• This topic

    MADA 2: KISWAHILI NA FASIHI SIMULIZI

    • Uwezo mahususi:

    Kusoma na kusimulia hadithi za masimulizi

    • Malengo ya kujifunza:

    - Kueleza maana ya fasihi,

    - Kutaja tanzu za fasihi,

    - Kuonyesha umuhimu wa Fasihi Simulizi,

    - Kutaja vipengele vya Fasihi Simulizi,

    - Kueleza maana ya hadithi,

    - Kusimulia hadithi,

    - Kukuza na kuhifadhi utamaduni, mila na desturi kupitia vipengele vya fasihi simulizi,

    - Kubaini na kuonyesha aina za maneno.

    Kidokezo

    Tazama kwa makini mchoro ufuatao kisha ujibu maswali yaliyotolewa hapo chini:

    OK

    Jibu maswali yafuatayo

    - Ni nini unachoona kwenye mchoro huu?

    - Unadhani kuwa watu hawa wanafanya nini?

    SOMO LA 2: DHANA YA FASIHI SIMULIZI

    Kazi ya 1

    Toa maelezo mafupi kuhusu mchoro huu.

    ok

    2.1. Kusoma na ufahamu: Dhana ya fasihi na umuhimu wake

    Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha ujibu maswali ya ufahamu

    Ilikuwa Jumatatu moja wakati mwalimu wetu wa Kiswahili alipoingia darasani, mkoba begani na madaftari mkononi. Kama kawaida alitusalimia huku akitabasamu. Wanafunzi wote katika madarasa ya mchepuo wa ualimu tulimpenda sana kwani alikuwa mwerevu, mcheshi, mzuri tena mpole. Tena alijali watu wote na wote wakamheshimu. Wakati huo, nami nilikuwa nikisoma katika mwaka wa pili mchepuo wa ualimu.

    Mwalimu alianza somo ambalo liliwavutia wanafunzi wote darasani. Sote tulikuwa na vitabu vya Kiswahili vya mwanafunzi na kila mwanafunzi alikuwa amefungua kitabu chake. Mwalimu alituomba kuunda makundi ili tusome kifungu kuhusu dhana ya fasihi na umuhimu wake katika jamii. Aliomba makundi yote kujiandaa kwa kazi yao. Baadaye, kila kundi lilipewa dakika kumi na tano za kuwasilisha hadharani matokeo ya kazi. Makundi yote yalikuwa yamejitahidi kufanya kazi vizuri. Sote darasani tulielewa vizuri kwamba fasihi ni sanaa ya lugha ambayo hushughulikia masuala yanayomhusu binadamu. Yaani kazi ya Sanaa inayomulika hisi, mawazo na malengo ya jamii kwa kutumia lugha.

    Makundi yote yaligundua kwamba fasihi huzungumzia na kuonyesha maisha ya jamii, kwa kueleza mambo yote yaliyomo katika jamii hiyo: matatizo, mitazamo, migogoro, itikadi, na shughuli mbalimbali za kijamii zilizopo huwa ni mambo yanayobainishwa katika kazi ya fasihi; yaani sanaa ambayo hutumia lugha. Vile vile, wanafunzi wote walielewa kuwa kila mtu anayejishughulisha na utunzi wa kazi ya fasihi hulenga kudhihirisha hisia alizo nazo kulingana na mazingira anamoishi. Yeye huitazama jamii yake na kueleza yote yatendekayo katika jamii hiyo kwa njia ya lugha.

    Makundi yote yalipomaliza kuwasilisha, mwalimu wetu alisisitiza kwamba fasihi hutumia lugha kisanaa na kuwa malengo ya fasihi ni kuelimisha wanajamii, kuwaburudisha na kuwastarehesha. Yeye alieleza kwamba fasihi huwaonya wanaotenda maovu kuacha maovu yao, na kuwahimiza wanaotenda mema kuendeleza matendo yao mazuri. Vilevile, fasihi ni kioo cha jamii na mwavuli wake. Inalinda jamii kwa kuhifadhi na kueleza vitendo vyake ambapo vitendo vizuri huhimizwa na kuchochewa ilhali vitendo vibaya hukatazwa. Msanii ambaye ni mwanafasihi huitumia lugha fulani kwa kujulisha jamii mengi yaliyomo katika utamaduni wake.

    Zaidi ya hayo, tuliona kuwa fasihi hugawanyika katika tanzu kubwa mbili yaani fasihi simulizi na fasihi andishi. Fasihi simulizi hutegemea zaidi usemi ilhali fasihi andishi hutegemea zaidi maandishi kwa kiasi kikubwa. Katika fasihi simulizi kuna tanzu ndogo ambazo huitwa vipera. Vipera vya fasihi simulizi kama vile hadithi, maigizo, ushairi (wa kimapokeo), methali, vitendawili, nahau, na kadhalika. Katika fasihi andishi kuna tanzu tofauti k.v. hadithi fupi, hadithi ndefu (riwaya), tamthilia na mashairi (ya kisasa). Kwa upande mwingine tuligundua kwamba kuna fasihi ya Kiswahili na fasihi katika Kiswahi. Fasihi ya Kiswahili ni ile inayohusu Waswahili, utamaduni wao na mazingira yao. Lakini Fasihi katika Kiswahili ni fasihi inayohusu jamii isiyo ya Waswahili iliyotungwa kwa lugha ya Kiswahili.

