• MADA YA 5 UANDISHI WA RIPOTI

    Malengo ya ujifunzaji

    -- Kutaja aina za ripoti na sifa zake muhimu,

    -- Kuonyesha mbinu na taratibu za kutunga ripoti za aina mbalimbali,

    -- Kubainisha mazingira mbalimbali ya kutolea ripoti,

    -- Kuonyesha vipashio vya tungo za Kiswahili.

    SOMO LA 10: MAANA YA RIPOTI
    10.1. Kusoma na Ufahamu: Ziara ya Kielimu

    Soma ripoti ifuatayo hapo kisha ujibu maswali ya hapo chini.
    Ripoti ya Ziara ya Kielimu Iliyofanywa na Wanachuo wa Mwaka wa 3
    Chuo cha Ualimu Busara katika Majumba ya Makumbusho mnamo
    Tarehe 10/7/2019 hadi 12/7/2019.

    Katika mchakato wa ukufunzi na ujifunzaji, wakufunzi na wanafunzi huhitaji kufanya
    ziara za kielimu ili kunoa ujuzi wao. Ndiyo maana kuanzia tarehe 10/7/2019
    hadi 12/7/2019 wanachuo wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Ualimu Busara
    walifanya ziara ya kielimu katika majumba ya makumbusho yanayopatikana
    hapa nchini Rwanda. Lengo kuu la ziara hizi lilikuwa kuelewa zaidi historia na
    utamaduni wa Wanyarwanda. Ziara hizi ziliongozwa na Mkufunzi Steven Kabera.
    Majumba ya Makumbusho Yaliyotembelewa

    i) Jumba la Makumbusho la Rukali-Nyanza
    ii) Jumba la Makumbusho la Huye
    iii) Jumbala Makumbusho la Nyarugenge

    Tarehe ya 10/7/2019 ndipo walianza ziara zao. Wanachuo na mkufunzi wao
    walianzia katika wilaya ya Nyanza, wakatembelea Jumba la Makumbusho
    linaloonyesha maisha ya wafalme. Katika jumba hilo, wanachuo walielezwa
    mengi kuhusu maisha ya wafalme walioongoza Rwanda. Hapo walionyeshwa
    vifaa tofauti vilivyokuwa vikitumiwa na wafalme hawa na Wanyarwanda kwa
    ujumla kabla ya ukoloni. Zaidi ya hayo, jumba hili la Rukali huhifadhi ng’ombe wa
    kupendeza macho “Inyambo” kwa Kinyarwanda na nyumba za kifalme.

    Walipopewa fursa ya kuuliza, wanachuo waliuliza maswali mbalimbali yaliyopata
    majibu kutoka kwa wahudumu wa Jumba hili.

    Kwenye tarehe ya 11/7/2019 ziara ya wanachuo ilielekezwa katika Wilaya ya
    Huye, katika jumba la makumbusho linalohusu maisha ya Wanyarwanda kwa
    ujumla. Katika jumba hili, wanachuo walitembezwa katika vyumba mbalimbali
    vinavyounda jumba hili na kuonyeshwa vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na
    Wanyarwanda. Mahali hapa, wanachuo walipewa maelezo ya kina kuhusu
    historia ya Wanyarwanda toka enzi za wafalme hadi utawala wa jamhuri.

    Kwenye tarehe ya 12/7/2019 usukani ulielekezwa jijini Kigali katika Jumba la
    Makumbusho la Nyarugenge. Katika jumba hili, wanachuo walielezwa namma
    ambavyo wakoloni walikuwa wakiongoza nchi ya Rwanda. Zaidi ya hayo,
    wanachuo hawa walielezwa kuwa jumba hili lilikuwa ofisi ya kiongozi wa kwanza
    wa kikoloni Dkt. Richard Kandt. Pia, waliambiwa kuwa huyu ndiye aliyefanya
    Kigali kuwa mji mkuu wa Rwanda. Vilevile, wanachuo walionyeshwa nyoka
    mbalimbali na mamba wanaohifadhiwa katika jumba hili.

    Ziara hizi zilipomalizika, wanachuo walikaa pamoja katika ukumbi wa chuo
    na kujadiliana kuhusu yale yote waliyoyaona. Kwa pamoja, waliamua kuwa
    wametosheka kabisa. Lakini walitoa mapendekezo yafuatayo:

    -- Wanaomba chuo kuandaa ziara za kielimu nyingine katika majumba mengine
    yaliyobakia kama Jumba la Makumbusho la Karongi (linahifadhi mambo
    ya kimazingira), Jumba la makumbusho la mapambano ya kujikomboa la
    Kimihurura, Handaki ya Mulindi wa Mashujaa (ku Mulindi w’Intwari), Jumba
    la Makumbusho la Mambo ya kisanaa la Kanombe, na kadhalika.

