• MADA 4:MIJADALA

    Kidokezo

    ok

    SOMO LA 5: MAANA YA MJADALA

    5.1. Kusoma na ufahamu: Maana ya mjadala

    Soma kifungu kuhusu “Maana ya mjadala” ili ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini

    Kuna mazungumzo ambayo hufanywa kuhusu suala fulani linalohitaji kujadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi. Mazungumzo ya aina hii ndiyo hujulikana kwa jina la mijadala. Kwa kawaida, mjadala ni mazungumzo juu ya jambo maalum ambayo hufanywa na watu kwa kutoa hoja zao kwa jambo fulani linalotakiwa ufafanuzi au ufumbuzi wa suala lililopo.

    Mjadala ni aina ya majadiliano ambayo huhusisha watu wengi wanaotoa hoja kuhusu mada fulani. Miongoni mwa watu wanaohusika katika mjadala huwa kuna kiongozi ambaye jukumu lake ni kuongoza majadiliano kwa kupanga muda wa kuzungumza kwa kila msemaji anayeshiriki katika mazungumzo hayo. Katika mjadala, hakuna msemaji ambaye anaruhusiwa kutoa hoja bila kumuomba fursa kiongozi wa majadiliano.

    Mjadala huwa na mada ambayo humulika hoja zote zinazotolewa wakati wa mazungumzo. Kama kuna wasemaji ambao wanataka kukiuka mada katika hoja zao, kiongozi wa mjadala huwarekebisha kwa kuwakumbusha mada inayotolewa hoja.

    Mjadala huwa na malengo ya kukuza uwezo wa kitaaluma na hali ya udadisi kwa washiriki wa majadiliano. Mjadala hukuza uwezo wa kushawishi watu hadharani ili wakubaliane na mawazo ya msemaji kuhusu jambo fulani. Aidha humwezesha mtu kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri wakati anapoandika insha au habari. Mjadala pia humsaidia mtu kutambua kipaji alicho nacho cha kuzungumza bila aibu mbele ya hadhira na kukuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kutumia msamiati na matamshi bora ya lugha. Humzoeza pia mtu kusikiliza maoni ya watu wengine, kupinga au kutetea maoni na hoja zao. Jambo muhimu ni kwamba majadiliano haya humpa fursa ya kuelewana na watu anaotofautina nao kimawazo.

    Wazungumzaji wanapofanya mjadala hukuza uwezo wao wa mazungumzo kuhusu suala fulani na hupanua kiwango chao cha msamiati na hupunguza woga wa kuongea hadharani. Isitoshe, mjadala hutumiwa kama nyenzo bora ya kutatua migogoro inayoweza kuzuka miongoni mwa wanajamii. Katika mjadala, watu wenye mawazo yaliyo kinyume na mada, hupata nafasi ya kujadiliana juu ya jambo fulani kwa madhumuni ya kutatua tatizo linalowakumba. Mjadala hutumiwa kwa kutatua tatizo na kuondoa migogoro miongoni mwa watu kwa njia ya amani.

    Katika mjadala, kama tulivyokwisha kusema, kunajitokeza wahusika ambao ni kiongozi wa mjadala na hadhira. Kiongozi ndiye ambaye ana jukumu la kuongoza mjadala. Kiongozi anaweza kuwa mtu mmoja au wawili kulingana na mada iliyochaguliwa au malengo ya majadiliano yenyewe. Ukichaguliwa kama kiongozi ni lazima uongoze mjadala ipasavyo na usikose kumpangia kila 51 msemaji muda atakaotumia ili waweze kuchangia mawazo yake.

    Kwa upande wa mjadala, kiongozi humruhusu yeyote atakaye kutoa mchango kwani hakuna makundi ya watetezi na wapinzani wa mjadala. Kiongozi huyu huwa na majukumu tofauti kwani ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa.

    Katika mjadala, kuna hadhira pia ambayo hushiriki katika mazungumzo kwa kusikiliza na kutoa mchango wao kuhusu suala linalojadiliwa. Kila mtu aliye na hoja hunyosha mkono kuomba fursa ya kuzungumza. Lengo la kwanza la kila msemaji katika mjadala si kupata ushindi, kwani si mashindano bali lengo la kila msemaji ni kutoa mawazo kwa nia ya kutatua tatizo fulani linalofafanuliwa na kujadiliwa kwa pamoja. Hivyo, katika mjadala hakuna kushindania ushindi; kila mtu ambaye ana la kusema huruhusiwa na hutoa hoja kama apendavyo kuhusu mada ile inayohusika bila kukiuka taratibu zilizowekwa.

