Topic outline

 • MADA NDOGO: LUGHA YA KISWAHILI

  Uwezo upatikanao katika mada: Kusikiliza, kusoma, kuzungumza na kuandika kwa minajili ya kuelewa lugha na umuhimu wake kama chombo cha mawasiliano katika jamii.

  Malengo:

  Baada ya mada hii, mwanafunzi atakuwa na uwezo wa:

          • Kufasili maana ya lugha.

          • Kueleza umuhimu wa lugha katika jamii.

          • Kueleza historia ya Kiswahili kwa ujumla.

          • Kueleza historia ya Kiswahili nchini Rwanda.

          • Kutunga sentensi zenye viambishi vya masharti.

  Kidokezo

          1. Kiswahili ni nini?

           2. Lugha ni nini?

           3. Taja nchi tano ambapo Kiswahili kinatumiwa.

           4. Asili ya lugha ya Kiswahili ni ipi ?

           5. Jadili kuhusu nafasi ya Kiswahili nchini Rwanda.


  SOMO LA 1: MAANA YA LUGHA

  Zoezi la 1: Tazama mchoro hapo juu kisha jibu maswali yanayofuatia:

  1. Eleza wahusika unaowaona kwenye mchoro huu.

      a. Andika kwa kina

      b. Fafanua zaidi

  2. Wahusika hao wako wapi? Wao wanafanya nini?

  3. Kuna uhusiano wowote kati ya mchoro huo na kichwa cha habari hapo chini?

  1.1 Kusoma na Ufahamu: Maana ya Lugha

  Soma kifungu cha habari kifuatacho kuhusu “Maana ya lugha” kisha jibu maswali yanayofuatia hapa chini.

  Ilikuwa jioni moja ambapo mzee Gakuba, mke wake na watoto wao walipokuwa wakizungumzia mambo kadhaa. Baba aliwasimulia mengi kuhusu maisha yake na safari alizofanya katika mataifa mengi ya Afrika Mashariki. Alisisitiza kwamba aliweza kubahatika sana na kufanikisha shughuli zake nyingi katika mataifa yote aliyoyatembelea. Kule Kenya, Tanzania na hata Uganda aliweza kufanya biashara mbalimbali na kujenga urafiki na wafanyabiashara wengine wengi kutoka mataifa hayo.

  Mara moja, Kagabo ambaye alikuwa kitindamimba akauliza: “Baba! Wewe ulikuwa mtu mzuri sana na uliweza kutembelea nchi nyingi za bara letu la Afrika.... Lakini....wewe na marafiki zako mlikuwa mnatumia lugha gani? Wao wanazungumza lugha yetu ya Kinyarwanda?”. Baba alikaa kimya kidogo akaanza kumjibu mtoto wake. “Unauliza swali zuri mtoto wangu. Mimi nikiwa na marafiki zangu kutoka nchi nyingi za Afrika hutumia lugha ya Kiswahili. Lugha hii ni lugha inayotuunganisha na wananchi wote katika nchi zote za Afrika Mashariki na hata bara zima”. Hapo Kagabo alitikisa kichwa kuonyesha kuridhika na jibu alilopewa na babake.

  Kitambo baada ya jibu hilo, Mutesi akakumbuka zoezi alilopewa na mwalimu kama kazi ya nyumbani. Mara alisimama akaenda kuleta daftari lake haraka na kumwomba baba ampe maoni yake kuhusu swali lake.“Baba umefanya vizuri kutuelezea kuhusu lugha ya Kiswahili. Mwalimu wetu alituambia mengi kuhusu lugha hiyo lakini yeye katuomba kutoa maana ya lugha. Wanafunzi wengi walimweleza kuwa lugha ni kama Kinyarwanda, Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, Kirundi na kadhalika. Hata hivyo, mwalimu wetu alisema kwamba kuna haja ya kujua lugha zaidi kuliko tulivyoeleza. “Je, lugha ni nini?” Mutesi aliuliza kwa hamu kubwa.

  Kwa hakika, Mutesi ambaye alikuwa kifungua mimba wa mzee Gakuba, alikuwa katika kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Mugari, alikuwa na shauku ya kuyasikia maoni ya babake ili aelewe swali aliloulizwa na mwalimu wao. Ilikuwa desturi kwake kuyajibu maswali yote aliyoulizwa darasani. Na mwalimu wake alizoea kumpongeza kwa maoni yake mazuri.

  Mzee Gakuba alilitafakari vizuri swali la mtoto wake kifungua mimba, kisha alianza kunena: “Lugha ni kitu muhimu sana katika maisha yetu. Mtu mmoja akiwa na habari fulani anaipeleka habari hiyo kwa watu wengine kwa kutumia maneno, yaani lugha. Huko kupeleka habari toka mtu mmoja hadi kwa watu wengine ndiko kunakofanya kuwepo na kuwasiliana. Kwa hivyo, lugha ni chombo cha kuwasiliana kati ya watu na mawasiliano hayo ndiyo yanayoonyesha umuhimu na lengo kubwa la lugha. Kwa mfano, unaona jinsi tunavyozungumza na kuelewana. Tunatumia lugha. Mnaniuliza maswali na mimi ninawajibu kwa kutumia lugha. Kwa kweli bila lugha tusingeweza kuzungumza na kuelewana”.

  Mutesi alifurahia sana jibu la baba yake na kusema kuwa angekuwa na mengi ya kusema darasani kuhusiana na mada waliyopewa na mwalimu wao.

  Lakini, kaka yake Simoni ambaye alikaa hapo mbele ya baba yao alinyosha mkono kuonyesha kuwa alikuwa na hoja nyingine. Baba alimuuliza ikiwa hakuridhika na maelezo yake kuhusu lugha. Bila kukawia, Simoni aliuliza: “Je, baba, wakati mwingine watu wanatumia lugha lakini wakawa hawaelewani. Hali hii inatokana na nini?” Baba alimpongeza mtoto wake kwa kiwango chake kizuri cha kutaka kujua mengi zaidi ya yaliyosemwa. Hapo baba aliendelea kwa kusema: “Lugha ni chombo kinachotumiwa kuwasiliana na kuelewana. Lakini, ili lengo hilo lifikiwe kuna mambo mengine muhimu ya kuzingatia. Lazima watu wanaowasiliana wawe wanaelewa lugha hiyo wanayoitumia. Nyote mnakumbuka Wimbo wa Taifa letu?” Watoto wote walitikisa kichwa kuonyesha kukumbuka wimbo huo. Baba alizidi kusema: “Wimbo huo hutueleza jinsi ambavyo lugha ya Kinyarwanda hutuunganisha sote kama Wanyarwanda. Kwa hivyo, tunaweza kusikilizana na kuelewana bila tatizo tunapotumia lugha ya Kinyarwanda.

  Baba alitulia kidogo kuwapa muda wa kuyatafakari maneno hayo matamu aliyoyatamka kwa watoto wake. Alishangaa kuona jinsi watoto wake walivyomfuata kwa makini na kufurahia hamu ya kujua mengi iliyowatambulisha wote na kujivunia malezi waliyoyapewa. Watoto wote walimshukuru baba yao kwa jinsi alivyowaelimisha na kumwambia kwamba walikuwa wameyazingatia mengi kuhusu maana ya lugha. Baada ya hapo, mama alileta chakula mezani, wote wakajiunga pamoja na kuanza kufurahia chakula chao cha jioni. Mama ambaye alikuwa anayafuata yote yakitendeka naye alisema, “Tungekuwa na muda wa kutosha tungezungumzia mengine mengi kuhusu lugha. Maana ya lugha ni pana sana na hugusia kila sehemu ya maisha ya binadamu.” Baada ya chakula chao, watoto wote ambao ni Mutesi, Simoni, Kagabo na Simbi walielekea kila mmoja katika chumba chake na wakaagana wakisema kwamba wangeamka mapema asubuhi ili wajiandae tayari kwenda shuleni.

  Maswali ya ufahamu

  1. Taja majina ya watu wote wanaotajwa katika kifungu hiki.

  2. Mzee Gakuba aliweza kutembelea mataifa gani?

  3. Ni faida zipi alizozipata katika safari zake?

  4. Mutesi alikuwa anajifunza katika shule gani?

  5. Mzee Gakuba alitumia lugha gani ili aweze kuwasiliana na marafiki zake?

  6. Kwa nini baba alimpongeza Simoni?

  7. Ni wakati gani watu wanaweza kukosa kuelewana?

  8. Mama ana maoni gani kuhusu maana ya lugha?

  9. Eleza maana ya lugha kwa kutumia maneno yako.

  10. Fupisha kifungu cha habari hapo juu kwa kutumia sentensi kumi tu.

  1.2 Msamiati Kuhusu Maana ya Lugha

  Zoezi la 2: Tunga sentensi kwa kutumia maneno yafuatayo ukizingatia namna yalivyotumika katika katika kifungu cha habari mlichosoma.

  1. Maana

  2. Kuwasiliana

  3. Kitindamimba

  4. Shauku

  5. Desturi

  6. Kupongeza

  7. Kutikisa

  8. Kuelewana

  9. Lugha

  10. Kuridhika

  Zoezi la 3: Tumia mshale kwa kuoanisha maneno yaliyopo sehemu A dhidi ya yale yaliyopo katika sehemu B

  Maelezo Muhimu

  Kiambishi [-nge-]

  Huonyesha kuwa tendo fulani halijafanyika na kwa hiyo, jambo jingine halijatokea lakini kuna uwezekano wa kufanyika tendo hilo na kisha jambo hilo litokee.

          • Katika hali ya kuonyesha uwezekano

         Mifano:

  1. Ningekuwa na pesa, ningenunua gari.Maana yake ni kuwa mimi sina pesa wala sikununua gari, lakini nikipata pesa sasa hivi ninaweza kununua gari.

  2. Ningemjua mwizi yule, ningemshauri kuacha tabia mbaya. Mana yake ni kwamba simjui mwizi yule, lakini kumjua kwangu kunaweza kusababisha kumpa ushauri wa kuacha tabia yake mbaya ya kuiba.

          • Katika hali ya kuonyesha majuto

  Mifano:

  1. Ningekuwa msichana yule aliyepata mimba, ningejilinda kujiunga na vijana wenye tabia mbaya za uasherati.

  Maana yake ni kuwa mimi si msichana yule aliyepata mimba. Lakini nikijiweka katika nafsi yake siwezi kujiunga na vijana wenye tabia ya uasherati.

  2. Ningekuwa kijana yule, ningeacha kuvuta sigara au kuchukua dawa za kulevya.

  Maana yake ni kuwa mimi si kijana yule anayevuta sigara na kuchukua dawa za kulevya; lakini nikijiweka katika nafsi yake siwezi kufanya kama anavyotenda.

  1.3 Sarufi: Matumizi ya Kiambishi chenye Dhana ya Masharti–nge-

  Zoezi la 4: Jadili kuhusu maana ya sentensi zifuatazo zenye kiambishi nge; halafu utunge sentensi tano zenye kiambishi hicho.

  1. Tungekuwa na muda wa kutosha tungezungumzia mengine mengi kuhusu lugha.

  2. Watoto wale wangejifunza vizuri wangepewa zawadi nyingi.

  Zoezi la 5: Zikamilishe sentensi zifuatazo ili zilete maana kamili. Kwa mfano:Tungepanda miti kwenye milima, tungepata hewa safi.

  1. Wangejua nia yangu katika kutetea haki za wanawake, ......................................

  2. Ungeonana na daktari, .....................................................................................................

  3. Vijana wangeyapiga marufuku mawigi, bila shaka ya...........................................

  4. Barabara zote zingekuwa za lami, kila eneo nchini Rwanda ...............................

  5. Wanafunzi wangeelewa somo vizuri,.............................................................................

  6. Wazazi wangezingatia ushauri kutoka kwa walimu wa watoto wao, ..............

  7. Wangejua kuwa lugha ni chombo cha mawasiliano, ...........................................

  8. ....................................., wangekiteua Kiswahili kuwa lugha rasmi nchini mwao.

  9. Wangechezea kiwanjani kwao, .........................................................

  10. ...................................., wangemjulisha habari za harusi ya dada Rehema.

  Zoezi la 6: Tunga sentensi tano kwa kutumia kiambishi -nge- cha masharti, kisha ueleze maana za sentensi hizo.

  1.4 Matumizi ya lugha: Maana za Maneno katika Miktadha Tofauti

  Zoezi la 7: Panga maneno yafuatayo kwa utaratibu unaofaa ili yaweze kuleta maana katika sentensi.

  1. kitabu watoto lugha nyumbani yetu alitununulia Kiswahili baba wote cha ambacho kimefurahisha

  2. anaishi ujumbe kwa hakuweza alipokea Kenya shangazi yangu ambaye baba kutoka lakini kumjibu

  Zoezi la 8: Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo: alipuliza, Rais, anacheza, rubani, ukaanza, nahodha, anafinyanga, anazungumza, anabweka, ananguruma, alitaga.

  1. Refa ---------- filimbi mchezo..........................

  2. Mwanamziki huyu -------------- ngoma vizuri sana.

  3. Mtoto wangu ------------- vizuri lugha ya Kiswahili.

  4. Mbwa -------------- nje ya nyumba yangu.

  5. Kuku wetu -----------------mayai mengi sana.

  6. Simba ---------------- huku msituni.

  7. Baba yake ----------- vyungu vizuri sana

  8. ------------- huyu ni bingwa wa kuendesha meli.

  9. ------------ wetu anaongoza nchi vizuri sana.

  10. ------------- yule anaendesha ndege za Rwandair.

  Maelezo muhimu kuhusu “Maana ya lugha”

  1. Lugha ni chombo muhimu katika mawasiliano ya watu.

  2. Lengo kuu la lugha yoyote ni kuwezesha watu kutoa fikra zao, kuelezeana mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao. Yaani lugha ni chombo kinachowezesha watu wa jamii fulani kufanikisha mawasiliano kati yao.

  3. Ili kuwepo na mawasiliano baina ya watu, ni lazima wawe wanaelewa lugha wanayoitumia.

  4. Ujuzi wetu wa lugha hutegemea kwa kiwango kikubwa jinsi tunavyoweza kuwasikiliza watu wengine wanaoizungumza lugha hiyo na jinsi tunavyoitumia katika shughuli zetu za kila siku.

  5. Lugha kwa upande wake inajengwa na sauti tunazozitoa na maneno tunayoyatumia.

  6. Ni lazima sauti zipangwe vizuri ili ziweze kuleta maana za maneno hayo.

  7. Ni lazima maneno yapangwe vizuri katika sentensi kwa ajili ya kuleta maana. Hali hii ya lugha ndiyo ambayo husaidia watu kuzungumza, kupashana habari, kutatua matatizo yao, kujadiliana, kuonyesha hisia zao; yaani kuwasiliana ili waweze kutosheleza mahitaji yao.

  1.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 9: Mkiwa watu wawili au zaidi, jadilini kuhusu “Nafasi ya lugha kati-ka mawasiliano”. Kila mmoja aandike hoja zilizotolewa na mwenzake na zile alizozitoa. Baada ya hapo, eleza kwa nini unakubaliana na hoja za mwenzako au kwa nini haukubaliani nazo

  1.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 10: Kwa kuzingatia matumizi ya kiambishi “nge”, tunga kifungu cha habari kuhusu mada ifuatayo: “Lugha ni chombo cha mawasiliano”.

  SOMO LA 2: UMUHIMU WA LUGHA


  Zoezi la 1:Eleza yale unayoyaona kwenye mchoro huu.

  2.1 Kusoma na Ufahamu: Umuhimu wa Lugha

  Soma kifungu kifuatacho kuhusu “Umuhimu wa lugha” kisha, jibu maswali uliyopewa hapo chini.

  Familia ya mzee Yakobo inaishi katika kijiji cha Nyamugari. Kila mara Mzee Yakobo huwahimiza watoto wake Maria na Petero kujifunza lugha mbalimbali kwa madhumuni ya maisha yao ya usoni. Tangu Maria alipoyasikia maneno ya baba yake aliyazingatia sana mawaidha aliyopewa na kujifunza vizuri lugha zote zilizopatikana kwenye ratiba yake ya masomo. Kwa sasa, yeye ni mkuu wa kitengo cha utalii katika taasisi inayoshughulikia masuala ya utalii na mazingira. Petero ni tofauti na ndugu yake Petero aliyeonyesha mtazamo hasi kuhusu ujifunzaji wa lugha. Yeye alipenda kusema: « Siwezi kupoteza muda wangu kujifunza lugha za watu wengine, lugha ninayozungumza inanitosha». Kwa kweli, alikuwa mtoto mtukutu asiyejali maonyo na mawaidha ya wazazi wake.

  Kwake, kujisomea hata sentensi fupi za Kiswahili lilikuwa jambo la ajabu! Alikuwa amesitisha masomo yake alipomaliza darasa la pili katika shule ya Sekondari ya Nyamugari ingawa baba yake hakuacha kumuonya kuhusu umuhimu wa elimu na nafasi ya lugha katika maisha ya binadamu.

  Siku moja Mzee Yakobo aliamua kwenda kumtembelea binti yake aliyeishi katika nchi jirani. Petero alimsihi waende pamoja kuwasalimia binamu zake ambao ni Kamugisha na Kana. Mzee Yakobo aliposikia maneno ya mtoto wake, hakusita kukubali wazo lake. Alifikiria kwamba mtoto wake angekutana na binamu zake wangemuuliza mengi kuhusiana na masomo yake. Kwa hivyo, Mzee Yakobo alimwomba mtoto wake Petero ajiandae kwa safari.

  Gari lao lilitoka Nyabugogo saa kumi na moja alfajiri. Walipofika njiani, Petero alishindwa kuvumilia njaa iliyokuwa ikimuuma kutokana na safari ndefu. Kwa bahati nzuri, walipofika katika mji mmoja, dereva aliamua kusimamisha gari ili wasafiri waweze kwenda haja na wengine waweze kujinunulia chakula na kinywaji kabla hawajaendelea na safari yao. Baba yake Yakobo alimwonea huruma mtoto wake na kumpa shilingi mia mbili ili aweze kwenda kujinunulia chakula. Petero alifurahi sana. Alikuwa na hamu ya kula mkate na kunywa juisi ya matunda iliyotengenezewa katika nchi jirani. Alienda haraka na kuingia dukani. Humu dukani alimkuta Bi Hassani aliyemkaribisha na kumuuliza alichotaka kununua dukani humo.

  Lo ! Petero alikosa neno. Alisimama akimkodolea macho kama aliyejiingiza baharini bila kujua kuogelea. Kweli alishindwa kuulizia kile kilichomleta pale. Alijitahidi kutumia ishara kumwonyesha sehemu palipowekwa mikate na vyakula vingine lakini mfanyabiashara hakuelewa alichokuwa anahitaji miongoni mwa vyakula vilivyokuwemo dukani. Petero aliposhindwa kusema alichukua shilingi zote alizokuwa nazo na kumkabidhi Bi Hassani. Hapo ndipo alipewa mkate na maji. Petero alipokea kwa shingo upande alichopewa na mwenye duka na kurudi haraka na kuziacha shilingi mia moja zilizobaki kwenye jumla ya bei ya mkate na maji. Kama angekwenda shuleni asingefanyiwa hayo.

  Mara moja, dereva alianza kugeuza gari ili waendelee na safari. Petero alikuwa ameketi kwenye kiti chake karibu na baba yake. “Salaalaa!” Yakobo alishikwa na bumbuazi alipoona mtoto wake ameleta chakula kilichokuwa kimepitisha tarehe ya kukila mwaka uliopita. “Wewe hujui kusoma wala kuhesabu! Tazama tarehe iliyoandikwa hapa! Huoni kuwa chakula hiki kingepaswa kuliwa kabla ya mwezi uliopita?” Kwa kweli, alianza kujiuliza mengi kuhusu maisha ya mtoto wake. Alisikitika sana na kumwomba asithubutu kula chakula hicho kwani kingeweza kuharibu afya yake. Petero alikunywa maji tu aliyoleta na kuvumilia njaa iliyokuwa ikimbana wakati huo. Alianza kujuta kwa kutofuata mawaidha aliyopewa na wazazi wake. Alifikiri, “Nisingepuuza mawaidha ya baba yangu, nisingekutana na matatizo haya”.

  Walipofika Dar-es-salaam, walifurahi kuonana na shangazi na binamu zake. Walipokelewa vizuri na kupata muda wa kutembelea mazingira mazuri ya jiji hilo. Tangu alipofika, Petero alifuatana na binamu zake kila wakati walipotoka kununua vitu ili asikilize walivyoweza kuwasiliana na watu wengine katika lugha ya Kiswahili. Hapo aliweza kuelewa umuhimu wa kujifunza lugha na aliamua kwamba angeanza kujifunza kwa bidii mara wakirudi nyumbani. Kwa sasa Petero amemaliza kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya Museta ambapo walimu wake wanampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha ya Kiswahili na lugha nyingine anazojifunza.

  Maswali ya Ufahamu

  1. Taja majina ya watu wanaozungumziwa katika kifungu hiki.

  2. Ni mawaidha gani mzee Yakobo aliyokuwa anawapa watoto wake ?

  3. Maria amefaidika vipi kutokana na ujuzi wake wa lugha mbalimbali ?

  4. Safari ya mzee Yakobo ilikuwa na lengo gani ?

  5. Ni hasara gani aliyoipata Petero aliposhindwa kuwasiliana na mfanyabiashara ?

  6. Eleza tabia za mfanyabiashara Bi Hassani mbele ya mteja wake?

  7. Ni jambo lipi lingetokea ikiwa mzee Yakobo hakumkataza mtoto wake Petero kula chakula alichokinunua ?

  8. Petero alikuwa na majuto gani? Kwa nini alijuta?

  9. Aliporudi nyumbani alifanya nini?

  10. Unajifunza nini kutokana na kifungu hiki cha habari?

  2.2 Msamiati Kuhusu Umuhimu wa Lugha

  Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo huku ukizingatia matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu.

  1. Kuhimiza

  2. Madhumuni

  3. Mawaidha

  4. Mtazamo

  5. Mtukutu

  6. Utalii

  7. Kwenda haja

  8. Kwa shingo upande

  9. Bidii

  10. Bumbuazi

  Zoezi la 3: Oanisha maneno katika sehemu A na maana zake zilizopo katika sehemu B.


  Zoezi la 4: Jaza nafasi kwa kutumia maneno mwafaka yafuatayo:bidii, madhumuni, kupuuza, maarufu, mawaidha, mtazamo, bumbuazi, ratiba, kwenda haja, shingo upande

  1. Nilianzisha mradi huu kwa ...................................ya kuhifadhi mazingira yetu.

  2. Kila mwanafunzi analazimishwa kuwa na .........................ya masomo ya kila siku.

  3. Usipofanya............................. basi hutafaulu mitihani yako.

  4. Aliposikia habari hiyo alishikwa na ............................... na kukosa la kufanya.

  5. Anaanza kujuta kwa kutofuata ....................................ya baba yake.

  6. Baada ya kufanya safari ndefu, wasafiri wamesimamisha dereva ili waweze ....................

  7. Sikubaliani na ...............................wako kuhusu uhifadhi mwafaka wa mazingira.

  8. Alipokea zawadi hiyo kwa.................................................

  9. Amekuwa mchezaji.....................................kutokana na ustadi wake wa kusakata mpira.

  10. Si vizuri ...............................fikra za mwenzako kabla hujamsikiliza.

  2.3 Sarufi: Matumizi ya Viambishi vyenye Dhana ya Masharti: -nge- kati-ka Tungo Kanushi

  Zoezi la 5:

  1. Tafuta sentensi zenye dhana ya masharti -nge- katika kifungu cha habari ulichosoma kuhusu “Umuhimu wa kujua lugha”, kisha ueleze maana za sentensi hizo.

  2. Tunga sentensi zako tano kwa kutumia kiambishi cha masharti “nge” katika hali kanushi.

  Maelezo muhimu

     • Tunapotunga sentensi zenye masharti huwa tunatumia kiambishi cha masharti “nge” katika sehemu zote mbili za sentensi.

      • Sentensi zenye masharti hukanushwa kwa kutumia kikanushi “si”

  Kwa mfano: Kama Petero asingekataa kujifunza kwa bidii, angezungumza na mfanyabiashara yule bila wasiwasi

  Zoezi la 6: Ziandike tungo zifuatazo katika hali kanushi.


  Zoezi la 7: Kamilisha sentensi zifuatazo ili zilete maana kamili.

  1. Wanafunzi wasingemuuliza mwalimu wao, ..............................................................

  2. Nisingepuuza mawaidha ya baba yangu, ..................................................................

  3. Tusingechelewa shuleni,..................................................................................................

  4. Mutoni asingetumia pesa zake vibaya,. ......................................................................

  5. Tusingetoroka shule,..........................................................................................................

  6. Binti yule asingeomba msaada, .....................................................................................

  7. Asingenunua gari hilo, .......................................................................................................

  8. Msingedharau ushauri wake, ...........................................................................................

  9. Mfanyabiashara huyu asingenijulisha shida zake,....................................................

  10. Tusingekuja, ...........................................................................................................................

  Zoezi la 8: Kanusha sentensi zifuatazo:

  1. Wangekuja, wangetukuta hapa.

  2. Msingekuwa hodari, pesa zenu zingemalizika.

  3. Mahali hapa pangeoshwa, pangependeza.

  4. Mngetusalimia, tungewajibu.

  5. Wangesoma wangejua.

  6. Tungepata tatizo, tungerudi kwetu kijijini.

  7. Mngeomba, mngepewa.

  8. Wasafiri wangekuja mapema, wangewahi basi kabla ya kuondoka.

  9. Wazee wangekuweko, mambo yangesawazishwa.

  10. Wangekuwa na ukakamavu, wangemshika mwizi.

  Zoezi la 9: Andika sentensi zifuatazo katika hali yakinishi:

  1. Gari hili lisingeoshwa, lisingependeza.

  2. Mtoto asingeanguka, asingevunjika.

  3. Msingepumzika, msingeshinda.

  4. Msingekuwa wajumbe, msingesaidia shule yetu.

  5. Msingekuwa na pesa msingefanya kitendo hicho.

  6. Msingekuja, msingetuona.

  7. Msingekuwa hodari, pesa zenu zingemalizika.

  8. Wazee wasingekuwepo, mambo yasingenyooshwa.

  9. Wasafari wasingekuja mapema, wasingewahi kuondoka kwa muda uliopangwa.

  10. Wasingekuwa makini siku ile, wasingemshika mwizi.

  2.4 Matumizi ya Lugha: Umuhimu wa Lugha

  Zoezi la 10: Soma maelezo yafuatayo, kisha ujibu maswali hapo chini.

  Maelezo muhimu: Umuhimu wa lugha

  Lugha ni mojawapo ya vipengele vya utamaduni wa jamii na tena ni chombo cha utamaduni. Hili ni kwa sababu chombo hiki hutumiwa kuwasilisha amali, mila na desturi zote za jamii. Lugha ndio uti wa mgongo wa utamaduni.

  Lengo kuu la lugha katika jamii ni pamoja na kuwafanya watu wawasiliane kwa kupashana habari. Kujua lugha fulani kunamwezesha mtu kujipatia marafiki, kukuza ujuzi kwa kusoma maandishi mbalimbali au kwa kufuata vipindi mbalimbali kwenye redio, runinga na tovuti.

  Kutumia lugha moja katika jamii kunaweza kuwa na faida pamoja na hasara mbalimbali kutokana na mazingira ya jamii. Rwanda kama nchi inayozungukwa na nchi zinazotumia Kiswahili, itanufaika kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Vilevile lugha ya Kiswahili ina umuhimu mkubwa sana katika Jumuia ya Afrika Mashariki kwa kuwa lugha hii ndiyo lugha rasmi inayotumiwa katika Jumuia hii.

  Maswali

  1. “Lugha ndio uti wa mgongo wa utamaduni.” Eleza

  2. Lipi ni lengo kuu la kuijua lugha?

  3. Jadili: “Kutumia lugha moja katika jamii kunaweza kuwa na faida pamoja na hasara mbalimbali”.

  2.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 11: Jadili kuhusu mambo yafuatayo:

  1. Matatizo yawezayo kujitokeza baina ya watu wawili wanaposhindwa kusikilizana kimawasiliano

  2. Umuhimu wa lugha katika jamii

  3. Mambo mbalimbali yanayoweza kukwamisha mawasiliano yenye kutumia lugha

  2.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 12: Kwa kutoa hoja zenye mifano, tunga kifungu chako kwa kutumia mada ifuatayo: “Lugha inapotumiwa vizuri hujenga jamii na ikitumiwa vibaya huangamiza jamii”.

  SOMO LA 3 : LUGHA KATIKA JAMII


  Zoezi la 1:Tazama mchoro hapo juu kisha utoe maoni yako kuhusu shughuli inayoendelea.

  3.1 Kusoma na Ufahamu: Lugha katika Jamii

  Soma kifungu cha habari kinachofuata kuhusu “Lugha katika jamii”, halafu jibu maswali uliyopewa hapo chini.

  Baadhi ya watu hawatambui nafasi ya lugha katika jamii. Wao huiona lugha kama kitu cha kawaida na hawachukui muda wao ili waweze kufikiria kwamba shughuli zote wanazozifanya huhitaji matumizi ya lugha. Kwa mfano, ni watu wachache wanaoweza kuelewa kwamba bila lugha watu hawawezi kuelewana na kutimiza wajibu wao katika jamii zao: shughuli za usafirishaji wa watu na vitu, ununuzi na uuzaji, ujenzi wa taifa, uongozi na utawala, huduma mbalimbali na shughuli nyingine nyingi zote haziwezi kufanikiwa bila kutumia lugha. Hivyo basi, nafasi ya lugha katika jamii ni pana kwani lugha huchukuliwa kama sehemu moja ya maisha ya watu wenye kutumia lugha hiyo.

  Lugha kama chombo cha mawasiliano huchukuliwa kama uti wa mgongo wa utamaduni wa watu wanaoitumia lugha hiyo. Thamani yake huweza kukadiriwa kupitia shughuli nyingi za maisha ya wanajamii wote na taratibu zinazowaongoza katika jamii yao: imani yao, sherehe wanazofanya, mila zao na desturi zote huelezewa katika lugha yao. Kwa sasa, ni jambo linaloeleweka kwamba mtu anayejua kuongea vizuri, anayetumia lugha sahihi na yenye kuvuta wengi ndiye anayepewa heshima na majukumu mengi katika jamii yake. Mathalani kuposa na shughuli zote zinazoambatana na kupeleka maombi ya kutaka kuoa binti anayetarajiwa kuolewa, kulipa mahari na sherehe za harusi zinazofuata, huhitaji mtu hodari wa matumizi ya lugha.

  Kila jamii huwa na lugha ambayo ndiyo huitambulisha jamii husika. Waswahili hutumia Kiswahili, Wanyarwanda hutumia Kinyarwanda, Warundi hutumia Kirundi, Waganda hutumia Luganda, na kadhalika. Kwa hiyo, ni rahisi kuelewa jinsi ambavyo lugha na jamii huingiliana. Hakuna jamii isiyo na lugha na hakuna lugha isiyo na jamii inayoitumia. Jambo hili ndilo linazifanya jamii nyingi ziweke mikakati ya kulinda na kuhifadhi lugha zao ili zisitoweke au zisichafuliwe na lugha nyingine zinazotumiwa katika jamii hiyo. Katika hali hii, lugha hufahamika kama sehemu ya utamaduni wa jamii ambapo kaida na maadili ya wanajamii yote hupatikana katika lugha ya jamii hiyo. Lugha hutuwezesha kuelewa historia ya watu, mila, desturi na teknolojia zilizopo katika jamii; yaani chombo kinachosaidia wanajamii kueneza na kutunza tabia zao njema na hata kukemea na kukomesha vitendo vibovu kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, ubakaji, ubaguzi, ulevi, uvivu, uzembe, uzururaji, umalaya, na kadhalika.

  Kweli, lugha hutumiwa na jamii na huisaidia kuimarisha na kutunza mengi yanayopatikana katika jamii hiyo. Kuhamasisha usawa wa kijinsia, maendeleo ya jamii, kulinda rasilimali na mazingira yake, kujenga tabia ya ushirikiano, mshikamano, uzalendo, upendo na moyo wa kuvumiliana baina ya wanajamii na mengine mengi hudhihirisha thamani ya lugha katika jamii.

  Maswali ya ufahamu

  1. Kwa nini watu hawatambui thamani ya lugha katika jamii?

  2. Ni shughuli zipi ambazo huhitaji matumizi ya lugha katika jamii?

  3. Jamii hufanya nini kwa kulinda na kuhifadhi lugha yake?

  4. Ni faida gani anazozipata mtu anayejua kuongea vizuri na kutumia lugha ya kuvutia katika jamii?

  5. Taja lugha nyingine zinazotumiwa na nchi zinazopakana na nchi ya Rwanda.

  6. Taja tabia mbaya zinazoweza kujitokeza katika jamii.

  7. Namna gani tabia mbaya hizo zinaweza kukomeshwa?

  8. Kungetokea nini ikiwa wanajamii wasingeelewana kimawasiliano?

  9. Ni uhusiano gani ulioko kati ya lugha na utamaduni katika jamii?

  10. Pendekeza kichwa kingine cha kifungu hiki?

  3.2 Msamiati Kuhusu Lugha katika Jamii

  Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo ukizingatia matumizi yake katika kifungu cha habari hapo juu.

  1. Wajibu

  2. Huduma

  3. Pana

  4. Uti wa mgongo

  5. Kukadiriwa

  6. Mila

  7. Imani

  8. Mathalani

  9. Kuposa

  10. Mahari

  Zoezi la 3: Oanisha maneno katika sehemu A na maana zilizopo katika sehemu B.


  Zoezi la 4: Jaza nafasi wazi kwa kutumia maneno yafuatayo kutoka kifungu cha habari: uzalendo, unadhihirisha, umalaya, usawa wa jinsia, uvivu,uvuvi, usafirishaji, kuhifadhi, maadili, mikakati.

  1. Ndege hurahisisha...............wa watu na bidhaa.

  2. Kila mwanafunzi anatazamiwa kufika kwenye kikomo cha masomo yake akiwa na .....................

  3. Utamaduni wa Kinyarwanda unapiga vita tendo la ............................................

  4. Rwanda imepiga hatua kuhusiana na.....................kati ya mume na mke.

  5. .................................. ilichukuliwa na serikali yetu kuhusu haki za kibinadamu.

  6. Kangabo ni ............................................ kwa sababu kazi yake ni kuvua samaki.

  7. Mashujaa wa taifa letu walikuwa na ................................. katika matendo yao.

  8. ........................................ ni sawa na uzembe.

  9. Usafi wa miji ya Rwanda ..................... kwamba Wanyarwanda hupenda usafi.

  10. Kwa kuweza ............................... mahindi kwa muda mrefu wilaya yetu ilijenga bohari kubwa.

  3.3 Matumizi ya Lugha: Lugha na Jamii

  Zoezi la 5: Kamilisha maneno yafuatayo kwa kutumia herufi zinazokosekana ili yaweze kuleta maana

  Mfano: 

   

  Zoezi la 6: Soma maelezo yafuatayo, kisha ujibu swali linalofuata hapo chini:

  Maelezo muhimu:
  • Lugha ni chombo muhimu katika mawasiliano kati ya wanadamu. Lugha hii ni kama ufunguo wa mawasiliano kati yao. Kwa kutumia lugha binadamu huwasilisha maoni yake, fikra zake, hisia zake, matata na nia zake kwa binadamu wengine.
  •   Lugha kama chombo muhimu katika jamii hufanikisha na kurahisisha mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake.
  •  Kila jamii hutambulishwa na lugha fulani na ndiyo inayosaidia kuitofautisha na jamii nyingine. Kusingekuwepo lugha katika jamii, kusingekuwepo mawasiliano na utamaduni wa jamii husika usingeelezewa na kuhifadhiwa.

  Swali:  1. Lugha ina umuhimu gani katika jamii?

  3.4 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 7: Kwa kuzingatia taratibu zote za majadiliano, jadili kuhusu mada ifuatayo: “Uhusiano kati ya lugha na jamii”.

  3.5 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 8: Kwa kutumia viambishi vya masharti tunga kifungu cha habari kuhusu mada ifuatayo (Tumia mistari isiyopungua kumi na mitano): “Nafasi ya lugha katika shughuli za binadamu”

  SOMO LA 4: FAIDA NA HASARA ZA KUTUMIA LUGHA MOJA

                                 

  Zoezi la 1: Toa maoni yako kuhusu nafasi ya lugha katika maisha ya wanajamii ukizingatia mchoro wa hapo juu.

  4.1 Kusoma na Ufahamu : Faida na Hasara za Kutumia Lugha Moja

  Soma kifungu cha habari kuhusu «Faida na hasara za kutumia lugha moja», kisha jibu maswali yaliyopendekezwa hapo chini

  Jamii huelezewa kama kundi la watu wanaoishi katika eneo moja. Watu hawa huwakilishwa na utamaduni mmoja na mara nyingi huwa na lugha moja inayowatambulisha kama kundi moja la watu. Katika jamii inayotumia lugha moja, watu hupata manufaa na faida za aina mbalimbali lakini watu wengi hukubaliana kuwa umoja, ushikamano, amani na ushirikiano ni mambo muhimu yanayodumishwa na matumizi ya lugha moja. Lugha hii huzungumzwa na hutumiwa katika jamii nzima.

  Faida nyingi za kutumia lugha moja kwa wanajamii huelekezwa pia kwenye shughuli za kuimarisha uchumi wa jamii yenyewe. Itokeapo kwamba mfanyabiashara atakuwa na uwezo wa kuwasiliana na kila mteja anayekuja kununua kwake, ni rahisi kuongeza pato lake kwa upande mmoja lakini pia na mteja huyu huweza kutafuta kile anachohitaji katika maeneo tofauti katika jamii yake bila kukutana na kikwazo cha mawasiliano. Yeye huweza kuulizia chochote anachotaka na huwa na nafasi kubwa ya kujichagulia na kutafutia kokote anakoenda bila wasiwasi. Mawasiliano yanapokosekana kati ya pande mbili basi huishia kuwa na upungufu katika mawasiliano. Hivyo huweza kuleta madhara kwenye uwanja wa uchumi kwa sababu wananchi wa jamii hizi husika hawatashirikiana kiuchumi.

  Lugha moja huweza kuwa kiungo kati ya wanajamii na viongozi wao. Katika hali kama hii, serikali huweza kutoa matangazo na maagizo mbalimbali katika lugha hiyo ambayo inaeleweka kwa wote na kuwa na uhakika kwamba yatazingatiwa. Jambo hili ndilo huzifanya serikali nyingi ziichague lugha moja ya taifa ambayo ndiyo huwaunganisha watawala na watawaliwa ili kuondoa vikwazo vyote vinavyoweza kujitokeza katika mawasiliano kati yao. Nchini Rwanda, Kinyarwanda huwaunganisha Wanyarwanda wote kama wanajamii na hutumiwa pia kuwaunganisha na viongozi wao.

  Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, lugha ya Kiswahili imeteuliwa ili kuunganisha wannachi wa nchi zote zinazounda jumuiya hiyo. Jambo hili linasaidia kuimarisha uchumi wa nchi zote za Jumuiya hiyo na kudumisha mshikamano kati ya raia wote wa nchi hizo. Kwenye uwanja wa siasa, utumiaji wa lugha moja utasaidia sana kwa kupitisha sera za serikali na kuzisambaza kwa raia wote kwa njia rahisi. Pamoja na hili, viongozi wanashirikiana na wananchi wao na hivyo wananchi hawa wanatoa mchango wao katika uongozi wa nchi au jamii yao.

  Lugha kama chombo cha mawasilino humwezesha mtu kuwasilisha mawazo na mitazamo yake kwa wanajamii wengine. Katika njia hii, binadamu hufaidika zaidi akipanua uwezo wake wa kutumia lugha ili aweze kuwasiliana na watu wengi iwezekanavyo. Mtu anayetumia lugha moja hujifungia mahali pamoja na kujiwekea mipaka ya kuwasiliana na ulimwengu mzima. Kwa mfano, katika uwanja wa elimu, mtu huyu hawezi kujisomea vitabu vingi vyenye elimu na tekinolojia zilizoandikwa katika lugha nyingine tofauti na lugha anayoizungumza. Zaidi ya hayo, mtu huyo hujinyima uwezo wake wa kujiunga na vyuo vingine vingi vilivyopo ulimwenguni ili kujiongezea elimu na maarifa mbalimbali.

  Maswali ya ufahamu

  1. Jamii ni nini?

  2. Toa faida za kiuchumi tunazopata kutokana na matumizi ya lugha moja miongoni mwa wanajamii.

  3. Kuna faida zozote za kisiasa zinazotokana na kutumia lugha moja? Eleza jibu lako.

  4. Ni madhara gani yanayoweza kujitokeza kwenye uwanja wa kiuchumi katika jamii inayotumia lugha moja?

  5. Kwa nini lugha huchukuliwa kama chombo cha mawasiliano katika jamii?

  6. Taja faida za kutumia lugha nyingi.

  7. Ni hasara zipi zinazoweza kujitokeza katika jamii kutokana na kutumia lugha moja?

  8. Bainisha mikakati iliyochukuliwa na Serikali ya Rwanda kuhusu utumiaji wa lugha nchini?

  9. Je, utumiaji wa lugha nyingi unaweza kuathiri utamaduni wa jamii? Eleza jibu lako.

  4.2 Msamiati Kuhusu Faida na Hasara za Kutumia Lugha Moja

  Zoezi la 2: Jaribu kutoa maana za maneno yafuatayo, kisha uyatumie katika sentensi zako.

  1. Eneo

  2. Manufaa

  3. Kufahamika

  4. Mteja

  5. Kikwazo

  6. Madhara

  7. Kusambaza

  8. Mtazamo

  9. Ulimwengu

  10. Maarifa

  Zoezi la 3: Jaza nafasi iliyoachwa wazi kwa kutumia maneno yafuatayo: chombo, kiungo, manufaa, madhara, watawala, lugha ya Kiswahili, utamaduni, imeteuliwa, zinazowatambulisha, pato.

  1. Kufuata kanuni zote za shule kulimletea .............................

  2. .............. inazungumzwa katika jamii nyingi barani Afrika.

  3. Watu hawa ......................... na sifa za ushikamano na ushirikiano.

  4. Lugha ni .......................................................... cha kupashana habari.

  5. .................... la mfanyabiashara huyu ni kubwa kwa sababu anapokea wateja wengi wenye lugha mbalimbali.

  6. Lugha huunganisha .................................... na watawaliwa.

  7. Ukataji wa miti ulileta .............................. mengi kwa sababu mvua iliponyesha kulitokea mmomonyoko wa ardhi.

  8. ..................... wa Wanyarwanda unadumisha amani, ushirikiano, upendo, kazi na kusaidiana.

  9. Daraja lile ni ............................... kati ya maeneo yale.

  10. Nchi yetu ..................... miongoni mwa nchi kumi zenye usalama duniani kote.

  4.3 Sarufi: Matumizi ya Viambishi vyenye Dhana ya Masharti: -ngeli-

  Zoezi la 4: Jadili kuhusu maana za sentensi zifuatazo zenye kiambishi -ngeli-; halafu utunge sentensi tano zenye kiambishi hicho.

  a. Tungelisoma vizuri tungelishinda mtihani huu.

  b. Wangelikuwa hapa tungeliwaeleza.

      • Kama viambishi -nge- tulivyoona hapo katika masomo yaliyotangulia somo hili, kiambishi –ngeli- huonyesha masharti yasiyowezekana katika hali yakinishi. Katika hali kanushi kikanushi -si- huongezewa na kufuatwa na -ngeli-.

  Zoezi la 5: Kamilisha sentensi zifuatazo ili zilete maana kamili.

  Mifano: Angelikuwa mfalme, angeliishi raha mustarehe.

                Asingelikuwa mfalme, asingeliishi raha mustarehe.

  1. Chumba hiki kingelikuwa kikubwa, ............................................

  2. Chumba hiki kisingelikuwa kikubwa, ..........................................

  3. Wali usingelikuwa mtamu, .................. ......................................

  4. Minazi ingelizaa madafu mengi, .................................................

  5. Minazi isingezaa madafu mengi, .................................................

  6. Mwanafunzi angelisoma kwa bidii, ................................................

  7. Ningelikuwa daktari, ................................................................

  8. Tungelikuwa na pesa, ............................................................

  9. Ungelikuwa na ujuzi kamili, .....................................................

  10. Wapishi wangelikuwa na viungo,................................................

  4.4 Matumizi ya Lugha: Mwenye Lugha Moja na Mwenye Lugha Nyingi

  Zoezi la 6: Soma mazungumzo yafuatayo kati ya Mwenye lugha moja na Mwenye lugha nyingi, kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini.

  Mwenye lugha nyingi

  Mwenzangu njoo karibu,

  Nikupe ya manufaa

  Uyapate ya wajibu,

  Uepuke na fazaa

  Usije kupata tabu,

  Dunia ina hadaa.

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni umuhimu.

  Mwenye lugha moja

  Niache nishike njia,

  Maneno hayo sitaki kusikia,

  Ufidhuli mwajipalia,

  Hewani mwaingia,

  Lugha yazidi kudidimia,

  Yeye mzazi analilia.

  Ujuzi wa lugha moja,

  Utamaduni ninatetea.

  Mwenye lugha nyingi

  Utamamaduni unaendelea,

  Siku zote hubadilika,

  Kukopesha si kukosea,

  Lugha ngeni ikainuka,

  Maarifa ukapokea,

  Usije ukajifunga.

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni muhimu.

  Mwenye lugha moja

  Usidhani nimeduwaa,

  Ninakusikia sababu,

  Sitatoka humu mtaani,

  Nitatumia ya mababu,

  Niyasemayo ni taa,

  Nionyeshe taratibu.

  Ujuzi wa lugha moja,

  Utamaduni ninatetea.

  Mwenye lugha nyingi

  Za ugeni unahitaji,

  Rafiki wamiminike,

  Ukipata huo mtaji,

  Utasafiri ufaidike,

  Utanena nini ukijifariji?

  Faida itakuponyoka.

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni umuhimu

  Mwenye lugha moja

  Mkalimani ana kazi ipi?

  Sitasita kuajiri ,

  Atasema nipate nazi,

  Hiyo tija nikapata.

  Atanena nipate vazi,

  Nguo nzuri nitakata. U

  juzi wa lugha moja,

  Utamaduni ninatetea

  Mwenye lugha nyingi

  Lugha nyingi zawezesha,

  Magazeti kujisomea

  Habari tele zikaja,

  Taarifa ukajipatia,

  Fununu hizo zikaisha,

  Ukweli ukajitambulia .

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni umuhimu.

  Mwenye lugha moja

  Kusoma kunaua macho,

  Wenye uwezo watanisomea,

  Kihabari wenye kuwa nacho,

  Nyumbani wataniletea,

  Nipate kile kijacho,

  Ujuzi ukinisogelea.

  Ujuzi wa lugha moja,

  Utamaduni ninatetea

  Mwenye lugha nyingi

  Usije ukajitia kizuizi,

  Jaribu kupata fahamu ,

  Kisha ukawa kama sisimizi,

  Ukajikuta umemeza sumu

  Kashika hata singizi,

  Kwa sababu huisomi fomu,

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni muhimu.

  Mwenye lugha moja

  Maisha ya binadanu,

  Yanatokana na Manani

  Ninarudi kutakadamu,

  Nililosema mwanzoni,

  Mtu akimeza sumu,

  Atakwenda mbio ugangani.

  Ujuzi wa lugha moja,

  Utamaduni ninatetea

  Mwenye lugha nyingi

  Kulumbana naachia,

  Ndugu yangu nipe kijia

  Maelezo unazuia,

  Umetia pamba sikioni,

  Ukitaka wajifunulia,

  Pazia inayokufunga.

  Katika ya manufaa,

  Ulumbi ni umuhimu.

  Mwenye lugha moja

  Ndugu yangu nimepiga goti,

  Ninaomba samahani,

  Ujinga ninaupiga shuti,

  Na mimi nimetoka hewani,

  Humu mtaani katikati,

  Nimepata kuelewa,

  Mbele ya manufaa kweli,

  Ulumbi ninapigia saluti.

  Jibu maswali yafuatayo

  1. Katika makundi ya wanafunzi watatu watatu, jadilieni kwa kubainisha faida za kujua lugha moja na zile za kujua lugha nyingi.

  2. Kwa nini Mwenye lugha moja anampigia magoti mwenye lugha nyingi ?

  Zoezi la 7: Tafuteni maana za maneno haya yafuatayo kulingana na matumizi yake katika kifungu mlichosoma hapo juu, kisha mtunge sentensi zenu kwa kutumia maneno hayo.

  1. Ulumbi

  2. Fazaa

  3. Hadhaa

  4. Nimeduwaa

  5. Mtaji

  6. Kujifariji

  7. Fununu

  8. Sisimizi

  9. Manani

  10. Kutakadamu

  Zoezi la 8: Tafuteni na kuandika maneno kumi yaliyotumiwa katika shairi kwenye jedwali lifuatalo:


  Maelezo muhimu kuhusu faida na hasara za kutumia lugha moja

  Maelezo Muhimu

  •  Utumiaji wa lugha moja katika jamii una faida na hasara zake.
  •  Kwa upande mmoja, utumiaji huu wa lugha moja hukuza umoja, ushikamano, ushirikiano, na amani miongoni mwa wanajamii wanaotumia lugha hiyo. Vilevile, utumiaji wa lugha moja katika jamii huweza kusaidia kiuchumi na kisiasa kwa sababu wafanyabiashara, viongozi na wananchi wote huwasiliana moja kwa moja bila kikwazo chochote cha lugha.
  • Kwa upande mwingine, hasara za kutumia lugha moja katika jamii nazo hujitokeza pale wanajamii hawawezi kuwasiliana na ulimwengu mzima. Wao hujifungia mahali pamoja na kujiwekea mipaka ya kupata habari na kujua yanayotendeka katika jamii nyingine. Kutojua yanayojiri nje ya jamii yao ni hasara kwa sababu katika dunia ya leo ambapo tekinolojia na sayansi zimeendelea na kuifanya dunia iwe kama kijiji kimoja. Leo hii, elimu, sayansi na tekinolojia ni mambo muhimu yanayomfanya mwanajamii atie bidii kujifunza lugha mbalimbali kwani lugha hizo humsaidia kuwasiliana na kujua mengi kutoka kwa jamii nyingine.

  4.5 Kusikiliza na Kuzungumza : Uigizaji wa Mazungumzo

  Zoezi la 9: Igizeni mazunguzo kati ya mtu anayezungumza lugha moja tu na mtu anayezungumza lugha nyingi.

  4.6 Kuandika : Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 10: Tunga kifungu chenye mada ifuatayo (Ukurasa mmoja): “Lugha ni ufunguo wa maisha mazuri kwa binadamu.”

  SOMO LA 5 : ASILI YA LUGHA YA KISWAHILI

                                        

  Zoezi la 1: Tazama mchoro hapo juu kisha utoe maoni yako kuhusu kile kinachoonekana kwenye mchoro huo.

  5.1 Kusoma na Ufahamu : Asili ya Lugha ya Kiswahili

  Soma kifungu cha habari kuhusu “Asili ya Lugha ya Kiswahili” kisha, jibu maswali yaliyotolewa hapo chini.

  Kiswahili ni lugha ya Kiafrika ambayo huhesabiwa katika lugha za Kibantu. Lugha hii ni maarufu sana ndani na hata nje ya bara la Afrika. Neno Kiswahili lilianza kutumika karne ya kumi na nne (Baada ya Kristo Kuzaliwa). Neno hili lilitoka kwa wageni wa Kiarabu waliokuja barani Afrika kwa shughuli zao za kibiashara. Wakati huo walifika Pwani ya Afrika Mashariki.

  Eneo hili ndilo lililopewa jina la “sawahil” (au sahel) kwa maana ya eneo la watu wa pwani; yaani sehemu iliyo kandokando ya bahari au mwambao. Wenyeji wa sehemu hiyo ndio walioitwa “sawahiliya”(Sawahel). Neno “Sahel” baadaye lilileta jina jingine “Kiswahili” kwa maana ya lugha ya watu wa sehemu hiyo ya pwani, ambapo watu wenyewe waliitwa Waswahili. Kiswahili ni lugha yenyewe. Watu wanaoizungumza lugha hiyo ni Waswahili wenye utu na utamaduni wao.

  Kuna mitazamo minne muhimu inayozungumzia kuhusu asili ya Kiswahili: Mtazamo wa kwanza ni ule unaotetea kuwa asili ya Kiswahili ni Kiarabu. Watu wanaoshikilia mtazamo huu wanahoji kwamba katika lugha ya Kiswahili kuna maneno mengi ya Kiarabu. Maneno hayo ni kama vile laki, elimu, fahamu, daima, enzi, mahabusi, ilani, ratibu, nadra, jasisi, kauli, na mengineyo. Watetezi wa hoja hii wanaeleza pia kwamba Kiswahili kilitumiwa na wenyeji wa sehemu hiyo ya mwambao waliokuwa Waislamu. Kwa kuwa Uislamu uliletwa na Waarabu, basi wao husisitiza kuwa lugha ya Kiswahili imeletwa na Waarabu hao.

  Mtazamo wa pili ni wa kusema kwamba Kiswahili ni lugha chotara; yaani mchanganyiko wa lugha za pwani na Kiarabu. Madai haya yanajikita kwenye hoja kwamba wakati Waarabu walipokuwa wakifanya biashara, waliamua kukaa pwani na kuoa wanawake kutoka sehemu hiyo ya pwani. Kwa hivyo, ndoa hiyo kati ya wenyeji wenye lugha za Kibantu na Waarabu wenye lugha ya Kiarabu ndiyo iliyozaa lugha mpya iliyochanganya lugha ya Kiarabu na lugha nyingine za Kiafrika ili kuleta lugha chotara. Maana yake Kiswahili; mchanganyiko wa Kiarabu na lugha za Kibantu.

  Mtazamo wa tatu hutetea Kiswahili kuwa lugha ya kibantu. Baadhi ya watetezi huchukua lugha ya Kiswahili kama lugha ya Kibantu ambayo ilikuwepo hata kabla ya majilio ya wageni; yaani lugha hii ilijitambulisha kama lugha ya Kibantu toka zamani. Wengine huitazama lugha ya Kiswahili kama lugha iliyotokana na mchanganyiko wa lugha tofauti za Kibantu zilizotumiwa sehemu ya pwani. Katika mawasiliano baina ya watumiaji wa lugha hizo, wao walilazimika kurahisisha lugha zao kwa kiasi fulani ili waweze kuelewana na kufanikisha shughuli zao katika maeneo mbalimbali.

  Katika hali hii kulizuka lugha moja iliyoeleweka kwa watu wote wa eneo zima la upwa wa Afrika Mashariki kuanzia Kaskazini hadi Kusini. Matokeo yake yalikuwa lugha zilizojulikana kama lahaja za Kiswahili; yaani lugha zilizohusiana sana kiasi kwamba wazungumzaji wake waliweza kuzitumia na kuelewana kwa urahisi. Mifano ya lahaja hizo za Kiswahili ni Kimakunduchi, Kihadimu, Kitumbatu, Kibajuni, Kisiu, na Kiamu kwa uchache

  Mtazamo wa nne ni ule unaokiangalia Kiswahili kama pijini na baadaye ikaendelea hadi kufikia kuwa Kreoli. Pijini hujitokeza pale ambapo watu wanaotumia lugha tofauti wanapokutana hujaribu kutafuta lugha rahisi ya kufanikisha mawasiliano ya pande hizo mbili. Kila upande huchangia kutoa msamiati. Sarufi ya pijini huwa rahisi sana. Hivyo Kiswahili kinatazamwa kama kilichoanza kama pijini iliyotokana na lugha za Kiafrika pamoja na lugha ya Kiarabu. Pijini hii ilivyokomaa ikawa krioli. Hivyoo huu ndio mtazamo wa nne kuhusiana na asili ya Kiswahili.

  Kwa kweli, ni lazima maoni ya watu mbalimbali kuhusu asili ya Kiswahili yachunguzwe kwa makini, ili yasiweze kupotosha watu wenye hamu ya kujua mengi kuhusu asili ya lugha hiyo, yenye thamani kubwa katika Afrika nzima na hata nje ya Afrika. Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye uhusiano na lugha nyingine za Kibantu kama Kinyarwanda, Kirundi na nyingine. Asili, maana yake chimbuko lake ni sehemu ya pwani ya Afrika Mashariki ambako kulizungumzwa lugha mbalimbali za Kibantu zilizofanana sana.

  Maswali ya ufahamu

  1. Neno “Kiswahili” lilianza kutumiwa lini?

  2. Neno “Kiswahili” lilitoka wapi? Eleza zaidi jibu lako.

  3. Katika kifungu chetu tunaweza kupata mitazamo minne ya asili ya lugha ya Kiswahili. Taja mitazamo hiyo yote kwa ufupi.

  4. Kwa nini baadhi ya watu walifikiria kuwa Kiswahili kilitokana na Kiarabu? Taja maneno matatu ya Kiarabu yanayopatikana katika Kiswahili.

  5. Kusema kwamba lugha ni “chotara” ni kumaanisha nini?

  6. Asili ya Kiswahili ni ipi?

  7. Taja lahaja za Kiswahili ambazo zinapatikana katika kifungu ulichosoma.

  8. Waarabu walifika kwenye sehemu za pwani Afrika Mashariki kwa lengo gani?

  9. Kwa nini ni lazima kuchunguza kwa makini maoni ya watu mbalimbali kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili?

