiana mifugo hasa ng’ombe. Wakati wa vita,
Wanyarwanda walikuwa wakipigania usalama wa nchi yao kwa pamoja bila
ubaguzi wowote. Kwa upande wa malezi, mtoto alikuwa akikanywa na mtu
mzima yeyote yule katika jamii.
Ndugu zangu wananchi, wakati wa enzi za ukoloni, umoja wa Wanyarwanda
ulivunjika. Kwanza, wakoloni hawa walidunisha ufalme na watu wengi wakaanza
kugoma. Walivunja nguzo zote zilizokuwa zikishikilia umoja wa Wanyarwanda.
Kitu kibaya mno walichotufanyia na ambacho hatuwezi kukisahau, walituletea
makabila. Makabila haya yalipofika yalitenganisha watu: ndugu, mzazi na mtoto,mke na mume, walianza kuangaliana kwa kijicho na husuda.
Baada ya uhuru, mambo yaligeuka balaa zaidi. Wanyarwanda wengi walianza
kuuawa na Wanyarwanda wenzao. Hawa wa nyuma waligawana mashamba
yao na mifugo yao, walichoma nyumba zao na kuwakimbiza hadi nchi jirani.
Uvunjikaji huu wa umoja wetu ndio uliotufikisha kwenye mauwaji ya kimbari dhidi
ya Watutsi yaliyotokea nchini mwetu mnano mwaka wa 1994.
Afisa: Umoja oyee!
Wasikilizaji: Oyee! Oyee!
Afisa: Amani oyee!
Wasikilizaji: Oyee! Oyee!
Afisa: Utengano zuu!
Wasikilizaji: Zuu!
Ndugu wananchi wenzangu, wahenga walisema yaliyopita si ndwele, tugange
yajayo. Yaliyopita yalipita lakini yalituachia kovu kubwa. Yawe somo kwetu. Siku
hizi tunapaswa kusimama kidete na kuendelea na safari yetu ya kuendeleza
nchi. Safari hii si ya mtu mmoja pekee bali ni safari ya sisi sote Wanyarwanda.
Kwa hiyo, ninawaomba tuungane mikono. Serikali yetu ilipewa jina zuri “Serikali
ya Umoja wa Wanyarwanda.” Umoja huu unapaswa kuwa uti wa mgongo wa
maisha yetu kama Wanyarwanda. Tuishi kwa umoja, tusaidiane vilivyo kwa lolote
lile. Haya yatakapotendeka, nchi yetu inakuwa paradiso ya Afrika na majirani zetu
watatumezea mate.
Ninawashukuru kwa kunitegea masikio na nina imani kuwa kuanzia leo
mnakwenda kuimarisha umoja wetu zaidi ya sasa.Asanteni!
Maelezo muhimu: Maana ya usemi wa asili na usemi wa taarifa
• Usemi wa asili
Ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza .
• Usemi wa taarifa
Iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa
na mtu mwingine bila kupotosha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo
analotaka kulitolea maelezo, basi maneno hayo anayoyasema ni ``usemi wa
Taarifa.``
• Mambo muhimu katika usemi wa taarifa
Wakati wa kuandika usemi wa taarifa kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa ili
usemi huo uwe wa taarifa sahihi.
Maelezo muhimu: Maana ya usemi wa asili na usemi wa taarifa
• Usemi wa asili
Ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza .
• Usemi wa taarifa
Iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa
na mtu mwingine bila kupotosha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo
analotaka kulitolea maelezo, basi maneno hayo anayoyasema ni ``usemi wa
Taarifa.``
• Mambo muhimu katika usemi wa taarifa
Wakati wa kuandika usemi wa taarifa kuna mambo muhimu ya kuzingatiwa ili
usemi huo uwe wa taarifa sahihi.
1. Nafsi ya kwanza hubadilika na kuwa nafsi ya tatu
Mimi hugeuka kuwa yeye
Sisi hugeuka kuwa wao
Mfano:
-- “Mimi ninasoma kwa bidi,” mtoto alisema.
• Mtoto alisema kuwa yeye alisoma kwa bidi.
-- “Sisi tulisoma kwa bidi,” watoto walisema.
• Watoto walisema kuwa wao walisoma kwa bidi.
2. Badala ya kutumia wakati uliopo, wakati uliopita –li- ndio hutumika.
Mfano: Nina kazi nyingi ofisini.