    Somo hilo lilitupendeza sote kiasi kwamba tuliamua kujifunza vizuri lugha ya Kiswahili ili tuweze kuitumia kisanaa. Leo hii, wanafunzi wengi tuliosoma pamoja enzi hizo tunajishughulisha na kazi mbalimbali za kisanaa zinazotumia lugha ya Kiswahili. Baadhi yao ni waimbaji, watunzi wa mashairi na wandishi wa vitabu kama mimi. Kila mwaka tunakutania katika tamasha za kitamaduni na kupata tuzo nyingi.

    Kazi ya 2

    Maswali ya ufahamu

    1. Kwa kuegemea kifungu cha habari, nini maana ya fasihi? 

    2. Andika tanzu kubwa za fasihi. 

    3. Fasihi simulizi ina tanzu ndogo au vipera gani? Vitaje vipera vitano. 

    4. Kwa sababu gani fasihi huchukuliwa kama kioo cha jamii? 

    5. Taja aina nne za umuhimu wa fasihi katika jamii. 

    2.2. Msamiati kuhusu fasihi

    Kazi ya 3

    Toa maana za maneno yafuatayo:

    1. Mkoba 

    2. Akitabasamu 

    3. Mcheshi 

    4. Itikadi 

    5. Kujiandaa 

    Kazi ya 4

    Tumia maneno yafuatayo kwa kujaza mapengo: hulenga, tamasha, itikadi, enzi, ilhali.

    1. Si vizuri kuwa na …...kali katika jamii. 

    2. Wewe unasema kuwa fasihi ni ngumu ……wenzako wanaiona rahisi. 

    3. Katika…….za ukoloni fasihi ya Kiafrika ilidharauliwa. 

    4. Fasihi ………kuelimisha na kuonya jamii husika. 

    5. Kila mwaka wasanii huhudhuria ………za kitamaduni na kumulika kazi zao.

    2.3. Sarufi: Aina za maneno

    Kazi ya 5

    Angalia sentensi zifuatazo ukichunguza maneno yaliyopigiwa mistari kisha ujibu maswali ya hapo chini.

    a. Mtoto anacheza mpira wake.

    b. Yeye ni mrefu sana

    • Maneno yaliyopigiwa mistari ni : nomino, kitenzi, kivumishi, kiwakilishi.

    ▫ Nomino/ jina

    a. Maana ya nomino

    Nomino au jina ni neno linaloita kitu chenye uhai au kisicho na uhai kwa kukitofautisha na vingine.

    b. Aina za nomino

    - Nomino za pekee: haya ni maneno yanayotaja majina maalum ya watu, mahali, vitu na hata Mungu ( Mifano : Kamali, Kigali, Nyange, Mola, 

    Muhanga, Kagoyire, Akagera, Nyabarongo, Rwanda)

    - Nomino za kawaida: haya ni maneno yanayotaja vitu vya kawaida ambavyo si mahususi, yaani maneno haya hutaja vitu kwa jumla.

     (Mifano : mtu, mto, ndege, kanzu, kofia, …)

    - Nomino za dhana au za dhahania: ni maneno yanayotaja vitu vya kufikirika au vya hisi tu (Mifano : uchungu, usingizi, uchoyo, uwili, …)

    - Nomino za jamii/ za makundi: ni maneno yanayotumiwa kurejelea vitu au watu wanaotokea kwa makundi (Mifano : jeshi, kamati, kaumu, umati, umma, taifa, familia, …)

    - Nomino za wingi: ni maneno yanayorejelea vitu ambavyo huwa katika hali ya wingi (Mifano: maji, mafuta, mawaidha, maziwa, manukato, …)

    - Nomino za kitenzi-jina: haya ni maneno yanayotokea kwa vitenzi lakini yanapotumika huwa ni nomino (Mifano : kucheza kunapendeza. Kuimba ni kuzuri. Kutembea kwao kunachosha.)

    Kitenzi 

    a. Maana ya kitenzi

    Kitenzi ni neno linaloeleza jambo linalotendwa au kufanywa na nomino au kiwakilishi chake.

    b. Aina za vitenzi

    - Kitenzi halisi: ni kitenzi kimoja kinachotumiwa katika sentensi. Vitenzi halisi huchukua viambishi mbalimbali.

    Mifano: 

    - Mwanafunzi anasoma kitabu.

    - Mgeni wetu atawasili kesho.