  10. Taja lugha za Kibantu zilizozungumziwa katika kifungu cha habari ulichosoma.

  5.2 Msamiati Kuhusu Asili ya lugha

  Zoezi la 2: Andika maana za maneno haya yafuatayo kwa kuzingatia matumizi yake katika kifungu ulichosoma hapo juu, kisha utunge sentensi kwa kutumia maneno hayo:

  1. Kibantu

  2. Chotara

  3. Chimbuko

  4. Pwani

  5. Mawasiliano

  6. Maarufu

  7. Utu

  8. Utamaduni

  9. Lahaja

  10. Watetezi

  5.3 Sarufi: Matumizi ya Viambishi vyenye Dhana ya Masharti: “-ngali-”

  Zoezi la 3: Soma sentensi ulizopewa hapo chini, kisha ueleze matumizi halisi ya kiambishi -ngali- katika sentensi hizo. Hakikisha unabainisha maana za kila sentensi iliyotumiwa.


  Maelezo muhimu:

  Kama kiambishi chenye dhana ya masharti -nge- ambacho tulikiona awali, kiambishi cha masharti -ngali- huweza kutumika kwa hali moja bila ya tofauti. Ni kusema kwamba kiambishi kimoja kinaweza kutumika badala ya kingine. Katika kukanusha kiambishi si huongezwa.

  Zoezi la 4: Jaribu kujaza sentensi zifuatazo zenye kiambishi -ngali- kufuatilia mfano uliotolewa hapa chini:

  Mfano: Tungalikuwa na muda wa kutosha tungalizungumzia mengi kuhusu lugha.

  1. Tungalikuja, ................................................... (kuonana).

  2. Tungalionana, ................................................. (kumaliza) kazi ya nyumbani.

  3. Tungalikuwa na pesa, ................................................ (kusafiri) kwa ndege.

  4. Wapishi wangalikuwa na viungo, ......................................... (kupika) chakula kitamu.

  5. Wafanyabiashara wale wangalilipa ushuru .............................. (kuadhibiwa).

  Zoezi la 5: Andika sentensi zifuatazo katika hali kanushi.

  1. Mngalipendana, mngalijenga umoja.

  2. Mngalifanya kazi vizuri, mngalifaulu mtihani.

  3. Wangaliomba, wangalipewa.

  4. Wazee wangalikuwepo, mambo yangalisawazishwa.

  5. Kioo kingalianguka, kingalivunjika.

  Zoezi la 6: Andika sentensi zifuatazo katika hali yakinishi

  1. Yeye asingalizungumza vizuri, tusingalielewana.

  2. Usingalijua hatari ya ukimwi, ungaliyafanya hayo.

  3. Chumba kisingalisafishwa, kisingalipendeza.

  4. Mwashi asingalikuwa makini, nyumba isingalikuwa imara.

  5. Gari lisingalikuwa zuri, tusingalifika mapema.

  5.4 Matumizi ya Lugha: Mitazamo Tofauti Kuhusu Asili ya Lugha ya Kiswahili

  Zoezi la 7: Someni kifungu kifuatacho kwa kujaza nafasi zilizoachwa wazi, ukitumia baadhi ya maneno kutoka kwenye kifungu ulichosoma hapo juu, ili kiweze kuleta maana kamili:

  Mzee Ngirimana na mke huwasiliana katika lugha ya Kinyarwanda. Lugha hiyo ni lugha ya .................. kama vile Kiswahili na Lingala. Mzee Hassan ambaye ni rafiki yake Mzee Ngirimana ni Muislamu. Kila Ijumaa huenda ..................... kusali katika lugha ya Kiarabu. Zabibu Binti yake Hassan aliolewa na mwanaume Mwarabu. Hivi sasa ................... watoto wawili. Watoto hao .................. katika mchanganyiko wa Kinyarwanda na Kiarabu. Lugha wanayoitumia huitwa................... Asili ya Kiswahili ni ........ ya Afrika .............. ilhali ya Kinyarwanda ni nchini Rwanda. Sasa .............ya lugha ya watoto hao ni ipi?Kasimu na Tumusifu, ............ wake Mzee Hassan wanasoma katika kidato cha nne mch epuo wa lugha. Jana mwalimu wa .................. aliwapa kazi ya nyumbani. Kazi hiyo ni ya kutaja ............ za Kiswahili.

       • Maelezo Muhimu kuhusu mitazamo mbalimbali kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili

  Zoezi la 8: Jadili kuhusu maelezo yafuatayo ili kubainisha hoja muhimu zinazoambatana na asili ya lugha ya Kiswahili .

  5.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 9: Kwa kushirikiana na wenzako, jadili mitazamo minne kuhusu asili ya lugha ya Kiswahili.

  Zoezi la 10: Jadili kuhusu mitazamo mbalimbali ya asili ya lugha ya Kiswahili, kisha udhihirishe msimamo wenye mashiko zaidi kuliko mengine.

  5.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 11: Tunga kifungu chenye mada ifuatayo: “Manufaa ya Kiswahili kwa wananchi wa Afrika Mashariki”

  SOMO LA 6: KUENEA KWA LUGHA YA KISWAHILI

       Tazama mchoro hapo chini, kisha ujibu swali lifuatalo hapo chini

  Zoezi la 1: Tazama michoro hapo juu kisha utoe maoni yako kuhusu mambo yanayoendelea.

  6.1 Kusoma na Ufahamu: Kuenea kwa Lugha ya Kiswahili

  Soma kifungu cha habari kuhusu maenezi ya lugha ya Kiswahili, kisha jibu maswali yaliyotolewa hapo chini.

  Tunaposema kuwa lugha fulani imeenea, tunamaanisha kuwa lugha hiyo imeongeza idadi ya watumiaji wake katika nchi inamotumika au hata na nje ya nchi hiyo. Idadi ya watumiaji wake huzidi kuongezeka hatua kwa hatua mpaka lugha hiyo ivuke mipaka ya awali na kusambaa mahali pengi. Leo hii, kwa mfano, lugha ya Kiswahili ambayo chimbuko lake la asili ni Pwani ya Afrika Mashariki, huzungumzwa katika nchi nyingi za Afrika kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji na mahali pengine pengi katika bara la Afrika na nje yake.

  Ueneaji wa lugha ya Kiswahili ulitokana na shughuli mbalimbali za watu waliokuwa wakitumia lugha hiyo. Wenyeji wa pwani pamoja na watumiaji wa lugha ya Kiswahili walihitaji kuwasiliana na watu wengine, hivyo mawasiliano hayo yakasaidia lugha ya Kiswahili kuweza kuenea katika sehemu nyingine ambapo Kiswahili kinatumiwa mpaka sasa. Safari za kibiashara baina ya watu kutoka pwani hadi bara zilikuwa zikifanywa mara kwa mara. Kwa njia hii matumizi ya lugha ya Kiswahili yalizidi kuenea katika nchi mbalimbali ambako biashara hizo zilikuwa zikifanyika. Sababu nyingine iliyochangia kueneza lugha ya Kiswahili ni misafara ya watumwa iliyokuwa ikifanywa na Waarabu. Kila mahali watumwa hao walipopitia, waliacha athari za lugha hii ya Kiswahili.

  Shughuli za kiutawala na utangazaji wa imani za dini nazo zilisaidia sana katika kuisambaza lugha hii ya Kiswahili. Ujenzi wa makanisa na misikiti, makao makuu ya utawala pamoja na shule ni miongoni mwa mambo mengi yaliyosaidia kuenea kwa Kiswahili. Katika hali hii, mchango wa wakoloni, wasafiri wa kiarabu na hata wamishenari kutoka sehemu za pwani hadi maeneo mengine ya bara la Afrika ulikuwa mkubwa sana. Wakoloni katika Afrika Mashariki waliwashurutisha watumishi wao kuzungumza na kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zao za kikazi kwani walifikiri kuwa lugha hii ya Kiswahili ilikuwa rahisi kujifunza kuliko lugha nyingine za kiasili.

  Aidha, katika mfumo wa kufanikisha utawala, Waafrika na Wakoloni walitumia Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano baina yao. Kwa mfano, Wajerumani katika kipindi chao kifupi cha utawala, huko Tanganyika walianzisha shule zilizotoa elimu kwa Kiswahili; na hii ilikuwa hatua muhimu iliyosaidia sana kueneza Kiswahili nchini kote. Waingereza walipofika nao walichangia sana kwa kuchukua hatua kubwa mnamo mwaka 1934 ambapo waliunda kamati kwa lengo la kufuatilia usanifishaji wa lugha ya Kiswahili. Wamishenari kwa upande wao, waliamua kutumia lugha ya Kiswahili kuwahubiria waumini wao mpaka wakajenga shule ambapo walifundisha lugha ya Kiswahili kwa madhumuni ya kuweza kueneza Injili.

  Tangu wakati huo, Kiswahili kimezidi kuenea na kuzagaa duniani kote kiasi kwamba siku hizi kimeishapata hadhi ya kuwa mojawapo ya lugha muhimu za kimataifa. Juhudi nyingine nyingi zinazidi kufanywa ili kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili barani Afrika na nje yake. Miongoni mwa shughuli muhimu zinazoweza kusisitiziwa hapa ni pamoja na uandishi wa vitabu vya Kiswahili, magazeti yanayotumia lugha ya Kiswahili, taasisi mbalimbali za kuendeleza Kiswahili na vyombo vya habari kama vile redio na televisheni zenye matangazo, habari na vipindi katika lugha ya Kiswahili.

  Nje ya bara la Afrika, Kiswahili hutumika sana katika shughuli nyingi za kibiashara, elimu, siasa na dini. Mpaka sasa idadi ya vyuo vinavyofundisha lugha ya Kiswahili imeongezeka huko Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Marekani ambapo watu wengi hujivunia kiwango cha masomo yanayotolewa katika lugha hii pamoja na kazi za utafiti zinazoendelezwa na wataalamu wa Kiswahili. Kumejitokeza idhaa za Kiswahili katika redio nyingi duniani, na watu wengi hufurahia vipindi na matangazo yanayotolewa kwa lugha hii. Vilevile, ni dhahiri kwamba lugha ya Kiswahili huzidi kuenea mahali pengi kwa kuwavutia wengi. Hivi sasa, idadi ya wapenzi wake huzidi kuongezeka kila kukicha.

  Maswali ya ufahamu

  Zoezi la 1: Soma kifungu hiki cha habari, kisha ujibu maswali yanayofuata.

  1. Mbali na nchi za Bara la Afrika, taja mahali pengine ambapo Kiswahili kinatumiwa.

  2. Tunaposema kwamba lugha imeenea ni kumaanisha nini?

  3. Ni shughuli zipi zinazochangia kueneza Kiswahili?

  4. Ni nini maana ya watumwa wanaozungumziwa katika kifungu hiki?

  5. Kwa nini wakoloni walizishurutisha baadhi ya nchi za Afrika kutumia Kiswahili?

  6. Kwa nini wamishenari waliamua kutumia lugha ya Kiswahili?

  7. Wakoloni walikuja barani Afrika kwa malengo gani?

  8. Ni lugha nyingine zipi za kimataifa zinazotumiwa katika eneo la nchi za Afrika zinazotumia Kiswahili?

  9. Kiswahili kimeathiri vipi lugha za kiasili katika nchi kinapotumiwa? Toa mifano.

  10. Ujuzi wa Kiswahili una umuhimu gani kwako?

  6.2 Msamiati Kuhusu Ueneaji wa Lugha ya Kiswahili

  Zoezi la 2: Tafuta maana za msamiati unaofuata kulingana na matumizi yake katika kifungu ulichosoma, kisha utunge sentensi kwa kutumia maneno hayo.

  1. Sambaa

  2. Wenyeji

  3. Watumwa

  4. Rasilimali

  5. Walishurutisha

  6. Kamati

  7. Mathalan

  8. Ubakaji

  9. Imani

  10. Kuimarisha

  Zoezi la 3: Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno haya: Sambaa, kuimarisha, watumwa, vituo, walishurutishwa, wakazi, kamati, imani, mamlaka, idhaa.

  1. Wanafunzi .................................. kuzungumza kwa lugha Kiswahili kama njia bora ya kujua lugha hiyo.

  2. ........................................ walisafirishwa kutoka Afrika kuelekea Marekani.

  3. Kiswahili .............................................. katika sehemu mbalimbali za dunia.

  4. ............................................ wa eneo hilo wamefurahishwa na shule waliyojijengea.

  5. Sehemu tofauti za pwani barani Afrika zilitumiwa kama ........................vya utumwa.

  6. Kuna ....................................mbalimbali zinazotangaza habari katika Kiswahili.

  7. Kumeundwa ............................ ya kushughulikia elimu ya watu wazima.

  8. Rais wa Jamhuri ya Rwanda amepewa ...............................ya kuiongoza nchi ya Rwanda.

  9. Kila madhehebu humuenzi Mungu kulingana na .......................................yake.

  10. Serikali ina jukumu la ........................................ amani nchini.

  6.3 Sarufi: Matumizi ya Viambishi Vyenye Dhana ya Masharti

  Zoezi la 4: Andika sentensi zifuatazo ukitumia viambishi vyenye dhana ya masharti -ngali-

  1. Mlipendana, mliunda umoja.

  2. Mlijifunza kwa bidii, mlishinda mtihani.

  3. Waliomba, walipewa.

  4. Wazazi hawakuwepo ndiyo maana mambo hayakusawazishwa.

  5. Mtoto hakuanguka ndiyo mana hakuvunjika.

  Zoezi la 5: Andika sentensi zifuatazo katika hali kanushi:

  1. Mngalionana, mngalisalimiana.

  2. Mngaliamka mapema, mngalifika shuleni kwa wakati ufaao.

  3. Wangaliomba msaada, wangaliupewa.

  4. Wazee wangalikuwepo, mambo yangalisawazishwa.

  5. Angalishiriki mashindano hayo, angalichaguliwa.

  6.4 Matumizi ya Lugha: Maenezi ya lugha ya Kiswahili

  Zoezi la 6: Chunguzeni jedwali hapo chini ili mwandike maneno kamili yaliyopo

  Kwa mfano: “WAARABU”


  Maelezo Muhimu Kuhusu Ueneaji wa Lugha ya Kiswahili

  Chunguza maelezo haya yafuatayo kuhusu ueneaji wa lugha ya Kiswahili kisha, fanya zoezi linalofuata hapo chini

  Maelezo muhimu

  Ueneaji wa Kiswahili ulitokana na wenyeji wa pwani pamoja na watumiaji wa Kiswahili waliohitaji kuwasiliana na watu wengine, hivyo mawasiliano hayo yakasaidia lugha ya Kiswahili kuweza kuenea katika sehemu nyingine ambapo Kiswahili kinatumiwa mpaka sasa.

  Kuna shughuli mbalimbali zilizochangia kueneza Kiswahili katika sehemu mbalimbali za dunia kama vile safari za kibiashara baina ya watu kutoka pwani hadi bara,uandishi wa vitabu vya Kiswahili, magazeti yanayotumia lugha ya Kiswahili, taasisi mbalimbali za kuendeleza Kiswahili na vyombo vya habari kama vile redio, televisheni na tovuti.

  Leo hii Kiswahili kimefika nje ya bara la Afrika kama vile Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Amerika ambapo Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu. Hivi sasa, idadi ya watumiaji wa Kiswahili inazidi kuongezeka kila kukicha.

  Zoezi la 7: Jadili kuhusu “Kuenea kwa lugha ya Kiswahili”

  6.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 8: Jadilieni kuhusu shughuli zilizosaidia kuenea kwa lugha ya Kiswahili na nafasi yake barani Afrika kulingana na lugha nyingine za kimataifa.

  6.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 9: Kwa kuzingatia matumizi ya kiambishi “-ngali”, tunga kifungu cha habari kuhusu mada ifuatayo: “Kiswahili ni Lugha ya Kimataifa”.

  SOMO LA 7: HISTORIA YA KISWAHILI NCHINI RWANDA

                               

  Zoezi la 1: Toa maoni yako kuhusu shughuli zinazoendelea kwenye mchoro hapo juu.

  7.1 Kusoma na Ufahamu : Mazungumzo kati ya Wanafunzi

  (Kabano na Mutesi ni wanafunzi wa kidato cha nne, mkondo wa Fasihi katika Kiingereza–Kiswahili-Kinyarwanda. Wao wamo katika chumba chao cha masomo kwa ajili ya kufanya kazi waliyopewa na mwalimu wao wa Kiswahili).

  Kabano : Hujambo dada!

  Mutesi: Sijambo kakangu!

  Kabano: Unafikiri nini kuhusu kazi tuliyopewa?

  Mutesi: Kazi gani hiyo? Ama unazungumzia kazi tuliyopewa jana kuhusu “Maendeleo ya Kiswahili nchini Rwanda?” Njoo hapa tushirikiane! Nafikiri kwamba mawazo tutapata. Mimi nimesoma vitabu vingi na wewe ulibahatika kuzungumza na babu yako ambaye alikuelezea mengi kuhusu historia ya lugha ya Kiswahili.

  Kabano: Angalia hapa... vilevile nimeleta vitabu hivi...nadhani vitatufaa sana. Ungelinijulisha jana, ningeliandika mengi kutoka kwa babu. Toa maoni yako tuanze kazi yetu.

  Mutesi: Mimi.... kwa maoni yangu, ninafikiri kwamba kazi hii tutaigawa katika vipengele vikuu vitatu: kipengele cha kwanza kinahusu “Kiswahili wakati wa ukoloni”, cha pili “Kiswahili baada ya ukoloni” na cha tatu “Kiswahili baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.”

  Kabano: Ni vizuri. Lakini wakati wa ukoloni nao tutatofautisha ukoloni wa Ujerumani na ukoloni wa Ubelgiji.

  Mutesi: Kabano! Niambie...kuhusu kuingia kwa Kiswahili nchini mwetu.

  Kabano : Kufuatana na historia, kitabu hiki kinaeleza kwamba mwaka 1892 ndipo nchi ya Rwanda ilianza kupokea wageni wa kwanza ambao walikuwa wakitumia lugha ya Kiswahili. Hun! Ningelikuwepo enzi hizo, ningeliwaona wageni hao wote na kusikiliza walivyozungumza lugha yetu ya Kiswahili!

  Mutesi: Kweli! Nami pia ningelipenda kuwaona kabisa. Lakini, mbali na hayo, kumbuka kwamba Kiswahili kiliingia nchini Rwanda kupitia sehemu mbili muhimu. Tusomapo kitabu hiki, tunapata kwamba sehemu ya kwanza ni ile iliyopitiwa na Mjerumani Daktari Oscar Bauman pamoja na watu wake. Wao walikuwa wanatumia Kiswahili katika mawasiliano yao na Wanyarwanda.

  Kabano: Ni kweli. Wakalimani wa siku hizo walifanya kazi ngumu ya kuwaelezea Wanyarwanda wengine yaliyokuwa yakizungumzwa katika lugha ya Kiswahili. Wengi wao walikuwa hawajaifahamu lugha hiyo.

  Mutesi: Ndiyo. Wakalimani hao walikuwa na kazi isiyo rahisi. Pia kuna sehemu nyingine ya pili ambapo ndipo Von Gotzen alipopitia. Yeye alivuka mto wa Akagera kupitia sehemu za Mashariki mwa Rwanda mnamo mwaka 1894. Jinsi Wajerumani hao walivyosonga mbele kwa kutaka kuonana na viongozi wenyeji wa Rwanda ndivyo Kiswahili kilivyojipenyeza katika jamii ya Wanyarwanda.

  Kabano: Lakini usisahau kitu kingine muhimu sana. Ni kupitia Magharibi mwa Rwanda ambapo Wabelgiji walipitia kutoka koloni lao la awali lililokuwa likijulikana kwa jina la Kongo ya Ubelgiji.Hawa walikuwa wakiongea Kingwana au Kiswahili cha Kongo. Hata hivyo, waandishi wengi hueleza kuwa chini ya utawala wa Wabelgiji Kiswahili hakikuendelea kupewa nafasi kubwa nchini Rwanda. Wao walipenda Kifaransa kitumike zaidi katika shughuli nyingi....na jambo hili lilitokea baada ya Wajerumani kushindwa Vita vya Kwanza vya Dunia.

  Mutesi : Hilo nalikumbuka vizuri. Ni mojawapo ya mambo aliyotuelezea mwalimu wetu wa Historia kuhusu vita hivyo. Tangu wakati huo, Kiswahili kilifumbiwa macho na utawala wa Wabelgiji, kikaanza kupoteza hadhi na nafasi yake katika jamii ya Wanyarwanda. Wengi waliokionea walikuwa wakiita lugha hii lugha ya watu wenye vitendo vibovu, majambazi na watu wengine wenye kukosa nidhamu na mienendo mizuri inayomtambulisha kila Mnyarwanda.

  Kabano: Hun! Mimi nisikiapo hali hii husikitika sana.Ningelikuwa hapo, ningelitetea lugha hii yenye kuvutia wengi na yenye sifa za uungwana. Huwezaje kupuuzwa mpaka kuhusishwa na watu wenye tabia hizo? Jambo hilo liliwafanya siku hizo Wanyarwanda wasione umuhimu wake. Mwalimu wetu alituambia kwamba baada ya uhuru ndipo Serikali ya Rwanda ilianza kushughulikia lugha ya Kiswahili kwa kuifundisha katika baadhi ya shule na kwa kutumiwa katika matangazo mbalimbali kwenye redio Rwanda. Mwalimu alisisitizia kwamba vipindi vilivyopitishwa kwenye redio ni pamoja na taarifa ya habari, salamu za wasikilizaji, matangazo ya mpira, ulimwengu tuishio, na vingine vya kuelimisha jamii.

  Mutesi: Je, hukumbuki kwamba mwalimu alisema pia kuwa miaka ya 1970 nchi za Rwanda na Tanzania ziliamua kushirikiana katika maswala kadhaa ambapo ufundishaji wa Kiswahili sanifu ulipewa kipaumbele? Tangu wakati huo, idadi ya shule za sekondari zilizokuwa zinafundisha Kiswahili iliongezeka. Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilijaribu kukuza na kuendeleza ufundishaji wa lugha hiyo, walimu wakaajiriwa, vitabu na vifaa vingine vya ujifunzaji vikanunuliwa.

  Kabano: Kweli! Kiswahili kilitoka mbali kabisa na kilipambana na changamoto nyingi kwa ueneaji wake nchini Rwanda.

  Mutesi: Jambo jingine muhimu sana, kumbuka vizuri! Mwalimu wetu alituelezea kwamba baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994 ndipo lugha ya Kiswahili iliweza kushamiri katika sekta nyingi za maisha ya kila siku ya Wanyarwanda. Tangu wakati huo, mtazamo wa Wanyarwanda kuhusu lugha ya Kiswahili ulibadilika na wakati huo wengi walikuwa na hamu ya kukijua na kukizungumza.

  Kabano : Hilo ni jambo muhimu sana. Thamani ya Kiswahili ilijibainisha waziwazi. Kiswahili kilitoka shuleni kikaingia katika shughuli za kila siku za Wanyarwanda.

  Mutesi : Mimi ninapojaribu kuchunguza hali hii kwa makini, ninatambua kuwa haya yalikuwa matokeo ya uongozi mzuri tuliokuwa nao. Wanyarwanda walianza kufahamu vizuri umuhimu wa kushirikiana na raia wengine kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo ndipo kitovu cha matumizi ya Kiswahili.

  Kabano: Hilo ni kweli kabisa. Serikali yetu hutuhimiza kuwa na mipango mizuri inayotuwezesha kufanikisha maisha yetu. Siku hizi Wanyarwanda wengi huvuka mipaka ya Gatuna, Kagitumba, Rusumo, Rusizi, Rubavu na Akanyaru, ili kuendeleza biashara zao. Wengi wao hujivunia ujuzi mzuri walio nao kuhusu lugha ya Kiswahili kwani hawakutani na tatizo lolote la kuwasiliana na watu wengine wanaokutana nao huko katika nchi jirani.

  Mutesi : Mimi ninaipongeza serikali yetu ya Rwanda kwa uamuzi mzuri wa kuidhinisha kuwa lugha hii iwe lugha rasmi. Jambo hili litasaidia sana katika kuendeleza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili miongoni mwa wananchi wote kwani leo hii Wanyarwanda wote wanaelewa vizuri umuhimu wake katika nyanja tofauti: Siasa, elimu, uchumi, diplomasia na nyingine nyingi. Hivyo basi, kupitia lugha ya Kiswahili, mahitaji yetu yatatoshelezwa bila wasiwasi.

  Kabano: Kutokana na umuhimu wa lugha hii, ni lazima sisi kama wanafunzi tutie bidii kujifunza vizuri ili tuweze kuizungumza na kuiandika kwa usahihi. Kumbuka kuwa siku hizi lugha hii hufundishwa katika shule zote za awamu ya kwanza ya masomo ya sekondari na katika michepuo mingi ya awamu ya pili ya shule hizi. Mimi ninajivunia kwamba katika mtihani wa taifa niliweza kupata daraja la A katika somo la Kiswahili.

  Mutesi : Hongera sana kaka. Nami nilipata daraja hilo na wazazi wangu walilifurahia sana.

  Kabano: Haya. Naona tumezungumzia mengi na kuyaandika vizuri kwenye karatasi hii. Acha tumalizie hapa tutaonana kesho asubuhi. Nina matumaini kwamba mwalimu atafurahia kazi yetu. Kwa heri ya kuonana!

  Mutesi: Asante kaka kwa mchango wako katika kazi yetu. Tuonane kesho.

  Maswali ya ufahamu

  1. Kabano na Mutesi wanazungumzia nini?

  2. Historia ya Kiswahili nchini Rwanda imeweza kugawanywa katika vipindi gani?

  3. Taja majina ya wageni waliosaidia kuenea kwa Kiswahili nchini Rwanda.

  4. Wakalimani walifanya nini?

  5. Kwa sababu gani kwenye utawala wa Ubelgiji, matumizi ya lugha ya Kiswahili yalipungukiwa?

  6. Taja mambo yaliyofanywa na Serikali ya Rwanda kati ya miaka ya 1962 na 1994 ambayo yalichangia kwa kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

  7. Kabla ya mwaka 1994, Kiswahili kilihusishwa na watu wenye tabia gani?

  8. Wanyarwanda walianza kubadili mtazamo wao kuhusu Kiswahili na kutambua umuhimu wake kuanzia lini? Unafikiri kuwa hali hii ilitokana na nini?

  9. Serikali ya Rwanda ilifanya nini tangu 1994 mpaka sasa ili kuimarisha matumizi ya Kiswahili nchini Rwanda?

  10. Ni funzo lipi unalolipata kutokana na kifungu cha mazungumzo ulichosoma?

  7.2 Msamiati Kuhusu Historia ya Kiswahili Nchini Rwanda

  Zoezi la 2: Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia neno sahihi kati ya haya kutoka kifungu chetu cha mazungumzo: wanajivunia, lugha rasmi, kushirikiana, Jumuiya Afrika Mashariki, taarifa ya habari, utawala, walipongeza, matokeo, waliajiriwa, huvuka, kipaumbele.

  1. Serikali ya Rwanda inapendekeza usawa wa jinsia kwa kila ngazi ya ................

  2. Bwana Karekezi ---------- mpaka wa Gatuna mara moja kwa wiki kwa ajili ya biashara zake nchini Uganda

  3. Wanyarwanda wengi ------------- Serikali ya Rwanda baada ya kuidhinisha kuwa Kiswahili ni ----------------.

  4. Wananchi wa Jamhuri ya Tanzania wanapenda ................... na Wanyarwanda katika shughuli nyingi za kibiashra.

  5. ------------------------ inaundwa na nchi sita: Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Tanzania na Sudani ya Kusini

  6. ---------------- ya mitihani yameshatoka, wanafunzi wote wameyafurahia.

  7. -------------------- kutoka redio ya taifa inasema kwamba kila mwananchi ana haki ya kusoma bila ubaguzi.

  8. Wazazi wetu walifurahia kuwa ufundishaji wa lugha ya Kiswahili umepewa ----------------- katika shule zote za Sekondari nchini Rwanda.

  9. Wafanyakazi hawa ----------------- mwaka jana ili wafanye kazi iliyowashinda wengi. Wao ------------------ matunda ya kazi yao na pato lao limeongezeka sana.

  Zoezi la 3: Eleza maneno yafuatayo kulingana na matumizi yake katika kifungu cha mazungumzo mlichosoma:

  1. Wenyeji

  2. Kupenyeza

  3. Nidhamu

  4. Kushirikiana

  5. Uungwana

  6. Kitovu

  7. Kujivunia

  8. Lugha rasmi

  9. Kutia bidii

  7.3 Sarufi: Matumizi ya Kiambishi Chenye Dhana ya Masharti “ngeli”

  Zoezi la 4: Soma kifungu cha mazungumzo hapo juu, kisha uandike sentensi zenye kutumia kiambishi ngeli, halafu ujadili kuhusu maana zake

  Zoezi la 5: Tunga sentensi tano kwa kutumia kiambishi “ngeli” chenye mashartiZoezi la 6: Kamilisheni tungo zifuatazo:

  1. ............................................, angeliishi bila ukimwi.

  2. Watoto wetu wangelifuata mashauri yetu kuhusu usawa wa jinsia, ...............................

  3. Watu wale wangelijua njia za kuhifadhi mazingira, ...........................................

  4. Ningelisomea Kiswahili nchini Tanzania, ............................................

  5. ................................., wangeliwashitaki watu wote kwa makosa yao.

  6. Angelitumia muda wake wa kusoma ipasavyo, .........................................

  7. ................................., angelimwandikia mwalimu wake wiki iliyopita.

  8. Familia yake ingelikuwa na fedha za kutosha, ..........................................

  9. Maria angelinipatia shauri yake kuhusu uzalishajimali, ....................................

  10. ................................., angelipata kula zote za wachaguzi.

  Maelezo muhimu

  1. Kiambishi cha masharti –ngeli- huonyesha kuwa kitendo fulani hakijafanyika na kwa hiyo, jambo fulani halijatokea wala hakuna uwezekano wa kufanyika kwa kitendo hicho.

  2. Katika sentensi yenye kiambishi hicho -ngeli-, mzungumzaji hutilia mkazo kwamba wakati umepita na kuwa hakuna uwezekano wa wakati huo kurudia.

  3. Matumizi ya ngeli katika sentensi huashiria kwamba kutowezekana huko kwa tendo fulani huambatana na majuto fulani.

  Mifano: 

  a. Ningelijua, ningelichanjwa ili kujikinga na ugonjwa wa kifua kikuu.

         • Maana yake ni kuwa sikujua wala sikuchanjwa; kwa hiyo, niliambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu.

  7.4 Matumizi ya Lugha: Historia ya Kiswahili Nchini Rwanda na Mazoezi ya Jumla

  Zoezi la 7: Chunguzeni herufi zilizopo kwenye jedwali hapo chini ili muweze kuunda maneno yenye maana katika lugha ya Kiswahili na kuyatumia katika kutunga sentensi.

  Kwa mfano:

       Maoni

       Mwanafunzi huyu ana maoni muhimu kuhusu jambo hili

  Zoezi la 8: Someni kifungu cha mazungumzo kuhusu “Historia ya Lugha ya Kiswahili Nchini Rwanda” kisha muyaigize mbele ya darasa.

      • Maelezo muhimu kuhusu Historia ya Kiswahili nchini Rwanda

  Zoezi la 9: Chunguza maelezo yafuatayo ili kubainisha mambo muhimu yaliyozungumziwa

  Historia ya Kiswahili nchini Rwanda
  •  Lugha ya Kiswahili iliingia nchini Rwanda pamoja na Wajerumani walioingia nchini miaka ya 1890. Watu waliofuatana nao walikuwa wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili na waliweza kuwasaidia Wajerumani hao kama wapagazi na wakalimani wao. Shughuli za kiutawala, kidini na kiabishara nazo zilichangia kueneza lugha ya Kiswahili.
  •  Baada ya Vita vya Kwanza ya Dunia na kuanguka kwa utawala wa Ujerumani, Rwanda ilitawaliwa na Ubelgiji ambao ulihimiza matumizi ya Kifaransa kilichochukua nafasi ya lugha ya Kiswahili.
  •  Tangu zama hizo Kiswahili hakikupewa heshima kwani Wanyarwanda wengi walianza kukichukulia kama lugha isiyofaa kuzungumzwa na mtu yeyote mwenye mienendo myema. Lugha ya Kiswahili ilihusishwa na watu wenye tabia mbaya kama vile wadanganyifu na watu wasioweza kuaminika katika jamii
  •  Baada ya kupata uhuru, Kiswahili kilishughulikiwa hata kama mtazamo mbaya wa Wanyarwanda wengi kuhusu lugha ya Kiswahili uliendelezwa. Kwa mfano, tangu wakati huo, Kiswahili kilifundishwa katika shule za upili na chuo Kikuu Cha Rwanda. Vilevile, matangazo mengi katika Kiswahili yalipitishwa kwenye redio Rwanda ambapo vipindi mbalimbali viliweza kufurahisha walioweza kuelewa lugha hiyo.
  • Baada ya Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994, matumizi ya Kiswahili nchini Rwanda yaliwafanya Wanyarwanda wengi wabadilishe mtazamo hasi waliokuwa nao kuhusu lugha hiyo. Wao walianza kuiona kama lugha muhimu ya kuwaunganisha na raia wengine kutoka mataifa mengine jirani. Hali hii ilijibainisha wazi wakati ambapo Serikali ya Rwanda ilipoamua kujiunga na nchi nyingine katika Jamuiya Afrika Mashariki.
  •  Kwa sasa, Serikali ya Rwanda imeidhinisha kuwa Kiswahili kiwe lugha rasmi kando ya lugha nyingine rasmi zinazotumiwa nchini Rwanda. Shuleni kinafundishwa katika shule nyingi , Wanyarwanda wengi wanaendelea kufurahia hatua zilizopigwa na huzidi kukitumia katika kushirikiana na wananchi wengine katika shughuli zao za kibiashara, kidini, kisiasa, kitamaduni, na kadhalika.
  •   Kiswahili kimetoka mbali na kufanya safari yenye mabonde, kikapiga mbizi katika bahari ndefu na kuibuka na ushindi unaoshangiliwa na kila Mnyarwanda. Sisi sote tunakipigia makofi na kukitakia maendeleo imara. Tuendelee kukipenda kama lugha yenye kuimarisha umoja wa Waafrika wote.

  7.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

  Zoezi la 10: Kwa kuzingatia hoja muhimu kuhusu lugha ya Kiswahili nchini Rwanda, jadili kuhusu “Historia ya lugha ya Kiswahili nchini Rwanda”. Mazungumzo yenu yazingatie:

  1. Wageni walioleta Kiswahili nchini Rwanda.

  2. Watu mbalimbali waliojihusisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

  3. Matatizo yaliyojitokeza kukwamisha maendeleo ya lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

  4. Hali ya kisasa ya lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

  7.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

  Zoezi la 11: Tunga kifungu cha habari chenye mada ifuatayo: “Umuhimu wa Lugha ya Kiswahili kwa Wanyarwanda.”

  Muhtasari wa Mada

  Mada hii ya kwanza “Lugha ya Kiswahili” ina vipengele saba yaani masomo sita yanayohusiana na mada husika. Somo la kwanza linaeleza maana ya lugha kama chombo cha mawasiliano. Somo la pili linashughulikia umuhimu wa lugha na kusema kwamba lugha ni mojawapo ya vipengele vya utamaduni wa jamii na tena ni chombo cha utamaduni. Somo la tatu na la nne yanatoa maelezo kuhusu matumizi ya lugha katika jamii na kuonyesha faida na hasara ya kutumia lugha moja kwa kusema kuwa lugha kama chombo muhimu katika jamii hufanikisha na kurahisisha mawasiliano miongoni mwa watumiaji wake na umuhimu wa kutumia lugha moja ni kukuza umoja, ushikamano, ushirikiano, na amani miongoni mwa wanajamii wanaotumia lugha hiyo. Hasara ni kuwa wanajamii hawawezi kuwasiliana na ulimwengu mzima. Somo la tano na la sita yanaeleza kwamba chimbuko la Kiswahili ni pwani ya Afrika Mashariki na lugha hiyo ilienea kwa kupitia shughuli mbalimbali kama vile safari za kibiashara baina ya watu kutoka pwani hadi bara, uandishi wa vitabu vya Kiswahili, n.k. Somo la saba linaonyesha kwamba lugha ya Kiswahili nchini Rwanda ilifanya njia ndefu kutoka mwaka 1890 mpaka leo. Sasa hivi ni lugha rasmi ya kuheshimiwa nchini Rwanda.

  Kila kipengele kinaundwa na vipengele vidogo vidogo kama vile maswali ya ufahamu, msamiati, matumizi ya lugha na sarufi.

  TATHMINI YA MADA YA KWANZA

  Jibu maswali yafuatayo:

  1. Onesha asili ya lugha ya Kiswahili, kisha eleza shughuli zilizochangia kuenea kwake katika sehemu mbalimbali ulimwenguni.

  2. Kwa kutumia viambishi nge, ngali na ngeli, tunga kifungu cha habari chenye kuzingatia mambo muhimu yafuatayo :

          a. Nafasi ya lugha ya Kiswahili nchini Rwanda

          b. Umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa Wanyarwanda

          c. Shughuli za kuimarisha na kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini Rwanda  • MADA NDOGO: FASIHI KATIKA KISWAHILI

   Uwezo upatikanao katika mada: Kuelewa fasihi katika Kiswahili kwa ujumla kama

   sanaa inayoshughulikia jamii kwa kurahisisha mawasiliano ndani yake; kutumia

   kwa ufasaha majina ya ngeli ya LI-YA

   Malengo ya mada

   Baada ya mada hii, mwanafunzi atakuwa na uwezo wa:

   • Kufasili maana ya sanaa.

   • Kufasili maana ya fasihi.

   • Kuhusisha fasihi na sanaa.

   • Kueleza umuhimu wa fasihi katika jamii.

   • Kutofautisha tanzu za fasihi simulizi na fasihi andishi.

   • Kutunga sentensi zenye majina ya ngeli ya Li-Ya pamoja na vivumishi.

   Kidokezo

   1. Eleza nafasi ya lugha katika mawasiliano.

   2. Unaelewa nini kuhusu usemi ufuatao: Asiyesikia la mkuu huvunjika guu ?

   3. Andika usemi mwingine unaofanana na usemi huo katika lugha ya

   Kinyarwanda.

   4. Tafuta semi nyingine tatu katika lugha ya Kiswahili na kueleza maana zake.

   5. Semi kama hizo huitwa vipi katika lugha ya Kiswahili?

   6. Kwa kuchunguza maneno yaliyotumiwa, linganisha sifa za semi hizo na

   maelezo yake

   7. Unelewa nini kuhusu maneno yafuatayo:

   a. sanaa 

   b. fasihi

   SOMO LA 8: DHANA YA SANAA


   Zoezi la 1: Tazama mchoro hapo juu na kutoa maoni yako kuhusu shughuli

   zinazopatikana. Maoni yako yatajibu maswali yafuatayo:

   1. Wahusika wanaopatikana kwenye mchoro huo wanafanya nini?

   2. Wahusika hao ni nani (husisha na kazi zao)

   3. Shughuli zao zina umuhimu gani kwa jamii?

   8.1 Kusoma na Ufahamu: Sanaa na Manufaa Yake

   Soma kifungu cha habari kuhusu Sanaa na manufaa yake, kisha jibu maswali

   yaliyotolewa hapo chini

   Sanaa ni kazi ya ustadi na ufundi wowote wa kuibusha mawazo yaliyomo katika akili ya binadamu na kuyaonesha kwa njia mbalimbali. Mtu hueleza hisia zinazomgusa kwa kutumia umbo fulani ambalo limesanifiwa. Kazi yoyote ya sanaa inategemewa ioneshe ufundi wa hali ya juu ili iwe na mvuto kwa hadhira  yake. Kazi yoyote ya sanaa inapaswa kuwa na sifa tatu muhimu: uzuri, upya na ujumbe.

   Sanaa ni za aina mbalimbali. Kuna sanaa za uoneshi ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa, hivi kwamba uzuri wake ukaendelea kupatikana wakati wowote ule. Hizi ni kama uchongaji, uchoraji, ufinyanzi, ufumaji, ushonaji, ususi na kadhalika. Tena kuna sanaa za vitendo ambazo uzuri wa sanaa hizi umo katika umbo la vitendo hivyo, ilimradi kuupata uzuri huo ni lazima kutazama vitendo vinavyofanyika au ukasikiliza yale yanayosimuliwa kama vitendo vyenyewe ni vya kimasimulizi. Sanaa hizi ni kama zile zinazoambatana na ngoma, utambaji, masimulizi na kadhalika.

   Wanyarwanda na Waafrika kwa ujumla wanasifiwa kwa kuwa na sanaa mbalimbali zinazowapendeza watu wengi. Miongoni mwa wasanii ambao hupendwa zaidi ni pamoja na wale wenye ustadi wa kuzingatia mfumo wa kijadi wa Kiafrika na wengine wanaotumia mbinu za kiteknolojia za kisasa. Hawa wote lengo lao ni kuendeleza jamii katika nyanja mbalimbali za maisha yake. Wao hutajirika kupitia shughuli zao za kisanaa ambazo huwaletea pato kubwa kila mwezi. Nchini Rwanda, wasanii wengi hujiunga katika vyama vya ushirika vyenye kuzalisha mali ambavyo huwanufaisha kwa namna tofauti. Mfano mzuri ni vyama vinavyopatikana katika maeneo mengi yaliyojengwa ili kurahisisha shughuli zao za kisanaa. Majengo hayo yanayojulikana kwa jina “AGAKIRIRO.” Aidha, yamejengwa katika sehemu mbalimbali za wilaya zote ili kurahisisha shughuli zinazofanywa na wasanii na kukuza vipaji vyao kiasi kwamba mafanikio na manufaa yao hayakadiriki.

   Muhire ni kiongozi wa Chama cha Ushirika cha Wafinyanzi ambao hupatikana katika sehemu moja ya wilaya ya Nyarugenge. Yeye huongoza vizuri chama chake na wanachama wote humpenda sana kwani yeye hujitolea sana kwa maendeleo ya chama chao. Yeye huwahimiza wanachama wote waungane na wadumishe ushirikiano kati yao ili pato lao liweze kuongezeka. Katika kazi zao, wao hutumia udongo maalumu wa kutengeneza vyungu vya kupikia, vyungu vya maua, mitungi, sanamu mbalimbali kama vile sanamu za watu walioacha vitendo muhimu katika jamii, mashujaa, ndege, wanyama na kadhalika. Udongo huu unaotumiwa unajulikana kwa wafinyanzi wote kuwa ni bora kwa shughuli zao kwani unanata na kushikana kwa urahisi. Ni udongo wenye umbile laini kiasi kwamba wateja wao hupenda bidhaa zao.

   Muteteri ni kiongozi wa shirika kubwa la maseremala ambao hutengeneza samani za kupendeza kwa kutumia mbao  : viti, vitanda, makochi, meza, madawati, makabati, na kadhalika. Wao hutengeneza pia milango na madirisha mazuri ya nyumba. Mara nyingine, kazi zao hufanyiwa nje ya karakana yao kwani watu wengi huwaita kuwatengenezea mapaa ya nyumba zao kwa kutumia miti na mbao za aina mbalimbali. Katika kazi zao maseremala hawa huhitaji misumeno, misumali, nyundo, randa, patasi, kekee na kadhalika. Licha ya kazi hii kuonekana kuwa ni ya kiume, Muteteri na wanawake wenzake hawana tabu ya kuifanya wakishirikiana na wanaume.

   Kazi hizi zote huwaingizia maseremala hawa kipato kikubwa sana kiasi kwamba mwaka uliopita waliweza kujinunulia gari kubwa la kuwabebea mbao kutoka maeneo mengi ya nchi ya Rwanda. Muteteri binafsi ameshakamilisha jengo la kifahari mjini Kigali ambalo nalo linamletea faranga nyingi kila mwezi.

   Mujyambere yeye ni msusi. Pamoja na wenzake kazi yao ni kutengeneza nywele za wanawake kwa kutumia mafuta, nyuzi na hata nywele bandia. Chama chao cha Ushirika kinachoitwa DUFATANYE kinaundwa na vijana wa kiume na wa kike walio na umri kati ya miaka 20 na 35. Wao hupendwa sana na kina mama kwa sababu wanaimudu vizuri kazi yao. Kila binti anayejiandaa kwa sherehe yoyote kama vile kufunga pingu za maisha ni lazima awaendee ili wamrembeshe ipasavyo.

   Manufaa yanayotokana na kazi za sanaa ni mengi mno. Mutesi na Kiza wao ni wapishi maarufu katika mgahawa mmoja upatikanao mjini Musanze. Kila asubuhi mgahawa huu hujaa wateja tele kwa sababu ya vitafunio na vyakula vinavyoandaliwa kwa usimamizi wao. Mutesi husimamia upishi wa kinyarwanda, naye Kiza husimamia upishi wa kizungu. Watu wengi wanaofika katika mgahawa wao hufurahia chakula wanachopewa pale. Viongozi wa hoteli nyingi maarufu mjini Kigali walitaka kuwaajiri lakini bosi wao akawapandishia mshahara ili wasimponyoke.

   Miongoni mwa wasanii maarufu wanaopata faida kubwa hatuwezi kusahau Agasaro na Mugemana. Wao ni walemavu wa miguu lakini wanaongoza Chama cha Ushirika cha wahunzi kinachopatikana mjini Rubavu. Agasaro ndiye Mkuu wa shirika hilo naye Mugemana Makamu wake. Kazi wanayoifanya pamoja na wanachama wenzao ni kufua madini ya chuma na bati kwa kutengeneza vifaa mbalimbali kama mashoka, panga, visu; mikuki na mishale ya kupambwa nyumbani. Madini haya yakikosekana wao hutumia vyuma vilivyozeeka. Katika kazi yao wahunzi hawa huwasha moto na kuingiza chuma ndani. Chuma hiki kikipata moto wao hukiweka juu ya fuawe na kukipigilia kwa kutumia nyundo hadi kikawa na sura ya kifaa wanachohitaji.

   Mbali na sanaa hizo zilizotajwa hapo juu, kuna sanaa nyingine zenye malengo ya kuburudisha, kustarehesha na kuelimisha wanajamii. Mathalani mwanamziki Kabeja ambaye anajulikana kwa nyimbo zake nzuri za kumsifu na kumtukuza Mungu. Bendi yake huimba nyimbo za aina mbalimbali: Nyimbo za kidini, za mapenzi, za kisiasa na nyingine za kijamii. Nyimbo hizi huwatumbuiza mashabiki wao kwa sauti zao laini na zenye mvuto na midundo inayowafurahisha watu wengi. Kila mwishoni mwa wiki wao hupanga tamasha kubwa ambapo bendi yao huimba nyimbo nzuri na kusimulia mashairi kwa watazamaji wao. Licha ya kazi hizi, bendi hii ina tena uzoefu wa kucheza michezo ya kuigiza. Katika kazi yao bendi hii hutumia ngoma, gitaa, zumari, marimba, tarumbeta na kadhakila. Kundi hili hualikwa tena katika sherehe mbalimbali na kutoka likiwa na kitita cha fedha.

   Kweli, kazi za sanaa ni nyingi na wasanii wengi hupata mafanikio mengi wanapofanya kazi zao kwa bidii. Wao huwa na nafasi kubwa katika jamii kwani ndio wanaoisaidia kutosheleza baadhi ya mahitaji yao muhimu katika maisha yao ya kila siku. Kutokana na umuhimu wao, Serikali ya Rwamda huwahimiza Wanyarwanda wote kufanya kazi mbalimbali kwa ubunifu katika mradi “Fanya kazi ujitegemee”. Ili kufikia lengo lake, sheria imewekwa kwa kulinda kazi zinazobuniwa na wasanii ili zisiigwe, kunakiliwa, kuingiliwa au kuibiwa na wenye hamu ya kula jasho la wengine. Wasanii wengi wameshaelewa umuhimu wa kujiweka pamoja na kushirikiana katika vyama mbalimbali vya kuzalisha mali kupitia sanaa zao. Wao hufikiria kama wahenga waliosema “jifya moja haliteleki chungu.”

   Maswali ya ufahamu

   1. Sanaa ni nini ?

   2. Kazi yoyote ya sanaa huwa na sifa zipi?

   3. Taja majina ya wasanii wanaosimuliwa katika kifungu hiki na kueleza kazi zao?

   4. “Ulemavu si ugonjwa.” Jadili msemo huu kwa kuhusisha na yale uliyoyasoma

   katika kifungu cha habari hapo juu.

   5. Unaelewa nini kuhusu methali isemayo “Jifya moja haliteleki chungu“?

   6. Kwa sababu gani wafinyanzi hawatumii udongo wowote?

   7. Kwa sababu gani Serikali ya Rwanda inawahimiza mafundi wengi kujiunganisha

   katika vyama vya Ushirika vya kuzalisha mali?

   8. Ni ushauri gani unaoweza kuwatolea vijana wengi wanaokaa bila kazi?

   9. Toa mifano miwili inayodhihirisha kuwa sanaa ni shughuli muhimu katika jamii.

   10. Taja mambo yaliyofanywa na Serikali ya Rwanda ili kuimarisha vipaji vya

   wasanii na kulinda kazi zao. 

   8.2 Msamiati Kuhusu Maana ya Sanaa

   Zoezi la 2: Andika maana za maneno haya yafuatayo kulingana na matumizi

   yake katika kifungu cha habari hapo juu, kisha tunga sentensi moja kwa

   kutumia maneno hayo.

   1. Ustadi

   2. Umbo

   3. Karakana

   4. Kuburudisha

   5. Chama

   6. Shabiki

   7. Madini

   8. Kutumbuiza

   9. Fuawe

   10. Sonara

   Zoezi la 3: Eleza maana ya maneno au vifungu vya maneno vilivyopigiwa

   mstari au tumia neno moja tu linaloelezea maelezo yanayofanuliwa na fungu

   lilolipigiwa mstari katika sentensi zifuatazo.

   1. Alijijengea nyumba ya kifahari mjini Kigali.

   2. Waafrika hawa wanajigamba kwa kuwa wana wasanii wengi.

   3. Kagabo ni mtu anayesuka nywele za wanawake.

   4. Nyirasafari aliongezewa fedha kwa mshahara.

   5. Musoni alipewa kazi.

   6. Mugeni ni kiongozi mkuu wa shirika la wavuvi naye Kalisa ni Msaidizi wake.

   7. Alipoingia katika polisi alijiunga na kundi la wanamuziki.

   8. Figa moja haliteleki chungu.

   9. Methali nyingi zilitokana na watu wa kale.

   10. Kazi nyingi za sanaa huwaletea wasanii fedha nyingi.

   Zoezi la 4: Jadili kuhusu vifaa vilivyomo katika sehemu A ili uvihusishe na mafundi wanaovitumia katika sehemu B


   8.3 Sarufi: Nomino za Ngeli ya LI-YA

   Zoezi la 5: Chunguza sentensi zifuatazo na kuandika viambishi nafsi

   vinavyopatikana katika vitenzi; kisha utunge sentensi nyingine tano zenye

   viambishi hivyo.

   1. Kundi la wanamuziki liliwatumbuiza watu jana.

   2. Mashirika haya yaliundwa na vijana mbalimbali.

   3. Koti hilo limeshonwa na mshonaji hodari.

   4. Makabati yalitengenezwa na maseremala.

   5. Gari zuri lile lilitengenezewa nchini Rwanda.

   Zoezi la 6: Andika nomino hizi katika wingi, kisha ueleza kile ulichokigundua.

   Umoja               Wingi

   1. Kabati       .....................................................

   2. Koti          .....................................................

   3. Bega        .....................................................

   4. Goti         .....................................................

   5. Panga     .....................................................

   6. Janga      .....................................................

   7. Jangwa    .....................................................

   8. Jina          .....................................................

   9. Jibu         .....................................................

   10. Jembe

   Zoezi la 7: Tunga sentensi zako katika umoja na wingi kwa kutumia nomino

   hapo juu katika zoezi la saba.

   Maelezo muhimu

   • Vitenzi vilivyomo katika sentensi hapo juu, vinatumia viambishi nafsi LI-YA

   • Matumizi ya viambishi hivi LI-YA yanategemea nomino zilizotumiwa katika

   sentensi hizo.

   • Nomino hizo zikiwa katika umoja kitenzi huchukua LI; zikiwa katika wingi

   kitenzi hutumia YA.

   • Nomino zilizopendekezwa katika umoja huchukua wingi wake kwa kuongeza

   ma- kwa jina hilo:   Zoezi la 8: Tunga sentensi tano zenye nomino zisizoweza kuingizwa katika umoja na ambazo zinatanguliwa na kiambishi ma-.

   Zoezi la 9: Andika sentensi zifuatazo katika umoja au wingi.

   1. Mimi nina lengo la kupambana na jangwa.

   2. Wewe utaondoa majani hayo makavu.

   3. Majani yalikauka.

   4. Shavu linaniuma.

   5. Kijana mrefu alibeba kasha kwenye bega.

   6. Debe hilo linavuja kwa sababu limetoboka.

   7. Watoto watano walilazwa hospitalini kwa sababu ya matatizo ya mapafu.

   8. Madaftari yanapaswa kuhifadhiwa vizuri.

   9. Tarumbeta lilitumiwa wakati wa burudani.

   10. Shirika la reli liliagiza garimoshi kubwa.

   8.4 Matumzi ya Lugha: Dhana ya Sanaa 

   Zoezi la 10: Soma maelezo yafuatayo kuhusu sanaa, kisha ujibu maswali

   yaliyotolewa hapo chini

   Sanaa ni ufundi wa kuwakilisha mawazo na hisia alizo nazo binadamu kwa njia ya ubunifu. Njia hizo zaweza kuwa wimbaji, uchoraji, ushonaji, ujenzi, ufinyanzi, masimulizi na kadhalika. Njia hizi tofauti ndizo zinatufanya tuwe na aina mbalimbali za sanaa. Kwa hivyo, kulingana na njia zilizotajwa hapa, ni dhahiri kwamba tutapata sanaa ya uimbaji, sanaa ya uchoraji, sanaa ya ujenzi, sanaa ya ufinyanzi, na kadhalika. Mtu anayeshughulikia sanaa huitwa msanii.

   Kila kazi ya sanaa inapaswa kuonyesha uzuri wa aina yake. Uzuri huu waweza kuonekana, kuguswa, kusikiwa au kuonjwa kulingana na aina ya sanaa inayohusika. Pia kazi ya sanaa inapaswa kuwa na upya. Upya ndio unaotofautisha sanaa za msanii fulani na za wenzake. Kisha kazi ya sanaa inapaswa kuwa na ujumbe. Kusema kuwa kazi ya sanaa inapaswa kuwa jambo fulani inalowasilisha katika jamii.

   Kila kazi ya sanaa ina nyenzo au zana zinazotumiwa kwa kufanikisha kazi hiyo. Kwa mfano mfinyanzi huhitaji udongo, mchongaji hutumia mawe au miti na sonara hulazimika kuwa na madini.

   Swali:

   1. Kwa ushirikiano na wenzako, jadilieni kuhusu umuhimu na nafsi ya sanaa katika

   maisha ya jamii. Mjadala wenu uzingatie:

   a. Maana ya sanaa

   b. Sifa za kazi ya sanaa

   c. Kazi mbalimbali za sanaa na umuhimu wake kwa wanajamii

   2. Taja aina moja ya sanaa na kujadili kuhusu namna ambavyo wasanii huweza

   kutimiza masharti yanayopatikana katika kazi yoyote ya kisanaa: uzuri, ujumbe

   na upya.

   Aina za sanaa

   Chunguza kwa makini maelezo yafuatayo kuhusu aina za sanaa na zana zake

   • Sanaa ni ufundi wowote wa kufichua mawazo yaliyomo katika akili na

   kuyaonyesha kwa njia mbalimbali.

   • Kuna sanaa za uonyesho (kama uchoraji, uchongaji, ususi, uhunzi, usonara,

   maandishi na kadhalika) na sanaa za vitendo (kama ngoma, masimulizi,

   utambaji na kadhalika).

   • Kazi zote za sanaa zinapaswa kuwa na uzuri, upya na ujumbe.

   • Kila kazi ya sanaa ina zana zake kama vinavyoonekana kwenye kielelezo

   kifuatacho (kinachoonyesha mifano ya sanaa):

   8.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

   Zoezi la 11: Kwa ushiririkiano na wenzako, jadilieni kuhusu Umuhimu wa vyama vya Ushirika vyenye kuzalisha mali kama mojawapo ya njia za kuondoa tatizo la ukosefu wa kazi pamoja na uzururaji miongoni mwa vijana.

   8.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

   Zoezi la 12: Tunga kifungu kuhusu mada ifuatayo: “Uwasilishaji wa Mawazo ya

   Binadamu ni wa Njia Nyingi Mno.”


   SOMO LA 9: DHANA YA FASIHI


   Zoezi la 1:Chunguza kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yafuatayo:

   1. Eleza wahusika unaowaona kwenye picha hii.

   2. Wahusika hao wako wapi?

   3. Eleza shughuli zinazoendelea kwenye mchoro huo. 

   9.1 Kusoma na Ufahamu: Dhana ya Fasihi

   Soma kifungu cha habari kuhusu dhana ya fasihi, kisha jibu maswali yaliyotolewa hapo

   chini. 

   Jumatatu moja mwalimu wetu wa Kiswahili aliingia darasani. Alikuwa na kikapu begani na madaftari matatu mkononi. Kama kawaida alitusalimia huku akitabasamu. Wanafunzi wote katika madarasa matano ya mchepuo wa lugha tulimpenda sana kwani alikuwa mwalimu mwerevu, mzuri na mpole. Tena aliheshimu watu wote na wote wakamheshimu. Wakati huo nami nilikuwa nikisoma katika kidato cha nne, mkondo wa lugha. Somo la siku hiyo lilikuwa somo la pili kati ya masomo ya sanaa ya lugha.