• Alisema kwamba alikuwa na kazi nyingi ofisini.
3. Alama za kufunga na kufungua maneno hazitumiki kwenye usemi wa
taarifa .
4. Alama za kuuliza na kushangaa hazitumiki kwenye usemi wa taarifa
5. Katika usemi wa taarifa mahali penye wakati ujao -ta- kwenye usemi
wa asili hugeuka kuwa -nge-
Mfano: “Nitaondoka kuelekea Kigali,” shangazi alisema.
• Shangazi alisema kuwa angeondoka kuelekea Kigali.
6. Baadhi ya maneno hubadilisha nyakati yanapotumika katika usemi wa
taarifa .
kama :
Hapa huwa hapo
leo huwa ---siku hiyo/ile
wakati huu ------------wakati huo
kwetu -------kwao
kwangu ------kwake
sasa -----wakati huo/ule
Mfano:
-- “Nitaondoka sasa,” mgeni alisema.
• Mgeni alisema kuwa angeondoka wakati huo/ule.
“Tutacheza leo uwanjani,” wanafunzi walisema.
• Wanafunzi walisema kuwa wangecheza siku hiyo/ile uwanjani.
7. Mojawapo ya maneno yafuatayo hutumika katika usemi wa taarifa
Kuwa----kama ----kwamba
Mfano: -” Utanikuta mjini jioni hii, “Juma alimweleza rafiki yake.
• Juma alimweleza rafiki yake kuwa angemkuta mjini jioni ile.
Hotuba
i) Maana ya hotuba
Hotuba ni maelezo maalumu yanayotolewa na mtu mmoja mbele ya kundi la
watu. Hotuba inaweza kutolewa kwa madhumuni ya kutaka kuhimiza kazi, kufanya
kampeni fulani, kutoa taarifa fulani kwa watu.
ii) Aina za hotuba
a) Mahubiri: Ni hotuba za mafundisho ya kidini, zinazotolewa makanisani,
misikitini, n.k.
b) Hotuba za kisiasa: Ni hotuba zihusuzo taarifa ya serikali kama vile
kuwahimiza watu na kuwaalika kutenda jambo fulani, n.k.
c) Mihadhara: Ni hotuba au mafundisho ya mwalimu shuleni anapofundisha
kundi la wanafunzi na hasa wanafunzi wa vyuo vikuu.
iii) Sifa za hotuba
-- Ukweli wa habari na taarifa
-- Kujua vizuri aina ya watu unaowatolea hotuba, umri wao, kazi zao, n.k.
-- Ufasaha wa lugha ili iweze kupendeza na kueleweka vizuri
-- Nidhamu au adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo mbele
ya watu
-- Mantiki nzuri au mfuatano mzuri wa mawazo
-- Sauti ya kusikika vizuri
-- Kuvaa vizuri.
iv) Tofauti kati ya hotuba na insha
A) HOTUBA
• Hotuba hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/hatibu/kiongozi
anapozungumzia hadhira kuhusu jambo fulani.
• Mwandishi wa hotuba hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza
hotuba yake
• Mara nyingi hotuba huwa katika nafsi ya pili
• Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi,
shirika fulani, daktari, n.k
• Hotuba huanza kwa kutambua hadhira (waliohudhuria mkutano)
• Waliohudhuria mkutano hutajwa kwa vyeo vyao kuanza kwa yule wa
cheo cha juu hadi wa chini k.m: Waziri wa Elimu, Mkuu wa Wilaya,
mabibi na mabwana,……..
• Hatibu akiwa anawazungumzia hadhira isiyomjua, lazima ajitambulishe
• Katika hotuba, hatibu hutoa mapendekezo
• Mwisho wa hotuba humalizika kwa shukurani.
B) INSHA
• Mwandishi wa insha anaweza kunukuu yaliyosemwa na wengine
• Insha inaweza kuwa na mada ambayo mwandishi anatakiwa kutetea au
kupinga
• Katika insha mwandishi hataji vyeo vya hadhira
• Katika insha nyingi, mwandishi hatoi mapendekezo
• Mwisho wa insha hupangwa katika aya na haumaliziki kwa shukurani
Maswali
1. Eleza maana ya hotuba
2. Hotuba hutolewa kwa lengo gani?
3. Taja aina za hotuba
4. Eleza sifa muhimu za hotuba
9.1. Kusoma na Ufahamu: Kazi ni Kazi
Soma hotuba ya Katibu mtendaji wa wilaya katika harakati za uzinduzi
wa elimu ya kujitegemea kwa vijana « Kazi ni Kazi » katika Tarafa yaAmani wilaya ya Tujitegemee
Katibu: Kazi oyee !