    -- Wanaiomba Serikali ya Rwanda, kupitia Bodi ya Maendeleo ya Rwanda

    (RDB) kutafuta mbinu thabiti za kulinda majumba haya ya makumbusho na

    kuhifadhi vitu na vifaa vyote vilivyomo humo.

    -- Wanawashauri Wanyarwanda kutembelea katika majumba haya ili kujua

    historia na utamaduni wao.

    Imetayarishwa na.

    Jina: Steven Kabera

    Cheo: Mkufunzi wa Kiswahili

    Saini: Stevkabera

    Tarehe: 13/7/2019

    Maelezo muhimu kuhusu sehemu za tungo

    i) Maana ya tungo

    Tungo ni fungu la maneno ambayo yanawakilisha nafsi, kitu kinachotendwa

    au jambo linalopasha habari kamili. Pengine tungo ni kipashio cha kimuundo

    kinachotokana na uwekaji pamoja wa vipashio sahili ili kujenga kipashio kikubwa

    zaidi. Kipashio ni kipande cha tungo ambacho huweza kujenga au kujengwa

    na tungo nyingine.

    ii) Aina za tungo

    Kiswahili kina tungo nyingi sana; nyingine ni fupi sana, nyingine ni ndefu sana.

    Ziko tungo zilizojengwa kwa neno moja tu, na nyingine kwa maneno mengi.

    Kwa mfano :

    -- Tunasoma.

    -- Masika yanakaribia.

    -- Mwana wao wa pekee aliwasaidia.

    Tungo za Kiswahili ni nyingi, lakini zinaweza kuwekwa katika makundi ya idadi

    ndogondogo kwa kufuata misingi fulani fulani ya kisarufi. Angalia mfano huu :

    a) Msingi wa muundo wa tungo

    b) Msingi wa maana za tungo

    Kwa msingi wa muundo wa tungo, tungo hugawanyika katika aina kuu tano :

    1. Tungo sahili (Mwanafunzi anafagia.)

    2. Tungo tegemezi (Aliyefika)

    3. Tungo changamano (Mwanafunzi aliyefika anafagia.)

    4. Tungo ambatano (Kijana amekuja na ameondoka.)

    5. Tungo shurtia (Mvua ingenyesha mapema tungepanda mahindi.)

    Kwa msingi wa wa maana za tungo, tungo hugawanyika pia katika

    aina nne

    1. Tungo sahili (Mwanafunzi amefika.)

    2. Tungo tegemezi (Aliyefika)

    3. Tungo nyofu: yenye maana moja tu. (Sipendi kunywa pombe)

    4. Tungo tata: yenye maana zaidi ya moja (Sipendi kunywa bia [ tanbihi:bia

    humaanisha pombe au ‘pamoja; kwa kushirikiana na mtu mwingine])

    iii) Sehemu za tungo

    Kwa kawaida tungo ya Kiswahili inaundwa na sehemu mbili kubwa. Sehemu hizo

    ni kiima na kiarifu/ kiarifa au prediketa.

    Kiima ni sehemu ya tungo inayoonyesha nafsi ya mtenda au mtendwa wa jambo

    linaloelezwa yaani kuarifiwa. Kiima huandikwa kushoto mwa kitenzi. Kiima ndiyo

    sehemu ambayo hutoa upatanisho wa kiambishi awali cha kitenzi.

    Kiarifu /kiarifa/prediketa ni sehemu katika tungo ambayo huzungumza

    juu ya kiima. Ni kusema sehemu ya sentensi yenye kitenzi na vipashio vyake

    (shamirisho na chagizo).

    i) Maana ya Ripoti

    Ripoti ni maelezo ya kuhusu mtu, kitu au jambo fulani lililotokea. Ni aina ya
    kumbukumbu ambazo huandikwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Ripoti
    inaweza kuwa ya uchunguzi wa utafiti kuhusu jambo fulani, inaweza kuwa ya

    polisi, daktari au ya tume fulani.