    - Vitenzi vikuu: kitenzi kikuu hueleza kitendo chenyewe kwa wakati uliotajwa. Wakati mwingine vitenzi viwili hutumika pamoja kueleza kitendo kimoja. Kitenzi cha kwanza huitwa kisaidizi na cha pili ndicho kitenzi kikuu.

    Mifano: 

    - Mtoto alikuwa akisoma.

    - Yeye anataka kuondoka.

    - Vitenzi visaidizi: kama tulivyoeleza hapo juu, vitenzi visaidizi hutumika pamoja na vitenzi vikuu katika kueleza taarifa kamilifu.

    Mifano: 

    - Maandishi yangali yanasomeka.

    - Zamani watu walikuwa wanasaidiana kazini.

    • Vitenzi vishirikishi: haya ni maneno ambayo hutumiwa katika sentensi kuonyesha ushirikiano au uhusiano baina ya nomino na kiwakilishi, kivumishi na momino. Vitenzi vishirikishi vina dhana ya kitenzi kuwa au kuwa na.

    Vitenzi vishirikishi huwa vya aina mbili kuu :

     Vitenzi vishirikishi vikamilifu: hivi ni vitenzi vishirikishi vinavyoweza kuchukua viambishi vya wakati na viambishi nafsi.

    Mifano:

    - Wavuvi wangali baharini.

    - Wewe umekuwa mzembe.

    - Vitenzi vishirikishi vipungufu: hivi ni vitenzi vishirikishi ambavyo vinaweza huchukua viambishi nafsi lakini havichukui viambishi wakati.

    - Walimu si waongo.

    - Wewe u mrefu.

    - Mimi ni mwalimu.

    - Mimi ndimi mwalimu.

    Maswali

    a. Taja aina za nomino katika sentensi zifuatazo:

    - Mheshimiwa Rais atakuja.

    - Katika jamii ya Wanyarwanda watu husaidiana 

    b. Tunga sentensi ukitumia vitenzi vifuatavyo:

    - ni

    - mkisoma

    - palilia

    - sambaza

    - utakuwa

    2.4. Matumizi ya lugha: Dhana ya fasihi na umuhimu wake

    Maelezo muhimu kuhusu Fasihi 

    Maana ya fasihi

    Fasihi ni kazi ya sanaa inayomulika hisia, mawazo na malengo ya jamii kwa kutumia lugha. Fasihi ni sanaa ya lugha inayoshughulikia masuala mbalimbali yanayohusu binadamu. Ni kusema kuwa maneno hutumiwa kisanaa. Fasihi inaweza kuelezwa kwa mitazamo miwili. Mtazamo wa kwanza ni Fasihi ya Kiswahili ambayo ni ile inayohusu Waswahili, utamaduni wao na mazingira yao. Mtazano wa pili ni Fasihi katika Kiswahili ambayo ni fasihi inayohusu jamii isiyo ya Waswahili lakini iliyotungwa kwa lugha ya Kiswahili sanifu.

    i. Dhima ya fasihi

    Fasihi ina kazi muhimu katika jamii. Wanafasihi wengi huichukua kama kioo cha jamii, wengine wakaifananisha na mwamvuli/ mwavuli mkubwa kwa kuwa inalinda utamaduni wa jamii kutoingiliwa na mambo kutoka tamaduni nyingine.  Vilevile, fasihi huchukuliwa kama daraja linalounganisha vizazi na vizazi.

    Isitoshe, fasihi ina umuhimu wa kuelimisha na kuonya jamii; kuburudisha na kuelekeza na kuendeleza jamii pamoja na kuhifadhi utamaduni. Pia, fasihi huchukuliwa kama silaha ya ukombozi.

    ii. Aina za fasihi

    Katika lugha ya Kiswahili kuna aina mbili za fasihi: 

    Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi. Fasihi Andishi ni aina ya fasihi inayohifadhiwa kimaandishi.

    Fasihi Simulizi ni masimulizi ya kale ambayo hayakuandikwa wala kunasiwa kwenye vinasasauti. Fasihi hii, ambayo ni asilia na kongwe zaidi duniani, ndiyo mzazi wa vipera vyote vya Fasihi Andishi. Kupitia kwenye fasihi hii,wanajamii husimuliana matukio, huelekezana kimaadili, huelimishana, hudumisha ushirikiano, huonyana na kupeana taarifa za malezi bora kwa njia ya kisanaa na ubunifu bila ya kutumia maandishi.

    iii. Vipera vya Fasihi Simulizi

    Fasihi Simulizi ina vipera vingi tofauti. Vipera hivyo ni kama ngano, hadithi, methali, nahau, misemo, methali, ushairi, n.k.

    a. Hadithi 

    Hadithi ni utungo wenye visa vya kubuni unaosimuliwa kwa lugha ya kinathari kwa kusudi la kuburudisha, kukuza maadili na kuunganisha jamii. Hadithi huwa na aina tofauti (hurafa/ kharafa, hekaya, ngano, miviga, mighani, visasili, n.k.).

    b. Methali/ mithali 

    Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya mafumbo. Ni tamko lenye kueleza wazo la busara la binadamu kwa ufupi sana.

