MADA YA 3:METHALI NA SEMI FUPIFUPI
• Uwezo mahususi wa mada:
Kutumia methali na semi fupi katika maisha ya kila siku.
• Malengo ya ujifunzaji:
- Kueleza maana ya methali,
- Kutoa maelezo ya nahau (semi fupi),
- kueleza ujumbe unaopatikana katika methali na semi fupifupi,
- Kuonyesha umuhimu wa methali na semi fupi katika jamii,
- Kutaja na kueleza matumizi ya aina za maneno,
- Kutumia methali na nahau katika mazungumzo,
- Kutumia kwa usahihi aina za maneno,
- Kuonyesha adabu na hehima kwa watu anaoongea nao.
Kidokezo
SOMO LA 4: LEO NI LEO
4.1. Kusoma na ufahamu: Leo ni Leo
Soma kifungu cha habari kifuatacho na baadaye ujibu maswali ya ufahamu yaliyotolewa hapo chini
Hapo zamani za kale palikuwa na mzee mmoja aliyejulikana kama Gahigi. Gahigi alisifika sana kwa uwezo wake wa kutoa mawaidha kwa kutumia lugha ya mafumbo yenye hekima. Kila siku alikuwa akitumia methali/ mithali nyingi sana. Wengi walimsifu na kumwita maktaba ya jamii. Katika mahakama za jadi Mzee Gahigi alikuwa mpatanishi pamoja na wazee wengine. Kila alipozungumza na mkewe, watoto, marafiki na wengine alikuwa akitoa maneno makavu yenye busara.
Siku moja mtoto wake Kagabo alichelewa kuamka asubuhi ili aende shuleni. Alimwamsha na kumwonya asizoee tabia mbaya ya kupenda kulala na kusahau kazi na majukumu muhimu kwa kumwambia, “Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.” Gahigi alikuwa bingwa katika matumizi ya lugha iliyoweza kuwaonya na kuwarekebisha waliokutana naye. Alikuwa mzee mwenye huruma na alikuwa akimhurumia kila aliyesahau kutekeleza jambo linalomngoja. Kwa hivyo alimwambia mtoto wake aamke haraka ili aende shuleni. “Mtoto wangu, ndege aamkaye asubuhi hula wadudu watamu. Acha kushika blangeti na shuka yako ili uweze kuvuna matunda ya jasho lako la baadaye. Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo. Mimi nimeanza kuzeeka lakini kama nisingetumika kazi vizuri msingeweza kusoma. Ukipoteza muda wako leo kesho hutaweza kuyarudia yaliyopaswa kutendeka leo.
Basi mtoto aliamka, akanawa mwili wake huku Gahigi akimsihi afanye haraka ili afike shuleni mapema. Alimwelezea mengi kuhusu hasara zinazowapata wavivu na jinsi wanavyoponyokwa na bahati zinazojitokeza maishani mwao. Alizidi kumwambia maneno matamu yenye busara ambayo Kagabo aliyapenda na kuyazingatia. Siku nzima yeye alikuwa akikumbuka methali moja iliyomvutia sana, “Titi la nyati hukamuliwa kwa mashaka,’’ na nyingine iliyomwambia kuwa “Wakati una mabawa.” Tangu siku hiyo Kagabo aliamua kuzingatia mawaidha ya babake na kujizoeza kuwa na bidii katika shughuli zake za kila siku. Alipowasikia wanafunzi wenzake wakimwambia kwamba “Haraka haraka haina baraka” aliwaambia kuwa wangeweza kujutia hayo baadaye.