    ii) Namna ya Kuandika Ripoti

    Kabla ya kuandika ripoti, lazima kuwe na ushahidi unaohusu suala au jambo
    linaloandikiwa ripoti hiyo. Kwa hiyo, ni lazima mtunzi afanye uchunguzi
    kwanza. Pia mtunzi anapaswa kufahamu kiwango cha elimu na uwanja wa mtu
    anayemwandikia ripoti hiyo. Kwa mfano kama ni polisi, daktari, mwanasheria,
    mfanyabiashara, n.k. Lugha atakayoitumia mwandishi au mtunzi izingatie

    muktadha wa matumizi. Lugha itegemee aina ya ripoti.

    i) Sehemu za ripoti

    a) Kichwa cha ripoti

    Kichwa cha ripoti hutambulisha kiini cha ripoti. Yaani ripoti inahusu nini, tarehe

    ya tukio au jambo linaloandikiwa ripoti na mahali palipotokea jambo hilo.

    b) Utangulizi wa ripoti

    Katika hatua hii mwandishi hueleza kwa muhtasari madhumuni ya ripoti.

    c) Kiini cha ripoti

    Katika sehemu hii mwandishi hueleza mambo aliyoyaona, chanzo chake na

    madhara au faida yake.

    d) Hitimisho

    Katika kuhitimisha ripoti mwandishi anaonyesha msimamo na mapendekezo
    yake. Baada ya hitimisho, mwandishi huandika au huonyesha aliyeandika ripoti,
    cheo chake (nafasi yake hasa katika ripoti hiyo) na tarehe ripoti hiyo ilipoandikiwa.

    Ikumbukwe kuwa aghalabu ripoti huandaliwa ili kutaka mageuzo fulani ya jambo.

    v) Aina za Ripoti

    Ripoti ni za aina nyingi:

    -- Za kielimu

    -- Za mikutano

    -- Kiuchumi

    -- Kijamii

    -- Kisiasa

    -- Kiusalama

    vi) Sifa za Ripoti

    Ripoti ni lazima iwe na mpangilio mzuri wenye mada zinazozungumziwa na labda
    hata mada ndogo ndogo zenye kuzingatia utaratibu wa nambari. Matumizi ya
    nambari husaidia kuipa ripoti mpangilio mzuri na wenye kueleweka kwa urahisi.
    Ripoti hazipaswi kuwa ndefu sana na zinapaswa kuwasilisha mambo muhimu
    kwa ufupi. Mwandishi wa ripoti hutumia mbinu za kufupisha lakini anahakikisha
    kuwa kila kitu kimezungumziwa. Ripoti hutumia sentensi fupi fupi zinazowasilisha
    mambo muhimu kwa uwazi. Ni vyema lugha inayotumiwa katika ripoti iteuliwe
    kwa uangalifu na isiwe na hisia au sifa ya kuathiri vibaya wanaoisoma.

    Jibu maswali yafuatayo :

    1. Ripoti ni nini?

    2. Taja angalau mambo matatu ya kuzingatia wakati wa kuandika ripoti.

    3. Taja sehemu za ripoti

    10.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano





    11.1. Kusoma na Ufahamu: Ripoti ya Maandalizi ya
    Mafunzo ya Elimu Jumuishi
    Soma ripoti ifuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini:

    Ripoti ya Maandalizi ya Mafunzo ya Elimu Jumuishi Yaliyofanyika
    tarehe 2/11-15/11/2019 katika chuo cha TUENDELEZE ELIMU.

    Mnamo tarehe 2/11/2019 hadi 15/11/2019 yalifanyika mafunzo kuhusu elimu

    jumuishi. Mafunzo haya ili yaweze kufanikiwa, yalihitaji ufasaha wenye maandalizi
    ya kutosha yaliyochukua wiki mbili. Ilifanyika hivi ili wakufunzi waweze
    kufanikisha kuandaa mada husika . Kufanikiwa kwa maandalizi hayo ni kutokana
    na juhudi za wakufunzi wenyewe kuwa na moyo wa kujituma, na ushirikiano
    mkubwa ulioonyeshwa na jopo la uongozi wa chuo cha Ualimu“TUENDELEZE
    ELIMU” kilichopo wilayani ya Matumaini.

    Wakufunzi tulifurahia ushirikiano kutoka chuo “TUENDELEZE ELIMU” kwani
    kila kitu tulichohitaji ili kufanikisha mafunzo yetu kilitolewa na uongozi wa chuo
    bila tatizo lolote. Ushirikiano wao ulikuwa katika vifaa vya maandalizi, chakula na
    malazi, posho kwa ajili ya kujikimu na usafiri. Hayo yote yalikuwa changamoto
    kwa wahadhiri na washiriki wa mafunzo.