    Mifano:

    - Mchumia juani hulia kivulini.

    - Mtegemea cha nduguye hufa maskini.

    - Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi.

    - Masukuzi ya leo ndio msitu wa kesho.

    - Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

    - Mtenda kazi asishe ni kama asiyetenda.

    - Usione vyaelea, vimeundwa.

    - Tamaa mbele mauti nyuma.

    - Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

    c. Nahau

    Nahauni semi zinazotofautiana na maana yake ya nje. Huwa ni semi zenye mvuto na utamu wa lugha. Nahau huundwa kwa lugha ya kawaida, kwa kuashiria wazo la picha kutoka katika hali halisi ya maisha, ambazo aghalabu huwa ni misemo ambayo mtumiaji huitumia katika mazungumzo au maandishi hata bila kujua kuwa anaitumia. Baadhi ya nahau hudai kitenzi maalum ndani yake ili ziwe na maana kamili.

    Mifano:

    - Kujikaza kisabuni

    - Kufua dau

    - Kukata tamaa

    - Kukaa chonjo

    - Kula chumvi nyingi 

    d. Misemo

    Misemo ni semi fupi fupi zinazotumia maneno ya kawaida lakini maana yakehuwa fiche. Tofauti na nahau, misemo haihitaji kitenzi ndani yake ili ziwe na maana kamili.

    Mifano:

    - Pua na mdomo 

    - Lila na fila 

    - Domo kaya

    - Mkia wa mbuzi

    e. Vitendawili

    Kitendawili ni tungo fupi ambayo huwa ni swali wazi yaani swali linaloulizwa kwa kutumia lugha ya mafumbo ili kuchemsha bongo ya hadhira. Majibu hutolewa kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake.

    Mifano: 

    - Mfalme katoa jicho jekundu: jua

    - Nanywa supu na kutupa nyama: mua

    - Mhuni wa ulimwengu: nyuki

    - Askari mlangoni: kufuli

    - Linakula lakini halimezi: shoka

    f. Ushairi simulizi 

    Ushairi ni mtungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato katika usemi, maandishi au wimbo. Mtungo huo hufuata utaratibu wa urari na muwala maalum unaoheshimu na kuzingatia kanuni za utunzi wa shairi unaohusika. Ushairi simulizi ni ushairi unaoghanwa tu.

    Ushairi hujumuisha mashairi ya aina tofauti, tenzi, ngonjera, nyimbo, n.k.

    Kazi ya 6

    Maswali 

    1. Fasihi ni nini? 

    2. Taja aina tano za umuhimu wa fasihi katika jamii. 

    3. Ni nini tofauti kati ya fasihi ya Kiswahili na fasihi katika Kiswahili? 

    4. Taja vipera vitano vya Fasihi Simulizi. 

    2.5. Kusilikiza na kuzungumza

    Kazi ya 7

    Shirikiana na mwenzako mtegeane na kuteguliana vitendawili.

    2.6. Kuandika 

    Kazi ya 8

     “Fasihi ni kioo cha jamii.” Jadili.

    SOMO LA 3: HADITHI

    ok

    Kazi ya 1

    Zungumzia mchoro hapo juu na vitendo vinavyofanyika.

    3.1. Kusoma na ufahamu: Wafalme wawili

    Soma hadithi hii inayofuata kuhusu “Wafalme Wawili”, kisha jibu maswali ya ufahamu uliyotolewa hapo chini.

    Hapo zamani za kale, kulikuwa na wanyama waliokuwa wanaishi msituni. Kila mnyama alikuwa anaishi na mke wake na watoto wake tu, bila kujali wanyama wengine. Msituni huko hakukuwa na mfalme wala kiongozi yeyote wa wanyama hao. Walikuwa na uhuru wa kuishi na kutembea mahali huku na kule.

    Siku moja, walipotazama namna wanyama wa misitu mingine walivyoishi, walidhani kuwa wanyama hao walikuwa na furaha zaidi kuliko wao, kwa sababu wanyama wa misitu mingine walikuwa na mfalme. Walisema, “Jamani, acheni tujichagulie mfalme kama wanyama wa misitu mingine.” Siku ya kuchagua mfalme ilipofika, walikutania kwa Bwana Nungunungu. Wote walikuwa mahali huko: simba, tembo, chui, twiga, ngiri, sungura, nguchiro, fisi, nyoka, mbogo, ndege na samaki. Wagombeaji walikuwa watatu: tembo, simba na sungura. Kabla ya uchaguzi, kila mmoja alijaribu kuomba kura huku akijaribu kuwashawishi wanyama wengine kuhusu namna anavyofaa kuchaguliwa kuwa mfalme kuliko wagombea wengine. Kila mgombeaji alijinadi kuwa yeye ana tabia nzuri zaidi kuliko washindani wake.