Kila siku alikuwa wa kwanza kufika shuleni na kufuata vizuri maelezo ya mwalimu na mambo yote aliyofundishwa darasani. Alipopewa kazi, aliifanya haraka na kuimaliza kwa muda uliotarajiwa. Aliongozwa na maneno ya baba yake kwamba “Fanya kitu kinachofaa katika muda unaofaa.” Yeye alikuwa akishangaa kuona baadhi ya wanafunzi walikuwa wakiyapuuza maonyo yake kwa kuendeleza tabia za uvivu. Kila alipowaona wamechelewa alikumbuka maneno ya baba yake, ‘‘Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako. ’’ Kagabo 3636 alijitahidi kufanya kila liwezekanalo ili asonge mbele masomoni kwa kutarajia maisha mazuri ya baada ya masomo yake kama alivyopenda kumwambia baba yake
Kagabo aliendelea kusoma kwa bidii akamaliza shule za msingi na kuingia katika shule za sekondari. Kazi zote alizoombwa kufanya alizifanya kwa makini akiongozwa na maneno ya baba, “Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo.” Alipomaliza shule za sekondari alijiunga na chuo kikuu katika kitivo cha Lugha na Sanaa. Hapo bidii zake hazikupungua hata kidogo. Yeye alijua kwamba “Mchumia juani hulia kivulini.” Alipomaliza masomo yake alipewa kazi ya Mhariri Mkuu kwenye Televisheni ya Taifa. Hiyo ilikuwa kazi nzuri iliyoweza kumletea pato kubwa kila mwezi. Kazi yake ilimruhusu kutembelea mataifa mengi duniani ili kuonana na wahariri wengine katika makongamano na mikutano ya aina mbalimbali. Miaka miwili baadaye, alikuwa anajulikana kwa kila mtangazaji maarufu na kampuni nyingi za utangazaji zilianza kumwita kutoa mafunzo ya muda kwa watangazaji wao. Hapo alianza kufurahia uwezo wake na kukumbuka methali nyingi alizoambiwa na babake. Miongoni mwa maneno aliyoyakumbuka na ambayo alipenda kuwaambia watangazji wenzake yalikuwa yanaihusu methali tamu “Mchumia juani hulia kivulini.” Yeye alipenda kazi yake na kuifanya kwa usahihi na viongozi wake walimjua.
Mwaka wa tatu baada ya masomo yake alikuwa amejijengea nyumba nzuri ya kisasa mjini na kujinunulia gari zuri la kisasa. Watu wengi waliomwona walishangaa kuona mtoto aliyetoka katika kijiji kisichojulikana amefikia kiwango kama hicho cha kutegemewa na wengi. Kwa kweli, utajiri wake ulikuwa umemwezesha kuwakumbuka wasiojiweza na kuwasaidia kwa moyo mkunjufu. Yeye hakuona taklifu au ugumu wowote kusaidia yeyote aliyemwendea. Yeye alishirikiana na viongozi wa kijiji chake katika mradi alioanzisha wa kusajili vijana wote waliokuwa wamesitisha masomo yao kwani alikuwa ameshajenga shule ya kiufundi huko kijijini. Kila wakati alipofika kijijini kwake, majirani wote walikuja na kukumbuka malezi aliyopewa na babake alipokuwa mtoto mchanga. Wote walifurahia matunda aliyoweza kuvuna babake Gahigi na kuambiana kati yao “Ivute ngozi ingali mbichi.” Wote walielewa kuwa watoto wao wangelizoezwa kutimiza wajibu wao mapema kama Kagabo wangeliweza kuwa na maisha mazuri kama yake.
Mzee Gahigi alikuwa mtu wa ajabu aliyewaonya wanakijiji wote. Kila walipokutania katika shughuli mbalimbali za kijamii na za kimaendeleo ya kijamii alipenda kuwaambia, “Hakuna kitu cha bure katika dunia yetu, lazima tuchape kazi kwa bidii ili tufike tunapotaka kufika. Maisha mazuri ya watoto wetu yatatokana na malezi mema tutakayowapatia nasi tutafurahia jambo hili baadaye. Fuata nyuki ule asali kwa kuwa mtu huvuna kile alichokipanda.’’ Wazazi wenzake wote walimpongeza kwa maneno yake ya busara naye akakumbuka jinsi alivyochukuliwa na mtoto wake katika sherehe ya mwaka uliotangulia. 37 Kwa kweli, Kagabo alikuwa amemnunulia ng’ombe wa kisasa kama zawadi ya malezi mazuri aliyopewa. Baba yake alifurahi sana na kumshukuru mtoto wake.