    Utoaji wa mafunzo
    Mafunzo yalifanyika kwa muda wa siku tano saa nane zilitumika kwenye mafunzo
    na saa mbili zilitumiwa kwenye majadiliano, kwa ajili ya chakula na mapumziko
    kwa wakufunzi, walengwa na uongozi.

    Zifuatazo ni mada mbalimbali zilizotolewa kwenye mafunzo haya:
    1. Njia Shirikishi katika Ujifunzaji
    Njia shirikishi katika kujifunza ilipewa kipaumbele katika muda wote wa mafunzo.

    Njia hii ilihamasisha wanachuo kushiriki zaidi katika mazoezi na kwa kiwango
    fulani iliwasaidia pia kushiriki katika kujifunza. Njia hii ilileta msukumo katika
    kutafuta majibu na kuunganisha pamoja taarifa kutoka vyanzo mbalimbali, badala
    ya kumtegemea tu mkufunzi kuongoza vipindi vyote vya masomo. Kwa sababu
    elimujumuishi si dhana rahisi ambayo inaweza kutumika kwa namna moja, katika
    sehemu zote, wanachuo katika mafunzo ya elimujumuishi wanapaswa kupewa
    mwongozo wa kutafuta na kupata habari sahihi na kutafuta njia bora ya kusonga
    mbele kwa kuanzia sehemu walizopo. Zaidi ya mazoezi yaliyokuwa yamepangwa
    kwenye ratiba, ushirikishwaji katika kujifunza ulifanywa pia katika majadiliano ya
    nje wakati wa mapumziko, na katika maktaba ndogo ambamo washiriki huweza

    kupata nafasi ya kujisomea katika muda wa ziada.

    2. Umuhimu na sifa za mafunzo haya
    Mafunzo yalilenga kuendeleza dhana kwamba hupaswi kujifanya mjuaji zaidi wa
    elimu jumuishi kwa kufanya peke yako matendo ambayo unadhani yanaifanya
    elimu iwe jumuishi zaidi. Kila mmoja ana mawazo na uzoefu wake ambapo yote
    ni muhimu katika kuendeleza mfumo wa elimu jumuishi na jamii nzima.

    3. Stadi za mawasiliano
    Ingawa kulitumiwa uwasilishaji wa mada au kazi za vikundi, tulihitaji stadi maalum
    za mawasiliano. Tunapaswa kuwaelezea watu kuhusu sisi wenyewe, kazi zetu,
    uzoefu wetu au mawazo yetu, na mara kwa mara tunahitaji uwezo wa kufanya
    hivi kwa muda mfupi. Ni kawaida kwa wanachuo kukosa ujuzi na/au kutojiamini
    katika mawasiliano. Hii inaweza kuathiri maendeleo na matokeo ya mafunzo
    hasa ukizingatia kwamba wanachuo wanatarajiwa kuchangia hoja na uzoefu
    na siyo kuwa wasikilizaji.

    4) Hitimisho
    Katika kuhitimisha ripoti waandaaji wa mafunzo walitoa shukrani zao kwa jopo
    zima la chuo na uongozi na watendaji wake kwa ushirikiano wao mzuri
    waliouonyesha kwa mijadala yao mizuri iliyowawezesha kujua tatizo lipo wapi
    na pia kuibua uzoefu uliopo na hatimaye kwa pamoja kuweza kutambua udhaifu
    upo wapi. Hatua hii itasaidia kutoa uzoefu wa namna ya kurekebisha ambapo

    hapakwendeka vizuri.

    Kipashio

    Kipashio ni neno moja au kifungu cha maneno chenye kazi maalum katika

    tungo. Vipashio hivi ndivyo ambavyo huungana pamoja na kujenga sehemu kuu

    za tungo yaani kiima na kiarifu.

    • Vipashio vya kiima

    Kiima kinaweza kuundwa na vipashio vya aina mbili: neno moja au fungu la

    maneno.

    a) Neno moja katika kiima

    i) Nomino (N): Kazi ni uhai.

    ii) Kiwakilishi (W): Yeye hapendi kushiriki ngono.

    -- Huyu ni kiranja wetu.

    iii) Kitenzi-jina: Kuimba kunapendeza.

    iv) Kishazi: Atakayevuta bangi ataadhibiwa.

    b) Fungu la maneno katika kiima

    i) Nomimo mbili (N+N): Baba na Mama wanafanya kazi za Umuganda.

    ii) Bwana Kagabo ni mcheshi.

    iii) Nomino na kivumishi (N+V): Mwanafunzi hodari hana wasiwasi.

    iv) Kiwakilishi na kivumishi (W+V): Huyu hodari hana wasiwasi.

    v) Nomino na kishazi: Mwanafunzi atakayevuta bangi ataadhibiwa.