    Simba na Sungura ndio waliotangulia kwa kujisifu. Ilipofika zamu ya Tembo kusema, alifungua domo lake na kusema: “Msituni hapa na misitu mingine yote hakuna mnyama aliyekuwa na nguvu kama mimi. Nikichaguliwa kuwa mfalme wenu, nitalinda usalama wenu, mabibi zenu na watoto wenu. Hakutakuwa na mnyama kutoka misitu mingine atakayewashambulia. Hata binadamu hataingia hapa tena.” Papo hapo akateuliwa kuwa mfalme wa wanyama wote msituni humo.

    Siku chache baadaye, Mfalme Tembo aliitisha mkutano wa wanyama wote. Wote waliitikia wito, wakafika mbele ya Mfalme. Hapo Mfalme Tembo alisema: “Tegeni masikio nyote kwa sababu jambo ninalotaka kuzungumzia ni zito na litaathiri kila mmoja wenu wakati wote...... Kazi ya kulinda usalama wenu ni kazi ngumu sana na inanilazimisha kula chakula kizuri kila siku. Mimi sitaendelea kula nyasi kuanzia leo. Hivyo inamaanisha kwamba kila siku ninahitaji wanyama watakaoniletea chakula ili nile vizuri!”

    Siku iliyofuata, Bwana Ngiri alitayarisha chakula. Siku nyingine, Nguciro akakiandaa chakula kizuri. Mambo yaliendelea namna hiyo mpaka wanyama wote majike kwa madume walipomaliza zamu yao. Ilipofika zamu ya Sungura, yeye alikimbia haraka kwa Mfalme Tembo kumuuliza swali moja. Alipofika hapo, Mfalme Tembo ndiye aliyekuwa wa kwanza kumuuliza Sungura: “Wewe raia mbaya unayedharau Mfalme, mbona hujaleta chakula? Unataka nife leo? Ama unataka wewe mwenyewe uwe chakula changu sasa hivi!”

    Sungura aliogopa sana na kuanza kutetemeka, lakini alijaribu na kumuuliza Mfalme swali moja lililobadilisha mambo msituni humo. “Kuna wafalme wangapi msituni humu? Sijui ni yupi atakayekuwa analetewa chakula kila siku kati yenu wawili” Sungura akasema. Mfalme Tembo kwa kusikia hayo, ghafla alifoka na kumuuliza Bwana Sungura, “Nani huyo mwendawazimu anayejidai kuwa Mfalme hapa? Twende ukanionyeshe haraka nikamfundishe somo moja ambalo hatalisahau maishani mwake!” Sungura alimwelekeza wakatembea kwa haraka sana kama kilomita tatu mpaka walipofika kwenye mto wenye kina kirefu.

    Sungura alimwonyesha Mfalme Tembo kwa kutumia kidole: “Tazama pale majini. Mfalme huyo anajificha ndani ya maji. Nenda kaongee naye. Lakini ujue kwamba yeye haogopi mnyama yeyote.” Sasa ndipo Mfalme Tembo alielekea kwenye mto kumtafuta mfalme huyo mwingine. Kwa kutazama ndani ya maji, aliona Tembo wa kiume mnono kama yeye na kumwambia, “Wewe raia mbaya sana, mjinga na shenzi! Toka hapo nikuonyeshe mfalme kati yetu!” Ghafla, Mfalme Tembo alijitupa ndani ya mto ili apigane na mfalme huyo. Lo! Alianza kupiga kelele kuomba msaada. “Mungu weee nisaidie..... nisaidie jameni ..... nisaidie .....!” Alilalama. Papo hapo, Sungura alishikwa na huruma sana na mara moja akaanza kupiga kelele kuomba wanyama wenzake kuja kumwokoa mfalme wao. Punde si punde wanyama wenye nguvu kama vile simba, vifaru, nyati na wengine wengi walikuja wakaogelea na kumwokoa mfalme wao.

    Baada ya tukio hilo, Tembo alihudumiwa kwa wiki tatu akapona. Siku tatu baadaye, Sungura alimsogelea mfalme wao na kuanza kumwelezea sababu iliyomfanya amdanganye mpaka ajitose majini. Mfalme Tembo alijuta kosa lake la kuwanyonya wenzake na kula mali zao mpaka akaamua kuwaita wanyama wote ili awaombe msamaha. Wanyama walipofika walifurahia kwamba mfalme wao ameweza kukiri kosa lake na kujiuzulu. Wao waliamua kumchagua Simba awe kiongozi wao naye akaahidi kwamba angekomesha tabia zote mbaya na mienendo mingine isiyofaa miongoni mwa wanajamii wote. Aliagiza sheria iwekwe na kila mwanajamii aheshimu wengine. Tangu siku hiyo, ndiye mfalme wa pori na wanyama wote huheshimu uamuzi wake.

    Huu ndio mwisho wa hadithi.