Kazi ya 1
Maswali ya ufahamu:
1. Taja majina ya wahusika muhimu wanaozungumziwa katika kifungu hiki?
2. Kwa nini watu wengi waliyapenda maneno ya Mzee Gahigi?
3. Mzee Gahigi alikuwa na kazi gani katika mahakama za jadi?
4. Eleza jinsi tabia ya Kagabo ilivyobadilika.
5. “Mchumia juani hulia kivulini.” Eleza jinsi usemi huu unavyohusiana na kifungu cha habari ulichosoma.
6. Kuna funzo lolote unalolipata kutokana na kifungu hiki? Eleza
4.2. Msamiati kuhusu methali
Kazi ya 2
Jaribu kutoa maana za maneno yafuatayo:
Mafumbo
Mawaidha
Maktaba
Shaka
Baraka
Kazi ya 3
Eleza maana ya methali zifuatazo:
1. Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo.
2. Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.
3. Ndege aamkaye asubuhi hula wadudu watamu.
4. Wakati titi la nyati hukamuliwa kwa mashaka.
5. Haraka haraka haina baraka.
6. Ngoja ngoja huumiza matumbo.
7. Wakati una mabawa.
8. Mchumia juani hulia kivulini
4.3. Sarufi: Sarufi kuhusu matumizi ya vielezi, viunganishi, vihusishi na vihisishi
Kazi ya 4
Taja aina za maneno ambayo yamepigiwa msitari katika sentensi hizi:
1. Mtoto aliposoma sawasawa alipewa biskuti na wazazi.
2. Nyimbo ziimbwazo kitoto huchekesha kwelikweli.
3. Tulipanda ndizi kwa jembe lilelile.
4. Vigelegele vililia lelelele lelelele juzi wakati wa harusi ya dada.
5. Ukichokorachokora sikio lako utajitia mashakani polepole.
Maelezo muhimu kuhusu vielezi
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi na vielezi vingine. Tazama aina mbalimbali za vielezi katika jedwali na matumizi yake.
Kazi ya 5
Tumia viunganishi mwafaka kuunganisha sentensi zifuatazo:
1. Hana nyuma. Hana mbele.
2. Musabyimana alikula staftahi. Musabyimana alienda ofisini.
3. Alimsogelea adui yake. Hakuwa na hofu.
Kazi ya 6
Tunga sentensi ukitumia viunganishi vinavyofuata:
1. Mbali na
2. Baada ya
3. Lakini
Maelezo muhimu kuhusu viunganishi
Viunganishi ni maneno yanayofanya kazi ya kuunganisha. Huonyesha uhusiano baina ya neno na neno, fungu moja la maneno na fungu jingine au sentensi na sentensi.
Mifano:
1. au: Utanunua shati jekundu au jeupe?
2. badala ya: Anatazama televisheni badala ya kucheza.
3. bali: Kusema Kiswahili si vigumu, bali ni rahisi.
4. basi: Nilitaka sana kula piza, basi nilienda mkahawani.
5. bila: Basi lilifika bila mama.
6. ijapo: Ijapo nitakufa, sitakubali uwongo.
7. ila: Kila mtu amelala ila baba.
8. ingawa: Anapenda familia yake ingawa yeye ni maskini.
9. kama: Ninahitaji televisheni kama hii.
10. kisha: soma mfano huu kisha usome sentensi ifuatayo.
11. kwa sababu: Nilienda darasani kwa sababu nilitaka kusoma Kiswahili.
