MADA YA 1: UANDISHI WA BARUA ZA KIRAFIKI, MWALIKO NA MATANGAZO
Uwezo mahususi
Kuandika barua za kirafiki, mwaliko na matangazo kwa watu mbalimbali
Malengo ya ujifunzaji
- Kutaja sehemu kuu za barua za kirafiki, mwaliko na matangazo
- Kuchunguza muundo wa barua za kirafiki, mwaliko na matangazo
- Kutofautisha aina za barua za kirafiki, mwaliko na matangazo
- Kuelezea lugha inayofaa kutumiwa katika uandishi wa barua za kirafiki,
mwaliko na matangazo
- Kutunga barua za kirafiki kwa watu mbalimbali, barua za mwaliko na
matangazo ya aina tofauti
- Kuonyesha adabu na hehima kwa watu anaowaandikia- Kueleza matumizi ya aina za maneno
KIDOKEZO
Tazama kwa makini mchoro ufuatao kisha ujibu maswali
yaliyotolewa hapo chini:
Jibu maswali yafuatayo
-- Ni nini unachoona kwenye mchoro?
-- Ni mambo gani tunayotumia kwa kuwasiliana kimaandishi?
SOMO LA 1: BARUA YA KIRAFIKI
1.1. Kusoma na ufahamu: Wema HauoziSoma barua ifuatayo kisha ujibu maswali ya ufahamu.
Mpendwa Amina,Chuo cha Ualimu cha AmahoroS.L.P. 100,NGORORERO16/11/2019
Salamu!
Ninakuandikia waraka huu nikiwa nimejaa furaha ghaya kama mzazi aliyejifungua
pacha salama salimini. Wewe u mzima? Wazazi wako hawajambo ? Nasi hapa
nyumbani kwetu Ngororero mambo ni shwari.
Nia yangu ya kukuandikia barua hii ni kukushukuru kwa dhati ya moyo wangu.
Zaidi ya hayo ni kule kunialika kuja katika harusi ya dada yako huko kwenu. Harusi
ile ilikuwa ya kukata na shoka kabisa. Ilinivutia sana, hasa nilivyoona kwamba
harusi yenyewe ilionyesha utamaduni wetu wa Wanyarwanda bila kuchanganya
mambo ya kizungu. Hilo ni jambo nadra sana siku hizi wakati ambapo watu wengi
wamebobea uzunguni. Harusi ilionyesha mitindo ya asili na jadi. Bibi na bwana
arusi walikuwa wakipendeza mno na wakachagua kufanana sana kama mboni za
macho. Ninawaombea baraka za Bwana.
Zaidi ya hayo, usafi uliokuwa nyumbani kwenu ulikuwa wa kuvutia. Ugani
kulikuwa kunametameta na kupendeza kutokana na maua yaliyokuwa yakitoa
harufu nzuri. Vyakula na vinywaji vilivyoandaliwa mezani vilikuwa safi kwenye
kiwango kinachohitajiwa.
Isitoshe, ninakushukuru tena kwa msaada ulionipatia ukanisaidia masomoni
wakati tulipokuwa shuleni. Msaada wako ulinifaa zaidi kwa sababu niliweza
kushinda vizuri. Jambo hili lilinionyesha kwamba u rafiki wa kweli. Unajua?
Nilipofika nyumbani wazazi wangu walinichinjia jogoo! Nami wakati wowote ule
utakapohitaji msaada kutoka kwangu niko tayari kukupatia kwa kuwa « wema
hauozi ».
Kisha nisalimie wazazi wako na ndugu zako, maana walinishughulikia kupita
kiasi. Kwa hakika, ninashindwa niandike yapi hata waweze kuelewa upeo wa
furaha yangu.
Wako,gahamanjosGAHAMANYI Jonasi
KAZI 1
Maswali ya ufahamu :
a) Ni nani aliyeandika barua hii?
b) Taja jina la aliyeandikiwa barua.
c) Mwandikaji wa barua anasomea katika shule gani?
d) Mwandikajibarua anaishi wapi?e) Madhumuni ya barua hii ni yapi?