    • Vipashio vya kiarifu

    Kiarifu kinaweza kuundwa na vipashio vya aina mbili: neno moja na fungu la

    maneno

    a) Neno moja katika kiarifu

    i) Kitenzi (T): Mama analima.

    b) Fungu la maneno katika kiarifu

    i) Kitenzi na Kitenzi (TS+T): Yeye anapenda kucheza.

    ii) Kitenzi na shamirisho (T+SH (N)): Yeye anacheza mpira.

    (T+SH(W)): yeye anapenda yule.

    iii) Kitenzi na chagizo (T+CH (E)): Yeye anacheza vizuri.

    (T+CH(HU)): Yeye alienda kwa mganga.

    iv) Kitenzi na kishazi: Yeye anacheza tunapolala.

    • Taratibu za kufuatilia wakati wa kuandaa ripoti

    Unapoandika ripoti unapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:

    • Hakikisha kuwa umeelewa shughuli inayohusika

    • Hakikisha unajua urefu unaohitajika na masuala unayopaswa kuyagusia

    • Kusanya maelezo yote unayohitaji kuhusiana na ripoti hiyo.

    • Yapange maelezo yako vizuri. Zipitie hoja zako ili uondoe mawazo

    ambayo yanaweza kuwa yamerudufishwa au yamerudiwa.

    • Yaangalie mawazo yako ili kubainisha ni yapi ambayo yanapaswa

    kutangulia na yanafuatwa na yapi.

    • Unapoandika ripoti yako hakikisha kuwa unaitumia lugha yako. Usiridhike

    tu na maneno unayoyapata wakati wa uchunguzi wako. Kuandika ripoti

    kwa lugha na maneno yako huonyesha kuwa umeielewa.

    • Unaweza kuuboresha uwezo wako wa kuandika ripoti kwa kujitahidi

    kuyaelewa maelezo yanayohusika na kujitahidi kuyaeleza kivyako.

    • Baada ya kuandika nakala ya kwanza ya ripoti unaweza kuiboresha kwa

    kupunguza mambo ambayo siyo muhimu katika ripoti hiyo.

    • Lugha inayotumiwa katika uandishi wa ripoti lazima izingatie wasomaji

    wa ripoti inayohusika. Kwa mfano, ikiwa wasomaji ni wanafunzi wa shule

    lugha yake haipaswi kuwa na ugumu au utata wa kisayansi.

    • Mifano ya mazingira ya kutolea ripoti

    • Kila jambo mtu analofanya kila mara nyingi huomba kutolewa ripoti. Kwa

    mifano:

    -- Mwanafunzi anaweza kutumwa kuwakilisha chuo chake katika kongamano

    la vilabu mbalimbali akatoa ripoti baadaye.

    -- Mwanfunzi anaweza kuenda kujizoeza kufundisha katika chuo fulani,

    anapomaliza akaombwa kutoa kuripoti kwa chuo chake.

    -- Mtangazaji wa habari anaweza kufanya utafiti kuhusu jambo fulani kisha

    akatoa ripoti kwa yale aliyoyaona.

    -- Mtafiti fulani anaweza kutumwa kuchunguza mambo fulani (ukiukaji wa

    haki za kibinadamu, kuenea kwa ugonjwa fulani, kiwango cha hongo, n.k)

    kisha akatoa ripoti.

    -- Maafisa wa kiserikali wanaweza kufanya utafiti kuhusu maisha ya jamii

    (uchumi, kilimo, ufugaji, …) wakatoa ripoti kwa serikali.

    • Mazingira ya kutolea ripoti ni mengi mno, ripoti zinaweza kutolewa katika

    mikutano, darasani, kwenye televisheni, redioni, katika hafla, katika vikao

    vya dharura, katika makongamano na kadhalika.

    Jibu maswali yafuatayo

    1. Uboreshaji wa ripoti hufanyika namna gani?

    2. Kwa sababu gani mwandishi wa ripoti analazimishwa kuzingatia vizuri

    lugha anayoitumia?

    3. Taja mazingira matatu ya kutolea ripoti.

    MADA YA HOTUBA 4 HOTUBAMADA YA 6 UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI SIMULIZI