    Watu wanaoshiriki katika mijadala huhakikisha kuwa mjadala ni njia ya kukuza uwezo wa kufikiri na kutafuta masuluhisho kwa masuala yanayoikumba jamii fulani. Katika mazungumzo haya, kiongozi ndiye anayeongoza majadiliano ili wazungumzaji watoe mchango wao kuhusu suala lililopo. Kiongozi humpa fursa mzungumzaji kwa kusema, “Simama utoe mchango wako.” Mzungumzaji huweza kutoa hoja zake kulingana na anavyofikiria kuhusu suala husika. Mara nyingi, mjadala huweza kufanyika katika makundi madogo madogo au makubwa. Kiongozi hubainisha mada ya mjadala na kuhakikisha kuwa wakati wote wa mjadala kuna mwenendo mwema unaowaongoza washiriki wa mjadala husika.

    Mzungumzaji katika mjadala ni lazima awe na uwezo wa kupanga mawazo yake kwa mfuatano bora wenye mantiki. Mjadala hutumiwa kama nyenzo bora ya kutatua migogoro inayoweza kuzuka miongoni mwa wanajamii. Katika mjadala, watu wenye mawazo yaliyo kinyume na mada, hupata nafasi ya kujadiliana juu ya jambo fulani kwa madhumuni ya kutatua tatizo linalowakumba au kuikumba jamii nzima. Mjadala hutumiwa kwa kutatua tatizo na kuondoa migogoro miongoni mwa watu kwa njia ya amani.

    Kwa upande wa mjadala, kiongozi humruhusu yeyote atakaye kutoa mchango kwani hakuna makundi ya watetezi na wapinzani wa mjadala. Kiongozi huyu huwa na majukumu tofauti kwani ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa.

    Mzungumzaji katika mjadala ni lazima awe na uwezo wa kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri. Yeye anakuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kuwa anaweza kuutumia msamiati na kujizoeza kutumia matamshi mazuri ya lugha.

    Jambo muhimu pia katika mijadala inayofanywa ni kwamba mazungumzo yanayofanywa huwazoeza wengi kusikiliza na kupima maoni na hoja za wenzao, kuelewana na wengine kutoka sehemu mbalimbali, kuheshimiana kulingana na mawazo tofauti yanayotolewa na kila mzungumzaji. Kwa hiyo, mjadala ni 5252 zoezi zuri kwa yeyote anayetaka kukuza uwezo wa mawasiliano, majadiliano, mahojiano, ujuzi wa kutoa maoni yake na kujitambua katika jamii yake.

    Mwisho, mjadala ni mazungumzo yanayoendeshwa na kushirikisha watu tofauti kwa kukidhi haja na malengo yanayotofautiana na kuingiliana kwa upande mwingine. Ni lazima kuelewa kuwa mjadala ni wenzo timamu wa kuimarisha stadi ya maongezi kuhusu mada fulani.

    Kazi ya 1

    Maswali ya ufahamu

    1. Eleza kwa ufupi maana ya mjadala.

    2. Ni zipi kazi za kiongozi wa mjadala ? 

    3. kwa sababu gani katika mjadala hakuna mshindi?

    5.2. Msamiati kuhusu Maana ya mjadala

    Kazi ya 2

    Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo:

    1. Suala

    2. Hadhira 

    3. Kiongozi

    4. Majadilano

    5. Migogoro

    6. Jukumu

    Kazi ya 3

    Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia maneno yanayofaa kati ya haya yafuatayo: kuwashirikisha, mjadala, kupanga, mazungumzo, hoja, kiongozi, mada, kipaji, mahojiano, hadhira.

    1. Mjadala humsaidia mtu kutambua …………alicho nacho cha kuzungumza bila woga mbele ya wengine.

    2. Aliyechaguliwa kuongoza majadiliano kwa kupanga muda wa kuzungumza kwa kila msemaji huitwa ………………..

    3. …………… ni jumla ya wasikilizaji, watazamaji au wasomaji wa kazi maalumu ya kifasihi. 