1.2. Msamiati kuhusu barua
KAZI 2
Baada ya kusoma barua ya hapo juu eleza maneno yafuatayo
-- Ghaya
-- Shwari
-- Nadra
-- Wamebobea
-- Dhati1.3. Sarufi : Aina za maneno ya Kiswahili
KAZI 3
Chunguza sentensi zifuatazo kisha utaje aina za maneno
yaliyopigiwa mistari.
-- Gahamanyi ni mwalimu wa chuo cha ualimu.
-- Darasa linasafishwa na wanafunzi wale.-- Yeye atakuja kesho.
• Gahamanyi, ualimu : ni nomino/majina
• Ni, linasafishwa ni vitenzi
• Cha, wale ni vivumishi• Yeye ni kiwakilishi
Maelezo muhimu kuhusu aina za maneno
Katika lugha ya Kiswahili kuna aina nane za maneno. Aina hizo ni kama vile
nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kihusishi, kielezi, kiunganishi na kihisishi.
Katika somo letu tutagusia kwenye aina nne yaani nomino, kivumushi, kiwakilishi
na kitenzi.
• Nomino (N)/ jina
a) Maana ya nomino
Nomino au jina ni neno linaloita kitu chenye uhai au kisicho hai kwa kukitoautisha
na vingine.
b) Aina za nonino
-- Nomino za pekee : Butare, Nyanza, Ngororero , Gahamanyi, Ibilisi,
Rukarara, Yesu, Akanyaru, …
-- Nomino za kawaida : ndege, gari, nyumba, kiongozi, tarafa, gunia, kobe,
miti …
-- Nomino za dhana au za dhahania : unyama, uzalendo, ualimu, utu,
ujinga, uroho…
-- Nomino za jamii/ za makundi : umma, familia, jamii, bodi, baraza,
genge, kikosi, jeshi, …
-- Nomino za wingi : mate, maji, mafuta, amani, madaraka, …
-- Nomino za kitenzi-jina : Kuishi kwingi kuona mengi. Kuimba kwakeni kuzuri.
KAZI 4
Baada ya kusoma maelezo ya hapo juu toa mifano mingine yaaina za nomino.
KAZI 5
Weka majina yafuatayo katika wingi
Vivumishi(V)
a) Maan ya kivumishi
Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu
vivumishi hutanguliwa na nomino.
b) Aina za vivumishi
• Vivumishi vya sifa
Mifano:
-- Mke mfupi yule ni mpole.
-- Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni.
• Vivumishi vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inayomiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi
hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali. Mizizi hiyo ni: -angu, -ako, -ake,
-etu, -enu, -ao.
Mifano :
-- Gari langu halina usukani.
-- jamii yao inaishi vizuri.
• Vivumishi vya idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi
vya idadi.a) Idadi kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
Mifano:
-- Mmomonyoko wa ardhi ulibomoa nyumba tatu katika kijiji kimoja.
-- Alipotaka kuoa wake wawili wanakijiji walimzuia.
b) Idadi Isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano: Chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani.
Mifano:
-- Watoto wengi waligeuka mayatima wakati wa mauaji ya kimbaridhidi ya
Watusi yaliyotokea mnamo mwaka wa 1994.
-- Mvua nyingi ilinyesha na kusababisha mmomonyoko wa ardhi.
• Vivumishi viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
-ngapi?, -pi? wapi?, gani?
Mifano:
-- Mtu yule ana miguu mingapi?
-- Ni mbuga ipi inayohifadhi simba nchini Rwanda?
• Vivumishi viashiria / vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Karibu: hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya.
Mbali kidogo: hapo, huyo, hiyo, hicho.
Mbali zaidi: pale, lile, kile. ule, wale, pale.