    Kazi ya 2

    Maswali ya ufahamu

    1. Ni sababu gani iliyowafanya wanyama msituni wajichagulie mfalme?

    2. Taja angalau majina matano ya wanyama waliohudhuria mkutano wa kuchagua mfalme.

    3. Kila mgombea kati ya wale watatu alipewa fursa ya kufanya nini?

    4. Ni juu ya kigezo kipi Bwana Tembo alichaguliwa kuwa mfalme wa wanyama?

    5. Alipoitisha mkutano wa wanyama wote baada ya kuchaguliwa, Mfalme Tembo aliwaambia nini?

    3.2. Msamiati kuhusu ‘‘Wafalme wawili’’

    Kazi ya 3

    Eleza maana ya maneno yaliyopigiwa mstari katika sentensi zifuatazo:

    1. Wanyama walimchagua Simba kuwa mfalme wao. 

    2. Walikuwa na uhuru wa kuishi kokote. 

    3. Kila mgombea uchaguzi alijaribu kuwashawishi wanyama wengine. 

    4. Tegeni masikio nyote nitakayowaelezea. 

    5. Meya yule aliposhindwa kutawala alijiuzulu. 

    3.3. Sarufi: aina za maneno ya Kiswahili

    Kazi ya 4

    Chunguza matumizi ya maneno yaliyopigiwa mistari ili uweze kubainisha aina zake

    1. Yeye ni mrefu.

    2. Nyumba nzuri imejengwa.

    3. Wewe ni nadhifu.

    • Maneno yaliyopigwa mistari ni vivumishi.

     ▫ Vivumishi

    a. Maana ya kivumishi

    Vivumishi ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino.

    b. Aina za vivumishi

    • Vivumishi vya sifa

    Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k

    Kwa mfano: kizuri, kali, safi, mrembo, …

    - Yule mama mpole hupika chakula kitamu.

    - Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.

    - Ghorofa hii ndefu ilijengwa na washi hodari.

    • Vivumishi vimilikishi/ vya kumiliki

    Vivumishi hivi hutumika kuonyesha kwamba nomino inaimiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali : -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao

    Kwa mfano: changu, lako, yake, kwetu, vyenu, zao.

    - Baraka hutumia talanta zake kwa manufaa ya familia yetu.

    - Flora aliweka kitabu chako sebuleni mwako.

    - Dada yako amepata nguo yake katika sanduku lao.

    • Vivumishi vya idadi

    Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi

    a. Idadi kamili au dhahiri - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.

    Kwa mfano : tatu, mbili, kumi, ishirini na nne. 

    - Msichana mmoja amewaua panya wawili. 

    - Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu.

     b. Idadi isiyodhihirika au idadi isiyo dhahiri - hueleza kiasi cha nomino kwa jumla, bila kutaja idadi kamili au dhahiri

    Kwa mfano: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani. 

    - Watu wengi waliokuwa sokoni walinunua bidhaa kadhaa.

     - Baba yangu amekuwa tajiri kwa miaka isiyo michache. 

    - Baraka ana pesa kidogo mfukoni mwake.

     • Vivumishi viulizi/ vya kuuliza

    Vivumishi viulizi hutumika kuulizia swali. 

    Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli.

    Kwa mfano: -ngapi?, -pi? 

    - Ni watumishi wangapi wamefukuzwa? - kuulizia idadi 

    - Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu?

    Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.

    Kwa mfano: gani? 

    - Unazungumza kuhusu kipindi gani

    - Je, uliwahi kutembelea nchi gani?

    • Vivumishi viashiria / vionyeshi/ vya kuonyesha

    Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.

    Kwa mfano: 

    Karibu - hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, huu, hawa.

     Mbali kidogo - hapo, huyo, hiyo, hicho, hizo. 

    Mbali zaidi - pale, lile, kile, zile, vile, wale. 

    - Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule

    - Jani hili la mwembe limekauka. 

    - Tupa hapa mpira huo.

    • Vivumishi visisitizi

    Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria

    Kwa mfano: huyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, kuko huko.

    - Jahazi lili hili. 

    - Wembe ule ule.

     - Ng’ombe wawa hawa.

    Mfano: 

    Ng’ombe hawa hawa ni wanono. 

     Mtoto yule yule ni mweledi.

     • Vivumishi virejeshi.

    Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-rejeshi vinavyotumika kurejelea nomino.

    Kwa mfano: ambaye, ambao, ambalo, ambacho.

     - Msichana ambaye alikuja ni Baraka Flora. 

    - Sauti ambayo uliisikia nje ya mlango ilikuwa ya Bi. Umutesi

     • Vivumishi vya KI-Mfanano

    Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine. Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI.

    Kwa mfano: wa kifalme, za kijeshi, ya kitajiri, n.k. 

    - Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimaskini.

     - Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu. 

    - Bi. Naliza huvaa mavazi ya kifalme.

    • Vivumishi vya A-unganifu

    Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ ngeli pamoja na kiambishi -a cha A-unganifu, kisha nomino.

    Kwa mfano: cha, la, kwa, za, ya.

     - Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri. 