    4. Katika mazungumzo lazima …………………mawazo kwa mfuatano mzuri.

    5. Uulizaji maswali ili kufahamu maarifa anayoyajua mtu hujulikana kama ………………..

    6. ………………… unahitajika kwa wanaohitaji ufafanuzi zaidi. 

    7. Mjadala huchukuliwa kama …………………………juu ya jambo maalumu.

    8. Watu wengi wanapojadiliana kuhusu mada fulani hutoa …………..ambazo husaidia wengine kuelewa ukweli fulani. 

    9. Mtu yeyote aliyehudhuria mkutano alipewa …………………ya kufanya jambo fulani.

    10. Mwalimu anaweza ……………………..wanafunzi katika uchaguzi wa mada.

    5.3. Sarufi: Matumizi ya viambishi rejeshi kulingana na ngeli za majina

    Soma na uchunguze sentensi zifuatazo: 

    Anavyokula ananitamanisha.

    Anamolala

    Anayecheka (umoja) wanaocheka (wingi)


    Maelezo muhimu

    Kiambishi ni kipande cha neno chenye maana ya kisarufi ambacho kinapachikwa kwa mfano kabla au baada ya mzizi wa neno katika vitenzi na kuwakilisha dhana fulani.

    -O- rejeshi hujitokeza katika shina amba-. Shina hili huongezewa viambihi vya 

    -o- rejeshi na kupata neno lionyeshalo urejeshi. Hapa tunapata maneno kama ambalo, ambaye, ambacho, ambazo, ambavyo, n.k. Haya ndiyo mazingira ya utokeaji wa -o- rejeshi. Zifuatazo ni dhima tano za -o- rejeshi:

    1. Huunganisha tungo mbili zenye dhana moja.

    Mfano:

    a. Mwalimu amefundisha.

    b. Mwalimu amehama.

    Jibu = Mwalimu ambaye amefundisha amehama.

    Kutokana na tungo hizi mbili tunaweza kupata tungo moja: Mwalimu ambaye amefundisha amehama

    2. Hudokeza idadi (umoja na wingi). Mfano: Anayecheka (umoja), wanaocheka (wingi).

    3. Kuonyesha mahali ambapo tendo hutendeka. Mfano: “Anamolala” (ndani)

    4. Huonyesha nafsi ya mtenda au mtendwa wa jambo. Mfano: Aliyeiba(umoja ) Walioiba (nafsi ya III wingi).

    Kazi ya 3

    Jaza nafasi. Tumia ‘o’ rejeshi iliyo mwafaka

    Kwa mfano :Wageni wasafirio wameondoka na mizigo yao. 

    1. Viatu viuzwa ------------- ni mitumba. 

    2. Safari ziandaliwa------------------zinatufurahisha. 

    3. Wateja wanunua-----------------wana pesa kama mchanga. 

    4. Mikate iokwa-------------itamalizwa yote.

    5. Watalii wafika------- hawatamani kuondoka. 

    6. Miche ipaliliwa-------- itanawiri vizuri.

    5.4. Matumizi ya lugha kuhusu ‘‘Maana ya mjadala ’’

    Kazi ya 4

    Soma maelezo yanayofuata ili kujibu maswali hapo chini

    • “Maana ya mjadala”

    ▫ Mjadala ni mazugumzo juu ya jambo fulani. Unaweza kufanyika katika makundi madogo madogo au makubwa. 

    ▫ Mjadala unaongozwa na mtu mmoja au watu wawili ambao wanazusha mawazo na kuhakikisha ikiwa kuna mwenendo mwema kati ya washiriki wa mjadala huo. 

    ▫ Kiongozi wa mjadala ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa. Mada zinazojadiliwa katika mjadala ni zile ambazo zinahitaji ufafanuzi kutokana na mchango wa mawazo ya wengi. 

    ▫ Anayetoa hoja yake, anaweza kuunga mkono maoni ya mwenzake au kuyapinga kwa minajili ya kutoa mchango wake wa kutatua tatizo linalojadiliwa.

    ▫ Katika mjadala mada hutolewa mawazo na ndiyo inamulikia mjadala. Kiongozi wa mjadala hulazimika kuwasaidia wasemaji kutokiuka mada.

