• MADA 1:MATUMIZI YA KISWAHILI KATIKA MAENEO YA UTAWALA

    • Uwezo mahususi:

    Kuzungumza na kuandika kwa ufasaha matini fupifupi kwa kutumia msamiati unaofaa katika mazingira ya utawala.

    • Malengo ya ujifunzaji:

    - Kutaja ngazi za utawala na viongozi wakuu wa serikali,

    - Kuonyesha msamiati unaofaa katika maeneo ya utawala,

    - Kuorodhesha sikukuu za kitaifa,

    - Kutaja aina mbalimbali za vitambulisho vinavyotumiwa,

    - Kutunga sentensi kwa kutumia majina ya viongozi na ngazi za utawala,

    - Kuchora kielelezo cha ngazi ya utawala nchini Rwanda, 

    - Kutunga matini fupi akitumia majina ya viongozi na aina mbalimbali za vitambulisho,

    - Kuheshimu viongozi na watu wengine wanaopatikana katika maeneo ya utawala,

    - Kueleza matumizi ya ngeli ya PA-M-KU.

    OK

    Kidokezo

    Zungumzia mchoro wa hapo juu

    SOMO LA 1: NCHI YETU RWANDA

    Kazi ya 1

    Angalia mchoro huu kisha ujibu maswali ya hapo chini.

    OK

    - Unaona nini kwenye mchoro huu?

     - Unafikiri kuwa watu hawa wanafanya nini?

    1.1. Kusoma na ufahamu: znchi yetu Rwanda

    Soma kifungu cha habari kifuatacho baadaye ujibu maswali ya ufahamu.

    Rwanda ni nchi ambayo inapatikana katika bara la Afrika, sehemu za Mashariki. Raia wake huitwa Wanyarwanda. Nchi ya Rwanda ni jamhuri inayotawaliwa na Rais.

    Utawala wa Rwanda unapatikana katika nyanja tatu. Nyanja hizo hushirikiana kama mafiga jikoni. Uwanja wa kwanza unahusiana na utungaji wa sheria. Kazi hii iko mikononi mwa bunge. Bunge la Rwanda lina vyumba viwili. Chumba cha wabunge wanaoongozwa na spika wa bunge na chumba cha seneti kinachoongozwa na spika wa seneti. Wabunge hutunga sheria na maseneta huchunguza sheria hizo na kuzithibitisha pamoja na kuchunga namna ambavyo serikali huweka sheria hizo matendoni.

    Uwanja wa pili ni wa kiutendaji. Uwanja huu unaongozwa na Rais akisaidiana na viongozi wengine kutoka ngazi za juu kufika ngazi za chini. Viongozi hao ni waziri mkuu na mawaziri wengine, wakuu wa mikoa, meya wa wilaya, makatibu watendaji wa tarafa na kata na wakuu wa vitongoji. Miongoni mwa viongozi hawa kuna wale wanaochaguliwa kwa upigaji kura, wanaoteuliwa na wengine wanaopitia katika mitihani.

    Uwanja wa tatu ni utawala wa kisheria unaohusiana na sheria, aina zake na jinsi sheria zinavyotumiwa. Sheria hizi hutumiwa wakati wa kuamua kesi mbalimbali zinazofikishwa mahakamani. Kuna mahakama za jadi, mahakama za ngazi ya chini, mahakama za ngazi za juu, mahakama za rufaa, mahakama maalum (za kibiashara, kijeshi) na mahakama kuu. Wanaosikiliza kesi na kutoa uamuzi huitwa majaji. Mashtaka hutayarishwa na waendeshamashtaka wakiongozwa na mwendeshamashtaka mkuu wa serikali.

    Rwanda ina majimbo/mikoa minne na Mji wa Kigali. Mikoa hiyo ni kama vile Mkoa wa Kusini, Mkoa wa Kaskazini, Mkoa wa Mashariki na Mkoa wa Magharibi. Kila mkoa unaongozwa na Mkuu wa mkoa au Gavana. Mikoa inagawanyika katika wilaya. Nchini Rwanda kuna wilaya thelathini. Kila wilaya inaongozwa na Mkuu wa wilaya au Meya akishirikiana na halmashauri ya wilaya. Wilaya inagawanyika katika Tarafa ambazo zinaongozwa na makatibu watendaji wakishirikiana na halmashauri ya tarafa. Tarafa nazo zinajengwa na kata/ mashina tofauti yaongozwayo na makatibu watendaji wa kata/mashina. Kila kata inajengwa na vijiji/vitongoji vinavyoongozwa na wakuu wa vitongoji.

