Topic outline

 • SURA YA 1: NADHARIA NA TANZU ZA FASIHI SIMULIZI YA KISWAHILI. SOMO LA 1: FASIHI YA KISWAHILI NI NINI?

  Kazi ya 1: Jiunge na mwenzako na kutazama picha ya hapa chini. Mtoe maoni yenu kuhusu picha hiyo.

  Kazi ya 2: Katika kundi hilo, mweleze maana ya jambo wanalolizungumzia.  Kazi ya 3: Katika kundi hilo, baada ya kukisoma kifungu cha habari cha hapa chini, mkihusishe na picha hiyo.

  Dhana ya fasihi na fasihi ya Kiswahili

  Somo hili si geni kwa mwanafunzi kwani ni mada iliyoshughulikiwa katika Kitabu cha Mwanafunzi, kidato cha nne. Hatuwezi kusema kuwa tulisoma mengi katika muktadha huu kwa sababu tulitoa maelezo bila kuingia katika undani. Mara hii, ndipo tunatarajia kufasili kwa kina fasihi ya Kiswahili.

  1. Nadharia ya fasihi na dhana yake

  Fasihi, kama dhana, ilielezwa na wataalamu wengi kwa kuegemea nadharia na mitazamo mbalimbali. Ieleweke kuwa nadharia ni taratibu, kanuni na misingi inayomwongoza mtafiti au mtaalamu. Nadharia husaidia katika kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo imara zaidi kuliko mtazamo mwingine. Nadharia kuhusu kueleza chanzo, ukuaji na ueneaji wa fasihi simulizi ni nyingi sana lakini zote zimegawanyika katika makundi makuu matatu:

  a. Nadharia ya kiulimwengu (au ya kiutandawazi): Nadharia hii imegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni ubadilikaji taratibu, msambao na nadharia ya kisosholojia);

  b. Nadharia ya utaifa;

  c. Nadharia hulutishi.

  Katika muktadha wa nadharia hizi, mitazamo mbalimbali iliendelea kumiminika:

  • Wengine waliitaja fasihi kama mwavuli wa mtu, jamii, utu, maisha, hadhi na taadhima;

  • Wengine waliitaja kama kioo na mwonzi wa maisha ya mtu na jamii;

  • Wengine walisema kuwa ni hazina ya kazi za sanaa zinazotumia lugha ili kuwasilisha ujumbe au fikra za fanani;

  • Wengine walipata kutaja sihiri kuwa ni chanzo kimojawapo cha dhana ya fasihi ilhali sihiri ni sehemu ya mila na desturi za jamii nyingi duniani;

  • Wengine wa kimagharibi walisisitizia kwamba fasihi humaanisha maandishi ya wakati, mtazamo ambao unaipuuza fasihi simulizi na kadhalika.

  Watu hawa wote tusiwabishie kwani waliendeleza utafiti kuhusu dhana hii. Isitoshe, ubishi si kiwango chanya cha usomi.

  Tukizingatia mitazamo hii na mingine ambayo haikutajwa, kinachoonekana ni kuwa fasihi:

  a. inagusa ufasaha wa lugha;

  b. chanzo chake kisitafutwe nje ya watu wa jamii husika;

  c. ni kongwe ndani ya kila jamii ya watu na kila jamii ina fasihi yake inayoelezwa kwa lugha yake.

  Maana inayopewa dhana ya fasihi huchukuana na mambo mbalimbali kama vile:

  • matumizi ya dhana yenyewe;

  • watu wanaohusika yaani jamii ya watu;

  • mahali dhana hiyo inamotokea;

  • kipindi au wakati husika.