    ▫ Mjadala huwa na malengo yafuatayo:

    - Kukuza uwezo wa kitaaluma na hali ya udadisi kwa washiriki wa mjadala.

    - Kukuza uwezo wa kushawishi watu hadharani ili wakubaliane na mawazo ya msemaji kuhusu jambo fulani.

    - Kumwezesha mtu kupanga mawazo yake kwa mfuatano mzuri wakati anapoandika insha au habari.

    - Kumwezesha mtu kutambua kipaji alicho nacho cha kuzungumza bila aibu mbele ya hadhira.

    - Kukuza stadi ya utumiaji wa lugha kwa kutumia msamiati na matamshi bora ya lugha.

    - Kumzoeza mtu kusikiliza na kupinga au kutetea maoni na hoja za wengine.

    - Kuwapa watu wasaa wa kuelewana na wengine kutoka maeneo mbalimbali.

    ▫ Wahusika katika mjadala ni kiongozi na hadhira.

    ▫ Katika mjadala kila yeyote anayetaka kutoa hoja anaruhusiwa na kiongozi kutoa hoja yake apendavyo

    ▫ Katika mjadala hakuna washindi, kiongozi anatoa suluhisho kutokana na mawazo yaliyotolewa. Mjadala si mashindano wala malumbano.


    Maswali:

    1. Mjadala unaweza kuongozwa na watu watano. Ni kweli au si kweli? Eleza.

    2. Ni ipi kazi ya kiongozi katika mjadala?

    3. Jadili malengo matatu ya mjadala mzuri.

    4. Kwa sababu gani katika mjadala hakuna mshindi? 

    5. Jadili wahusika katika mjadala.

    5.5. Kusikiliza na Kuzungumza

    Kazi ya 5

    Jadili mada ifuatayo: “Maendeleo nchini huyafanya maisha ya Wanyarwanda yabadilike kwa kiwango cha juu.”


    5.6. Kuandika

    Kazi ya 6

    Andika mjadala kuhusu mada “Ubaya wa dawa za kulevya katika maisha ya binadamu.” Usizidi kurasa mbili.


    SOMO LA 6: MAANDALIZI NA UTEKELEZAJI WA MJADALA

    Kazi ya 1

    Jibu maswali yafuatayo:

    a. Mjadala ni nini?

    b. Taja watu wanaoshiriki katika mjadala.

    c. Unafikiri kuwa majukumu ya watu hao ni yapi?


    6.1. Kusoma na ufuhamu: “Mchango wa wazazi katika malezi ya watoto wao”

    Soma kifungu hiki kisha ujibu maswali ya ufahamu

    Kiongozi: Waheshimiwa mabibi na mabwana mliokusanyika hapa, kwanza ninataka niwakaribishe katika mjadala huu. Kama mnavyotuona hapa mbele yenu, mimi ninayewakaribisha ni kiongozi wa mjadala huu. Pembeni pangu mnayemwona ni kiongozi msaidizi. Mada ya mjadala wetu wa leo ni kama mnavyoisoma mbele yenu “MCHANGO WA WAZAZI KATIKA MALEZI YA WATOTO WAO.” Karibuni sana nyote na bila kupoteza muda, ningetaka kumkaribisha mshiriki aliye tayari atoe mchango wake.

    Mshiriki wa kwanza: Ninawashukuru sana viongozi na wasikilizaji washiriki wenzangu. Ni kweli kabisa wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao. Kama inavyojulikana malezi ya kwanza kwa mtoto huanzia nyumbani. Nyumbani ndipo mtoto anapopata malezi ya msingi ambayo humulikia maisha yake. Malezi haya ya kwanza yapatikanayo nyumbani humsaidia mtoto kufanikiwa katika maisha yake. Malezi haya yanatolewa na wazazi ambao ndio walezi muhimu wa watoto wao. Bila mchango wa wazazi, watoto hawawezi kupata elimu. Kwa hiyo, wazazi wana jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao. Ahsanteni kwa kunitega sikio.

    Kiongozi: Asante sana kwa hoja yako. Kama mlivyosikia, msemaji huyu ameeleza kwamba wazazi ndio wanaowapatia watoto wao malezi ya msingi ambayo yanawasaidia kufanikiwa maishani mwao. Tafadhalini, naomba mjaribu kutoa maoni mengine kuhusu suala hilo. Karibu bibi!