    Taifa la Rwanda ni Jamhuri yenye nembo yake, bendera na Wimbo wa Taifa. Ina askari jeshi, askari polisi, askari kanzu na askari enyeji mbalimbali. Wanyarwanda ni watu wanaopenda kuchapa kazi ili kuendeleza nchi yao. Kila mwishoni mwa mwezi Wanyarwanda hufanya msaragambo kwa kufanya kazi za mikono (kujenga nyumba, kusafisha viwanja na barabara, kuzibua mifereji ya kupitisha maji na kadhalika). Baada ya kazi hizi Wanyarwanda huketi chini, viongozi wakawatangazia sera za serikali na kutatua mizozo mbalimbali.

    Katika maisha yao raia wa Rwanda na wengine wanaoishi au wanaoitembelea nchi ya Rwanda huwa na vitambulisho mbalimbali. Vitambulisho hivi ni kama vile kitambulisho cha utaifa, kadi ya upigaji kura, kadi ya huduma za afya, kadi ya ukimbizi (kwa wakimbizi), ruhusa ya kuendesha magari/pikipiki na pasipoti. Wafanyakazi hupewa kadi mbalimbali zinazotambulisha kazi zao na wanafunzi hupewa kadi zinazowatambulisha na kadhalika.

    Nchini Rwanda kuna sikukuu za kitaifa kama katika nchi nyingine. Sikukuu hizo ni kama Sikukuu ya Mwaka Mpya, Krisimasi, Idi (Idd-ul-fitr/Eid al-fitr), Pasaka na nyinginezo. Mara nyingi sikukuu hizi huambatana na shughuli za kidini. Sikukuu zinazohusiana na mambo ya kiutawala ni kama Sikukuu ya Mashujaa, Sikukuu ya Ukombozi, Sikukuu ya Wafanyakazi, Sikukuu ya Walimu pamoja na Sikukuu ya Uhuru. Wakati wa sikukuu zote hizi na nyinginezo ambazo hazikutajwa, Wanyarwanda hufurahi sana na kuchangia vyakula na vinywaji mbalimbali.

    Kazi ya 2 

    Maswali ya ufahamu

    1. Nchi ya Rwanda inapatikana kwenye bara gani? 

    2. Utawala wa Rwanda ni wa aina gani? 

    3. Kiongozi mkuu nchini Rwanda ni nani? 

    4. Taja nyanja tatu za uongozi wa Rwanda. 

    5. Kwa sababu gani Wanyarwanda husemekana kuwa wachapakazi? 

    6. Taja majina mawili ya:

    - viongozi wa kuchaguliwa 

    - viongozi wa kuteuliwa 

    - wanaopitia katika mitihani

    1.2. Msamiati kuhusu kifungu cha habari

    Kazi ya 3

    Toa maana za maneno yafuatayo:

    - Jamhuri 

    - Kura 

    - Kuteuliwa 

    - Majimbo 

    - Halmashauri

    Kazi ya 4

    Husisha sikukuu na tarehe

    OK

    1.3. Sarufi: Matumizi ya ngeli ya PA-M-KU

    Kazi ya 5

    Angalia sentensi zifuatazo ukichunguza majina na mofimu vilivyopigiwa mistari na kuzungumzia kwa ufupi matumizi yake katika sentensi hizo.

    a. Barabarani pamechafuka.

    b. Mezani kuna sahani mbili.

    c. Mfukoni mwangu mna fedha nyingi.

    d. Chumbani humu mna wanafunzi.

    e. Mahali hapa pamesafishwa.

    Maelezo muhimu 

    • Majina yaliyopigiwa mistrari yamo katika ngeli ya PA-M-KU

     • Majina ya ngeli hii si mengi sana. Kwa hiyo, Kiswahili kilichagua kupachika kiambishi -ni mwishoni mwa majina ya kawaida ili kupata majina ya ngeli hii.

    Mifano : 

    - Chumba+ni: chumbani

    - Kichwa+ ni: kichwani

    • Katika kitenzi, ngeli hii huwakilishwa na viambishi pa-, m- na ku-.

    Pa- : huonyesha mahali panapotambulika.

    M- : huonyesha ndani ndani mwa.

    Ku- : huonyesha juu ya na mahali pasipotambulika.

    • Wingi wa majina ya ngeli hii hutokana na wingi wa majina ya kawaida pamoja na kiambishi -ni. Majina haya hufuatwa na kitenzi chenye viambishi pa-, m- na ku-.

    PK

    OK

    Kazi ya 6

    Tumia viambishi mwafaka katika sentensi zifuatazo:

    a. Darasani –na wanafunzi. 

    b. Nyumbani kwetu –nanukia sana.

    c. Kichwani –na upara.

    d. Mahali hapa –tasafishwa. 

    e. Chumbani –mechafuka.