12. kwamba; kuwa: Ninaona kwamba / kuwa mnyama huyu ni mkali.
13. lakini: Uwera anacheka lakini Kabera analia.
14. na: Nitanunua kalamu na daftari dukani.
15. pamoja na: Nilienda dukani pamoja na mama yangu.
16. tena: Sijui mtoto huyu, tena sijamwona.
17. wala: Hakuna mchele wala unga.
18. isipokuwa: Wanafunzi hawa ni wazuri isipokuwa Gakwaya.
19. baada ya: Tulienda mkahawani baada ya darasa.
20. kabla ya: Nilizungumza na mwalimu kabla ya kuingia hapa.
21. ikiwa: Ikiwa nitapita mtihani, nitapata digrii yangu.
Kazi ya 7
Tumia vihusishi vifuatavyo kukamilisha sentensi: Sawa na, karibu na, baada ya, hadi, moja kwa moja.
1. Kitabu hiki ni ………………………………. kile.
2. Alikimbizwa ………………………………. nyumba yake.
3. ………………………………….. kula chakula tulinawa mikono.
4. Walisoma ……………………………. usiku wa manane.
5. Alienda ……………………………… kwa mwalimu mkuu.
Maelezo muhimu kuhusu vihusishi
Vihusishi ni maneno yanayoonyesha uhusiano baina ya watu au vitu viwili au zaidi. Kuna vihusishi vya kuonyesha mahali, wakati na hali.
Mifano:
1. kabla ya: Kabla ya kuimba nitakunywa chai.
2. baada ya: Baada ya darasa nitasoma.
3. nje ya: Niko nje ya nyumba.
4. ndani ya: Nyoka ameingia ndani ya shimo.
5. juu ya: Miti ilianguka juu ya nyumba.
6. chini ya: Viatu vyangu viko chini ya meza.
7. baina ya: Ninasoma kitabu baina ya Nimugire na Bariho.
8. kati ya: Mimi hunywa pombe kati ya Ijumaa na Jumapili.
9. mbele ya: Vitabu vipo mbele ya dirisha.
10. nyuma ya: Paka analala nyuma ya kochi.
11. karibu na: Ninaishi karibu na mji wa Huye.
12. mbali na: Nyumba yako iko mbali na pwani.
13. kando ya: Wilaya ya Nyamasheke iko kando ya ziwa Kivu.
14. mpaka; hadi: Nitasoma kutoka saa nne hadi saa tano asubuhi.
Nilikimbia kutoka saa nane mpaka saa tisa mchana.
15. kisha: Ninaenda sokoni kisha nitarudi nyumbani.
16. tangu; toka: Nilisoma Kiswahili tangu saa mbili hadi saa tano asubuhi.
Yeye atakaa hotelini toka Jumanne mpaka Ijumaa.
17. katika: Tunazungumza katika Kiswahili.
18. miongoni mwa: Mtoto anaimba miongoni mwa wazee.
19. usoni pa: Anaishi usoni pa duka.
20. pembeni mwa: Anakaa pembeni mwa darasa.
21. ubavuni pa: Mtoto amekaa ubavuni pa mama.
Kazi ya 8
Soma sentensi zifuatazo kisha utaje aina za maneno yaliyopigiwa msitari.
1. Haki ya Mungu! Mimi sikuiba.
2. Rais wetu, oyee!
3. Ala! Vipi mtu kujitia wazimu namna hii!
4. Afanaalek! Nimesahau kabisa kuwa leo ni siku ya kuzaliwa kwangu.
5. Huree! Tumemaliza kujenga nyumba.
Maelezo muhimu kuhusu vihisishi
Vihisishi ni maneno ambayo yanaonyesha hisia za mtu za ndani kwa mujibu wa hali na muktadha. Yanaonyesha hangaiko la moyo ama kudokeza mguso wa moyo ama hata wa akili. Kwa mfano: kuna kukosekana kwa matumaini, furaha, huruma, mshangao, hasira, wasiwasi na kadhalika. Ili kuonyesha baadhi ya mahangaiko haya, yapo maneno fulani yanayotumiwa.