    Mshiriki wa pili: Asante sana kiongozi kwa fursa hii ya kuniruhusu kutoa mchango wangu. Kwa maoni yangu, ni kweli wazazi wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto wao. Lakini, kuna matatizo makuu 57 ambayo wazazi hawatilii mkazo katika malezi hayo. Chunguza jinsi watoto na vijana wengine wanavyotumia dawa za kulevya. Siku hizi, idadi ya wanaokumbwa na matumizi ya dawa za kulevya huzidi kuongezeka. Wazazi wenzangu, mjue kwamba dawa za kulevya ni hatari sana kwa binadamu. Dawa hizi husababisha magonjwa mengi na huharibu ubongo wa watoto. Kwa upande wangu, kila mzazi lazima ashiriki katika malezi ya watoto wote anaokutana nao badala ya kuwafikiria watoto wake tu. Wazazi wote wakilitilia maana tatizo hili, lingemalizika haraka sana, watoto wetu wakaishi maisha mazuri.

    Kiongozi: Ninamshukuru sana mshiriki kwa maoni yake. Anaeleza kwamba wazazi hawazingatii wajibu wao kwa kutoa mchango wao kukomesha matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana. Anaeleza pia kwamba malezi ya mtoto ni jukumu la kila mtu. Tunamshukuru sana. Hebu, tumsikilize pia mshiriki yule aliyenyosha mkono pale ili naye atoe hoja zake.

    Mshiriki wa tatu: Mheshimiwa kiongozi na wasikilizaji washiriki wenzangu. Watu ambao wako karibu sana na watoto ni wazazi wao ambao wana mchango wa kwanza katika malezi ya watoto hao. Wao huwatunza watoto wao, tangu wanapozaliwa na wakati wa kwenda shule unapofika, wao ndio wanaopiga hatua ya kwanza kuwapeleka shuleni. Wajibu wa kila mzazi ni kupeleka mtoto wake shuleni kwani anapata mwenendo mwema utakaomsaidia maishani mwake. Watoto wanapofika shuleni, ni vyema wazazi wao wawajibike kufuatilia malezi ya watoto wao kwa kuwashauri, kuwafundisha kuwa na mienendo mizuri, kuwanunulia vifaa vya shule na kuwalipia karo. Waheshimiwa wasikilizaji, kama mnavyoelewa, bila mchango wa wazazi, watoto hawawezi kupata elimu inayotolewa shuleni kwani wao ndio wanaorahisisha kila jambo linalotendewa mtoto, awe shuleni, nyumbani na mahali pengine. Asante sana kwa kunitega sikio, hayo ndiyo maoni yangu.

    Kiongozi: Waheshimiwa wasikilizaji washiriki, mawazo hayo ya mwenzetu mmeyasikia. Sasa ninataka kumkaribisha msemaji mwingine yeyote ambaye ana la kusema ili naye atoe mchango wake kwa ufumbuzi wa suala letu. Karibu sana bibi.

    Mshiriki wa nne: Asante sana kiongozi na wasikilizaji washiriki kwa kunipa fursa hii. Wapendwa wasikilizaji washiriki, taifa letu hufanya mengi ili iweze kukomesha matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wananchi. Kwa nini wazazi tusiwasaidie viongozi wetu kupambana na janga hili ili tupige marufuku madawa ya kulevya ambayo huangamiza maisha ya watoto wetu? Serikali yetu imechukua uamuzi mzuri wa kuanzisha mradi wa elimu kwa wote ambapo kila mtoto anapelekwa shuleni akaendelea na masomo yake mpaka anapomaliza shule za sekondari. 5858 Kwa hivyo, ni lazima walimu na viongozi wa shule waelewe kwamba wanahitaji kushirikiana na wazazi ili waweze kutimiza wajibu wao mkubwa wa kubadilisha mienendo ya vijana wanaowalea hasa vijana wale wanaopatikana wakitumia madawa ya kulevya. Bila mchango wa wazazi kwa vijana hao, shule zetu haziwezi kufanikiwa kuwapatia watoto hao maadili yanayotakiwa. Kwa mfano, utamkuta kijana mmoja akikosekana shuleni kwa siku moja au mbili na akifika huwadanganya viongozi kwamba alikuwa ameenda nyumbani na viongozi hawa hukubali bila kuuliza wazazi wa mtoto huyo kuhusu ukweli wa yale aliyosingizia. Kwa kumaliza, ni vyema kila mtu anayehusika na malezi ya watoto awe mwalimu, kiongozi wa shule na hata majirani waelewe kwamba wazazi wana nafasi kubwa katika urekebishaji wa mienendo mibaya ya watoto wetu. Ahsanteni sana kwa kunitega sikio.