  Hivyo basi, tukiziangalia fasili zote na kuzifafanua ipaswavyo, tunaweza kusema kuwa fasihi:

  a. ni hazina ya kazi za kubuni za sanaa inayotumia lugha yaani maneno kama njia ya kuwasilisha mambo yake;

  b. inatumia lugha mahususi, yenye mvuto na mguso wa kusisimua. Fasihi hutawaliwa na kaida na masharti ya kisanaa, ni kusema kuwa maneno hupangwa kwa kisanaa);

  c. inaweza kutumia lugha kwa njia ya masimulizi na kuitwa “fasihi simulizi”. Inapotumia lugha kwa njia ya maandishi huitwa “fasihi andishi”. Hizi ndizo nyanja kuu za fasihi;

  d. inaundwa na kazi za sanaa zinazowasilisha ujumbe fulani kwa hadhira inayokusudiwa. Ni kusema kuwa fasihi hulenga hadhira fulani ambayo huiathiri. Ujumbe huo hutokana na hisia za binadamu katika maisha yake ya kila siku;

  e. inahusu maisha ya jamii husika lakini si kwa kutoa picha ya moja kwa moja kama historia.

  Kwa machache, fasihi ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala mbalimbali yanayomhusu binadamu kama vile:

  • matatizo yake;

  • ndoto zake;

  • matumaini yake;

  • migogoro yake na jinsi anavyoingiliana na mazingira yake.

  2. Dhima ya fasihi

  Kila fasihi ina umuhimu wake kwa jamii ya watu husika. Jambo hili linatokana na hali ile ya fasihi kujishughulisha na ubinadamu na mazingira yake ya kila siku. Umuhimu huo unaweza kujitokeza katika taaluma mbalimbali kama vile:

  a. uchumi;

  b. siasa;

  c. dini;

  d. michezo;

  e. tabia na kadhalika.

  Fasihi inaweza:

  • Kuburudisha, kufurahisha na kuchangamsha jamii: Kupitia tanzu mbalimbali kama vile hadithi, mashairi, nyimbo na vitendawili, fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.

  • Kuelimisha jamii: Fasihi hutumika kama nyenzo ya kufundisha wanajamii kuhusu vipengele mbalimbali vya maisha. Hapa tunaweza kutaja:

  - kuishi kwa amani na kuendeleza jamii;

  - kujikomboa kifikra na kiuchumi;

  - ubaya wa ufisadi;

  - kufichua uozo wa jamii;

  - kumkomboa mnyonge kutoka dhuluma na kadhalika.

  • Kuionya jamii na kuipa mwelekeo: Fasihi inasaidia katika kuhakikisha kama wanajamii wana maadili yanayotakiwa na jamii husika. Hivyo, wanajamii wanapewa mwongozo kuhusu jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii. Mwelekeo mzuri ni kama ule unaowahimiza wanajamii kushughulikia:- usawa wa kijinsia;

  - kuepukana na mabaya kama vile mauaji ya kimbari;

  - kutilia mkazo elimu isiyo na ubaguzi na kadhalika.

  • Kuhifadhi historia na utamaduni wa jamii: Wanajamii hufahamishwa kifasihi historia yao, chimbuko lao, jadi zao. Kwa hiyo, wao huweza kujielewa vizuri na kujitambua.

  • Kuunganisha jamii na vizazi: Mila, tamaduni na itikadi husika za vizazi hurithishwa kwa vizazi vingine kwa kupitia kazi za fasihi. Kizazi huweza kujinasibisha na maisha ya kizazi kilichotangulia kunapokuwa na uwiano wa amali, mwelekeo na maadili.

  • Kukuza na kuendeleza kipawa cha lugha: Fasihi hutumia lugha kufikisha ujumbe wake kwa jamii. Lugha hio ni ya kisanaa zaidi na yenye mvuto kwa wasikilizaji au wasomaji wanaohitaji kuwa na utajiri mkubwa huo wa lugha. Mtu anaposikiliza au kusoma kazi ya fasihi anapata ujuzi wa lugha unaotokana na vipengele imara mbalimbali vya fasihi. Kwa hiyo, fasihi inajitokeza kama chombo cha kukuza lugha.

  • Kukuza uwezo wa kufikiri: Kazi nyingi za fasihi kama vile vitendawili, nahau, hadithi,...huichochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. Katika kuweza kufikiri, ndipo inatuimarisha kuwa na ujasiri wa kujiamini na uwezo wa kugundua dharau au kedi inayotuhusu. Kwa mfano, inasemekana kuwa SENGO, mwanafasihi Mtanzania mmoja, aliulizwa na mtu mwenzie mmoja akiwa Ulaya “Je, ni kweli kwamba Afrika kuna manyani weusi wengi?” Alipoligundua lililokuwa linamaanishwa, ndipo alijibu, “Ni kweli, kama walivyo manyani weupe wengi huku Ulaya!” Ujuzi mkubwa anao katika lugha kutokana na fasihi ulimwezesha kujitetea ipaswavyo na kutokosa sifa zake za kimsingi na utu wake.