Mifano :
-- Kaeni mahali hapa.
-- Kijana yule ni mchezaji.
• Vivumishi visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria.
Mifano:
-- Amekuja pahali papa hapa.-- Kiongozi yuyu huyu anatutawala vizuri.
• Vivumishi virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa
vivumishi vya O-/-ye rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino.
Mifano:
-- Raia ambaye atakamatwa akiuza au akinunua magendo ataadhibiwa.
-- Wanyama ambao ni wakali sana ni simba na chui.
• Vivumishi vya A-unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki
nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na
kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino.
Mfano: cha, la, kwa, za, ya, wa, …-- Uchungu wa mwana aujuaye mzazi.
KAZI 6
Pigia mstari vivumishi katika sentensi zifuatazo:
a) Jua kali hili husababishwa na uharibifu wa mazingira yetu.
b) Maneno matamu yalimtoa nyoka yule pangoni mle.
c) Koti hilo refu limekugeuza mzee.
d) Usafi utafanywa na sisi sote wenyewe.e) Ni walimu gani watakaofundisha somo la Kiswahili?
a) Maana ya viwakilishi
Viwakilishi (w)
Viwakilishi vya nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishihakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.
b) Aina za viwakilishi
• Viwakilishi vya nafsi
-- Viwakilishi nafsi huru: Mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao.
-- Viwakilishi nafsi viambata : Ni-, u-, a-, tu-, m-, wa-, mi-, li-, ya-, ki-, vi-,i-, zi-, ku-, pa-
• Viwakilishi viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia
kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.
-- Haya ni madhara ya uharibifu wa mazingira.-- Wale wanahitaji amani.
• Viwakilishi visisitizi
Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia kiashiria chake mara mbili mfululizo.
Kwa mfano: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, zizi hizi,
→ Yuyu huyu ndiye rafiki yangu.
• Viwakilishi vya sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
Kwa mfano: -chungu, -eupe, -dogo, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, -gumu,
-kali, ekundu.
→ Cheupe Kinapendeza.
• Viwakilishi vya idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
a) Idadi Kamili - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino
-- Ukikata mmoja panda miwili.
-- Anafuga watatu tu.
b) Idadi isiyodhihirika - huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja
idadi kamili.
Mifano:
-- Tutasikiliza maoni ya wengi baada ya kuuratibu mpango huu.
-- Mengi yalisemwa kuhusu maradhi ya UKIMWI.
• Viwakilishi viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli.
Mifano:
-- Uko wapi?
-- Unahitaji vingapi?
• Viwakilishi vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
-- Kwetu kuna maji safi.
-- Zao zilibomolewa na mvua kali.
• Viwakilishi virejeshi
Hutumia O-/-ye-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino.
Kwa mfano: ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule.
-- Ambao walizaliwa mwaka huu watapimwa.
-- Ambaye anahitaji fedha za shule
• Viwakilishi vya A-unganifu
Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomilikiwa na nomino hiyo. Huundwa
kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha
a-unganifu.
Kwa mfano: cha, la, kwa, za, ya
-- Cha mlevi huliwa na mgema.-- La kuvunda halina ubani.
KAZI 7
Taja aina za viwakilishi vinavyopatikana katika sentensi zifuatazo:
-- Wao hawajafika kwangu.
-- Yule mweusi aende nyumbani.
-- La kuvunja halina rubani.-- Wengi walipanda miti kupambana na jangwa.
1.4. Matumizi ya lugha
KAZI 8
Soma upya barua uliyopewa hapo awali kisha utoe maana yabarua ya kirafiki na uonyeshe sehemu zake kuu.
Maelezo muhimu kuhusu barua ya kirafiki
a) Maana ya barua
Barua au waraka ni maandishi yaliyopangwa kwa utaratibu na mtiririko maalum
kwa minajili ya kuwasilisha ujumbe fulani. Barua ni risala au mmjumbe mwepesi
anayemwakilisha mtungaji wake kwa mtu mwingine na kuwasilisha taarifa yakekwa mtu huyo.