Vijana: oyee ! Oyee ! Oyee !
Katibu: Uzembe zii !
Vijana: Zii !
Mheshimiwa Katibu Mtendaji wa Tarafa ya Amani,
Waheshimiwa wakurugenzi wa shule na vyuo
Waheshimiwa vijana,
Mabwana na mabibi mliokusanyika hapa,
Hamjambo?
Vijana ni nani ambaye hapendi kuishi? Sote tunapenda kuishi tena bila shaka
kwa raha. Licha ya hivyo, ili tuishi maisha ya raha mstarehe tunahitaji kufanya kazi.
Kazi ndio msingi wa uhai wa binadamu. Mtu asipofanya kazi hawezi kuyapata
mahitaji yake ya kila siku.
Kazi siyo adhabu kwani binadamu ameumbwa ili afanye kazi; ndiyo maana ana
akili, mikono, miguu, na viungo, vingine vya mwili. Viungo vyote hivi lazima vifanye
kazi ili maisha yawe mazuri. Mtu anahitaji kula, kuvaa na kuishi mahali pazuri. Lakini
ili kuyapata mahitaji yote, ni lazima afanye kazi. Hivyo basi, tunalazimika kufanya
kazi kwa kuwa kazi ni kitendo cha maendeleo. Maendeleo ya mtu huletwa na
kazi. Binadamu hupiga hatua za kwenda mbele kimaendeleo akifanya kazi kwa
bidii. Bila kufanya kazi, maendeleo ya nchi husimama ama hurudi nyuma.
Kazi ni za aina nyingi. Kuna kazi zinazotolewa na serikali au makampuni fulani na
kazi za kujitegemea. Kazi zote hizo ni kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, uchukuzi,
ulindaji wa usalama, ufanyabiasha na kadhalika. Kazi hizi zote zipo ili kujenga
nchi yetu. Hii ni kwa sababu nchi yetu itajengwa na mikono ya wananchi wake.
Siku hizi kuna wale wanaochagua kazi na kupuuza nyingine ati si kazi za heshima.
Msemo wa Kinyarwanda unasema « Hakuna kazi mbaya isipokuwa kuiba na
kuroga. » na Waswahili husema « Kazi mbi si mchezo mwema.»
Siku hizi kuna ongezeko la wasomi. Ongezeko hili halilingani na kazi zinazotolewa
na serikali yetu au makampuni na mashirika ya kibinafsi. Ndiyo maana tunahimizwa
sisi wenyewe kujitengenezea kazi za kibinafsi (kujiajiri). Sote hatuwezi kukaa
ofisini. Tuna mikono na akili, tengeneza kazi na usitegemee wengine kwani
« Mtegemea cha nduguye hufa maskini. »
Kazi ni wajibu wa kila mtu. Kila mtu analazimika kufanya kazi ili atoe mchango
wake katika maendeleo ya jamii. Mtu ni sehemu ya jamii. Kama mtu hafanyi kazi
hulegeza maendeleo ya jamii na matokeo yake ni kwamba jamii hukumbwa na
umaskini. Vijana, mnataka nchi yetu iendelee kuitwa maskini? Hapana! Nchi yetu
inapaswa kusonga mbele kama nchi nyingine zilizoendelea. « Mkiona vyaelea
vimeundwa. » Nchi zile zilizoendelea zilifikia kwenye kiwango kile kutokana
na juhudi, uzalendo na bidii ya raia wao. Kwa hiyo fukuzeni uvivu, ugoigoi nauzembe. Saidieni serikali yetu katika kazi za « umuganda.»
Vijana kumbukeni kuwa kazi ni bakora ya kuondosha umasikini maishani. Ili kuwa
na maisha bora, ni lazima kufanya kazi. Kumbuka kuwa hakuna mtu mwingine
atakayekufanyia kazi. Aidha, kumbuka kuwa jamii isiyofanya kazi ni jamii yenye
watu waliokufa. Kwa hiyo, kila mmoja akumbuke kutimiza wajibu wake. Msemo
wa Kinyarwanda unasema « Asiyefanya kazi hapaswi kula. »
Leo ningependa nitie nanga hapa. Ninawashukuru kwa kunitegea masikio.