Mifano ya baadhi ya vihisishi ni hii ifuatayo: Aa!, hmmm!, Ebo!, eti!, alaa!, basi!, afanaalek!, ajabu!, pole!, sasa/tena!, haki ya Mungu!, ewe!, inshallah!, ohoo!, kumbe!, oyee!, hata!, salaale!, la hasha!, Alhamdulillah!, maskini! lo!, haya!, na kadhalika
4.4. Matumizi ya lugha: Methali na nahau
A. Methali
Kazi ya 9
Soma maelezo muhimu yanayofuata, kisha ujibu maswali hapo chini.
Maelezo muhimu: Maana ya methali
Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya mafumbo. Ni tamko lenye kueleza wazo la busara la binadamu kwa ufupi sana. Misemo hiyo huzingatia maneno yenye kuvutia masikio ya watu wanaozitumia na huelezea mambo mengi kwa kutumia maneno machache iwezekanavyo. Methali nyingi huwa na sehemu mbili: Sehemu ya kwanza hutoa hoja nayo sehemu ya pili hutoa suluhisho au matokeo.
Mifano: Chelewa chelewa, utamkuta mtoto si wako.
(Hoja) (Matokeo)
Wakati titi la nyati, hukamuliwa kwa shaka.
(Hoja) (Suluhisho)
Mchumia juani, hulia kivulini.
(Hoja) (Matokeo)
Methali huhitaji hekima ili kujua maana yake. Inatumika kwa minajili ya kusema jambo fulani kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kama tanzu nyingine za fasihi simulizi, methali huwa na maana ya nje (maana inayopatikana kutokana na maana za maneno yaliyotumika kuundia methali husika) na maana ya ndani (maana inayosemwa kwa ufiche/ maana fiche).
Mifano:
1. Mpanda ngazi hushuka
Maana ya nje: Mtu yeyote anayepanda juu ya ngazi ni lazima itafika muda wake kushuka kutoka juu ya ngazi hiyo.
Maana ya ndani: Katika maisha mtu anayepata cheo au madaraka kuna siku anaweza kuyapoteza madaraka au cheo hicho.
2. Leo ni leo asemaye kesho ni mwongo
Maana ya nje: Siku hii ni siku hii, anayenena siku ifuatayo ni mdanganyifu.
Maana ya ndani: Tendo linalowezekana kufanyika sasa lazima lifanyike, lisiahirishwe.
Katika jamii methali zina umuhimu wa kuonya, kurekebisha, kutoa mafunzo, kutahadharisha na kuunganisha jamii.
Maswali:
1. Fafanua maana ya methali.
2. Toa mifano miwili ya methali, kisha ubainishe sehemu zake mbili: hoja na matokeo au suluhisho.
3. Toa methali mbili, kisha uonyeshe maana yake ya nje na maana yake ya ndani kwa kubainisha wakati wa kuitumia au namna inavyoweza kutumiwa katika mazungumzo ya watu
Kazi ya 10
Husisha methali kutoka safu A na methali yenye maana sawa na methali hiyo katika safu B.
Kazi ya 11
Linganisha methali toka safu A na maana mwafaka kutoka katika safu B.
B. Nahau
Maelezo muhimu kuhusu nahau
Nahau ni semi zinazotofautiana na maana yake ya nje. Huwa ni semi zenye mvuto na utamu wa lugha. Nahau huundwa kwa lugha ya kawaida, kwa kuashiria wazo la picha kutoka katika hali halisi ya maisha, ambazo aghalabu huwa ni misemo ambayo mtumiaji huitumia katika maazungumzo au maandishi hata bila kujua kuwa anaitumia. Ni msemo wa picha ambao huwa na maana iliyofichika. Nahau huwa na undani wa kimaana kuliko baadhi ya misemo inayopatikana katika lugha fulani. Kutumia semi hizi kunaonyesha kuwa mtumiaji wa lugha amepevuka katika lugha kwani ufafanuzi wa picha zilizomo unahitaji ujuzi mkubwa wa lugha.