    Kiongozi: Ninamshukuru mshiriki mwenzetu kwa maelezo yake ambayo yamewagusa wengi. Yeye amesema kwamba ni lazima kuisaidia serikali katika kulinda watoto wetu dawa za kulevya. Ameeleza pia kwamba kila mtu anayehusika na malezi ya watoto aitambue kwanza nafasi ya wazazi kwa kujaribu kuwashirikisha kwa kila uamuzi kuhusu mienendo na tabia za watoto wao. Kwa hivyo, tunamshukuru sana kwa mawazo yake. Kama mnavyoona, mengi yamekwishaelezwa na muda unazidi kuyoyoma. Hebu nichukue fursa hii kuwakaribisha washiriki wengine wawili kabla ya kutamatisha mjadala wetu. Karibu sana.

    Mshiriki wa tano: Ahsante sana kiongozi kwa kunipa muda huu ili nami nitoe maoni yangu. Washiriki wenzangu, mawazo yaliyotolewa na waliotangulia ni mazuri sana na yanaeleweka waziwazi. Ni ukweli mtupu kwamba wazazi ndio wenye jukumu la kwanza katika malezi ya watoto wao na ndiyo maana wahenga walisema, “Mtoto hutazama kisogo cha mama yake”. Mzazi ni mfano unaoigwa na mtoto wake. Kama mzazi ana tabia nzuri mtoto naye bila shaka ataathiriwa vizuri na itakuwa kinyume kama mzazi ana tabia zisizopendeza. Kwa hivyo, mimi ningependa kuhimiza wazazi wote kukuza na kuendeleza tabia nzuri mbele ya watoto wao ili waweze kuigwa na kutumiwa kama mifano mizuri kwa malezi ya watoto wao kwani mtu hutoa kile alicho nacho na pia huvuna kile alichopanda. Ahsanteni.

    Kiongozi: Ahsante sana mshiriki kwa mawazo yako mazuri. Naona kuna wengine wanaonyosha mikono yao ili kutoa michango yao kuhusu suala letu. Lakini, hebu tumsikilize mzazi yule ili tukamilishe mazungumzo yetu. Karibu sana.

    Mshiriki wa sita: Kiongozi na wasikilizaji washiriki wenzangu! Ni lazima tuelewekwamba mtoto hulelewa na watu wote wanaomzunguka 59 kwani hawa nao wana nafasi kubwa kwa kumwathiri vizuri au vibaya kulingana na mienendo na tabia zao. Mtoto afikapo shuleni, malezi yake huwa zaidi mikononi mwa walimu na viongozi wa shule ambao hufanya kazi kubwa ya kuwalea watoto na kuwaelimisha. Watoto humaliza muda mrefu mikononi mwa walimu na viongozi wa shule wanaomsaidia kurekebisha tabia mbaya na kuendeleza tabia nzuri huku wakimpa elimu itakayomfaa katika maisha yake. Mbali na hayo, mtoto akitembea barabarani, njiani na akienda kwingine anakotumwa na wazazi wake hukutana na watu ambao si wazazi wake, mtoto akipewa ruhusa ya kwenda kuangalia familia yake pana hukutana na watoto wengine katika familia hizo na hata watu wengine ambao si wazazi wake.

    Kwa hivyo, mimi naona kuwa watu wote wanamzunguka mtoto kuanzia wale wanaokaa naye nyumbani kama vile wazazi wake, ndugu zake na watumishi wa nyumbani, majirani na wengine ambao hukutana naye nao wanaweza kuathiri sana malezi ya mtoto na hata kuliko wazazi wake wanavyoweza kufanya. Ni mara ngapi tunasikia habari kwamba watoto wameathiriwa na watumishi wa nyumbani kwa kujiingiza katika vitendo na mienendo mibaya kama vile uzinzi, ulevi, matumizi ya maneno yasiyo na maadili, na kadhalika?