Barua huandikwa kwa madhumuni mbalimbali kama kuarifu, kuomba kitu kama
vile kazi, ruhusa; kuagiza bidhaa, n.k.
Kuna aina nyingi za barua lakini katika kitabu hiki tutashuhulikia barua tatu tu
ambazo ni:
-- Barua za kikazi zenye madhumuni ya kazi.
-- Barua za mwaliko zenye lengo la kualika mtu katika sherehe au sikukuu
fulani
-- Barua za kirafiki : ni zile ambazo huandikiwa na mtu au watu mbalimbali
walio na uhusiano wa karibu na anayeandika; k.v rafiki, ndugu, n.k. Barua
hizi zina uhuru mkubwa katika kuziandika. Hazidai utaratibu wa kipekee
sana. Mtu huwa huru kuandika apendalo ilimradi halimvunjii mtu heshima
yake.b) Sehemu za barua ya kirafiki
-- Anwani ya mwandikaji na tarehe: huandikwa kwenye pembe ya juu
upande wa kulia wa karatasi. Mwandikaji anaandika mahali anapoandikia
barua (au anapoishi). Anaweza kuongeza nambari za sanduku la posta
(S.L.P.) na mji, nambari ya simu na akaunti ya barua pepe. Tarehe huandikwa
chini ya anwani kwa kuacha nafasi ya mstari mmoja.
-- Jina la mwandikiwa: huja chini ya tarehe lakini kwenye upande wa
kushoto.
-- Salamu: sehemu hii hutoa maamkizi kwa mwandikiwa na huandikwa
chini ya jina la mwandikiwa.
-- Utangulizi: hujitokeza katika aya ya kwanza. Mwandikaji humjulisha hali
yake ilivyo,na kuuliza hali ya mwandikiwa na hata wenzake kwa jumla.
-- Barua yeynyewe: huu ni ujumbe kamili wa barua. Mwandikaji anaweza
kutumia aya moja au zaidi kulingana na urefu wa barua yake.
-- Hitimisho la barua: ni sehemu ya mwisho ya barua. Sehemu hii
huandikwa kwa aya moja na hujumlisha mambo ya kumuaga mwandikiwa.
Kwenye sehemu hii unaongeza maneno ya kuvutia (Wako, Wako mpendwa,
Mwanako, Wako mwaminifu, n.k.). Maneno haya huandikwa kwenye
upande wa kulia kabla ya kutia sahihi.
-- Sahihi ya mwandishi: huja chini ya hitimisho kwa upande wa kushoto.
-- Jina la mwandikaji: huja chini ya sahihi ya mwandikaji.
c) Aina za barua za kirafiki
Barua za kirafiki zinaweza kuwa mwana kwa mzazi au mzazi kwa mwana, za
mapenzi, za kindugu (kati ya ndugu), za kijamaa, n.k.
1.5. Kusikiliza na kuzungumza
KAZI 9
Tunga barua kisha uisomee wenzako hadharani kwa kuonyesha vitabia
1.6. Kuandika
KAZI 10
Mwandikie rafiki yako barua ukimwomba muende pamojakutembelea Mbuga ya Wanyama ya Akagera.
SOMO LA 2: BARUA YA MWALIKO
2.1. Kusoma na ufahamu: Ndoa ya dadangu
Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha ujibu maswali ya ufahamu.NDOA YA DADANGU
Ilikuwa Jumamosi tarehe 15 mwezi wa Novemba wakati nilipohudhuria harusi ya
dada yangu Mukashema Maria aliyefungana pingu za maisha na Mutabazi Joni.
Harusi yenyewe ilikuwa ya kukata na shoka.