    ▫ Vivumishi vya ngeli ya PA-M-KU

    Kazi ya 7

    Chunguza maneno yenye wino uliokolea na kusema ni aina gani ya maneno.

    a. Nyumbani kupi kuna uchafu?

    b. Mnaenda mahali papi?

    c. Safisha mahali hapa.

    d. Chumbani mwa mtoto mna giza totoro.

    e. Mahali penyewe ni hapa

    f. Nyumbani humu mna usafi.

    g. Mezani kwetu kuna vitabu vingi.

    h. Safisha mahali hapa.

    i. Chumbani mwangu mna giza totoro.

    • Vivumishi vya kurejesha/ virejeshi

    a. Mfukoni mwenyewe

    b. Mezani kwenyewe

    c. Mahali penyewe


    • Vivumishi vya kuunganisha/ viunganishi/ vya A-unganifu

    a. Chumbani mwa mtoto.

    b. Nyumbani kwa Gapfizi

    c. Mahali pa kuchezea 

    • Vivumishi vya kuuliza

    a. Unaenda pahali papi ?

    b. Ni chumbani mpi ambamo hamna taa?

    c. Umeviweka vitambaa mezani kupi?

    • Vivumishi vya kumiliki/ vimilikishi

    OK


    • Vivumishi vya kuonyesha/ vionyeshi

    a. Chumbani humu/humo/mle

    b. Mezani huku/huko/kule

    c. Mahali hapa/hapo/pale


    • Vivumishi vya sifa

    a. Mahali pazuri

    b. Mezani kuzuri

    c. Chumbani mzuri


    Kazi ya 8

    Jaza nafasi kwa kutumia kivumishi mwafaka.

    a. Alitia maji mtungini…………..(pale, kule, mle, yule). 

    b. Nyumbani ……… kuna wanyama wengi wa mifugo (mwetu, petu, kwetu).

    c. Mezani……. hakuna uchafu (humu, huku, hapa, mle).

    d. Mezani huku ni…………….(mzuri, mazuri, kuzuri).

    e. Nimekutunza moyoni…… (kwangu, pangu, mwangu).

    f. Chumbani…………mlikuwa mchafu (kwenyewe, mwenyewe, penyewe).

    g. Nyoka ameingia chumbani…….Kamana (kwa, pa, cha, mwa).

    h. Unaishi mahali…….(ipi, hapi, papi, yapi)?

    i. Mahali ………pamejengwa nyumba nzuri (mwenyewe, kwenyewe, penyewe).

    j. Kichwani………mzee yule kuna mvi (mwa, cha, kwa, pa).

    1.4. Matumizi ya lugha: Maelezo muhimu kuhusu msamiati katika maeneo ya utawala

    Kazi ya 9

    Soma maelezo haya kuhusu msamiati katika maeneo ya utawala baadaye ujibu maswali ya hapo chini. 

    Katika maeneo ya utawala kuna misamiati mingi tofauti. Msamiati huo unahusiana na nyanja za utawala, ngazi za utawala, viongozi, vitambulisho vinavyotumiwa pamoja na sikukuu zinazoshehekewa katika nchi fulani. Hali hii inapatikana nchini Rwanda. Misamiati inayotumiwa ni kama hii ifuatayo:

    - Nchi: ni sehemu ya ardhi katika ulimwengu iliyogawanyika kisiasa kwa mipaka na kutambulikana kwa taifa yake.

    - Taifa: ni jamii ya watu wanaoishi katika nchi moja na wanaounganika kutokana na matukio ya kihistoria.

    - Taifa lisilokuwa jamhuri huitwa ufalme.

    - Nchi huru inaongozwa na katiba

    - Rwanda ni nchi, taifa na jamhuri. Uongozi wa Rwanda unaonyeshwa na Kielelezo kifuatacho:

    OK

    Maswali

    1. Ni nini tofauti iliyoko baina ya taifa na nchi?

    2. Ni nini tofauti iliyoko baina ya ufalme na jamhuri?

    3. Ni nini maana ya katiba?

    1.5. Kusikiliza na kuzungumza

    Kazi ya 10

    Sikiliza taarifa ya habari redioni baadaye ujadiliane na wenzako kuhusu msamiati katia maeneo ya utawala

    1.6. Kuandika

    Kazi ya 11

    Tunga mazungumzo ukibainisha msamiati kuhusu maeneo ya utawala, ukitilia mkazo kwenye matumizi ya majina ya ngeli ya PA-M-KU.


    Tathmini ya mada ya kwanza

    1. Taja nyanja tatu za uongozi wa Rwanda. 

    2. Taja aina tano za vitambulisho vinavyoweza kupatikana nchini Rwanda.

    3. Taja majina ya viongozi wanaochaguliwa na wale wanaoteuliwa pamoja na wale wanaopitia mitihani.

    4. Ni nini tofauti iliyoko baina ya ufalme na jamhuri?

    5. Kwa sababu gani Rwanda ni jamhuri?


    MADA 2: KISWAHILI NA FASIHI SIMULIZI