    Haya yote yanathibitisha kwamba malezi ya watato yanahusu watu wote wanaomzunguka mtoto huyo na kwamba wito unapaswa kutolewa kwao ili watambue wajibu wao kumlea mtoto. Wazazi humwelekeza mtoto wakati angali mchanga lakini aanzapo kwenda shuleni na kukutana na watu wengine, nafasi ya wazazi katika malezi yao huendelea lakini wanaomwathiri zaidi huwa ni watu wote anaokutana nao katika mazingira na shughuli zake mbalimbali. Asanteni sana kwa kunitega sikio; hayo ndiyo yalikuwa maoni yangu

    Kiongozi: Ninakushukuru sana kwa maelezo yako. Nasikia kwamba wewe unatilia mkazo kwamba watu wote wanapaswa kutoa mchango wao kwa kumlea mtoto badala ya kufikiria kwamba wazazi ndio wenye nafasi kubwa. Asante sana kwa mawazo hayo. Inaonekana kwamba watu wengi wangependa kutoa mchango wao lakini muda wetu hauturuhusu kuendelea kusikiliza hoja nyingine. Mjadala wetu unakaribia kufikia mwisho na ningependa kuwapongeza ninyi nyote kwa maoni na mawazo mazuri mliyoyatoa katika mjadala huu. Asante sana kwa wote mlioshiriki katika mjadala huu. Kichwa cha mjadala wa leo kilikuwa “MCHANGO WA WAZAZI KATIKA MALEZI YA WATOTO WAO.” Miongoni mwa hoja mlizozitoa ni wajibu wa wazazi kuwalinda watoto kutumia dawa za kulevya, kuwapeleka watoto shuleni na kufuatilia masomo na mienendo yao kokote wanakoenda, viongozi wa shule na walimu kushirikisha wazazi katika malezi ya watoto wao na watu wengine wanaokutana 6060 na mtoto kuelewa kwamba nao wanaweza kumwathiri mtoto huyo vizuri au vibaya. Waheshimiwa mabibi na mabwana hoja zote mlizozitoa zimezingatiwa na zimeeleweka vizuri. Ahsanteni sana kwa mchango wenu katika kupigania malezi bora kwa watoto wetu. Mjadala wa leo unaishia hapa. Njooni tena wakati mwingine kwa mada nyingine. Ahsanteni sana kwa kushiriki.

    Kazi ya 2

    Maswali ya ufahamu

    1. Malezi ya msingi mtoto huyapata wapi?

    2. Dawa za kulevya zina madhara gani kwa maisha ya vijana?

    3. Kwa nini mzazi ana wajibu wa kuwapeleka watoto shuleni?

    4. Eleza nafasi ya Serikali katika malezi ya watoto kama ilivyozungumziwa katika mjadala huu. 

    5. Viongozi na walimu hutakiwa kufanya nini kwa kuzingatia nafasi ya wazazi katika malezi ya watoto wao?

    6. Nini maana ya msemo ‘‘mtoto hutazama kisogo cha mama yake?’’

    7. Eleza msemo huu’’Mtu haulizwi kitu asichokuwa nacho’’

    8. Ni masomo gani uliyofaidika kutokana na mjadala huu huu baada ya kuusoma 


    6.2. Msamiati kuhusu «Andalio la mjadala»

    Kazi ya 3

    Tunga sentensi sahihi kwa kutumia maneno yafuatayo yanayotumika katika mjadala:

    1. Mchango

    2. Elimu 

    3. Dawa za kulevya

    4. Kisogo

    5. Kulea

    6. Kukaribisha

    7. Kiongozi 

    8. Ulevi

    9. Uzinzi

    10. Serikali

    Kazi ya 4 

    Husisha maneno yaliyoko katika sehemu A na maelezo yaliyopo katika sehemu B.

    ok

    6.3. Sarufi: Matumizi ya viambishi rejeshi kulingana na ngeli za majina

    Soma na uchunguze sentensi zifuatazo: 

    - Ng’ombe walionunuliwa walikuwa wanono.

    - Miti itakayopandwa itasaidia katika hali ya hewa.