Kabla ya wiki mbili za arusi kufanyika familia mbili zilikuwa katika pilikapilika za
hapa na pale ili kuandaa sherehe hii ya harusi. Kwa upande wa familia yangu sisi
watoto tulikuwa tukitumwa huku na kule kwa kuwaalika watu watakaohudhulia
harusi hii. Wazazi wangu waliwaalika wazee majirani na dada yangu akawaalika
wenzake hasa wa rika lake. Wote walikuwa wakipelekewa barua za mialiko.
Siku moja kabla, nyumbani kwetu tulifanya usafi na majirani walikuwa wakimsaidia
baba kutayarisha pombe ya mtama, ya ndizi na juisi. Wengine walikuwa
wakipamba uga na kujenga nyumba za mahema.
Siku hiyo ilipowadia watu walimiminika kuelekea nyumbani kwetu. Asubuhi
majira ya saa nne hivi, familia ya bwana harusi ilifika kwetu na kukaribishwa kwa
taadhima. Walikuwa wamekuja kuposa na kutoa mahari. Waliandaliwa vyakula
na vinywaji mezani wakafurahi sana. Furaha yao ilipandishwa na nyimbo pamojana ngoma za wachezaji waliokuwa hapo.
Baada ya hapo bi harusi alivishwa veli. Bwana harusi alirudi kumchukua akiwa
na gari la kifahari wakaenda kanisani ili kuvishana pete mbele ya Bwana. Nasi
tuliandamana nao tukiwa katika magari kadhaa. Watu walipoona mlolongo wa
magari hayo waliduwaa wakidhani kuwa kulikuwa na kongamano la kimataifa
katika kijiji chetu.
Tulipotoka kanisani, tulifurika bustanini kama ilivyoelezwa kwenye barua za
mwaliko walizopewa watu. Watu walikuwa wengi sana na sherehe ilifana sana.
Tuliandaliwa vinywaji na vyakula tele tele. Watu wote walifurahi sana na kuchezangoma na nyimbo za utanaduni
KAZI 1
Maswali ya ufahamu
a) Harusi inayosimuliwa ilifanyika lini ?
b) Harusi hiyo ilikuwa ya kina nani ?
c) Ni vinywaji gani vilivyotayarishwa siku moja kabla ya sherehe?
d) Watu waliokuja harusini walipataje habari hizo?e) Kwa sababu gani watu walioona magari walishangaa?
2.2. Msamiati
KAZI 2
Eleza maneno yafuatayo
a) Aliyefungana pingu za maisha
b) Pilikapilika
c) Kifahari
d) Mahemae) Veli
2.3. Sarufi: Aina za maneno
KAZI 3
Tazama sentensi zifuatazo kisha ueleze maneno yaliyopigiwa
mistari
a) Nyumbani humu mna usafi.
b) Tia taka nje.c) Simba anaishi ndani ya msitu ule.
Maelezo muhimu kuhusu aina za maneno
Katika lugha ya Kiswahili kuna aina nane za maneno. Aina hizo ni kama vile
nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kihusishi, kielezi, kiunganishi na kihisishi.
Katika somo letu tutagusia kwenye aina tatu yaani kitenzi, kielezi na kihusishi.
• Kitenzi
a) Maana ya kitenzi
Kitenzi ni neno linaloeleza jambo linalotendwa au kufanywa na nomino au
kiwakilishi chake.
b) Aina za vitenzi
-- Kitenzi halisi: Ni kitenzi kimoja kinachotumiwa katika sentensi.
Mifano :
-- Raia walifanya msaragambo.
-- Meya amekuja hapa.
-- Vitenzi vikuu na vitenzi visaidizi: Wakati vitenzi viwili hutumika pamoja
kueleza kitendo kimoja, kitenzi cha kwanza huitwa kisaidizi na cha pili
ndicho kitenzi kikuu.
Mifano :
-- Yeye alikuwa akicheza.
-- Wao wanahitaji kula vizuri.
• Vitenzi vishirikishi: Vitenzi vishirikishi vina dhana ya kitenzi kuwa au
kuwa na.