    - Chai ya daktari imemwagika.

    Kazi ya 5

    Pigia mstari vivumishi katika sentensi zifuatazo: 

    a. Kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, hapatapatikana mazao bora. 

    b. Jambo zuri la kufanya ni kujitenga na mambo maovu duniani.

     c. Nguo ile imempendeza kijana yule. 

    d. Kiti hicho kimevunjika, niletee kile pale. 

    e. Ni mwanafunzi gani anaugua?

    • Viwakilishi 

    a. Maana ya viwakilishi

    Viwakilishi vya nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa, bali huiwakilisha nomino hiyo.

    b. Aina za viwakilishi

     • Viwakilishi vya nafsi

    Viwakilishi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi

    Kwa mfano: Mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao ni viwakilishi nafsi huru.

     Ni, u, a, tu, m, wa ni viwakilishi nafsi viambata.

    OK

    - Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa. 

    - Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria

    Tnbh.: Viwakilishi mie na sie si sanifu. Vilivyo sanifu ni “mimi” na “sisi”.

    Viwakilishi viashiria

    Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.

    Kwa mfano: huyu, yule, hapa, huyo, hao, n.k. 

    - Hiki hakina maandishi yoyote.

    - Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi.

     - Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.

    • Viwakilishi visisitizi

    Hutumika kwa niaba ya nomino kwa kutumia kiashiria chake mara mbili mfululizo.

    Kwa mfano yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, kuko huko 

    - Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana. 

    - Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena.

    • Viwakilishi vya sifa

    Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.

    Kwa mfano: -eupe, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo. 

    - Vyekundu vimehamishwa. 

    - Warembo wamewasili. 

    - Kitamu kitaliwa kwanza. 

    - Wema hutuzwa.

    • Viwakilishi vya idadi

    Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake. 

    a. Idadi kamili/ dhahiri - hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino

    Kwa mfano: saba, mmoja, ishirini, wanne, hamsini na mbili. 

    - Wawili wamefukuzwa kazini leo jioni. 

    - Alimpatia mtoto wake elfu kununua chakula.

    b. Idadi isiyodhihirika/ idadi isiyo dhahiri- hueleza kiasi cha nomino kwa jumla, bila kutaja idadi kamili.

    Kwa mfano: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani. 

    - Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.

     - Wengi wamepita mwaka wa kwanza.

    • Viwakilishi viulizi

    Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino kuulizia swali. 

    Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli.

    Kwa mfano: -ngapi?, -pi?

     - Vingapi vinahitajika? - kuulizia idadi.

    - Zipi zimepotea?

    Kuna viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.

    Kwa mfano: nini?, nani, vipi? 

    - Yule mvulana alikupatia nini?

     - Uliongea naye vipi? 

    - kuulizia namna.

     - Nani amemwaga maji sakafuni? 

    - Nani anayeitwa?

    • Viwakilishi vimilikishi

    Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.

    Kwa mfano: -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao.

     - Kwetu hakuna umeme. 

    - Lake limepigwa pasi. 

    - Zao zimeharibika tena.

    • Viwakilishi virejeshi

    Hutumia O-rejeshi kurejelea na kuwakilisha au kusimamia nomino

    Kwa mfano: ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule.

     - Ambalo lilipotea limepatikana. 

    - Ambaye hana mwana, aeleke jiwe.

    • Viwakilishi vya A-unganifu

    Huwakilisha nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine ikaandama.

    Kwa mfano: cha, la, kwa, za, ya 

    - Cha mlevi huliwa na mgema. 

    - Za watoto zitahifadhiwa.

    Kazi ya 6

    Pigia mistari viwakilishi katika sentensi zifuatazo kisha sema ni vya aina gani. 

    a. Kati ya haya mawili utachagua lipi? 

    b. Wengine wao walipomaliza masomo yao walirejea kule kule kuendelea na kazi. 

    c. Chochote afanyacho hufanikiwa. 

    d. Wengi wa wanafunzi ni wa kupita mtihani wowote.

     e. Miti ile iliyopandwa huko ni mingapi?

    3.4. Matumizi ya lugha: Maelezo muhimu kuhusu hadithi

    Kazi ya 7

    Soma maelezo muhimu yafuatayo kisha ujibu maswali ya hapo chini

    a. Maana ya hadithi

    Hadithi ni tungo za fasihi za masimulizi ambazo zinatumia lugha ya nathari (lugha ya mjazo, ya maongezi ya kila siku). Tena hadithi ni mambo ya kubuni huwa yanaeleza ukweli fulani katika jamii husika.

    b. Aina za hadithi 

    • Hekaya: Ni hadithi ambayo wahusika wake kwa kawaida ni binadamu tu. 

     • Hurafa: Ni aina ya hadithi ambayo wahusika wake huwa ni wanyama au vitu vingine ambavyo huwa vinapewa uhai. Wanyama hao husimamia aina ya tabia ya aina fulani ya binadamu. Katika hadithi za kiafrika na hasa za kibantu, wanyama kama sungura, tembo, fisi, kobe, simba, mbwa, nyoka, mjusi na wengineo husikika sana.