   Mwalimu wetu alipoanza somo alituuliza kwanza maswali kuhusu maana ya sanaa na tulimjibu vizuri kwa kutoa mifano mingi aliyoifurahia. Somo la sanaa ndilo lililokuwa limefunga muhula wa kwanza na wakati huo tulikuwa tumeanza muhula wa pili. Mwalimu aliendelea na somo jipya ambalo liliwavutia wanafunzi wote darasani. Sote tulikuwa na vitabu vya Kiswahili vya mwanafunzi na kila mwanafunzi alikuwa amefungua kitabu chake.

   Mwalimu alituomba tuunde makundi ili tusome kifungu kimoja kuhusu dhana ya fasihi na umuhimu wake katika jamii. Baadaye, aliomba makundi yote kujiandaa kwa kazi yao. Kila kundi lilipewa dakika kumi na tano za kuwasilisha mbele ya wanafunzi wengine kuhusu mambo muhimu yaliyojadiliwa katika kundi lao. Makundi yote yalikuwa yamejitahidi kufanya kazi vizuri. Sote darasani tulielewa vizuri dhana ya fasihi kwamba fasihi ni sanaa ya lugha ambayo hushughulikia masuala yanayomhusu binadamu. Makundi yote yaligundua kwamba fasihi huzungumzia na kuonyesha maisha ya jamii, kwa kuelezea mambo yote yaliyomo katika jamii hiyo.

   Matatizo, mitazamo, migogoro, itikadi, na shughuli mbalimbali za kijamii zilizopo huwa ni mambo yanayobainishwa katika kazi ya fasihi; yaani sanaa ambayo hutumia lugha. Vile vile, wanafunzi wote walielewa kuwa kila mtu anayejishughulisha na utunzi wa kazi ya fasihi hulenga kudhihirisha hisia alizo nazo kulingana na mazingira anamoishi. Yeye huitazama jamii yake na kueleza yote yatendekayo katika jamii hiyo kwa njia ya lugha.

   Makundi yote yalipomaliza kuwasilisha, mwalimu wetu alisisitiza kwamba fasihi hutumia lugha kisanaa na kuwa sanaa hiyo huwavutia wengi. Katika hali hii alisema kuwa malengo ya fasihi ni kuelimisha wanajamii, kuwaburudisha na kuwastarehesha. Yeye alieleza kwamba fasihi huwaonya wanaotenda maovu kuacha maovu yao, na kuwahimiza wanaotenda mema kuendeleza matendo yao mazuri. Haya yote yanayozungumziwa katika fasihi hudhihirisha jinsi fasihi ni kioo cha jamii na mwavuli wake.

   Fasihi huilinda jamii kwa kuhifadhi na kueleza vitendo vyake ambapo vitendo vizuri huhimizwa na kuchochewa ilhali vitendo vibaya hukatazwa. Msanii ambaye ni mwanafasihi huitumia lugha fulani kwa kujulisha jamii mengi yaliyomo katika utamaduni wake. Somo hilo lilitupendeza wote kiasi kwamba tuliamua kujifunza vizuri lugha ya Kiswahili ili tuweze kuitumia lugha hii kisanaa.

   Leo wanafunzi wengi tuliosoma pamoja enzi hizo tunajishughulisha na kazi mbalimbali za kisanaa zinazotumia lugha ya Kiswahili. Baadhi yao ni waimbaji, watunzi wa mashairi na waandishi wa vitabu kama mimi. Kila mwaka tunakutania katika maonyesho ya kitamaduni na huwa tunapata faranga nyingi.

   Maswali ya Ufahamu 

   1. Kifungu cha habari hiki kinazungumzia nini?

   2. Taja sifa za mwalimu anayezungumziwa katika kifungu cha habari.

   3. Taja mambo matano yanayoweza kugusiwa katika kazi ya fasihi.

   4. Kwa nini wanafunzi waliamua kujifunza vizuri lugha ya Kiswahili?

   5. “Fasihi hutumia lugha kisanaa”. Eleza.

   6. Ni namna gani fasihi huweza kutumiwa kama njia ya kufundisha jamii?

   7. Fasihi ni kioo na mwavuli wa jamii. Eleza.

   8. Fasihi inahusianaje na utamaduni ?

   9. Msimulizi anafanya nini kwa sasa?

   10. Katika mistari mitano, eleza maana ya fasihi na umuhimu wake katika jamii. 

   9.2 Msamiati Kuhusu Dhana ya Fasihi

   Zoezi la 2: Tunga sentensi kwa kutumia maneno haya:

   1. Hisia

   2. Kuvutia

   3. Mtendamaovu

   4. Kuburudisha

   5. Kudhihirisha

   6. Kuhimiza

   7. Kioo

   8. Mwavuli

   9. Mwanafasihi

   10. Kuchochea

   Zoezi la 3: Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno yanayofuata:

   sanaa, mwanafasihi, jamii, utamaduni, imani, mtazamo, wanajishughulisha,

   fasihi, maovu, waliamua.

   1. ............................... anatarajiwa kutumia vizuri vipaji vyake vya kisanaa.

   2. Sote tunalazimika kukuza ................................... wa usafi katika kazi.

   3. Mimi nitaendelea na masomo ya ..................................... chuoni.

   4. ................................... wake kuhusu michezo shuleni ni tofauti na ule wa mkurugenzi.

   5. Fasihi kama ................................ inaweza kumpa mtu faida na kumtunza.

   6. Baada ya majadiliano marefu ....................................... kusikilizana kwa ajili ya kuishi

   kwa amani kati yao.

   7. Kila mwanadamu anatarajiwa kuepuka mambo .............................

   8. Watu wengi ambao tuliosoma pamoja ........................ na kazi mbalimbali za kisanaa

   wakitumia lugha ya Kiswahili.

   9. Ninapenda ........................ yetu ya Rwanda kwani inapiga marufuku ubaguzi

   wowote.

   10. Ndugu zangu wana ................................... kwamba watamaliza masomo yao na

   kuwa wasanii maarufu.

   9.3 Sarufi: Matumizi ya Vivumishi vya Idadi Katika Ngeli ya LI-YA

   Zoezi la 4: Soma kifungu cha habari hapo juu kuhusu “Dhana ya fasihi” huku

   ukiandika vivumishi vya idadi vilivyotumiwa.

   Zoezi la 5:Andika sentensi zifuatazo kwa kutumia vivumishi vilivyomo ndani ya

   mabano.

   1. Mawe .................... yamewekwa kando ya barabara (tatu).

   2. Madirisha ........................... yamefunguliwa. (tano)

   3. Meno ...................... yameng’oka. (mbili)

   4. Matunda ....................... yameiva. (nane)

   5. Mabega ........................................ (nne)

   6. Madarasa .............................. (tatu)

   7. Taja mambo ............................ yanayozingatiwa katika kazi ya fasihi. (tatu)

   8. Makoti ................................... yameuzwa na mfanyabiashara huyu. (tano)

   Maelezo muhimu

   • Katika matumizi ya ngeli ya li-ya na vivumishi vya idadi, tarakimu mbili

   ambayo hugeuka -wili, tatu, nne, tano pamoja na nane huchukua kiambishi

   ma- katika wingi. Vivumishi hivyo huwa mawili, matatu, manne, matano, na

   manane

   Zoezi la 6: Chunguza sentensi zifuatazo, kisha ueleze muundo wa vivumishi

   vilivyotumiwa.

   1. Jibu moja limepatikana.

   2. Mawe sita yameanguka chini.

   3. Matunda saba yameiva.

   4. Madarasa tisa yanasafishwa.

   5. Makoti kumi yatashonwa.

   Kinyume na matumizi ya ngeli ya li-ya na vivumishi vya idadi tulivyoona hapo juu,

   tarakimu, sita, saba, tisa na kumi havichukui kiambishi ma- katika wingi. Vivumishi

   hivyo hubaki vile vilivyo yaani, sita, saba, tisa, na kumi.

   Nomino za ngeli “li-ya” huweza kutumiwa na vivumishi vya idadi ya jumla /isiyo kamili / isiyo dhahiri:

   Kwa mfano: 

   Matendo mengi mazuri yamefanywa na watu hawa

   Zoezi la 7: Chunguza mifano mingine ya vivumishi vya idadi isiyo dhahiri ya

   ngeli ya “li-ya”, kisha utunge sentensi zenye vivumshi hivyo.

   1. Macho machache yanatazama majigambo ya watoto

   2. Katika kongamano la Kiswahili mambo mengi ya kuendeleza lugha hiyo

   yaligusiwa

   3. Makundi kadhaa ya wanafunzi yanawatembelea wagonjwa hospitalini.

   4. Gari langu linateleza sana kwa sababu maji tele yanajaa barabarani.

   5. Mawese kidogo yananunuliwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

   Zoezi la 8: Kamilisha tungo zifuatazo kwa kutumia vivumishi vya idadi: toka

   moja hadi arobaini (Andika katika maneno)

   1. Kanuni za Mungu ni ........................

   2. Mwaka una miezi .............................

   3. Ni rahisi kujua kwamba wiki moja ina siku .....................

   4. Watu wa zamani walipika kwa kuweka chungu juu ya mafiga ...........................

   5. Wanyarwanda huwapa majina watoto wao katika siku ya ...................................

   6. Nchi ya Rwanda ina majimbo/ mikoa.........................

   7. Nchi yetu inapakana na nchi........................

   8. Dunia ina mabara............................

   9. Rwanda ina milima ya volkeno..................

   10. Katika mchezo wa soka, timu moja inakuwa na wachezaji ...................uwanjani.

   11. Siku moja ina saa...........................

   9.4 Matumizi ya Lugha: Dhana ya Fasihi

   Zoezi la 9: Kwa kushirikiana na wenzako, someni kwa makini maelezo

   yafuatayo kisha mjibu maswali hapo chini.

   • Fasihi ni sanaa ya lugha, inayoshughulikia masuala yanayomhusu binadamu: matatizo

   yake, ndoto zake, matumaini yake, migogoro yake na mazingira yake.

   • Fasihi kama sanaa huwasilisha ujumbe unaohusu maisha ya jamii kwa kutumia lugha.

   • Kwa kutoa maudhui yake, fasihi inatumia lugha; yaani maneno ambayo hutamkwa au

   huandikwa, lugha ambayo ni sehemu ya utamaduni.

   • Msanii ambaye ni mwanafasihi hutumia maneno hayo kwa namna yake ili kuwakilisha

   fikra na mtazamo wake kuhusu jamii na mazingira yake. 

   • Fasihi hutumiwa kama chombo cha kuelezea, kulinda na kuhifadhi utamaduni wa

   jamii; yaani fasihi humulika na kuonyesha yote yanayotendeka katika jamii. Katika

   hali hii, fasihi hutumiwa kama njia ya kuelimisha, kuonya na kurekebisha jamii kwa

   kutumia lugha. 

   Maswali:

   1. Fafanua dhana ya fasihi?

   2. Toa mifano ya kazi za fasihi unazozifahamu.

   3. Mwanafasihi hutumia zana zipi katika kazi zake za kifasihi.

   4. Maudhui ya fasihi huhusu nini?

   5. Toa maelezo muhimu kuhusu tanzu za fasihi.

   Zoezi la 10: Ukishirikiana na wenzako, chunguzeni maelezo yafuatayo kuhusu

   fasihi na tanzu zake, kisha mjibu maswali hapo chini.

   • Fasihi ni sanaa muhimu ya matumizi ya lugha inayohusiana na tungo za sanaa:

   mashairi, tamthilia, misemo, hadithi, vitendawili, nahau na kadhalika.

   • Tungo hizi za kisanaa huwasilishwa kwa maneno teule ambayo yanaweza kuandikwa

   au kusimuliwa kwa mdomo.

   • Sanaa ya kifasihi inatokana na ubingwa, ufundi na ufasaha wa kuwasilisha mawazo

   kwa kuonyesha hali halisi ya maisha ya binadamu:

   • Furaha, huzuni, matatizo na mengine huelezewa katika fasihi kwa njia hiyo ya

   kisanaa; yaani kwa kutumia maneno yaliyoteuliwa.

   • Fasihi hutumia fani au ufundi fulani katika masimulizi au maandishi kwa lengo la

   kuwasilisha maudhui fulani yanayolingana na nia ya mwanafasihi:

   • Mwimbaji anatumia maneno fulani yenye kuwasilisha picha anayotaka kuieleza;

   kama ni mtunzi wa mashairi anachagua lugha au maneno yenye kuelezea maudhui

   au mawazo anayotaka kuzungumzia na kuelezea hadhira yake; yaani wale

   anaowasiliana nao kupitia kazi yake ya kisanaa.

   • Kimsingi, fasihi hugawanyika katika tanzu mbili kuu: Fasihi simulizi na fasihi andishi.

   • Uainishaji wa makundi haya hutegemea njia zinazotumiwa kwa kutunza na

   kuhifadhi, kuwasilisha, kupokezana na nyenzo za kazi za kifasihi zinazohusika katika

   uainishaji huo.

   • Fasihi simulizi hutegemea zaidi usemi kuliko fasihi andishi.

   • Fasihi andishi hutegemea zaidi maandishi kwa kiasi kikubwa.

   • Tofauti hii inajibainisha wazi, lakini huwa tunaweza kuipata fasihi andishi iliyopewa

   sura ya usimulizi na fasihi simulizi iliyopewa sura ya kimaandishi au iliyowasilishwa

   kimaandishi. 

   Jibu maswali yafuatayo:

   1. Eleza tungo za kisanaa zilizozungumziwa katika maelezo hapo juu.

   2. Tungo hizo huwasilishwa kwa kutumia nini?

   3. Unaelewa nini na:

   a. Fani

   b. Maudhui

   c. Hadhira

   4. Uainishaji wa kazi za fasihi unategemea nini?

   5. Taja na kueleza tanzu kuu za fasihi.

   6. Kuna tofauti gani kati ya tanzu hizo za fasihi?

   7. Toa mifano ya kazi unazozifahamu kwa kila utanzu wa fasihi

   9.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

   Zoezi la 11: Ukishirikiana wa wenzako, jadilieni kuhusu “Uhusiano kati ya fasihi

   na kazi nyingine za kisanaa.”

   9.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

   Zoezi la 12:Tunga kifungu cha habari kwa kutumia kichwa kifuatacho (maneno

   yasiyopungua mia moja): “Fasihi ni kioo cha jamii”

   SOMO LA 10: DHIMA YA SANAA KATIKA JAMII


   10.1 Kusoma na Ufahamu: Sanaa katika Jamii

   Soma kifungu cha habari kuhusu “Sanaa katika jamii”, halafu jibu maswali yaliyotolewa

   hapo chini

   Mwishoni mwa mwezi Oktoba wa kila mwaka, viongozi wetu hutoa tangazo la kuwaalika vijana wote kutoka tarafa zetu ili wakusanyike kwenye uwanja wa mpira wa wilaya yetu kuhudhuria mashindano ya maonyesho ya vipawa mbalimbali. Mwaka uliopita, vijana walioshiriki katika mashindano hayo walikuwa vijana wengi mno. Makundi mengi yalikuwa yamejisajili kwa kushiriki katika mashindano hayo na kila mwanakundi alikuwa akijigamba kwa uwezo wake akijilinganisha na wenzake waliotoka katika tarafa mbalimbali. Makundi ya wanamuziki, wacheza ngoma, wachoraji, wafinyanzi, wanafasihi, wafumaji, watarizi, wasusi, na wengine kutoka kila tarafa walikuwa wamejiandaa kwa sanaa zao za kuvutia. Watazamaji wote walikuwa na hamu kubwa ya kuona kundi litakaloshinda wengine kwa kuonyesha vipaji vyao na kuwavutia watazamaji.

   Uwanja ulikuwa umefurika, hapa mashabiki wa kila kundi wakishangilia kundi lao kwa kelele nyingi, ngoma, vifijo na nderemo. Baada ya muda mfupi, jopo la tathmini lilifika hapo na kila mwanajopo akachukua kiti chake. Jopo lenyewe lilikuwa limeundwa na watu watatu  : waume wawili na mwanamke mmoja. Sote tuliamrishwa kutulia na kufuata maelekezo yaliyotolewa na mkuu wa jopo hilo. Makundi yote yalitakiwa kuchagua mwakilishi wao wa kuja kuchagua nambari ya itakayoonesha zamu yao kupita jukwaani. Huu ulikuwa wakati wa tumbo joo, hivi kila kundi likiwa na woga wa kutangulia makundi mengine. Kundi la ngoma lilitangulia kupanda kwenye jukwaa na watu wote wakasimama kushabikia. Kundi hili lilikuwa limesindikizwa na wasichana pamoja na wavulana waliokuwa wakicheza ngoma hizo kwa ustadi mkubwa huku wapigaji ngoma kwa upande wao, wakijigamba na kuruka kiufundi huku na kule. Muda wao wa kuigiza ulipokwisha, walipongezwa na kupigiwa makofi mengi nao wakarudi kwenye nafasi yao. Huu ulikuwa sasa wakati wa kundi la uchoraji. Washindani katika kundi hili walikuwa watano: wavulana wawili na wasichana watatu, kila mmoja akiwa na vifaa vyote vya uchoraji vilivyohitajika. Waliambiwa kufanya mchoro wa ng’ombe watatu pamoja na mchungaji wao kwa dakika tano hivi wakionyesha ustadi wa kuchanganya rangi.

   Watu wengi walistaajabu kusikia hilo, wakidai kwamba haiwezekani kufanya mchoro wa namna hiyo kwa dakika tano tu. Mwamuzi alipokipuliza kipenga cha kuanza, umati wote ulisimama na kuangalia kwa makini jinsi vijana hao walivyoonyesha ustadi wao katika uchoraji. Filimbi ya mwisho ilipopigwa msichana mmoja alikuwa amekwishamaliza. Hawa wote watano wakaambiwa kuonyesha michoro yao. Umati wote ulishangilia na kustaajabu sana walipoona jinsi mchoro wa msichana yule ulivyofanywa kwa ufundi wa hali ya juu kushinda michoro mingine. Yeye alichukuwa nafasi ya kwanza na kufuatwa na mvulana ambaye pia alikuwa na ulemavu wa miguu. Huyu alikuwa amemaliza mwaka mzima baada ya kunusurika katika ajali ya gari alipotoka Kampala kushiriki katika Mashindano ya Kimataifa ya Wachoraji wenye umri wa chini ya miaka ishirini.

   Makundi yote yalipewa muda wa kujitokeza na kuonyesha vipawa vyao kwenye jukwaa lililokuwa limetengenezwa kwa ajili ya mashindano hayo. Waigizaji wa mashairi walipewa nafasi yao ya kuonyesha umahiri wao katika utunzi wa mashairi. Katika kundi hili Karasira na Mukamwiza ndio walioibuka na ushindi. Karasira aliimba wimbo mzuri sana uliowafurahisha wengi. Yeye alionekana kuwa na sauti nzuri, nyororo na maneno matamu aliyoyatumia yaliwafurahisha wengi. Maudhui ya wimbo wake yalielekea kuwasifu wazazi wote kwa jumla kwa kudhihirisha jinsi wanavyojitolea kuwatafutia kila wanachohitaji na kuwapatia malezi mema tangu utoto hadi wenapokuwa watu wazima. Kundi lake lilikuwa moja kati ya makundi mengine yaliyoigiza vipawa mbalimbali vya kifasihi. Makundi mengine ya kifasihi yaliyoshiriki katika mashindano hayo yalihusisha watunzi wa mashairi, Watambaji hadithi, waigizaji wa michezo mbalimbali kama vile wacheshi walionyesha ubingwa na ubunifu mkubwa katika matumizi ya lugha. Badhi ya watambaji hadithi walikuwa wametunga hadithi kwa kusimulia matukio mbalimbali kuhusu sungura na wanyama wengine.

   Upande wa mashairi nao ulichangamsha sana umati uliokuwepo. Watunzi wengi wa mashairi walizingatia maudhui yaliyolenga umuhimu wa fasihi katika jamii. Pamoja na shairi hili, umma uliweza kuelimika na kufungua macho mpaka wengi wakatangaza kuwa waliweza kutambua udhaifu uliojitokeza katika jamii na mambo mbalimbali yaliyotakiwa kurekebishwa na kupewa mwelekeo katika jamii yao. Wanamashairi hao waliwafundisha mengi, wakaburudika mpaka walipoanza kutokwa na machozi kwa furaha tele. Kupitia mashairi mengi yaliyosimuliwa pale, watu walipata mwanya wa kuthamini umuhimu wa fasihi, yaani sanaa ya kuitumia lugha. Wazee waliokuwepo waliwaelezea vijana wengi kwamba fasihi au sanaa ya kuitumia lugha ni njia bora ya kuonesha mawazo ya wasanii kwa kuitumia lugha.

   Watazamaji wote waliweza kuelewa utamu uliopatikana katika misemo ya washindani waliokuwepo kushangaa kuona jinsi uzuri huo uliweza kuambatanishwa na umuhimu wa sanaa hiyo katika jamii. Wengi walikuwa wakisema kuwa fasihi huendeleza, huhifadhi na kurithisha utamaduni, mila na desturi za jamii na pia kwamba fasihi huwaelimisha wanajamii kwa njia moja au nyingine. Pamoja na hayo yote, watu wote waliahidi kuithamini walipotambua kuwa iliweza kulinganishwa na jiwe kubwa la thamani linalohitaji kuhifadhiwa na kutunzwa vizuri. Wao waliweza kuelewa jinsi lugha inavyotumiwa na kuvutia masikio ya wote waliokuja kushiriki katika mashindano hayo. Mwishoni mwa tamasha hilo watazamaji wote walikuwa wamechangamka kwa vicheko na furaha kubwa.

   Mkuu wa kamati la majaji alisimama na kuyashukuru makundi yote yaliyokuwa yamehudhuria tamasha hilo. Washindani walikuwa tayari kuyasikiliza matokeo ya michezo na maonyesho yao. Kwa kweli, mioyo yao ilikuwa ikiwadundadunda walipokuwa wakisubiri maneno yaliyotarajiwa kutangazwa na Mkuu wa Jopo. Lakini, kama wasemavyo wahenga  : “Asiyekubali kushindwa si mshindani”. Watu wote walikuwa wametulia tuli kama maji mtungini. Punde si punde mkuu wa jopo alitangaza washindi kulingana na sanaa zote zilizoshirikishwa na zawadi nyingi zikatolewa. Watazamaji walitoka wakicheka na kuwapongeza sana wanafasihi wote walioshiriki katika mashindano kwa sauti kubwa “Fasihi  ! Fasihi  ! Fasihi  ! Oyeeee ! Oyeeee !”. Wao walifurahia maonyesho yote ya kifasihi na jinsi washindani walivyoonyesha ufundi mkubwa katika mawasilisho yao.

   Maswali ya ufahamu

   1. Kazi ya jopo la tathmini ilikuwa ipi ? Jopo hilo liliundwa na nani ?

   2. Kwa nini wachezaji ngoma walipongezwa?

   3. Wachoraji waliambiwa kufanya nini? Nani aliweza kushinda kati ya wachoraji

   wote?

   4. Ulemavu wa kijana mvulana aliyechukua nafasi ya pili ulitokana na nini?

   5. Maudhui ya wimbo wa Karasira yalihusu nini?

   6. Maudhui yaliyozungumziwa katika mashairi yalihusu nini?

   7. Taja makundi yote ya kifasihi yaliyoshiriki katika mashindano.

   8. Umma ulifaidika namna gani kutokana na mashairi yaliyosimuliwa?

   9. Kutokana na kifungu hiki fafanua maana ya fasihi.

   10. Kwa nini fasihi ilinganishwe na jiwe lenye thamani kwa jamii?

   11. Eleza usemi “Asiyekubali kushindwa si mshindani”.

   10.2 Msamiati kuhusu Sanaa katika Jamii

   Zoezi la 2: Eleza maana ya maneno yafuatayo kulingana na muktadha wa

   matumizi yake katika kifungu cha habari mlichosoma, kisha utunge sentensi

   kwa kutumia maneno hayo.

   1. Umahiri

   2. Umati

   3. Jopo

   4. Mashindano

   5. Kuthamini

   6. Kuahidi

   7. Kuburudisha,

   8. Kuelimisha,

   9. Kuhifadhi,

   10. Desturi

   Zoezi la 3: Tumia mshale kwa kuoanisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.


   10.3 Sarufi: Nomino za ngeli ya LI-YA na Vivumishi vya Kumiliki

   Zoezi la 4: Soma kifungu cha habari hapo juu kuhusu “Sanaa katika jamii”,

   kisha andika sentensi zenye nomino za ngeli ya LI-YA.

   Zoezi la 5: Tunga sentensi tano zenye nomino za ngeli ya LI-YA.

   Zoezi la 6:Andika wingi wa sentensi hapa chini, kisha utoe maelezo kuhusu

   muundo wa umoja na wingi wa nomino zilizotumiwa.

    Umoja                                                                Wingi

   1. Jembe langu limepotea.                           -------------------------------------------

   2. Janga kubwa limesababisha maafa.       -------------------------------------------

   3. Jaribio la leo limesahihishwa.                  -------------------------------------------

   4. Jeshi lao lina askari wengi.                       -------------------------------------------

   5. Jeraha lake lina uchafu sana.                    -------------------------------------------

   6. Jambo hili liliwafurahisha wengi.             -------------------------------------------

   7. Jicho lake linaoona mbali sana.                -------------------------------------------

   8. Jiwe langu lina thamani kubwa.              -------------------------------------------

   9. Jino lako limeng’oka?                              -------------------------------------------

   10. Jiko langu limeharibika.                         -------------------------------------------

   • Maelezo muhimu kuhusu umoja na wingi wa nomino za ngeli ya LI-YA

   Soma maelezo yafuatayo hapo chini

   Nomino za ngeli ya LI-YA huwekwa katika wingi kwa kuongeza kiambishi MAkwenye nomino hiyo


   Zoezi la 7: Chunguza mifano ya sentensi hapa chini, kisha ueleze aina za

   maneno yaliyopigiwa mstari.

   1. Nilikosa koti langu.

   2. Magari yao yameibwa.

   3. Nitakununulia koti jingine

   4. Majengo yote yalijengwa karibu na ziwa.

   5. Nipe embe lolote la kula.

   Zoezi la 8: Tunga sentensi tano kwa kutumia nomino za ngeli ya LI-YA pamoja na vivumishi vya kumiliki.

   Maelezo muhimu:

   Vivumishi vya kumiliki ni -angu, -ako, -ake, -etu, -enu na -ao. Vivumishi hivi katika

   ngeli ya Li-Ya huchukua kiambishi konsonanti l- katika umoja na y- katika wingi.

   Zoezi la 9: Andika sentensi zifuatazo katika wingi.

   Umoja                                            Wingi

   1. Koti langu limechafuka                          . ………………………………………..

   2. Shirika lako linajulikana sana.             ………………………………………..

   3. Gari lake ni la kifahari.                        ………………………………………..

   4. Jumba letu linapendeza                     ……………………………………….. 

   Zoezi la 10: Andika sentensi zifuatazo katika hali kanushi.

   1. Koti langu linanipendeza

   2. Gari lake limepata ajali.

   3. Mashirika yenu yataimarishwa.

   4. Mavuno yetu yamekuwa mazuri mwaka huu.

   5. Jumba lake limekarabatiwa.

   10.4 Matumizi ya lugha: Dhima za Fasihi katika Jamii

   Soma maelezo yafuatayo ili kubainisha dhima za fasihi katika jamii:

   Kimsingi fasihi ina dhima zifuatazo:

   Kuelimisha jamii: Fasihi hukosoa, huionya na kuierekebisha jamii. Fasihi

   huchambua na kuchochea umma na kuwafumbua macho wanajamii ili

   waweze kufichua uwezo au udhaifu uliomo katika jamii.

   Kuburudisha jamii: Fasihi huburudisha, yaani husisimua kimwili na kiakili

   msikilizaji au msomaji na kuvutiwa kihisia na kazi ya fasihi aliyoisoma,

   aliyoitazama au kuisikiliza.

   Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii: Fasihi hutunza na kuhifadhi mila na

   desturi za jamii kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

   Kudumisha na kuendeleza lugha: Kadiri lugha inavyotumiwa na watunzi,

   ndivyo inavyokua na kupevuka. Maneno mengi yatumiwayo leo katika lugha

   mbalimbali yalibuniwa na kuenezwa na watunzi wa mashairi, riwaya, nyimbo,

   tamthilia, sanaa za maonyesho, n.k.

   Kuunganisha jamii: Fasihi huleta pamoja watu katika jamii

   Kukuza uwezo wa kufikiri: Tanzu nyingi za fasihi huwahamasisha hadhira

   kufikiri sana ili kupata suluhisho: vitendawili, vitanzandimi

   Kumtajirisha msanii: Fasihi inaweza kumletea pato msanii.

   Kuikomboa jamii: Mara nyingi fasihi ilitumiwa kama silaha ya ukombozi kwa

   kumwezesha mwanadamu kueleza yale yote yaliyokuwa yakimsumbua na

   kupigania uhuru wake.

   10.5 Kuzungumza na Kusikiliza: Majadliano

   Zoezi la 11: Jadilini kuhusu “Madhara yanayoweza kujitokeza katika jamii pale

   fasihi inapotumiwa vibaya”.

   Zoezi la 12: Jadilieni kuhusu dhima za fasihi zifuatazo huku mkitoa mifano ya

   kudhihirisha maoni yenu.

   1. Kuelimisha jamii

   2. Kuburudisha jamii,

   3. Kuhifadhi na kurithisha amali za jamii,

   4. Kudumisha na kuendeleza lugha

   5. Kuunganisha jamii,

   6. Kukuza uwezo wa kufikiri,

   7. Kumtajirisha msanii,

   10.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

   Zoezi la 13: Tunga kifungu cha habari chenye mada hii: “Umuhimu wa Fasihi

   katika Jamii”

   SOMO LA 11: HADITHI

   Chunguza mchoro ufuatao ili ujibu maswali yanayofuata hapo chini


   Zoezi la 1: Jibu maswali yafuatayo kulingana na uchunguzi ulioufanya kwenye

   mchoro huu

   1. Ni wanayama gani unaowaona kwenye mchoro hapo juu?

   2. Unafikiri ni shughuli ipi inayoendelea kwenye mchoro huo. Eleza jibu lako huku

   ukilihusisha na kichwa cha habri kinachofuata.

   11.1 Kusoma na Ufahamu: Sungura na Kobe

   Soma hadithi hii ya “Sungura na Kobe”, kisha jibu maswali uliyopewa katika sehemu ya

   ufahamu.

   Siku moja Sungura alikuwa akirukaruka huku akijivunia ustadi wake wa kukimbia mbio kuliko wanyama wengine wengi waishio msituni. Njiani alimkuta Kobe aliyekuwa akitembea kwa mwendo wake wa polepole kama kawaida. Sungura alimuamkia Kobe kwa kiburi akisema “Vipi bwana Kobe? Unaenda wapi na mwendo wako huo? Ninaona unaringa. Unafikiria wewe ni kiongozi wa msitu huu?” Kusikia hayo Kobe alihuzunika sana na kushikwa na hasira kwa maneno hayo ya Sungura.

   Yeye alikuwa ametambua jinsi Sungura alivyomchokoza kwa kumdharau! Kisha alimwambia, “Sungura! Usimdharau yeyote kabla hujajua uwezo wake! Hata kama unajidhania kuzidi mbio wanyama wengi, usifikiri kwamba mimi ni miongoni mwa hao!” Sungura alimcheka sana na kusema “Maskini weee! Unadai una uwezo gani wewe? Eti! Wewe unataka kusema kuwa unaweza kukimbia kama mimi?” Kobe alimjibu, “Ni dhahiri kwamba wewe una mwendo wa kasi lakini haimaanishi kwamba unaweza kunishinda katika mashindano ya kukimbia.”Aliposikia hayo, Sungura alicheka sana na kusema “Ukinishinda katika shindano hilo mimi nitakuheshimu na kukiri kwamba mimi ni mjinga kuliko wanyama wote waishio katika msitu huu!”

   Wote wawili walikubaliana siku ya mashindano, wakarudi kwao kila mmoja akaanza kujitayarisha awezavyo ili aweze kuwa mshindi. Kila mmoja alijitafutia mashabiki wa kumuunga mkono. Siku ya mashindano ilipowadia wanyama wengi walikuwepo: kina fisi, tembo, twiga, nyati, nyani, ngorombwe, pundamilia, chui na wanyama wengine wengi. Wote walikuwa na hamu ya kuona mshindi katika shindano hilo la mbio. Kwenye mstari wa kuanzia mbio hizo palikuwepo Sokwe ambaye alipewa wajibu wa kuanzisha mchezo na kuwa mwamuzi wake. Sehemu walipotarajiwa kumalizia mbio zao, yaani kwenye mstari wa kikomo palikuwa na farasi kama mwamuzi wa kuthibitisha mshindi wa shindano hilo.

   Sokwe aliwaita Sungura na Kobe kusogelea mbele kwenye mstari wa kuanzia. Papo hapo sokwe alipuliza filimbi mbio zikaanza. Sungura na majivuno yake alianza kurukaruka kidogo ili kuonyesha kwamba hawezi kushindwa na mnyama kama Kobe, kisha akakimbia kwa kasi na kumuacha Kobe mbali sana. Baada ya muda mfupi Sungura aligeuka na kuangalia nyuma lakini hakumuona Kobe. Sungura alifurahi sana akawaza “Hivi ni dhahiri kwamba Kobe hawezi kunishinda. Naona kwamba hajajitokeza karibu nami, hii ina maana kwamba yuko mbali sana na itambidi atumie muda mrefu kufika hapa nilipo, basi ni vizuri nipumzike kidogo niendelee baadaye na mbio zangu”.

   Sungura alikaa chini na kuanza mapumziko yake. Kwa kuwa alikuwa amemaliza siku tatu akiwazia jinsi atakavyojionyesha kwa ustadi wake wa mbio mbele ya wanyama wenzake, hakuweza kupumzika kwa muda mrefu. Hivyo basi, aliendelea kupumzika. Kobe, kwa mwendo wake wa polepole aliendelea na mchezo kama alivyoanza. Alisonga mbele hatua kwa hatua bila kukata tamaa. Alipofika mbele kidogo alimkuta Sungura chini ya mti amelala. Kobe hakujisumbua kwa kuwazia kile Sungura alichokuwa akifanya huko. Alifikiria kuwa ni maringo yake ya kawaida…. na kuendelea na safari yake. Njiani kote alikopitia wanyama wengine walikuwa wakimtia moyo Kobe kwa kumpongeza: Kobe! Kobe! Kobe! Endelea! Endelea! Karibu utafika!”

   Kobe hakusema lolote aliendelea bila kuangalia huku na kule. Baada ya muda mrefu, Sungura alishtuka kwa kusikia kelele za wanyama wengine. “Lo! Kumbe nilikuwa nimesinzia hapa! Kobe yuko wapi? Hajafika hapa kweli? Acha niendelee nadhani dakika mbili nitakuwa nimefika!” Sungura alikimbia haraka.

   Alipofika mbele kidogo alitazama kule walipotarajia kufikia katika shindano lao na kumuona Kobe akikaribia mstari wa kumalizia mchezo wao. Hivyo, alishikwa na bumbuwazi naye akatumia nguvu zake ili ampite Kobe, lakini haikufua dafu kwani alikuwa amechelewa mno. Kobe alikuwa karibu sana na mstari wa mwisho kiasi kwamba Sungura alipokaribia kikomo, Kobe akamtangulia kukanyaga mstari huo, wanyama wote wakamshangilia kwa kusema “Mshindi Kobe! Mshindi Kobe! Oyeee! Kobeee Oyeee!”

   Farasi aliyekuwa mwamuzi wa mashindano hayo alipuliza filimbi na kuinua mkono wa Kobe huku akithibitisha ushindi wake. Wanyama wote walistaajabu kuona Kobe na mwendo wake ameweza kushinda Sungura ambaye alijulikana kwa uwezo wake wa kukimbia mbio sana kuliko wanyama wengi msituni huko. Sungura alishikwa na aibu, naye akamuomba Kobe msamaha kwa maneno aliyomwambia siku ile walipokutana. Alimsihi amsamehe kwa kusema, “Asiyekubali kushindwa si mshindani, tangu leo sitadharau yeyote kwani kila mnyama hapa huwa na uwezo wake. Ni lazima tuheshimiane.” Tangu siku hiyo Sungura na Kobe waliishi kwa amani kila mmoja akimuheshimu mwenzie wakaendelea kuwa marafiki.

   Huu ndio mwisho wa hadithi!

   Maswali ya ufahamu

   1. Ni wahusika gani wanaozungumziwa katika hadithi hii?

   2. Tukio hili lilitokea wapi?

   3. Kobe alikasilishwa na nini aliposalimiwa na Sungura?

   4. Taja majina ya mashabiki waliohudhuria shindano hili.

   5. Waamuzi wa shindano hili walikuwa kina nani?

   6. Kwa nini Sungura aliamua kupumuzika wakati shindano lilikuwa likiendelea?

   7. Unadhani Sungura alishindwa na nini?

   8. Sungura alifanya nini baada ya kushindwa?

   9. Linganisha tabia za Sungura dhidi ya tabia za Kobe.

   10. Umejifunza nini kutokana na hadithi hii?

   11.2 Msamiati kuhusu Hadithi

   Zoezi la 2: Eleza maana za maneno haya kulingana na jinsi yalivyotumiwa

   katika kifungu cha habari hapo juu.

   1. Kiburi

   2. Hamu

   3. Wajibu

   4. Kukata tamaa

   5. Haikufua dafu

   6. Kikomo

   7. Kupongeza

   8. Kuunga mkono

   9. Ilipowadia

   10. Dhahiri

   Zoezi la 3: Jaza mapengo katika sentensi zifuatazo ukitumia mojawapo

   ya maneno yafuatayo: wajibu, kikomo, kata tamaa, hamu, dhahiri, kiburi,

   haikufua dafu, ilipowadia.

   1. Wazazi wana ………………….. wa kuwalisha na kusomesha watoto wao.

   2. Tarehe ya kufanya mtihani ………………………… sote tulikuwa tayari.

   3. Timu ya mpira ilitumia mbinu nyingi kupata bao, lakini .…………………

   4. Ni ……………………. kwamba mvua itanyesha leo hii.

   5. Mtoto wake amemsihi waende pamoja Rubavu kwa sababu alikuwa na

   …...……………… ya kuona ziwa la Kivu.

   6. Si vizuri kuonesha …………………….. unapozungumza na marafiki zako.

   7. Muda tuliokuwa nao hapa umefikia ……………………, ni lazima tuondoke.

   8. Asinge …………………… angefikia malengo yake.

   11.3 Sarufi: Matumizi ya Vivumishi vya Kuuliza katika Ngeli ya LI-YA

   Zoezi la 4: Tafuta vivumishi vya kuuliza vilivyotumiwa katika hadithi ya

   Sungura na Kobe. 

   Zoezi na 5: Tunga sentensi zenye nomino za ngeli ya LI-YA

   Zoezi la 6: Tumia vivumishi viulizi ambavyo ulipewa ndani ya mabano kujaza

   sentensi.

   1. Jibu .............. limeishapatikana? (-pi)

   2. Mawe ................. yamewekwa kando ya barabara. (-ngapi)

   3. Madirisha .............. yamefunguliwa. (gani)

   4. Meno ................ yameng’oka. (-pi)

   5. Tunda ................ limeiva. (gani) 

   Zoezi la 7: Andika sentensi zifuatazo katika umoja ama wingi.

   1. Jengo lipi ni kubwa?

   2. Mapapai yapi yameiva?

   3. Tukupe magunia mangapi?

   4. Mashirika gani yanasaidia wakulima?

   5. Sasa wewe unataka nikupe jembe lipi?

   Maelezo muhimu

   • Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali kuhusu nomino. Vivumishi hivi

   vinapotumiwa katika sentensi ni sharti sentensi hiyo ikamilishwe kwa alama

   ya kiulizi. Vivumishi viulizi ni vitatu:-pi?, -ngapi? na -gani? Vivumishi viulizi

   -ngapi? na -pi? huchukua viambishi vya ngeli lakini kiulizi “gani” hakichukui

   kiambishi chochote cha ngeli.

   Kwa mfano: 1. Gari lipi linatembea? - Magari yapi yanatembea?

    2. Je, nyumba yako ina madirisha mangapi?

    3. Unapenda shirika gani? – Unapenda mashirika gani?

   11.4 Matumzi ya Lugha: Aina za Hadithi

   Zoezi la 8: Jadilini kuhusu maelezo yanayofuata ili uweze kueleza aina za

   hadithi.

   Maelezo muhimu kuhusu maana ya hadithi

   • Hadithi ni tungo za fasihi za masimulizi ambazo zinatumia lugha ya nathari

   (lugha ya ujazo, ya maongezi ya kila siku). Masimulizi hayo hupangwa

   katika mtiririko wa vituko unaokamilisha kisa. Ili kisa hiki kikamilike, hadithi

   huwa na wahusika ambao ndio nyenzo ya kukiendesha kisa chenyewe,

   vivyo hivyo hadithi huwa na maudhui.

   Maelezo muhimu kuhusu aina sita za hadithi:

   Ngano: Hizi ni hadithi za kimapokeo ambazo zinatumia wahusika kama

   wanyama, wadudu, mizimu, miungu, miti, watu, na viumbe visivyo na uhai

   kama mawe, miamba, n.k. kueleza au kuonya kuhusu maisha. Ngano ni

   hadithi ambazo husimiliwa katika mazingira ya starehe.

   Tarihi : Ni masimulizi kuhusu matukio ya kihistoria pamoja na tarehe za

   kutokea kwa matukio muhimu..

   Visasili: Ni hadithi ambazo husimulia mambo yanayohusiana na maumbile

   ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai. Hadithi hizi hutumia

   wahusika wa aina mbalimbali pamoja na miungu na binadamu. Mara

   nyingi hutambwa kwenye miviga.

   Vigano: Ni hadithi fupi ambazo zinaeleza makosa au uovu wa watu fulani

   na kueleza maadili yanayofaa. Mara nyingi kigano hutumia methali kama

   msingi wa maadili yake.

   Soga: Hizi ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Soga husema ukweli

   unaoumiza, lakini ukweli huo unajengewa kichekesho ili kupunguza ukali

   wa ukweli huo. Wahusika wa soga ni watu wa kubuni lakini wanapewa

   majina ya watu walio katika mazingira hayo.

   Visakale/ Migani: Ni hadithi zinazohusu watu waliotenda matendo ya

   kishujaa na wanaosifiwa katika jamii fulani.

   Hekaya: Ni hadithi ambayo licha ya kuweza kuwa ni kisa, inayo sifa moja kuu

   kwamba inaeleza pia mambo ya ajabu, mfano wa miujiza, yasiyowezekana

   kwa nguvu za kawaida za binadamu. Wahusika wa hekaya kwa kawaida

   ni binadamu, au mchanganyiko wa binadamu na wanyama au viumbe

   vingine, pia Mungu na miungu.

   Hurafa: Ni aina ya hadithi ambayo wahusika wake huwa ni wanyama au

   vitu vingine ambavyo huwa vinapewa uhai. Katika mapokeo ya Waafrika,

   wanyama husimamia aina Fulani ya binadamu. Wanyama hao husimamia

   aina ya tabia ya aina Fulani ya binadamu. Katika hadithi za kiafrika na

   hasa za kibantu, wanyama kama fisi, kobe, simba, mbwa, nyoka, mjusi na

   wengineo husikika sana.

   Umuhimu wa hadithi

   • Hadithi hutoa sababu za hali mbalimbali katika dunia kama jamii inavyoiona.

   Husifu mema na kukashifu maovu. Hadithi hutoa maonyo, huadhibu,

   huelimisha na kushauri. Hutoa mafunzo na maadili ya kufuatwa na jamii

   na kuiwezesha kubadili tabia. Hadithi huzingatia historia na utamaduni

   wa jamii. Huendesha uhusiano wa jamii kwa kuiburudisha na kuboresha

   uwezo wa kukumbuka.

   Zoezi la 9: Oanisha aina ya hadithi katika kundi A na ufafanuzi wake katika kundi B, kisha utoe mifano miwili miwili kwa kila aina ya hadithi iliyopendekezwa (mifano hiyo itolewe kutoka hadithi za jamii ya Wanyarwanda)


   Hadithi husimuliwa na huwa na fomula yake katika utangulizi na mwisho

   wake

   Mianzo ya hadithi za kimapokeo

   Mtambaji: Paukwa

   Hadhira: Pakawa

   Mtambaji: Paukwa

   Hadhira: Pakawa

   Mtambaji: Kaondokea chanjagaa

                    Kajenga nyumba kaka

                    Mwanangu mwana siti

                    Vijino kama chikichi

                    Cha kujengea kikuta

                    Na vilango vya kupitia

                   Atokeani

                   Hapo zamani za kale………………….

   1. Mtambaji: Paukwa

   Hadhira: Pakawa

   Mtambaji: Sahani!

   Hadhira: Ya mchele!

   Mtambaji: Giza

   Hadhira: La mwizi

   Mtambaji: Baiskeli

   Hadhira: ya mwalimu! n.k.

   Mtambaji: Hadithi hadithi!

   Hadhira: Hadithi njoo!

   Mtambaji: Hadithi hadithi!

   Hadhira: Hadithi njoo!

   Mtambaji: Hapo zamani za kale palikuwepo na …………………………

   2. Msimulizi: Atokaeni!

   Hadhira: Naam Twaibu!

   Msimulizi: Kaondokea chanjagaa, n.k.

   Hadithi huwa pia na miisho yake

   Tunasema : “Huu ndio mwisho wa hadithi” au “Hadithi inakomea hapa.”

   11.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

   Zoezi la 10: Jadilini kuhusu maswali yafuatayo:

   1. Eleza kwa kifupi mambo muhimu yaliyoelezewa hapo juu.

   2. Taja aina za hadithi zilizozungumziwa katika kifungu cha habari hapo juu.

   3. Hadithi ni nini?

   4. Hadithi zina umuhimu gani?

   5. Kwa kutumia lugha ya Kiswahili, simulia wenzako hadithi unayoifahamu kutoka

   jamii ya Wanyarwanda.

   Zoezi la 11: Mbele ya wanafunzi wenzako, simulia hadithi moja unaoyoifahamu kwa kuzingatia mianzo na miisho ya hadithi za kimapokeo kama zilivyoonyeshwa hapo juu.

   11.6 Kuandika: Utungaji wa Hadithi

   Zoezi la 12: Kwa kutumia Kiswahili fasaha, andika hadithi moja unayoifahamu

   kutoka katika jamii ya Rwanda.

   SOMO LA 12: METHALI

   Tazama mchoro ufuatao, kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini:


   Zoezi la 1: Jibu maswali yafuatayo:

   1. Eleza wahusika unaowaona kwenye mchoro.

   2. Ni shughuli zipi zinazoendelea kwenye mchoro huo?

   12.1 Kusoma na Ufahamu : Leo ni leo

   Soma kifungu cha habri kuhusu “Leo ni leo” ili kujibu maswali ya ufahamu yaliyotolewa

   hapo chini

   Hapo zamani za kale palikuwa na mzee mmoja aliyejulikana kama Gahigi. Gahigi alisifika sana kwa uwezo wake wa kutoa mawaidha kwa kutumia lugha ya mafumbo yenye hekima. Kila siku alikuwa akitumia methali nyingi sana. Wengi walimsifu na kumwita maktaba ya jamii. Katika mahakama za jadi Mzee Gahigi alikuwa mpatanishi pamoja na wazee wengine. Kila alipozungumza na mkewe, watoto, marafiki na wengine alikuwa akitoa maneno makavu yenye busara.

   Siku moja mtoto wake Kagabo alichelewa kuamka asubuhi ili aende shuleni. Alimwamsha na kumwonya asizoee tabia mbaya ya kupenda kulala na kusahau kazi na majukumu muhimu kwa kumwambia, “Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.”

   Gahigi alikuwa bingwa katika matumizi ya lugha iliyoweza kuwaonya na kuwarekebisha waliokutana naye. Alikuwa mzee mwenye huruma na alikuwa akimhurumia kila aliyesahau kutekeleza jambo linalomngoja. Kwa hivyo alimwambia mtoto wake aamke haraka ili aende shuleni. “Mtoto wangu, ndege aamkaye asubuhi hula wadudu watamu. Acha kushika blanketi na shuka lako ili uweze kuvuna matunda ya jasho lako la baadaye.Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo. Mimi nimeanza kuzeeka lakini kama nisingefanya kazi vizuri msingeweza kusoma.Ukipoteza muda wako leo kesho hutaweza kuyarudia yaliyopaswa kutendeka leo.”

   Basi mtoto aliamka, akanawa mwili wake huku Gahigi akimsihi afanye haraka ili afike shuleni mapema. Alimwelezea mengi kuhusu hasara zinazowapata wavivu na jinsi wanavyoponyokwa na bahati zinazojitokeza maishani mwao. Alizidi kumwambia maneno matamu yenye busara ambayo Kagabo aliyapenda na kuyazingatia. Siku nzima yeye alikuwa akikumbuka methali moja iliyomvutia sana, “Titi la nyati hukamuliwa kwa mashaka;’’ na nyingine iliyomwambia kuwa “Wakati una mabawa”. Tangu siku hiyo Kagabo aliamua kuzingatia mawaidha ya babake na kujizoeza kuwa na bidii katika shughuli zake za kila siku. Alipowasikia wanafunzi wenzake wakimwambia kwamba “haraka haraka haina baraka” aliwaambia kuwa wangeweza kujutia hayo baadaye.

   Kila siku alikuwa wa kwanza kufika shuleni na kufuata vizuri maelezo ya mwalimu na mambo yote yaliyofundishwa darasani. Alipopewa kazi, aliifanya haraka na kuimaliza kwa muda uliotarajiwa. Aliongozwa na maneno ya baba yake kwamba “Fanya kitu kinachofaa katika muda unaofaa.” Yeye alikuwa akishangaa kuona baadhi ya wanafunzi walikuwa wakiyapuuza maonyo yake kwa kuendeleza tabia za uvivu. Kila alipowaona wamechelewa alikumbuka maneno ya baba yake, «  Chelewachelewa utamkuta mtoto si wako ». Kagabo alijitahidi kufanya kila liwezekanalo ili asonge mbele masomoni kwa kutarajia maisha mazuri ya baada ya masomo yake kama alivyopenda kumwambia baba yake.

   Kagabo aliendelea kusoma kwa bidii akamaliza shule za msingi na kuingia katika shule za sekondari. Kazi zote alizoombwa kufanya alizifanya kwa makini akiongozwa na maneno ya baba, “Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo.” Alipomaliza shule za sekondari alijiunga na chuo kikuu katika kitivo cha Lugha na Sanaa. Hapo bidii zake hazikupungua hata kidogo. Yeye alijua kwamba “Mchumia juani hulia kivulini.” Alipomaliza masomo yake alipewa kazi ya Mhariri Mkuu kwenye Televisheni ya Taifa. Hiyo ilikuwa kazi nzuri iliyoweza kumletea pato kubwa kila mwezi. Kazi yake ilimruhusu kutembelea mataifa mengi duniani ili kuonana na wahariri wengine katika makongamano na mikutano ya aina mbalimbali. Miaka miwili baadaye, alikuwa anajulikana kwa kila mtangazaji maarufu na kampuni nyingi za utangazaji zilianza kumwita kutoa mafunzo ya muda kwa watangazaji wao. Hapo alianza kufurahia uwezo wake na kukumbuka methali nyingi alizoambiwa na babake. Miongoni mwa maneno aliyoyakumbuka na ambayo alipenda kuwaambia watangazji wenzake yalikuwa yanaihusu methali tamu “mchumia juani hulia kivulini”. Yeye alipenda kazi yake na kuifanya kwa usahihi na viongozi wake walimjua.

   Mwaka wa tatu baada ya masomo yake alikuwa amejijengea nyumba nzuri mjini na kujinunulia gari zuri la kisasa. Watu wengi waliomwona walishangaa kuona mtoto aliyetoka katika kijiji kisichojulikana amefikia kiwango kama hicho cha kutegemewa na wengi. Kwa kweli utajiri wake ulikuwa umemwezesha kuwakumbuka wasiojiweza na kuwasaidia kwa moyo mkunjufu. Yeye hakuona ugumu wowote kusaidia yeyote aliyemwendea. Yeye alishirikiana na viongozi wa kijiji chake katika mradi alioanzisha wa kusajili vijana wote waliokuwa wamesitisha masomo yao kwani alikuwa ameshajengea shule ya kiufundi huko kijijini. Kila wakati alipofika kijijini kwake, majirani wote walikuja na kukumbuka malezi aliyopewa na babake alipokuwa mtoto mchanga. Wote walifurahia matunda aliyoweza kuvuna babake Gahigi na kuambiana kati yao “Ivute ngozi ingali mbichi.” Wote walielewa kuwa watoto wao wangelizoezwa kutimiza wajibu wao mapema kama Kagabo wangeliweza kuwa na maisha mazuri kama yake.

   Mzee Gahigi alikuwa mtu wa ajabu aliyewaonya wanakijiji wote. Kila walipokutania katika shughuli mbalimbali za kijamii na za kimaendeleo ya kijamii alipenda kuwaambia, “Hakuna kitu cha bure katika dunia yetu, lazima tufanye kazi kwa bidii ili tufike tunapotaka kufika. Maisha mazuri ya watoto wetu yatatokana na malezi mema tutakayowapatia nasi tutafurahia baadaye. Fuata nyuki ule asali kwa kuwa mtu huvuna kile alichokipanda.’’ Wazazi wenzake wote walimpongeza kwa maneno yake ya busara naye akakumbuka jinsi alivyochukuliwa na mtoto wake katika sherehe ya mwaka uliotangulia. Kwa kweli, Kagabo alikuwa amemnunulia ng’ombe wa kisasa kama zawadi ya malezi mazuri aliyopewa. baba yake alifurahi sana na kumshukuru kijana wake..

   Maswali ya ufahamu:

   1. Taja majina ya wahusika muhimu wanaozungumziwa katika kifungu hiki?

   2. Kwa nini watu wengi waliyapenda maneno ya Mzee Gahigi?

   3. Mzee Gahigi alikuwa na kazi gani katika mahakama za jadi?

   4. Eleza jinsi tabia ya Kagabo ilivyobadilika.

   5. “Mchumia juani hulia kivulini”. Eleza jinsi usemi huu unavyohusiana na kifungu

   cha habari ulichosoma.

   6. Mtoto huyu alisoma masomo gani chuo kikuu?

   7. Kagabo alipomaliza masomo ya chuo alipata kazi gani?

   8. Kwa sababu gani Kagabo alipendwa na kila mtu?

   9. Kwa sababu gani Mzee Gahigi alipewa zawadi na mtoto wake?

   10. Kuna funzo lolote unalolipata kutokana na kifungu hiki? Eleza. 

   12.2 Msamiati kuhusu Methali

   Zoezi la 2: Jaribu kutoa maana za maneno yafuatayo:

   1. Mafumbo

   2. Mawaidha

   3. Maktaba

   4. Hekima

   5. Mpatanishi

   6. Shaka

   7. Baraka

   8. Bidii

   9. Nyati

   10. Runinga

   Zoezi la 3: Tumia maneno hayo katika sentensi zenye maana kamili.

   Zoezi la 4: Tumia neno jingine lenye maana sawa na liliopigiwa mstari.

   1. Alipoenda katika mbuga ya wanyama ya Akagera aliwaona mbogo.

   2. Kagabo anapenda kutumia lugha fiche.

   3. Nyuni aamkaye asubuhi hula wadudu wazuri.

   4. Kamana alikuwa mdanganyifu katika maneno yake yote.

   5. Nyumba ya vitabu isichomwe moto.

   6. Mzee Gahigi alikuwa msuruhifu.

   7. Maneno aliyowaambia wanafunzi wake walizingatia yote.

   8. Wakati wa kujibu darasani ni vizuri wanafuzi kusimama.

   9. Televisheni inapaswa kutangaza habari zenye uhakika.

   10. Alitumia juhudi katika masomo.

   Zoezi la 5: Eleza maana ya methali zifuatazo:

   1. Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo.

   2. Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.

   3. Ndege aamkaye asubuhi hula wadudu watamu.

   4. Wakati titi la nyati hukamuliwa kwa mashaka.

   5. Haraka haraka haina baraka.

   6. Ngoja ngoja huumiza matumbo.

   7. Wakati una mabawa.

   8. Mchumia juani hulia kivulini.

   12.3 Sarufi: Vivumishi vya Kuonyesha katika Ngeli ya Li-Ya

   Zoezi la 6: Chunguza katika kifungu cha habari mlichosoma na uonyeshe

   vivumishi vya kuonyesha katika ngeli ya Li-Ya.

   Maelezo muhimu

   • Vivumshi vya kuonyesha hili, hilo, lile hufuata nomino katika umoja.

   • Vivumishi vya kuonyesha haya, hayo, yale hufuata nomino katika wingi.

   Mifano


   Zoezi la 7: Chagua neno sahihi katika mabano kwa kujaza pengo.

   1. Debe ………….. lilitoboka (hii, haya, hili, hiyi).

   2. Jambazi ……….liliadhibiwa (yule, hii, lile, hiyo).

   3. Tafadhali kunja majamvi………..(ayo, hizo, hayo, halo).

   4. Anakuomba umnunuliye chungwa ………….(hizo, hayo, yayo).

   5. Jahazi …….ni kubwa (lili, hile, jile, lile).

   Zoezi la 8: Sahihisha sentensi zifuatazo:

   1. Kabati kale kalivunjwa na wezi.

   2. Maji haya alimwagwa ovyo sakafuni.

   3. Alipotaka kujenga nyumba alitafuta majiwe makubwa.

   4. Mafuta haya haamwagwi ziwani kwa sababu anaweza kuua samaki.

   5. Maboga haya matikitiki yana manufaa nyingi kwa mwili wako.

   12.4 Matumizi ya Lugha: Methali

   Zoezi la 9: Soma maelezo muhimu yanayofuata, kisha ujibu maswali hapo

   chini.

   Maelezo muhimu: maana ya methali

   • Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya

   mafumbo. Ni tamko lenye kueleza wazo la busara la binadamu kwa ufupi sana.

   Misemo hiyo huzingatia maneno yenye kuvutia masikio ya watu wanaozitumia

   na huelezea mambo mengi kwa kutumia maneno machache iwezekanavyo.

   • Methali nyingi huwa na sehemu mbili: Sehemu ya kwanza hutoa hoja nayo

   sehemu ya pili hutoa suluhisho au matokeo. 


   • Methali huhitaji hekima ili kujua maana yake.

   • Methali hutumika kwa minajili ya kusema jambo fulani kwa njia isiyo ya moja

   kwa moja.

   • Kama tanzu nyingine za fasihi simulizi, methali huwa na maana ya nje (maana

   inayopatikana kutokana na maana za maneno yaliyotumika kuunda methali

   husika) na maana ya ndani (maana inayosemwa kwa ufiche).

   Mifano:

   1. Mpanda Ngazi hushuka

   • Maana ya nje: Mtu yeyote anayepanda juu ya ngazi ni lazima itafika muda wake

   yeye kushuka kutoka juu ya ngazi hiyo

   • Maana ya ndani: Katika maisha mtu anayepata cheo au madaraka kuna siku

   anaweza kuyapoteza madaraka au cheo hicho

   2. Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo

   • Maana ya nje: Siku hii ni siku hii, anayenena siku ifuatayo ni mdanganyifu.

   • Maana ya ndani: Tendo linalowezekana kufanyika sasa lazima lifanyike,

   lisiahirishwe.

   Katika jamii methali zina umuhimu wa:

   • Kuonya

   • Kutahadhalisha

   • Kutoa mafunzo

   • Kuunganisha jamii

   i. Jibu maswali yafuatayo:

   1. Fafanua maana ya methali.

   2. Toa mifano miwili ya methali, kisha ubainishe sehemu zake mbili: hoja na

   matokeo au suluhisho.

   3. Toa methali mbili, kisha uonyeshe maana yake ya nje na maana yake

   ya ndani kwa kubainisha wakati wa kuitumia au namna inavyoweza

   kutumiwa katika mazungumzo ya watu .

   ii. Onyesha hoja na matokeo au suruhisho katika methali zifuatazo:

   • Bandu bandu humaliza gogo.

   • Chovya chovya humaliza buyu la asali.

   • Asiye funzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu.

   • Mtoto akililia wembe mpe.

   • Mtoto umlevyo ndivyo akuavyo.

   • Mchelea mwana kulia hulia yeye.

   • Heri kufa macho kuliko kufa moyo.

   • Atangaye sana na jua hujua.

   • Kuishi kwingi kuona mengi.

   • Tamaa mbele mauti nyuma.

   iii. Tafuta methali kumi zinazozingatia malezi bora kutoka lugha ya Kinyarwanda, kisha uandike methali zenye maana sawa nazo katika lugha ya Kiswahili.

   i. Oanisha methali kutoka orodha ya A na methali yenye maana sawa na methali hiyo katika orodha ya B   12.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

   Zoezi la 10: Kwa ushirikiano na wenzako, jadilini kuhusu mada zifuatazo:

   1. Umuhimu wa methali katika jamii.

   2. Akili ni mali.

   12.6 Kuandika: Utungaji wa Insha ya Methali

   Zoezi 11: Tunga kifungu cha habari chenye moja kati ya mada zifuatazo:

   1. Mchumia juani hulia kivulini.

   2. Chovyachovya humaliza buyu la asali.

   3. Asiyekubali kushindwa si mshindani.

   SOMO LA 13: NAHAU

   Umewahi kusikia kuhusu nahau? Toa mifano ya nahau

   Nahau zinatofautiana vipi na methali?

   Kwa maneno yako, eleza maana ya nahau

   13.1 Kusoma na Ufahamu: Fitina ni Mzigo

   Soma hadithi ifuatayo ili ujibu maswali uliyopewa chini yake.

   Hapo zamani za kale kulikuwepo marafiki wawili: Simba na Sungura. Hawa walikuwa marafiki wa kufa na kupona kwa miaka mingi tangu utotoni mwao. Simba alikuwa anampenda rafiki yake kwa undani na kila siku alikuwa tayari kumsaidia kwa tendo alilolitekeleza. Wakati huo wote hawa wawili walikuwa tayari kujipatia jiko. Lakini, kwa kweli Sungura alikuwa anampaka mafuta kwa mgongo wa chupa huyo rafiki yake. Kwani Sungura alikuwa na malengo mengine mabaya dhidi ya rafikiye Simba.

   Simba alikuwa na mchumba mrembo sana, binti aliyependwa na vijana wengine kutokana na urembo wake. Vijana wengi walikuwa wakimzunguka kama sisimizi wazungukavyo mafuta. Atembeapo njiani vijana walimtazama kwa macho ya upole kwani wote walimmezea mate. Wengine walipomwona walikuwa wakimtamania kwa kuyatia maneno yao chumvi na kusema: “anang’aa kama dhahabu”.

   Kijana Simba alikuwa na kazi nzuri ya kulinda usalama mjini. Kazi hiyo haikumpendeza rafiki yake Sungura kutokana na tabia yake ya fitina. Hivyo basi, alikaa chini na kuanza kupanga kisirisiri ili kijana Simba apigwe kalamu mahali alipokuwa akifanyia kazi. Alitumia hila zote ili kumchonganisha na mkuu wa kazi; yaani mkuu wa walinzi wa usalama mjini pote. Kwa kuwa Kijana Simba alikuwa akifanya kazi yake vizuri na kupendwa na mkuu wake wa kazi, mipango ya Sungura haikumwathiri kwa namna yoyote. Sungura alikasirika na kuwaza namna ya kumwangusha. Yeye alifikiria kuwa binti mpenzi wake alimpenda kwa sababu ya kazi nzuri aliyokuwa nayo.

   Siku moja kijana Sungura, kama kawaida, alipita nyumbani kwa kijana Simba kumpa salamu zake. Wakati huo alimkuta amelala fofofo kitandani mwake. Sungura alirudi haraka nyumbani kwake kuleta pombe kali aliyokuwa amenunua kwa ajili ya sherehe ya kufunga mwaka. Kitambo alifika kwa Simba na kuweka vinywaji hivyo karibu na kitanda chake. Kwa kweli vinywaji vilikuwa vingi na vya aina tofauti kwani vinywaji vingine alimwaga chini. Hapo alianza kumpiga picha rafikiye Simba akiwa anasinzia usingizi mnono. Baadaye, aliiba suti yake aliyokuwa akiivaa katika sherehe maalumu akiwa na kipenzi chake.

   Asubuhi, kijana Simba alipoamka alishangaa kuona kwamba pombe imemwagwa sakafuni na chumba chake kinanuka. Alimwita rafiki yake Sungura aje amwonyeshe yaliyompata. Alipofika hapo, Sungura naye alishikwa na bumbuazi. Alimwahidi kwamba angemsaidia kutafuta aliyetenda maovu hayo ili waweze kumshitaki mahakamani. Alipokata tamaa kufikiria aliyekuwa adui yake aliweka mavazi yake ya kikazi na kuanza kuelekea kazini. Alipofika kazini, aliitwa ofisini na kiongozi wake na kuulizwa maswali mengi kuhusu mwenendo wake wa ulevi. Kwa hakiki, taarifa yote ilikuwa imemfikia mkuu wake wa kazi na aliyoyauliza yalikuwa na uthibitisho. Kijana Simba alishangaa kuona hali hiyo na kuanza kujitetea. Kiongozi alipoona hamwelewi alimwonyesha gazeti moja lililokuwa limetangaza habari hizo na picha zimeambatishwa. “Nani huyu?”. Kiongozi akamuuliza.

   Simba alijaribu tena kueleza kwamba hakufahamu aliyemfanyia mipango hiyo. Baada ya kiongozi wake kuona kwamba ilikuwa njama iliyopangwa na adui yake alimsaidia kupeleka malalamiko yake kwenye kituo cha polisi. Miezi miwili baadaye, kipenzi chake alikuwa ameanza kutembea na Sungura. Yeye alihakikisha kwamba angekuwa na aibu kubwa ya kutembea na aliyekuwa rafiki yake mlevi. Sungura alifurahi sana na kuanza kumsengenya Simba kwa maneno yenye ukali! Wewe ulijifanya tajiri na ukajiona ni kipenzi cha msichana mrembo kama yule! Acha uone …. Mjinga wewe! Simba alishangaa kuyashuhudia aliyokuwa akitendewa na Sungura ambaye alikuwa rafikiye wa kufa na kupona. Kwa hakika alifikiria kuwa ndiye angechukua nafasi ya kwanza kumfariji katika shida zote alizokutana nazo. Lakini “Mungu yu mwema kila wakati!” Mapenzi ya Sungura na binti huyo hayakudumu muda mrefu. Mwezi mmoja ulipopita Polisi walikuwa wameshatambua aliyekuwa na hatia. Sungura alipelekwa gerezani akafungwa kifungo cha mwaka mzima kutokana na vitendo vyake vibaya. Aidha, alilazimishwa pia kulipa faranga elfu hamsini za Rwanda kwa kosa la wizi.

   Kijana Simba alimshukuru mkuu wake wa kazi kwa kutotilia maanani yaliyosemwa na Sungura. Zaidi ya hivyo, alimshukuru kwa kumsaidia kuendesha kesi yake mpaka akagunduliwa aliyejihusisha na vitendo vya kumpaka masizi na kumwaibisha. Binti aliyekuwa rafiki yake, alimuomba radhi Simba. Urafiki wao ukaanza upya. Baada ya miezi miwili, walifunga pingu za maisha. Sasa hivi wanaishi kwa amani kama mume na mke. Zaidi ya hivyo, Simba amepandishwa cheo kazini kwake kutokana na uchapa kazi.

   Maswali ya ufahamu

   1. Taja wahusika wanaozungumziwa katika kifungu hiki.

   2. Sungura alikuwa na tabia gani?

   3. Kwa sababu gani Sungura hakumpenda Simba?

   4. Kwa sababu gani vijana wengi wanampenda binti aliyekuwa mchumba wa

   Simba?

   5. Kuna uhusiano gani kati ya kichwa cha habari na kifungu cha habari ? Toa

   maelezo.

   6. Je, Simba alifukuzwa kazini ? Eleza.

   7. Sungura alifanya nini ili Simba afutwe kazi?

   8. Kwa nini Simba alishangaa kuona mabaya aliyokuwa akitendewa na Sungura?

   9. Kwa nini mapenzi kati ya binti yule na Sungura hayakudumu?

   10. Kwa nini Sungura aliadhibiwa ? Alipewa adhabu gani?

   11. Ni mafunzo gani unayoyapata kutokana na kifungu hiki cha habari?

   13.2 Msamiati kuhusu Nahau

   Zoezi la 2: Toa maelezo ya msamiati ufuatao kutoka kifungu cha habari hapo

   juu, kisha utunge sentensi kwa kutumia maneno hayo.

   1. Kushuhudia

   2. Fitina

   3. Mchumba

   4. Mrembo

   5. Kulewa

   6. Kukata tamaa

   7. Njama

   8. Bumbuazi

   9. Kuomba radhi

   10. Kung’aa 

   Zoezi la 3: Tumia mshale kwa kuhusisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.


   13.3 Sarufi: Nomino za Ngeli ya LI-YA na Vivumishi vya Pekee

   Zoezi la 4: Chunguza sentensi zifuatazo ili kueleza aina za maneno

   yaliyopigiwa mstari:

   1. Mwalimu kwa kuandika andalio la somo lake alitumia lengo lenye maana kamili

   2. Niliongea na makundi yenyewe bila kutuma watu wengine.

   3. Kwenye hotuba ya kiongozi wa wilaya yetu, mambo yote yanatuhimiza kuwa na

   tabia ya kufundisha watoto wote bila ubaguzi wowote.

   4. Nyumba yake iliporomoka baada ya kujengwa kwa sababu ya kutumia mawe

   yote bila kuchagua mawe mazuri.

   5. Mzee wangu anamaliza kujenga jengo lingine/jingine mjini. 

   Maelezo muhimu

   Vivumishi vya –enye huonyesha hali ya “kuwa na” na” kumiliki”.

   -enyewe hutumiwa katika sentensi kuonyesha jambo au kitu kinachotarajiwa.

   • -ote huonyesha kila sehemu ya kitu hasa katika umoja (mfano: kundi lote

   limewasilisha kazi ) na kuonyesha kila kitu(mfano: makundi yote yamewasilisha

   kazi.)

   • -o-ote huonyesha mojawapo ya vitu au baadhi ya vitu bila kubagua.

   • -ingine : kivumishi hiki kinaonyesha kitu tofauti na kile kilichotajwa au kilichopo,

   kuonyesha kitu zaidi / nyongeza, na kuonyesha «baadhi ya».

   • -ingineo ni» zaidi ya» na kuonyesha hitimisho ya orodha ambayo haikukamilika.

   • Vivumishi -enye, -enyewe, -ote, o-ote, katika ngeli ya LI-YA huchukua

   konsonanti l- na y- katika wingi.

   Vivumishi -ingi, -ingineo katika ngeli ya LI-YA huchukua konsonanti j- au lkatika umoja na kiambishi me- katika wingi.

   Zoezi la 5: Tunga sentensi tano kwa kutumia nomino za ngeli ya LI-YA pamoja na vivumishi vya pekee: enye, enyewe, ote, o-ote, ingine.

   Zoezi la 6: Andika sentensi zifuatazo kati wingi

    Umoja                                                      Wingi

   1. Gari lenye magurudumu makubwa.    ……………………………….....

   2. Jiwe lenyewe ni hili.                             ……………………………….....

   3. Tamasha lote lilikuwa nzuri.                 ……………………………….....

   4. Kundi lolote linapaswa kujitayarisha.   ……………………………….....

   5. Alifua koti lingine.                                 ……………………………….....

   6. Kamati yote imefika.                              ……………………………….....

   13.4 Matumizi ya Lugha: Nahau

   Nahau ni semi zinazotofautiana na maana yake ya nje. Huwa ni semi zenye

   mvuto na utamu wa lugha. Nahau huundwa kwa lugha ya kawaida, kwa

   kuashilia wazo la picha kutoka katika hali halisi ya maisha, ambazo aghalabu

   huwa ni misemo ambayo mtumiaji huitumia katika maazungumzo au

   maandishi bila kujua kuwa anaitumia.

   • Nahau ni msemo wa picha ambao huwa na maana iliyofichika. Nahau huwa

   na undani wa kimaana kuliko baadhi ya misemo inayopatikana katika lugha

   fulani. Kutumia semi hizi kunaonyesha kuwa mtumiaji wa lugha amepevuka

   katika lugha kwani ufafanuzi wa picha zilizomo unahitaji ujuzi mkubwa wa

   lugha

   Zoezi la 7: Kwa ushirikiano na wenzako, jadilini kuhusu semi (nahau) zifuatazo katika sehemu A na maana zake katika sehemu B, kisha mtunge sentensi kwa kutumia nahau hizo.


   13.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

   Zoezi la 8: Kwa ushirikiano na wenzako, jadilini kuhusu maana na matumizi ya

   nahau zifuatazo:

   1. Kuchemsha bongo

   2. Kuchongea mtu

   3. Kubeza mtu

   4. Kuchungulia kaburi

   5. Kufafanua kinaga-ubaga

   13.6 Kuandika: Utungaji wa Kifungu cha Habari

   Zoezi la 9: Tunga kifungu cha habari ambacho kinadhihirisha matumizi ya

   nahau zisizopungua tano. 

   Baadhi ya nahau mnazoweza kutumia na maana zake.

   1. Kuchukua sheria mkononi: kulipiza kisasi kwa jambo baya

   2. Kuenda aste aste: kuenda pole pole / taratibu

   3. Kuenda chapu chapu: kuenda haraka

   4. Kuenda kasi: kuenda haraka haraka

   5. Kufanya hila: kutenda jambo la udanganyifu

   6. Kufanya masihara / mizaha: kutenda mambo kwa mchezo

   7. Kufanya uchuro: hali ya kuwa na kisirani ; mkosi

   8. Kufanya utani: kufanya mzaha au mchezo

   9. Kufanya uzohali:kuwa na uvivu; kuzembea

   10. Kufuja mali: kuharibu mali, kutumia pesa vibaya

   11. Kufunga virago: kuondoka; kusafiri

   12. Kugaragara kitandani: kugeukageuka kitandani

   13. Kujifungua mtoto: kuzaa kwa mwanamke

   14. Kukata kamba: kufariki

   15. Kukaza kamba: kujitahidi

   16. Kula chumvi nyingi: kuishi miaka mingi

   17. Kula kiapo: kuapa

   18. Kumpa mtu heko: kupongeza mtu

   19. Kumpa mtu mgongo / kisogo: kufanyia mtu mambo yaliyo kinyume na

   matarajio

   20. Kumpa mtu nyama ya ulimi: kumpa mtu maneno matamu

   21. Kuona cha mtemakuni: kujuta; kupata adhabu kali

   22. Kuona kilichomnyima nyoka miguu: kupata adhabu kali

   23. Kuona kilichomnyima kanga manyoya: kupatwa na ubaya

   24. Kupanda mbegu za chuki: kuchochea watu wachukiane

   25. Kupiga marufuku: kukataza kitu kisheria

   26. Kuvunja mbavu: kuchekesha; kufanya au kusema maneno yanayochekesha

   27. Kuvunja nyumba: kuharibu hali ya maisha baina ya mume na mke

   Muhtasari wa Mada

   Mada hii ya pili” Lugha katika Sanaa” ina vipengele sita yaani masomo makuu sita

   yanayohusiana na mada husika. Kila somo lina vipengele vidogo kama vile: mchoro,

   kifungu cha habari, maswali ya ufahamu, matumizi ya msamiati, matumizi ya lugha,

   kusoma na kuandika, sarufi, na maelezo muhimu. Somo la kwanza linaeleza maana

   ya sanaa, aina ya sanaa na zana za sanaa. Somo la pili linaeleza maana ya fasihi.

   Somo la tatu linaeleza kuwa vipawa vinasaidia jamii kwa kukuza utamaduni na

   kujipatia pesa. Somo la nne linaeza maana ya fasihi katika fasihi simulizi, aina ya

   fasihi, na umuhimu wake katika jamii. Somo la tano linaeleza maana ya methali,

   matumizi ya methali, muundo, na umuhimu. Somo la mwisho linaeleza maana ya

   nahau, umuhimu wa nahau katika jamii, na badhi ya nahau na maana yake.

   TATHMINI YA MADA YA PILI

   Jibu maswali yafuatayo

   1. Toa mfano wa hadithi kutoka jamii ya Wanyarwanda inayosimulia kuhusu mambo ya

   ushujaa.

   Hadithi huishia kwa fomula gani?

   2. “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Jadili

   3. Toa mfano wa methali inayoweza kutumiwa wakati mtu fulani ameshindwa kutimiza

   aliyoyasema?

   4. Eleza nahau zifuatazo:

   a. Kupigwa kalamu

   b. Kumpa nyama ya ulimi

   5. Tunga kifungu chenye maneno yasiyopungua 300 kwa kuzingatia mambo muhimu

   yanayojitokeza katika utanzu wa fasihi. Hakikisha kwamba umetumia nomino

   zisizopungua tano za ngeli ya LI-YA kwa kupiga msitari chini yake.

   a. Maana ya sanaa

   b. Aina mbalimbali za sanaa

   a. Umuhimu kazi za kisanaa kwa binadamu

   b. Fasihi simulizi na umuhimu wake katika jamii

   c. Nafasi ya fasihi katika kuimarisha amani na kukomesha utengano katika jamii. 


   • MADA NDOGO: MUHTASARI, FANI NA MAUDHUI KATIKA HADITHI ZA MASIMULIZI

    Uwezo upatikanao katika mada

    Kuelewa na kufuata mtindo wa kuandika muhtasari wa hadithi aliyoisikiliza au kuisoma; kuchambua hadithi za Kiswahili kwa kuzingatia fani na maudhui yanayojitokeza katika hadithi; kusimulia hadithi rahisi za masimulizi; kujua mabadiliko ya kisarufi katika matumizi ya majina ya ngeli ya PA-M-KU

    Malengo: 

    Baada ya mada hii, mwanafunzi atakuwa na uwezo wa:

    • Kuchambua hadithi mbalimbali za Kiswahili kutokana na ujuzi wa uchambuzi

    aliopata.

    • Kutoa tathmini ya hadithi aliyochambua kulingana na mtindo maalum wa

    uhakiki aliofuata.

    • Kusimulia tena hadithi aliyowahi kusimuliwa au kuisoma.

    • Kuandika muhtasari wa hadithi aliyoisoma au kuisikiliza.

    • Kutunga na kusahihisha sentensi sahihi kwa kuzingatia matumiziya majina ya

    ngeli ya PA-M-KU-.

    Kidokezo 

    Chagua hadithi moja unayoijua katika Kiswahili au katika lugha nyingine. Fikiria muhtasari wake kisha jadili mambo yafuatayo:

    Simulia kwa kifupi hadithi yoyote uliyowahi kuisoma

    Umezingatia nini ili uweze kuisimulia hadithi hiyo kwa kifupi?

    Unaelewa nini na muhtasari?

    Kwa maoni yako, uhakiki wa kazi ya fasihi ni nini?

    Ni mambo gani muhimu yanayozingatiwa kuihakiki hadithi simulizi?

    SOMO LA 14: MAANA YA MUHTASARI NA SIFA ZAKE


    Zoezi la 1: Tazama kwa makini picha zilizopo hapo juu, baadaye zizungumzie kwa mwongozo ufuatao:

    1. Unaona nini kwenye picha hizi?

    2. Unafikiri picha hizi zinaonyesha nini?

    3. Picha hizi zinakukumbusha nini katika maisha yako ya kifasihi?

    14.1 Kusoma na Ufahamu: Umoja ni Nguvu, Utengano ni Udhaifu 

    Soma kifungu cha habari kinachofuata kuhusu «Umoja nI nguvu, utengano ni udhaifu», kisha jibu maswali uliyopewa hapo chini.

    Hapo zamani za kale palikuwa na mzee mmoja na jina lake ni Sebahire. Alikuwa anaishi katika kijiji kiitwacho Chapakazi. Palikuwa mahali pazuri, safi na pakuvutia sana. Nyirabagenzi alikuwa mkewe Sebahire. Sebahire na Nyirabagenzi walibahatika kupata watoto watano. Wavulana watatu watanashati na wasichana wawili warembo sana. Tegemeo la wanakijiji hiki cha Chapakazi lilikuwa kulima mashamba madogo madogo na kufuga mifugo mbalimbali kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku kwa uchache .

    Jitegemee alikuwa kifungua mimba wa mzee Sebahire na Nyirabagenzi. Yeye alikuwa anafanya juu chini katika shughuli zake za kilimo na ufugaji ili apate mapato mengi zaidi ya kutunza familia yake na yale ya kupeleka sokoni hapo kijijini kwao na hata nje ya kijiji. Kutokana na juhudi zake, Jitegemee alifaidika sana. Yeye alikuwa tajiri lakini alikuwa kila kukicha akisikika akisema, “Eti, ningekuwa na mtu mwingine mwenye bidii kama mimi katika familia yangu, sote nyumbani tungefaidika sana na kuishi vyema”. 

    Mugeni aliamua kushirikiana bega kwa bega na kaka yake Jitegemee. Kitambo, ndugu hawa wawili walikuwa wameshafaidika sana na kupiga hatua nzuri za kimaendeleo. Walikuwa mfano mzuri kwa vijana wenzao na hata wanakijiji wote kwa ujumla.

    Ndugu watatu waliobaki, walikuwa ni mzigo mkubwa kwa wazazi wao. Hawakufuata mawaidha na maonyo ya wazazi hata ndugu zao wengine. Badala ya kuchapa kazi kama ndugu zao, Jitegemee na Mlegevu zoezi lao lilikuwa la kuzururazurura na kulala usiku na mchana bila mpango. Hali hii iliwahuzunisha wazazi wao hata na wazee wengine katika kijiji hicho cha Chapakazi. 

    Miaka nenda rudi, mzee huyu alizidi kuzeeka na kupungukiwa na nguvu. Alifika katika hali ambayo macho yake hayakuona vyema na hata masikio yake hayakusikia. Mgongo wake ulipinda na vidole vya mikono yake kila mara vikatetemeka kama mtu ambaye ameugua malaria. Licha ya hali hii ngumu, mawazo ya mzee Sebahire yalikuwa yanazunguka juu ya watoto wake hususan wale ambao walikuwa wanaaibisha familia yake. 

    Asubuhi moja, Sebahire aliwaita watoto wake wote watano na kuwaonya kuhusu ukweli wa maisha. “Wanangu, niliwalea katika hali ya umaskini hohehahe, bila mshahara wowote wala mifugo. Nilikuwa nikitegemea shamba lile dogo tu. Kilichoniwezesha kuwatunza ni umoja timamu uliokuwepo kati yangu na mama yenu. Kila asubuhi mapema tulikuwa tukiamka kuelekea shambani hadi saa saba za mchana”, mzee Sebahire aliwasimulia watoto wake. Vijana nao wakatingisha vichwa vyao kama ishara ya kuelewa. 

    Baada ya hayo, aliwatolea fimbo tatu zilizokuwa zimefungwa na Kamba kwa pamoja. Kwanza alimwita Jitegemee na kumwomba azivunje bila kuzitenganisha. Kijana huyo alikuwa mwenye nguvu sana. Alijaribu iwezekanavyo lakini kazi bure. Baada ya kushindwa, zoezi lilimfikia Mugeni. Huyu alikuwa mwenye nguvu kuliko kaka yake wa kwanza. Alijaribu kwa uwezo wake na kutumia mbinu zote lakini hakufaulu. Kulikuja mtoto wa tatu Rulinda. Alikuwa anawashinda ndugu zake wote kwa nguvu. Alifika na kuchukua fimbo hizo na kujaribu kuzivunja. Kwa mara ya kwanza hakuweza, mara ya pili akaamua kutumia magoti. Kwa bahati mbaya na mbinu hii ya mwisho haikuzaa matunda.


    Baada ya mtihani huu mgumu, mzee Sebahire alizichukua fimbo na kuzitenganisha moja kwa moja. Alimpatia fimbo mtoto wa nne na wa tano na kuwaomba wazivunje. Hawa walifanikiwa kwa urahisi. Mzee aliwaambia watoto hao, “Wanangu, nawaomba mshirikiane bega kwa bega. Mkiwa na umoja hakuna adui yeyote atakayewaingilia na kuwatendea mabaya wala kuwachonganisha. La sivyo, utengano wenu utawaletea hasara kubwa ya kuvunjika kama ilivyotokea kwenye fimbo hizi.


    Watoto wake walimshukuru baba yao na kuchukua uamzi wa kushirikiana milele na milele katika maisha yao ya kila siku. “Ndugu zangu, tegeni sikio mawaidha yangu: Tukishirikiana katika kazi za kilimo katika shamba letu iwapo ni dogo bila shaka tutasikika matajiri ulimwenguni mzima”, Jitegemee aliwaambia ndugu zake. 

    Miongoni mwa ndugu zake wazembe, kijana mmoja alisimama na kuhakikisha, ”Tungelishirikiana toka mwanzoni ni kweli tungelitajirika. Kwa bahati mbaya tuliongozwa na roho mbaya ya kudharauliana pamoja na kutosikilizana. Hasara tuliyo nayo leo ni kubwa sana. Kwa hiyo ningewaomba kutosahau methali isemayo kuwa umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.”

    Maswali ya ufahamu 

    Zoezi la 2: Baada ya kusoma kifungu cha habari kwa ufasaha, jibu maswali ya ufahamu yafuatayo:

    1. Familia ya mzee Sebahire ilikuwa inaishi katika kijiji kipi?

    2. Ni watu gani wanaozungumziwa katika hadithi hii?

    3. Watoto wa mzee Sebahire na mkewe Nyirabagenzi walikuwa katika makundi

    mawili tofauti ya kitabia. Je, unakubaliana na ukweli huu? Eleza msimamo wako.

    4. Mzee sebahire alitumia picha katika kulinganisha umoja na utengano. Tetea

    msimamo huu.

    5. Baada ya mashauri kutoka kwa baba yao, watoto hawa waliamua nini?

    6. Kama mwanafunzi, ni ujumbe gani ambao umeupata kutoka hadithi hii?

    7. Husisha kichwa cha hadithi na yaliyomo katika hadithi. 

    14.2 Matumizi ya Msamiati wa Msingi 

    Zoezi la 3: Baada ya kutoa maana ya maneno yafuatayo, yatumie katika sentensi zako binafsi.

    1. Kifunguamimba

    2. Juhudi

    3. Mawaidha

    4. Kutingisha

    5. Maskini

    6. Kutenganisha

    7. Kuchonganisha

    8. Timamu

    9. Uamuzi

    10. Maendeleo

    Zoezi la 4: Tumia mshale kwa kuoanisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.


    14.3 Sarufi: Usanifishaji wa Majina ya Ngeli ya pa- m- ku

    a. Sebahire na Nyirabagenzi walikuwa wanaishi mahali pazuri, safi na patakatifu.

    b. Mahali hapa ni pachafu

    c. Mjini humu mna mahali pazuri pa kutembelea.

    Zoezi la 5: Tazama maneno ambayo yameandikwa kwa rangi ya kukoleza kisha ujibu maswali yafuatayo:

    1. Katika aina za maneno ulizojifunza, maneno haya ni ya aina gani?

    2. Yanabeba dhana gani?

    Neno mahali na pahali ni maneno yanayowekwa katika ngeli ya majina iitwayo PAM- KU. Vivumishi vya sifa huanzwa na Pa- kama ifuatavyo:

    Pahali pachafu pamefagiliwa.

    Mahali pabaya panaepushwa.

    Mahali patakatifu panatembelewa sana.

    Mahali pazuri panapendeza

    Mahali papana pamepandwa miti ya kuhifadhia mazingira.

    Mahali pafupi panaonekana kwa urahisi.

    Mahali papya pamejengwa nyumba za kisasa.

    Mahali padogo panaingiwa na watu wachache

    Tanbihi : Kiswahili sanifu hakiruhusu matumizi ya pa- kwenye kivumishi cha sifa safi.

    Kwa hiyo hatusemi wala hatuandiki mahali pasafi. Usanifishaji wake ni mahali safi.

    Zoezi la 6: Sahihisha sentensi zifuatazo kwa kuzingatia matumizi bora ya vivumishi vya sifa.

    1. Sipendi kutembea mahali mabaya yasipo na mazingira bora.

    2. Nchini Rwanda kuna pahali mzuri pa kutembelea.

    3. Nilimkuta katika baa, mahali kubaya sana.

    4. Mukamana hapendi kukaa mahali mchafu.

    5. Wakiristo wa makanisa tofauti huomba Mungu mahali takatifu.

    Zoezi la 7: Chagua jibu sahihi kati ya yale ambayo yamewekwa katika mabano.

    1. Rukundo atatembelea mbuga za wanyama. Ni mahali ……. (kuzuri, pazuri, mzuri)

    2. Tunapaswa kuishi mahali ……………. (pasafi, safi, kusafi)

    3. Si vizuri kulala mahali …………… (mbaya, kubaya, habaya, pabaya) kwa sababu

    panaweza kuharibu maisha yako.

    4. Mahali …………. (mchafu, chafu, pachafu, kuchafu) huweza kuambukiza

    maradhi.

    5. Mahali …………… (patakatifu, takatifu, kutakatifu) hupatikana katika nchi

    chache duniani. 

    14.4 Matumizi ya Lugha: Muhtasari 

    Zoezi la 8: Kwa ushirikiano na wenzako, someni tena kifungu cha habari hapa juu kuhusu “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”. Toeni muhtasari wake kimazungumzo na kimaandishi. Baadaye mjibu maswali yafuatayo:

    1. Muhtasari wa habari ni nini ?

    2. Kwa maoni yako, mhutasari mzuri una sifa gani ?

    Maelezo muhimu: Maana ya muhtasari

    Muhtasari ni taaluma ya kufupisha sentensi au habari bila kupotosha wazo au mawazo ya awali ya msemaji au mwandishi.

    Sifa za muhtasari mzuri 

    • Unapaswa kuwa na mawazo makuu yanayoeleweka.

    • Mhutasari mzuri unapaswa kuwa si zaidi ya theluthi moja ya kifungu cha habari chote.

    • Lugha inayotumiwa ni lazima iwe lugha ya mkato.

    • Mhutasari unaweza kuwa katika aya moja au nyingi.

    • Muhtasari mzuri unapaswa kumwezesha msikilizaji au msomaji kupanua msamiati. 

    Zoezi la 9: Kwa mwongozo wa maelezo hapo juu fanya muhtasari wa kifungu hiki cha habari cha hapo chini kwa njia ya maandishi na masimulizi. 

    Sungura na Mamba 

    Hapo zamani mamba alikuwa na meno mazuri sana. Wanyama wengi waliyapenda meno yake. Baadhi yao walisikia wakitia chumvi kuwa meno ya mamba yalikuwa na thamani sawa na dhahabu. 

    Mamba huyo alipotangaza nia yake ya kujipatia jiko karibu kila mnyama aliyekuwa na binti mzuri alitaka binti yake aolewe naye. Hivyo mabinti wengi walionekana wakijipitisha mbele ya mamba huku mmoja akiwa amejipamba vizuri ili kuweza kuliteka penzi lake.

    Hali hiyo haikumpendeza kabisa Sungura. Kwani miongoni mwa hao wasichana waliojitokeza, alikuwepo mmoja aliyependwa sana na Sungura. Hivyo, Sungura wakati wote alikuwa akiwaza la kufanya ili kumwangusha Mamba. 

    Siku moja Sungura alipita nyumbani kwa Mamba, na kumkuta amelala fofofo chini ya kivuli cha mti huku meno yake mazuri yakionekana waziwazi. Hapo Sungura aliweza kuyaona maganda mengi ya karanga na akagundua kuwa Mamba alikuwa akitafuna karanga. 

    Siku nyingine Sungura alikuja tena nyumbani kwa Mamba. Akamwambia, “Rafiki yangu nimekuchukulia zawadi nzuri uipendayo.’’Zawadi gani?” “karanga”, alijibu Sungura huku akimwonyesha mamba mfuko uliojaa karanga. 

    Mamba alipouona mfuko huo, aliurukia mfuko akaliingiza domo lake refu ndani na kuanza kutafuna kwa pupa. ‘‘Mama wee !’’ Mamba alisikika akilia huku mikono yake akishikilia mdomo wake ambao sasa umejaa damu. Meno yake mengi yaling’oka pia. Kumbe ndani ya mfuko ule Sungura aliweka mawe mengi na njugu nyasa chache tu. Mamba alipojaribu kutafuna alichofikiria kuwa ni karanga, meno yake mengi yaling’oka. Sungura alipoona mbinu yake imefaulu, aliondoka na kuelekea kwake kwa furaha. 

    Siku hiyo jioni, wanyama wengi walishangaa kumuona Sungura alikuwa amevaa miwani na kupepesuka ovyo. Kumbe alikuwa akisherekea ushindi wake dhidi ya mamba.

    Habari za Mamba kung’olewa meno yake zilienea kwa haraka sana. Wasichana wote walipopata habari hizo, walibadilisha mawazo yao ya kutaka kuolewa na Mamba ambaye sasa alikuwa kibogoyo na kuchukiza sana.

    14.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Ufupishaji

    Zoezi la 10: Tega sikio kwa makini kifungu cha habari ambacho umesomewa au umesimuliwa. Fanya muhtasari wake kimazungumzo na kimaandishi.

    Zoezi la 11: Kwa ushirikiano na wenzako, jadili masuala yafuatayo :

    1. Kuna umuhimu gani wa wanafamilia kuishi kwa umoja na ushirikiano??

    2. Ni matendo gani muhimu tunayohimizwa kama wanafunzi kuyafanya ili tuimarishe umoja wetu shuleni na nyumbani?

    14.6 Kuandika: Uandishi wa Muhtasari

    Zoezi la 11: Angalia sifa za muhtasari mzuri, kisha utunge aya moja ambayo inazieleza wazi


    SOMO LA 15: TARATIBU ZA KUTOA MUHTASARI MZURI

    Zoezi la 1: Soma habari hii kwa makini na kujibu maswali yanayofuata: 

    Mzee Sebahire na mkewe Nyirabagenzi waliishi katika kijiji cha Chapakazi. Walikuwa na watoto watano. Mzee huyo alikuwa anawashauri watoto wake kufanya kazi kwa bidii. Wawili walifuata nyao ya baba yao, wengine watatu walikuwa wazembe. 

    Siku moja, mzee Sebahire aliwaita watoto wake na kuwaonya kuhusu ukweli wa maisha. Aliwaambia kwamba wanapaswa kuwa na umoja. Aliwaletea fimbo zilizokuwa zimefungwa kwa pamoja na kuwaomba kuzivunja. Walijaribu lakini wote walishindwa. Baadaye Mzee Sebahire alifumbua fumbo lake kwa kuzitenganisha fimbo hizo na kuwaomba vijana wake kuzivunja moja kwa moja. Kazi hii ikawa rahisi kwao. Mzee aliwaelezea sababu ya kielelezo hiki cha fimbo, na kuwaonya kuongozwa na umoja kati yao pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

    Maswali

    1. Kifungu cha habari hiki kinahusu nini?

    2. Toa maoni yako kutetea msimamo wako

    Zoezi la 2: Linganisha kifungu cha habari «Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu» na hiki hapo juu kwa kuzingatia mambo yafuatayo:

    1. Tofauti au uhusiano baina ya vifungu vya habari hivi viwili.

    2. Urefu wa kifungu cha habari

    3. Mtiririko wa visa

    4. Yaliyomo

    5. Matumizi ya lugha

    15.1 Kusoma na Ufahamu: Mchango Wangu 

    Soma kifungu cha habari kuhusu “Mchango wangu” kisha jibu maswali yanayofuata hapo chini

    Zamani za kale palikuwa na familia nzuri iliyokuwa na watu wanne hodari sana. Gatete alikuwa baba na Kamaliza mama. Watoto wao walikuwa Mucyo na Muhoza. Familia hii ilikuwa inaishi katika kijiji cha Bananeza. Ilikuwa ina upendo mkubwa baina yao na dhidi ya majirani wote. Majirani wote walikuwa wanaisifu sana familia hii. Nyumbani kwa familia hii kulitawaliwa na amani, usafi, adabu, uhifadhi wa mazingira, uzalendo, ushirikiano, na utu.


    Wazazi hawakusahau mara kwa mara kusisitizia tabia ya umoja na ushirikiano kwa watoto wao. Walikuwa wanakubali kuwa kuishi kwa amani na utulivu hutegemea tabia ile. Watoto walifuata vyema maadili ya wazazi wao. 

    Mucyo na Muhoza walikuwa wanasoma katika shule ya Sekondari ya Bananeza. Walionyesha ubingwa katika masomo yao na kushirikiana ana kwa ana na wanafunzi wenzao. Walikuwa marafiki na kijana aitwaye Gakire. Familia ya kijana huyu ilikuwa jirani ya familia yao. Kila siku walikuwa wanakwenda na kutoka shuleni pamoja.


    Siku moja, Muhoza na Mucyo walipokuwa wametoka shuleni, walizungumzia maisha yao ya kila siku nyumbani kwao. Walimwelezea Gakire kwamba familia yao ilikuwa inaishi kwa amani bila utengano. Kwa upande wake,

    Gakire aliwasimulia rafiki zake juu ya maisha ya familia yake. “Nyumbani kwetu tunaishi maisha mabaya. Wazazi wangu kila siku huwa wanagombana na hawakubaliani kamwe katika mipango yote ya familia. Tunaishi katika hali ya malalamiko kutokana na fitina isiyo kifani. Mara nyingi wazazi wangu humaliza wiki nzima bila kuwasiliana,’’ Gakire aliwaelezea rafiki zake. 

    Aliposikia jinsi familia ya Gakire ilivyokuwa inaishi, Mucyo alisikitika sana. Alimwambia Gakire, “Pole sana kwa maisha hayo! Nyumbani kwako ni tofauti sana na kwetu. Je, tunaweza kukusaidia nini?” 

    “Ingawa bado hatuwezi kufanya mabadiliko yoyote kutokana na umri wetu lakini ni lazima tuchukue uamuzi. Mchango wetu kama watoto ni kuiombea dua familia yenu ili iwe na uelewano kati ya wazazi wako”, aliongeza Muhoza. 

    “Dadangu Muhoza, hayo tu hayatoshi. Kumbuka yale tuliyojifunza kuhusu dalili za itikadi ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yaliyotokea nchini humu! Fitina hiyo hukua na kuzaa kitu kibaya sana. Ndiyo sababu tunapaswa kuwaarifu wazazi wetu hali hiyo ili tushirikiane kuzuia ukatili wowote unaoweza kuiletea balaa familia ya mwenzetu Gakire”, alisisitiza Mucyo. Walipofika karibu na nyumbani kwake Gakire, walimwaga na kumwacha. Walimwahidi kutimiza wajibu waliokuwa wamezungumzia. 

    Walipofika nyumbani kwao, Mucyo na Muhoza waliwaelezea wazazi wao hali mbaya ya familia ya rafiki yao. Waliwaomba wazazi kuitembelea familia ya Gakire na kuishauri kuacha ugomvi huo. Gatete na mkewe walipigwa na bumbuazi kwa kusikia habari hii. Waliwaambia watoto wao kuwa siku moja suala hili litatatuliwa bila shaka. Wakati wa usiku, Gatete na mkewe walijadiliana kuhusu mbinu za kutumia kurejesha amani katika familia ya jirani yao. Walikubaliana kutumia watoto wao kama njia ya utatuzi wa suala hili. 

    Asubuhi, wazazi waliwaita watoto wao na kuwaambia “ Watoto wapendwa, masikitiko yenu kuhusu familia ya rafiki yenu Gakire yanaeleweka wazi. Tumelizungumzia suala hili na kukubaliana kuwa nyinyi watoto mtakuwa chanzo cha suluhisho la kudumu katika familia ile.” 

    “Hilo litawezekana je?”, Mucyo alimwuliza baba yake. Baba yake alijibu,”Leo mkitoka shuleni, nendeni pamoja na Gakire nyumbani kwake. Mimi na mama yenu tutawakuta pale jioni”. 

    Baada ya masomo, marafiki wote walitoka shuleni pamoja kama kawaida. Mucyo na Muhoza walimsindikiza Gakire hadi nyumbani. Waliwakuta wazazi wake Gakire nyumbani kule. Mama yake Gakire aliwakaribisha na kuwaletea chakula. Hakumwuliza mtoto wake Gakire wenzake hao ni nani kwa sababu alikuwa anawajua wazi wazazi wao.

    Karibu saa kumi na mbili za jioni, Gatete na mkewe waliwasili hapo. Waliwasalimu watoto pamoja na wazazi wake Gakire. Wazazi wa Gakire walifurahia sana ziara ya majirani hao lakini walijiuliza sababu yake. “Kwa nini majirani hawa wamekuja hapa pamoja na watoto wao?”, walikuwa wakifikiri. 

    Hapo hapo, Gatete na mkewe walipata fursa ya kuwaomba baba Gakire na mama yake kukaa pembeni mbali ya watoto na kuongea. “Samahani kuwatembelea bila kuwaarifu. Tumekuja kwa ajili ya masikitiko yaliyotufikia kutoka kwa watoto wetu. Tulihuzunishwa sana na kupata habari kuhusu hali ya migogoro inayoongoza familia yenu. Ni athari kubwa kwa utulivu wa mtoto wenu pamoja na watoto wetu kama marafiki. Kwa hiyo tumekuja pamoja na watoto kutoa mchango wetu. Je, mnaweza kutuelezea sababu za umoja wenu kuzorota?”, wageni walitoa maoni yao. 

    Mwanzoni baba yake Gakire hakuonyesha nia ya kujadili suala hili. Kadiri mawasiliano yalivyokuwa yamesonga mbele, bwana alibadilika kimawazo na kukubali kutoboa siri ya mzozo huo. Baada ya kutega sikio, wazazi wa pande mbili walitoleana mawaidha ya kuleta upya usikilivu mwema katika familia hiyo ya majirani. 

    Mwishoni mwa majadiliano, wazazi waliwaita watoto wao na kuwatolea matokeo ya mkutano wao. Watoto waliifurahia sana hatua hiyo ya kurudisha amani na umoja katika familia husika. Toka siku hiyo, familia ya wazazi wake Gakire ilirekebisha tabia mbaya zote za utengano. Leo ni mojawapo ya familia zenye utulivu tele katika kijiji cha Bananeza.

    Maswali ya ufahamu

    Zoezi la 3: Baada ya kusoma kifungu cha habari kwa makini, jibu maswali ya ufahamu yafuatayo:

    1. Habari hii imetokea wapi?

    2. Ni watu gani wanaozungumziwa katika hadithi hii?

    3. Ni tatizo gani la msingi linalojadiliwa hadithini?

    4. Ni malengo yapi yaliyokuwa yanatawala katika familia ya Gatete na mkewe?

    5. Mucyo, Muhoza na Gakire walikuwa marafiki sana. Tetea msimamo huu.

    6. Ni sifa gani unazopata kutoka Gatete na mkewe? Eleza.

    7. Watoto wanaweza kutoa mchango wao katika njia ya amani na umoja katika familia yao. Husisha ukweli huu na yaliyozungumziwa katika hadithi.

    8. Kutokana na upatanisho uliofikiwa katika familia ya wazazi wake Gakire, unadhani ni matendo gani yaliyofanywa ili familia hii iishi katika utulivu tele? 

    15.2 Matumizi ya Msamiati wa Msingi 

    Zoezi la 4: Eleza maana ya maneno yafuatayo kulingana na muktadha wa matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma. Kisha tunga sentensi zako kwa kutumia maneno haya:

    1. Kusifu

    2. Utulivu

    3. Kupambana

    4. Dua

    5. Jirani

    6. Kurekebisha

    7. Chanzo

    8. Ugomvi

    9. Kudumu

    10. Kuwasili

    Zoezi la 5: Unganisha sehemu A kwa sehemu B.


    15.3 Sarufi: Nomino za Ngeli ya PA- M- KU na Vivumishi vya Kumiliki

    a. Mahali kwenu ni tofauti sana na mahali kwetu.

    b. Mahali kwako ninapajua

    c. Nyumbani kwao kuna watoto

    d. Pahali pangu panajulikana

    • Maneno kama : kwangu, kwenu, kwetu, kwako, kwao ni vivumishi vya kumiliki vya ngeli ya PA- M-KU-. 

    Mifano katika sentensi


    Zoezi la 6: Tazama maneno hapa juu ambayo yameandikwa kwa rangi na kujibu maswali yafuatayo:

    1. Katika aina za maneno ulizojifunza, maneno haya ni ya aina gani?

    2. Yanabeba dhana gani ?

    Zoezi la 7: Chagua jibu sahihi kati ya yale ambayo yamewekwa katika mabano

    1. Mimi ninaishi mahali pazuri. Mahali (changu, kwangu, pao) panafurahisha.

    2. Mukaneza anapenda kulala pahali safi. Pahali (kwangu, pake, kwao) ni safi.

    3. Tunatembea mahali panapopendwa na watu kadhaa. Mahali (yetu, kwetu, yao) panajulikana.

    4. Wanafunzi wangu husomea mahali papana. Mahali (yangu, mwao, kwetu) ni pazuri pa kusomea.

    5. Mtoto yule analala mahali panapopendwa na wazazi wake. Mahali (yako, kwake,yetu) panapendwa na wazazi. 

    15.4 Matumizi ya Lugha:Taratibu za Kutoa Muhtasari Mzuri

    Zoezi la 8: Soma tena kifungu cha habari “Mchango wangu” na kujibu maswali haya:

    1. Toa muhtasari wake kimazungumzo na kimaandishi.

    2. Kwa maoni yako, ni taratibu gani ulizozitumia ili ufanye muhtasari wa kifungu

    hiki?

    Taratibu za kutoa muhtasari mzuri

     • Kusoma habari husika zaidi ya mara moja ili kuweza kuielewa.

    • Ni lazima kuzingatia mawazo makuu na kuyaandika.

    • Kuchagua au kuteua mambo muhimu au kiini cha habari huku tukijiepusha na maelezo ya ziada, mifano, vielezi au tamathali za usemi.

    • Hakikisha kwamba maneno yote ya maana yaliyokusudiwa na makala au habari ya awali yamebaki.

    • Hakikisha pia kwamba muhtasari wako una urari au mfuatano mzuri wa mawazo.

    • Zingatia urefu wa muhtasari unaohitajika.

    • Kuandika kwa mtiririko mambo muhimu tuliyoyateua kwa hati nadhifu. 

    Zoezi la 9: Kwa njia ya maandishi na masimulizi, andika kifungu cha habari kisha ukifanyie muhtasari 

    15.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadaliano 

    Zoezi la 10: Tega sikio kwa makini vifungu vya habari vinavyowasilishwa na wenzako darasani. Chagua kifungu kimoja na ukitolee muhtasari wake kimazungumzo na kimaandishi.

    1. Nini umuhimu wa kuishi katika familia yenye maelewano mazuri?

    2. Ni hasara gani kwa familia iishiyo katika hali ya vurugu?

    3. Kama watoto, ni mchango upi tunaoweza kutoa katika kuimarisha amani, umoja na maridhiano katika familia zetu?

    4. Kulingana na historia ya Rwanda kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, ni dalili zipi za itikadi ya mauaji ya kimbari tunazotakiwa kuepukwa? 

    15.6 Zoezi la Kuandika: Utungaji wa Hadithi Fupi  

    Zoezi la 12: Kwa kutumia vivumishi vya kumiliki vya majina ya ngeli ya Pam-ku, tunga hadithi fupi kisha uitolee muhtasari mzuri.


    SOMO LA 16: FANI KATIKA HADITHI SIMULIZI 

    Zoezi la 1: Kumbuka hadithi simulizi moja unayojua katika Kiswahili au katika lugha nyingine. Uwasimulie wenzako kisha jadili kwa pamoja maswali yafuatayo:

    1. Hadithi simulizi hii inabeba ujumbe gani?

    2. Ni wahusika gani wanaopatikana katika hadithi hii?

    3. Mtambaji au mwasilishaji ameitumiaje lugha ya masimulizi?

    16.1 Kusoma na Ufahamu: Urithi wa Wazazi

    Soma kifungu cha habari kinachofuata kuhusu “Urithi wa Wazazi”, kisha jibu maswali yaliyopo hapo chini

     Zamani za kale palikuwa na familia moja ya mzee Furaha na mkewe Shukuru. Wao walibahatika kuwazaa watoto watatu. Faida alikuwa kifunguamimba, Kagabo pamoja na Fikiri aliyekuwa kitindamimba. 

    Familia hii ilikuwa inaishi mahali penye matatizo kadhaa. Kila mahali palikuwa na malalamiko kutokana na mateso ya njaa. Mzee Furaha alikuwa anatumia muda mrefu kufikiri jinsi familia yake ingeliweza kupambana dhidi ya ufukara uliokuwa umeshamiri katika familia yake. Kila usiku alikuwa anajiuliza mwenyewe, “Ni njia ipi nitakayoitumia kuokoa familia yangu?” Jibu kwa swali hili bado lilikuwa halipatikani siku nenda rudi. 

    Siku moja kulitokea ndege mmoja ambaye alikuja na kutua juu ya mti pembeni mwa nyumba ya mzee Furaha. Ndege huyu alianza kuimba na Mzee Furaha akamsikia. Wimbo wa ndege huyu ulikuwa ufuatao: 

    “Swi swi swi! Mzee Furaha nakuletea ujumbe wa utajiri. Swi swi swi! Njoo karibu ya mti usikilize ujumbe wangu wa kuiokoa familia yako dhidi ya umaskini.” 

    Mzee Furaha aliukaribia mti na kutega sikio. Ndege aliendelea na wimbo wake, “Swi swi swi! Mimi ni mjumbe kutoka nchi ya Utajiri. Mahali pale ni tofauti na huku. Kwetu hakuna njaa. Lakini mahali humu watu wengi wameteseka sana kwa ukosefu wa chakula.”


    Alipoyasikia hayo, mzee Furaha alijihisi mdundo wa ngoma moyoni mwake na kumuuliza ndege, “Mpendwa ndege, ni njia gani ya kupitia na kuelekea katika nchi hiyo? Samahani nifumbulie!” 

    Ndege alicheka sana na kusema, “Swi swi swi! Ukiviona vinaelea vimeundwa! Utajiri hautoki hewani. Utajiri unapiganiwa. Utajiri unafichuliwa. Mwisho utajiri unarithiwa.” 

    Mzee Furaha hakuelewa kamwe fumbo la ndege. Alimuuliza, “Unamaanisha kwamba nichukue silaha na kwenda kugombania utajiri?” “Ndiyo, lakini silaha yako iwe: heshimu kazi yoyote bila upendeleo, usikate tamaa katika matatizo na halafu watendee mema wengine.” Ndege alimwonya mzee Furaha. 

    Mzee Furaha alimuuliza ndege, “Maonyo mawili ya mwisho nitajaribu. Lakini lile la kwanza la kuiheshimu kazi yoyote bila upendeleo sioni utekelezaji wake rahisi ambapo sijawahi kuajiriwa hata siku moja toka nizaliwe.” 

    “Ni kweli, hujapata kazi na hilo ninalijua sana. Lakini haimaanishi kuwa kazi haiko.” Ndege alihakikisha. “Huku na kule nchini kuna ardhi yenye mbolea. Ardhi hii ingelitumiwa katika kazi za kilimo ingelizaa matunda mengi na kuinua familia yako. Tatizo kubwa ni hili: mnalidharau zoezi la kilimo na ufugaji na kutegemea tu msaada kutoka mahali pasipojulikana. Mzee Furaha, hiyo si haya kweli kwa familia kama yako yenye mikono na akili kuishi katika mateso ya ufukara? Tokea leo nakuomba ufikiri kikamilifu. Nenda ukalime shamba lako, panda mahindi hapa na pale, kisha subiri kitakachotokea baadaye.” 

    Mzee Furaha alifurahia shauri hilo na kumshukuru sana ndege kwa msaada huo. Baada ya ndege kuruka na kurudi kwake, mzee Furaha alimwita mkewe na kumsimulia kisa cha ndege aliyewatembelea.

    Mkewe aliunga mkono mpango uliotolewa na ndege na kumwahidi mumewe kushirikiana bega kwa bega. Punde si punde mbegu za mahindi zilikuwa zimepandwa na baada ya mwaka mmoja mavuno yalikuwa yameanza kubadili mambo mengi katika familia ya mzee Furaha na mkewe Shukuru. Mwaka mmoja baadaye, Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Wakimbizi kutoka nchi jirani lilikuja kwa mzee Furaha na kuweka sahihi kwenye makubaliano ya kununua mahindi yote kwa bei ghali sana.


    Familia ya mzee Furaha ilitajirika sana na kujulikana mahali kote nchini kama familia iliyoendelea kwa njia ya kilimo cha mahindi. Watoto wote watatu wa mzee Furaha na Shukuru walibahatika kulipiwa karo za kwenda kusomea nje ya nchi katika vyuo vikuu vinavyojulikana kwa kutoa mafunzo ya hali ya juu katika sayansi na teknolojia. Wao walirudi baadaye pamoja na vyeti vyao vya ngazi ya juu. Majirani zake, wa mbali na karibu, watoto yatima, walemavu, wajane na watu wote waliokuwa katika hali mbaya ya kimaisha walipata huduma kutoka familia hii. Kwa kweli, familia hii ilitawaliwa na usikivu mwema, huruma na upendo kwa watu wote waliokuwa wanaiomba huduma. 

    Siku moja Mzee Furaha na mkewe Shukuru walipanga sikukuu ya kufurahia hali ya maisha waliyokuwa nayo. Walitayarisha chakula na vinywaji na kuwaalika majirani wote. Walipokaribia mwisho wa sherehe, Mzee Furaha alisimama na kuwaomba wote kumtega sikio. “Ukiviona vinaelea vimeundwa.”

    Methali hii niliifundishwa siku moja na ndege mjumbe ambaye alinifungua macho.” Mzee Furaha alisema. Aliwasimulia kisa chote cha ndege mjumbe na jinsi ujumbe wake ulivyotekelezwa. 

    Wakati huo, Mzee alipata fursa ya kuwaita watoto wake na kuwapatia urithi wa utajiri alioupata kutoka kwa ndege mjumbe. “Watoto wangu, mnajua kuwa nilifanya iwezakanavyo ili mjifunze, mpate akili, muwe wasomi na wataalamu katika mambo muhimu ya kuendeleza jamii yetu. Huo ungekuwa urithi wenu. Lakini urithi wa kweli ambao ningetaka mhifadhi moyoni ni huu ufuatao: heshimu kazi yoyote bila upendeleo, usikate tamaa katika matatizo halafu ongozwa na moyo wa kuwatendea wengine mema. Huu ndio urithi mimi na mama yenu tunaowapatia leo.

    ” Watoto na waalikwa kwenye sherehe hiyo walimpigia makofi mzee Furaha kwa urithi huo. Wote waliahidi kuunga mkono na kuukuza katika familia zao kama desturi nzuri ya kuendelezwa nchini kote. Huu ndio mwisho wa hadithi.

    Maswali ya ufahamu

    1. Taja wahusika wote wanaozungumziwa katika kifungu cha habari.

    2. Kifungu cha habari hiki kinabeba ujumbe gani?

    3. Kifungu hiki cha habari kinaweza kuwekwa katika utanzu upi wa fasihi simulizi?

         Eleza msimamo wako.

    4. Ni tatizo gani lililokuwepo na kumleta ndege mjumbe kwa mzee Furaha?

    5. Unadhani tatizo hilo lilikuwa limesababishwa na nini?

    6. “Ukiviona vyaelea vimeundwa”. Husisha methali hii na kifungu cha habari.

    7. Mzee Furaha aliwapatia urithi wa aina tatu zifuatazo: akili, utajiri pamoja na utu.               Je, unakubaliana na kauli hii? Tetea msimamo wako.

    8. Kumbuka ujumbe uliotolewa na ndege. Je, mzee Furaha aliuzingatia?                                  Eleza jibu lako kulingana na yaliyojitokeza katika kifungu cha habari.

    16.2 Matumizi ya Msamiati wa Msingi 

    Zoezi la 2: Baada ya kutoa wewe binafsi maana ya msamiati ufuatao na kuchunguza maana yake kamili katika Kamusi sanifu ya Kiswahili, utumie katika kutunga sentensi fupi.

    1. Urithi

    2. Kitindamimba

    3. Kuonya

    4. Uahidi

    5. Kuhifadhi

    6. Kutekeleza

    7. Kukuza

    8. Kupata fursa

    9. Kuangamiza

    Zoezi la 3: Jaza sentensi zifuatazo kwa kutumia msamiati kama vile: karo, mtoto yatima, mjane, walemavu, bei ghali, maonyo.

     1. ………........……ni watu wa kuheshimiwa kama watu wengine. Wanapaswa kupewa haki zao na kuhudumiwa kisheria bila ubaguzi wowote. 

    2. Aliyefiwa na wazazi wake huitwa...……………. lakini aliyepoteza mumewe huitwa…………………………… 

    3. Urithi bora kwa mtoto leo ni akili. Kwa hiyo kila mzazi ana wajibu wa kuwalipia watoto wake .........................…………. za shule. 

    4. Mwanafunzi yeyote ambaye anafuata ………….................… ya wazazi wake pamoja na walimu wake huwa na mwenendo mwema. 

    5. Amenunua vifaa vya nyumbani kwa…………………………….. 

    Zoezi la 4: Bainisha nahau au misemo pamoja na methali zilizotumiwa katika hadithi “Urithi wa wazazi” 

    Zoezi la 5:Husisha A na B kwa kuzingatia maana ya nahau au misemo husika.


    16.3 Sarufi: Usanifishaji wa Majina ya Ngeli ya PA-M-KU

    Hapa na kule palikuwa panajulikana malalamiko kutokana na mateso ya njaa.
    Mahali pale ni tofauti na huku. Kwetu hakuna njaa. Lakini mahali humu watu wengi wameteseka sana kwa ukosefu wa chakula.

    Zoezi la 6: Tazama maneno yaliyokolezwa hapo juu na kujibu maswali haya: 

    1. Maneno haya ni ya aina gani? 

    2. Yamehusishwaje na majina yanayoambatana nayo? 

    Maelezo muhimu 

    • Maneno kama vile hapa, pale, kule, humu, humo, huko ni vivumishi vya kuonyesha. Vimeambatana na maneno yenye dhana ya mahali au maeneo kama vile mahali, nchini, mezani, n.k. Kundi la majina haya huunda majina ya ngeli ya PA-M-KU. 

    • Matumizi ya vivumishi hivi vya kuonyesha huchukua mofimu pa-, m- pamoja na ku- kulingana na umbali wa eneo kitu au mtu anakopatikana. 

    Kwa mfano


    Tazama sentensi hizi:

    • Mahali hapa ni pazuri.

    • Mahali hapo pamejulikana sana kwa usalama wa kutosha.

    • Mahali pale paliendelezwa na wananchi wenyewe.

    • Nchini humu mna amani na usalama.

    • Chumbani humo mnatayarishiwa nini?

    • Shuleni kuleku mefundishwa masomo ya umoja na maridhiano.

    Zoezi la 7: Chagua jibu sahihi kati ya haya yaliyowekwa katika mabano.

    1. Mahali ………….. (humu, hapa, kule) panaitwa Umoja wetu.

    2. Darasani…………(pale, mle, huku) mnaonekana uchafu.

    3. Barabarani…….. (kule, humu, pale) kumewekwa ndoo za taka.

    16.4 Matumizi ya Lugha: Kuikabili Fani katika Hadithi Simulizi 

    Zoezi la 8: Soma tena kifungu cha habari “Urithi wa wazazi”. Chunguza kwa makini mambo yafuatayo:

    1. Maana ya fani katika hadithi

    2. Aina ya wahusika wanaojitokeza hadithini pamoja na tabia zao

    3. Mahali au mandhari hadithi ilipotokea

    4. Muundo na mtindo wa hadithi

    5. Lugha aliyoitumia msanii wa hadithi.

    Mambo muhimu ya kuchunguza katika kuikabili fani katika hadithi simulizi 

    Fani ni nini? 

    Fani ni ufundi au mbinu anayoitumia msanii wa fasihi ili kutoa au kufikisha ujumbe kwa watu aliowakusudia. 

    Ni mambo gani muhimu yanayozingatiwa katika fani ya hadithi simulizi? 

    Katika fani vipengele muhimu vifuatavyo hutiliwa mkazo.

    1. Wahusika 

    Wahusika ni watu, wanyama, vitu, hata viumbe vya kufikirika ambavyo msanii wa hadithi hutumia ili kufanikisha ujumbe kwa jamii husika. Katika hadithi msanii huwagawa wahusika katika makundi mawili: wahusika wakuu na wahusika wadogo. Wahusika wakuu ni wale ambao wanajitokeza kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa hadithi na ndio huwa msingi wa hadithi husika. Wahusika wadogo ni wale wote ambao wanajitokeza mara chache au sehemu mbalimbali katika kazi ya fasihi na huwasaidia wahusika wakuu katika kubeba maudhui. maudhui.

    Wahusika katika hadithi za masimulizi hutegemea aina ya hadithi simulizi. Kwa mfano: 

    Ngano: Hadithi ambayo wahusika wake ni kama wanyama, wadudu, mizimu, miungu, miti, watu, na viumbe visivyo na uhai kama mawe, miamba, n.k. 

    Hekaya: Hadithi ambayo wahusika wake kwa kawaida ni binadamu, au mchanganyiko wa binadamu na wanyama au viumbe vingine, pia Mungu na miungu. 

    Hurafa: Hadithi ambazo wahusika wake huwa ni wanyama wanaopewa tabia na vitendo vya kibinadamu. 

    Visasili: Hadithi hizi hutumia wahusika wa aina mbalimbali pamoja na miungu na binadamu.

    Soga: Hizi ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Wahusika wake ni watu wa kubuni lakini wanapewa majina ya watu walio katika mazingira hayo. 

    Visakale au Migani: Ni hadithi ambazo wahusika wake ni watu waliotenda matendo ya kishujaa na wanaosifiwa katika jamii fulani. 

    Tabia za wahusika katika hadithi za masimulizi 

    Wahusika katika hadithi simulizi hupewa tabia za aina mbalimbali. Kwa mfano:

    • Wahusika wanaosimamia binadamu utawakuta wakionyesha tabia tofauti (tabia nzuri kama vile utu, umoja, upole, upendo, n.k. pamoja na tabia mbaya kama vile uchoyo, uvivu, ukatili, wivu, n.k.) 

    • Kwa upande mwingine, wanyama kama wahusika hupewa tabia kama ifuatavyo:

    Sungura: Mara nyingi Sungura hupewa tabia za ujanja, ndiyo sababu huonekana mahali pengi kama Sungura-mjanja. Kwa hiyo, Sungura huwakilisha watu wenye ujanja kwa madhumuni ya kula jasho la wengine, kuwaangamiza adui zao au kuwaangusha mtegoni pamoja na kuwategua wanyama wakubwa kama vile simba. 

    Simba: Mnyama huyu hutumika mara nyingi kama kiongozi au mfalme. Katika familia ya binadamu huwakilisha watu wenye ukali katika jamii, ambao wakiongea husikika na huogopewa sana. 

    Fisi: Mnyama huyu huonekana kama mhusika mwenye tamaa na ulafi ambaye fikra zake zimetawaliwa na tamaa yake. Pia fisi hupewa tabia ya uchoyo, woga pamoja na ujinga. Fisi hutumika kuwakilisha wanadamu woga, wazembe na wajinga, wasiopenda kufikiria sana kwani mawazo yao yametawaliwa na tamaa zao. 

    Nyani: Katika hadithi, nyani hudhihirisha hekima na uwezo wa kufanya uamuzi wa busara. Hutumika sana kama hakimu na huwakilisha viongozi wenye hekima katika jamii. 

    Nyoka: Mnyama huyu hupewa tabia ya hila na huwakilisha watu wenye hila katika jamii. 

    Kobe: Huwakilisha watu wanyamavu, ambao japo wanajua kufanya kitu, hawapendi kuchangia, lakini mwisho huibuka washindi; watu wasiokimbilia kufanya mambo. 

    Ndovu: Huwakilisha watu wenye kimbelembele, ambao hujisifu na kujitafutia umaarufu. Watu wa aina hii hupenda kuwa katika mstari wa mbele japo huenda hawana ujuzi wa kutosha katika jambo hilo.

    2. Mtindo 

    Mtindo ni mbinu ya kipekee kwa kila msanii katika ufundi wake wa kifasihi. Kwa mfano, namna msanii anavyotumia lugha, anavyoteua msamiati wa msingi, namna anavyosimulia hadithi yake (anaweza kutumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu, anaweza kutumia nyimbo kwa ajili ya burudani, n.k.).

    3. Muundo 

    Ni mpangilio wa kiufundi anaoutumia msanii katika kupangilia zoezi lake, mpangilio na mtiririko wa hadithi, kwa upande wa visa na matukio. Kuna aina mbili za kupangilia matukio kama vile:

     - Msago

    Ni namna ya moja kwa moja ya kusimulia matukio, yaani kuanzia tukio la kwanza hadi la mwisho kwa namna yalivyotukia. Huu ni muundo wa moja kwa moja.

     - Urejeshi

    Ni usimuliaji wa kurukaruka hatua, yaani msimuliaji anaweza kuanzia katikati, akaja mwisho na kumalizia na mwanzo 

    4. Mandhari 

    Ni sehemu ambayo matukio ya hadithi au masimulizi hutokea. Mandhari huweza kuwa halisi kama vile nyumbani, baharini, njiani, msituni, kijijini, mjini au ya kufikirika kama vile kuzimuni, mbinguni, peponi n.k. 

    5. Lugha 

    Lugha ndiyo wenzo mkubwa wa msanii katika kazi za fasihi. Miongoni mwa vipengele vya lugha ni tamathali za usemi pamoja na semi. 

    Semi 

    Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:

    Nahau- Ni usemi unaotumia maneno ya kawaida kwa lengo la kufikisha maana iliyo tofauti na maana ya kawaida ya maneno hayo. Kwa mfano: kutega sikio ; Kupiga makofi, kupiga magoti, kwenda haja ndogo, kwenda haja kubwa, n.k. 

    Misemo- Ni fungu la maneno litumiwalo na jamii ya watu kwa namna maalumu ili kusimamia maana fulani. 

    Kwa mfano: punde si punde, kushirikiana bega kwa bega, siku nenda rudi, n.k.

    16.5 Kusikiliza na Kuzungumza : Usimuliaji wa Hadithi na Majadiliano 

    Zoezi la 9: Tega sikio hadithi fulani uliyopewa. Bainisha wahusika, eleza sifa zao, lugha iliyotumiwa, mandhari pamoja na muundo na mtindo. 

    Zoezi la 10: Toa hadharani muhtasari wa hadithi hiyo pamoja na kuzungumzia fani yake. 

    Zoezi la 11: Kwa ushirikiano na wenzako, jadilieni maswala yafuatayo: 

    1. Ni sababu gani zinazoweza kuiangusha familia fulani katika umaskini? 

    2. Ni sifa gani zinazotakiwa kwa mfanyakazi ili kumudu kazi yake na kuizalisha matunda? Eleza kwa ufupi. 

    16.6 Utungaji: Utungaji wa Hadithi 

    Zoezi la 11: Buni hadithi yako binafsi kwa kuzingatia sifa zote za fani zilizozungumziwa.

    SOMO LA 17: MAUDHUI KATIKA HADITHI SIMULIZI 

    Zoezi la 1: Kumbuka hadithi simulizi “Urithi wa wazazi”. Isimulie hadharani kisha ueleze ujumbe unaojidhihirisha kutoka hadithi hiyo. 

    17.1 Kusoma na Ufahamu: Mbayuwayu na Kobe


    Hapo zamani za kale palikuwa na Kobe na Mbayuwayu. Kobe alikuwa mnyamavu, mshindani pamoja na mtaratibu. Kila wakati alikuwa hafanyi jambo lolote hovyo hovyo wala kwa pupa. Kwake, kila kitu kilikuwa na mpango wake kabla ya kuingia matendoni. 

    Kwa upande mwingine, Mbayuwayu alikuwa ndege mpinzani, mjuaji, mpuuzi na mwenye majivuno. Wakati mwingi alikuwa anafanya kazi bila mpangilio, yaani bila tarajio. 

    Siku moja Kobe na Mbayuwayu walikutana wakisherehekea arusi ya mtoto wa Mfalme Simba. Walikuwa wamekaa pamoja. Kwa hiyo, walipata fursa ya kuongea sana. Sherehe ilipokuwa imeendelea, Kobe alishangaa sana kumwona Fisi amekuja akikimbia mno. Alikuwa amechelewa kuhudhuria sherehe. Kobe hakuamini macho yake na kumwonyesha Mbayuwayu, “Angalia pale jinsi Fisi anavyokimbia kwa mwendo mkali. Ameharakisha kasi mithili ya gari katika mashindano. Bila shaka hakuna mnyama hata ndege yeyote anayeweza kumshinda katika mashindano ya riadha.


    Mbayuwayu hakuridhika kamwe na maoni hayo ya Kobe kuhusu Fisi. Mara moja alimgeukia na kumuuliza kwa dharau, “Je, una hakika kwa hayo yote ambayo umeyatamka? Nani aliyekuambia kuwa Fisi yule anaweza kuthubutu kunishinda mimi? Kama wewe ni mlemavu wa miguu na mabawa usidhani kuwa sisi sote ni sawasawa na wewe.

     Kobe alijaribu kumshawishi akisema, “Samahani rafiki yangu! Hii siyo sababu ya kukasirika bure! Ukweli mtupu ni kwamba mimi ninaamini kwamba Fisi anaweza kunishinda katika zoezi la mashindano ya kukimbia. Lakini, wewe sahau hilo! Huwezi, huwezi na huwezi kamwe! Maishani mwangu wanyama wawili pamoja na ndege mmoja ndio niwaogopao katika mashindano ya namna hii. Hao ni Fisi, Sungura pamoja na kunguru. Wengine hapana!” 

    Mbayuwayu alivimba na kumwambia mwenzake, “Huna haya kuhakikisha hayo mbele yangu? Tusingelikuwa hapa mbele ya mfalme ningelikufunza sana!” Kobe hakutaka kuendelea kutia chumvi wala kuliacha jambo hili lipambe moto. Hivyo aliamua kutoa suluhu la kimatendo. “Acha tukubaliane kwenye mashindano ya kukimbia kilomita mbili wakati wa dakika sitini. Atakayeibuka mshindi ndiye atakayekuwa kiongozi mheshimiwa kati yetu.” Kobe alipendekeza. 

    Bila kusitasita, Mbayuwayu alikubaliana na Kobe hivi wakiamua siku, mahali pamoja na wakati wa mashindano. Sherehe iliendelea kama ilivyopangwa; lakini, Kobe hakupata tena utulivu. Alikuwa ameanza kufikiri juu ya mbinu atakazotumia kujinyakulia ushindi dhidi ya Mbayuwayu.

    Siku moja kabla ya mashindano kutokea, Kobe alikaa peke yake na kufikiri. “Wazazi wangu kabla ya kuaga dunia, walinitolea maonyo ambayo sitayasahau hata siku moja. Wakati mmoja waliniambia ‘Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako’ na Wakati mwingine ‘bandubandu humaliza gogo’.” Kobe aliyakumbuka mashauri ya wazazi. Kutokana na haya, Kobe alijiambia moyoni mwake, “Linalowezekana leo lisingoje kesho”. Hapo hapo aliamua kuandaa matembezi yake asubuhi mapema. 

    Saa kumi na mbili asubuhi alikuwa ameishatoka nyumbani kwake kuelekea mahali pa mashindano. Njiani alimkuta nyoka na kumsalimu. Nyoka alimwuliza, “Je, unaelekea wapi?” “Kijiji kimoja, tarafa ya Maendeleo”, Kobe alimjibu nyoka. “katika Kijiji kipi mnapatikana tarafa hiyo?” Nyoka alimwuliza tena. “Kijiji kimoja kiitwacho Ushindi.” Kobe alijibu. “Unakwenda kufanya nini pale?” Nyoka aliendelea.

    Kobe aligundua kuwa ni hila la nyoka kupiga soga. Alimwambia “Tafadhali, acha niendelee na safari yangu. Kama una nia ya kushiriki nami, njoo baadaye utanikuta barabarani”. “Barabarani kupi?” Aliuliza Nyoka lakini Kobe hakutaka kuendelea na mawasiliano hayo. 

    Kobe alitembea, akatembea na kutembea. Saa nane za mchana, Kobe alikuwa amesogelea mti mkubwa ambapo alikuwa amekubalina na Mbayuwayu kuwa kikomo cha mashindano. Wakati huo ndipo Mbayuwayu alikumbuka kuwa siku hiyo ilistahili kuwa siku ya mashindano kati yake na Kobe. Alishtuka kwa ghafla na kuruka haraka kwa mwendo usio wa kawaida. Aliruka na kuruka! Lahaula! Alipokuwa umbali wa mita karibu mbili, Kobe alikuwa amejinyakulia ushindi, hivi akishangilia kwa furaha tele.


    Mbayuwayu alipomwona Kobe alipoteza nguvu za kuendelea kuruka na kuanguka chini. Kobe alisikia huruma moyoni na kumsogelea Mbayuwayu, “Pole sana ndugu yangu. Katika mashindano ni lazima kuwepo mshindi na mshindwa.

    Lakini siyo mwisho wa dunia. Somo kubwa kutokana na mashindano haya ni kwamba uwezo mkubwa wa kuruka pekee hautoshi, jambo muhimu zaidi ni maandalizi, akili na maarifa ya kufanikisha lengo lolote”. 

    Mbayuwayu aliona haya na kufunga mdomo wake. Baada ya dakika chache, aliamka na kumwambia Kobe, “Leo nimeona kuwa kila kitu kinawezekana maishani. Sina budi kukubali ushindi wako kwa sababu asiyekubali kushindwa si mshindani. Nimepiga saluti kwa heshima zako mheshimiwa.”

    Maswali ya ufahamu

    1. Taja wahusika wote wanaozungumziwa katika kifungu cha habari.

    2. Kifungu cha habari hiki kinabeba ujumbe gani?

    3. Msanii alifauluje kufikisha ujumbe wake kwa jamii?

    4. Fananisha tabia za wahusika waliozungumziwa hadithini.

    5. Kwa nini Kobe alijinyakulia ushindi dhidi ya Mbayuwayu?

    6. “Wakati una mabawa”. Husisha methali hii na hadithi hii.

    7. Ni somo gani ambalo umelipata kutoka hadithi hii?

    17.2 Matumizi ya Msamiati wa Msingi 

    Zoezi la 2: Baada ya kutoa wewe binafsi maana ya msamiati ufuatao na kuchunguza maana yake kamili katika Kamusi sanifu ya Kiswahili, utumie katika kutunga sentensi fupi.

    1. Mbayuwayu

    2. Tarajio

    3. Mpuuzi

    4. Majivuno

    5. Kuandaa

    6. Kasi

    7. Riadha

    8. Ghafla

    Zoezi la 3: Jaza sentensi zifuatazo kwa kutumia msamiati kama vile: kuharakisha, kuhudhuria, tele, budi, kukiri.

    1. Wanafunzi hawana ……….... kukubali matokeo ya mtihani wowote.

    2. Waalikwa wengi walikuja ………………… sherehe za mwaka mpya.

    3. Viongozi waliulizwa maswali ……………. uhusu hatua za kupigana dhidi ya umaskini pamoja na rushwa.

    4. …………… kosa ni sifa muhimu kwa kila binadamu.

    5. Tunapaswa ………….. kazi yetu ili imalizike kwa wakati.

    Zoezi la 4: Orodhesha methali zote zilizotumiwa katika hadithi “Mbayuwayu na Kobe” na kuzitolea maana yake. 

    Zoezi la 5: Husisha A na B kwa kuzingatia maana ya nahau husika.


    Zoezi la 6:

    1. Kamilisha methali zifuatazo

    2. Zitolee maana yake

    3. Zihusishe na zile za Kinyarwanda unazojua

              • …………………. utamkuta mtoto si wako

              • Bandu bandu…………………………………..

              • ……………………………lisingoje kesho

              • Wakati una…………………………………….

              • Asiyekubali kushindwa………………………….

    17.3 Sarufi: Usanifishaji wa Majina ya Ngeli ya PA-M-KU

    Zoezi la 7: Tazama maneno yaliyotiliwa mkazo na kujibu maswali haya :

    1. Maneno haya ni ya aina gani?

    2. Yanahusishwaje na majina ambatana?

    Nyoka alimwuliza, “Je, mahali papi unapoelekea?”

    Mambo muhimu ya kuchunguza katika kuyakabili maudhui katika hadithi simulizi 

    Nini maana ya maudhui? 

    Katika kazi ya fasihi maudhui ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi yake ya kifasihi. 

    Mambo muhimu yanayozingatiwa katika maudhui ya hadithi simulizi 

    Katika maudhui vipengele vifuatavyo ni lazima vizingatiwe: dhamira, migogoro, falsafa, ujumbe pamoja na msimamo wa msanii.

     1. Dhamira 

    Dhamira huelezwa kama wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Kwa kawaida, dhamira zinagawika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo. 

    a. Dhamira kuu: Ni kiini cha wazo kuu la msanii ambalo linaongoza ujumbe autakao msanii kufikisha kwa jamii. Dhamira kuu huweza kuhusu jamii, siasa, uzalendo, uchumi, ushirikiano, utajiri, ufukara, malezi bora, mapenzi, n.k. 

    b. Dhamira ndogondogo: Ni zile dhamira mbalimbali zinazogusiwa na msanii ili kuendeleza dhamira kuu. Dhamira hizi huja kuunga mkono dhamira kuu katika mbinu yake ya kujidhihirisha.

    2. Migogoro 

    Migogoro ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi za fasihi. Migogoro inaweza kuwa kati ya wahusika, familia zao, matabaka yao, au hata katika nyadhifa mbalimbali. Vilevile migogoro yaweza kuwa ya kiuchumi, kijamii, migogoro ya nafsi, migogoro ya kisiasa, n.k. 

    3. Falsafa 

    Kimsingi, falsafa ni elimu ya asili; busara au hekima. Falsafa ya msanii hugusiwa kutokana na jinsi anavyoelewa matatizo ya jamii na jinsi anavyoyatolea suluhisho kwa njia ya busara, amani na utulivu.

    4. Ujumbe 

    Kila kazi ya sanaa huwa na ujumbe maalumu ambao msanii anataka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi za kifasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana ndani ya kazi hiyo. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi wakati ambapo dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi. 

    5. Msimamo wa msanii 

    Katika kazi ya fasihi, mawazo au dhamira, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Misimamo hiyo hujitokeza wakati msanii anapoamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Kwa hiyo itakuwa balaa kwa kazi ya sanaa ambayo msanii wake ni kigeugeu, yaani haonekani akishikilia msimamo fulani. 

    UHUSIANO WA FANI NA MAUDHUI 

    Fani na maudhui ni dhana mbili ambazo hazitenganiki. Kimoja hutegemea kingine ili kazi ya fasihi iweze kuwa bora zaidi. Kazi ya fasihi ambayo maudhui yamezidi fani huwa chapwa au fani ikizidi maudhui, kazi hiyo ya fasihi huwa chapwa, hivyo maudhui na fani ni dhana ambazo hutegemeana. Fani na maudhui lazima vilingane na kushabihiana ili kazi yenyewe iweze kuwa bora na yenye mvuto zaidi. 

    Tukichukua mfano wa barua, itaeleweka wazi kuwa barua ikiandikwa ovyoovyo bila mpango pamoja na makosa tele ya kisarufi pamoja na ya kintaksia, vilevile itakuwa vigumu sana kwa ujumbe kupatikana kwa urahisi. Ndiyo sababu wataalamu wengi wa fasihi hulinganisha fani na maudhui kama roho na mwili, gari na injini, mwili na moyo, n.k. Kwa ukosefu au ulegevu wa kimoja kingine hakiwezi kuwa na ubora wake.

    17.5 Kusikiliza na Kuzungumza : Usimuliaji wa Matukio na Majadiliano 

    Zoezi la 10: Tega sikio hadithi ambayo umepewa. Bainisha dhamira kuu, ujumbe, migogoro, falsafa pamoja na msimamo wa msanii. 

    Zoezi la 11: Zungumzia haya yote mbele ya darasa. Zoezi la 12: Kwa ushirikiano na wenzako, jadili misimamo ifuatayo kulingana na ukweli wa maisha ya jamii ya leo:

    • Muda ni mali.

    • Muda uliopotea haurudi tena.

    • Mwanafunzi aingiaye darasani bila ratiba ya masomo ya siku ni sawa na mkulima aendaye shambani bila jembe.

    17.6 Kuandika: Utungaji wa Hadithi 

    Zoezi la 13: Buni hadithi yako binafsi kwa kuzingatia maudhui kama yalivyoelezwa hapo juu.

    SOMO LA 18: UHAKIKI WA HADITHI SIMULIZI 

    Zoezi la 1: Jadili maswali yafuatayo ambayo yatakuelekeza katika kukabiliana na kifungu cha habari hapa chini. 

    1. Ni mambo gani muhimu yanayoiunda fani katika hadithi simulizi? 

    2. Maudhui katika hadithi simulizi huundwa na vipengele vipi? 

    18.1 Kusoma na Ufahamu: Sikio la Kufa Halina Dawa

    Soma kifungu cha habari kuhusu “Sikio la Kufa Halina Dawa” kisha jibu maswali uliyopewa hapo chini 

    Miaka mingi sana iliyopita aliishi mwindaji katika kijiji cha Tusaidiane. Mwindaji huyu alikuwa hodari sana katika utumiaji wa mishale kwani hakuweza kumkosa mnyama yeyote yule aliyejitokeza machoni pake. Mwindaji huyu alijulikana kwa jina la Mupenzi na mkewe Mariamu. Mariamu naye alionyesha uhodari mwingi katika kazi zake za ndani na nje ya nyumba. 

    Katika maisha yao ya miaka nenda rudi hawakujaliwa kupata mtoto. Waliamua kwenda kwa mganga ili waaguliwe na kupata dawa ya ufumbuzi wa tatizo hilo. Baada ya kushughulika kwa muda mrefu, Mariamu alionekana kuwa mjamzito, jambo ambalo lilitabiri matunda ya mtoto katika miezi minane mingine ijayo. Mupenzi kwa upande wake hali hii aliiona kama ndoto ya mwendawazimu ambayo ni vigumu kuamini kuwa yaweza ikatokea katika siku za usoni.

     Lakini hauchi hauchi unakucha. Siku iliwadia wakati Mariamu alipojifungua mtoto wa kiume. Furaha ya siku hiyo katika familia hii haikuwa na kifani maana isingewezekana kuikadiria. Katika shamrashamra hizo mtoto alipewa jina la Fujofujo. 

    Fujofujo katika kukua kwake alionekana mtoto mzembe, mdadisi wa mambo mbalimbali tena kupe. Badala ya kutumia akili zake kupigana na shida za kimaisha, yeye alikuwa anaishi kwa jasho la wengine. Kila asubuhi mapema alikuwa anaamka na kwenda porini kutegua mitego ya wawindaji wengine. Alikuwa ametoka huko akibeba aina tofauti za mizoga. Leo ni Sungura mmoja, kesho swala wawili na kesho kutwa paa watatu. 

    Wakati mmoja alifika nyumbani akibeba mzigo wa mizoga miwili, nyani pamoja na pundamilia. Baba yake alipomwona hakuamini macho yake na kuuliza, “Mtoto wangu we, toka wiki iliyopita umeishategua mitego ya wenzangu katika mahali patano. Habari ilienea kijijini kote kuwa mahali pawili au patatu pote uliitegua mizoga yenye thamani.” 

    Mupenzi na mkewe walipoona mtoto wao ambaye ni wa pekee amejizamisha sana katika mambo hayo ya wizi na ukatili hawakupendezwa na jambo hilo.

    Waliingiwa na hofu kuwa mwana wao anaweza kudhuriwa wakati yuko porini. Kwa hiyo walimwita Fujofujo na kumshauri aache tabia hiyo na kujishughulisha na kazi isiyo na dalili ya kumwingiza katika fitina dhidi ya majirani zao. Mtoto huyo hakuweza kuyasikiliza mawaidha ya wazazi wake; yaliingilia sikio la kulia na kutokea la kushoto. Walipoona kuwa wameshindwa kumshauri waliamua kwenda kwa mganga na kutafuta dawa ya kuweza kumzinga ili akae hapo hapo nyumbani. Lakini nyakati hizo Mupenzi alikuwa anazidi kuzeeka. Kwa hiyo kazi ya kutafuta dawa ilimkabili Mariamu. Baada ya kutafuta dawa na kuitumia, dalili ya kuleta mategemeo haikuweza kuonekana. 

    Fujofujo alizidi kufanya bidii katika kazi yake ya uharibifu na kuwa mtukutu zaidi hata akaweza kuwategua wanyama wakali kama vile Simba, chui na kadhalika. 

    Baada ya siku nyingi kupita, Fujofujo aliona dalili ambazo zilionyesha kuwa maisha yake katika kazi ya pori yalikuwa hatarini. Siku moja Fujofujo alitokewa na mzuka huko porini ambao ulimpa fadhaa na matatizo mengi. Fujofujo aliingiliwa na woga mwingi na kuamua kukimbilia kwake. 

    Fujofujo baada ya kurudi nyumbani na kuwasimulia wazazi wake yote yaliyomsibu, wazazi walizidi kumwonya na kumwambia kuwa kadiri mambo yanavyozidi kubadilika huko porini ni ishara kuwa kifo kinamkodolea macho. Badala ya kuwasikiliza wazazi wake kijana huyo aliendelea na wembe ule ule jambo ambalo liliwanyima raha wazazi wake na kuwakatisha tamaa, maana waliona zao lao la pekee litashindwa kuzaa matunda. 

    Zilipopita siku chache Fujofujo aliamua kwenda tena porini ingawaje alitambua hali halisi iliyokuwa ikimkabili; alijua hatari. Ilimngojea kuanzia mlangoni hadi porini lakini kwa moyo wake mgumu aliamua kujitoma tena katika pori zito na nene ambalo hali yake ilionyesha kutisha. Mara baada ya kuwemo porini kwa muda wa kama saa moja akiitafuta mitego; Fujofujo alikutana na joka kubwa lenye vichwa saba. 

    Kijana ambaye alionekana shujaa siku zote alishindwa kutawala woga wake kwa sababu aliona kuwa wakati wake wa kuaga dunia ulikuwa umefika. Aliyakumbuka maneno ya wazazi wake, “Jinsi mambo yanavyozidi kubadilika porini ndivyo kifo kinavyokukodolea macho”. Alijuta kwa nini hakusikia maneno ya wazazi wake, lakini wapi alikuwa amekwisha kuchelewa. Joka lilimwahi na kuanza kumshambulia. Alipotumia upanga wake alifaulu kukata kichwa kimoja tu, hapo ukawa ndio mwisho wake. 

    Nyumbani wazazi wake walingojea kwa matumaini madogo na wasiwasi mkubwa. Siku zake za kurudi zilizopita bila ya dalili ya kuonekana kwa mwana wao ndipo walipopoteza matumaini na kubaini kwamba mtoto wao mpendwa amepoteza maisha yake. Jambo ambalo lilisababishwa na ukaidi na kutosikiliza mawaidha ya wazazi.

    Maswali ya ufahamu

    1. Taja majina ya wanyama wanaozungumziwa katika hadithi.

    2. Eleza jinsi maisha ya familia ya Mupenzi na Mariamu yalivyo.

    3. Ni kitu gani kinachoonyesha kwamba Mupenzi alikuwa hodari sana katika kazi

    yake ya uwindaji ?

    4. Wazazi wa Fujofujo walikuwa wanampenda sana mtoto wao. Je, unakubaliana na

    kauli hii?

    5. Fujofujo alipata cha mtemakuni gani wakati alipokuwa akitegua mitego?

    6. Kwa nini Fujofujo alijuta wakati alipokuwa porini?

    7. Wazazi wake Fujofujo walikufa katika hali ya upweke. Kwa nini?

    8. Sikio la kufa halina dawa. Husisha methali hii na yaliyozungumziwa katika hadithi.

    18.2 Matumizi ya Msamiati wa Msingi 

    Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Hakikisha kwamba umechunguza matumizi yake katika kifungu cha habari hapo juu

    1. Mwindaji

    2. Kutabiri

    3. Kupe

    4. Mzoga

    5. Kujuta

    6. Mtukutu

    7. Kifo

    8. Joka

    9. Mawaidha

    10. Upweke 

    Zoezi la 3: Jaza nafasi wazi kwa kutumia maneno yafuatayo kutoka kifungu cha habari:mshale, mjamzito, mwendawazimu, mdadisi, swala, hudhuru,dalili, matumaini, uharibifu, hofu.

    1. Mtu yule huonekana kama ………… kutokana na maradhi yake ya akili.

    2. ………wa masuala haya ametoweka.

    3. …… …ni mnyama anayefanana na mbuzi.

    4. Kula vyakula vya mafuta kila wakati …………….. mwili hasa moyo

    5. Mwindaji alimuua twiga kwa kutumia ………… wake.

    6. Inaonekana kwamba mama yule ni …….. . anakaribia kuzaa mtoto.

    7. Kabla ya mvua kunyesha, mawingu hujitokeza kama…………ya mvua hiyo.

    8. Wanafunzi wale wana ………..............… ya kushinda mtihani wa Kiswahili mwaka huu.

    9. ……............………........... wa mazingira ni mwiko kwa kila binadamu.

    10. 10. Usiwe na ……..............……........…ya kutoa wazo lako hadharani. 

    18.3 Sarufi: Vivumishi vya Idadi vya Majina ya Ngeli ya PA-M-KU 

    Zoezi la 4: Tazama maneno yaliyopigiwa mistari hapa chini na kujibu maswali yatakayofuata. 

    Mtoto wangu we, toka wiki iliyopita umeishategua mitego ya wenzangu katika mahali patano. Habari ilienea kijijini kote kuwa mahali pawili au patatu pote uliwategua mizoga yenye thamani. 

    1. Maneno haya ni ya aina gani ? 

    2. Yanahusishwaje na majina yanayokuwa pamoja nayo?

    Maelezo muhimu 

    Maneno kama pawili, patatu, patano, ni vivumishi vya idadi vya majina ya ngeli ya Pa- m- ku. Vivumishi hivi hutumiwa kuonyesha idadi ya mahali fulani.

    Mifano katika sentensi

    • Pahali pamoja panajulikana kama kivutio cha utalii.

    • Pahali pawili patajengwa vituo vya mafunzo dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

    • Pahali patatu palipandwa miti ya aina nyingi.

    • Pahali panne palisikika kutumia chandarua kwa kujilinda malaria.

    • Pahali patano palifaulu kupigana dhidi ya rushwa.

    • Pahali sita pamefunguliwa mashirika ya ushirikiano wa kiuchumi.

    • Pahali pengi pameendelezwa na wananchi wenyewe.

    Tanbihi: Vivumishi vya idadi kama vile sita, saba, na tisa havichukui kiambishi pa

    Mfano: 

    Hatusemi                                          Tunasema 

    Mahali pasita                                   Mahali sita 

    Mahali pasaba                                 Mahali saba

    Zoezi la 5: Chagua jibu sahihi kati ya haya yaliyowekwa katika mabano.

    1. Pahali…………..(matatu, patatu, kutatu) patatembelewa wiki ijayo.

    2. Pahali ………… (pasita, msita, sita) panapatikana usafi.

    3. Kalisa atamwonyesha mtoto wake pahali (tano, patano, mtano) pa kupanda miti.

    4. Pahali ……………. (mwili, pawili, kuwili) palifundishiwa masomo ya usawa wa jinsia.

    5. Wageni wale waligundua pahali ………… (mwingi, pengi, nyingi) pa kutembelea sokwemtu.

    6. Usafi unatakiwa pahali ……… (nyingi, pengi, wengi).

    18.4 Matumizi ya Lugha: Uhakiki wa Hadithi Simulizi 

    Zoezi la 6: Soma tena kifungu cha habari “Sikio la kufa halina dawa”. Jishughulishe na uhakiki wa fani na maudhui kwa kuzingatia vipengele vya fani na vile vya maudhui. 

    Zoezi la 7: Toa mbele ya darasa mhadhara wa uhakiki wako. 

    Uhakiki wa kazi ya fasihi ni nini? 

    Ni kazi au kitendo cha kuchambua na kufafanua vipengele vya fani na maudhui katika kazi ya fasihi. Vipengele vya fani na maudhui ni pamoja na wahusika, muundo, mtindo, maadili na ujumbe.i. Hivyo mhakiki sharti asome kazi ya fasihi andishi au kusikiliza masimulizi kwa makini ili aweze kuyatolea uhakiki. 

    Kwa maana nyingine ni kitendo cha kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Hii ina maana ya kwamba uhakiki wa kazi za fasihi hautoki katika ombwe, kuna kanuni na taratibu mbalimbali zinazoongoza kufanya uhakiki, na hii ndio sababu kuna nadharia kadha wa kadha za uhakiki wa kazi za kifasihi. Au kwa lugha rahisi, uhakiki ni uchambuzi wa kina wa kazi za fasihi kwa lengo la kufafanua vipengele vya fani na maudhui.

    Kinachotiliwa mkazo katika uhakiki wa hadithi simulizi

    1. Fani

    • Wahusika

    • Mtindo

    • Muundo

    • Lugha

    • Mandhari

    2. Maudhui

    • Dhamira

    • Migogoro

    • Falsafa

    • Ujumbe

    • Msimamo wa msanii

    Nini wajibu wa mhakiki wa kazi za fasihi?

    Mhakiki wa kazi za fasihi huwa na majukumu yafuatayo:

    1. Kuisoma kazi ya fasihi kwa makini na kuielewa

    2. Kuchambua vipengele vya fani na maudhui katika kazi hiyo

    3. Kueleza ubora na udhaifu wa matumizi ya vipengele vya fani na maudhui

    katika kazi hiyo.

    Nini umuhimu wa kuhakiki kazi za fasihi?

    Umuhimu wa kuhakiki kazi za fasihi unaelezeka kama ifuatavyo:

    1. Kuchambua na kuweka wazi funzo ambalo linatolewa na kazi ya fasihi

    simulizi.

    2. Kuchambua na kufafanua picha za kisanii zilizotumika katika kazi ya fasihi.

    3. Kumshauri mtunzi ili afanye kazi bora zaidi.

    4. Kumwelekeza msikilizaji ili apate faida zaidi kuliko yale ambayo angeweza

    kuyapata bila ya dira ya mhakiki.

    5. Kuhimiza na kushirikisha fikira za kihakiki katika kazi za fasihi.

    6. Kuweka, kubakiza, na kukuza kiwango cha utunzi wa kazi za fasihi.

    18.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano

    Zoezi la 8:Tega sikio hadithi fulani uliyopewa. Zungumzia wahusika wake, dhamira pamoja na ujumbe, baadaye wasilisha kazi yako mbele ya darasa. 

    Zoezi la 9: Kwa ushirikiano na wenzako, jadili kauli zifuatazo: 

    1. Maendeleo ya familia hutokana na umoja na ushirikiano kati ya mume na mke. 

    2. Zamani kazi ya uwindaji porini ilikuwa rasmi na yenye kuisaidia jamii. Leo kazi hii badala ya kuiendeleza nchi huangamiza sana uchumi wake. 

    18.6 Kuandika: Utungaji wa Hadithi Simulizi

     Zoezi la 10: Tunga hadithi simulizi yenye aya sita kwa kuzingatia vipengele vya fani na maudhui kuhusu dhamira kuu ya ushirikiano.

    Muhtasari wa Mada 

    MUHTASARI, FANI NA MAUDHUI KATIKA HADITHI SIMULIZI ni mada ya tatu katika kitabu cha Kiswahili, Kidato cha nne. Mada hii imeundwa na masomo matano kama ifuatavyo:

    Somo la kwanza: Maana ya muhtasari na sifa zake 

    Somo hili linagusia maana ya muhtasari wa habari pamoja na sifa zihitajiwazo ili muhtasari uwe unapendeza.

    Somo la pili: Taratibu za kutoa muhtasari mzuri 

    Kama mojawapo ya kazi za kifasihi, muhtasari huwa na taratibu za kufuata wakati wa kutoa muhtasari wa kazi ya fasihi fulani. Kwa hiyo, somo hili limezizingatia taratibu muhimu za kuiongoza kazi ya kutoa muhtasari mzuri.

    Somo la tatu: Fani katika hadithi simulizi

    Kila kazi ya sanaa huwa na umbo lake linaloitofautisha na kazi zingine. Umbo au funiko hilo ndilo liitwalo fani. Somo hili limeyataja mambo muhimu yanayoiunda fani ya hadithi simulizi. 

    Somo la nne: Maudhui katika hadithi simulizi 

    Fani yenyewe haitoshi kuifanya kamilifu kazi ya sanaa. Ni lazima maudhui yashirikishwe kuunga mkono na kuambatanishwa na fani. Katika somo hili la nne, vipengele vya maudhui ndani ya hadithi simulizi vilitiliwa mkazo ili mwanafunzi aweze kueleza kimsingi tofauti iliyopo kati ya fani na maudhui. 

    Somo la tano: Uhakiki wa hadithi simulizi 

    Msanii wa kazi za fasihi simulizi huongozwa na fani na maudhui katika ufundi wake. Ndipo anapohitilafiana na wasanii wengine kulingana na ubingwa wake wa kuoanisha fani na maudhui katika kazi yake. Katika somo la tano, mwanafunzi amefahamu maana ya uhakiki, mhakiki ni mtu gani pamoja na kuhakiki kazi ya sanaa. Ameshirikishwa pia kimatendo kuihakiki hadithi simulizi kwa kuzingatia pamoja vipengele vya fani na maudhui.

    Somo la tano: Uhakiki wa hadithi simulizi 

    Msanii wa kazi za fasihi simulizi huongozwa na fani na maudhui katika ufundi wake. Ndipo anapohitilafiana na wasanii wengine kulingana na ubingwa wake wa kuoanisha fani na maudhui katika kazi yake. Katika somo la tano, mwanafunzi amefahamu maana ya uhakiki, mhakiki ni mtu gani pamoja na kuhakiki kazi ya sanaa. Ameshirikishwa pia kimatendo kuihakiki hadithi simulizi kwa kuzingatia pamoja vipengele vya fani na maudhui.

    TATHMINI YA MADA YA TATU 

    Soma hadithi ifuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini.

    Jongoo na Chura Jongoo na Chura walikuwa marafiki wakubwa sana. Kila wakati walitembeleana. Siku moja Chura alimwuliza rafiki yake Jongoo, “Rafiki yangu, huwa unafanya nini na ngozi yako? Mbona inang’aa sana? Tazama ngozi yangu, siyo laini. Ningependa iwe kama yako. Hebu nidokezee kidogo”.

    Jongoo alifurahi kuambiwa kwamba alikuwa na ngozi nyororo. Alianza kumpa rafiki yake ushauri kama ifuatavyo, “Rafiki yangu Chura, ngozi hii nyororo unayoiona ni kazi kubwa ambayo mke wangu amekuwa akifanya kwa muda wa miaka mingi. Kila asubuhi huweka kikaango motoni kisha hujaza mafuta na…” 

    Kabla hajamaliza, Chura alimkata kauli rafiki yake, “Basi, basi! Nimekwisha kuelewa. Huna haja ya kunielezea zaidi. Yote hayo nitayatenda na utaona nitakavyonawiri”. Jongoo alijaribu kumshawishi amsikilize lakini Chura alisisitiza kwamba kwa utangulizi ule alikwisha kuelewa kila kitu. Marafiki wale waliachana. Jongoo alikwenda kwake na Chura pia alikwenda nyumbani kwake. Alipofika tu, Chura alimwita mke wake. 

    “Rwe! Rwe! Rwe!”. 

    Naye mkewe aliitika, “Kororo! Rwe! Rwe!” Chura alianza kumweleza mkewe, “Mke wangu, leo rafiki yangu amenieleza jinsi ya kuifanya ngozi yangu iwe nyororo na ya kung’ara kama yake.Sasa hivi nataka uweke chungo jikoni. Hakikisha jiko lina moto mkali sana.” Mke alifanya kama alivyoelezwa. 

    Chura aliendelea kutoa maagizo, “Nataka utie mafuta ya kukaangia mboga mengi sana na yakisha kuchemka nieleze mara moja”. Mkewe alitekeleza maagizo na mara akampa taarifa kwamba mafuta yalikwisha chemka. Chura aliingia jikoni akamwambia mkewe, “Sasa nitumbukize kwenye mafuta kwani ninataka niibabue ngozi ya juu ili ibaki nyororo iliyopo chini yake”. 

    Mkewe alimjibu akiwa amepigwa na bumbuazi, “Mume wangu, mbona unaniambia nifanye kitu cha hatari? Kwani unataka kuniambia ukitumbukizwa katika mafuta yaliyochemka utapona! Haiwezikani hata kidogo. Balaa hilo lituepukie mbali!” Chura alisisitiza kutumbukizwa katika mafuta na wakati huo alifanya hivyo kwa ukali. 

    “Mimi nimekuwa nikikuambia siku zote kwamba ngozi hii inanitia aibu. Leo nimepata njia ya kuiondoa nawe unapinga? Kaa chonjo tusikilizane. Si unaona jinsi ninavyokuaibisha kwa ngozi yangu yenye magamba! Ninatamani kuwa na ngozi nyororo mithili ya ile ya Jongoo. Nichemshie mafuta kisha unitumbukize katika kikaango. 

    Ewe mume wangu! Huoni kuwa nikikutumbukiza chunguni utaangamia? Haiwezekani. Katu katakata! Balaa hilo tuliepukie mbali. Alipokuwa akisema hayo, mzee chura alimkatiza na pupa akajitumbukiza katika kikaango na kuanza kulia “yoyoorwe! yoyoorwe!” 

    Mara moja mkewe akamuokoa kwa kumnyanyua toka katika kikaango na kumlaza mkekani. Halafu akawaita majirani kwa msaada, Mzee Chura akapelekwa mahututi hospitalini mara moja. Chura alipewa kitanda wiki nzima huku akijuta kuwa angalisikia shauri la mkewe msiba huo usingalimsibu.

    Baada ya wiki kupita, Chura alirudi nyumbani. Alipoulizwa sababu ya kitendo cha kujitoma katika mafuta ya moto, alijieleza hivi: “ Haya yote yalitokana na rafiki yangu Jongoo, nilipomuuliza sababu ya kung’aa kwa ngozi yake na kuwa nyororo alianza kuniambia alichofanyiwa na bibi yake kwamba anampaka mafuta yaliyochemshwa nikamkata ulimi bila kuyamaliza maelezo yake. Nilipofika nyumbani nilimshurutisha mke wangu kunichemshia mafuta na kunitumbukiza ndani ya kikaango. Sikujua kuwa haya yote yangetokea.”

    Alidai kwamba alishasoma mawazo yangu na hivyo alijua nilitaka kumaliza maelezo yangu vipi. Mara aliondoka akaja zake huku nyumbani.” Wazee waliokuwepo pale waliamua kwamba Jongoo hakuwa na kosa, bali Chura alisababisha balaa hiyo mwenyewe kwa ujinga wake. Alijifanya kuelewa wakati ambapo hakuna alichoelezwa kikamilifu.

    Na huu ndio mwisho wa hadithi. 

    Hadithi hii msingi wake ni kutoka: Wizara ya Mafunzo ya Msingi na Sekondari (1987), Kitabu cha Kiswahili IV-VA, Kitabu cha Mwanafunzi, Régie de l’Imprimerie Scolaire, Kigali, uk: 9-11.

    Maswali

    Fanya muhtasari wa hadithi hii.

    Fanya uhakiki wa fani na maudhui wa hadithi hii.

    Bainisha majina ya ngeli ya PA-M-KU- yaliyotumiwa hadithini na kueleza kanuni za matumizi yake.


    • MADA NDOGO: MIDAHALO NA MIJADALA


     Uwezo upatikanao katika mada:
     Kuandaa midahalo na mijadala, kuongoza midahalo na mijadalo na kushiriki katika shughuli za mazungumzo na majadiliano kwa kuzingatia mada zilizotolewa kujadiliwa, kuweza kuandika muhtasari wa hoja zinazotolewa na kutoa amri kwa kutumia vitenzi vyenye miundo tofauti.

     Malengo
     Baada ya mada hii, mwanafunzi atakuwa na uwezo wa:
          Kufasili maana ya mdahalo na mjadala.
          Kutofautisha mdahalo na mjadala.
          Kutoa mfano na kuigiza mdahalo na mjadala.
          Kutunga sentensi zenye hali ya kushurutisha.

     Kidokezo
        Majadiliano ni nini?
        Kuna aina zipi za majadiliano?
        Mdahalo ni nini?
        Mjadala ni nini?
        Jadili umuhimu wa mdahalo na mjadala


     SOMO LA 19: MAANA YA MJADALA NA MDAHALO

     Tazama kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yanayofuata hapo chini
      

     Zoezi 1: Jibu maswali yafuatayo:
     1. Watu unaowatazama kwenye mchoro huo wanafanya nini?
     2. Eleza kile wanachofanya watu hao kwenye mchoro hapo juu.
     3. Kuna uhusiano wowote kati ya mchoro huo na kichwa cha habari hapo chini?

     19.1 Kusoma na Ufahamu: Maana ya Mdahalo na Mjadala
     Soma kifungu cha habri kuhusu «Maana ya mdahalo na mjadala», halafu jibu maswali uliyopewa hapo chini
     Kila mwaka chama cha wanafunzi wa Kiswahili wa vyuo vikuu nchini Rwanda hukutana katika shughuli za mazungumzo na majadiliano kwa madhumuni ya kukuza uwezo wao wa kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili. Mazungumzo wanayoyafanya katika mikutano yao hujulikana kwa majina ya mdahalo na mjadala. Katika mazungumzo hayo wao hujigawa katika makundi tofauti kulingana na mada zilizoandaliwa ili kutoa maoni yao kwa masuala mbalimbali yanayozikabili jamii mbalimbali za Kiafrika.

     Miongoni mwa mazungumzo yanayofanywa kila mwaka, mdahalo ndio unaopendwa na wanafunzi wengi. Wao husema kuwa katika mazungumzo haya wazungumzaji hupata fursa ya kuonyesha fikra zao na mawazo yao kuhusu mada iliyotolewa. Kwa kuwa majadiliano haya huzihusisha pande mbili zenye misimamo tofauti. Watu wengi wanaosikiliza majadiliano ya aina ya mdahalo hufurahia jinsi wazungumzaji wanaotetea mada hushikilia mawazo yenye kuunga mkono mada kwa kutafuta hoja muhimu zinazowachangamsha wasikilizaji waliopo. Kwa upande mwingine wapinzani nao hutafuta hoja na mifano ya kuthibitisha maoni yao ili kujaribu kuwaridhisha wanaosikiliza kwa minajili ya kutaka waungwe mkono na wengi wao. Hivyo basi, watu wengi hufurahia mashindano haya ambapo watetezi na wapinzani hushindana kimawazo kulingana na mada ya kusisimua iliyochaguliwa kuzungumziwa.

     Katika mazungumzo haya ni lazima kuwepo na mwenyekiti ambaye anaendesha mdahalo kwa kuufungua, kumpa fursa atakayesema na kuhakikisha kwamba kila msemaji anatumia muda aliopangiwa. Hali kadhalika mhusika huyu anahakikisha kwamba kunakuwa na nidhamu wakati wa kuendesha mdahalo. Mazungumzo yanapofikia kikomo, mwenyekiti hufunga mdahalo baada ya kupigisha kura ili kujua ni upande gani ulioshinda. Ili kufanikisha shughuli hii, mwenyekiti husaidiwa na katibu ambaye kazi yake muhimu ni kuandika hoja zinazotolewa na wasemaji na kuisomea hadhira hoja hizo zilizotolewa na kutangaza matokeo ya kura zilizopigwa. Mwenyekiti hulipongeza kundi lililoshinda kwa kusema, “Hongera. Pigieni makofi washindi.” na wakati huo huo hadhira huwapigia makofi.

     Kabla ya kuanza mazungumzo, mlezi wa chama cha wanafunzi wa shule hizi huchukua fursa ya kutoa maelezo kuhusu umuhimu wa mazungumzo ya aina hii kwa kuwachochea wanafunzi wengi kushiriki katika mazungumzo yaliyopangwa ili kuwapa uzoefu wa kuzungumza hadharani na kutoa hoja zenye kujaribu kutaka kuungwa mkono na hadhira iliyopo. Mashindano mengi hufanywa baina ya wanafunzi wa chuo kimoja na wanafunzi wa chuo kingine kiasi kwamba zawadi tele hutolewa kwa washindi.

     Pengine, mazungumzo mengine katika mikutano ya wanafunzi hawa huchukua utaratibu tofauti kidogo na ule unaozingatiwa katika mdahalo. Hapa mazungumzo hufanywa kuhusu suala fulani linalohitaji kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Mazungumzo ya aina hii ndiyo hujulikana kwa jina la mijadala. Wanafunzi wanaoshiriki katika mijadala mingi, husema kuwa hii ni njia pia ya kukuza uwezo wao wa kufikiri na kutafuta masuluhisho kwa masuala yanayoikumba jamii fulani. Katika mazungumzo haya ni lazima kuwepo pia na mwenyekiti ambaye anaongoza majadiliano kwa kuchagua wazungumzaji ili watoe mchango wao kuhusu suala lililopo. Mwenyekiti humpa fursa mzungumzaji kwa kusema, “Simama utoe mchango wako.”

     Mzungumzaji aliyechaguliwa huweza kutoa hoja zake kulingana na anavyolifikiria suala bila kushikilia upande wowote. Mara nyingi, mjadala huweza kufanyika katika makundi madogo madogo au makubwa na kiongozi huzusha mawazo na kuhakikisha ikiwa kuna mwenendo mwema kati ya washiriki wa mjadala huo.

     Kiongozi huyo wa mjadala huwa na majukumu tofauti kwani ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa. Mada zinazojadiliwa katika mjadala ni zile ambazo zinahitaji ufafanuzi kutokana na mchango wa mawazo ya wengi na kila mshiriki anayetoa hoja zake, huweza kuunga mkono maoni ya wenzake au kuyapinga kwa minajili ya kutoa mchango wake wa kutatua tatizo linalojadiliwa. Wanafunzi wengine wanaoshiriki katika mijadala inayoandaliwa hubainisha umuhimu na nafasi yake ya kukuza uwezo wa kitaaluma, kukuza fikra na hali ya udadisi kwa wanafunzi.

     Kama ilivyo midahalo, mijadala humpa mwanafunzi uwezo wa kushawishi watu katika hadhira na kutambua binafsi kipawa chake cha kuzungumza na haiba yake mbele ya wenzake. Mwanafunzi anayeshiriki katika mjadala na mdahalo anazoea kuheshimu muda aliopewa na kuweza kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri. Yeye anakuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kuwa anaweza kuutumia msamiati na kujizoeza kutumia matamshi mazuri ya lugha.

     Jambo muhimu pia katika midahalo na mijadala inayofanywa na wanafunzi wa Kiswahili wa vyuo vikuu nchini Rwanda ni kwamba mazungumzo yanayofanywa huwazoeza wengi kusikiliza na kupima maoni na hoja za wenzao, kuelewana na wengine kutoka sehemu mbalimbali za nchi, kuheshimiana kulingana na mawazo tofauti yanayotolewa na kila mzungumzaji, kudumisha udugu, umoja, amani na maridhiano kati yao. Kwa hiyo, mjadala na mdahalo ni zoezi zuri kwa mwanafunzi yeyote anayetaka kukuza uwezo wa mawasiliano, majadiliano, mahojiano, ujuzi wa kutoa maoni yake na kujitambua katika jamii yake.

     Maswali ya ufahamu
     1. Ni kwa sababu gani wanafunzi hukutana kila mwaka?
     2. Eleza maana ya mdahalo.
     3. Toa maana ya mjadala.
     4. Ni nani anayeongoza mdahalo?
     5. Kazi ya katibu ni ipi katika mdahalo?
     6. Kuna pande ngapi katika mdahalo?
     7. Kuna pande ngapi katika mjadala?
     8. Mjadala una lengo gani?
     9. Taja stadi nne zinazopatikana katika mdahalo na mjadala.
     10. Unajifunza nini kutokana na kifungu hiki?

     19.2 Msamiati kuhusu Maana ya Mdahalo na Mjadala
     Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi
     yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu maana ya mdahalo na mjadala.
     1. Mdahalo                        6. Kupinga
     2. Mjadala                         7. Kuhakikisha
     3. Hoja                              8. Nidhamu
     4. Maoni                           9. Mwenendo
     5. Kutetea                      10. Haiba

       Zoezi la 3: Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.


     Zoezi la 4: Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo:kipawa,
     kuheshimu, kuelewa, kushiriki, anaandika, matamshi, mjadala, mdahalo, lugha, mazungumzo.
     1. Katika .........................mwenyekiti ndiye ambaye anachagua atakayesema.
     2. Anayeshiriki katika mazungumzo anakuza utumiaji wa ...................
     3. Washiriki wa ....................ni lazima watoe maoni yao bila kuegemea kwa upande wowote.
     4. Mjadala ni ...................yanayohusisha watu wengi.
     5. Midahalo na mijadala humsaidia mwanafunzi kutambua ...............chake.
     6. Mdahalo humsaidia mshiriki kuwa na moyo wa..........mawazo ya wengine.
     7. ....................mada ni chanzo cha kutoa maoni mazuri.
     8. Katibu wa mdahalo ...............hoja zilizotolewa na wasemaji.
     9. Kila mtu aliyealikwa anaombwa ..................katika majadiliano.
     10. Mwanafunzi wa lugha anajizoeza kutumia.............mazuri wakati wa mdahalo.

     19.3 Sarufi: Matumizi ya Hali ya Hushurutisha katika Vitenzi vyenye Kiambishi Tamati -a Hali Yakinishi.
     Zoezi la 5: Jadili kuhusu maana ya sentensi zifuatazo; halafu utunge sentensi tano kama hizo.
     1. Simama utoe maoni yako.
     2. Pigieni makofi washindi.

     Maelezo muhimu
     Katika hali ya kushurutisha au ya kuamrisha, vitenzi vya silabi zaidi ya moja na vyenye kiambishi tamati-a, huondolewa tu kiambishi cha kitenzi ku- katika umoja hali yakinishi. Katika wingi, vitenzi hivi huondolewa kiambishi ku- pamoja na kiambishi tamati-a, halafu vikachukua kiambishi -eni badala ya kiambishi -a cha mwishoni.

     Mfano: Kitenzi: kusimama
                  Umoja: (Wewe) Simama
                  Wingi: (Nyinyi/Ninyi) Simameni

     Zoezi la 6: Zikamilishe sentensi zifuatazo kwa kutumia hali ya kushurutisha kwa vitenzi ambavyo vimo katika mabano.

     Kwa mfano: Swali: Mwalimu aliwaambia wanafunzi: “.......madaftari yenu”. (kuchukua)
     Jibu: Mwalimu aliwaambia wanafunzi: “Chukueni madaftari yenu”.
     1. “............... kazi yako ya shule kuhusu mjadala”. Mama alimuamrisha mtoto wake. (kutimiza)
     2. Mwalimu alimuomba mwanafunzi akisema: “............... ubao tuandike mada ya mdahalo”. (Kufuta)
     3. Baada ya kuamkia wanafunzi, mwalimu aliwaambia: “......... kwa makundi ya utetezi na upinzani”. (kujiunga)
     4. Kama uko kwenye upande wa utetezi:.............mada iliyotolewa (kutetea)
     5. Kama uko kwenye upande wa upinzani...........mkono wapinzani. (kuunga)
     6. Mwenyekiti alimuambia msemaji mkuu: “..............mawazo yako”. (kutoa)
     7. .................. makofi washindi. (kupigia)
     8. Kiongozi wa mjadala aliiambia hadhira: “..............tuanze mjadala”. (kunyamaza)
     9. Katibu aliombwa na mwenyekiti: “...................mawazo yote yatakayotolewa”. (kuandika)
     10. Ikiwa unataka kukuza maongezi yako ya lugha, .................midahalo na mijadala. (kuhudhuria)

     Zoezi la 7: Tunga sentensi kumi kwa kutumia hali ya kushurutisha.

     19.4 Matumizi ya Lugha: Maana za Mdahalo na mjadala
                        • Mazoezi ya jumla

     Zoezi la 8: Panga maneno yafuatayo kwa utaratibu unaofaa ili yaweze kuleta maana katika sentensi
     1. uwezo kukuza wa kitaaluma mwanafunzi na hali kukuza humsaidia ya udadisi mjadala.
     2. kuepukana hadharani wa huwafanya na kuzungumza mdahalo wanafunzi uoga.
     3. ambaye ishara huonyesha ana kila kusema mjadala la katika yeyote.

     Maelezo muhimu kuhusu maana ya mdahalo na mjadala

     Zoezi la 9: Chunguza maelezo haya kuhusu maana ya mdahalo na mjadala kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini

     Maelezo muhimu kuhusu “Maana ya mdahalo na mjadala”
     Mdahalo ni majadiliano baina ya watu wengi juu ya mada fulani. Unahusisha pande mbili yaani upande wa utetezi na upande wa upinzani.
     • Mdahalo unawasasidia wanafunzi kushiriki katika utetezi au upinzani wa jambo fulani.
     • Mdahalo unaongozwa na mwenyekiti akisaidiwa na katibu.
     • Mjadala ni mazugumzo juu ya jambo fulani. Unaweza kufanyika katika makundi madogo madogo au makubwa.
     • Mjadala unaongozwa na mtu mmoja ambaye anazusha mawazo na kuhakikisha ikiwa kuna mwenendo mwema kati
        ya washiriki wa mjadala huo.
     • Mwenyekiti wa mjadala ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa. Mada zinazojadiliwa katika mjadala ni
        zile ambazo zinahitaji ufafanuzi kutokana na mchango wa mawazo ya wengi.
     • Anayetoa hoja yake, anaweza kuunga mkono maoni ya mwenzake au kuyapinga kwa minajili ya kutoa mchango wake
        wa kutatua tatizo linalojadiliwa.

     Maswali ya kujadiliana
     1. Unaelewa nini na maana ya mdahalo?
     2. Eleza maana ya mjadala
     3. Jadili wajibu wa kiongozi wa mjadala.
     4. Ni watu gani wanaoshiriki katika mdahalo?
     5. Bainisha watu wanaoshiriki katika mjadala.

     19.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
     Zoezi la 10: Jadilieni kuhusu “nafasi ya midahalo na mijadala katika jamii”

     19.6 Kuandika: Utungaji wa Kufungu cha Habari
     Zoezi la 11: Kwa kuzingatia maana ya mdahalo na mjadala, tunga kifungu cha habari kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo:
     • “Majadiliano Huimarisha Ushirikiano”
     • “Nafasi ya Mijadala katika Maendeleo ya Jamii”

     SOMO LA 20: UHUSIANO NA TOFAUTI KATI YA MDAHALO NA MJADALA

     Tazama mchoro huu kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini ya mchoro.


     Zoezi la 1: Eleza yale unayoyaona kwenye mchoro hapo juu.

     20.1 Kusoma na Ufahamu: Mdahalo na mjadala
     Soma kifungu cha habari kifuatacho kuhusu “Mdahalo na Mjadala”, kisha jibu maswali uliyoyopewa hapo chini.

     Watu wengi wakiwemo wapenzi wa lugha ya Kiswahili hujiuliza maswali mengi kuhusu midahalo na mijadala. Kuna wale wanaofikiria kuwa mdahalo ni sawa na mjadala ilhali wengine huziona shughuli za mdahalo na mjadala kama shughuli tofauti zinazofanywa na watu walio na malengo tofauti. Hata hivyo, ni wazi kwamba mdahalo na mjadala ni mazungumzo yanayoendeshwa na kushirikisha watu tofauti kwa kukidhi haja na malengo yanayotofautiana na kuingiliana kwa upande mwingine.

     Mdahalo ni majadiliano kati ya watu wengi juu ya mada maalum. Katika mdahalo mada nyingi hutolewa na mada moja huchaguliwa kwa kupiga kura ili kuhakikisha kwamba mada iliyochaguliwa ni ile ambayo ilipata kura nyingi. Mdahalo ni kama mashindano ya maneno au labda, ni kama mchezo ambapo wazungumzaji wawili au zaidi hutoa hoja zao kwa nia ya kushawishiana. Kwa upande mwingine mjadala ni mazungumzo juu ya jambo maalum ambayo hufanywa na watu kwa kutoa hoja zao kwa jambo fulani linalotakiwa ufafanuzi au ufumbuzi wa suala lililopo kwa mchango wa mawazo hayo ya watu wanaoshiriki katika mazungumzo hayo.

     Mdahalo na mjadala ni aina mbili za majadiliano ambazo huhusiana kwa namna moja ama nyingine. Uhusiano wa kwanza uliopo kati ya mdahalo na mjadala ni kwamba mdahalo na mjadala huhusisha watu wengi wanaotoa hoja kuhusu mada fulani. Watu hao wanaohusika katika mdahalo na mjadala ni lazima wamchague kiongozi ambaye jukumu lake ni kuongoza majadiliano kwa kupanga muda wa kuzungumza kwa kila msemaji anayeshiriki katika mazungumzo hayo. Katika mdahalo na mjadala hakuna msemaji ambaye anaruhusiwa kutoa hoja bila kumuomba fursa kiongozi wa majadiliano.

     Uhusiano mwingine ambao huhusisha mdahalo na mjadala ni mada. Mada ni kiini cha jambo linalozungumziwa. Mdahalo na mjadala huwa na mada ambayo humulika hoja zote zinazotolewa wakati wa mazungumzo. Ingawa msemaji mmoja huweza kumuunga mkono au kutokubaliana na msemaji mwingine, hoja zote zinazodokezwa hujikita zaidi kwenye mada ambayo ni mhimili timamu wa mdahalo na mjadala. Kama kuna wasemaji ambao wanataka kukiuka mada katika hoja zao, kiongozi wa mdahalo au mjadala huwarekebisha kwa kuwakumbusha mada inayotolewa hoja.

     Pengine, malengo ya mdahalo ni kama yale ya mjadala. Mdahalo na mjadala huwa na malengo ya kukuza uwezo wa kitaaluma na hali ya udadisi kwa washiriki wa majadiliano. Mdahalo na mjadala hukuza uwezo wa kushawishi watu hadharani ili wakubaliane na mawazo ya msemaji kuhusu jambo fulani. Aidha humwezesha mtu kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri wakati anapoandika insha au habari. Mdahalo na mjadala pia humsaidia mtu kutambua kipaji cha kuzungumza alicho na cho bila aibu mbele ya hadhira na kukuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kutumia msamiati na matamshi bora ya lugha. Humzoeza pia mtu kusikiliza maoni ya watu wengine, kupinga au kutetea maoni na hoja zao na jambo muhimu ni kwamba majadiliano haya humpa wasaa wa kuelewana nao.

     Wanafunzi wanapofanya mdahalo na mjadala hukuza uwezo wao wa maongezi ya lugha ya Kiswahili na hupanua kiwango chao cha msamiati na hupunguza uoga wa kuongea hadharani. Vilevile, mdahalo na mjadala hutumiwa kama wenzo bora wa kutatua migogoro inayoweza kuzuka miongoni mwa wanajamii fulani. Kwa namna ya mjadala na mdahalo watu wenye mawazo tofauti hupata nafasi ya kujadiliana juu ya jambo fulani kwa madhumuni ya kutatua tatizo linalowakumba. Mdahalo na mjadala hutumiwa kwa kutatua tatizo na kuondoa migogoro miongoni mwa watu kwa njia ya amani.

     Ingawa mdahalo na mjadala huwa na uhusiano, haimanishi kwamba ni mambo sawa. Kuna mambo kadhaa ambayo huufanya mdahalo uhitilafiane na mjadala.

     Tofauti ya kwanza iliyopo kati ya mdahalo na mjadala ni wahusika. Katika mdahalo kuna wahusika ambao ni mwenyekiti. Mwenyekiti ndiye ambaye ana jukumu la kuongoza mdahalo.

     Ukichaguliwa kama mwenyeketi, usishindwe kuongoza mdahalo ipasavyo. Usiuongoze ovyoovyo na usikose kumpangia kila msemaji muda atakaotumia. Katika mdahalo kuna katibu ambaye ana wajibu wa kuandika hoja zote zinazotolewa kwenye mdahalo. Kuna pia wasemaji wakuu wa upande wa utetezi na upinzani ambao hutoa hoja kwa kutetea au kutokubaliana na mada. Kuna tena hadhira au wasilikizaji wanaofuata mdahalo.

     Lakini katika mjadala wahusika ni kiongozi wa mjadala ambaye huweza kuwa mtu mmoja au wawili kulingana na mada iliyochaguliwa au malengo ya majadiliano yenyewe. Katika mjadala kuna hadhira pia ambayo hushiriki katika mazungumzo kwa kusikiliza na kutoa mchango wao kuhusu suala linalojadiliwa. Katika mjadala hakuna katibu wala wasemaji wakuu wa upande wa utetezi au wa upinzani. Kila yeyote aliye na hoja hunyosha mkono kuomba fursa ya kuzungumza.

     Tofauti nyingine kati ya mdahalo na mjadala ni namna ambavyo wasemaji hupangiwa fursa za kutoa hoja zao. Katika mjadala kiongozi humruhusu yeyote atakaye kutoa mchango kwani hakuna makundi ya watetezi na wapinzani wa mjadala. Lakini katika mdahalo kunakuwepo makundi mawili; yaani utetezi na upinzani. Kila kundi huwa na wasemaji wakuu sawa kwa idadi na wa kundi jingine. Kama msemaji mkuu wa upande wa utetezi anamaliza kutoa mawazo yake kwa kutetea mada, msemaji mkuu wa upande wa upinzani hupata fursa ya kutoa mawazo yake kwa kutokubaliana na mada na kuyapinga yale mawazo yanayotolewa na msemaji mkuu wa upande wa upinzani.

     Vilevile, katika mdahalo wasemaji wa pande mbili hutoa hoja zao kwa kutetea au kutokubaliana na mada ili upande wao uweze kupata ushindi. Wasemaji wakuu katika mdahalo wanaweza kutetea mawazo ambayo na wao wenyewe kwa ukweli hawakubaliani nayo au kuyapinga yale ambayo wao binafsi hujua kwamba ni ukweli kwa madhumuni ya kuibuka washindi wa mdahalo tu. Jukumu la kwanza la wasemaji wakuu wa mdahalo ni kupata ushindi, tofauti na kwenye mjadala ambapo lengo la kwanza la kila msemaji si kupata ushindi. Mjadala si mashindano bali lengo la kila msemaji ni kutoa mawazo kwa nia ya kutatua tatizo fulani linalofafanuliwa na kujadiliwa kwa pamoja ili kutafuta ufumbuzi na suluhisho linalofaa na kupata namna bora ya kutenda mambo yanayozungumziwa. Katika mjadala hakuna kuwania ushindi; yeyote ambaye ana la kusema huruhusiwa na hutoa hoja kama apendavyo kuhusu mada ile inayohusika bila kukiuka ukweli uliopo.

     Mwisho, ni lazima kuelewa kuwa mdahalo na mjadala huhusiana na huhitilafiana kwa namna moja au nyingine. Ninyi nyote mnaohusika na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili msisahau kwamba mdahalo na mjadala ni nyenzo timamu za kuimarisha stadi ya maongezi ya lugha ya Kiswahili na msichague mada ambazo hazitawawezesha kutimiza malengo yenu kwani zinazozungumziwa katika midahalo hutofautiana na zile zinazojadiliwa katika mijadala.

     Maswali ya ufahamu
     1. Watu wanaohusika na lugha ya Kiswahili hujiuliza maswali kuhusu nini?
     2. Mada ya mdahalo huchaguliwa vipi?
     3. Toa dhima nne za mdahalo na mjadala kwa wanafunzi.
     4. Eleza mambo manne yanayohusisha mdahalo na mjadala.
     5. Toa tofauti mbili zilizopo kati ya mdahalo na mjadala.
     6. Tofautisha wahusika wa mdahalo na waahusika wa mjadala.
     7. Katika mdahalo watetezi hutoa hoja zao namna gani?
     8. Katika mjadala wasemaji hutoa mawazo yao namna gani?
     9. Tofautisha mwisho wa mjadala na mwisho wa mdahalo.
     10. Ni ushauri gani unaowapa wale wanaoandaa midahalo na mijadala?

     20.2 Msamiati kuhusu “Midahalo na Mijadala”
     Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu uhusiano na tofauti kati ya mdahalo na mjadala.

     1. Ushindi                                6. Fursa
     2. Kupiga kura                         7. Kutokubaliana
     3. Kuunga mkono                    8. Msemaji mkuu
     4. Kuhitilafiana                         9. Kwa madhumuni
     5. Hadharani                           10. Migogoro

       Zoezi la 3: Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.       Zoezi la 4: Tafuta katika mraba wa hapo chini maneno kumi yanayoweza kutumiwa kwenye majadiliano.

     Zoezi la 5: Jaza nafasi kwa kutumia maneno mwafaka yafuatayo:migogoro, msemaji mkuu, mdahalo, mjadala, uhusiano, ishara, anayeruhusiwa, unaohusisha, kushindana, kukiuka.
     1. Madhumuni ya mjadala si .............. bali ni kutoa hoja kuhusu jambo fulani.
     2. Wasemaji wakuu kwa upande wa utetezi katika.......... wanaitetea mada.
     3. Mwenyekiti ndiye anayempangia ........... muda wa kutoa hoja.
     4. Katika ........... hakuna kuwania ushindi.
     5. Uhusiano ...........mdahalo na mjadala ni lengo la kukuza uwezo wa maongezi miongoni mwa wanafunzi
         kwa kukuza kiwango chao cha msamiati.
     6. Katika mdahalo msemaji mkuu anaweza.......... ukweli kwa lengo la kupata ushindi.
     7. Katika mdahalo na mjadala hakuna ...............kutoa hoja bila kuomba fursa.
     8. Mdahalo na mjadala ni nyenzo bora za kutatua .......... inayoweza kuzuka kati ya watu au kati ya makundi.
     9. Watu wanapaswa kufahamu kwamba kuna tofauti na ......... kati ya mdahalo na mjadala.
     10. Katika mdahalo, kila mtu ambaye ana la kusema hutoa ............. ya kumjulisha kiongozi kwamba anahitaji fursa ya kusema.

     20.3 Sarufi: Matumizi ya Hali ya Kushurutisha kwa Vitenzi vyenye Kiam-bishi Tamati –a- katika Hali Kanushi.
     Zoezi la 6:
     1. Soma kifungu cha habari kuhusu “Uhusiano na Tofauti kati ya Mdahalo na Mjadala” huku ukitafuta sentensi zenye
        vitenzi ambavyo viko katika hali ya kushurutisha; kisha ueleze ikiwa vitenzi hivyo viko kwenye hali yakinishi au kanushi.
     2. Kwa kuiga mifano inayopatikana kwenye kifungu cha habari, ulichokisoma, tunga sentensi kumi ambazo zina vitenzi
          vyenye silabi zaidi ya moja na vyenye kiambishi tamati “-a” kwa umoja na wingi katika hali kanushi hali ya kushurutisha.

     Maelezo muhimu
     • Hali ya kushurutisha kwa vitenzi ambavyo vina silabi zaidi ya moja na ambavyo vina kiambishi tamati “-a” katika hali
       kanushi, huchukua kiambishi “si-” baada ya kiambishi cha umoja “u” cha nafsi ya pili kiambishi cha wingi “m” cha nafsi ya pili.
     • Katika hali kanushi ya vitenzi hivi, ni lazima kuweka kiambishi tamati “-e” katika umoja wingi.
      

     Maswali: Weka sentensi za hapo chini katika wingi au umoja.
     3. Usiseme hadharani bila ruhusa.
     4. Usipige kelele kwenye mdahalo au mjadala.
     5. Usiwaangalie watu kwa shingo upande wakati wa mdahalo na mjadala.
     6. Usiwazomee watu wakati wa maongezi.
     7. Usitoe mawazo hadharani kwa mawazo ambayo huyajui.
     8. Usionyeshe kuwa una uoga wa kuongea hadharani.
     9. Usimnyime fursa yule ambaye ana hoja.
     10. Usilete fujo kwenye mdahalo au mjadala.
     11. Usijidanganye kuwa mdahalo ni maana ya pili ya mjadala.
     12. Usiwazuie wanafunzi kufanya majadiliano.

     Zoezi la 8: Weka sentensi za hapo chini katika hali ya kushurutisha. Hali yakinishi au kanushi.
     Mfano 1: Kalisa anapenda mdahalo.
     Jibu : Kalisa, penda mdahalo

     Mfano 2:Wanafunzi hawakosi muda wa kujadiliana.
     Jibu : Wanafunzi, msikose muda wa kujadiliana
     1. Wewe unachagua mada ya mjadala.
     2. Walimu hawaandai midahalo ambayo si lazima.
     3. Ninyi hampendi fujo katika mjadala.
     4. Wewe unaandaa mdahalo kuhusu usawa wa kijinsia.
     5. Walimu hawakatazi wanafunzi kutoa hoja kuhusu mada fulani.
     6. Ninyi hamkubaliani na upande mwingine.
     7. Wapinzani hawaungi mkono watetezi.
     8. Watetezi wanatetea mada.
     9. Mwenyekiti anaongoza majadiliano
     10. Washiriki wanatoa mchango wao.

     Zoezi la 9: Weka sentensi za hapo chini katika hali kanushi.
     1. Piga kelele katika mdahalo.
     2. Kiongozi, mpangie kila msemaji muda mrefu sana.
     3. Walimu, mwambieni wanafunzi kufanya mdahalo kila mara.
     4. Wapinzani, teteeni mada.
     5. Wanafunzi, zungumzeni hadharani kila wakati.

     20.4 Matumizi ya Lugha: Mdahalo na Mjadala
     Zoezi la 10: Panga maneno yafuatayo kwa utaratibu unaofa:
     1. iliyojadiliwa anatoa kiongozi kuhusu suluhisho wa mada mjadala
     2. na mbili hakuna katika mpinzani yaani utetezi pande mjadala
     3. huwawezesha na hadharani kuongea wanafunzi mdahalo mjadala

     Zoezi la 11: Soma maelezo muhimu yafuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini.
      Mjadala na mdahalo ni mambo mawili yanayohusiana na kutofautiana.
     Uhusiano kati ya mjadala na mdahalo
     1. Mjadala na mdahalo huhusisha watu wengi wanaojadiliana kuhusu jambo Fulani.
     2. Katika mjadala na mdahalo kuna mada ambayo hutolewa mawazo, na mada hiyo ndiyo ambayo inamulika mjadala na
         mdahalo. Kiongozi wa mdahalo au mjadala hulazimika kuwaonya wasemaji kutokiuka mada.
     3. Mdahalo na mjadala huwa na malengo sawa ya:
         a. Kukuza uwezo wa kitaaluma na hali ya udadisi kwa washiriki wa mjadala na mdahalo
         b. Kukuza uwezo wa kushawishi watu hadharani ili wakubaliane na mawazo ya msemaji kuhusu jambo fulani.
         c. Kumwezesha mtu kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri wakati anapoandika insha au habari.
         d. Kumwezesha mtu kutambua kipaji alicho na cho cha kuzungumza bila aibu mbele ya hadhira.
         e. Kukuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kutumia msamiati na matamshi bora ya lugha.
         f. Kumuzoeza mtu kusikiliza na kupinga au kutetea maoni na hoja za wengine.
        g. Kuwapa watu wasaa wa kuelewana na wengine kutoka maeneo mbalimbali.

     Tofauti kati ya mdahalo na mjadala
     1. Tofauti ya kwanza kati ya mdahalo na mjadala ni wahusika. Katika mdahalo kuna mwenyekiti, katibu, wasemaji wakuu wa
         upande wa utetezi na upinzani na hadhira lakini kwenye mdahalo kuna kiongozi na hadhira tu.
     2. Katika mdahalo kuna wasemaji wakuu wanaotetea au wasiokubaliana na mada lakini kwenye mjadala kila yeyote anayetaka
         kutoa hoja anaruhusiwa na kiongozi.
     3. Kwenye mdahalo kuna pande mbili yaani upande wa utetezi na wa upinzani lakini kwenye mjadala hakuna makundi ya
         utetezi na upinzani.
     4. Mdahalo ni mashindano na mwishoni mwake washindi hupigiwa makofi lakini kwenye mjadala hakuna washindi; kiongozi wa
         mjadala anatoa suluhisho kutokana na mawazo yaliyotolewa. Mjadala si mashindano.

     Maswali
     1. Kwa kutumia maneno yako binafsi, eleza uhusiano uliopo kati ya mdahalo na mjadala.
     2. Jadili tofauti iliopo kati ya mjadala na mdahalo.

     20.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
     Zoezi la 12: Jadili nafasi na umuhimu wa midahalo na mijadala katika kudumisha amani na mshikamano katika jamii.

     20.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari
     Zoezi la 13: Kwa kuzingatia uhusiano na tofauti kati ya mdahalo na mjadala, tunga kifungu cha habari kuhusu mada ifuatayo: “Mijadala ndiyo njia ya kuinua uchumi katika jamii nyingi za kiafrika.”

     SOMO LA 21: UTEKELEZAJI WA MDAHALO


     Zoezi la 1: Tazama kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yanayofuata hapo chini
     Jibu maswali yafuatayo:
     a. Eleza wanachofanya watu unaowaona kwenye mchoro.
     b. Eleza wajibu wa mzazi katika malezi ya mtoto.
     c. Fafanua majukumu ya walimu katika elimu ya watoto.

     21.1 Kusoma na Ufahamu: Mdahalo
     Soma mdahalo ufuatao wenye mada: “Wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao”, halafu, jibu maswali yaliyopo hapo chini
     Mwenyekiti:  Waheshimiwa mabibi na mabwana mliokusanyika hapa leo, kwanza ninataka niwakaribishe katika mdahalo huu.
                           Hapa mbele yenu, mimi ni mwenyekiti, jina langu ni Alice. Pembeni mwangu upande wa kushoto mnamwon
                           katibu wa mdahalo wetu Muhire.Mdahalo wetu unazihusisha pande mbili : upande wa utetezi na upande wa 
                           upinzani. Mada ya mdahalo wa leo kama mnavyoisoma ubaoni ni “WAZAZI NDIO WENYE JUKUMU LA
                           KWANZA KATIKA MALEZI YA WATOTO WAO”. Kila msemaji atakayepewa fursa ya kuzungumza asizidi dakika
                           tatu. Bila kupoteza muda, ningependa kumkaribisha bwana Mutabazi ambaye ni msemaji mkuu wa kwanza wa  
                           upande wa utetezi ili atoe hoja zake kuhusu mada yetu.

     Mutabazi: Ninawashukuru sana mwenyekiti, katibu, wapinzani, watetezi na wasikilizaji washiriki wote mnaoshiriki katika
                       mdahalo huu. Ni kweli kabisa kwamba wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao.
                       Kama  inavyojulikana, malezi ya kwanza kwa mtoto huanzia nyumbani. Nyumbani ndipo mtoto anapopata
                       malezi ya msingi ambayo humulika maisha yake. Malezi haya ya kwanza yapatikanayo nyumbani humsaidia
                       mtoto kufanikiwa katika maisha yake. Malezi haya yanatolewa na wazazi ambao ndio walezi muhimu wa
                       watoto  wao. Bila mchango wa wazazi, watoto hawawezi kupata elimu. Kwa hiyo, wazazi wana jukumu la
                       kwanza katika malezi ya watoto wao. Bila wazazi hakuna malezi kwa watoto. Ahsanteni kwa kunitega sikio.

     Mwenyekiti: Asante sana Bwana Mutabazi kwa hoja zako. Kama mlivyosikia, msemaji huyu ameeleza kwamba wazazi
                          ndio wanaowapatia watoto wao malezi ya msingi ambayo yanawasaidia kufanikiwa maishani. Vipi wa upande
                           wa upinzani, mnakubaliana na Mutabazi? Acha tumkaribishe msemaji mkuu wa kwanza wa upande wa
                           upinzani Kayitesi ili naye atoe hoja zake.

     Kayitesi: Mwenyekiti, katibu, watetezi, wapinzani wenzangu na wasikilizaji washiriki, ahsanteni sana kwa kunipa fursa hii
                      ili nami nitoe maoni yangu kuhusu mada ya madahalo wetu. Mimi sikubaliani kabisa na hoja alizozitoa
                      Mutabazi. Yeye amesema kwamba wazazi ndio ambao wanawapatia watoto malezi ya msingi yanayomulika
                      maisha yao. Kwa upande wangu, kila mzazi lazima ashiriki katika malezi ya watoto wote anaokutana nao badala
                      ya kufikiria watoto wake tu. Kumbukeni kuwa jambo hili ni miongoni mwa maadili mema yanayotutambulisha
                      kama Wanyarwanda. “Mlee mtoto yeyote kama wako”.


                      Hivyo basi, ni lazima tufahamu kwamba mtoto anajifunza kwa kuangalia mazingira yanayomzunguka. Mtoto,
                      anatazama na kuiga tabia na matendo ya watu wote anaowaona mahali anapoishi wakiwemo wazazi, ndugu,
                      wanafamilia, majirani na watu wengine wote wanaokuja nyumbani. Mwenendo na vitendo vya watu hao
                      wanaomzunguka mtoto humwathiri vizuri au vibaya; yaani hayo yote ndiyo yanayomlea mtoto huyo. Majukumu ya
                      watu hao wote wanaomzunguka  mtoto lazima wahakikishe kuwa mtoto huyo ameathirika vizuri kutokana na  
                       matendo yao mazuri.Kwa hiyo, wazazi sio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto bali walezi muhimu
                       wa mtoto ni watu wote wanaomzunguka mtoto.

     Mwenyekiti: Ninamshukuru sana Bi Kayitesi kwa maoni yake. Yeye ameeleza kwamba malezi ya mtoto si jukumu la wazazi
                          tu bali ni jukumu la kila mtu. Je, Watetezi, mnasema nini kuhusu maoni yake Kayitesi? Ningependa kumkaribisha
                           msemaji mkuu wa pili wa upande wa utetezi. Uwamahoro, simama ili utoe maoni yako na uheshimu muda
                           uliopangwa.

     Uwamahoro:Mheshimiwa mwenyekiti, katibu na wasikilizaji washiriki, mimi ninataka kuyahakiki mawazo ya mpinzani Kayitesi.
                           Yeye amesema kwamba malezi ya msingi kwa watoto ni jukumu la kila mtu anayeishi pamoja na mtoto. Kama
                           ninavyoona,maoni yake hayatofautiani na maoni yetu kama watetezi, na ninamshukuru sana kutuunga mkono.
                           Watu ambao wako karibu sana na watoto ni wazazi wao ambao wana mchango wa kwanza katika malezi ya
                           watoto hao.Huwatunza watoto wao, tangu wanapozaliwa na wakati wa kwenda shule unapofika, wao ndio
                           wanaopiga hatua ya kwanza kuwapeleka shuleni. Hili si jukumu la kila mtu bali ni wajibu wa kila mzazi kupeleka
                           mtoto wake shuleni. Hata na wakati watoto wanapofika shuleni ndipo wazazi huwajibika kufuatilia malezi ya
                           watoto wao. Wao huwashauri watoto wao, huwafundisha kuwa na mwenendo mwema, huwanunulia watoto vifaa
                           vya shule na kuwalipia karo watoto wao. Waheshimiwa wasikilizaji, kama mnavyoelewa, bila mchango wa wazazi,
                           watoto hawawezi kupata elimu inayotolewa shuleni kwani wao ndio wanaorahisisha kila jambo linalotendewa
                           mtoto kwa kumlea vizuri.

     Mwenyekiti: Naam, waheshimiwa wasikilizaji washiriki, mawazo hayo ya Uwamahoro mmeyasikia. Sasa ninataka
                           kumkaribisha msemaji mkuu wa pili wa upande wa upinzani Mugisha ili naye atoe maoni yake. Karibu sana
                           Bwana Mugisha,toa hoja zako kuhusu mada yetu.


     Mugisha:Mwenyekiti, katibu, na wasikilizaji washiriki asanteni sana kwa kunipa fursa hii. Mimi ninaunga mkono kabisa
                     wazo lililoelezwa na mwenzangu Kayitesi ambaye alisema kwamba malezi ya mtoto ni jukumu la kwanza la
                     kila mtu. Wapendwa wasikilizaji washiriki, kabla ya kutoa mawazo yangu, kwanza nina maswali kwa watetezi
                     wa mada yetu. Uwamahoro alisema kwamba bila ya wazazi, watoto hawawezi kupata malezi na kwenda
                     shuleni. Lakini, taifa ndilo ambalo huchukua nafasi ya kwanza katika malezi ya watoto, maana shule
                     nyingi hujengwa na serikali ili watoto wapate malezi bora. Na kama mnavyojua siku hizi kila mtoto ana
                     haki ya kupelekwa shuleni na kufuata masomo yake bila kulipa chochote toka shule za msingi hadi shule
                     za upili. Kwa kweli, hilo ni jukumu la serikali ya nchi kujenga shule hizo ambapo wazazi hupeleka watoto
                     wao kwa ajili ya kupata elimu. Kwa hiyo, ni wazi kwamba serikali inawajibika kwanza kuzijenga shule na
                     wazazi huja baadaye kupeleka watoto wao. Serikali hugharamia mafunzo hayo kwa watoto na huweza
                     kuwalipia wengi wanaotaka kuendelea na viwango vingine vya elimu katika vyuo vikuu na shule za
                     ufundi. Vilevile, familia ambazo hazijiwezi kiuchumi, watoto wao hupata misaada mingi kutoka serikali
                     katika malezi yao.

                     Kutokana na hayo yote na mengine ambayo sikutaja hapa, ni dhahiri kusisitiza kwamba wazazi ndio wenye
                     mchango wa kwanza katika malezi ya watoto ni kujidanganya na kupotosha ukweli wa mambo. Kufanya hivi
                     ni kama kupuuza mchango wa watu wengine kama vile serikali ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa
                     katika malezi ya watoto kuliko wazazi wao. Wasikilizaji washiriki, Waheshimiwa wapendwa nyote mliokusanyika
                     hapa, tusidanganyike sana kuwa wazazi ndio wenye mchango mkubwa katika malezi ya watoto wao. Asante
                     sana kwa kunitega sikio.

     Mwenyekiti:Ninamshukuru Bwana Mugisha kwa maoni yake ambayo yamewasisimua wengi. Yeye alisema kwamba
                          jukumu la kwanza katika malezi ya watoto ni la taifa, yaani Serikali na watu wengine. Ninadhani kwamba
                          watetezi wangesema mengi kuhusu mawazo hayo, lakini ninapoangalia saa yangu naona muda
                          unazidi kuyoyoma. Lakini kwa hakika, mengi yamekwishatolewa na wasemaji wakuu wa pande zote
                          mbili. Sasa ebu nichukue fursa hii kuwakaribisha wasikilizaji washiriki ambao nao wana la kusema ili
                          watoe hoja zao kuhusu mada yetu. Tafadhali, atakayechukua fursa awe anasema kwa machache na
                          asizidi dakika mbili. Wale ambao wanahitaji kupewa fursa ya kusema wanakaribishwa.
                          
                          (wale ambao wanahitaji fursa wanaonyesha mwenyekiti ishara na yeye anamkaribisha Bwana Furaha)

                           Karibu Bwana Furaha!

     Furaha: Bibi mwenyekiti, Bwana katibu, mabibi na mabwana, mawazo yaliyotolewa na pande mbili ni mazuri sana
                    na yanaeleweka waziwazi. Lakini, mimi sikubaliani na mawazo ya wapinzani. Ndiyo sababu ninataka
                    kuwaunga mkono watetezi wa mada kwa kusisitiza kwamba wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika
                    malezi ya watoto wao. Wahenga walisema: “Mtoto hutazama kisogo cha mama yake”. Mzazi ni mfano
                    unaoigwa na mtoto wake. Kama mzazi ana tabia nzuri mtoto naye bila shaka ataathiriwa vizuri na itakuwa
                    kinyume kama mzazi ana tabia zisizopendeza. Wazazi ndio wanaowamotisha watoto kwenda shuleni kupata
                    elimu. Vilevile, kama mtoto ana tatizo shuleni, mzazi ndiye wa kwanza ambaye huitwa, tena, mzazi ndiye
                     anayechunguza ikiwa mtoto wake anafanikiwa shuleni na kutatua matatizo anayokutana nayo katika malezi yake.

     Mwenyekiti: Asante Bwana Furaha kwa mawazo yako. Naona kuna wengine wanaonyosha mikono yao kwa kutoa
                          michango. Karibu sana bibi! Toa maoni yako na jaribu kupaza sauti ili sote tuweze kukusikiliza vizuri.

     Mugeni:   Bibi Mwenyekiti, katibu, wasikilizaji washiriki! Msifikiri kwamba mawazo yaliyotolewa na watetezi yanagusia
                      uhalisi wa mambo. Mimi sikubaliani na maoni yao na haswa hoja zilizotolewa na Bwana Furaha. Ni lazima
                      waelewe kwamba kila wakati mtoto hulelewa na watu wote wanaomzunguka ambao huweza kumwathiri
                      vizuri au vibaya kulingana na mienendo na tabia zao. Mtoto afikapo shuleni, malezi yake huwa zaidi
                      mikononi mwa walimu na viongozi wa shule ambao hufanya kazi kubwa ya kuwalea watoto na kuwaelimisha.
                      Kwa upande wangu, sikubali kwamba wazazi ndio wenye mchango mkubwa katika malezi ya mtoto kwani
                       mtoto huyo humaliza muda mrefu mikononi mwa walimu na viongozi wa shule wanaomsaidia kurekebisha
                       tabia mbaya na kuendeleza tabia nzuri huku wakimpa elimu itakayomfaa katika maisha yake. Wasikilizaji
                       wenzangu, mimi ninaona kwamba walimu na viongozi hao wa shule ndio wenye mchango mkubwa zaidi
                       katika malezi ya watoto. Ahsanteni sana kwa kunitega sikio.

     Mwenyekiti: Asante sana Bi Mugeni. Ninawashukuru nyote kwa kuhudhuria mdahalo wa leo. Sasa inaonekana
                          kwamba mdahalo wetu unakaribia kufikia mwisho. Ebu nimkaribishe Bwana katibu ili atusomee mawazo
                          yote yaliyotolewa na washiriki wa mdahalo huu.

     Katibu:    Bibi mwenyekiti, watetezi, wapinzani na wasikilizaji washiriki, ahsanteni sana. Kwanza kabisa ningependa
                     kuwapongeza ninyi nyote kwa maoni na mawazo yenu mliyotoa katika mdahalo huu.

     Wasemaji wa upande wa utetezi walitetea mada kwa kutoa mawazo yafuatayo:
     • Wazazi ndio wanaotoa malezi ya msingi kwa watoto wao.
     • Wazazi wana jukumu la kuwatunza watoto.
     • Wazazi huwanunulia watoto vifaa vya shule.
     • Wazazi hulipa karo kwa elimu ya watoto wao.
     • Wazazi hufuatilia jinsi watoto wao wanavyoelimishwa na kushauri watoto wao.
     • Watoto huiga tabia za wazazi wao.

     Kwa upande mwingine, wapinzani hawajakubaliana na watetezi. Wao walisisitiza kwamba wazazi sio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao na walitoa maoni yafuatayo:
     • Malezi ya mtoto ni jukumu la kwanza la kila mtu.
     • Watu mbalimbali wanaomzunguka mtoto ndio wanaochangia sana katika malezi yake.
     • Serikali ina wajibu mkubwa katika malezi ya watoto.
     • Serikali hujenga shule kwa ajili ya elimu ya watoto.
     • Serikali ndiyo ambayo huwahimiza wazazi kupeleka watoto shuleni.
     • Walimu na viongozi wa shule nao wana mchango mkubwa katika malezi ya watoto kuliko wazazi wao.

     Walimu na viongozi wa shule hulea watoto kwa kuwasaidia kurebisha tabia mbaya na kuwa na mienendo mizuri.

     Walimu na viongozi wa shule huelimisha watoto.

     Mwenyekiti: Waheshimiwa mabibi na mabwana mliokuja hapa leo, mawazo yote mmesomewa. Sasa ni wakati wa
                           kupiga kura ili tujue washindi wa mdahalo. Wale mnaowaunga mkono watetezi, njooni hapa mbele,
                           na wale mnaowaunga mkono wapinzani bakini pale mnapoketi.

                          (Katibu anawahesabu wanaounga mkono kila upande.)

     Katibu: Upande wa utetezi umepata kura ishirini na nne ( anaandika 24 ubaoni) na upande wa upinzani umepata
                   kura ishirini na mbili (anaandika 22 ubaoni).

     Mwenyekiti: Mabibi na mabwana, kama inavyodhihirishwa na matokeo ya kura, ushindi katika mdahalo wa leo
                          umekwenda upande wa utetezi. Naomba muwapigie makofi.

                         (Hadhira inawapigia makofi watetezi.)

                          Ninawashukuru nyinyi nyote, mdahalo wa leo umemalizika. Kwaherini.

     Maswali ya ufahamu
     1. Mada ya mdahalo huu ni ipi?
     2. Taja jina la katibu wa mdahalo huu.
     3. Ni nani ambaye ametoa hoja ya kwanza kwenye upande wa utetezi? Alitoa hoja gani?
     4. Kayitesi yuko katika upande gani? Eleza maoni yake kuhusu mada ya mdahalo.
     5. Je, Uwamahoro anakubaliana na mawazo ya Kayitesi? Kwa sababu gani?
     6. Taja majina ya watu wote ambao walitoa mawazo wakiitetea mada ya mdahalo.
     7. Fafanua mawazo matatu ambayo yalitolewa na upande wa utetezi.
     8. Eleza maoni mawili ya wasemaji wa upande wa upinzani.
     9. Kati ya watetezi na wapinzani ni kina nani waloibuka washindi?
     10. Kutokana na mdahalo huu, mtazamo wako ni upi?

     21.2 Msamiati kuhusu Mfano wa Mdahalo
     Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu mfano wa mdahalo.

     1. Malezi                                      6. Kuunga mkono
     2. Kumkaribisha                           7. Sikubaliani
     3. Elimu                                        8. Serikali
     4. Maisha                                      9. Bakini
     5. Hawawezi                                10. Karo

        Zoezi la 3: Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.          Zoezi la 4: Panga vizuri herufi za hapo chini ili ziunde maneno ya Kiswahili sanifu.


     Zoezi la 5: Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo: wazazi, jukumu, malezi, mada, wasikilizaji washiriki, hupiga kura, zinaathiri, sikubaliani, ninaunga mkono, maoni.
     1. Mwenyekiti anawaomba ................. kuwapigia makofi washindi wa mdahalo.
     2. Walimu nao wana umuhimu mkubwa katika ........... ya watoto.
     3. Tabia za watu wanaoishi karibu na mtoto .............. malezi yake.
     4. Mimi ............... na msemaji aliyesema kwamba wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto.
     5. Waheshimiwa mliokusanyika hapa leo, .......... ya majadiliano yetu ni “Wake na waume wana uwezo sawa”.
     6. Malezi ya watoto ni ........la kila mwananchi.
     7. Ahsante sana Kayitesi kwa kutoa ........... yako.
     8. .........wana mchango mkubwa katika mwenendo mwema wa watoto wao.
     9. Nami ..........mtazamo wa wapinzani wa mada.
     10. Baada ya kusomewa mawazo yaliyotolewa, hadhira ..........

     21.3 Sarufi: Matumizi ya Hali ya Kushurutisha katika Vitenzi vya Mkopo, Hali Yakinishi na Hali kanushi.

     Zoezi la 6: Jadili kuhusu maana ya sentensi zifuatazo zenye kitenzi ambacho kiko katika hali ya kushurutisha; halafu tunga sentensi tatu ukitumia hali ya kushurutisha katika hali yakinishi na kanushi.
     1. Wapinzani, bakini pale mnapoketi.
     2. Msifikiri kwamba mawazo yaliyotolewa na watetezi ni kweli.
     3. Jaribu kupaza sauti.

     Maelezo muhimu

     Hali yakinishi

     Vitenzi vya Kiswahili vyenye viambishi tamati -i , -e na ¬-u, katika hali ya kushurutisha au ya kuamrisha vinaondolewa kiambishi cha kitenzi ku- katika umoja hali yakinishi.Katika wingi, vinaondolewa kiambishi ku-, halafu vikachukua –ni baada ya viamishi tamati –i, -e na –u.
       

     Zoezi la 8: Zikamilishe sentensi zifuatazo kwa kutumia hali ya kushurutisha ya vitenzi ambavyo vimo katika mabano.

     Kwa mfano: Swali: Kama wewe ni katibu, ........... kuandika mawazo yote yanayotolewa. (kujaribu: hali yakinishi)

     Jibu: Kama wewe ni katibu, jaribu kuandika mawazo yote yanayotolewa.
     1. Ninyi.................. katika maongezi. (kushiriki, hali yakinishi)
     2. ..........wenzako wanaotoa mawazo kinyume na yako.(kukejeli, hali kanushi)
     3. Wewe ................ mtu kuwatukana wengine ambao hawaungi mkono mawazo yake. (kuruhusu: hali kanushi)
     4. .........vibaya malezi ya mtoto wako. (kuathiri, hali kanushi)
     5. Wewe ............ kwamba majadiliano ni Wenzo bora wa kudumisha amani na upendo. (kuamini, hali yakinishi)

     Zoezi la 9: Soma maelezo muhimu kuhusu hali kanushi ya vitenzi vyenye viambishi tamati ambavyo ni –e, -i na –u kisha ujibu maswali yalipo hapo chini.

     Maelezo muhimu
     Hali kanushi

     Katika hali ya kushurutisha kwa vitenzi vyenye viambishi tamati -i, -e na ¬-u ,katika hali kanushi kwa umoja vinachukua “si-“ mwanzoni na kwa wingi vinachukua “si-“ vikabaki na viambishi tamati -i, -e na ¬-u.  

     Maswali: Weka sentensi za hapo chini katika wingi au umoja
     1. Usidharau mawazo ya wengine katika mdahalo.
     2. Msisahau kutumia matamshi bora katika majadiliano.
     3. Usimdhuru mwenzako.
     4. Usikubali kushindwa kwa sababu ya kutopaza sauti.
     5. Msidhani kwamba midahalo ni kama mijadala.
     6. Usimsamehe mtu anayenyanyasa mwanamke.
     7. Usisalimu hadhira kwa uoga.
     8. Ukipewa jaribio kuhusu mfano wa mdahalo, usinakili.
     9. Usiwasihi watu kukubaliana na mawazo ambayo hayalengi kudumisha amani.
     10. Usijaribu kusema uongo wakati wa majadiliano.

     21.4 Matumizi ya lugha: Utekelezaji wa Mdahalo
     Zoezi la 10: Chunguza maelezo haya kuhusu utekelezaji wa mdahalo kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini.

     Maelezo muhimu kuhusu mfano wa mdahalo:
     Ingawa watetezi ndio ambao walipata ushindi katika mdahalo wa hapo juu, haimanishi kwamba wazazi ndio pekee wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto. Kuna watu wengi sana wanaohusika katika malezi ya watoto wakiwemo walimu, viongozi wa shule, ndugu, wanafamilia, taifa na wengine. Wananchi wote wanatakiwa kushikamana ili watoto wetu wapate malezi bora.

     Wakati mdahalo unapofanywa:
     • Mwenyekiti huwa na majukumu ya kuongoza mdahalo kama ipasavyo, kumpangia kila msemaji muda wa kutoa maoni
       yake, kuongoza upigaji kura ili kujua washindi na kutoa suluhisho la mdahalo.
     • Katibu ana jukumu la kuandika mawazo yote yaliyotolewa na kila msemaji na kuyasomea hadhira mwishoni mwa
        mdahalo. Katibu tena huandika , huhesabu na hutangaza matokeo ya kura.
     • Wasemaji wakuu kwa kila upande wanalazimika kutoa maoni yao kwa kutetetea au kutokubaliana na mada kutokana
        na pande zao. Wanatoa mawazo yao ili pande zao ziweze kushinda. Kila anayepewa fursa analazimika kutumia
        muda aliopangiwa.
     • Washiriki nao wanafuata mdahalo na wanaweza kushiriki kwa kuungama upande mmoja kati ya utetezi na upinzani,
        pia wanashiriki kwa kupiga kura ili washindi wa mdahalo wapatikane.

     Mambo ya kuepuka katika mdahalo:
     • Kupiga kelele• Kusababisha fujo
     • Kupoteza muda bure
     • Kutumia lugha yenye matusi
     • Kutoheshimu wenzako
     • Kukejeli amri kutoka kwa mwenyekiti

     Maswali:
     1. Taja wadau wote wanaohusika katika malezi ya watoto.
     2. Eleza wajibu wa kila mhusika anayehusika na malezi ya watoto.
     3. Fafanua majukumu ya wahusika wa mdahalo.
     4. Eleza mambo mabaya ya kuepuka katika mdahalo.

     21.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
     Zoezi la 11: Kwa kushirikiana na wenzako, jadili kuhusu mada moja kati ya hizi hizi zifuatazo:
     1. Wavulana wana uwezo sawa na wasichana
     2. Ukimwi ndio ugonjwa wa kwanza unaooathiri zaidi maendeleo ya jamii.
     3. Malezi kwa wote ni jukumu la kila mwanchi.

     21.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari
     Zoezi la 12: Andika kifungu cha habari kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo:
     1. Serikali ndiyo ambayo ina jukumu kubwa la elimu ya watoto.
     2. Bila elimu hakuna maendeleo.

     SOMO LA 22: UTEKELEZAJI WA MJADALA

     Tazama kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yanayofuata hapo chini


     Zoezi la kwanza: Jibu maswali yafuatayo:
     • Eleza wahusika unaowaona kwenye mchoro huu.
     • Dhihirisha matatizo yanayosababishwa na matumizi ya madawa ya kulevya?
     • Umejifunza nini kutokana na unayoyaona kwenye mchoro?

     22.1 Kusoma na Ufahamu: Mjadala
     Soma mjadala ufuatao wenye mada: “Matatizo Makuu Yanayokwamisha Maendeleo katika Jamii ya Rwanda”, kisha jibu maswali uliyopewa hapo chini.

     Mwenyekiti wa mjadala:  (Anasimama) Waheshimiwa mabibi na mabwana mliokusanyika hapa leo, mada ya mjadala
                                               wetu kama mnavyoiona hapo mbele yenu, ni “MATATIZO MAKUU YANAYOKWAMISHA
                                               MAENDELEO KATIKA JAMII YA RWANDA”.Karibuni sana nyote na bila kupoteza muda,
                                               ningetaka kumkaribisha mshiriki aliye tayari atoe mchango wake.

     Msemaji wa kwanza:       Asante sana mwenyekiti kwa fursa hii ya kutoa mchango wangu. Kwa maoni yangu, matatizo
                                               makuu yanayokwamisha maendeleo ya jamii yetu ni pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya.
                                               Siku hizi, watu wengi hasa hasa vijana, wanakumbwa na matumizi ya madawa ya kulevya kama
                                               kokeni, heroini, bangi na miraa. Madawa ya kulevya ni hatari sana kwa binadamu, kwa kuwa
                                               yanasababisha magonjwa mengi na kuharibu ubongo wa mwanadamu.

     Kiongozi:                          Asante sana kwa maoni yako. Mmesikia kuwa madawa ya kulevya yanaharibu sana maisha
                                               ya binadamu na yakawa kipingamizi kwa maendeleo. Ebu tumsikilize msemaji mwingine atupe
                                               maoni yake.
                           
                                              Msemaji wa pili: Asante sana mwenyekiti wa mjadala wetu kwa kunipa fursa hii ili nitoe maoni
                                              yangu kuhusu matatizo yanayokwamisha maendeleo katika jamii yetu. Kwa upande wangu, zaidi
                                              ya yale yaliyozungumziwa na msemaji aliyenitangulia, mimi ninafikiri kuwa magonjwa mbalimbali
                                              kama Malaria, Ukimwi, Kisukari na mengine, nayo yanaweza kukwamisha maendeleo ya jamii ya
                                              Rwanda. Kwa hakika, watu wenye maradhi hayo wanatumia mali nyingi kutibiwa, wakapoteza muda
                                              mrefu wakiwa hospitalini. Kwa hiyo, wao hukosa muda wa kujiendeleza na kuendeleza nchi yao.
                                              Magonjwa haya yanapojitokeza yanaiangamiza sana jamii na husababisha vifo vya watu wengi
                                              ambao wangetoa mchango wao wa kuendeleza nchi. Juhudi zilizopo za kupambana na magonjwa
                                              haya zinahitaji kutiliwa mkazo.

                                             Kuhusu ukimwi kwa mfano, ni lazima watu waepukane na tabia na mienendo mibaya inayosababisha
                                             maambukizi mapya. Wale ambao wameishaambukizwa nao lazima walifikirie suala hili ili watoe
                                             mchango wao wa kukomesha maambukizi mengine. Wachukue madawa kwa kuzingatia
                                             mawaidha wanayopewa na madaktari. Ninadhani kwamba hapa kila mtu anajua kuwa ukimwi
                                             ni ugonjwa ambao mpaka sasa hauna dawa wala chanjo na dawa zilizopo ni zile ambazo
                                             huwasaidia watu kuendelea kuishi ikiwa wanafuata maonyo na maagizo ya madaktari. Asante
                                             sana hayo ndiyo maoni yangu.

     Mwenyekiti:                    Asante sana msemaji kwa maoni yako mazuri. Tumsikilize pia yule mwanamke mwenye kanga
                                             nyekundu pale... Karibu bibi.

     Msemaji wa tatu:           Asante sana mwenyekiti. Mimi ninataka kumuunga mkono msemaji wa kwanza. Madawa ya kulevya
                                             ni hatari kabisa na ni kipingamizi kikubwa kwa maendeleo ya jamii. Watu wanaotumia madawa ya
                                             kulevya hawawezi kufikiri vilivyo. Hawawezi kufanya jambo lolote la kujiendeleza na kuendeleza
                                             jamii nzima. Unapowaita, “njooni tufanye miradi ya kujiendeleza,” wao wanakujibu kuwa hawakosi
                                             chochote. Hali kadhalika, ninataka kusisitiza kuhusu utumiaji wa pombe. Pombe nayo inaweza
                                             kuharibu sana maisha na matumizi yake yanakwamisha maendeleo ya jamii. Walevi wa pombe,
                                             badala ya kufanya kazi za kuwaendeleza, huzururazurura vilabuni tu. Ukiwaonya, “Msinywe pombe
                                             kwa kuwa pombe ni hatari kwa maisha yenu,” wao wanakuambia, “wewe hujui unachosema!” Na
                                             kukuchukulia kama mjinga. Jamani, tuwalinde na tuwashawishi vijana wetu wasinywe pombe kwa
                                             sababu ni mbaya kwa maisha ya watu. Tena, ikumbukwe kwamba pombe zinakatazwa hasa hasa
                                             kwa watoto wenye umri wa miaka chini ya kumi na minane.

     Mwenyeki:                      Asante sana kwa maoni yako. Matumizi mabaya ya pombe yanakwamisha maendeleo ya jamii na
                                             yanaharibu maisha ya watu. Namuona yule anayekaa pale, naye amenyosha mkono kwa kusema.
                                             Karibu sana.

     Msemaji wa nne:           Mimi ninadhani kuwa umasikini nao ni tatizo kuu linalokwamisha maendeleo ya jamii ya Rwanda.
                                             Watoto wanaotoka katika familia zinazokumbwa na ufukara hawawezi kupata elimu kwa urahisi. Na
                                             wanapojaribu kwenda shuleni, hawawezi kuendelea na masomo yao kwa sababu ya ukosefu wa
                                             uwezo wa kupata vifaa vya kutumia ili kuendelea na masomo yao. Vilevile, kama familia ni maskini
                                             haiwezi kupanga miradi ya kujiendeleza kwani haiwezi kupata rasilimali au mtaji wa kuanzisha miradi
                                             hiyo. Kila wakati, kazi wanazozifanya ni za kuwapatia posho ya kujikimu tu. Kwa hiyo, naona kuwa
                                             ufukara nao ni tatizo kuu linalokwamisha maendeleo ya jamii nchini.

     Mwenyekiti:                   Ninakushukuru sana kwa mchango wako. Inaonekana kwamba watu wengi wanataka kutoa mchango
                                            wao. Ebu nimkaribishe kijana yule huko nyuma. Karibu sana.

     Msemaji wa tano:         Asante sana mwenyekiti wa mjadala huu. Mimi sikubaliani na maoni ya msemaji aliyenitangulia.
                                            Serikali ya Rwanda ilizindua miradi chungu nzima ya kupunguza ufukara. Miradi hiyo imeinua maisha
                                            ya jamii ya Wanyarwanda. Serikali tena ilianzisha mpango wa elimu ya msingi kwa wote ya miaka
                                            tisa na miaka kumi na miwili ambayo huwasaidia wanafunzi kupata elimu ya msingi hadi shule za
                                            upili bila malipo yoyote. Kwa upande wangu, tatizo kubwa linalokwamisha maendeleo katika jamii ni
                                            mienendo mibaya inayojitokeza miongoni mwa baadhi ya wanajamii. Mimi nakubaliana na
                                            mwenzangu aliyezungumzia suala la matumizi ya madawa ya kulevya. Vijana wengi wenzangu
                                            huathiriwa na tabia mbaya za wenzao wanaotumia madawa ya kulevya na wakati huo wao hukosa
                                            nguvu za kulitumikia taifa lao kwani miili yao huwa imedhoofika sana kutokana na madawa hayo.

     Kiongozi:                      Mmm! Asante sana kijana. Naona muda unazidi kuyoyoma lakini, kabla ya kufunga mjadala wetu,
                                           ebu tusikilize maoni ya watu wengine wawili. Wewe hapo nyuma, toa mchango wako.

     Msemaji wa sita:          Ninakushukuru sana mwenyekiti kwa fursa hii uliyonipa. Kwa maoni yangu, ninataka kuunga mkono
                                           msemaji aliyenitangulia kwamba tabia na mienendo ya wanajamii ndiyo matatizo makubwa
                                           yanayokwamisha maendeleo. Ni lazima serikali yetu na viongozi wa shule wafikirie namna ya
                                           kukomesha mienendo hiyo haswa kwa watu walioelimishwa. Shida kubwa ni kwamba wengi wa wale
                                           wanaotumia madawa ya kulevya, walevi wa pombe na kadhalika ni watu waliosoma ambao sote
                                           tungewafikiria kuwa ndio mifano mizuri kwa wale ambao hawakubahatika kwenda shuleni.
                                           Chunguza vizuri katika kijiji chetu, ni wangapi wanaolala kwenye baa au vilabuni pindi wapokeapo
                                           mishahara yao ya mwezi? Hawa wote mara nyingi huwa ni watu walio na elimu ambayo ingewasaidia
                                           kufanya mambo mengi ya kuendeleza nchi yetu. Kwa hiyo, ni lazima jamii ya Rwanda iwe na tabia
                                           nzuri na iwe na nidhamu ya kuisaidia kufikiri vizuri na kupata uamuzi bora maishani kwani kupata
                                           elimu ni jambo moja, na kuitumia vizuri ni jambo jingine.

     Mwenyekiti:                  Asante sana kwa mchango wako. Ebu tumusikilize msemaji wa mwisho kabla ya kupata suluhisho.

     Msemaji wa saba :       Asante sana mwenyekiti. Mawazo yangu hayatofautiani sana na ya wale walionitangulia kuzungumza.
                                           Ni ukweli kwamba tatizo kuu linalokwamisha maendeleo ya Wanyarwanda ni matumizi ya madawa
                                          ya kulevya ambayo yanaingiliana na suala la ujinga. Kila mtu anaelewa kwamba mtu anapokosa
                                          uwezo wa kutofautisha jambo zuri na jambo baya, huyo huhesabiwa kati ya wajinga ambao
                                          hawapambanukiwi na mambo yaliyo muhimu zaidi. Kwa hiyo, awe mtu aliyesoma au mtu ambaye
                                          hakufika shuleni wote watawekwa miongoni mwa wajinga ambao hawajali maendeleo yao na ya
                                          nchi yao. Kutokana na jambo hilo, ni lazima kila mtu atoe mchango wake katika kuimarisha mienendo
                                          mizuri, maadili na mitazamo imara inayotutambulisha kama Wanyarwanda. Kila mtu anapaswa
                                          kuelewa kwamba jamii haiwezi kuendelea wakati ambapo ina watu wasio na fikra timamu. Vijana
                                          ndio wenye nguvu zaidi, sisi sote tunatakiwa kulea watoto wetu vizuri, kuwazoeza kufanya kazi
                                          mapema na kufikiria kupanga miradi ya kimaendeleo.

     Mwenyekiti:                Asante sana kwa maoni yako. Asante sana ninyi nyote mlioshiriki katika mjadala huu. Kichwa cha
                                         mjadala wa leo kilikuwa “Matatizo makuu yanayokwamisha maendeleo katika Jamii ya Rwanda”.
                                         Miongoni mwa matatizo hayo tuliyoyaona ni madawa ya kulevya, pombe, maradhi mbalimbali,
                                         ufukara, ujinga na uvivu. Asante sana mabibi na mabwana. Mjadala wa leo unaishia hapa. Njooni
                                         tena wakati mwingine kwa mada nyingine. Kwaherini.

     Maswali ya ufahamu
     1. Kutokana na mjadala uliosoma, tatizo la kwanza linalokwamisha maendeleo ni lipi? Eleza.
     2. Unakubaliana na maoni ya msemaji wa kwanza? Kwa nini?
     3. Toa mifano minne ya madawa ya kulevya.
     4. Ni madhara gani yanayotokana na matumizi ya madawa ya kulevya?
     5. Ni tatizo gani lililotajwa kwa mara ya pili. Lieleze.
     6. Unasemaje kwa hoja kwamba utumiaji wa pombe unaweza kukwamisha maendeleo ya jamii.
     7. Ni watu gani wanaoruhusiwa kunywa pombe?
     8. Umasikini unawezaje kukwamisha maendeleo ya jamii?
     9. Ni kweli kwamba ujinga unaweza kukwamisha maendeleo katika jamii? Eleza.
     10. Mjadala huu unakufundisha nini?

     22.2 Msamiati kuhusu Mfano wa Mjadala
     Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu mfano wa mjadala.
     1. Kukwamisha                                         6. Kipingamizi
     2. Jamii                                                     7. Maradhi
     3. Kukaribisha                                           8. Kuangamiza
     4. Madawa ya kulevya                              9. Ukimwi
     5. Kuharibu                                              10. Umaskini

          Zoezi la 3: Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B
      

     Zoezi la 4: Kamilisha maneno yafuatayo kwa kutumia herufi zinazokosekana ili yaweze kuleta maana

     Mfano     22.3 Sarufi: Matumizi ya Hali ya Kushurutisha katika vitenzi vyenye sila-bi moja hali yakinishi na kanushi
     Zoezi la 5: Jadili kuhusu maana ya sentensi zifuatazo; kisha utunge sentensi tano kama hizo.
     1. Njooni tupange miradi ya kujiendeleza.
     2. Mwingine atupe maoni yake.
     3. Msinywe pombe kwa sababu pombe ni hatari kwa maisha.

     Maelezo muhimu
          • Vitenzi vya silabi moja ni vitenzi vinavyobaki na silabi moja wakati vinapoondolewa kiambishi cha kitenzi ku-
          • Vitenzi vya silabi moja katika hali ya kushurutisha kwa umoja, hali yakinishi huchukua kiambishi ku- cha kitenzi,
            vinapowekwa kwa wingi katika hali yakinishi, vitenzi hivyo huchukua -eni badala ya kiambishi tamati a-
      
      
        • Vitenzi vya silabi moja vinapowekwa katika hali ya kushurutisha kwa hali kanushi, vinaondolewa kiambishi cha kitenzi ku-,
          vinachukua si- kwa umoja na wingi. Kiambishi tamati kikawa -e badala ya -a
        
       
     Zoezi la 6: Jadili kuhusu maana ya sentensi zifuatazo zenye kitenzi ambacho kiko katika hali ya kushurutisha; halafu tunga sentensi tatu ukitumia hali ya kushurutisha katika hali yakinishi na kanushi.
     1. Mama alimkataza mtoto wake “...............pombe”. (kunywa)
     2. ............chakula hiki ukimalize upate afya nzuri. (kula)
     3. Mkurugenzi alimshauri mzazi “............mtoto malezi bora (kupa)
     4. ............tuhudhurie mjadala wa leo. (kuja)
     5. Ukitaka kuwa na maisha mazuri..........chakula chenye mafuta mengi. (kula)

     Tanbihi: Usichanganye hali ya kushurutisha na hali ya kuomba au kusihi. Katika hali ya kuomba, vitenzi vinawekwa katika nafsi ya kwanza wingi, nafsi ya pili na ya tatu umoja na wingi
           

     Zoezi la 7: Tunga sentensi kumi kwa kutumia hali ya kuomba.

     Maelezo muhimu

     Hali yakinishi

     Vitenzi vya Kiswahili vyenye viambishi tamati -i , -e na ¬-u, katika hali ya kushurutisha au ya kuamrisha vinaondolewa kiambishi cha kitenzi ku- katika umoja hali yakinishi. Katika wingi, vinaondolewa kiambishi ku-, halafu vikachukua –ni baada ya viamishi tamati –i, -e na –u.

      

     22.4 Matumizi ya Lugha: Utekelezaji wa Mjadala
     Zoezi la 8: Kamilisha sentensi hizi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo: Suluhisho, walevi, ukimwi, kiongozi, ufukara, msemaji, mchango, miradi, ujinga, madawa ya kulevya,
     1. Mshiriki aliye tayari aje atoe............wake.
     2. Matumizi ya .............ni hatari kwa maisha ya watu.
     3. Tumtege sikio ............mwingine atoe maoni yake.
     4. .............hauna dawa wala chanjo.
     5. Watu wanaolewa wanaitwa..............
     6. Watu wanaokumbwa na.............nao wanaweza kujiendeleza.
     7. ............... mbalimbali imeanzishwa kupambana na umasikini.
     8. Elimu huondoa ........ katika jamii.
     9. Mjadala unaanzishwa na kufungwa na .............
     10. Mwishoni mwa mjadala kiongozi wake anatoa ............

     Zoezi la 9: Chunguza maelezo haya kuhusu mfano wa mjadala kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini.

     Maelezo muhimu kuhusu mfano wa mjadala
     Mjadala ulikuwa na mada isemayo “Matatizo makuu yanayokwamisha maendeleo katika jamii ya Rwanda.” Baada ya majadiliano, matatizo makuu yanayokwamisha maendeleo katika jamii ya Rwanda.yaliyotolewa na wahusika wa mjadala ni haya yafuatayo: matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, maradhi tofauti, ujinga na ufukara. Matumizi ya madawa ya kulevya ni hatari kwa binadamu. Yanaharibu maisha na yanayeyusha ubongo. Wanaotumia madawa ya kulevya hawawezi kuendelea kamwe. Pombe tena ni mbaya kwa maisha ya mwanadamu. Unapotaka kuendelea si vizuri kunywa pombe sana.

     Maradhi yanayoangamiza jamii ya Rwanda na kukwamisha maendeleo ni pamoja na Malaria, Ukimwi, Kisukari, na mengineyo. Ni lazima tujilinde kwa kufuata shauri za waganga na wengine wanaohusika na afya katika jamii.Jamii ya Rwanda inaombwa kupata elimu ili iweze kuepuka na ujinga na iweze kujiendeleza.

     Mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa mjadala:
     • Kutumia vizuri muda uliopangwa
     • Kuepuka na fujo na kelele
     • Kupaza sauti unapotoa maoni kuhusu mada
     • Kutoa maoni kwa madhumuni ya kutimiza lengo la mjadala
     • Kutumia lugha isiyo ya matusi
     • Kuwaheshimu wengine
     • Kupanga mawazo yako kabla ya kupata fursa

     Maswali
     1. Ni matatizo gani mengine yanayoweza kukwamisha maendeleo ya jamii ya Rwanda?
     2. Kwa maoni yako matatizo haya yanaweza kuepukwa namna gani?
     3. Eleza mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa mjadala.

     22.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadaliano
     Zoezi la 10: Jadili kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo::
     1. Namna bora ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi
     2. Mikakati ya kuepuka maambukizi ya malaria

     22.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari
     Zoezi la 11: Kwa kuzingatia mfano wa mjadala, tunga kifungu cha habari kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo:
     1. Juhudi zinazoweza kufanyika ili kuzuia vijana kutumia madawa ya kulevya
     2. Juhudi zinazoweza kufanyika ili kutoa malezi kwa wote

     Muhtasari wa Mada
     Mada hii ya nne” Midahalo na Mijadala” ina vipengele vinne yaani masomo makuu manne yanayohusiana na mada husika. Kila somo lina vipengele vidogo kama vile: mchoro, kifungu cha habari, maswali ya ufahamu, matumizi ya msamiati, matumizi ya lugha, kusoma na kuandika, sarufi, na maelezo muhimu. Somo la kwanza linaeleza maana ya mdahalo na mjadala. Somo la pili ni uhusiano na tofauti kati ya mdahalo na mjadala. Somo la tatu linafafanua utekelezaji wa mdahalo na Somo la nne linaloeleza utekelezaji wa mjadala. Katika kila somo kuna kipengele cha sarufi ambacho kinagusia hali ya kushurutisha ya vitenzi vya Kiswahili sanifu.

     TATHMINI YA MADA KUU YA NNE
     1. Fanya kazi zifuatazo kuhusu mdahalo
         a. Andaa mdahalo kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo:
          • Walimu wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto kuliko wazazi wao.
          • Bila malezi ya watoto ya kushirikianawatu wote, nchi ya Rwanda haiwezi kuendelea.
          • Madawa ya kulevya hukwamisha maendeleo zaidi kuliko magonjwa.
        b. Kwa kushirikiana na wenzako, tekelezeni mdahalo mlioandaa.
     2. Fanya kazi zifuatazo kuhusu mjadala
         a. Andaa mjadala kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo.
          • Usawa wa jinsia katika kuimarisha maendeleo ya nchi
          • Malezi kwa wote ni jukumu la kila mwananchi
          • Madhara yanayosababishwa na magonjwa yasiyoambukizwa
        b. Kwa kushirikiana na wenzako, tekelezeni mjadala mlioandaa.
     3. Tunga kifungu kifupi cha habari ukitumia vitenzi tofauti katika hali ya kushurutisha.


     • MADA NDOGO: INSHA ZA MASIMULIZI AU KUBUNI NA UANDISHI WA RIPOTI 

      Uwezo upatikanao katika mada: Kumwezesha mwanafunzi kuzingatia mwongozo wa kutunga insha za masimulizi kulingana na mada iliyotolewa na kuzitolea muhtasari darasani kwa njia ya mazungumzo; kuandika ripoti rahisi; kuelewa jinsi ya kumnukuu mtu mwingine.

      Malengo

      • Baada ya mada hii, mwanafunzi atakuwa na uwezo wa:

      • Kufasili maana ya insha na aina zake mbalimbali.

      • Kutunga insha

      • Kufasili maana ya ripoti na aina zake mbalimbali.

      • Kutunga mfano wa ripoti.

      • Kubadilisha sentensi kutoka usemi wa asili/ halisi katika usemi wa taarifa.

      Kidokezo

      • Nini maana ya insha?

      • Eleza vipengele muhimu vya insha?

      • Taja aina nne za insha?

      • Kwa kutunga insha mwandishi au mtunzi anafuata taratibu zipi?

      • Nini maana ya ripoti ?

      • Ripoti ni za aina tofauti. Eleza

      SOMO LA 23: INSHA

      Tazama kwa makini mchoro ufuatao kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini:


      Zoezi la 1: Eleza wahusika unaowaona kwenye mchoro huu.

      1. Wahusika hao wapo wapi? Wanafanya nini?

      2. Kuna uhusiano wowote kati ya mchoro huo na kichwa cha habari hapo chini?

      23.1 Kusoma na Ufahamu: Insha

      Wataalamu wengi wanasema kwamba insha ni aina ya utungaji ambao hulenga kumpa mwanafunzi uwezo wa kutunga habari yeye mwenyewe na kuiwasilisha kwa watu wengine kwa kutumia njia ya mazungumzo au maandishi. Katika utungaji wa insha, mwanafunzi huhitaji kujieleza zaidi kwa njia ya kinathari ambayo ni mtindo wa kutumia lugha ya kawaida ambayo si ya kishairi.

       Katika hali ya kawaida, mtungo wa insha hutumia maneno kwa kuelezea jambo fulani na huhusishwa kwa maandishi au makala yanayotoa habari na maoni kuhusu kitu, mtu, tukio au jambo lolote. Mtungo huu ni nyenzo muhimu sana kwa mtu kwa kumwezesha kubuni, kutafiti, kujieleza, kuwasilisha na kupanga mawazo yake na hoja muhimu kuhusu matukio na matatizo na hali mbalimbali zinazomhusu katika maisha yake ya kila siku. Katika hali hii, utungaji wa insha humpa pia fursa nzuri ya kuendeleza na kukuza kipawa chake cha kutumia lugha.

      Insha yoyote ina sehemu kuu tatu muhimu. Vitabu vingine vinasema kuwa katika sehemu kuu za insha kichwa cha insha kimo. Sehemu ya kwanza ni mwanzo au utangulizi wa insha. Sehemu hii huzingatia fasili ya jambo linalozungumziwa . Utangulizi unafaa uwe wa kuvutia ili msomaji awe na hamu ya kuendelea kuisoma insha hiyo. Kwa hiyo, mwandishi hueleza maana ya mada ambayo huchukuliwa kama anwani au kichwa cha insha alichopewa. Endapo methali ni kichwa cha insha, mwandishi ataeleza maana ya incha, maana ya ndani, na matumizi ya methali aliyopewa katika jamii husika. Endapo ni insha ya mjadala, baada ya kueleza maana ya mada, mwandishi ataeleza kama anaunga mkono au ataupinga mjadala. Lakini pia anaweza kuamua kutoa maelezo ya pande zote mbili na halafu atoe uamuzi wake. Kwa kawaida, utangulizi hauzidi aya moja.

      Sehemu ya pili ya insha ni kiini cha insha. Hii ndiyo sehemu kuu ya insha na huzingatia mawazo makuu ambayo hupangwa katika aya zenye mtiririko wa mawazo. «Aya ni mkusanyiko wa sentensi kadhaa zinazoeleza wazo moja..». Kamusi ya karne 21 inaeleza. Katika utunzi wa insha, kila aya hujitosheleza kwa kila kitu katika kulielezea jambo moja tu au hoja moja tu. Sehemu hii huonyesha kwa undani maana ya jambo linalotungwa, kwa hoja na uthibitisho.Wingi wa aya hutegemea wingi wa maudhui au mawazo aliyonayo mwandishi wa insha. Urefu wa aya hutegemea uwezo wa mwandishi wa kufafanua wazo linalozungumziwa katika aya hiyo.

      Sehemu ya tatu ni hitimisho. Sehemu hii ya insha inaelezea muhtasari wa maudhui yote yaliyoelezwa katika insha nzima. Hutoa msisitizo kwa yaliyojadiliwa na huwa na maoni na mapendekezo ya mwandishi kuhusu jambo lililotungiwa insha.

      Kutokana na maelezo haya, ni dhahiri kwamba utungaji wa insha humfanya mwanafunzi aweze kukuza uwezo wake wa kutunga habari mbalimbali na kuzungumzia mambo mengi anayokutana nayo katika maisha yake ya kila siku. Mazoezi mengi ya utungaji wa insha ni muhimu ili kumwezesha mwanafunzi kukuza uwezo wake wa kubuni, kuelezea kwa uthibitisho wa mawazo, na hata kujadili hoja mbalimbali kwa lugha fasaha.

      Maswali ya Ufahamu

      1. Eleza maana ya insha.

      2. Njia gani zinazotumiwa kwa kuwasilisha habari?

      3. Hii ni aina gani ya insha? Eleza

      4. Somo la insha linamsaidia nini mwanafunzi?

      5. Eleza sehemu kuu za insha.

      6. Kwa sababu gani tunasema ni lazima utangulizi uwe wa kuvutia?

      7. Kwa sababu gani wandishi husema kuwa kiini ni sehemu kuu ya insha?

      8. Nini tofauti kati ya utangulizi na hitimisho

      9. Je, mwanafunzi anahitaji ujuzi kuhusu insha katika maisha yake ya kila siku? Eleza.

      10. Kwa sababu gani wanafunzi wengi wanaogopa swali la kutunga insha?

      23.2 Msamiati kuhusu Insha 

      Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo kutoka kwenye kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu “ maana ya insha”

      1. dhahiri

      2. Nathari

      3. Mtungo

      4. Mantiki

      5. Kubuni

      6. Kutafiti

      7. Kipawa

      8. Kuvutia

      9. Uamuzi

      10. Aya

      Zoezi la 3: Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B. 

      Zoezi la 4: Kamilisha sentensi kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo: mtungo, utangulizi, kiini, hitimisho, aya, tatu, utungaji, insha, nyenzo,sehemu

      1. Kwenye......................... mwandishi hueleza maana ya mada/anwani/kichwa

      alichopewa.

      2. Insha ni aina ya .............ambao humpa mwanafunzi uwezo wa kubuni.

      3. Insha ina sehemu kuu ..................: utangulizi, kiini na hitimisho

      4. Sehemu kuu ya insha ni……………………….

      5. Kila .....................hujitosheleza kwa kila kitu katika kulielezea jambo moja tu au hoja moja tu.

      6. ...................linaelezea muhtasari wa maudhui yote yaliyoelezwa katika insha nzima.

      7. Insha ni .................wa maneno kwa mtindo wa kinathari juu ya jambo fulani.

      8. .....................ina sehemu kuu tatu.

      9. Mtungo huu ni ...............muhimu sana kwa mtu kwa kumwezesha kubuni.

      10. ................. kuu ya insha ni kiini.

      23.3 Sarufi: Usemi wa Asili na Usemi wa Taarifa (katika wakati uliopo) 

      Zoezi la 5: Chunguza sentensi katika sehemu A na sentensi ulizotolewa katika sehemu B ili uweze kujibu maswali yanayofuata hapo chini.


      Maswali:

      1. Ni tofauti gani kati ya sentensi za sehemu A na B?

      2. Kuna uhusiano gani kati ya maana ya sentensi kwenye sehemu A na B?

      3. Toa mifano ya sentensi kutoka kifungu « insha » ambazo zina muundo sawa na hizi sentensi hapa juu.

      Zoezi la 6: Soma maelezo kuhusu maana na tofauti kati ya usemi wa asili na usemi wa taarifa kisha ujibu maswali yanayofuata hapo chini. 

      Usemi wa taarafa na usemi wa asili 

      Katika usemi halisi au usemi wa asili, maneno yaliyosemwa na mtu hurudiliwa na mwingine jinsi alivyoyasema bila kuongeza au kutoa kitu. Ni namna ya kunukuu maneno ya mtu mwingine. 

      Maana ya Usemi wa Taarifa

       Iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa na mtu mwingine bila ya kupotosha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo analotaka kulitolea maelezo, basi maneno anayosema huitwa Usemi wa Taarifa

      Ni wazi kwamba unapoyarudia maneno yaliyazungumzwa na mtu mwingine ingawa unakidhi maoni yake, lakini kuna mabadiliko ya kisarufi yanayojitokeza. 

      Tanbihi : Katika wakati uliopo kwa kugeuza usemi mmoja katika usemi mwingine hakuna mabadiliko ya wakati ikiwa kitenzi kinachodokeza usemi kiko katika wakati uliopo. Mabadiliko mengine yanajitokeza kama vile nafsi, uakifishaji, n.k.

      Maswali : Geuza sentensi zifuatazo katika usemi halisi au usemi wa taarifa.

      1. Kabanyana anatangaza kwamba mama yake amekufa leo.

      2. “Mtoto mzuri anamsaidia mlemavu.” Wazazi wanasema.

      3. “Mama yangu anapanda miti ili tuwe na hewa nzuri.” Anasema Rurangwa

      4. Muhorakeye anasema kuwa anaunda kundi moja na yule kijana mweye matatizo ya kuona.

      5. “Baba yangu anafanya biashara,” Kankindi anasema.

      23.4 Matumizi ya Lugha: Insha 

      1. Kipawa-utungaji-kuendeleza-fursa-ya-wa-insha-humpa-kukuza-nzuri-pia-na-.

      2. Mwandishi-hutegemea-kufafanua-wazo-urefu-wa-aya-wa-wa-uwezo

      3. Mfukusanyiko-aya-sentensi-wazo-moja-wa-zinazoendeleza-ni

      4. Aya- moja- utangulizi- kwa –hauzidi-kwaida

      5. Muhimu-sehemu-insha –yoyote-tatu-kuu-ina

      Maelezo muhimu kuhusu Insha.

      Zoezi la 8: Soma maelezo haya yafuatayo kisha ujibu maswali hapo chini:

      Fasili ya insha: Utungaji ni neno linalotokana na kitenzi “tunga”. Kitenzi hiki kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2004:414) linamaanisha “toa mawazo kutoka ubongoni na kuyakusanya, kisha kuyadhihirisha kwa maandishi, kwa kusimulia, kwa kuyaimba au kwa muziki. 

      Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa, utungaji ni utoaji wa mawazo binafsi kutoka akilini mwa mtu kuhusiana na mambo mbalimbali katika jamii, kisha kuyaweka wazi kwa njia ya mdomo au maandishi. 

      Sehemu kuu za insha: Insha hugawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: 

      • Utangulizi (Mwanzo) Katika sehemu hii inampasa mwandishi atoe maelezo mafupi na maana ya habari aliyopewa.

       • Kiini cha insha (Kati) Inamlazimu mwandishi afafanue kwa mapana mada anayoishughulikia huku akitoa mifano hai inayoendana na hali halisi. Kwa kawaida sehemu hii hueleza kwa ukamilifu kila hoja iliyodokezwa katika utangulizi.

      • Hitimisho (Mwisho) 

      Inampasa mwandishi kutoa mapendekezo (maoni) ya msingi au kusisitiza kwa ufupi yale aliyoyaelezea katika habari yenyewe. Mwisho wa insha huonyesha uhusiano uliopo kati ya utangulizi na maelezo yaliyomo katika mwili.

      Taratibu za kutunga insha:

      • Soma kwa makini mada/kichwa/anwani uliyopewa zaidi ya mara moja, ili uielewe vizuri.

      • Ifikirie mada/kichwa/anwani kwa muda.

      • Yaandike mambo muhimu yatakayokuongoza katika kuiandika insha

      • Maelezo yote yatolewe kwa undani na kwa njia ya kuvutia.

      • Kutumia vizuri alama za uakifishaji.

      • Kupanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki.

      • Tumia msamiati mwafaka kwa kutegemea mada.

      • Lugha iwe ya adabu na isiyo ya matusi.

      • Andika methali, misemo na nahau ambazo unadhania zinaweza kukufaa katika

      utungaji.

      Maswali

      1. Kwa maoni yako nini maana ya insha ?

      2. Kwa sababu gani katika utungaji wa insha ni lazima kuheshimu sehemu za insha ?

      3. Andika sifa kuu tano za insha.

      23.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadaliano

      Zoezi la 9: Jadili kuhusu nafasi ya insha katika masomo tofauti.

      23.6 Utungaji wa Insha

      Zoezi la 10: Tunga insha kwenye ukurasa mmoja ya mada unayotaka. Usisahau kuheshimu sehemu kuu za insha na kufuata taratibu za kutunga insha.

      SOMO LA 24: AINA ZA INSHA

      Tazama kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yanayofuata hapo chini


      Zoezi la kwanza:Tazama michoro hapo juu kisha ujibu maswali yafuatayo.

      1. Elezea wahusika unaowaona kwenye michoro hii.

      2. Wahusika hao wapo wapi? Wanafanya nini?

      3. Kuna uhusiano wowote kati ya michoro somo hili?

      24.1 Kusoma na Ufahamu: Usafi wa Mavazi Yetu

      Soma kifungu kifuatacho kuhusu “Usafi wa mavazi yetu”, kisha jibu maswali uliyopewa hapo chini 

      Vazi ni nguo ya aina yoyote inayovaliwa mwilini. Binadamu huhitaji mavazi kujikinga na hali ya hewa ya aina mbalimbali. Wakati wa joto huhitaji vazi jepesi na wakati wa baridi huhitaji vazi linaloweza kumtilia joto mwilini. Hii ndiyo sababu wakati wa baridi watu hujifunika mavazi kama migolole, makoti, makabuti, makaniki, vikoi, na masweta .

      Mavazi ni hifadhi ya staha ya utu wa mtu. Mavazi hukusudia pia kuficha utupu wa mtu. Hoja hii hutegemea sana utamaduni wa jamii, ila kimsingi vazi ni kifaa cha kuficha utupu pia. 

      Mavazi ni pambo kwa binadamu. Vazi humfanya mtu aonekane maridadi na apendeze zaidi. Labda hii ndiyo sababu kuwepo kwa aina mbalimbali za mavazi na mitindo tofauti inayomfanya mtu avutie.

      Mavazi pia huonyesha utamaduni wa watu. Kusema kwamba mtu akivaa nguo ya mtindo fulani mara nyingi utamaduni wake au asili yake hutambulika waziwazi. Hata mtu awe mweupe anayetoka Ulaya au Marekani, akivaa mgolole, kanga, kitenge, atakuwa akiiga vazi la utamaduni wa Afrika kwa ujumla. Hadi leo, kuna mavazi unayoweza kusema kuwa ni ya Kichina, Kihindi, Kiarabu, Kizungu, Kinyarwanda, Kiganda, Kimasai na kadhalika. Tena mtu anaweza kuvaa nguo kwa mtindo wa aina fulani akafikiriwa kuwa ni Mkongomani, Mganda, Mmasai, raia kutoka Afrika Magharibi na kadhalika.

      Mavazi ni ya aina nyingi na mitindo tofauti. Lakini mavazi hayo yote huweza kupangwa katika aina kuu tatu: mavazi ya kike, ya kiume na mavazi mahususi. 

      Kwa upande wa kwanza, mavazi ya kike ni mavazi ambayo kwa kawaida huvaliwa na watu wa jinsia ya kike. Kuna mavazi au nguo za ndani, ambazo huvaliwa na wanawake na hazipaswi kuonekana ovyo. Na hizo ni kama chupi, fulana na sidiria. Tena ,kuna nguo za nje ambazo ndizo zionekanazo mara nyingi. Hizo ni kama sketi, blauzi, shati, jaketi, gauni, kanga, kaniki, kitenge, kaptula, suruali na kadhalika. 

      Kwa upande mwingine, wanaume nao huwa na nguo za staha yaani nguo za ndani kama chupi na fulana. Pia wana nguo zinazoonekana nje kama kaptula, suruali, shati, koti, tai, suti, kanzu na kadhalika.

      Zaidi ya hayo, kuna mavazi mahususi ambayo ni mavazi rasmi kwa ajili ya shughuli maalum au kazi maalum. Mfano wa mavazi haya ni kama mavazi ya viongozi wa kidini, masista, makasisi, mapadri na mashehe. Kundi la aina hii huwa na nguo zao maalum kwa ajili ya kazi zao na pia huwasaidia kujitambulisha kwa urahisi kwa umma au jamii. Baadhi ya nguo hizo ni kama kasiki, joho, kanzu, kilemba na nguo zinazofanana na hizo. Tena kuna nguo zisizo za kila siku ambazo huvaliwa mara chache. Hizo ni kama veli. 

      Mfano mwingine ni mavazi rasmi kama ya askari jeshi, askari polisi, askari magereza, wafanyakazi wa forodha, walinda usalama wa mashirika ya kujitegemea, waganga na wauguzi, wafanyakazi wa mashirika ya ndege, wachezaji na hata wanafunzi. Hawa wote wana mavazi yao rasmi kwa ajili ya shughuli zao. Mtu akivalia nguo ya aina fulani, hujitokeza kuwa yeye ni mtu wa namna fulani au kazi fulani. 

      Mavazi yetu yote ni lazima yawe na usafi. Usafi wa mavazi yetu ni muhimu sana kwa sababu jambo hili husaidia mambo mengi maishani mwetu. 

      Kwanza tunaposafisha nguo zetu, tunajiepusha na magonjwa yanayotokana na wadudu wanaoweza kuishi katika nguo chafu. Wadudu hawa ni kama chawa, tekenya, viroboto na kadhalika. Nguo chafu hasa zile za ndani huweza kusababisha madhara katika sehemu za uzazi na kuleta magojwa mbalimbali kutokana na vidudu ambavyo vinaweza kusababishwa na uchafu.

      Pili, mtu akiwa na nguo chafu hutoa harufu mbaya ambayo husumbua wenzake wanapomsogelea. Na mtu akiwa katika hali hii kila mtu humkimbia na popote aingiapo akakaribishwa kwa shingo upande. 

      Kwa kusafisha nguzo zetu, wenye kuwa na uwezo mkubwa hutumia mashine za kufulia na wenye kipato kidogo hutumia beseni na sabuni. Nguo zikiisha fuliwa ni lazima zianikwe kwenye jua ili bakteria au vijasumu viweze kufa. Kisha kama vinawezekana, nguo lazima zipigwe pasi kwa kumaliza bakteria walioepuka miali ya jua. Tena nguo zetu zikichanika lazima zishonwe. 

      Isitoshe, usafi wa mavazi yetu lazima uende sambamba na usafi wa miili yetu. Ama si hivyo kazi ya kusafisha nguo itakuwa ya bure bilashi. Usafi wa mwili unahusiana na kuoga, kunyoa nywele, malaika (hasa ya kwapani na ya sehemu za siri) na ndevu, kupiga mswaki na kukata kucha. 

      Kwa ujumla, mavazi yetu ni ya aina nyingi na mitindo tofauti. Mavazi haya yana umuhimu sana katika maisha yetu. Ndiyo maana tunalazimika kuyatunza vizuri na kuyasafisha ili tuwe na usafi wa kutosha. Usafi huu lazima uende bega kwa bega na usafi wa miili yetu. 

      (Kifungu hiki msingi wake ni kutoka : Ndalu A. (1997) Mwangaza wa Kiswahili, East African Educational Publishers Ltd, Nairobi Kenya.

      Maswali ya Ufahamu

      1. Vazi ni nini ?

      2. Kwa sababu gani vazi ni kifaa muhimu sana kwa binadamu?

      3. Taja aina kuu tatu za mavazi.

      4. Ni kwa namna gani vazi linaweza kutambulisha utamaduni wa anayevaa vazi hilo? Eleza kwa kutoa mifano ya kutosha.

      5. Taja mifano mitatu ya nguo mahususi.

      6. Veli linaweza kutambulika kama vazi la aina gani miongoni mwa aina za mavazi tulizotaja hapo juu?

      7. Eleza jinsi ambavyo mavazi hutegemea sana utamaduni wa jamii husika?

      8. Taja majina ya wadudu wanaoishi ndani ya mavazi machafu.

      9. Kwa sababu gani nguo zilizofuliwa ni lazima zipigwe pasi baada ya kukaushwa na jua?

      10. Ni ushauri gani unaweza kutoa kulingana na kifungu hiki?

      24.2 Msamiati kuhusu Usafi wa Mavazi

      Zoezi la 2: Toa maana za maneno yafuatayo:

      1. Pamba

      2. Staha

      3. Pambo

      4. Maridadi

      5. Mahususi

      6. Akiiga

      7. Chawa

      8. Tekenya

      9. Kiroboto

      10. Malaika

      Zoezi la 3: Tunga sentensi kwa kutumia maneno ya hapo juu.

      Zoezi la 4: Tafuta majina kumi ya mavazi katika jedwali lifuatalo:


      Zoezi la 5: Unganisha fungu la A na fungu la B ili kujenga sentensi zenye maana


      24.3 Sarufi: Usemi wa Asili na Usemi wa Taarifa katika Wakati Uliopita na Wakati Uliotimilika

      Zoezi la 6: Chunguza sentensi zifuatazo kisha uzigeuze katika usemi wa taarifa.

      1. “ Mwanafunzi alifua sare zake.” Kagabo anasema.

      2. “Mwanafunzi alifua sare zake.” Kagabo amesema.

      3. “Mwanafunzi amefua sare zake.” Kagabo amesema.

      4. “Mwanafunzi alifua sare zake.” Kagabo alisema.

      5. “Mwanafunzi amefua nguo zake.” Kagabo alisema.

      Chunguza maelezo yafuatayo

      Wakati wa kubadili sentensi kutoka usemi wa asili hadi usemi wa taarifa katika wakati uliopita na wakati uliotimilika mambo yafuatayo hujikokeza:

      • Kama kitenzi kinachodokeza usemi kimo katika wakati uliopo, hakuna mabadiliko yatakayojitokeza katika usemi wa taarifa.

      • Kama kitenzi kinachodokeza kimo katika wakati uliopo au uliotimilika, hakuna madadiliko ya kitenzi ikiwa kimo katika wakati uliopita au uliotimilika.

      • Kama kitenzi kinachodokeza kimo katika wakati uliopita, wakati uliotimilika hugeuka wakati uliopita.

      Mifano:


      Zoezi la 7: Geuza sentensi zifuatazo katika usemi wa taarifa.

      1. “Wanafunzi walipanda miti shuleni.” Mkurugenzi alimwambia mkuu wa wilaya.

      2. “Kalisa hakuhudhuria shule vizuri kwa sababu ya ugonjwa.” Mama amemuelezea

      mkurugenzi.

      3. “Wanafunzi wamesafisha darasa.” Mwalimu alimwambia mwenzake.

      4. “Nguo za shule zilichanika. Umepaswa kutafuta nyingine mpya.” Mwalimu mkuu alimwambia mtoto.

      5. “Mimi sikuiba vitabu maktabani.” Kamasa aliapa mbele ya wazazi wake.

      6. “Kwa nini umechelewa?” Mwalimu alimuuliza mwanafunzi.

      7. “Ulizaliwa wapi?” Mkuu wa tarafa amemuuliza mwananchi.

      8. “Rwanda ilitawaliwa na Wajerumani.” Mwanahistoria anaeleza.

      9. “Jana usiku mtoto alitapika mara ngapi?” Muuguzi alitaka kujua.

      10. “Mimi sijafanya kitendo chochote cha uhalifu.” Mshukiwa amedai mahakamani.

      Zoezi la 8: Geuza sentensi zifuatazo katika usemi wa asili

      1. Daktari wa meno aliambiwa na mgojwa kwamba aling’olewa jino bovu hapo awali.

      2. Mkurugenzi alimueleza Waziri wa Elimu kuwa wanafunzi walipanda miti kwenye mlima wa Nyamagumba mwaka uliopita.

      3. Mama ametaka kujua ikiwa mwanawe amepewa maziwa.

      4. Walindausalama walieleza kwamba walikamata wezi watatu.

      5. Waziri wa Utamaduni aliwaambia wananchi kwamba Wanyarwanda walikuwa wakiishi kwa amani na upendo katika enzi za jadi.

      6. Mzee aliwaambia wajukuu wake kuwa uungwana ulikuwa nguzo ya maisha ya Wanyarwanda.

      7. Polisi wa doria alitaka kujua sababu iliyomruhusu dereva kutojifunga mkanda wa gari.

      8. Mwalimu ametaka kujua tarehe ya kuzaliwa kwa mwanafunzi.

      9. Mwalimu wa Historia aliwaambia wanafunzi kuwa mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi yalirudisha nyuma nchi yetu katika nyanja zote.

      10. Waziri wa Afya aliliambia Baraza la Mawaziri kwamba serikali ilitayarisha chanjo dhidi ya polio.

      24.4 Matumizi ya Lugha: Aina za Insha na Mazoezi ya Jumla

      Zoezi la 9: Andika neno moja lenye maana ya maneno yote yaliyopo kweny orodha:

      Mfano: Kanzu, lubega, koti, stokingi: nguo

      1. Uashi, ususi, utarizi, uhunzi

      2. Dunia, Zohali, Mushtara, Zuhura

      3. Kifaru, kiboko, tembo, Simba

      4. Mbu, tekenya, dumuzi, nzi

      5. Kiti, dawati, kabati, meza

      Maelezo muhimu kuhusu aina za insha

      Zoezi la 10: Soma maelezo muhimu kuhusu aina za insha kisha ujibu maswali ya hapo chini.

      • Insha ni za aina nyingi kulingana na namna zilivyoandikwa au kulingana na kusudi lake. Katika utungaji wa insha kuna insha za wasifu, insha za picha, insha za mdokezo, insha za masimulizi, insha za methali, insha za hoja na insha za kubuni. 

      1. Insha za Wasifu

       Insha za wasifu ni aina za insha ambazo hueleza sifa za mtu, kitu au jambo fulani. Insha za aina hii husimulia sifa, maisha au maelezo mengine muhimu kuhusu mtu fulani, kitu fulani au jambo fulani. Ni kusema kuwa katika aina hizi za insha mwandishi anaandika kuhusu uzuri au ubaya wa mtu, kitu au jambo fulani. 

      2. Insha za Picha

       Insha za picha ni aina za insha ambazo hueleza picha iliyotolewa. Kusema kwamba mwandishi hueleza mambo anayoyaona kwenye picha/mchoro ni kusema kwamba mwandishi huyu analazimika kufanya andiko lenye mfuatano wa mawazo kulingana na mfuatano wa picha au michoro aliyopewa. 

      3. Insha ya Mdokezo 

      Insha za mdokezo ni aina za insha ambazo mwandishi hupewa mwongozo wa kufuatilia katika utunzi wake. Kwa mfano, mwandishi anaweza kupewa orodha ya hoja kadhaa kutokana na kichwa kilichotolewa akajenga insha. Vilevile anaweza kupewa utangulizi au kimalizio cha insha na kuagizwa aendelee na insha au aanze insha aliyopewa.

       4. Insha za Methali 

      Insha ya methali ni aina ya insha ambayo mada yake huwa ni methali ambayo mwandishi anaomba kujadilia. Katika uandishi wa insha ya aina hii, mwandishi ni lazima atoe hoja kwa kukubaliana na methali iliyotolewa. Hili ni kwa sababu methali hujaa mambo ya hekima.

      5. Insha za Hoja 

      Insha za hoja ni aina ya insha ambazo mwandishi analazimishwa kutoa hoja zinazotetea mada na nyingine zinazopinga mada. Mwishoni mwa insha hii, mwandishi anaonyesha msimamo wake kulingana na mada iliyotolewa. 

      6. Insha za Masimulizi

       Insha za masimulizi ni aina ya insha ambazo ndani yake mwandishi anasimulia au anaeleza tukio fulani maalum la kweli au la kubuni kwa njia ya kisanaa. 

      7. Insha za Kubuni

       Insha za kubuni ni aina ya insha ambazo hutungwa kuhusu mawazo yanayozuliwa na ambayo si matukio ya kawaida. Ni kusema kwamba mwandishi hubuni mandhari, wahusika, matukio, nk.

      Maswali

      1. Taja aina za insha.

      2. Kifungu ulichokisoma ni aina gani ya insha? Kwa sababu gani?

      3. Ni nini tofauti iliyoko baina ya insha ya wasifu na insha ya masimulizi.

      4. Kwa sababu gani mara zote mwandishi wa insha ya methali hulazimishwa

      kutetea methali aliyopewa?

      24.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadaliano

      Zoezi la 11: Ukishirikiana na wenzako, jadilieni kuhusu

      1. “Umuhimu wa mavazi”.

      2. “Umuhimu wa kuvaa sare za shule kwa wanafunzi.”

      3. “Umuhimu wa kusafisha nguo zetu”

      24.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari

      Zoezi la 12: Tunga kifungu cha habari kuhusu mojawapo ya mada zifuatazo:

      1. “Mabadiliko ya mavazi nchini Rwanda”.

      2. “Utengenezaji wa mavazi ya kijadi nchini Rwanda.”

      3. “Umuhimu wa kutotumia nguo za mitumba nchini Rwanda.”

      4. “Wadudu wanaotokana na uchafu na madhara yao.”

      SOMO LA 25 : INSHA YA MASIMULIZI

      Jibu maswali haya :

      1.Unaelewa nini kuhusu insha za Masimulizi?

      2.Kuna uhusiano gani uliopo kati ya masimulizi na insha ?

      25.1 Kusoma na Ufahamu: Mafanikio ya Kudumu

      Soma kifungu hiki kuhusu “ Mafanikio ya Kudumu” kisha jibu maswali uliyopewa hapo chini

      Ilikuwa tafrija ya kijiji kizima, tuliposherehekea siku ya kupata tuzo kwa kijana hodari ambaye aliyamudu maisha yake kiasi cha kuigwa na vijana wengine. Kabatesi, kijana aliyezaliwa mwanapekee katika familia yake hakubahatika kulelewa na wazazi wake kwani walifariki angali mdogo akachukuliwa na kulelewa na shangazi yake. 

      Alipomaliza masomo yake katika shule za sekondari, Kabatesi alipata cheti cha kuhitimu masomo ya sekondari huku akiwa na alama nzuri. Jambo hili liliwafurahisha watu wengi: walimu na majirani zake. Wengi waliompongeza siku hiyo walimletea zawadi nyingi. Alikuwa mwanafunzi mwenye bidii tangu shule za chekechea hadi kiwango alichofikia. Muda mfupi baadaye, alijiunga na vijana wenzake kufuata masomo ya muda mfupi yaliyokuwa yakitolewa kijijini mwake. Masomo hayo yaliwalenga vijana wote waliokuwa wamemaliza masomo yao ya shule za sekondari na yalilenga kuwawezesha kuandaa miradi midogo midogo ya kujiendeleza na jinsi ya kuifanikisha.

      Masomo hayo yaliwafurahisha vijana wengi na Kabatesi aliyafuata kwa makini, jambo lililokuwa desturi kwake. Alikuwa msichana mwenye mawazo na mtazamo imara wa maisha kiasi kwamba watu walishangaa kutokana na tabia na mienendo yake. 

      Kabla ya mafunzo kuanza, Kabatesi alikuwa na fikira nyingi kuhusu jinsi ya kutumia shamba lake kubwa aliloachiwa na wazazi wake. Mawazo mengi yalimjia kichwani lakini hakuweza kupata mtaji ili aanzishe mradi huo. Kwa hivyo, alipokubaliwa kufuata mafunzo pamoja na vijana wengine alielewa kwamba hiyo ilikuwa njia nzuri ya kupata suluhisho na ufumbuzi wa tatizo lililokuwa likimkera kwa muda mrefu. Mafunzo yalifanyika kwa muda wa mwaka mzima akapewa cheti katika fani ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.

      Mwezi mmoja uliofuata Taasisi ya Maendeleo ya Rwanda ilihitaji kuajiri vijana waliokuwa wamemaliza masomo yao katika mkondo wa lugha ili wasaidie katika kazi za ukalimani na upelekaji wa watalii kwenye vivutio vya utalii. Vivutio hivi vinapatikana katika sehemu mbalimbali za nchi. Kabatesi alipeleka ombi lake na baada ya muda mfupi akaitwa kwa mtihani. Hili lilikuwa jambo jepesi kwake kwani aliufaulu mtihani vema na hivyo akaajiriwa na taasisi hiyo. Kazi ilipoanza alifikiria kwamba hiyo ilikuwa fursa nzuri ya kuonyesha uwezo wake na kutekeleza mengi aliyokuwa amejifunza katika shule za sekondari. Alifanya kazi yake kwa bidii kiasi kwamba watalii wengi walifurahia huduma yake, wakampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha nyingi tofauti na bidii aliyoonyesha kazini. 

      Kabatesi aliendelea na kazi yake, akafungua akaunti kwenye benki moja na kuanza kuhifadhi sehemu ya mshahara wake. Kwa kweli, alikuwa msichana asiyekata tamaa na kila aliposhikilia jambo alilifuatilia mpaka lilipokamilika. Kwa hivyo, alipoona akaunti yake imeshakua na pesa za kutosha, aliamua kuomba mkopo ili aweze kutekeleza mengi aliyokuwa amejifunza katika maandalizi na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo. Mawazo yake yalikuwa kwenye shamba lake kubwa ambalo mpaka wakati huo lilikuwa halijatumiwa vizuri. Aliandaa vizuri mradi wa kilimo na ufugaji, akajenga vibanda vya mifugo yake, akawaajiri baadhi ya vijana waliokuwa pamoja katika mafunzo ya muda ule mfupi, kila mmoja akapewa jukumu lake.

      Pamoja na kazi yake ya ukalimani, Kabatesi alifuata vizuri mradi wake akanunua vifaa vilivyohitajika. Mwaka mzima baadaye, alikuwa ameshapata mali nyingi na kuanza kujulikana kote nchini kwa uwezo wake wa kufanya mambo mengi kwa muda mfupi na kwa ukamilifu. Ninakumbuka kuwa mwaka jana, serikali yetu ilipotoa tuzo kwa watu waliochangia kubadilisha maisha ya watu wengine, Kabatesi alikuwa miongoni mwa watu waliochangia kuyaboresha maisha ya majirani zao. Kila mtu katika kijiji chetu aliitikia mwaliko wake na wengi tulikuwa tunajivunia kuwa na kijana mwerevu kama yeye. Kwa sasa ameanza kuendelea na masomo yake katika Chuo kikuu cha Rwanda ambapo anatarajia kupata shahada yake ya kwanza katika uwanja wa Ukalimani na Mawasiliano ya Umma. 

      Kabatesi amekuwa mfano mzuri kwa vijana wengine wengi ambao wanapoyakumbuka maisha yake, huyaamini yaliyosemwa na wahenga kwamba” Mchumia juani hulia kivulini” na “mvumilivu hula mbivu”. Wema kwa kila mtu, utulivu na upendo ni baadhi ya sifa zinazomtambulisha kijana huyu ambaye amewashangaza wengi wanaofahamu alipotoka.

      Maswali ya ufahamu

      1. Eleza hali ya maisha ya Kabatesi alipokuwa mtoto mdogo.

      2. Kwa nini Kabatesi alipewa zawadi nyingi baada ya kumaliza masomo yake ya shule za Sekondari?

      3. Masomo ya muda mfupi aliyoyafuata yalihusu nini?

      4. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kufaidika kutokana na masomo ya muda mfupi.

      5. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kufaidika kutokana na masomo yake ya Sekondari.

      6. Ni mambo gani yanayokudhihirishia kwamba Kabatesi alikuwa kijana asiyekata tamaa?

      7. Eleza jinsi ambavyo Kabatesi aliweza kuboresha maisha ya watu wengine.

      8. Kwa nini Kabatesi alipewa tuzo?

      9. Kwa kifupi, eleza tabia na mienendo ya Kabatesi.

      10. Kwa nini Kabatesi anachukuliwa kuwa mfano kwa vijana wengine?

      11. Umepata funzo gani kutokana na kifungu hiki?

      12. Kulingana na kifungu hiki, eleza maana ya methali hizi:

      a. Mvumilivu hula mbivu

      b. Mchumia juani hulia kuvulini

      25.2 Msamiati kuhusu Kifungu cha Habari

      Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari hapo juu.

      1. Mafanikio

      2. Karo

      3. Akaunti

      4. Tafrija

      5. Ajira

      6. Tuzo

      7. Vibanda

      8. Mradi

      9. Kukata tamaa

      10. Kuanda 

      Zoezi la 3: Husisha maneno kutoka sehemu A na maana yake kwenye sehemu B.


      Zoezi la 4: Panga vizuri herufi za hapa chini ili ziunde maneno ya Kiswahili.


      Zoezi la 5: Kamilisha sentensi kwa kutumia maneno unayoona yanafaa kati ya yafuatayo:: Bidii, suluhisho, inawapongeza, ukalimani, utulivu, anahifadhi, jukumu, vibanda, shule za chekechea, ukamilifu.

      1. Hapa nchini Rwanda watoto wengi wanaanzia masomo yao ………………….

      2. Ili wanafunzi wafaulu katika mtihani wa taifa ni lazima wasome kwa ………….

      3. Wanakijiji wengi wanaomba mkopo kutoka benki kama ……………..la ukosefu wa mitaji ya kifedha.

      4. Kuna uhusiano wa karibu wa kazi ya …………….na utafsiri.

      5. Wanafunzi wenye tabia ya …………wanapata alama nzuri katika masomo yao.

      6. Serikali ya Rwanda ……………………wasichana wanaosoma sayansi.

      7. Wanafunzi waliofanya kazi katika makundi kwa .................wamepata alama nyingi.

      8. Kalisa ……………pesa zake kwenye benki ili aruhusiwe kupata mkopo.

      9. Wazazi wana ……………..ya kuwalisha na kulipa karo za watoto wao.

      10. Mjomba wangu alijenga …………….vitatu vya kuku wake

      25.3 Sarufi: Usemi Halisi na Usemi wa Taarifa.

      Zoezi la 6: Soma maelezo muhimu kuhusu usemi halisi (wakati ujao) na usemi wa taarifa kisha ujibu maswali hapa chini:

      Maelezo muhimu kuhusu usemi halisi na usemi wa taarifa( wakati ujao) 

      • Katika usemi halisi au usemi wa asili, maneno yaliyosemwa na mtu hurudiwa na mwingine jinsi alivyoyasema bila kuongeza wala kutoa kitu. Ni namna ya kunukuu maneno ya mwingine 

      • Katika usemi wa taarifa, maneno ya mtu huyo hurudiwa lakini sisi tunabeba uhusika wake. Ni kusema kuwa tunaripoti taarifa iliyotolewa na msemaji halisi. 

      • Mabadiliko ya wakati ujao ni haya: kiambishi cha wakati ujao”-ta-” katika usemi halisi hugeuka kikawa “ -nge- “ katika usemi wa taarifa.

      Mfano:

       «Utanikuta mjini jioni hii.»Juma alimwambia rafiki yake.

      • Juma alimwambia rafiki yake kuwa angemkuta mjini jioni ile.

      Andika sentensi zifuatazo kwa usemi wa taarifa:

      1. «Nitamsaidia mama yangu kuosha vyombo nyumbani.» Kalisa alituambia.

      2. «Wanafunzi watacheza pamoja na wale wenye matatizo ya kutembea.» mwalimu alisema darasani.

      3. «Mtashinda mtihani wa taifa mwaka huu.» Waziri wa Elimu alisema.

      4. Kalisa alitukumbusha, « Mtasoma kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya

      Watutsi mwaka 1994.»

      5. «Tutawasaidia wototo wenye matatizo ya kutembea vizuri katika maisha yao ya kusoma.» Mkuu wa kata alisema katika mkutano.

      6. «Wewe utalima mahindi na yule dada yako.» Baba alimwambia mtoto.

      7. «Tutacheza mpira wa miguu na timu jirani.» Mwanafunzi alimwambia mzazi wake.

      8. «Tutalipwa mishara yetu kabla ya kuondoka.» Mfanyakazi alisema katika mkutano.

      9. « Shamba langu litahitaji kupaliliwa.» Gasore alimshauri mkulima.

      10. « Nitatoa mchango wangu kuhusu mazingira na maendeleo ya kumudu.» Mama yangu aliniambia.

      25.4 Matumizi ya Lugha: Insha ya Masimulizi

      Zoezi la 7: Chunguza maelezo haya kuhusu insha za masimulizi kisha jibu maswali yanayofuata hapa chini:

      Utungaji wa masimulizi ni sehemu ya mawasiliano ambayo hutolewa kwa njia ya mdomo 

      Aina hii ya insha, mwandishi anasimulia tukio maalumu la kweli au la kubuni kwa njia ya kisanaa. Ni kusema kwamba mtungo wa aina hii huwa ni wa masimulizi kuhusu tukio fulani, kisa au tukio la kweli au la kubuni.

      Sifa kuu za aina hii ya utungo kama huu ni 

      • Matamshi na lafudhi ni lazima yawe sahihi. 

      • Ni lazima mazungumzo haya yagawanyike katika sehemu kuu tatu: mwanzo, kati, na mwisho. 

      • Utungaji wa masimulizi ni lazima uzungumzie ukweli wa jambo linalozungumziwa.

       • Uwasilishaji wa hali , matukio, na mazingira yanayodhihirika waziwazi. 

      • Mtiririko wa mawazo wenye mshikamano. 

      • Msimuliaji ni lazima azungumze kwa nidhamu na kwa lugha sanifu inayoeleweka kwa watu wote.

       • Mfulilizo wa matukio ya haraka haraka.

      • Masimulizi yawe ya kupendeza sana, pengine ya kuchekesha na yenye kuteka hisia kwa maelezo ya kushangaza au yenye kujaa taharuki. 

      • Kutoa funzo maalumu kutokana na hadithi yenyewe, yaani maadili fulani kuhusu maisha kwa ujumla.

      Mazoezi

      1. Nini maana ya insha ya masimulizi?

      2. Je, unalazimishwa kufanya nini ili kazi ya uandishi wa insha ya masimulizi ifaulu?

      25.5 Kusikiliza na kuzungumza: Majadiliano

      Zoezi la 8: Serikali ya Rwanda inawahimiza wananchi kujitafutia ajira kutokana na uhaba wa kazi. Jadili kuhusu namna ya kujitafutia kazi.

      25.6 Utungaji wa insha ya masimulizi

      Zoezi la 9: Baada ya kusoma kifungu kuhusu insha za masimulizi “mafanikio ya kudumu. “Wewe mwanafunzi, tunga insha ya masimulizi kuhusu tukio fulani, kisa au tukio la kweli au la kubuni kwa kuheshimu vipengele muhimu vya insha ya msimulizi na taratibu zake.

      SOMO LA 26: INSHA ZA KUBUNI

      Zoezi la 1

      Jibu maswali haya

      1. uliwahi kusikia neno insha ?

      2. wahusika katika insha walikuwa akina nani?

      3. Eleza mambo mawili uliyofaidika nayo katika insha hiyo

      4. Kuna maadili yoyote uliyoyapata kutokana na insha hiyo?

      26.1 Kusoma na Ufahamu: Kioja katika Mbuga ya Mwanga

      Soma kifungu kifuatacho kuhusu “ Kioja katika Mbuga ya Mwanga”, kisha jibu maswali ya ufahamu yanayofuatia hapo chini. 

      Siku ya mazishi ya Mzee Ngedere ilikuwa siku tukufu kwa wanyamapori wote wa Mbuga ya Mwanga. Waliamua asindikizwe kwa sherehe maalum kwa sababu mbili. Kwanza, alikuwa mpatanishi wao mwenye busara. Mizozo ilipokuwa ikizuka mbugani alikuwa akiitatua bila kupendelea upande wowote. Pili, Mzee Ngedere alikuwa mganga bingwa wa kienyeji aliyeheshimika sana. 

      Baada ya kifo cha Mzee Ngedere umoja wa wanyama ulivunjika. Baadhi yao walikuwa wakipendekeza mganga huyu arithiwe na Bwana Chui na wengine wengi wakimpendekeza Bi Tembo. Siku hii ya mazishi, Mfalme Simba aliamua kulifumbia jicho jambo hili la urithi wa uganga ili Marehemu asisindikizwe kwa zogo na vurumai.

      Waombolezaji walimiminika kwa wingi: wafalme na wanyama kutoka mbuga jirani, pia walihudhuria. Wanyama walijaa uwanjani hata pasipatikane nafasi ya kuweka sindano. Kila mnyama kutika mbuga ya Mwanga alijiandaa kila iwezekanavyo kuifanikisha siku hiyo. Lakini wote walifanya hivi nyoyo zikisumbuka kwa majonzi kwa kumpoteza mshauri na mganga wao. 

      Kikundi maalum cha wanyamapori kilitengewa mahali maalum pa kupikia chakula; kilitengeneza meko na kuteleka vyungu. Isitoshe, kikundi hiki kilipasuliwa kuni na kuletewa maji na wanyama mabarobaro. Majimbi, ng’ombe na mbuzi wa kijiji cha Mwanga walikatiziwa starehe zao kwa kufanywa kuwa kitoweo cha wageni na wenyeji. 

      Kabla ya sala ya wafu kuanza, waombolezaji walijipanga kwa mstari mrefu na kumuaga mpatanishi na tabibu wao kitamaduni. Waliimba nyimbo za kuomboleza na kubeba mikoba yake ya utabibu pamoja na mgwisho wake wa uungwana. Gunia lenye maiti lilibebwa kutoka nyumba ya Mzee Ngedere hadi kaburi lililokuwa karibu na kasri la Mfalme Simba.

      Baada ya msafara huo kufika makaburini, msoma ratiba, Binti Sungura, alimkaribisha Kasisi Nyati kuongoza sala. “Karibu Kasisi Nyati! Tafadhali karibia uanze kazi yako!” Alisema Binti Sungura. Wasemaji wote waliopewa fursa walikariri sifa za marehemu. “Mzee alipendwa na wanyama wengi kwa kuwa na moyo mkunjufu na kwa ujuzi wake wa kuamua mizozo.” Alitoboa Mzee Kobe. “Kijiji kizima kitahasirika mno kwa kumkosa tabibu mwenye uzoefu mkubwa.” Mfalme Simba akanena. “Maskini wa Mungu weee! Hasara ilioje jamani?” Alilalamika Bibi Tai huku akipangusa machozi. “Tumempoteza mpatanishi na tabibu mashuhuri. Alikuwa akitujali sisi sote wanawake. Ewe Mungu! Tafadhali uilaze roho yake mahali pema!” Alipasua. 

      Kipindi cha salamu za rambirambi kilipomalizika, jua lilikuwa likiwaka sana. Kila kiumbe kilikuwa kikitokwa na jasho. Wakati wa kufundisha Neno la Bwana ulipofika, kasisi wa Mbuga ya Mwanga, Mzee Nyati, alichukua fursa akamsifu Mungu na kuvuta nyoyo za wanyama zimhimidi Mungu wao. Yeye alisimama , akivaa miwani sawasawa na kufungua jarida la karatasi. Baada ya kusafisha koo lake alianza kuzungumza. Alizungumza na kuzungumza hadi wanyama wengine waanze kuota mizizi kwa sababu ya kukaa na wengine kusimama kwa muda mrefu. “ Maliza maneno yako haraka, tukamzike Mzee Ngedere! Bwana Chui alimwamrisha Kasisi Nyati. 

      Bwana Chui alisema haya huku akipanga kumrithi Mzee Ngedere kwa sababu alikuwa makamu wake. Aliposikia hayo, Bi Simba alilia kwa kwikwi huku akimwomba Mungu amrudishe mpatanishi wao kwa sababu Bwana Chui alikuwa akiogopwa na wanyama wengi kwa ukatili wake. Alikuwa hawapokei vizuri walipokuwa wakimpelekea malalako yao.

      Kimya kizito kilitawala kati ya wanyamapori. Kitambo, wingu jeusi lilipita na kuwatisha wale wote waliokuwa hapo. “Shetani kapita!” Alisema Kunguru huku moyo ukimdundadunda na kujitayarisha kukimbia. “Acha kututisha wee!” Mfalme Simba alimkatiza Kunguru. 

      Mara gunia lilianza kutikisika na kuonyesha dalili ya kuwa ndani mlikuwamo kiumbe hai. Kasisi Nyati alipoona hayo alianza kutokwa na jasho kubwa hadi mwili mzima ukalowa maji. Lo! Wanyama wengi walitimka na kutawanyikia vichakani na porini. Kasisi Nyati naye hakuweza kuhimili kioja hicho. Bila ya kuvua joho lake ,naye alitimua mbio na kufuata wafuasi wake. Mfalme Simba na Bwana Chui walijizatiti na kubaki pale ili wajionee kilichokuwa kikijiri hapo. “Tafadhali msikimbie!” Walisikika wakiwaambia wenzao. Baada ya muda mfupi, walimwona Mzee Fuko na wake zake wawili wakijitokeza chini ya gunia wakidai kuja kumzika Mzee Ngedere. “Kwa sababu gani mmefunga njia yetu?” Mzee Fuko aliuliza. “Samahani Mzee Fuko, hatujafanya jambo hili kwa makusudi.” Alieleza Mfalme Simba. Bi Fuko alipotaka kujua sababu iliyowafanya wanyama kutimka, alielezwa kwamba labda walidhani kwamba Mzee Ngedere amefufuka. Bada ya hapo, Bwana Chui alitumwa kuwarudisha wanyama kwa sababu kulikuwa hakuna jambo la kuwafanya wakimbie. 

      Baada ya kupata taarifa, wanyama walirudi na kumzika mganga na mpatanishi wao mpendwa. Mazishi yalipomalizika, Bi. Tembo alichaguliwa kuwa mpatanishi. Nafasi ya makamu ikapewa Binti Sungura. Bwana Chui alipotaka kuzusha ghasia alionywa kuwa angefunguliwa mashtaka kwa kosa la uchochezi wa ghasia. Kwa kusikia hayo aliomba msamaha, akaahidi kugeuka mzalendo mwema. Aliwaambia wafuasi wake kutimiza masharti ya Mfalme Simba. Tangu siku hiyo hali ya utulivu ilirudi. Upendo na amani yakatawala katika Mbuga ya Mwanga.

      Maswali ya ufahamu

      1. Taja sifa mbili muhimu za Marehemu Mzee Ngedere.

      2. Wanyama walifanya matayarisho gani kabla ya sala ya wafu kuanza?

      3. Ni waombolezaji gani waliokuwa hapo?

      4. “Kijiji kizima kitaharibika mno”. Aliyesema haya alitaka kumaanisha nini?

      5. Dua ya Bi Tai ilikuwa ipi?

      6. Kasisi Nyati alikuwa akivaa namna gani?

      7. Ni nani aliyesema kwamba shetani alipita?

      8. Kwa sababu gani Bwana Chui alipendekeza kumzika Mzee Ngedere haraka?

      9. Kwa sababu gani gunia lilikuwa likitikisika?

      10. Kwa sababu gani mwili wa Kasisi Nyati ulilowa maji?

      26.2 Msamiati Kuhusu Kifungu cha Habari

      Zoezi la 2: Toa maana za maneno yafuatayo:

      1. Kioja

      2. Mazishi

      3. Waliamua

      4. Walimiminika

      5. Nyoyo

      6. Majonzi

      7. Kasri

      8. Joho

      9. Walijizatiti

      10. Uchochezi

      Zoezi la 3: Toa neno jingine lililotumiwa katika kifungu lenye maana sawa na ya lile lililopigiwa mstari chini.

      1. Leo ni siku nzuri sana.

      2. Bwana Kagabo alikuwa tabibu mashuhuri.

      3. Baada ya kifo cha Maria watoto wake walilia kwa simanzi.

      4. Miongoni mwa vitambulisho vya mfalme wa kijadi  mlikuwamo usinga.

      5. Rais wa Jamhuri yetu anawathamini wananchi wake.

      6. Kila siku Runinga ya

      Taifa hutuonyesha yale yanayotendeka ulimwenguni.

      7. Si vizuri mtu awe ibilisi wa mwenzake.

      8. Maishani mtu anapaswa kuvumilia mateso yote.

      9. Kalisa alinyeshewa na mvua nguo zake zikatota.

      10. Mhubiri alikuwa akihubiri Neno la Mungu.

      Zoezi la 4: Maneno yafuatayo yana maana zaidi ya moja. Kwa kila neno, tunga sentensi mbili kwa kuonyesha maana hizo tofauti.

      1. Fuko

      2. Paa

      3. Chungu

      4. Kanga

      5. Wimbi

      6. Kiboko

      7. Kifaru

      8. Duma

      9. Swala 

      Zoezi la 5: Kamilisha methali zifuatazo:

      1. Teke wa kuku ..................

      2. Jongoo la shamba ................

      3. Kunguru mwoga ...................

      4. Simba mwenda kimya...................

      5. Kila ndege .............................

      6. Kelele za chura ....................

      7. Kuku mgeni ........................

      8. Usihesabu vifaranga ................

      9. Mgema akisifiwa, ......................

      10. Mwenda juu kipungu,.......................

      Zoezi la 6: Jaza nafasi.

      Mfano: Twasema kifaranga kwa kuku.

      Hapa tutasena namna gani?

      1. Simba:................................

      2. Kondoo:..............................

      3. Mbwa:.................................

      4. Sungura:.............................

      5. Ndege:...............................

      Zoezi la 7: Jaza pengo .

      Mfano: Mume ni kwa mke na mvulana ni kwa msichana.

      1. Fahali ni kwa...... au...... na ..... ni kwa mbuzi.

      2. ..........ni kwa Jongoo au.......... na mjomba ni kwa.........

      3. Malkia ni kwa............... na ............ni kwa kaka.

      4. Nyanya ni kwa ............. na yaya ni kwa .............

      5. ............... ni kwa ndege na kasri ni kwa ............

      26.3 Sarufi: Usemi wa Asili na Usemi wa Taarifa katika Hali ya Kuamrisha na Hali ya Kuomba.

      Zoezi la 8: Chunguza sentensi zifuatazo kisha uziweke katika usemi wa taarifa.

      1. “Maliza maneno yako haraka, tukamzike Mzee Ngedere!” Chui alimwamrisha Kasisi Nyati.

      2. “Acha kututisha wee!” Mfalme Simba alimkatiza Kunguru.

      3. “Ewe Mungu! Tafadhali uilaze roho yake mahali pema!” Mzee Kobe alisema.

      4. “Njoo ukaanze kazi yako!” Alisema Binti Sungura.

      5. “ Tafadhali msikimbie!” Bwana Chui alisikika akiwaambia wenzake

      Maelezo muhimu 

      Wakati wa kubadili sentensi kutoka usemi wa asili hadi usemi wa taarifa katika hali ya kuamrisha na hali ya kuomba mambo yafuatayo hujikokeza:

       • Hali ya kuamrisha hugeuka hali ya kawaida ya halisi ya kitenzi au ikageuka hali ya kushawishi. Na vitenzi vinavyodokeza huwa kutaka, kuamrisha, n.k.


      • Hali ya kuamrisha hugeuka hali ya kawaida ya halisi ya kitenzi au ikabaki kama ilivyokuwa mwanzoni. Na vitenzi vinavyodokeza huwa kunasihi, kusihi, kubembeleza, kuonya, n.k.


      Zoezi la 9: Geuza sentensi zifuatazo katika usemi wa taarifa

      1. “Toka nje!” Mama alimwambia mtoto.

      2. “Hebu safisheni darasa!” Mwalimu aliwaambia wanafunzi.

      3. “Njoo nikutume!” Mama alimwita Kalisa.

      4. “Tafadhali usigombane na wenzako tena!” Maria alimwonya Rubyogo.

      5. “Ngozi ivute ingali mbichi!” Baba alimwambia mtoto wake

      Zoezi la 10: Geuza sentensi zifuatazo katika usemi wa asili

      1. Mwalimu aliwaonya wanafunzi wake kwa kutotunza vitabu vizuri.

      2. Shangazi alitutaka tuwakaribishe wageni.

      3. Mama aliwakanya watoto wasisogee karibu na moto.

      4. Daktari aliniambia nikaonane naye baada ya wiki mbili.

      5. Dakatari wa meno alimshauri mgonjwa kupiga mswaki mara mbili kwa siku.

      26.4.1 Matumizi ya lugha: Insha za Kubuni na Mazoezi ya Jumla

      Zoezi la 11: Jaza jedwali lifuatalo kwa kuchagua majina katika orodha ya hapo chini.


      Duma, pakashume, bundi, njiwa, mbweha, dura, fisi, funo, kikwara, tai, ngiri, ngedere, swala, koho, choroa, flamingo, gogota, kulungu, kware, kanga, nungu, chui, hua.

      26.4.2 Maelezo muhimu kuhusu insha za kubuni

      Zoezi la 12: soma maelezo muhimu kisha ujibu maswali ya hapo chini.

      Maelezo muhimu kuhusu insha za kubuni

      Insha za kubuni ni aina ya insha ambazo hutungwa kuhusu mawazo yanayozuliwa na ambayo si matukio ya kawaida. 

      Insha za namna hii humhitaji mwandishi kujitia, kimawazo, katika hali fulani ya kubuni na kutunga hadithi katika hali hiyo. Kwa hivyo ili mwandishi afaulu katika uandishi wake, ni sharti awe na uwezo wa kubuni mawazo kwa undani na pia kuweza kuyaeleza mawazo hayo kwa njia ya kuaminika kwa wasomaji.

      Tanbihi: Kuwepo kwa insha za kubuni hakuondoi ukweli unaosema kwamba insha zote hutokana na ubunifu wa mwandishi. Hivi ni kwa sababu aina zote za insha huwa zinaandikwa kwa mawazo yanayobuniwa na akili ya mwandishi.

      Maswali

      1. Kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu Kioja katika Mbuga ya Mwanga ni aina gani ya insha? Kwa sababu gani?

      Chunguza:

      a. Wahusika na matendo yao

      b. Mandhari

      c. Yanayosimuliwa katika kifungu cha habari.

      2. Ndiyo! Ninakubaliana na hoja hii kwa sababu kazi yoyote ya utungaji inatokana na ubunifu wa mwandishi. Mwandishi anakaa na kufikiri namna ya kutunga kazi hiyo.

      26.5 Kusikiliza na Kuzungumza: Majadaliano

      Zoezi la 13: Ukishirikiana na wenzako, jadilieni kuhusu

      1. “Umuhimu wa Wanyamapori kwa Nchi ya Rwanda”.

      2. “Umuhimu wa Wanyama Wafugwao Nchini Rwanda.”

      26.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari

      Zoezi la 14: Tunga kifungu cha habari kuhusu mojawapo ya mada zifuatazo:

      1. “Mikakati ya Kulinda Wanyamapori Nchini Rwanda.”

      2. “Umoja wa Wananchi ni Uti wa Mgongo wa Maendeleo ya jamii.”

      SOMO LA 27: RIPOTI

      Zoezi la 1:Jibu maswali haya

      1. Ulishawahi kusoma ripoti ?

      2. Ilikuwa inahusu nini?

      3. Kuna uhusiano wowote na kichwa cha utakachokisoma hapo chini?

      27.1 Kusoma na Ufahamu: Ripoti

      Soma kifungu kifuatacho kuhusu “Ripoti” kisha jibu maswali yaliyopo hapo chini yake. 

      Ripoti ni maelezo yanayotolewa kuhusu mtu, kitu au jambo fulani lililotokea. Aidha, ripoti ni taarifa inayohusiana na shughuli au jambo fulani lililofanywa au kufanyika. Ripoti huandikwa kwa madhumuni ya kutoa taarifa ili iweze kufanyiwa kazi au kuhifadhiwa kama kumbukumbu. Ripoti huandikwa pia kwa madhumuni ya kuarifu watu kuhusu mabadiliko muhimu au maendeleo ya shughuli fulani. Ripoti inaweza tena kuagiza utekelezaji fulani, kupendekeza kufanyika kwa jambo fulani na kupima au kutathmini utendaji kazi fulani au maendeleo yaliyofikiwa. 

      Watu mbalimbali huweza kuandaa ripoti na kuiandika kulingana na majukumu yao ya kikazi. Kwa hiyo, baadhi ya ripoti huhitaji uchunguzi wa kiutafiti kuhusu jambo fulani ambapo tume fulani, ya polisi au ya kazi yoyote ile huweza kuundwa kwa ajili ya uchunguzi wao wa suala lililopo na ambalo lahitaji ufumbuzi kutegemeana na ripoti yao. 

      Matokeo yanayoandikwa, uchunguzi unaofanywa na mapendekezo yanayotolewa huwa ni ripoti maalum ambazo hutokana na utafiti uliofanywa na tume iliyowekwa kwa ajili hiyo. Maendeleo yaliyofikiwa, maisha ya kawaida na utendaji kazi, matumizi ya fedha na mapato, haya yote hufanyiwa ripoti.

      Muundo wa ripoti unategemea kwa kiasi kikubwa aina ya ripoti inayohusika. Lakini kimsingi, ripoti ni lazima iwe na mpangilio mzuri wenye mada zinazozungumziwa na labda hata mada ndogo ndogo zenye kuzingatia utaratibu wa nambari. Matumizi ya nambari husaidia kuipa ripoti mpangilio mzuri na wenye kueleweka kwa urahisi. Ripoti hazipaswi kuwa ndefu sana na zinapaswa kuwasilisha mambo muhimu kwa ufupi. Mwandishi wa ripoti hutumia mbinu za kufupisha lakini anahakikisha kuwa kila kitu kimezungumziwa. Ripoti hutumia sentensi fupi fupi zinazowakilisha mambo muhimu kwa uwazi. Ni vyema lugha inayotumiwa katika ripoti iteuliwe kwa uangalifu na isiwe na hisia au sifa ya kuathiri vibaya wanaoisoma. 

      Ripoti ina sehemu kuu nne ambazo ni kichwa, utangulizi, kiini na mwisho wa ripoti. Kila sehemu ina namna inavyoandikwa na mambo inayoyazingatia. Kichwa cha ripoti kinaandikwa kwa maelezo machache. Mambo muhimu yanayozingatiwa katika kichwa cha ripoti ni mahali tukio au jambo lilipofanyika, aina ya tukio au jambo lililofanywa, tarehe na muda wa tukio au jambo lililoshughulikiwa na ripoti hiyo. Baada ya kuandika kichwa cha ripoti, mwandishi anaandika utangulizi wa ripoti ambao unaonyesha lengo na madhumuni ya ripoti. Katika kiini cha ripoti, mwandishi anaeleza kwa ufasaha mambo yaliyotokea, chanzo chake, ukubwa wake na madhara au faida yake. Mwisho wa ripoti huonyesha msimamo, mapendekezo na maoni ya mwandishi wa ripoti. Baadaye ni lazima ripoti ionyeshe jina la mwandishi, cheo chake pamoja na terehe ripoti hiyo ilipoandikwa na iwekewe viambatisho vya kuthibitisha yaliyozungumziwa ikiwa vinahitajika. 

      Ingawa ripoti zina sehemu sawa, ukubwa na uzito wake unatofautiana kutokana na mambo na masuala yanayoripotiwa, madhumuni pamoja na aina ya ripoti. Ripoti ya polisi ni tofauti na ripoti ya daktari. Vilevile, ripoti ya tume ni tofauti na ile ya utafiti au ya kazi na kadhalika. Mwandishi wa ripoti anaweza kutoa ushahidi unaohusu suala au jambo fulani. Katika hali hii, mshahidi anasema kuwa alishiriki katika jambo hilo au anahakikisha kuwa aliona yaliyotokea.

      Ripoti hutolewa kwa mkuu aliyeagiza uandishi wa ripoti hiyo na huhitaji umakini wa yule aliyepewa wajibu huo. Kwa hivyo, ni lazima anayepewa ripoti achunguze jambo kwa uangalifu ili aweze kutoa ufafanuzi mzuri wa jambo hilo kwani mapendekezo yake huathiri kwa kiwango kikubwa uamuzi unaochukuliwa kulihusu jambo hilo.

      Maswali ya ufahamu

      1. Ripoti ni nini?

      2. Madhumuni au malengo ya ripoti ni yapi?

      3. Taja na kueleza aina za ripoti zilizozungumziwa katika kifungu hiki.

      4. Utaratibu wa nambari unasaidia nini katika muundo wa ripoti?

      5. Sentensi zinazotumiwa katika ripoti ni za aina gani?

      6. Jadili matumizi ya lugha katika ripoti.

      7. Jadili umuhimu wa ripoti.

      8. Kwa nini mwandishi wa ripoti hutakiwa kuwa mwangalifu zaidi ?

      9. Eleza sehemu kuu za ripoti.

      10. Kwa maoni yako, ripoti nzuri ni ipi?

      27.2 Msamiati kuhusu Ripoti

      Zoezi la 2: Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari ulichosoma hapo juu kuhusu maana ya ripoti.

      1. Matokeo 6. Kuarifu

      2. Ripoti 7. Kupendekeza

      3. Taarifa 8. Utendaji kazi

      4. Shughuli 9. Mbinu

      5. Madhumuni 10. Kiini

      Zoezi la 3 : Husisha maneno katika sehemu A na maana zake katika sehemu B      27.3 Sarufi: Matumizi ya Usemi Halisi na Usemi wa Taarifa katika Hali ya Kuuliza

      Zoezi la 4: Chunguza hali ya sentensi zifuatazo; halafu utunge sentensi tano kama hizo.

      1. Sentensi A: ‘‘Utaandika ripoti kesho?’’ Mama yake alitaka kujua.

      Sentensi B: Mama yake alitaka kujua ikiwa angeandika ripoti siku ingefuata.

      2. SentensiA: ‘‘Baba yako anakupenda sana?’’ Vumilia aliuliza.

       Sentensi B: Vumilia aliuliza ikiwa baba yake alimpenda sana.

      Maelezo muhimu kuhusu matumizi ya usemi halisi na usemi wa taarifa katikahali ya kuuliza

      Usemi halisi/usemi wa asili ni unukuu wa maneno asili kama yalivyosemwa na msemaji. Herufi kubwa zinatumiwa kuutanguliza, alama za kunukuu na zile za kuuliza hutumika.

      Mifano: “Kwa nini pesa hazipatikani siku hizi?” Mugisha aliuliza.

                      “Utarudi lini ?”Baba aliuliza mtoto wake.

      Usemi wa taarifa ni usemi wa kimaelezo ambapo maneno halisi yaliyosemwa na msemaji hutolewa maelezo tu bila kuyanukuu. Ni maneno ya mtu fulani akieleza alivyosema mtu mwingine. Ni ripoti ya yale aliyoyasema mtu mwingine.

      Mifano: 1. Mugisha aliuliza sababu pesa hazikupatikana siku hizo.

                      2. Baba aliuliza mtoto wake wakati angerudi.

      • Katika kutoa ripoti, katika hali ya kuuliza wakati ujao unaoonyeshwa na

      kiambishi cha wakati –ta- unabadilika na kuwa hali ya -nge-

      • Nafsi ya kwanza na ya pili inabadilika ikawa nafsi ya tatu.

      • Wakati au siku (kesho) huwa siku ingefuata

      • Alama za kunukuu na alama ya kuuliza hazitumiki.

      • -angu na -ako huwa -ake ; -etu na –enu huwa -ao

      Zoezi la 5: Geuza sentensi zifuatazo ziwe katika usemi wa taarifa :

      1. “Wewe ni mwalimu?” Mtoto aliuliza.

      2. “Utafanya ripoti ya mkutano lini?” Mwenyekiti alitaka kujua.

      3. “Utaenda shule lini?” Mama aliuliza.

      4. “Kwa nini ripoti ya kifedha haijaonekana?” Katibu mtendaji aliuliza.

      5. “Mlichagua mada gani?” Mwalimu alitaka kujua.

      Zoezi la 6:

      1. geuza sentensi zifuatazo ziwe katika usemi halisi/usemi wa asili:

      2. Karisa alitaka kujua ikiwa mgeni wake angerudi siku ambayo ingefuata.

      3. Kariza aliuliza sababu ya kukosa kazi.

      4. Mwalimu aliuliza wanafunzi jinsi wangeshinda mtihani wakati hawataki kujifunza.

      5. Mama aliwauliza watoto wake ikiwa walifanya kazi aliyowapatia.

      6. Manzi alitaka kujua kwamba angeshiriki katika mkutano.

      27.4 Matumizi ya Lugha: Mazoezi ya Jumla

      Zoezi la 7: Kamilisha maneno yafuatayo kwa kutumia herufi zinazokosekana ili yaweze kuleta maana:      Zoezi la 8: Jadili mada zifuatazo kuhusu ripoti :

      1. Ripoti kuhusu ziara ya wanafunzi wa shule yako waliyofanya katika jumba la

      makumbusho.

      2. Ripoti kuhusu kongamano la lugha ya Kiswahili uliloshiriki.

      27.5 Kusikiliza na Kuzungumza : Majadiliano

      Zoezi la 9: Jadilini mawazo yanayoweza kupatikana katika ripoti za mada zifuatazo:

      1. Ripoti kuhusu mchango wako kama mwanafunzi katika maisha yako hapo

      shuleni kwako.

      2. Ripoti kuhusu klabu za wanafunzi katika shule zinazopatikana katika tarafa yako.

      27.6 Utungaji wa Kifungu cha Habari

      Zoezi la 10: Kwa kuzingatia maana ya ripoti, tunga kifungu cha habari kuhusu mada moja kati ya hizi zifuatazo:

      1. Shida za wanafunzi shuleni.

      2. Kuboresha elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu.

      SOMO LA 28: UTUNZI WA RIPOTI

      Tazama kwa makini mchoro huu na kujibu maswali yanayofuata hapo chini


      Zoezi la kwanza:Jibu maswali yafuatayo:

      • Elezea kuhusu wahusika unaowaona kwenye mchoro huu.

      • Wahusika hao wako wapi? Wanafanya nini?

      • Kuna uhusiano wowote kati ya mchoro huo na kichwa cha habari hapo chini?

      28.1 Kusoma na Ufahamu: Mfano wa Ripoti

      Soma ripoti ifuatayo kuhusu kazi za umuganda zilizofanyika katika Tarafa za Kabaya na Hindiro Wilayani Ngororero tarehe 27 Aprili hadi tarehe ya 10 Mei 2018; kisha, jibu maswali uliyopewa katika sehemu ya ufahamu.

      Utangulizi 

      Kazi za Umuganda ni mojawapo ya kazi muhimu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla. Nchi ya Rwanda imeamua kutumia sera hii ya shughuli za umuganda ili kupunguza gharama ambayo inatumiwa kuboresha uchumi, maisha na maendeleo ya wanajamii wote. Sheria Namba 52. 2007 tarehe 17.11. 2007 kuhusu kazi za Umuganda, inasema kuwa kazi za Umuganda hufanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi nchini kote ambapo kila mtu aliye na umri wa miaka 18 hadi 65 hutakiwa ashiriki katika shughuli hizo.

      Kulingana na mahitaji ya wanajamii katika eneo fulani, viongozi hushirikiana na wanajamii ili kuamua kwa pamoja kuhusu shughuli muhimu wanazozifanya kila mwezi, yaani katika kazi za Umuganda. Miongoni mwa kazi zinazotekelezwa katika mradi huu ni kama zile za ujenzi wa nyumba, vyoo, madaraja, ukarabati wa miundo mbinu, usafi wa mazingira, na upandaji wa miti.. 

      Mnamo mwezi wa Aprili 2018, mvua iliyonyesha katika maeneo mengi nchini Rwanda, iliharibu mali nyingi ambapo nyumba, mazao na vitu vingine viliharibika sana kutokana na mmomonyoko wa ardhi. Wilaya ya Ngororero ni miongoni mwa wilaya ambazo ziliathirika kutokana na maafa yaliyotokana na mmomonyoko huo wa ardhi. Kwa hivyo, Wizara ya Serikali za Mitaa, kwa kushirikiana na Wizara ya Maafa, ziliunda kamati iliyopewa wajibu wa kuchunguza athari za maafa katika kusuluhisha tatizo hilo. Kamati iliundwa na watu watano ambapo watu wawili walitoka Wizara ya Serikali za Mitaa na watu watatu wakatoka Wizara ya Maafa. Shuguli yenyewe ilianza tarehe ya 27 Aprili hadi tarehe ya 10 Mei 2018 ambapo tarafa mbili zilitembelewa. 

      Katika kutekeleza shughuli hiyo, tarafa za Kabaya na Hindiro zilitembelewa wakati wa shughuli za umuganda za mwezi Aprili. Ili kufanikisha kazi yao, kamati ililenga kukutana na wananchi walioshiriki katika shughuli za Umuganda mwezi wa Aprili mwaka 2018, Katibu Mtendaji wa kila tarafa iliyohusika, kisha viongozi wote wa wilaya ambapo wanakamati walimhoji Bwana Meya na makamu wake baada ya kuzunguka maeneo mbalimbali na kuzungumza na watu waliokuwa wameathirika.

      Yafuatayo ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa kuhusu nafasi ya shughuli za Umuganda katika kupunguza maafa ya mmomonyoko wa ardhi wilayani Ngororero. Ripoti ya uchunguzi huu imebainisha maafa na athari za mmomonyoko wa ardhi katika Tarafa za Kabaya na Hindiro, shughuli za Umuganda zilifanywa na wanajamii ili kupunguza athari hizo. 

      1. Athari na Maafa yaliyosababishwa na Mmomonyoko wa Ardhi

       Mvua kubwa zilisababisha mmomonyoko wa udongo na kuharibu mimea, nyumba, barabara na miundombinu mingine katika Wilaya ya Ngororero. Nyumba zilizobomoka kwa mmomonyoko wa ardhi ziliacha wakazi wengi bila makazi na wengi wao wakapoteza mali nyingi. Barabara ziliharibika na kuathiri safari za magari kwa muda fulani. Mtiririko wa maji hasa hasa katika mabonde umeharibu mazao mengi na kuacha mashamba mengi yakiwa yameathirika. Hata hivyo, kuna watu na wanyama waliopoteza maisha yao. Takwimu zilionyesha kwamba nyumba mia moja na ishirini ziliporomoka, ekari mia mbili za mazao zikaharibika pamoja na barabara nyingi za mitaa.

      2. Shughuli Zlizofanywa Kupunguza 

      Maafa ya Mmomonyoko wa Ardhi. Kwa kukabiliana na maafa ya mmomonyoko wa ardhi, kama inavyotendeka katika sehemu nyingine za nchi ya Rwanda, kuliandaliwa kazi maalumu zijulikanazo kama kazi za Umuganda ili kupunguza maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa katika Tarafa za Kabaya na Hindiro Wilayani Ngororero. Miongoni mwa kazi zilizofanywa ni pamoja na kazi za ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu, uboreshaji ,usafi na uhifadhi wa mazingira. 

      2.1 Ujenzi na Ukarabati wa Miundo mbinu 

      Kazi zilizotekelezwa katika ujenzi na ukarabati ni pamoja na ujenzi wa nyumba zilizobomoka kwa maji na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi wa vyoo, ukarabati wa madarasa, barabara na madaraja vilivyoharibika. Alipohojiwa kuhusu jinsi ujenzi na ukarabati hutekelezwa katika kazi za Umuganda, Meya wa Wilaya ya Ngororero alisema kwamba wanaanzia kwenye vitendo vinavyohitaji msaada wa dharura kama vile nyumba za watu wasiojiweza, mathalan wazee, watu wenye ulemavu pamoja na watu wengine wanaohitaji msaada maalumu. Ili kufanikisha kazi hizi, waliohudhuria walijigawa katika makundi, na kila kundi likapewa kazi ya kutekeleza wakiongozwa na kiongozi mmoja kutoka kwenye ngazi ya Tarafa au ngazi ya Wilaya. 

      2.2 Kazi za Usafi 

      Mvua kubwa zilizonyesha katika Wilaya ya Ngororero zilisababisha uchafu. Katika hali hii, kazi za usafi zililenga usafishaji wa barabara zilizokua zimejaaa takataka kutoka kwenye nyumba zilizoporomoka, kutengeneza barabara kwa kufukia mashimo ya maji, kujenga na kukarabati vyoo vilivyoporomoka na kukata nyasi na vichaka kando ya barabara. ‘‘Usafi ni njia bora ya kujikinga na maradhi yatokanayo na uchafu.” Alisema makamu wa Meya. Akaongeza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha kwamba kuna usafi wa kutosha nyumbani kwake, kimwili, kimavazi na kwenye mazingira yanayomzunguka. Katika mwelekeo huu, Katibu mtendaji wa Tarafa ya Hindiro akishirikiana na mwenziye wa Tarafa ya Kabaya waliwakumbusha wananchi kukata vichaka na nyasi kando ya makazi yao na kuziba madimbwi ya maji kwa kuharibu mazalio ya mbu asababishaye maradhi ya malaria. 

      2.3 Uhifadhi wa Mazingira 

      Kwa upande wa uhifadhi wa mazingira, kazi zilizofanywa zilitia mkazo upandaji wa miti kwenye milima na kando ya barabara kwa kukabiliana na mmomonyoko wa ardhi. Kulichimbwa pia mifereji na mashimo ya kudhibiti maji katika msimu wa mvua. Katika hatua hii, wakazi wa Tarafa hizi walitakiwa pia kupanda miti ya matunda kwa kuboresha lishe yao.

      3 Matokeo ya Shughuli za Umuganda katika 

      Wilaya ya Ngororero Zipo faida kubwa za kazi za umuganda zilizofanyika katika Wilaya ya Ngororero. Wananchi walioulizwa walieleza kwamba kazi hizi zina manufaa mengi kwa wananchi kwa kuwa wananchi wenyewe hutekeleza kazi ambazo zingegharimu Serikali pesa nyingi. Pesa hizi zinazookolewa zinatumiwa katika miradi mingine ya kimaendeleo. Meya wa Wilaya ya Ngororero alieleza kuwa kazi zote zilizotekelezwa siku hiyo katika tarafa hizo mbili ziligharimu takriban pesa milioni nne faranga za Rwanda. Aliongeza kuwa pesa hizo zingejenga darasa moja au kufanya kazi zingine kwa manufaa ya wananchi. Faida nyingine za kazi za umuganda ni kwamba baada ya kazi hizi, wananchi walikaa pamoja na viongozi wao na kujadili kuhusu masuala mtambuka mbalimbali. Waliarifiwa kuhusu sera mbalimbali za Serikali kisha wakapewa muda wa kuuliza maswali mbalimbali na kupewa majibu papo hapo. 

      4 Mapendekezo 

      Kama ilivyobainika wakati wa utekelezaji wa kazi za umuganda ni kwamba kuna kasoro kadhaa ambazo zinapaswa kuboreshwa ili kazi hizi ziweze kufikia malengo yake. Kasoro hizi zilijidhihirisha kwa uhaba wa vifaa maalumu vya kutumia katika kutekeleza kazi fulani kama vile rato, toroli, fyekeo, ngazi za kisasa, sululu, nyundo n.k. Kamati inashauri tarafa kununua vifaa hivi ili kufanikisha kazi hizo.

       Ilibainika kwamba kuna kazi zinazohitaji ujuzi maalum wa kiufundi. Lakini kazi hizi hazifanywi vilivyo kutokana na uhaba wa mafundi katika kuzitekeleza kazi hizo. Inapendekezwa kuwa ni jukumu la viongozi wa serikali za mitaa kutatua tatizo hili kwa kuwatayarisha mafundi wa kusaidia katika kazi hizo maalumu. 

      Inapendekezwa kuwa pana umuhimu wa kuwepo kwa juhudi za kuwaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kazi za umuganda kwani ilibainika kuwa kuna wale ambao bado hawajauona umuhimu wa kazi hizi, wakati nguvu za wannachi wote zinahitajika kwa kulijenga taifa. 

      Hitimisho 

      Kama ilivyobainika katika ripoti hii, ni kwamba kazi za umuganda zina faida kwa uchumi wa nchi. Ni njia moja ya kujitegemea bila kumsubiri mtu mwingine kutoka ng’ambo kuja kufanya jambo ambalo wananchi wenyewe wanaweza kulitekeleza kwa nguvu zao. Unapochunguza gharama ya kazi hizi, kwa mwaka mzima, utagundua kuwa ni kiasi kikubwa cha pesa ambazo Serikali ingezitumia kutekeleza kazi hizo. Pesa hizi zinazookolewa ndizo huchangia kujenga miundo mbinu na shughuli nyingine za kimaendeleo. Hivyo, ni lazima sisi sote tuwajibike katika kuimarisha kazi za umuganda na kuzidumisha katika mila na desturi zetu, hivyo nchi yetu itazidi kujijenga na kujitegemea kiuchumi.

      Imetayarishwa na:

      Jina: ……………………………………..

      Cheo……………………..........................

      Saini………………………………...........

      Tarehe……………………………………

      Maswali ya ufahamu

      1. Andika kichwa cha kifungu hiki.

      2. Tukio hili lilitokea wapi? Na wakati gani?

      3. Ni wakina nani waliyoiunda kamati iliyotumwa katika Wilaya ya Ngororero?

      4. Ni nini lilikuwa lengo la ziara hiyo ?

      5. Maafa yaliyoikumba Wilaya ya Ngororero yalisababishwa na nini?

      6. Kwa nini Serikali ya Rwanda imeipa kipaumbele sera ya kazi za umuganda?

      7. Ni shughuli zipi zilizofanywa kwa kupunguza maafa ya mmomonyoko wa ardhi?

      8. Kuna umuhimu wa kupanda miti kwenye milima? Eleza kwa ufupi.

      9. Ni vifaa gani maluumu ambavyo mwandishi wa ripoti anapendekeza vinunuliwe?

      10. Kwa nini mwandishi wa ripoti anapendekeza kuwepo kwa juhudi za kuwaelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kazi za umuganda?

      28.2 Msamiati kuhusu Mfano wa Ripoti

      Zoezi la 2: Tunga sentensi zako kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha ripoti ulichosoma hapo juu.

      1. Kuchochea

      2. Dharura

      3. Wajibu

      4. Madimbwi

      5. Vichaka

      6. Shurutisha

      7. Msimu

      8. Mradi

      9. Masuala mtambuka

      10. Athirika

      11. Changia

      12. Miundombinu

      13. Ng’ambo

      14. Fyekeo

      Zoezi la 3: Tumia mshale kwa kuhusisha maneno katika sehemu A na maana zake  katika sehemu B


      Zoezi la 4: Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno haya: Masuala mtambuka, mradi, fyekeo, kudhihirisha, miundombinu,

      1. Alikuwa anatumia ............................... kwa kukata nyasi zilizoota kando ya barabara.

      2. Usawa wa jinsia ni mojawapo wa .....................................................katika nchi ya Rwanda.

      3. Chapakazi alifanya kazi aliyopewa kwa muda mfupi kwa .....................ubingwa wake.

      4. Maendeleo ya nchi yoyote hutegemea ujenzi wa .....................................................

      5. Tulianzisha ....................................wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha saruji.

      28.3 Sarufi: Usemi Halisi na Usemi wa Taarifa

      Zoezi la 5: Tazama kwa makini sentensi zinazofuata, kisha utoe maoni yako kuhusu

      Muundo wake.

      1. ‘‘Usafi umekuwa tabia kwa wananchi wote’’ Mkuu wa tarafa alisema.

      2. Mtu mmoja alisema ‘‘Wakati usipofanya hivyo ni wewe mwenyewe utaathirika na maradhi yatokanayo na uchafu.”

      3. “Mtoto ni mtoto, awe wa kiume au wa kike "Alisema mjomba.

      4. “Leo nitakuonyesha wazazi wangu "Mtoto alimuambia mwenzake.

      5. “Furaha, kwa nini leo umechelewa darasani?” Mwalimu aliuliza.

      Maelezo muhimu 

      Muundo wa sentensi hapo juu unaonyesha kwamba kauli ya moja kwa moja kutoka kwa msemaji hadi kwa msikilizaji haikufanyiwa mageuzi yoyote. Kauli hii huitwa usemi halisi. 

      Usemi halisi ni unukuu wa maneno yaliyosemwa na msemaji fulani yakiwa katika hali yake ya kwanza. Katika usemi huu hakuna kugeuza maoni ya msemaji. 

      Katika usemi halisi yafuatayo huzingatiwa : 

      • Alama za mtajo au alama za kufungulia na za kufungia maneno hutumiwa mwanzo na mwisho wa maneno yaliyosemwa. {“ ”} 

      • Kila baada ya kufungua, sentensi huanza kwa herufi kubwa m.f :“Tutaondoka kesho” Alituambia 

      • Alama ya hisi au mshangao (!), kiulizo( ?), mkato (,) na nukta (.) huja kabla ya alama za kufunga. m.f : ‘‘Hunipendi?’’ Alimuuliza 

      • Msemaji mpya anapoanza kusema, tunaanza aya mpya ; maneno ya wazungumzaji wawili tofauti hayawekwi katika aya moja.

      Zoezi la 6: Tazama kwa makini sentensi zifuatazo, kisha uweke alama zinazokosekana.

      1. Ninampenda mke wangu Karangwa alisema

      2. Umewezaje kuubeba mzigo huu peke yako Mama aliniuliza

      3. Utarudi kesho Mama yake alitaka kujua

      4. Malizeni kazi mliyopewa mwalimu alituamrisha

      5. Mtahitaji vikombe vingapi vya chai mwenye hoteli alituuliza


      Zoezi la 7: Tazama sentensi zinazofuata kisha utoe maoni yako kuhusu muundo wake.

      1. Mkuu wa Tarafa alisema kwamba usafi umekuwa tabia kwa wananchi wote.

      2. Mwananchi mmoja alisema kuwa wakati mtu usipofanya hivyo ni yeye

      mwenyewe angeathirika na maradhi yatokanayo na uchafu.

      3. Mjomba alisema kuwa mtoto ni mtoto awe wa kiume au wa kike.

      4. Mtoto alimuambia mwenzake kwamba angemuonyesha wazazi wake siku hiyo.

      5. Mwalimu aliuliza Furaha sababu ya kuchelewa darasani siku hiyo.


      Muundo wa sentensi hapo juu unaonyesha kwamba:

      • Alama za kufungulia au kufungia maneno yaliyotamkwa haziwekwi.

      • Alama ya kuuliza na ya mshangao hazitumiwi.

      • Maneno ‘kuwa’ na‘kwamba’ au ‘ya kwamba’hutumiwa.

      Hivyo, iwapo mtu anataka kuwaambia wengine maneno ambayo yalizungumzwa na mtu mwingine bila ya kubadilisha, kupunguza au kuongeza maana ya jambo analotaka kulitolea maelezo, maneno hayo anayosema huitwa Usemi wa taarifa. 

      Usemi wa taarifa ni usemi wa kimaelezo ambapo maneno halisi yaliyosemwa na msemaji hutolewa maelezo tu bila kuyanukuu.

      Mifano

      1. ‘‘Usafi umekuwa tabia kwa wananchi wote’’ Mkuu wa tarafa alisema.Mkuu wa

      Tarafa alisema kwamba usafi umekuwa tabia kwa wananchi wote.

      2. Mwananchi mmoja alisema ‘‘Wakati usipofanya hivyo ni wewe mwenyewe utaathirika na maradhi yatokanayo na uchafu.”

          Mwanachi mmoja alisema kuwa wakati mtu usingefanya hivyo ni yeye mwenyewe angeathirika na maradhi yatokanayo na uchafu.

      3. “Mtoto ni mtoto, awe wa kiume au wa kikeˮAlisema mjomba.

            Mjomba alisema kuwa mtoto ni mtoto awe wa kiume au wa kike.

      4. “Leo nitakuonyesha wazazi wangu ˮ Mtoto alimuambia mwenzake.

      5. Mtoto alimuambia mwenzake kwamba angemuonyesha wazazi wake siku hiyo.

      5. “Furaha, kwa nini leo umechelewa darasani?” mwalimu aliuliza.

            Mwalimu aliuliza Furaha sababu ya kuchelewa darasani siku hiyo.au

            Mwalimu alitaka kujua sababu ya Furaha kuchelewa darasani siku hiyo.

      Ni wazi kwamba unapoyarudia maneno yaliyosemwa na mtu mwingine, ingawa unakidhi maoni yake, lakini kuna mabadiliko ya kisarufi yanayojitokeza. 

      Mabadiliko yanayojitokeza      Zoezi la 8: Geuza sentensi hizi ziwe katika usemi halisi.

      1. Baba alituahidi kwamba angetupeleka mjini kutembea tungeshinda mtihani mwaka ambao ungefuata.

      2. Katibu alitangaza kuwa kungekuwa na mkutano wa wanachama wote ambao walikuwa wamesajiliwa mwezi huo Jumanne iliyopita.

      3. Mshauri aliwasisitizia watoto kuwa kuna umuhimu kuwatii wazazi wao kwani hili lingeongeza siku zao duniani.

      4. Kiranja alitaka kujua sababu ya Afida kuchelewa darasani siku hiyo.

      5. Mwenye hoteli alitaka kujua jumla ya vikombe vya chai tungehitaji.

      6. Mwanafunzi alimwambia kwamba angefaulu katika somo la Kiswahili.

      7. Mkuu wa shule alitahadharisha wanafunzi kutoharibu miti.

      8. Mwalimu alitaka sote twende uwanjani tukashangilie timu yetu.

      9. Kasisi alimshauri Kazimoto kuacha tabia zake za ulevi.

      10. Chapakazi alisema kuwa aliyekuwa akimtesa hakuwa adui yake bali alikuwa rafiki yake wa karibu.

      Zoezi la 9: Geuza sentensi zifuatazo ziwe katika usemi wa taarifa.

      1. ‘‘ Sitathubutu kumpa pesa zangu’’ Zawadi alisema

      2. ‘‘Ninampenda mke wangu sana’’ Yohana anatuarifu

      3. ‘‘Mimi nitawakaribisha wageni leo jioni kisha nitaondoka kwenda kwangu kesho’’ Fatuma alimwambia Juma.

      4. ‘‘Rudieni darasani’’ mwalimu aliamuru wanafunzi.

      5. ‘‘Mkiendelea na tabia yenu, hamtashinda vizuri katika mtihani’’ Mwalimu aliwaonya wanafunzi.

      6. ‘‘Mabasi hayapiti hapa siku hizi, kwanini ?’’ Maria aliuliza

      7. Mama alinionya ‘‘Unamochezea mna hatari.’’

      8. Mwalimu mkuu alisema ‘‘Nyote mliorudi shuleni mkichelewa mtafanya mtihani mwingine maana wenzenu walimaliza kufanya mtihani tangu juzi.’’

      9. ‘‘Ulienda shule jana? Bakari aliniuliza.

      10. ‘‘Toka nje’’ Mama alimuamuru mwanawe.

      Zoezi la 10: Andika sentensi hizi katika usemi halisi au usemi wa taarifa

      1. ‘‘Utaondoka lini?’’ Mama alimuuliza mgeni.

      2. ‘‘Njoo hapa.’’ Baba aliniamuru.

      3. Mwalimu aliniuliza jinsi nilivyofanya kazi ya nyumbani.

      4. Mama alituagiza kusafisha sebule kabla ya kwenda shuleni.

      5. ‘‘Hatutakuwa na mvua ya kutosha mwaka huu.’’ Wakulima walisema.

      6. ‘‘Jua ni gimba kubwa lenye nuru kali lililoko angani ambalo hutoa mwanga na

      joto.’’ Mwalimu alituarifu.

      7. ‘‘Tafadhali, msivute bangi kamwe kwani ni hatari kwa afya yenu’’ Mwalimu mkuu

      aliwasihi wanafunzi.

      8. Baba alituahidi kuwa angetununulia zawadi za kupendeza tungefanya vizuri

      katika mtihani.

      Maelezo muhimu

      Unapoandika ripoti inapaswa kuzingatia mambo yafuatayo:

      1. Hakikisha kuwa umeelewa shughuli inayohusika

      2. Hakikisha unajua urefu unaohitajika na masuala unayopaswa kuyagusia

      3. Kusanya maelezo yote unayohitaji kuhusiana na ripoti hiyo.

      4. Yapange maelezo yako vizuri. Zipitie hoja zako ili uondoe mawazo ambayo

      yanaweza kuwa yamerudufishwa au yamerudiwa.

      5. Yaangalie mawazo yako ili kubainisha ni yapi ambayo yanapaswa kutangulia na yanafuatwa na yapi.

      6. Unapoandika ripoti yako hakikisha kuwa unaitumia lugha yako. Usiridhike tu na maneno unayoyapata wakati wa uchunguzi wako. Kuandika ripoti

      kwa lugha na maneno yako huonyesha kuwa umeielewa.

      7. Unaweza kuuboresha uwezo wako wa kuandika ripoti kwa kujitahidi kuyaelewa maelezo yanayohusika na kujitahidi kuyaeleza kivyako.

      8. Baada ya kuandika nakala ya kwanza ya ripoti unaweza kuiboresha kwa kupunguza mambo ambayo sio muhimu katika ripoti hiyo.

      9. Lugha inayotumiwa katika uandishi wa ripoti lazima izingatie wasomaji wa ripoti inayohusika. Kwa mfano, ikiwa wasomaji ni wanafunzi wa shule lugha yake haipaswi kuwa na ugumu au utata wa kisayansi.

      Zoezi la 11: Jadili mambo muhimu ambayo yanaweza kuzingatiwa katika maandalizi ya ripoti inayohusu kujitoa shuleni kwa wanafunzi. 

      28.5 Kusikiliza na kuzungumza: Majadiliano 

      Zoezi la 12: Fikiria kwamba unataka kuandika ripoti kuhusu sherehe ya ndoa uliyoishiriki kijijini kwenu. Fanya mazungumzo na wenzako ukilenga yale ambayo unataka kuyaripoti.

      28.6 Utungaji wa Ripoti

      Zoezi la 13: Tunga ripoti kuhusu mojawapo kati ya mada zifuatazo.

      • Ziara uliyoifanya.

      • Kongamano la lugha ya Kiswahili uliloshiriki.

      • Taarifa ya habari uliyoisikiliza au ulioiyosoma.

      • Mchezo wa mpira baina ya timu ya shule yenu na shule jirani.

      Muhtasari wa Mada

      Mada hii ya tano” Utungaji: insha za masimulizi au kubuni na uandishi wa ripoti” ina vipengele sita yaani masomo makuu sita yanayohusiana na mada husika. Kila somo lina vipengele vidogo kama vile: mchoro, kifungu cha habari, maswali ya ufahamu, matumizi ya msamiati, sarufi, matumizi ya lugha, kusikiliza na kuzungumza, kuandika, na maelezo muhimu. Somo la kwanza linaeleza maana ya insha. Somo la pili niaina za insha.Somo la tatu ni insha ya masimulizi. Somo la nne ni insha ya kubuni. Somo la tano linaeleza dhana ya ripoti na aina zake. Somo la sita ambalo ni la mwisho linahusu utunzi wa ripoti. Katika kila somo kuna kipengele cha sarufi ambacho kinagusia usemi wa asili na usemi wa taarifa.

      TATHMINI YA MADA YA TANO

      Andika insha ya masimulizi kuhusu mada zifuatazo.

      Siku ya kuadhimisha mwaka mpya.

      Safari yangu mjini Kigali.

      Utoto wangu.

      Likizo iliyopita.

      Umeteuliwa kuchunguza athari ya madawa ya kulevya na pombe haramu katika tarafa yako, andika ripoti yenye mapendekezo ya namna ya kupambana na tatizo hilo. Hakikisha umetumia mifano ya usemi halisi na usemi wa taarifa katika ripoti yako

      Geuza sentensi zifuatazo ziwe katika usemi wa taarifa au usemi halisi.

      Mwalimu alitushurutisha sote kwenda uwanjani kashangilia timu yetu.

       “Mtoto ni mtoto, awe wa kiume au wa kikeˮ Alisema Katibu mtendaji wa tarafa.

      “Faida, kwa nini leo umechelewa darasani?” Mwalimu aliuliza.

      Mkuu wa shule alitahadharisha wanafunzi kutoharibu mazingira.

       ‘‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’’ Mama alisema.

      Mwanafunzi alimwambia kwamba angefaulu katika somo la Kiswahili.

      ‘‘Mwezi ni gimba linalozunguka dunia na linang’ara usiku.’’ Mwalimu alituarifu.

      Katibu alitangaza kuwa kungekuwa na mkutano wa wanachama wote mwezi huo Jumanne ambayo ingefuata. 


      • Kitula G.K., (2014), Taaluma ya Uandishi, JKF, Nairobi

       Kitula G.K., (2010), Mazoezi na Marudio ya Kiswahili, Kenya Literature Bureau, Nairobi

       Mdee J.S, K. Njogu, Shafi (2012), Kamusi ya Karne ya 21, Longhorn Publishers, Nairobi

       Method S. A. et al., (2013), Johari ya Kiswahili. International print -o- Pac Limited Dar es salaam.

       Mlaga. W. K. (2017). Misingi ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Fasihi Karne ya 21. Heko Publishers Ltd. Dar es salaam

       Mlaga. W. K. (2017). Historia ya Kiswahili Nchini Rwanda: Kielelezo cha Nafasi ya Utashi wa Kisiasa katika Ustawi wa Lugha, Katika Jarida la Kioo cha Lugha., Juz. 15, kur. 1 – 17

       Mohamed, Mohamed A. (1996), Sarufi Mpya, Press And Publicity Centre, Dar es salaam

       Ndalu A. (1997), Mwangaza wa Kiswahili, Printpack, Nairobi.

       Niyirora E. & Ndayambaje L. (2012). Kiswahili Sanifu kwa Shule za sekondari, Tan Prints Publisher, New Delhi

       Niyomugabo C. (2013). Mafunzo ya Kiswahili, Fountain Publisher, Kampala

       Nkwera V. M.F. (1978) Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Dar-es-salaam: Tanzania Publishing House:

       Ntawiyanga S., na Jacqueline M. Kinya (2016), Kiswahili kwa Shule za Rwanda, Kidato cha 2. Longhorn Publishers, Nairobi.

       Ntawiyanga S., Muhamud A, Kinya J.M. na Sanja L (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda, Kidato cha 3. Longhorn Publishers, Dar es salaam.

       Nyangwine, J.A. Masebo Nyambari (2010), Kiswahili kidato cha 3&4, Nyambari Nyangwine Publishers, Dar es Salaam.

       REB (2015), Muhtasari wa Somo la Kiswahili, kidato cha 4-6, Mchepuo wa Lugha, Bodi ya Elimu Rwanda.

       REB (2016), Masomo ya Kiswahili Sanifu, Morani, Nairobi.

       REB (2016), Masomo ya Kiswahili Sanifu, Maorani, Nairobi.

       Salim K. Bakhressa, Islam K. Islam, Fuad A ali (2008), Kiswahili Sanifu, Oxford University Press, East Africa Ltd, Kigali.

       TUKI (1996), English-Kiswahili Dictionary, Mkuki na Nyota Publishers, Dar es salaam.

       TUKI (1996), Kamusi ya Kiswahili Toleo la pili, English Press Ltd, Nairobi.

       TUKI (2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la pili, Oxford University Press, Nairobi.

       TUKI (2013), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo laa 3, Oxford University Press, Dar es Salaam.

       Wamasati W.A, (-), Quick Fire Revision Kiswahili, Bookmania Stationers, Nairobi.

       Wamitila, K.W., (2011), Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi, Focus Books, Nairobi.

       Wamitila, K.W., (2009), Mwenge wa Uandishi Mbinu za Insha na Utunzi, Printwell Industries LTtd, Nairobi

       Wizara ya mafunzo ya Msingi na Sekondari (1987), Kitabu cha Kiswahili IV B, Taasisi ya Elimu ya Rwanda, Kigali.

       Wizara ya mafunzo ya Msingi na Sekondari (1987), Kitabu cha Kiswahili IV – VA, Taasisi ya Elimu ya Rwanda , Kigali.

       Wizara ya mafunzo ya Msingi na Sekondari (1987) Kitabu cha Kiswahili IV- VC,Taasisi ya Elimu ya Rwanda, Kigali.


       • KISWAHILI Kwa Shule za Rwanda Mchepuo wa Lugha Kidato cha 4

        Kiswahili kwa Shule za Rwanda, Michepuo Mingine, kidato cha 4, ni kitabu kinachokidhi haja ya ujifunzaji na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kulingana na mahitaji ya silabasi ya Somo la Kiswahili yenye kuegemea katika uwezo.

        Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha nyepesi ili kumwezesha mwanafunzi kupata maarifa, stadi na mwenendo mwema kupitia mada mbalimbali zilizojadiliwa. Msamiati uliotumiwa, miundo ya sentensi katika vifungu vya habari pamoja na mazoezi yaliyopendekezwa, yote yamezingatia kiwango cha mwanafunzi mlengwa wa somo hili la Kiswahili.

        Michoro ya kuvutia na ya kunasa akili ya mwanafunzi imetumiwa ili kurahisisha na kufanikisha ujifunzaji na ufundishaji wa somo hili.

        Masomo mbalimbali yaliyotolewa yamezingatia vipengele muhimu katika ujifunzaji na ufundishaji wa lugha ambavyo ni hivi vifuatavyo :
                  
               • Vifungu vya ufahamu na maswali ambata yenye kudhamiria kumjenga mwanafunzi katika uwezo wake wa kutafakari
                 na kugundua mambo mbalimbali yatendekayo katika jamii
               • Msamiati wa aina mbalimbali ambayo humsaidia kukuza na kuendeleza uwezo wake katika kuitumia lugha ya Kiswahili
               • Sarufi ambayo imejikita katika uchambuzi wa sentensi na minyambuliko wa vitenzi
               • Matumizi ya lugha yenye kumwezesha mwanafunzi kuitumia lugha ya Kiswahili kwa njia mwafaka
               • Utungaji ambao umelenga kumpa mwanafunzi uwezo wa kukuza stadi ya kimaandishi
               • Mazoezi mengine yenye kumwezesha kuendeleza uwezo wake katika kusoma, kusikiliza, kuzungumza na kuandika

        Kitabu hiki kina mwongozo ambao utamsaidia mwalimu kwa kumpa maelezo kamili kulingana na mbinu na mikakati muhimu ya kuzingatia katika ujifunzaji na ufundishaji wa kila somo, tangu maandalizi yake hati tathmni ya masomo yote yaliyopendekezwa katika kitabu hiki.