Vitenzi vishirikishi huwa vya aina mbili kuu :
• Vitenzi vishirikishi vikamilifu: Hivi huchukua viambishi vya wakati
na viambishi nafsi.
Mifano :
-- Wanafunzi wangali usingizini
-- Yeye atakuwa mzembe.
• Vitenzi vishirikishi vipungufu : Hivi huchukua viambishi nafsi lakini
havichukui viambishi wakati.
-- Walozi si wazuri.
-- Yeye yu mkweli.-- Nyinyi ni walimu wa kesho.
KAZI 4
Tunga sentensi ukitumia vitenzi vifuatavyo :
• - yu
• - kimuona
• - u
• - kaa• - ni
• Vielezi
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi
hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi na vielezi vingine.
Kuna vielezi vya namna, vielezi vya wakati, vielezi vya mahali na vielezi vya kiasi.
Mifano :
-- Mwanafunzi-mwalimu yule ameshinda mtihani vizuri (Kielezi cha
namna).
-- Mvua ilinyesha jana (kielezi cha wakati).
-- Samaki huishi baharini (kielezi cha mahali).-- Anamtembelea mara kwa mara (kielezi cha kiasi).
KAZI 5
Onyesha na utaje aina za vielezi vinavyopatikana katika sentensi
zifuatazo:
-- Simba huenda kimya anapowinda.
-- Vijana wa siku hizi huvaa kizungu, kichina na kihindi mara chache.
-- Wewe uliitwa mara kadhaa na hujaitika leo.
-- Gunia hili limejaa sana inafaa lipakuliwe.-- Imenyesha mchana kutwa
• Vihusishi (H)
Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano baina ya watu au vitu viwili auzaidi. Kuna vihusishi vya mahali na vya wakati.
Mifano:
-- Tutaonana baada ya wiki moja .
-- Si vizuri kuishi kando ya mto.
-- Ng’ombe hulala ndani ya zizi.
-- Ameondoka hapa kabla ya mvua kunyesha.-- Wao wanaishi pamoja kwa amani.
KAZI 6
Tumia vihusishi vifuatavyo kwa kujaza mapengo: katika, kabla ya,
mbele ya, baada ya, pembeni mwa.
a) Miti ilipandwa................nyumba.
b) .................mvua kunyesha unaona dalili zake.
c) Watu wengi waliangamia ..............ajali ya ndege iliyotokea nchini
Kongo.
d) ...............kuondoka tulimfuata huko.e) Hakuna mtu anayeishi...............shimo siku hizi nchini Rwanda.
2.4. Matumizi ya lugha
KAZI 7
Jibu maswali yafuatayo
a) Mtu anapowakaribisha wengine karamuni anatumia nini?
b) Mtu anaweza kuwaalika wengine kwa madhumuni gani?
KAZI 7
Maelezo muhimu kuhusu barua za mwaliko
Maana ya barua za mwaliko
Barua ya mwaliko ni ujumbe unaotolewa kwa kumkaribisha mtu kuhudhuria
shughuli au hafla fulani. Barua za mwaliko zinaweza kuwa na madhumuni
yafuatayo:
Sherehe
Karamu
HarusiUbatizo
Sikukuu ya kufunga mwaka
Sikukuu ya kupata cheti au digrii
Kuadhimisha miaka fulani, n.k
Mambo ya kuzingatiwa katika uandishi wa barua ya mwaliko
Jina la mwalikwa
Sababu ya mwaliko
Mahali ukaribisho utakapofanyika, terehe na saa
Jina na anwani ya mkaribishaji
a) Mifano ya barua za mwaliko• Barua ya mwaliko kwenye harusi
Karibu sana!RWEMA Eric
2.5. Kusikiliza na Kuzungumza
KAZI 8
Shirikiana na wenzako mzungumzie kuhusu uandishi wa barua za mwaliko.2.6. Kuandika
KAZI 9Mkaribishe mwenzako kwenye sikukuu yako ya kuzaliwa
SOMO LA 3: MATANGAZO
KAZI 1
Tazama kwa makini mchoro ufuatao kisha ujibu maswaliyaliyotolewa hapo chini:
Jibu maswali yafuatayo:
–– Ni nini unachoona kwenye mchoro huu?–– Unafikiri kuwa mtu huyo mwenye kipazasauti anafanya nini?
3.1. Kusoma na ufahamu: Tangazo la ajira
Soma tangazo lifuatalo kisha ujibu maswali ya ufahamu.
TANGAZO LA AJIRA
Wilaya ya CHAPAKAZI inayo furaha ghaya ya kuwatangazia watu wote wenye
uwezo kwamba ina nafasi za ajira za ufundishaji katika shule za chekechea na
msingi. Nafasi hizo ni kama zifuatazo:
1. Walimu wa Kiswahili katika shule za msingi (nafasi kumi)
2. Walimu wa Kinyarwanda katika shule za msingi (nafasi tatu)
3. Walimu wa Hisabati katika shule za msingi (nafasi tano)
4. Walimu wa Kifaransa katika shule za msingi (nafasi tano)
5. Walimu wa Kiingereza katika shule za msingi (nafasi tano)
6. Walimu wa Mafunzo ya kijamii katika shule za msingi (nafasi tano)
7. Walimu wa Sayansi katika shule za msingi (nafasi mbili)
8. Walimu katika shule za chekechea (nafasi ishirini)
Anayehitaji kazi hizo anapaswa kuwa na sifa zifuatazo:
1. Kuwa Mnyarwanda,
2. Kuwa na astashahada ya ukufunzi (A2),
3. Kuwa na uwezo wa kutumia tarakilishi na vifaa vingine vya TEHAMA,
4. Kuwa na uwezo wa kutumia Kinyarwanda na Kiingereza kwa ujumla.
Kwa wakufunzi wa Kiswahili wanapaswa kuwa na uwezo wa kutumia
kinyarwanda, Kiingereza na Kiswahili. Wakufunzi wa Kifaransa wanapaswa
kuwa na uwezo wa kutumia Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa.
5. Kuwa na afya bora,
6. Kuwa na umri usiozidi miaka thelathini,
7. Kuwa na uwezo wa kufanyia kazi katika eneo na mazingira yoyote.
Barua zenye maombi ya kazi pamoja na viambatisho vingine kama vile wasifu kazi,
kitambulisho cha uraia na astashahada, vitapokelewa hadi tarehe 20/12/2019katika ofisi ya katibu wa wilaya. Tarehe ya kusailiwa mtaijuzwa baadaye.
Tangazo limetolewa tarehe 1/12/2019.
Meya wa Wilaya ya Chapakazi
(Saini + mhuri)GAHIZI Musa
KAZI 2
Jibu maswali yafuatayo
Tangazo hili ni la aina gani?
Tangazo hili linalenga nani ?
Tangazo hili linatangaza nini ?
Neno TEKNOHAMA ni ufupisho wa nini ?Kwa sababu gani Meya wa wilaya alitia saini yake kwenye tangazo?
KAZI 3
3.2. Msamiati kuhusu tangazo
Eleza maneno yafuatayo :
-- Ajira
-- Shule za chekechea
-- Viambatisho
-- Astashahada-- Mhuri
3.3. Sarufi: Aina za maneno ya kiswahili
KAZI 4
Chunguza sentensi zifuatazo kisha utaje aina za maneno
yaliyopigiwa mistari.
-- Kobe na Kijumbamshale walikaa chini ya mti ili kuzungumza.
-- Lo! Umemwona mshamba yule!-- Fisi wala Simba hawakucheza mchezo wa riadha.