    - Chakula tulichopata kilikuwa kitamu.

    - Mwizi aliyeiba mbuzi wangu ni yule.

    - Viti vilivyoletwa vilikuwa safi

    Maelezo Muhimu

     Kiambishini kipande chanenochenye maana yakisarufiambacho kinapachikwa kwa mfano kabla au baada ya mzizi wa neno katika vitenzi na kuwakilisha dhana fulani.

    -o- rejeshi hujitokeza katika shina amba-. Shina hili huongezewa viambihi vya 

    -o- rejeshi na kupata neno lionyeshalo urejeshi. Hapa tunapata maneno kama ambalo, ambaye, ambacho, n.k. haya ndiyo mazingira ya utokeaji wa -o- rejeshi.

    Kazi ya 5

    Kamilisha sentensi zifuatazo kwa kutumia ‘o ’rejeshi:

    1. Asiyekuwe ---- na lake halipo.

    2. Ngoma ivuma……………. ndiyo ya kupasuka. 

    3. Akufaa--- kwa dhiki ndiye rafiki yako.

    4. Zimwi likujua----- halikuli likakukumaliza.

    5. Wageni wafika ………. sasa ndio wetu. 

    6.4. Matumizi ya lugha: Maandalizi na utekelezaji wa mjadala

    Kazi ya 6

    Soma maelezo muhimu hapo chini kisha ujibu maswali yanayofuata:

    Maelezo muhimu kuhusu “Andalio la mjadala” 

    Mjadala ni mazugumzo juu ya jambo fulani. Unaweza kufanyika katika makundi madogo madogo au makubwa.

     • Mjadala unaongozwa na mtu mmoja au watu wawili ambao wanazusha mawazo na kuhakikisha ikiwa kuna mwenendo mwema kati ya washiriki wa mjadala huo. 

     • Kiongozi wa mjadala ndiye anayetoa muhtasari wa mawazo yaliyotolewa katika mjadala. 

     • Anayetoa hoja yake, anaweza kuunga mkono maoni ya mwenzake au kuyapinga kwa minajili ya kutoa mchango wake wa kutatua tatizo linalojadiliwa.

     • Mjadala unapomalizika, kiongozi huwapongeza waliohudhuria mjadala na kuwaalika katika mjadala mwingine.

    Mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa mjadala:

    • Kutumia vizuri muda uliopangwa,

    • Kuepukana na fujo na kelele,

    • Kupaza sauti unapotoa hoja kuhusu mada,

    • Kutoa maoni kwa madhumuni ya kutimiza lengo la mjadala,

    • Kutumia lugha ya adabu, isiyo ya matusi,

    • Kuwaheshimu wengine,

    • Kupanga mawazo yako kabla ya kupata fursa ya kuongea.

    Maswali 

    1. Eleza maana ya mjadala.

    2. Ni watu gani wanaoshiriki katika mjadala? Eleza. 

    3. Jadili mambo mawili ya kuzingatia katika uandalizi wa mjadala

    6.5. Kusikiliza na Kuzungumza

    Kazi ya 7

    Jadili na mwenzako kuhusu mada hii kisha muwasilishe maoni yenu kwa darasa.

    1. Faida na hasara za kuishi katika miji mikubwa. 

    6.6. Kuandika

    Kazi ya 8

    Andika mjadala kwenye ukurasa mmoja kuhusu “Malezi bora nchini Rwanda” huku ukitoa maoni yako kuhusu namna serikali na taifa zima linavyoweza kuwasaidia wanafunzi.

    Tathmini ya mada ya nne

    1. Eleza uhusiano na tofauti kati ya mjadala na mdahalo.

    2. Eleza mambo ya kuzingatia katika utekelezaji wa mjadala.

    3. Eleza mambo ya kujiepusha katika mjadala.

    4. Chagua na kujadili mada moja kati ya hizi zifuatazo:

    a. Wakoloni walileta mabaya mengi kuliko mazuri.

    b. Shule za bweni ni bora kuliko shule za kutwa.

    c. Uzuri wa mtu si urembo bali ni tabia.

    d. Kutoa si utajiri bali ni moyo.

    MADA YA 3:METHALI NA SEMI FUPIFUPIMADA 5:UTUNGAJI WA INSHA ZA MASIMULIZI