Mifano ya nahau:
1. Kuchukua sheria mkononi: kulipiza kisasi kwa jambo baya
2. Kuenda aste aste: kuenda pole pole / taratibu.
3. Kuenda chapu chapu: kuenda haraka
4. Kuenda kasi: kuenda haraka haraka.
5. Kufanya hila: kutenda jambo la udanganyifu
6. Kufanya masihara / mizaha: kutenda mambo kwa mchezo
7. Kufanya uchuro: hali ya kuwa na kisirani ; mkosi
8. Kufanya utani: kufanya mzaha au mchezo
9. Kufanya uzohali: kuwa na uvivu; kuzembea
10. Kufuja mali: kuharibu mali, kutumia pesa vibaya
Kazi ya 12
Tumia mshale kwa kuhusisha nahau katika sehemu A na maana zake katika sehemu B.
Kazi ya 13
Kwa ushirikiano na wenzako, husisha semi (nahau) zifuatazo katika safu A na maana zake katika safu B, kisha mtunge sentensi kwa kutumia nahau hizo.
4.5. Kusikiliza na Kuzungumza: Majadiliano
Kazi ya 14
Shirikiana na wenzako katika utafutaji wa maana ya nahau zinazofuata:
1. Kuchemsha bongo
2. Kuchongea mtu
3. Kubeza mtu
4. Kuchungulia kaburi
5. Kufafanua kinaga-ubaga
6. Kupigwa kalamu
7. Kumpa nyama ya ulimi
4.6. Kuandika: Utungaji wa insha ya methali
Kazi ya 15
Tunga kifungu cha habari chenye mada ifuatayo: “Mchumia juani hulia kivulini.”
Hakikisha kwamba unatumia vielezi, viunganishi, vihusishi, vihisishi na baadhi ya nahau ambazo zinafuata:
Kufunga virago: kuondoka; kusafiri
Kugaragara kitandani: kugeukageuka huku na huko kitandani
Kujifungua mtoto: kuzaa kwa mwanamke
Kukata kamba: kufariki, kutoroka
Kukaza kamba: kujitahidi
Kula chumvi nyingi: kuishi miaka mingi
Kula kiapo: kuapa
Kumpa mtu heko: kupongeza mtu
Kumpa mtu mgongo / kisogo: kufanyia mtu mambo yaliyo kinyume na matarajio
Kumpa mtu nyama ya ulimi: kumpa mtu maneno matamu
Kuona cha mtemakuni: kujuta; kupata adhabu kali
Kuona kilichomnyima nyoka miguu: kupata adhabu kali.
Kuona kilichomnyima kanga manyoya: kupatwa na ubaya.
Kupanda mbegu za chuki: kuwachochea watu wachukiane
Kupiga marufuku: kukataza kitu kisheria
Kuvunja mbavu: kuchekesha; kufanya au kusema maneno yanayochekesha.
Kuvunja nyumba: kuharibu hali ya maisha baina ya mume na mke.
Tathmini ya mada ya tatu
1. Nini dhana ya methali?
2. Maana ya nahau ni ipi?
3. Taja umuhimu wa methali katika jamii.
4. Taja aina za maneno ambayo yamepigiwa mistari katika sentensi zifuatazo:
a. Nitakuonyesha kitabu changu kipya kesho.
b. Mchungaji anahubiri mbele ya Wakristo.
c. Angalia! Kalamu yako inaangukia chini ya meza.
d. Timu ya Amavubi oyeee!
e. Musaniwabo na Beneyo wanakwenda sokoni.
5. “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Jadili kwa kutozidi ukurasa mmoja.