Maelezo muhimu kuhusu aina za maneno
KAZI 5
Soma maelezo yafuatayo kisha ujadili kuhusu matumizi ya maneno
yanayounganisha sentensi:
Katika lugha ya Kiswahili kuna aina nane za maneno. Aina hizo ni kama
vile nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi, kihusishi, kielezi, kiunganishi nakihisishi. Katika somo letu tutaona aina mbili yaani kiunganishi na kihisishi.
• Viunganishi (U)
Viunganishi ni maneno yanayofanya kazi ya kuunganisha. Huonyesha uhusiano
baina ya neno na neno, fungu moja la maneno na fungu jingine au sentensi na
sentensi.
Mifano:
a) Unataka maji au juisi?
b) Anasoma kitabu badala ya kupiga ubwana.
c) Kufanikiwa maishani si bahati bali ni kujishughulisha na kujitolea.
d) Alishinda mtihani ijapokuwa alipatwa na ugonjwa mkali.
e) Alienda shuleni bila kupata chakula.
KAZI 6
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia viunganishi vifuatavyo:
a) Halafu
b) Kisha
c) Ili
d) Ingawae) Kama
• Vihisishi (I)
Vihisishi ni maneno ambayo yanaonyesha hisia za mtu za ndani kwa mujibu wa
hali na muktadha. Yanaonyesha hangaiko la moyo ama kudokeza mguso wamoyo ama hata wa akili.
Mifano:
Mtume! Umefika asubuhi hii!
Lo! Mvua imenyesha!Salaa! Inawezekana mtu kunywa chupa ishirini za juisi!
KAZI 7
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia vihishi vifuatavyo:
a) Mungu wangu!
b) Mama wee!
c) Ng’o!
d) Barabara!e) Masalale
3.4. Matumizi ya lugha
KAZI 8
Soma upya tangazo la hapo juu kisha ujadiliane na wenzako kuhusu muundowa matanganzo.
Maelezo muhimu kuhusu matangazo
Maana ya tangazo
Tangazo au ilani ni mpangilio wa maandishi kwa mtindo maalumu kwa lengo la
kupasha habari ama kupokeza ujumbe fulani wa kidhalura au muhimu. Taarifa
inayosambazwa kwa tangazo inaweza kuwa kifo, mkutano, taratibu za kutumia
barabara vizuri, kazi na mengineyo.
Aina za matangazo
Zipo aina nyingi za matangazo
Matangazo ya kibiashara
Matangazo ya kifo
Matangazo ya serikali, n.k.
Mambo ya kuzingatiwa katika uandishi wa matangazo
Kwa kuandika tangazo ni lazima kuzingatia mambo yafuatayo :
Kichwa cha tangazo
Kutaja anayetoa tangazo
Kutaja walengwa wa tangazo
Ujumbe wa tangazo
Sahihi na jina la anayetoa tangazo (tangazo lisilokuwa na sehemu hii huitwa
tetesi, fununu au uvumi)Mfano wa tangazo
3.5. Kusikiliza na Kuzungumza
KAZI 9
Sikiliza matangazo redioni kisha ujadiliane na wenzako kwakuzingatia maudhui, aina ya matangazo na lugha iliyotumiwa.
3.6. Kuandika
KAZI 10Tunga tangazo la kibiashara
Tathmini ya mada
1. Eleza maana ya barua.
2. Taja aina za barua tulizoona.
3. Zitaje sehemu kuu za barua ya kirafiki.
4. Ni mambo gani muhimu yanayopaswa kuonekana kwenye barua ya
mwaliko?
5. Tunga tangazo la kazi.
6. Taja aina za meneno yanayojenga sentensi zifuatzo.
-- Eeh! Unataka kitu gani?
-- Wao walikufa hapa na kuondoka haraka.
-- Mama alikuwa akipalilia maharagwe yake katika bonde lile.
-- Ingawa mvua ilinyesha vizuri, mavuno yanaendelea kudidimia.-- Chukua hicho kizuri ila hakitoshi.