Kuanzia leo tuzidi kuchapa kazi ipasavyo. Hii ni kwa kuwa “Kazi ni kazi, la muhimu
mtu amudu maisha.”Asanteni!
Maelezo Muhimu
Usemi wa asili ni yale maneno yanayotamkwa na mtu katika hali ya kwanza lakini
usemi wa taarifa ni kurudia maneno yaliyosemwa na mtu kwa njia nyingi bila
kupotosha maana ya kwanza. Usemi wa asili hutumia alama za mtajo, kuuliza
na kushangaa lakini usemi wa taarifa huishia kwa nukta. Katika usemi wa taarifanyakati na nafsi za vitenzi vilivyotumiwa katika usemi wa asili hubadilika.
9.4. Matumizi ya Lugha: Maelezo muhimu Kuhusu Muundo
wa Hotuba
Soma maelezo yafuatayo kisha ujibu maswali hapo chini.
• Muundo wa hotuba
Hotuba ina sehemu zifuatazo:
1. Anwani: Anwani, mada au kichwa cha hotuba huchukua mada ya hotuba.
Hiki ndicho kichwa chake hotuba.
Mfano: Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda katika Sikukuu ya Mashujaa.
2. Utangulizi: Mazungumzo katika utangulizi yanatoa mwangaza ama
picha ya habari inayokusudiwa kuzungumzwa. Anza hotuba yako kwa
kuwatambua waliohudhuria mkutano. Wataje kwa majina au vyeo vyao
kuanzia kwa yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana.
Kumbuka kwamba huhitaji kuwasalimia. Kuwatambua kwa vyeo vyao vya
pekee kunatosha.
Mfano: Waziri wa Elimu, Gavana wa Jimbo la Kusini, Mkuu wa Wilaya ya Nyanza,
Wanachama wa kikundi hiki cha Elimu Bora, mabibi na mabwana. Ni matumaini
yangu kwamba nyote mna afya nzuri.
3. Mwili/Kiini: Hakikisha kuwa kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi
mwisho. Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisi wala si
wa taarifa. Panga mawazo kufuatana na uzito ama umuhimu wake. Wazo
muhimu lazima lianze kuzungumziwa kwa ukamilifu halafu lifuatiwe na
mawazo mengine, nayo kwa kikamilifu.
4. Mwisho: Hapa mazungumzo yajumlishe mawazo yote yaliyozungumziwa
kwa maelezo fasaha. Ni vizuri kwa hotuba kufungwa kwa picha inayofanana
na ile ya utangulizi ili kumbukumbu ya habari ibaki katika mawazo ya
wasikilizaji.
• Sifa za hotuba
Hotuba safi huzingatia mambo haya:
• Ukweli wa habari na taarifa: Ni lazima mhutubi ahakikishe kuwa yale
anayozungumzia yana uhusiano na ukweli.
• Ufasaha wa lugha: lazima mhutubi kutumia lugha fasaha, nzuri, safi
na yenye kusikika vizuri kwa kila msikilizaji. Si vizuri kutumia lugha ya
mafumbo.
• Mantiki nzuri: Ni lazima kuweka kwa mfuatano mzuri wa mawazo au
fikra.
• Nidhamu: Yaani adabu njema ya mzungumzaji mwenyewe asimamapo
mbele ya watu.
• Sauti ya kusikia wazi pamoja na ishara zinazoeleweka na zinazohusianana yasemwayo. -Ishara hizo si za lazima iwapo hotuba inatolewa kwa
njia ya redio.
• Umuhimu wa hotuba
Hotuba huwa na umuhimu kwa mhutubu na kwa wanaohutubiwa.
Umuhimu huo ni kama vile:
• Kujenga ushirikiano
• Kuheshimiana
• Huondoaa ubaguzi wa kijinsia
• Huhamasisha watu kuwa viongozi walio bora
• Huwahamasisha watu kukuza vipawa na kushiriki katika kuonyesha
vipaji mbalimbali kama michezo ya kuigiza n,k kwa kusikiliza hotuba
zitolewazo.
Maswali
1. Hotuba inatarajiwa kuwa na sehemu zipi?
2. Katika kuanza hotuba yake, mhutubi hufanya nini?
3. Habari yenyewe hutolewa katika sehemu gani? Kwa nini?
4. Mwisho wa hotuba una maumbile gani?