  3. Fasihi ya Kiswahili

  Kila jamii ya watu ina fasihi yake inayotumia lugha ya jamii hiyo husika. Hivyo, Wanyarwanda wana fasihi yao ya Kinyarwanda; Waswahili wanajishughulisha na fasihi yao ya Kiswahili na kadhalika.

  Fasihi ya Kiswahili inatumia lugha ya Kiswahili ili kuupeleka ujumbe kwa hadhira husika. Ni fasihi iliyokuwepo kabla ya majilio ya wageni huko sehemu za pwani ya Bahari ya Hindi. Mahali hapo panajulikana kama makazi ya Waswahili. Hili linatokana na kuwa ukuwepo wa kila fasihi unakwenda sambamba na ukuwepo au uundaji wa jamii husika ya watu. Walakini, Mswahili si kila mkazi wa pwani hiyo. Waswahili walikuwa na eneo lao, jadi zao, vyakula vyao tofauti na vile vinavyopendelewa na Wakongo. Waswahili pia ndio wenyewe wa lugha ya Kiswahili.

  Fasihi ya Kiswahili inaundwa na nyanja kuu mbili yaani fasihi simulizi ambayo ni ya kale na fasihi andishi ambayo ni changa. Lakini, si kusema kwamba siku hizi hatuwezi kuzipata kazi mpya za fasihi simulizi. Wapo watu mbalimbali wanaoendelea kubuni kazi zao za kifasihi kwa njia ya masimulizi. Ndiyo sababu tunaweza kuipata fasihi simulizi ya kale na fasihi simulizi ya kisasa. Kila uwanja wa fasihi una tanzu zake ambazo zitashughulikiwa katika sura nyingine.

  4. Fasihi kwa Kiswahili

  Kazi za sanaa za fasihi ya Kinyarwanda au ya Kirundi au ya Kiingereza zikiandikwa kwa Kiswahili haziwezi kuitwa kazi za fasihi ya Kiswahili. Hili linatokana na kuwa ili kazi ya fasihi iingizwe katika fasihi ya Kiswahili ni lazima:

  a. izungumzie utamaduni wa Waswahili;

  b. na itungwe katika Kiswahili.

  Wajamaika walioko Uingereza kwa miaka na karne nyingi hawajakubalika kuwa ni Waingereza. Hivi ndivyo zilivyo kazi za kifasihi zilizotafsiriwa katika Kiswahili. Kazi za fasihi ya Kinyarwanda au ya Kiingereza zinahusu utamaduni wa Wanyarwanda au Waingereza ilhali zimetafsiriwa katika Kiswahili. Hizi kazi zote za kifasihi zisizo za Waswahili zinaingia katika “fasihi kwa Kiswahili”.

  Kazi ya 4: Sikiliza jinsi mwalimu au wenzako wanavyokisoma kifungu cha habari hicho.

  Kazi ya 5: Na wewe, soma kwa sauti na ufasaha kifungu cha habari hicho.

  Kazi ya 6: Soma sentensi mbalimbali zifuatazo na kuchagua sehemu ya pili ambayo inaweza kukamilisha ipaswavyo ile ya kwanza kwa kila sentensi:


  Kazi ya 7: Simama mbele ya darasa na kukamilisha sentensi zifuatazo mwanzoni, katikati au mwishoni kama zilivyotumiwa katika habari:

  1. ...............................................miaka na karne nyingi hawajakubalika kuwa ni Waingereza.

  2. Fasihi ya Kiswahili inaundwa na nyanja kuu mbili yaani.................na fasihi andishi ambayo ni changa.

  3. Nadharia husaidia katika kulielezea vema jambo fulani kwa mtazamo imara............................

  Kazi ya 8: Tazama picha ifuatayo. Sema ni utanzu gani wa fasihi simulizi inaouwakilisha: