MADA 5:UTUNGAJI WA INSHA ZA MASIMULIZI
• Uwezo mahususi wa mada ndogo:
Kutunga insha fupifupi za masimulizi kwa kuzingatia kanuni za utungaji.
• Malengo ya ujifunzaji:
- Kutoa maana ya insha za masimulizi,
- Kuonyesha sifa za aya njema,
- Kutaja sehemu kuu za insha,
- Kutoa na kueleza aina mbalimbali za insha,
- Kutaja aina za alama za vituo,
- Kukusanya hoja kuhusu mada husika na kuzipanga kwa mfuatano mzuri,
- Kutunga insha za masimulizi kulingana na mada husika,
- Kutumia kwa usahihi alama za vituo katika uandishi wa insha za masimulizi,
- Kusimulia hadharani kiini cha insha iliyotungwa,
Kidokezo
SOMO LA 7: MAFANIKIO YA KUDUMU
7.1. Kusoma na ufahamu: Mafanikio ya kudumu
Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali uliyopewa hapo chini
Masengesho, kijana aliyezaliwa mwanapekee katika familia yake hakubahatika kulelewa na wazazi wake kwani walifariki angali mdogo akachukuliwa na kulelewa na shangazi yake ambapo alikuwa akisoma. Alipomaliza masomo yake katika shule za sekondari alipata cheti cha kuhitimu masomo hayo akiwa na alama nzuri. Jambo hili liliwafurahisha watu wengi wakiwemo walimu na majirani zake. Ndiyo maana ilikuwa tafrija ya kijiji kizima, tuliposherehekea siku ya kupata tuzo kwa kijana hodari ambaye aliyamudu maisha yake kiasi cha kuigwa na vijana wengine.
Wengi waliompongeza siku hiyo walimletea zawadi nyingi. Alikuwa mwanafunzi mwenye bidii tangu shule za chekechea hadi kiwango alichofikia. Muda mfupi baadaye, alijiunga na vijana wenzake kufuata masomo ya muda mfupi yaliyokuwa yakitolewa kijijini mwake. Masomo hayo yaliwalenga vijana wote waliokuwa wamemaliza masomo yao ya shule za sekondari na yalilenga kuwawezesha kuandaa miradi midogo midogo ya kujikimu, kujiendeleza na jinsi ya kuifanikisha miradi hiyo. Masomo hayo yaliwafurahisha vijana wengi na Masengesho aliyafuata kwa makini, jambo lililokuwa desturi kwake.
Masengesho alikuwa msichana mwenye mawazo na mtazamo imara wa maisha kiasi kwamba watu walishangaa kutokana na tabia na mienendo yake. Mafunzo yalifanyika kwa muda wa mwaka mzima akapewa cheti katika fani ya maandalizi na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo. Mwezi mmoja uliofuata Taasisi ya Maendeleo ya Rwanda ilihitaji kuajiri vijana waliokuwa wamemaliza masomo yao ili wasaidie katika kazi za ukalimani na upelekaji wa watalii kwenye vivutio vya utalii. Masengesho alipeleka ombi lake na baada ya muda mfupi akaitwa kwa mtihani na kuufaulu. Kazi ilipoanza aliifanya kwa bidii kiasi kwamba watalii wengi walifurahia huduma yake, wakampenda kwa uwezo wake wa kuzungumza lugha tofauti na bidii aliyoonesha kazini.
Alifungua akaunti kwenye benki moja na kuanza kuhifadhi sehemu ya mshahara wake. Alipoona akaunti yake imekuwa na pesa za kutosha, aliamua kuomba mkopo ili aweze kuzalisha mali shamba lake kubwa ambalo mpaka wakati huo lilikuwa halijatumiwa vizuri. Aliandaa vizuri mradi wa kilimo na ufugaji, akajenga vibanda vya mifugo yake, akawaajiri baadhi ya vijana waliokuwa pamoja katika mafunzo ya muda ule mfupi, kila mmoja akapewa jukumu lake. Pamoja na kazi yake ya ukalimani, Masengesho alifuata vizuri mradi wake akanunua vifaa vilivyohitajika. Mwaka mmoja baadaye, alikuwa ameishapata mali nyingi na kuanza kujulikana kote nchini kwa uwezo wake wa kufanya mambo mengi kwa muda mfupi na kwa ukamilifu.
Serikali ya Rwanda ilipotoa tuzo kwa watu waliochangia kubadilisha maisha ya watu wengine, Masengesho alikuwa miongoni mwa watu waliochangia kuyaboresha maisha ya majirani zao. Kila mtu katika kijiji chetu aliitikia mwaliko wake na wengi tulikuwa tunajivunia kuwa na kijana mwerevu kama yeye. Kwa sasa ameanza kuendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Rwanda ambapo anatarajia kupata Shahada yake ya kwanza katika uwanja wa Ukalimani. Masengesho amekuwa mfano mzuri kwa vijana wengine wengi ambao wanapoyakumbuka maisha yake, huyaamini yaliyosemwa na wahenga kwamba “Mchumia juani hulia kivulini” na kamba “Mvumilivu hula mbivu”. Wema kwa kila mtu, utulivu na upendo ni baadhi ya sifa zinazomtambulisha kijana huyu ambaye amewashangaza wengi wanaofahamu alipotoka.
Kazi ya 1
Maswali ya ufahamu
1. Eleza hali ya maisha ya Masengesho alipokuwa mtoto mdogo.
2. Kwa nini Masengesho alipewa zawadi nyingi baada ya kumaliza masomo yake ya shule za sekondari?
3. Masomo ya muda mfupi aliyoyafuata yalihusu nini?
4. Kwa nini Masengesho alipewa tuzo?
5. Umepata funzo gani kutokana na kifungu hiki?
6. Kulingana na kifungu hiki, eleza maana ya methali hizi:
a. Mvumilivu hula mbivu.
b. Mchumia juani hulia kuvulini.
7.2. Msamiati kuhusu kifungu cha habari
Kazi ya 2
Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo. Chunguza matumizi yake katika kifungu cha habari hapo juu.
1. Mafanikio
2. Akaunti
3. Tafrija
4. Mradi
5. Kukata tamaa
Kazi ya 3
Husisha maneno kutoka sehemu A na maana yake katika sehemu B
7.3. Sarufi kuhusu matumizi ya alama za vituo
Kazi ya 4
Angalia sentensi ambazo zinafuata na kujadili na mwenzako unavyoziona:
1. Ehee! Kumbe yeye ni mwizi!
2. Mwalimu wa mitaala wa shule yetu ni mtu mpole kabisa.
3. Ninaenda sokoni kununua vitu vingi: kuku, maembe, mapapai, machungwa, madaftari, na kalamu.
4. Nyinyi mnaona vipi siku za leo?
5. Masomo haya si ya kukuangamiza; masomo haya ni ya kuboresha hali ya maisha yako.
Ndani ya sentenzi hizi kuna matumizi ya alama za vituo mbalimbali kulingana na maumbile ya kila sentensi. Kuna alama ya kushangaa, alama ya nukta au kituo, alama ya nuktambili au koloni, alama ya mkato wa chini au koma, alama ya kuuliza au kiulizi au ulizo pamoja na alama ya nukta na mkato au semikoloni
Maelezo muhimu
ALAMA ZA UANDISHI (ALAMA ZA UAKIFISHAJI) NA MATUMIZI YAKE
Kuandika ni tofauti na kuzungumza, katika maandishi ili yaweze kusomeka na kueleweka vizuri ni muhimu sana kuzingatia uakifishaji (matumizi ya alama za vituo). Sasa kabla hatujashika kalamu na kuanza kuandika insha zetu, ni vyema tukazijua alama hizi na jinsi zinavyotumika.
1. Matumizi ya nukta (.): Nukta au kituo kikuu hutumika kama ifuatavyo:
Kuonyesha mwisho wa sentensi.
Kwa mfano:
- Mtoto amelala.
- Jua limechomoza mapema.
- Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
Katika kufupisha maneno.
Kwa mfano:
- S.L.P.
- Dkt. Mukeshimana
- n.k.
Kuonyesha saa.
Kwa mfano: Sasa nii saa 8.00
Katika hesabu kuonyesha desimali.
Kwa mfano: Nimepata alama 40.5
2. Matumizi ya mkato au koma (,): Mkato au koma hutumika kama ifuatavyo:
Kuonyesha orodha ya vitu.
Kwa mfano: Usisahau kununua mkate, soda, kitumbua na chapati.
Kugawanya mawazo katika sentensi.
Kwa mfano: Baada ya kusikiliza kesi yake, hakimu alimhukumu kifungo chamiaka 10 jela.
3. Matumizi ya alama za mtajo (vinukuu) (‘) na (“): Alama za mtajo hutumika kwa:Kunukuu usemi halisi.
Kwa mfano: “Ukiniletea zawadi nitakupenda sana,” Mugenga alimwambia Ndayizigiye.
Kuonyesha maneno yasiyo ya Kiswahili unapochanganya ndimi katika sentensi.
Kwa mfano: Huyu ndiye mchezaji “number one.”
4. Alama ya kuuliza (kiulizi/ ulizo) (?): Kiulizi hutumika:Kuulizia swali.
Kwa mfano: Ulikuwa wapi muda wote huo?
5. Alama ya hisi (mshangao) (!): Matumizi ya alama ya hisi ni:
Kuonyesha hisia k.v mshangao, hasira, furaha, n.k.
Kwa mfano: Hoyeeeee!
Haiwezekani!
Kuigiza tanakali za sauti.
Kwa mfano: Maji yalimwagika mwaaaa!
6. Matumizi ya nukta-mkato/ semi-koloni (;): Nukta-mkato hutumika:
Kuorodhesha vitu au mawazo hasa ikiwa yana maneno zaidi ya moja.
Kwa mfano: Maria alinituma nimpelekee kitabu cha kufundishia Kiswahili kwa
Wageni; madaftari mawili makubwa; baiskeli ndogo za watoto na vikombe vinne.
Kuunganishia vishazi huru viwili.
Kwa mfano: Tuliandamana kwa moyo wa kizalendo; tukapata haki yetu.
7. Matumizi ya nuktambili (nukta pacha/ koloni) (: Nuktambili hutumika:
Kuonyesha mwanzo wa orodha.
Kwa mfano: Ukifika sokoni nunua vitu vifuatavyo: maembe 2, sukari kilo 1, unga wa ngano kilo 6, vitunguu kilo 1, mafuta ya kupikia lita 10 na unga wa mahindi mfuko mmoja.
Kunukuu ukurasa wa Bibilia.
Kwa mfano: Yohana kutoka 20:4 Biblia inasema….
Kuonyesha msemaji katika tamthilia au mchezo wa kuigiza.
Kwa mfano: Mkulima: Nyinyi walanguzi mnatukandamiza sana.
Mlanguzi: Viwanda hakuna, sasa unadhani sisi tutauza kwa faranga ngapi?
Hatuwakandamizi, serikali yenu ndiyo inayowakandamiza.
8. Matumizi ya kistari kifupi (-): Kistari kifupi hutumika:
Kuunganisha maneno mawili.
Kwa mfano: Mfa-maji
Mwana-harakati
Kuonyesha hadi, au mpaka.
Kwa mfano: Umeme umepanda kutoka elfu 20 – 60 kwa mwezi.
9. Alama za mabano ya mduara/ parandesi : Mabano hutumika:
Kutoa maelezo zaidi.
Kwa mfano: Wanafunzi wote (wasichana na wavulana) wanaweza kujua Kiswahili.
Kufungia herufi za kuorodheshwa.
Kwa mfano:
a. huelimisha
b. huburudisha
c. huonya
10. Mkwaju (/): Hutumiwa kuonyesha kuwa kitu mojawapo ya vitu vilivyotajwa chaweza kutumiwa badala ya vingine.
Kwa mfano: Uwayo alikaa kimya/ alitulia.
7.4. Matumizi ya lugha
Kazi ya 5
Weka alama za vituo katika dondoo la insha ambayo inafuata ili iwe na maana
Hmm Unataka nikuambie sifa za mtu ninayempenda Bila shaka ninampenda sana baba Baba yangu anaitwa John Mugabo Yeye ni mrefu na mweupe Baba ana macho mazuri na nywele nyingi nyeusi kichwani Yeye hupenda kuvaa mavazi tofauti suti kanzu mashati meupe na suruali nyeusi kila wakati isipokuwa Jumamosi tunapoenda kucheza kandanda naye Baba ni mchezaji hodari sana katika kandanda na yeye hufurahia sana mchezo huu Baba yangu ni mwalimu mkuu katika shule ya sekondari ya Kigali Anaheshimiwa sana na walimu wote wanafunzi na hata wazazi Sifa zake nzuri ndizo zimfanyazo baba apendwe na kila mtu.
Kazi ya 6
Soma kuhusu sehemu za insha ya masimulizi kisha ujibu maswali:
Insha ya masimulizi huwa na kichwa cha habari cha insha ambacho ni maneno machache, takribani matano, ambayo ndiyo jina la insha. Kichwa cha habari huandikwa juu, katikati kwenye ukurasa wa kwanza wa insha. Mara nyingi, huandikwa kwa herufi kubwa na hubeba wazo kuu la insha. Insha ya masimulizi huwa na utangulizi ambao ni sehemu ya mwanzo yenye urefu usiozidi aya moja. Utangulizi hudondoa kwa ufupi kabisa kile kinachoelezwa kwenye insha.
Kiini cha insha ya masimulizi ni sehemu tunayoweza kusema kwamba ni insha yenyewe. Kwenye kiini ndipo ufafanuzi wote hutolewa. Ufafanuzi huu hupangwa katika aya moja au zaidi. Hapa ndipo mwandishi hubainisha mawazo yake, huthibitisha, hushawishi, huhimiza na hufafanua. Baada ya kiini huja hitimisho, yaani sehemu ya mwisho wa insha ya masimulizi ambayo haizidi aya moja. Katika sehemu hii, mwandishi anaweza kurejelea kwa ufupi sana yale aliyoyazungumzia katika insha yake. Anaweza kuonyesha msimamo wake, anaweza kutoa mapendekezo, au kuwahimiza walengwa wake kuchukua hatua fulani.
Katika kuandika insha ya masimulizi, mwandishi atazingatia mambo haya: atabaini ni mada gani ya kuandikia na kuielewa vema; atapanga mawazo katika mtiririko wenye mantiki, atatumia mtindo unaoendana na kusudi la insha ya masimulizi. Kwa mfano, mtindo wa masimulizi unafaa kwa hadithi au insha nyingine za kisanaa. Atatumia lugha fasaha na inayoeleweka, atafuata kanuni za uandishi, kwa mfano matumizi ya alama za uandishi, aya, herufi kubwa na herufi ndogo. Mwandishi atapanga insha katika msuko au muundo wake, yaani kichwa, utangulizi, kiini na hitimisho
Maswali:
1. Kwa sababu gani utangulizi mzuri ni muhimu katika insha?
2. Jadili sehemu kuu za insha.
3. Jadili mambo ya kuzingatia katika uandishi wa insha.
7.5. Kusikiliza na kuzungumza
Kazi ya 7
Sikiliza mkufunzi anavyosoma maelezo kuhusu aina za insha, soma maelezo kwa kumwiga mkufunzi na kujibu maswali yanayofuata.
Insha ni za aina nyingi kulingana na namna zilivyoandikwa au kusudi lake. Katika utungaji wa insha kuna insha za masimulizi, insha za wasifu, insha za picha, insha za mdokezo, insha za methali, insha za hoja na insha za kubuni. Insha za masimulizi ni aina ya insha ambazo ndani yake mwandishi anasimulia au anaeleza tukio fulani maalum la kweli kwa njia ya kisanaa, ambapo insha za wasifu ni aina za insha ambazo hueleza sifa za mtu, kitu au jambo fulani. Insha za aina hii husimulia sifa, maisha au maelezo mengine muhimu kuhusu mtu fulani, kitu fulani au jambo fulani. Ni kusema kuwa katika aina hizi za insha mwandishi anaandika kuhusu uzuri au ubaya wa mtu, kitu au jambo fulani.
Insha za picha hueleza picha iliyotolewa. Ni kusema kwamba mwandishi hueleza mambo anayoyaona kwenye picha au mchoro. Analazimika kufanya andiko lenye mfuatano wa mawazo kulingana na mfuatano wa picha au michoro aliyopewa. Insha za mdokezo ni zile ambazo mwandishi hupewa mwongozo wa kufuatilia katika utunzi wake. Kwa mfano, mwandishi anaweza kupewa orodha ya hoja kadhaa kutokana na kichwa kilichotolewa akajenga insha. Vilevile anaweza kupewa utangulizi au kimalizio cha insha na kuagizwa aendelee na insha au aanze insha aliyopewa.
Insha ya methali ni insha ambayo mada yake huwa ni methali ambayo mwandishi anapaswa kujadilia. Katika uandishi wa insha ya aina hii, mwandishi ni lazima atoe hoja kwa kukubaliana na methali iliyotolewa. Insha za hoja ni insha ambazo mwandishi analazimishwa kutoa hoja zinazotetea mada na nyingine zinazopinga mada. Mwishoni mwa insha hii, mwandishi anaonesha msimamo wake kulingana na mada iliyotolewa. Kwa kumaliza, insha za kubuni ni zile ambazo hutungwa kuhusu mawazo yanayozuliwa na ambayo si matukio ya kawaida. Ni kusema kwamba mwandishi hubuni mandhari, wahusika, matukio, na kadhalika.
Maswali
1. Taja aina za insha.
2. Kifungu ulichokisoma ni aina gani ya insha? Kwa sababu gani?
3. Ni nini tofauti iliyoko baina ya insha ya wasifu na insha ya masimulizi.
4. Kwa sababu gani mara zote mwandishi wa insha ya methali hulazimishwa kutetea methali aliyopewa?
7.6. Kuandika kuhusu utungaji wa insha ya masimulizi
Kazi ya 8
Soma maelezo muhimu hapo chini kisha uandike insha ya masimulizi kuhusu mada ifuatayo kwa kufuata uandishi mzuri wa aya na hata wa insha yenyewe.
Mada: Rafiki yako anayesoma katika kidato cha tano amefukuzwa shuleni kwa sababu anatumia dawa za kulevya na kushiriki ulevi. Simulia kilichoendelea.
Maelezo muhimu
Aya katika uandishi wa insha: Aya ni fungu au mkusanyiko wa sentensi ambazo zinazungumzia wazo moja kuu. Zifuatazo ni namna za kuandika aya nzuri, sifa za aya nzuri na mbinu za kuelekeza uandishi na upangaji wa aya.
1. Ujongezaji wa maandishi: Hii ndiyo sifa ya kwanza inayobainisha kuwepo kwa aya katika maandishi. Ni nafasi ya msitari mmoja au miwili inayoachwa kati ya aya moja na aya nyingine. Neno la kwanza la aya linaweza pia kusukumwa mbele kidogo kabla ya kuanza aya kama ishara ya aya mpya katika maandishi.
2. Matumizi ya sentensi-mada: Hii ni sentensi kuu inayomwelekeza msomaji juu ya kile kitakachozungumziwa katika aya husika. Mara nyingi sentensi hii huwa ya kwanza katika aya na maneno yanayofuata yakiwa yanazunguka au yanaeleza yale yaliyotangulizwa katika sentensi mada hiyo.
3. Aya huhusika kuwa na dhamira kuu: Kila aya huwa na wazo kuu moja inalozungumzia. Hairuhusiwi kuzungumzia dhamira mbili tofauti katika aya moja
4. Muundo wa kimantiki: Aya inapaswa kuwa na mantiki; yaani hoja zilizomo katika aya moja zinapaswa kuwa na mantiki kiasi kwamba hakuna jambo lililomo katika aya lisiloendana na kile kilichokusudiwa na mwandishi wa aya.
5. Aya kuwa na sifa ya ubayana: Ni lazima kila aya iweze kuwa inajieleza kwa msomaji, maana yake haipaswi kuwa tatanishi.
6. Muwala na ushikamanifu: Aya inapaswa kuwa na ushikamanifu au upatanifu wa kimuundo. Kila hoja inapaswa kuwa kiendelezo na mjazo wa ile iliyoitangulia.
7. Maneno ya mpishano: Haya ni maneno yanayosukuma aya ya chini na kuihusisha na aya ya juu ili kuleta umoja katika hoja za aya zinazokaribiana. Maneno haya ni kama viunganishi ama maneno mengine ya upatanishi wa kisarufi.
Tathmini ya mada ya tano
1. Nini maana ya insha za masimulizi?
2. Sehemu za insha ya masimulizi ni zipi?
3. Taja aina za insha.
4. Weka alama za vituo kwenye sentensi zifuatazo:
a. Afanalek Kumbe nimesahau kuwa leo ni siku yangu ya kuzaliwa
b. Wanafunzi wa kidato cha tano wanakosa miaka mingapi kumalizia shule za upili
c. Nipelekee kwenye ofisi yangu vyombo vifuatavyo kalamu karatasi meza viti deski na makabati
d. Mwalimu alisema Fanyeni kazi hii katika dakika arobaini tu
e. Watu wote wanaume na wanawake watashiriki katika mkutano wa kijiji chetu
5. Tunga insha ya masimulizi yenye matumizi ya alama za vituo sahihi kuhusu shule yako. Usizidi ukurasa mmoja.
Marejeo
1. Bakhressa, S.K na Wenzake (2008). Kiswahili Fasaha. Kitabu cha Mwanafunzi. Kidato cha Tatu. Oxford University Press, East Africa Ltd, Nairobi, Kenya.
2. TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la Pili. Oxford University Press.
3. Bakhressa, S.K na Wenzake (2008). Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi. Darasa la Saba. Oxford University Press, East Africa Ltd, Elgon Road, Upper Hill, Nairobi, Kenya.
4. Nkwera, F.M.V. (1978). Sarufi na Fasihi Sekondari na Vyuo. Tanzania Publishing House, Dar Es Salaam.
5. HARERIMANA, F. (2017). Tujivunie Lugha Yetu. Kitabu cha Mwanafunzi, Kidato cha 5. MK Publishers (R) Ltd. Kigali, Rwanda.
6. Ndalu, A. E. (2016). Masomo ya Kiswahili Sanifu. Kitabu cha Mwanafunzi. Kidato cha 2. Moran (E.A) Publishers Limited.
7. Ntawiyanga, S. (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo wa Lugha, Kidato cha 5. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
8. Kenya Literature Bureau (2006). Kiswahili kwa Darasa la Nane. Kitabu cha Wanafunzi. Kenya Literature Bureau, Nairobi, Kenya.
9. Ntawiyanga, S. na Wenzake (2017). Kiswahili kwa Shule za Rwanda. Mchepuo wa Lugha, Kidato cha 6. Longhorn Publishers (Rwanda) Limited. Kigali, Rwanda.
10. Niyirora, E. & Ndayambaje, L. (2012). Kiswahili Sanifu kwa Shule za Sekondari. Kitabu cha Mwanafunzi Kidato cha Tano. Tan Prints (India) Pvt. Ltd.