    • Ngano: Hizi ni hadithi za kimapokeo ambazo zinatumia wahusika kama wanyama, wadudu, mizimu, miungu, miti, watu, na viumbe visivyo na uhai kama mawe, miamba, n.k. kueleza au kuonya jamii kuhusu maisha.

     • Visasili/ miviga: Ni hadithi ambazo husimulia mambo yanayohusiana na maumbile ya watu, wanyama, miti na vitu visivyo na uhai.

     • Soga: Hizi ni hadithi fupi za kuchekesha na kukejeli. Soga husema ukweli unaoumiza, lakini ukweli huo unajengewa kichekesho ili kupunguza ukali wa ukweli huo. Wahusika wa soga ni watu wa kubuni lakini wanapewa majina ya watu walio katika mazingira hayo.

    • Visakale/ Mighani: Ni hadithi zinazohusu watu waliotenda matendo ya kishujaa na wanaosifiwa katika jamii fulani.

    c. Umuhimu wa hadithi

    Hadithi hutoa sababu za hali mbalimbali katika dunia kama jamii inavyoiona. Husifu mema na kukashifu maovu. Hadithi hutoa maonyo, hurekebisha, huadhibu, huelimisha na kushauri. Hutoa mafunzo na maadili ya kufuatwa na jamii na kuiwezesha kubadili tabia. Hadithi huzingatia historia na utamaduni wa jamii inayohusika. Huendesha uhusiano wa jamii kwa kuiburudisha na kuboresha uwezo wa kukumbuka.

    • Hadithi husimuliwa na huwa na fomula yake katika utangulizi na mwisho wake

    Mifano ya mianzo ya hadithi za kimapokeo:

    1. Mtambaji: Paukwa!

    Hadhira: Pakawa!

    Mtambaji: Paukwa!

    Hadhira: Pakawa!

    Mtambaji: Kaondokea chanjagaa,

                          Kajenga nyumba kaka,

                         Mwanangu mwana siti;

                         Kijino kama chikichi,

                        Cha kujengea kikuta,

                         Na vilango vya kupitia,

                         Atokeani?

    Hadhira: Naam twaibu!

    Mtambaji: Hapo zamani za kale…………………

    2. Mtambaji: Paukwa!

    Hadhira: Pakawa!

    Mtambaji: Sahaniǃ

    Hadhira: Ya mcheleǃ

    Mtambaji: Giza

    Hadhira: La mwizi

    Mtambaji: Baiskeli

    Hadhira: Ya mwalimuǃ n.k.

    Mtambaji: Hadithi hadithi! 

    Hadhira: Hadithi njoo!

    Mtambaji: Hadithi hadithi!

    Hadhira: Hadithi njoo!

    Mtambaji: Hapo zamani za kale palikuwepo na …………………………

    • Hadithi huwa pia na miisho yake

    Tunasema: “Huu ndio mwisho wa hadithi” au “Hadithi inakomea hapa.”

    Maswali

    1. Hadithi ni nini? 

    2. Taja aina tano za hadithi. 

    3. Kwa sababu gani tunatumia wanyama katika hadithi? 

    4. Kuna tofauti gani kati ya hekaya na mighani? 

    5. Jaribu kuonyesha wanyama wanaotumiwa sana katika hadithi na uonyeshe tabia zao

    3.5. Kusikiliza na kuzungumza

    Kazi ya 8

    Mbele ya wanafunzi wenzako, simulia hadithi moja unaoyoifahamu kwa kuzingatia mianzo na miisho ya hadithi za kimapokeo kama zilivyoonyeshwa hapo juu.

    3.6. Kuandika

    Kazi ya 9

    Kwa kutumia Kiswahili fasaha, andika hadithi moja unayoifahamu kutoka katika jamii ya Rwanda, ukizingatia matumizi ya ngeli ya PA-M-KU.

    Tathmini ya mada ya pili

    1. Fasihi ni nini?

    2. Kwa sababu gani fasihi ina umuhimu katika jamii? (mambo matano)

    3. Je, inawezekana kutenganisha fasihi na jamii? Kwa nini? Eleza.

    4. Kwa sababu gani tunalinganisha fasihi na mwavuli/ mwamvuli mkubwa?

    5. Ni ipi maana ya hadithi?

    6. Taja aina tano za hadithi.

    7. Taja aina za maneno katika sentensi zifuatazo

    a. Yeye ana mkono mrefu, atafungwa.

    b. Nchi yetu ni nchi ya amani.

    c. Baba alikuwa akiendesha gari.

    d. Wengine warefu wamewasili.

    e. Dawa ya moto ni moto.


    MADA 1:MATUMIZI YA KISWAHILI KATIKA MAENEO YA UTAWALAMADA YA 3:METHALI NA SEMI FUPIFUPI